Elections 2010 Rostam aibiwa zana za kumng’oa Selelii

Zak Malang

JF-Expert Member
Dec 30, 2008
5,404
233
Rostam aibiwa zana za kumng’oa Selelii

VIFAA vya kampeni vya Mbunge wa Igunga (CCM), Rostam Aziz, vimedaiwa kuibwa katika mazingira ya kutatanisha.

Wizi huo ulifanyika ofisi za kampuni ya New Habari (2006) iliyoko Sinza Kijiweni jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita.

Vifaa vilivyoibwa vimetajwa kuwa pikipiki na baiskeli. Viliwekwa katika ofisi hizo Alhamisi iliyopita na vilitakiwa kusafirishwa kesho yake kwenda Igunga na Nzega mkoani Tabora.

Pikipiki 50 na baiskeli 50 zilikuwa bado hazijaunganishwa na imeelezwa kwamba zingeunganishwa mara baada ya kuwasilishwa majimboni.

Vyanzo vya habari vya kuaminika vimelieleza gazeti hili kwamba pikipiki 25 na baisikeli 25 zilikuwa zikipelekwa Igunga na kiasi hichohicho kilikuwa kikipelekwa jimbo la Nzega.

Wizi huo uligundulika wakati gari la kusafirisha vifaa hivyo lilipofika ofisini hapo.

Kwa sasa, jimbo la Nzega linashikiliwa na Lucas Selelii (CCM) ambaye anadaiwa kuwa hasimu wa kisiasa wa Rostam Aziz ambaye ni mbunge wa Igunga.

Uhasimu wa kisiasa kati ya wanasiasa hao wawili ulichochewa zaidi na kashfa ya Richmond ambayo ilisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ajiuzulu.

Tangu kipindi hicho, Selelii amekuwa akihusishwa na kundi la wabunge wapambanaji dhidi ya ufisadi lililokuwa katika vita kali dhidi ya akina Rostam kiasi cha kuundwa kwa kamati maalumu kuwapatanisha.

Vyanzo vya kuaminika vya gazeti hili vimeeleza kuwa baisikeli na pikipiki hizo zilikuwa chini ya Hussein Bashe, mmoja wa watumishi wa kampuni hiyo anayetajwa kutaka kuwania ubunge wa jimbo la Nzega kupitia CCM.

Bashe pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mmoja wa vijana wanaodaiwa kuwa na nguvu kubwa ndani ya umoja huo.

Simu ya mkononi ya Rostam ilikuwa ikiju kuwa hapatikani na hata alipoandikiwa ujumbe wa simu akiombwa kueleza kilichotokea katika kampuni yake, hakujibu.

Badala yake, katika muda upoatao dakika 10 tangu apelekewe ujumbe, Bashe alipiga simu kwenye gazeti hili na kusema “kilichoibwa ni fulana na kalenda.”

Alisema fulana hizo zina picha yake na amezitengeneza kwa ajili ya kuzitumia mara chama kitakapotoa ruhusa kwa wagombea kujitangaza katika majimbo wanayotaka.

“Hakuna baiskeli iliyoibwa ndugu yangu. Kilichoibwa ni fulana na kalenda zenye picha yangu ambavyo niliandaa kuvitumia mara tutakaporuhusiwa na chama kujitangaza,” alisema Bashe katika mazungumzo yake na gazeti hili.

Mazingira ya wizi huo yamezua utata mkubwa kwa vile ofisi za kampuni hiyo zina walinzi na zimezungushiwa uzio imara wa matofali ya saruji na hakuna uvunjaji wala matumizi ya aina yoyote ya vitisho vilivyotumika wakati wa wizi huo.

Hata hivyo, mwanasheria mmoja aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina alisema ni vigumu kwa walinzi wa kampuni hiyo kutiwa hatiani kama hawakupewa maelekezo ya kuvilinda.

“Kama vifaa vyenyewe viliingizwa ofisini kinyemela, itakuwa vigumu kumtuhumu mlinzi. Pengine ndiyo maana hawajawapeleka walinzi polisi.

Hata hivyo, MwanaHALISI lina taarifa kwamba wafanyakazi wa New Habari (2006) hawajalipwa mishahara kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu., Kuna madai kuwa baadhi yao hawakufurahishwa na ununuzi wa vifaa vya kampeni wakati wenyewe “wana hali mbaya.”

“Yaani badala ya kuhangaikia sisi tulipwe mishahara kwa kazi tunayofanya, mwajiri anafikiria mambo yake ya kisiasa tu? Hili limetuumiza sana,” ameeleza mmoja wa wafanyakazi.

Naye Selelii alipoulizwa iwapo baisikeli na pikipiki zilikuwa zikipelekwa jimboni kwake, Nzega ili kutumika kumg’oa, alisema hana taarifa na hilo.

Alimweleza mwandishi kwa njia ya simu kwamba yuko katika kijiji cha Puge, kilometa 60 kutoka Nzega mjini.

Hata hivyo, alisema “Tunazisubiri kwa hamu pikipiki na baiskeli hizo. Wananchi wa Nzega wanahitaji baiskeli kwa shughuli zao. Wazilete tu. Bali mimi najua sikuchaguliwa kwa baiskeli.”

Hii ni mara ya pili kwa Rostam kukumbwa na matukio ya wizi katika kipindi cha kuelekea kampeni.

Mwaka 2005, mmoja wa wasaidizi wake, Tabu Omari, aliibiwa mamilioni ya shilingi za kampeni wakati akizipeleka kwa Rostam katika eneo la Mtaa wa Mindu, Upanga jijini Dar es Salaam.

Chanzo: Mwanahalisi toleo na. 186
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom