Riwaya za Kijasusi

Don san tan

JF-Expert Member
May 23, 2015
562
433
RIWAYA: HUJUMA 1
MTUNZI: richard R. MWAMBE


UTANGULIZI
Tanzania inasonga katika nyanja ya sayansi na teknolojia, inapate uwezo wa kutengeneza silaha kubwa na za kisasa, vitu mbalimbali vya thamani na weredi wa hali yajuu.
Meli kubwa ya kivita ya JW inatekwa na maharamia wakiwa na lengo la kupora makombora makubwa yaliyokuwa yakisafirishwa kwenda ng'ambo.
Jw inaingia katika mgogoro mzito na watekaji wa meli hiyo wasio na chembe ya huruma......
Richard Mwambe anakuja tena na riwaya HUJUMA... keti nae jamvini mwanzo mwisho upate kujua nani kahujumu na kwa nini HUJUMA?

CHAPISHO LA 01
1
Bahari ya indi
MANOWARI ya kijeshi kubwa kabisa ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania kikosi cha wanamaji cha Kigamboni ilikuwa ikikata maji kwa kasi, ikitokea Tanzania kuelekea Urusi. Ilikuwa ni safari ya kusafirisha makombora kumi na mbili ya kisasa, makubwa yenye nguvu, makombora ya kisasa ambayo Urusi na Tanzania zilishirikiana kuyaunda ndani ya ardhi ya Tanzania. Kiwanda kikubwa kilikuwa kimejengwa maeneo ya pwani ya Mtwara eneo la Msanga mkuu, maalum kwa kazi hiyo.
Baada ya uchunguzi wa muda mrefu uliochukua takribani miaka kumi na tano hatimaye wataalamu wa milipuko wa jeshi la Urusi na wale wa Tanzania walikuwa wamekamilisha kuunda makombora hayo yenye nguvu aina ya R-36 ambayo teknolojia yake ni ya kule Urusi tangu miaka mingi ‘Intercontinental ballistic missile’, yenye urefu wa mita 32.2 (futi 106) na kipenyo cha mita 3.05 (futi 10), linaloweza kusafiri kwa kasi ya kilomita isiyopungua 7.9 kwa sekunde. Ni makombora yanayokwenda kasi ya ajabu na yenye mlipuko usio wa kawaida. Baada ya kuundwa katika kituo hicho maalum huko Msanga mkuu, Mtwara, sasa yalikuwa yakipelekwa kwa majaribio katika jangwa kubwa la Ryn lililoko Kusini Mashariki mwa Urusi, Maghalibi mwa Khazakistan, Kaskazini mwa bahari ya Caspian. Manowari kubwa ya Tanzania Kirov Class yanye urefu wa futi 827 iliyotengenezwakati ya miaka ya 1970 na 1990 huko Urusi na kuiuza kwa serikali ya Tanzania ndiyo ilifanya kazi hiyo ya kubeba makombora hayo makubwa kumi na mbili kuyapeleka huko bahari ya Caspian kwa majaribio.
Wanamaji waliokuwa ndani ya meli hiyo walikuwa wakiendelea kula raha kwa kucheza michezo mbalimbali kama bao, karata, draft na mingineyo mingi huku manaodha nao wakiwa kwenye kebini yao wakabadilishana mawazo. Wengi wa wanamaji hao walikuwa kutoka Tanzania na wacahache walikuwa kutoka Urusi, jumla yao ilikuwa ni kama ishirini na tano hivi. Ilikuwa ni wakati wa pekee wa wapiganaji hawa kubadilishana uzoefu wa kazi yao, ukiachilia wanamaji hao pia kati yao kulikuwa na wataalam wa milipuko nao walikuwamo. Siku hizo kulikuwa na wimbi kubwa la utekeji meli za mizigo, mafuta na nyinginezo katika bahari ya Indi hasa eneo la Somalia.
Usiku wa manane kila mtu akiwa kasinzia katika lile saa la shetani yaani saa nane kwenda saa tisa, kila mmoja alijibwaga ndani ya kitanda chake akiwa kabebwa na usingizi wa ajabu, kwa kuwa chombo hicho kilikuwa kikijiongoza kwa mitambo maalumu ya kompyuta hakikuwapa tabu waongozaji kujipumzisha japo kwenye viti vyao.
Mara ghafla kioo kikubwa katika chumba cha nahodha kilipasuka na kumwagika sakafuni, nahodha mmoja alishtuka kwa kelele za kioo hicho na upepo mkali ulikuwa ukiingia ndani ukipeperusha karatasi huku na kule, wasaidizi wa nahodha huyo nao wakaamka lakini kabla hawajakaa sawa, mmoja alibamizwa ukutani alikuwa amerushwa kwa risasi nzito ya mdunguaji, damu ikaanza kumwagika, kabla nahodha hajaminya ile nobu ya kengele ya hatari, naye alijikuta chali kifua chote kikiwa fumu kwa risasi nyingine ya mdunguaji. Msaidizi mmoja aliyebaki akaona isiwe tabu akaamua kutimua mbio kutoka chumba cha nahodha ili kuwahi mlango wa kuingia ndani ambako wengine walikuwa wamelala, alipotoka tu kwenye deki akajikuta akimulikwa na mwanga mkali sana uliomfanya ajizibe macho asiweze kuuona.
Helkopta kubwa ya kijeshi ilikuwa angani si mbali sana na uwanja wa meli hiyo ambao uliweza kuruhusu helkopta kama hiyo kutua juu yake, alipotaka kukimbia tena la haikuwezekana, alitunguliwa risasi ya mgongo na kujibwaga chini kwa kiwewe kilichomshika akakimbia na kujitumbukiza baharini, lile helkopta likashuka taratibu na kukanyaga sehemu ya juu ya manowari hiyo.
Giza nene likaivamia meli hiyo ghafla, kila mtu akashtuka ndani ya meli hiyo na kukurupuka kujiweka sawa kujua kulikoni, wamechelewa. Kila kona kulikuwa kumetanda watu walioficha nyuso zao wakiwa na silaha nzito za kisasa za kivita, walikuwa ni wengi maana mara tu baada ya ile helkopta kutua zilifuata boti nyingi ziendazo kasi zikaizunguka manowari ile, Maharamia. Kiongozi wa wale maharamia akatoa amri ya kuikagua ile manowari, na kuhakikisha kila binadamu mwenye uhai anateremshwa. Wale wapiganaji wote wakatolewa nje na kuwekwa mstari mmoja huku wakimulikwa na taa kubwa la ile helkopta.
“Karibuni sana Somalia, hii ndiyo Pwani ya Shetani, asikwambie mtu, hapa kila goti litapigwa,” yule Kiongozi alikuwa akiongea kwa kujigamba huku mkononi mwake amekamata bunduki kubwa yenye kilo nyingi, usoni akiwa kijifunika na soksi jeusi ili hasionekane uso wake, akatoa amri myingine na wale wafuasi wake wakawafunga kamba wale wapiganaji na kuwavisha kila mmoja soksi usoni baada ya kuwavua makombati waliovaa juu.
Kishapo wakawapakia kwenye boti zao na kuondoka nao eneo lile. Maharamia wanaojua kuongoza vyombo kama hivyo waka shika usukani wa Manowari hiyo kubwa kabisa na kuigeuza kuipeleka pwani ya Somalia, Mogadishu.
MOGADISHU
Maharamia waliwafikisha mateka wao katika pwani ya Mogadishu na kuwashusha wakiwaswaga mpaka kwenye malori yaliyokwisha andaliwa kisha wakaondoka nao kuelekea kusikojulikana.
Alkadhalika, ile manowari nayo ilifikishwa Mogadishu na mara moja usiku ule ule ilianza kazi ya kupakuwa yale makombora na kuyaficha kwenye ghala kubwa lililojengwa chini ya maji karibu kabisa na bandari kuu ya Mogadishu, yalifichwa hivyo ili kama wakija kuwakomboa wenzao basi waikute meli tupu kisha wale maharamia nao wakaondoka eneo lile.
§§§§§
Jamhuuriyadda Federaalka Soomaaliya, ‘Jamhuri ya Shirikisho la Somalia’, ni nchi iliyoko katika pembe ya Afrika, sehemu kubwa upande wa Mashariki ni bahari ya Indi. Somalia ni nchi iliyokuwa katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi kirefu na vikundi mbalimbali vya kigaidi kama Al-Shabab walitokea ndani ya nchi hiyo kutokana na tofauti za kisiasa.
Wimbi la utekaji vyombo vya majini liliibuka katika pwani ya nchi hiyo na kulaaniwa na kila taifa, kila serikali, kila taasisi ya kibinadamu duniani zikitoa wito kwa mataifa makubwa kukomesha uharamia huo.
Ilikuwa ni vigumu sana kutimiza lengo hilo la kukomesha wimbi la utekaji vyombo vya majini, haikujulikana sababu ni nini hasa ya kushindikana kwa juhudi hizo. Ilikuwa ni kitendawili kisicho na mteguaji. Hali kwa ujumla ilikuwa ni ya kuogofya katika eneo hilo, maharamia wa Somalia walikuwa hawaogopi hata sheria za maji makubwa, wao walichojua ni kuteka meli ilimradi wapate pesa, ukiwaona maharamia hao wanavovaa utasema ni masikini wakutupwa, lakini majumba hayo wanayomiliki ndani ya mji wa Mogadishu na viunga vyake ni kufuru kwa nchi hiyo isiyo na serikali kwa kipindi kirefu, kila mtu akiwa anajiamulia madaraka yake mkononi.
§§§§§
Jazeera Palace Hotel
Saa 2:10 asubuhi
Pembezoni kabisa mwa barabara ya Uwanja wa ndege ‘Airport road’,gari aina ya Jaguar nyeusi ilikuwa ikikunja kona kuingia katika hoteli ya Jazeera Palace asubuhi hiyo, moja kwa moja ikaingia katika maegesho na kuegeshwa sawasawa kabisa. Bwana mmoja wa makamo akateremka kutoka katika katika gari hiyo ya kifahari na kuuendea mgahawa wa hotel hiyo akachagua siti moja na kuketi. Haikupita hata dakika tano akaja mtu mwingine mnene kiasi mwenye upara unaong’aa ulioonekana wazi baada ya kuvua ile balaghashia yake na kuiweka mezani.
“Nipe habari,” yule bwana mwenye upara akamwambia Yule mwingine.
“Kila kitu tayari mzigo tunao, kilichobaki ni kuhesabiana tu, sisi wenyewe tunajua jinsi ya kuifikisha mahali husika,” alijibu bwana Shalabah, kiongozi wa maharamia. Ilikuwa ni biashara kubwa ya pesa nyingi za kigeni, nah ii ndio hasa waliokuwa wakiifanya maharamia hawa, safari hii walikuwa wamefanya biashara kubwa ya makombora hayo mazito.
“Ok, hatuna muda wa kupoteza, pesa iko tayari lini?” bwana Shalabah alimuuliza Yule mwenye upara.
“Pesa, pesa kitu gani? Kama wewe tayri una mzigo basi pesa utapata,” Yule mwenye upara alijibu.
“Kuna makombora 12, yenye uzito wa hali ya juu, ukipiga New York mpaka Ontario watatetemeka kwa hofu,” bwana Shalabah alimweleza Yule mwenye upara umadhubuti wa makombora hayo.
“Umenishtua sana, usijali nitwasiliana na washika dau ili tuyachukue yote 12 tuyapeleke huko maskani, sasa yako wapi japo niyaone,” Yule mwenye upara akamwambia Shalabah.
”Huwezi kuyaona, na wala hutakiwi kujua yako wapi, unachotakiwa kufanya wewe ni kuwasiliana na watu wako ili tufanye biashara, basi, hakuna kingine,” Shalabah alimueleza. Kisha akavuta mkoba wake na kufungua, akatoka kijitabu Fulani wakaandikiana mawasiliano yao na kisha wakaagana, kila mtu akachukua hamsini zake.
Shalabah akaikunja miguu yake na kuiweka kwa mtindo wa nne na kuagiza kinywaji kikali, alipoletewa alikuwa akinywa taratibu akisubiri miadi mingine, mara hii ya watu wake. Haikupita hata saa moja vijana watatu warefu, wembamba wakaingia na land cruiser pick up, wakateremka na kuungana naye katika kinywaji hicho.
 
RIWAYA: HUJUMA 2
MTUNZI: richard R. MWAMBE
MAHALI: LINDI

CHAPISHO LA 02

“Mmekuja?” akawauliza wakati akiwaona.
“Ndio, mkuu, tumeitika wito,” wakajibu
“Sasa, nimeona kazi mliofanya, hongereni sana, lakini kama kuna jambo nataka kuwaambia ni kuimarisha ulinzi pale gahalani, silaha za safari hii hawa jamaa hawatakubali zipotee hivihivi lazima watakuja, hivyo muweke ulinzi wa kutosha kwa maana jamaa wako tayari na wanataka kuchukua mzigo wote kwa pesa iliyotakata sana. Mimi jioni ya leo nitakwenda kuonana na Top ili tuone mgao wenu mpaka hapa mlipofanikisha unakuwaje,” Shalabah alikuwa akiwaeleza wale vijana mpango ulivyo kwa ujumla.

Maharamia hawa walikuwa tayari kufanya biashara ya makombora hayo na kikundi kimoja kinachoendesha mapigano yasiyokoma huko katika jangwa la Pakistan mpaka Afghanistan, kutokana na kuishiwa na silaha nzito waliingia mkataba na maharamia hawa ili wawatafutie silaha nzito na zenye nguvu ili kuwaadabisha mahasimu wao, safari hii wakazipata. Pesa waliokubaliana kuyanunua ilikuwa ni pesa ambayo inaweza kulisha Tanzania nzima kwa miezi kumi na moja kwa milo mitano ya mlo kamili kwa kila mwananchi bila kujali mtoto au mtu mzima. Ilikuwa ni biashara haramu kuliko haramu yenyewe.

Mr SHALABAH aliendelea kuketi pale alipoketi mara baada ya kuiachana na wale vijana wake, akiwa katika kuburudika na kinywaji chake mara akajikuta hayupo peke yake katika meza hiyo, mbele yake kulikuwa na kijana mkakamavu aliyevalia suruali ya jeans na shati jepesi, usoni akiyaficha macho yake kwa miwani nyeusi iliyomkaa sawia.
“Biashara imeenda?”Shalabah akauliza.

“Kama kawaida, hakuna kinachoharibika hapa,” Yule kijana akajibu.
“Ok, mzigo uko kamili?” Shalabah akarusha swali lingine.

“Mzigo hauna shaka, uko sawa, mmetusaidia sana na mapinduzi yanaendelea,” Yule kijana akajibu. Akaisukuma briefcase ilikuwa chini kwa mguu wake wa kushoto, ikamgusa Shalabah, Shalabah akaitazama na kuiinua akaiweka mezani, akaifungua na kuchungulia kidogo, manoti ya dola za kimarekani yalikuwa yamejipanga kwa mtindo wa kupendeza, akatabasamu na kutikisa kichwa. Akaingiza mkono katika mkoba wake mdogo na kutoa kamashine kadogo, akabofya hapa na pale akatoa kijikaratasi Fulani na kukiweka saini kisha akampa Yule kijana na kuagana naye. Alipohakikisha amepotelea nje, akanyanyuka na kuibeba ile briefcase naye akaielekea gari yake aina ya Jaguar aliyoiacha kwenye maegesho na kuondoka kwa kasi katika hoteli hiyo.

§§§§§

Breki ya kwanza aliikanyaga mbele ya jumba kubwa la kifahari katika mtaa wa Wadada Jaziira, Ndani ya mji wa Mogadishu. Jumba hilo ambalo nyuma yake lilikuwa limepakana na bahari ya Indi lilikuwa limejitenga na majumba mengine, lilikuwa mbali kabisa na makazi. Shalabah alikunja kona na kulifikia geti kubwa la jumba hilo, na mara lile geti likafunguka lenyewe na kuruhusu Shalabah aingie, akakanyaga mafuta kuifuata barabara inayoelekea katika jumba hilo ambalo lilijengwa umbali wa kilomita moja kutoka getini, aliegesha gari yake katika eneo maalumu, akashuka na ile briefcase mkononi na kuelekea mlango mkubwa wa jumba hilo. Vijana wawili wenye bunduki kubwa zenye nguvu walikuwa wamesimama katika mlango huo, mmoja huku na mwingine kule, walimkagua Shalabah na kuhakikisha hana silaha yoyote mwilini mwake, wakamruhusu kuingia ndani ya jumba hilo.

Jumba lote lilikuwa kimya kabisa, ni viatu vya Shalabah tu vilivyokuwa vikisikika wakati huo, akapanda ngazi kuelekea juu mpaka ghorofa ya kwanza, akapita tena katika korido ndefu iliyopambwa kwa sakafu na kuta za mbao safi ambazo polishi iliyopakwa na kung’aa sawia ilikufanya mpitaji ujione pande zote nne. Baada ya milango kama sita hivi, Shalabah alifika katika mlango wa saba akageuka na kuutazama, kulikuwa na kidubwasha chenye tarakimu tisa, akabofya tarakimu hizo kwa mtindo anaoujua yeye na mara ule mlango ukafunguka, Shalabah akaingia ndani ya kijichumba hicho kidogo na ule mlango ukajifunga, kisha kile chumba kikaanza kuteremka chini, kikaiacha ile mandhari ya mbao na kubaki kioo tupu, Shalabah aliweza kuona samaki aina mbalimbali na mandhari nzuri ya chini ya bahari, mara kile chombo kikaingia tena katika mandhari nyingine ya mbao zenye kung’aa kama zile za mwanzo, mara ikasikika sauti Fulani ikabip, ule mlango ukafunguka na Shalabah akateremka na kuifuata njia nyingiine ndefu mbele kulikuwa na mlango mwingine, ukafunguka kabla hata ya kuugusa, akaingia na kujikuta kwenye sebule pana yenye vitu vya thamani sana.

“Karibu Mr Shalabah,” sauti ilimkaribisha. Shalabah akaketi katika moja ya viti vilivyomo katika sebule hiyo. Mbele yake katika ukuta kukajitokeza luninga kubwa ‘flat’ na hapo aliweza kumuona Yule anayeongea naye.
“Ndiyo Mr. Shalabah, nipe ripoti kwa ujumla,” Yule mtu kwenye ile screen alimwambia Shalabah.
Shalabah alitoa taarifa kamili ya mchakato mzima wa utekaji wa manowari ya kijeshi iliyotoka Tanzania, pia akamweleza kuhusu pesa aliyolipwa na Yule kijana kwa biashara nyingine waliyokuwa wameifanya siku chache za nyuma.
“Vizuri sana,” Yule bwana kwenye ile luninga akajibu, kisha akaendelea, “Sasa kuna mpango gani kuhusu hizi silaha za sasa?” akuliza.

“Kwanza wale jamaa walitaka makombora lakini hawakusema idadi, sisi tumepata makombora makubwa kumi na mbili na silaha nyingine nyingi za kufaa,” Shalabah alieleza.

“Ok, hakikisha kila kitu kinakwenda sawa, imarisha ulinzi ijapokuwa naamini hakuna wa kutuumiza kichwa kwani kwa taarifa ambazo ninazo mpelelezi mkorofi wa Tanzania hayupo kazini kwa kipindi kirefu na nafasi yake imechukuliwa na mwingine, hakikisha kila mtu anayekuja kuhusiana nah ii shughuli unamuua, hakuna kumpa mtu nafasi hata ya robo sekunde, weka watu kila mahali, kila sehemu nyeti hakikisha umeweka kinasa sauti kilicho hai na Yule mdunguaji niliyekwambia umkodi ulimpata?” Yule bwana kwenye luninga alijaribu kupanga na kuuliza.

“Bila shaka mzee, nimempata na leo jioni nitaingia naye mkataba,” Shalabah akajibu.
“Sasa umwambie mkataba wetu utakwisha pale tu jamaa hawa watakapochukua mzigo wao, na hao mateka hakikisha tunawauza kwa vikundi vya ugaidi kwani nao ni silaha nzuri sana,” yule mtu kwenye luninga alimaliza na kisha ile luninga ikadidimia chini, pale ilipokuwapo pakatoakea picha kubwa ya mwanamke aliyelala uchi.

Mlio wa bip ukasikika, Shalabah akainuka na kuiacha ile briefcase palepale akatoka na kuingia katika kijichumba kile alichotokea mwanzo, kikampandisha na kumleta juu kabisa, akashuka na kuondoka zake huku akiliacha lile jumba nyuma yake likifanya mandhari safi inayolipamba jiji la Mogadishu.

Shalabah alikanyaga mafuta mpaka eneo linguine kabisa la mji, hapo palikuwa na jengo kama shule kubwa, Shalabaha akaingia na kupita moja kwa moja kwenye jengo linguine lililokuwa limejengwa ndani yake.
“Karibu sana bwana mkubwa, tukusaidie nini?” mlinzi wa eneo hilo aliuliza kwa sauti ya majigambo huku akimtunishia kifua Shalabah.

“Nahitaji kumuona bosi wako,” Shalabah akajibu.
“Unaitwa nani na umetoka wapi?” Yule mlinzi akauliza.

“Shalabah, kutoka Uranus,” akajibu. Yule mlinzi akainua simu na kupiga sehemu fulani, kisha akaongea maneno machache na alipoirudisha simu hiyo mahala pake, akamruhusu Yule bwana kuingia ndani. Shalabah alijikuta kwenye uwa mkubwa uliokuwa na watoto wengi waliokuwa katika mafunzo makali ya karate na kungfu, mkufunzi wao aliyekuwa mbele kabisa alionekana kuwa stadi sana kwa minyumbuliko aliyokuwa akifanya akiwaelekeza jinsi ya kukunja mikono na jinsi ya kusimama kimapambano.

Shalabah alipitishwa kwenye ujia mrefu mpaka katika mlango mmojawapo kati ya mingi, akaingizwa ndani na kuketi katika sebule kubwa lenye nakshi za kuvutia, zuria la gharama liliificha sakafu safi ya terrazzo, Shalabah alikuwa akiitalii sebule hiyo kubwa ya kuvutia iliyokosa kitu kimoja tu, muziki, muziki mororo ambao ungemfanya aliyeketi katika moja ya matandiko hayo ama achezeshe mguu au kichwa kufuatisha midundo ya muziki huo. Shalabah akiwa katika mawazo hayo mara akasikia mlango ukifungwa nyuma yake, akageuka lakini hakumuona mtu, aliporudisha uso wake mbele alikutana na mtu aliyekwishaketi tayari katika tandiko moja wapo mbele yake. Mtu aliyevalia juba la kibuluu lililoficha mwili wote na kuaacha macho mawili tu yaliyokuwa yakionekana kwa taabu kidogo. Shalabah hakujua kama mtu huyo ni mwanamke ama mwanaume kutokana na vile alivyovaa vazi lake hilo.

“Mr Kalabah, karibu sana katika himaya yangu,” Yule mtu alimkaribisha, Kalabah alimtambua kuwa ni mwanamke kutokana na sauti yake.
“Nimekwishakaribia, shukrani,” kalabah alishukuru.
“Tusipoteze muda, niambie shida yako,” Yule mwanamke alimweleza.
“Bimekuja kutoka Uranus, nina shida ya kikazi kama ofisi ilivyonituma,” Shalabah akiwa aneleza lililomleta, akaktishwa na sauti ya nhuyo mwanamke.

“Kazi au biashara?” akauliza.
“Si biashara kwa kuwa hakuna tunachotaka kukuuzia, ila kazi kwa kuwa tunataka ututekelezee jambo Fulani,” Shalabah akaeleza.

“Ok, linahusu damu ya mwanadamu?” Yule mwanamke akauliza.
“Ndiyo, litahusisha,” Shalabah akajibu.

“Sikila Mr. Shalabah, kwa hilo unalotaka tuongee hapa si mahali pake, nitakuelekeza wapi tuonane, hatuwezi kufanya biashara ya damu katika kasri hili tukufu, kasri la marehemu baba yangu alilotumia kuabudu, wewe nenda na mimi nitakujulisha wapi tuonane,” Yule mwanamke akamaliza kuzungumza na kuinuka kutoka pale alipokuwa ameketi akatokomea katika mlango mmoja wapo. Shalabah akainuka tayari kutoka ndani ya jumba lile, msichana mrembo wa uso alikuwa tayari kumwongoza kumtoa nje ya kasri hilo.

Shalabah alitolewa nje ya jengo lile kwa kupitia njia ileile lakini mara hii ali[pofika kwenye ule uwa akasimama na kushangaa anachokiona, mara ya kwanza alikuta watoto wakifanya mafunzo ya kungfu na karate, lakini mara hii alikuta uwa wote umeota nyasi na wanyama kama mbuzi walikuwa wakiburudika, alishindwa kuuliza akaamua kupitiliza mpaka nje ambako aliagana na Yule msichana akalielekea gari lake. Alipoketi nyuma ya usukani ndipo alipoiona kadi ndogo nyeupe ikining’inia katika swichi ya kuwashia vifuta maji (wipers) vya gari hiyo, akainyakuwa na kuisoma.
‘…Dar es salaam Club, saa 3:00 usiku…’

Akainyakuwa na kuitia mfuko wa shati, kisha akawasha gari na kuondoka zake.
 
RIWAYA: HUJUMA 3
MTUNZI: richard R. MWAMBE
MAHALI: LINDI



CHAPISHO LA 03

2
Makao makuu ya jwtz
Lugalo – dar es salaam

TAARIFA za kupotea kwa manowari ya jeshi la Tanzania na wapiganaji wake zilifika katika makao makuu ya jeshi hilo pale Lugalo mnamo majira ya saa tatu ausbuhi muda ambao manowari ile ilitakiwa kuwa imefika katika moja ya vituo vyake kabla ya kuwasili katika bahari ya Caspian siku mbili zinazofuata. Jeshi la Urusi lilipowasiliana na lile la Tanzania ilionekana wzi kuwa manowari hiyo imepotelea katika bahari ya Indi usiku uliotangulia, kwani kila walipojaribu kuitafuta kwa vifaa vya kisasa walishinda kabisa kuiona ilipo lakini waliweza kuona ilipoishia safari yake.

Wakipiga picha ya eneo hilo wanakuta ilikuwa sehemu za Somalia ijapokuwa ilikuwa katika maji makubwa, maji ya kimataifa.

Mkuu wa majeshi, brigedia jenerali Kamsumi alikuwa ameketi na viongozi wake wa ngazi ya juu kabisa jeshini wakijaribu kujadili juu ya upotevu wa manowari hiyo. Ulikuwa ni mkutano mzito ambao kila mshiriki alionekana kushikwa na jazba au hasira.

“Hao ni maharamia tu, si wengine, siku hizi wamekuwa wakiteka meli nyingi bila kujali sheria za kimataifa kuwa meli hizo ziko katika maji ya kimataifa, kwa nini tunawadekeza?” alilalama mmoja wa washiriki aliyekuwa katika jopo hilo.
“Meli sio tatizo, lakini vipi kuhusu makombora hayo ambayo gharama tu ya kuyatengeneza ilikuwa ni kubwa ijapokuwa tumepata ufadhili wa asilimia Fulani ya Warusi, tukiyaacha hawa jamaa si watatugeuka wenyewe?” Mjumbe mwingine alieleza.

“Hivyo vyote havina maana, wapiganaji wetu, watoto wetu wametekwa au kupotea pamoja na manowari hiyo kwa nini tuvumilie? Tuna makomandoo hapa tutume japo wawili tu wakaitafute hiyo meli kisha tuikomboe,” mjumbe wa tatu alikuwa akiongea mpaka anatoa machozi.

Baada ya majadiliano marefu na yaliyokuwa hayana mwisho, muada ulifika wa kufanya video conference na amiri jeshi mkuu. Luninga iliyokuwa ukutani ikachukua uhai na moja kwa moja mbele yao akainekana mheshimiwa Rais. Mkuu wa majeshi akaeleza kwa kifupi waliyojadiliana wajumbe katika kikao kile.

“Sikilizeni, hatuwezi kuvumilia wala kuwapa nafasi, ile ni pesa ya kodi za Watanzania, kwa nini ipotee hivihivi? Isitoshe kuna watoto wetu, vijana wetu na wapiganaji wetu, lazima waokolewe kwa gharama yeyote,” amiri jeshi mkuu aliongea kwa ukali sana, “Ninyi mna kitengo cha upelelezi ndani ya JW, haya mara moja chagueni mtu au watu wakafanye kazi hiyo, nitahitaji ripoti haraka,” mwisho wa maneno hayo ile luninga ikazimika. Kila mshiriki alishusha pumzi ndefu. Ilikuwa ni sentensi ndefu kidogo iliyowatetemesha wakuu hao wa jeshi waliokuwa wakibishana bila kupata muafaka katika lipi la kufanya. Kutokana na kauli ya aamiri jeshi mkuu, hakukuwa na mjadala mwingine kilichoangaliwakilikuwa ni nani apewe kazi hiyo.

“Lakini jamani ee, tuiangalie hii kazi kwa ugumu na upana wake,” kiongozi mmoja alisema.

“Yeah ni kweli kuliko kudharau na kupeleka mtu ambaye atafika na kushindwa kufanya lolote. Nani tumtume akafanye kazi hiyo, kazi yan hatari kuliko hatari mwenyewe. Chekecha chekecha ikapita, Jamil Semindu, komandoo aliyemeliza mafunzo yake siku si nyingi nchini Cuba, jina lake lilipitishwa tayari kwa kazi hiyo. Mchana wa siku hiyo kijana huyo aliitwa makao makuu ya jeshi kutoka kambi ya Lugalo kule Mwenge. Naye hakukataa wito bali aliamini msemo wa wahenga, ;usikatae wito kataa neno’.

Majira ya saa nane mchana, Jamil Semindu alikuwa amesimama wima kiukakamavu mbele ya mkuu wa majeshi. Hakuwa peke yake, pembeni yake kulikuwa na mtu mwingine wa makamo, aliyavalia nguo nadhifu ya kijeshi.
“Jamil Semindu, Gwamaka Mwakajinga, tunatambua umuhimu na mchango wa kazi yenu katika jeshi letu tukufu la wananchi wa Tanzania. Nimekuiteni hapa kuwapa kazi maalum ambayo inatakiwa kuanzwa mara moja, kama mnavyojua au milivyosikia, manowari yetu ya jeshi la Tanzania, Kirov Class, ndani yake ikiwa na wapiganaji ishirini na tano pamoja na makombora kumi na mbili ya R-36 imepotea katika maji ya kimataifa huko Somalia, inahisiwa kuwa huenda ikawa imetekwa na maharamia kama iloivyotokea kwa meli zingine za mizigo. Tunawatuma muende mkafanye kazi, kwanza mkawaokoe wapiganaji wetu, pili mkaokoe makaombora yetu, tatu mkailete na meli yenyewe, mambo yote yamekwisha andaliwa mkitoka hapa tu mtaelezwa cha kufanya,” alimaliza mkuu jeshi. Wale wanajeshi wawili wakapiga salute na kisha kutoka nje ya ofisi hiyo.

Gwamaka Mwakajinga alikuwa mpelelezi wa kijeshi aliyeaminika sana hasa kwa kuzisoma nyanyo za adui, na kujua wapi alipo. Kijana huyu ndiye aliyewaongoza wenzake katika vita ya ukombozi huko visiwa vya Komoro, vita ya kumng’oa madarakani aliyekuwa rais wan chi hiyo. Alishiriki pia kupeleleza vizuri sana makazi ya waasi wa M23 pamoja na kujua maisha yao ya kila siku, mwisho wa siku aliwapa ramani yote majeshi ya Umoja wa Mataifa yakiongozwa na Tanzania na kuwafutilia mbali waasi hao. Jopo lililokaa kuchagua wawili hao liliangalia mambo mengi na tofautitofauti.
Gwamaka na Jamil wakapeana mikono na kusalimiana wakati wakiwa nje ya jengo hilo, kisha wote wawili wakaelekea katika jengo linguine kama walivyoongozwa.

“Unaonaje Meja, hawa vijana watawaweza wale maharamia wanaokunywa damu?” Luteni kanali Gogo alimuuliza mwenzake aliyekuwa naye, kapteni Kamazima.
“Wataweza tu, tuweke imani,” Meja Kamazima alimjibu.
“Maana wale maharamia kuwapata ni kazi, nao pia wamejikamilisha kwa silaha na upiganaji wa silaha,” Luteni Kanali Gogo alionesha waziwazi wasiwasi wake katika hili.
“Wataweza tu usihofu,” Meje Kamazima alimjibu na kumtia moyo mwenzake.

Taratibu zote zilikamilishwa za safari za hao jamaa, na siku iliyofuata kwa kutumia ndege ya shirika la ndege la Ethiopia waliondoka Tanzania kuelekea Somalia kupitia Addis Ababa.

“Sijacheza michezo hii siku nyingia sana,” Jamil alimwambia Gwamaka.
“Michezo midogo sana hii, nilikuwa Kivu juzijuzi tu kuwasaka M23 hivyo bado damu ya moto,” akazungumza Gwamaka. Walibadilishana mawazo wakiwa katika ndege hiyo safarini kuelekea Mogadishu.
“Sasa sikia Jamil, unajua hawa jamaa ni wajanja sana, kwa vyovyote lazima wanajua kama tunakwenda, tukifika naomba tushuke kila mtu kivyake na tusijuane isipokuwa tuwasiliane kwa simu tu kila mtu atakapofikia,” Gwamaka alijaribu kupanga mpango.

“No, tufikie hotel moja lakini tutofautishe vyumba kwa umbali mrefu kama kuna ghorofa basi mmoja ya juu mwingine ya chini,” Jamil naye akatoa pemdekezo ambalo lilikubaliwa na wote.
“Tutafanyaje operesheni yetu?” Jamil akauliza.

“Kutokana na kazi zetu, mi nitakuwa nafanya uchunguzi nakupa information na wewe unakwenda kumaliza kazi maana we ni jeshi la mtu mmoja,” wote wakacheka na kugonga viganja vyao.

RAMADA PLAZA HOTEL

Ramada plaza hoteli, ni hotel tulivu iliyo jirani na bahari katika jiji la Mogadishu, ikitazamana na bandari ya zamani ya jiji hilo. Mandhari safi, chakula na mazingira ya kuvutia viliwafanya wapiganaji hawa kuvutiwa na mahali hapo.
Alikuwa Gwamaka wa kwanza kuingia katika hotel hiyo, akapanga chumba ghorofa ya tatu juu. Baadae jamil nae akafika na kuchukua ghorofa ya chini kabisa, wakiwa tayari kikazi na wamekamilika.

Kutoka ghorofa ya tatu Gwamaka aliweza kutumia darubini yake kuangalia upande wa baharini kila baada ya nusu saa na kuandika kwenye kidaftari chake mambo anayoyajua mwenyewe. Jioni ya siku hiyo wakiwa chakulani walibadilishana mawazo hili na lile na kupanga nini cha kufanya.
 
RIWAYA: HUJUMA 04
MTUNZI: richard R. MWAMBE

CHAPISHO LA 04

DAR ES SALAAM CLUB

BW. SHALABAH aliegesha gari yake katika maegesho ya club hiyo ya usiku, akateremka na kuufunga mlango nyuma yake. Kisha kwa hatua za taratibu aliuendea mlango mkubwa. Kwa upande wa nje zaidi ya walinzi walioonekana kuangalia usalama wa mali za wateja, hakukuwa na vurugu wala hakukusikika kelele yoyote ya kitu chochote, mtaa ulikuwa kimya kabisa. ni wale tu waliokuwa hawafuati sawasawa misingi ya dini yao ndiyo waliokusanyika katika klabu hiyo pamoja na wageni kutoka Katika nchi za pembezoni na zile za mbali.

Shalabah alizipanda ngazi na alipofika katika mlango wa kuingilia alisimamishwa na akatakiwa kusalimisha kama ana aina yoyote ya silaha, alikuwa na bastola moja na kisu cha kukunja, akaviacha na kuandikisha, akapewa namba na kuingia ndani.
Tofauti na nje, ndani ya klabu hiyo kulikua na kila aina ya starehe, muziki laini ulikuwepo na wale waliopenda disco walitakiwa kuteremka chini kabisa. watu walikula na kunywa wakifurahia maisha. Shalabah alijipenyeza taratibu katika makundi ya watu mpaka akaifikia kaunta kubwa.

“Nikusaidie nini?” akauliza mtu aliyekuwa kaunta. Shalabah hakujibu isipokuwa alitoa sigara na kumuonesha, kisha yule jamaa akatoa kiberiti na kukiwasha lakini hakuiwasha ile sigara. Sekunde chache tu mwanadada mrembo aliyekuwa na nywele mpaka kiunoni alimjia Shalabah na kumshika begani. Shalabah akamfuata. Wakapenya penya katika makundi ya watu, wakapita nyuma ya jukwaa la wacheza uchi wakaingia kwenye pazia la kumetameta, ndani ya mlango mkubwa na mzito wa kioo, hakukuwa na kelele yoyote, palikuwa kama nyumbani, huko kulikuwa na vyumba vingi sana.

809, yule mwanadada akasimama na kubofya kitufe Fulani, mlango ukafunguka, wakaingia. Ndani ya chumba hicho kulikuwa na chumba kimoja kidogo na mwanadada mrefu aliyekuwa na upara kichwani mwake huku akivuta mtemba kinywani mwake alikuwa amekunja nne kwenye sofa moja pana na kuiachia nguo yake yenye mpasuo mrefu kumwagika kwa chini na kuruhusu mapaja yake laini kuonekana kwa ukamilifu.

“Karibu Kijana,” yule mwanamke akamkaribisha.
“Asante sana,” Shalabah akajibu.
“Haya tuna dakika tano tu za kuzungumza, nipe mzigo, nikupe kipimo,” yule mwanamke mwenye upara akamwambia Shalabah.

“Nafikiri unatufahamu, sasa tuna biashara nzito sana ya kufanya, ijapokuwa hatuna hofu na usalama kutokana na biashara zetu zilizopita, ila hii tumetahadharishwa sana, kuna watu tunatakiwa kuwaondoa haraka iwezekanavyo lakini pia tunahitaji usaidizi wa kiteknolojia katia kuyatambu makombora kumi na mbili tuliyoyateka,” Shalabah alieleza.
“Ha ha ha ha nyie watu mna biashara za hatari sana, kwa kuwa tuliingia mkataba huo tangu mwanzo na tajiri wenu hamna tabu, haya kazi ya kwanza itafanyika, nipe picha za hao watu na wapi wamefikia, kuwatungua si tatizo, kisha tutaliona la pili,” yule mwanamke mwenye upara akaeleza. Shalabah akatoa Ipad yake na kuparazaparaza vidole vyake kwenye kioo cha chombo hicho, kisha akamkabidhi yule mwanamke. Akachukua na kutazama, naye akaparaza hapa na pale na zile picha zikahamia kwenye simu yake ya kisasa kwa njia ya Bluetooth.

“Ok Mr. kila kichwa dola 1000 za kimarekani, nimemaliza, fanya mchakato kama tunavyofanya kila wakati,” yule mwanamke akanyanyuka na vazi lake likamfunika vyema, akafungua mlango wa nyuma yake na kutokomea. Shalabah alitoka ndani ya chumba kile na kutembea taratibu kurudi ukumbini, kisha akatoka nje ya klabu ile.

§§§§§

Ndani ya bahari ya Indi katika bandari ya zamani ya Mogadishu, maharamia wateka meli walikuwa katika ulinzi wa aina yake. Walionekana ni watu masikini kimavazi lakini ukiwatazama silaha walizobeba mikononi mwao utakubali tu. Wapo waliokuwa juu muda wote wakitazama usalama kwa kujifanya wana shughuli mbalimbali. Na daima walikuwa wakifuatilia sana nyendo za wageni wanaoingia Somalia hasa wale kutoka nchi za maghalibi kwa maana walikwishateka meli kadhaa za mataifa hayo na kuwaweka mateka wanajeshi wao. Hata zile nchi zilipojaribu kutaka kuwapata watu hao ilikuwa ngumu kutokana na nchi ya Somalia kutokuwa na serikali ambayo unaweza ukafanya mazungumzo nao.

Wapiga mbizi kadhaa walikuwa ndani ya maji wakikagua makombora hayo, upande wa wale wanaouza ambao ni hao maharamia na wale wanaouziwa wapiganaji waasi kutoka huko Pakistani na Afghanistani, walikuja na wataalamu wao na wakati huo maharamia hao nao walikuwa na mtaalamu wao wa silaha, mwanamke yule mwenye upara. Ukaguzi ulifanyika chini ya maji kwa muda takribani wa dakika thelethini, kisha wapiga mbizi hao wakatokea ndani kwa ndani na kuingia katika chumba kilichojaa maji ambacho kuna ngazi unapanda na kutokea chumba cha juu kisicho na maji. Hapo wakavua mitambo yao walioibeba migongoni na kubaki katika nguo zao za kawaida. Kisha wakafuatana kutoka na kuingia katika gari iliyoandaliwa wakaelekea mjini.

Kepteni Gwamaka Mwakajinga akashusa darubini yake kutoka katika uso wake akaichia ining’inie kifuani.
“Wametoka,” Gwamaka akawasiliana na Jamil aliyekuwa kwenye gari nyingine.
“Wasindikize, unambie wanapoishia,” Jamil akamwambia Gwamaka. Kwa mwendo wa taratibu Gwamaka akaingiza gari barabarani na kuendessha kuelekea kule ambako gari ile ilikwenda. Alihakikisha haipotezi kabisa gari hiyo katika macho yake.
Aliendelea kuwafuata akiwa peke yake ndani ya gari.
“Gwamaka, kuna gari imenipita kasi sana hapa hebu iwekee tahadhari,” Jamil aliwasiliana na Gwamaka wakati gari hyo aliyoisema ikiwa mbele yake kama mita kumi tu. Walipoiacha barabara ya Corso Somalia na kuupita mzunguko kisha kuikamata barabara ya Jidka Jannaral Daud ndipo komandoo Jamil alipoona hila ya watu hao, akajua wazi kuwa wako matatani na hana budi kumsaidia mwenzake aliyekuwa mbele.

“Nimeiona,” akajibu.
“Kaa tayari, jamaa wameandaa silaha nahisi wanataka kufanya shambulizi la ghafla,” Komandoo Jamil alimwambia Gwamaka.
“Natafuta mbinu ya kufanya,” Gwamaka akamwambia Jamil.
Haikupita sekunde thelathini, wakati wanakaribia kabisa shule ya sekondari ya Jan Daud, ile gari nyuma ya Gwamaka ikaovateki ghafla na kukaa upande wake wa kushoto, Gwamaka akawa tayari amekwishaiona, akaipa sekunde mbili ilipokuwa tayari inakaribia nusu ya gari yake kuovateki, nae akaitoa gari yake kushoto, na kusababisha dereva wa wale jamaa kuyumba, ile gari ikagonga nguzo ya umeme, cheche zikawaka na transifoma la jirani likalipuka.

“Usisimame, wafuate,” Komandoo Jamil akamwambia Gwamaka kwa simu yake ya upepo yeye akiwa katika gari iliyokuwa nyuma yao umbali wa mita kama hamsini hivi, aliishuhudia ile gari ikigonga nguzo na ule moto wa umeme uliolipuka ukafanya gari ile kushika moto. Jamil alishuhudia watu wale walivyokuwa wakijaribu kutokea madirishani.
“Safi sana Gwamaka!!!!” Komandoo Jamil aliikubali mbinu iliyofanywa na Gwamaka, akaongeza mwendo na kuzipita gari mbili zilizo katikati yake. Akapunguza mwendo na kushuhudia wawili wakiungua vibaya kwa kushindwa kutoka ndani ya gari, na mmoja akiwa ndiye anajinasua dirishani. Komandoo Jamil, akaegesha gari pembeni na kuteremka kwa minajiri ya kutoa msaada, akamuendea yule wa dirishani na kumnasua katika kioo, akambeba na kumtia kwenye gari yake.

“Wapi Hospitali?” akawauliza watu waliokuwa eneo lile kwa lugha ya kiarabu ambapo walielewana vizuri, hilo halikumfanya yeyote kutia mashaka juu ya Jamil, akaondoka kwa kasi mapaka njia panda ya Siinay akakunja kushoto na kuendesha gari hiyo kwa kasi ya ajabu, mpaka akauacha mji na kufika maeneo yaiyo na watu, jangwa lilianza kumkabili, akaegesha gari pembeni, akamshusha yule jamaa.

“Hapa ndo hospitali?” yule majeruhi aliuliza kwa tabu kidogo.
“Aliyekwambia mi mwezi mwekundu nani hata nikupeleke wewe hoapitali?” Jamila akajibu na kumvuta akambwaga kwenye mchanga ulioshika joto kali la jua. Akamkanyaga pajani ambapo palikuwa na donda kubwa la moto.
“Nani mwajiri wako?” akamwuliza. Yule jamaa hakujibu isipokuwa akamtolea macho Jamil. “Nakuuliza nani unamfanyia kazi? Aliyewatuma kuifuatilia ile gari,” akaongeza swali linguine, yule jamaa akawa mgumu kujibu, Jamila akamuinamia na kuchomoa kisu, akachoma mchomo mmoja kwenye paja. Yuele jamaa akatoa yowe la uchungu sana.
“Nitakwambia, nitakwambi, nitakwambia,” akapiga kelele.
“Haya nambie,” Jamil akamsikiliza.

“Sharon, Sharon, kamanda Sharon,” akajibu.
“Ndiyo nani?” akauliza tena Jamil.
“Kiongozi wetu, aliwaona mkitufuatilia, akatutuma tumuue yule mwingine, wewe hakukuona,” yule bwana akajibu huku akilia kwa uchungu.

“Anaishi wapi huyo Sharon?” Jamil akahoji. Yule bwana akawa jeuri kujibu, kila alipolazimishwa hakujibu. Jamil akashika kile kisu kilichodinda katika nyama ya paja la yule jama na kukizungusha, yowe kali lilimtoka tena yule bwana akalia mpaka akawa akipigapiga ngumi kwenye mshanga.

“Jidka Dabaqayn,” akajibu huku akilia. Jamil akamuacha na kuchomoa kile kisu. Kitendo cha ghafla yule jamaa kutoka pale chini akajinyanyua na kutaka kumvamia Jamil, Jamil akaliona hilo haraka, akaachia makonde mawili makali yaliyomrudisha chini na kumtoa roho. Akamuendea na kumsukasuka kwa mguu wake, ameshakufa. Akampekua mifukoni hakuna cha maana alichokipata zaidi ya picha moja ya msichana mbichi aliyepiga akiwa uchi wa nyama, akaichukua na simu yake pia na akaondoka navyo. Jamil akaliendea gari lake na kuondoka akiuacha mwili wa yule jamaa palepale jangwani yeye akarudi mjini.
 
RIWAYA: HUJUMA 05
MTUNZI: richard R. MWAMBE
CHAPISHO LA 05


Gwamaka aliendelea kuifuata ile gari mpaka pembezoni mwa mji, ikaingia katika jengo moja kubwa lililoonekana kama kiwanda Fulani, yeye akapitiliza na kwenda kuegesha gari mbele kidogo. Akateremka na kurudi polepole mpaka kwenye mgahawa uliokuwa ukitazamana na jengo lile. Akaketi upenuni mwa mgahawa huo na kuagiza kinywaji huku macho yake yakitazama mara kwa mara jengo lile. Moqdisho textile, ni maandishi yaliyolipamba godown lile kwa upande wa juu, Gwamaka akachukua kijidafutari chake na kuandika jina hilo, jina la barabara na namba ya kiwanja, akahifadhi mfukoni mwake. Akaendelea taratibu kupata kinywaji chake.

Akiwa bado anaendelea mwanadada mmoja alitoka ndani ya mgahawa huo na kuketi katika kiti cha mbele yake, wakasalimiana, ijapokuwa Gwamaka alikuwa akibabaisha kusalimiana kwa lugha yao. Akabadilisha lugha na kuanza kuongea kiingereza. “Inaonekana ni mgeni wewe hapa?” yule mwanamke akamwuliza Gwamaka.

“Ndiyo, ni mgeni hapa, nimesimama kidogo nipate kinywaji, si waona jua lilivyo kali,” Gwamaka akamweleza.
“Aa yah ni kweli, wewe watokea wapi?” yule mwanamke akamwuliza.

“Mimi ninatokea Kenya naitwa Charles Musungu,” Gwamaka akajitambulisha kwa jina la bandia.
“Oh, jina zuri, mi naitwa Fatma, huu mgahawa hapa ni wa familia,” Fatma akaendelea kuzungumza, baada ya hapo mazungumzo mengi yakaendelea kati ya wawili hao, Gwamaka akachukua kadi ya kibiashara ya Fatma na kuihifadhi. Wakati wakiendelea kuzungumza, aliiona ile gari aliokuwa akiiangalia akaiona ikitoka na kuondoka.
“Fatma, maadam nina namba yako, basi nitakupigia jioni, vipi unaweza kuungana nami jioni ya leo?” Gwamaka akamwambia Fatma huku akiwa amenyanyuka tayari kuondoka.

“Bila shaka Charles,” Fatma akaitika huku akimshuhudia Gwamaka akaiziacha ngazi za mgahawa huo na kuingia mtaani, aliichuku gari yake na kuondoka kwa kasi kuifukuza ile gari, si mwendo mrefu aliikuta, akaipa nafasi gari ile na kuifuata taratibu.
“Braza,” sauti ikaita katika earphone yake.
“Hey Jamil,” Gwamaka akajibu.
“Uelekeo,” Jamil akauliza.
“Bado nawinda, nitakucheki,” Gwamaka akajibu.
“Copy,” Jamil akaitikia.

Msafara wa ile gari ukaelekea uwanja wa ndege moja kwa moja. Gwamaka akaendele kuwatazama watu wale wakiagana, akachukua kamera yake na kupiga picha kadhaa. Aliporidhika na zoezi hilo akaingia kwenye gari yake na kurudi mjini.

Gwamaka alikuwa akiendesha gari taratibu huku akipiga mruzi, mbele yake akaona kibao kilichoandikwa SHELL, alipotazama mshale wa mafuta ulimuonesha tanki lake liko mbioni kumalizika, akawasha indiketa ya kulia na kuingia katika kituo hicho cha kujazia mafuta. Moja kwa moja akaegesha katika moja ya pampu sita zilizofungwa hapo.

“Full tank tafadhali,” akamwambia kijana aliyekuwa akihudumia pampu hiyo, na kijana yule akafanya kazi yake kama ilivyotakiwa. Gwamaka akalipa na kuondoka eneo lile kurudi hotelini kwake. Akaingia kwenye maegesho ya magari na kuliweka gari lake vizuri, akatulia kwanza kabla ya kushuka, baada ya dakika kama kumi hivi akateremka na kuvuta hatua ndefundefu huku mikono ikiwa mfukoni na, akazipanda ngazi za hotel hiyo mpaka katika chumba chake, alipofika mlangoni akatulia kidogo akatzama mitego yake akagundua ama kuna mtu aliingia au ameingia, akachomoa bastola yake na kuishika barabara kwa mkono wake wa kulia kisha taratibu akanyonga kitasa na kuufungua mlango huo, akaingia ndani na kutazama huku na kule, akaangalia kila kona ambayo anajua kama imeguswa au la, kwa jinsi alivyokiacha chumba chake alijua tu kuna mtu aliyepekuwa kitaalamu sana kiasi kwamba kwa amtu ambaye ni wa kawaid hatoligundua hilo lakini haikuwa kwa Gwamaka.

Alipojiridhisha kuwa usalama upo akaketi kitandani na kuvua fulana aliyokuwa ameivaa. Akaliendelea dirisha ambalo alikuwa amefunga darubini yake ya jicho moja, akachungulia kuona nini kinaendelea upande wa bandari ya zamani ya Mogadishu ambako inasemekana huko ndiko maharamia wale wanakoficha nyara zao. Hakuna jipya zaidi ya kuona walinzi walewale wakivuta bangi na kuendelea kulinda maeneo yao. ‘Nchi isiyo na serikali ni shida tupu’ akajisemea wakati akitoka pale dirishani.

§§§§§

Mwanamke mwenye upara akashusha darubini yake iliyokuwa ikimwangali Gwamaka alipofika chumbani kwake, akaiacha ining’inie kifuani mwake.

“Amerudi,” Fasendy akawaambia vijana wake machachari. Wakanyanyuka mara moja, “hakikishenu mnamleta mzima, tunataka tumtoe sadaka kesho ijumaa,” akaongezea maneno hayo kisha akavuta kiti akaketi na kuwasha sigara akaipachika kinywani. Wale vijana walifanya kama walivyoagizwa, wakafika Ramada hotel na kukamata kila mtu kona yake kisha wawili kati yao wakaingia ndani na kupanda ghorofani kukifuata chumba cha Gwamaka. Hawakugonga hodi wala kuuliza, wakapiga teke mlango nao ukafunguka, wakajitoma ndani kwa ustadi ikiwa na kutanguliza mtutu wa bunduki, hakuna mtu. Wakaingia mpaka ndani na kutazama kila mahali lakini bado hawakuona mtu, uvunguni kwenye makabati kote Gwamaka hayupo. Wale jamaa wakashusha pumzi ndefu kung’uta mashuka yote inua kitanda, hakuna Gwamaka.

“Aisee, huyu mtu ameondoka hayupo hapa,” mmoja wao akasema kumwambia mwenzake, kisha wakatoa taarifa kwa redio na kutoka nje ya chumba kile.

Gwamaka aliibuka kutoka katika beseni kubwa la kuogea lililojengewa pembeni kabisa mwa bafu hilo, wakati jamaa hao walipokuwa wakipekua kumtafuta, yeye tayari alikwishajizamisha kwenye beseni hilo lililojaa maji ya sabuni ambayo haiukuwa rahisi mtu kuona kilichopo ndani yake.

Alitoka na kusimama pembeni huku nguo zake zikimwagika maji, akatulia kimya akisubiri kuona kama watu hao wamekwishatoka au la. Alipoona ukimya umetawala akampa taarifa Jamil aliyekuwa bado hajafika mahala pale.
Plaza hotel iliwekwa chini ya nuangalizi wa siri na wapiganaji maharamia wakiwahofia watu hao kutoka Afrika Mashariki, walidhamiria kuwamaliza vijana hao, kwa maana walishaona hatari itakayosababishwa nao. Waliizingira hotel ile kwa siri, wengine wakijifanya kuja kula, wengine wakifanya jambo hili au lile ilimradi tu ni kutaka kujua kama watu hao wapo au hawapo ili watekeleze azma yao.

“Usitoke ndani, jamaa inaonekana bado wapo,” Jamil alimwambia kwa simu ya upepo. Gwamaka akaendelea kutulia chumbani mwake, akisubiria asikie nini ataambiwa na Jamil ambaye alikuwa nje ya hotel hiyo.
Jamil alikuwa akiegesha gari yake nje ya hotel hiyo alipojikuta akiwekewa mtutu wa Short Machine Gun sikioni mwake.

“Sihitaji kukuuliza wala kuniuliza, shuka kwenye gari,” Jamil aliamrishwa na mtu mmoja mwenye bunduki hiyo aliyeishika madhubuti mkononi mwake, ikiwa imefungwa kwa mkanda uliomzunguka nyuma ya bega lake. Jamil hakuwa na ujanja kwani aliona wazi kuwa jamaa huyo hana masihara hata kidogo, alikuwa ni mwembamba mrefu mwenye macho mekundu, kinywani mwake alikuwa akitafuna mirungi.

Jamil akateremka kutoka katika gari lake, lakini kabla hajatoka kabisa alidondosha vikolokolo vyote alivyochukua kutoka kwa yule mateka wake aliyemuua jangwani, kisha akatoka nje.

“Weka mikono kichwani,” aliamuriwa, akafanya hivyo na kuswagwa mpaka kwenye jeep moja iliyokuwa upande wa pili wa barabara, Jamil alipokuwa akipanda kwenye hile jeep akafanya hila ambayo hawakuigundua, akabofya kitufe cha redio yake ambayo iliunganishwa kwa ndani ya shati lake juu karibu na mdomo, wakati huo alikuwa amevua zile earphone zake, hivyo moja kwa moja ikaunganisha kwa Gwamaka. Gwamaka akaanza kusikia lugha ya kisomali ikiongelewa na watu waliokuwa wakibadilishana mawazo.

“Hatari nimetekwa,” Jamil alinong’ona na sauti ile ilisafiri moja kwa moja mpaka kwa Gwamaka.

“Unaongea na nani?” akauliza mtu mmoja aliyekuwa na rifle mkononi mwake, akaiinua na kumpiga kwa kitako cha bunduki hiyo, jamili akaenda chini ndani ya bodi ndogo ya gari ile.

“Shiiit,” Gwamaka akang’aka, akachukua bastola zake mbili, na kuziweka magazine na nyingine akajaza mifukoni katika jeans, akatoka mlangoni, bila hadhari yoyote akitaka kuwahi kujua jamil anapelekwa wapi. Lilikuwa ni kosa kubwa sana alilolifanya, hakuna kingine alichokihisi zaidi ya maumivu makali kichwani mwake, kizunguzungu kikafuatia, akadondoka chini.

Mwanamke mwenya upara alisimama pembeni yake.
“Mlivyosema hayupo na huyu ni nani?” akawauliza wafuasi wake. Hakuna aliyejibu, wakamnyanyua Gwamaka na kutoka naye kupitia mlango wa nyuma, wakampakia kwenye gari yao na kuondoka naye.
 

Similar Discussions

7 Reactions
Reply
Back
Top Bottom