RIWAYA YA KUSISIMUA:- Vuta N'Kuvute - Shafi Adam Shafi

Jemima Mrembo

JF-Expert Member
Jul 19, 2021
2,791
8,005
Sura ya Kwanza
Mara tu baada ya kuvunja ungo, Yasmin aliozwa mume. Alikuwa mume
wa jamii yake ya Ithnashiria ambaye alikuwa akiishi jirani naye hapo
Mtendeni.

Alikuwa ni mume asiyelingana naye hata kidogo. Si kwa umri wala
tabia kwani wakati Yasmin ni kigoli wa miaka kukmi na tano tu, mumewe
Bwana Raza alikuwa zee la miaka hamsini na mbili. Wakati Bwana Raza
keshazeeka, Yasmin alikuwa mtoto mbichi asiyeelewa kitu chochote.
Kukubali kwake kuolewa ilikuwa ni kwa sababu ya kuwaridhi wazee
wake tu. Yeye mwenyewe hakuona fahari ya kuolewa na mzee anayeweza
kumzaa. Hakupenda kufuatana na mumewe pahala popote pale na hata ile
siku inayotokea wakaenda senema, basi yeye huwa hapendi kukaa karibu
naye.

Yasmin alikuwa na kijiuso kidogo cha mdawari mfano wa tungule
na macho makubwa ambayo kila wakati yalionekana kama yanalengwa
lengwa na machozi. Alikuwa na pua ndogo, nyembamba na chini ya pua
hiyo ilipangana midomo miwili mizuri iliyokuwa haitulii kwa tabia yake ya
kuchekacheka, huku akionyesha safu mbili za meno yake mazuri. Alikuwa
na kichaka cha nywele nyeusi zilizokoza ambazo zilianguka kwa utulivu
juu ya mabega yake. Alikuwa si mrefu lakini hakuwa mfupi wa kuchusha,
na matege aliyokuwa nayo yalizidi kuutia haiba mwendo wake wakati
anapotembea.

Yasmin hakupenda hata kidogo kuolewa na mume kama yule kwani yeye
mwenyewe angelipenda sana kupata mume kijana kama yeye mwenyewe.
Alipenda ampate mume ambaye yeyote angelimwona angelisema, “Kweli
Yasmin kapata mume.” Alikuwa anatamani kupenda lakini hakumpata wa
kumpenda. Yeye alitaka kijana wa makamu yake ambaye angelimwonyesha
pendo na yeye angelimiminia pendo lote moyoni mwake.

Kama desturi ya Wahindi wengi Afrika Mashariki Bwana Raza alikuwa
mfanyabiashara mashuhuri pale mtendeni. Alikuwa na duka kubwa la
biashara ya rejareja. Kwa kuwa duka hilo lilikuwa barabarani, basi kutwa
lilivamiwa na washitiri waliokuwa na haja mbalimbali. Mara huyu kataka
kibao cha mchele, huyu kataka fungu la tungule, huyu kataka bizari ya
nusu shilingi na kutwa Bwana Raza alikuwa na kazi ya kupigizana kelele
na washitiri wake. Tokea kuolewa kwake, Yasmin alikuwa ndiye msaidizi
mkubwa wa Bwana Raza katika kazi hiyo.

Kutokumpenda Bwana Raza pamoja na utumishi wa kutwa dukani pale
kulimfanya Yasmin ayachukie maisha ya unyumba na mumewe. Alitamani
kufa kuliko kujitolea mwili wake kwa bwana yule. Inapofika usiku yeye
huwa amejichokea na hulala mara tu baada ya kukiweka kichwa chake
juu ya mto.

Hata baada ya kulala, Yasmin alikuwa haipati ile raha ya usingizi kwani
mara kwa mara alikuwa akishituliwa na sauti nene ya kukwaruza ya
mumewe ikimwita toka ukumbini kumwuliza swali hili au lile..
“Yasmin! Leo Bi. Mashavu alileta vitumbua vingapi?” Bwana Raza
aliuliza, ameshughulika anafanya hesabu ya biashara ya siku ile. Yasmin
huwa hajali maswali hayo na huendelea na usingizi wake bukheri.

Anapokuwa hapo Bwana Raza hushughulika kweli hataki mzaha hata
kidogo na mara kwa mara Yasmin humsikia akikasirika na kugombana
peke yake. Inapokuwa hivyo huwa amekwisha pata hasara ya kitu fulani.
Malalamiko ya kupata hasara yalikuwa hayamwishi na hata siku moja
hutamsikia akisema amepata faida. Hiyo ilikuwa ni siri aliyoijua yeye
mwenyewe tu.

Anapokuwa katika kazi hiyo ya kufanya hesabu Bwana Raza huvuta biri
moja baada ya moja na moshi wa biri hizo huhanikiza harufu yake mbaya
nyumba nzima. Baada yakumaliza hesabu zake Raza hufululiza moja kwa
moja mpaka kitandani ambapo humkuta Yasmin amelala fo fo fo.
Chumba cha Bwana Raza kilikuwa kimejaa makorokocho. Mifuko ya
unga, mikungu ya ndizi, maboksi ya majani ya chai makopo ya maziwa. Kuta
za chumba hicho zilikuwa zimepambwa na picha mbili tu, moja ni picha ya
maandishi yaliyokuwa kwa nakshi ya Kiarabu majina ya Fatma, Ali, Hassan
na Hussein. Picha ya pili ilikuwa ni ya farasi aliyebeba mkono ulioonyesha
vidole vyote vitano. Mlikuwa na kiti kizuri cha msaji kilichochongwa kwa
nakshi pembeni na miguuni. Bwana Raza alinunua kiti hicho Darajani
kwenye mnada. Kwenye pembe nyingine ya chumba hicho mlikuwa na
kiti cha marimba na juu yake palikuwa na rafu iliyogongomelewa kwa
misumari ukutani. Kwenye rafu hiyo palitundikwa maguo machafu na
kwenye kijiti cha mwisho cha rafu hiyo ilining’inia tasbihi ndogo.

Chumba hicho hakikuonyesha kuwa ni pahala pa mtu kupumzika.
Palikuwa ni pahala pa kupitisha usiku tu, kuche, asubuhi ifike biashara
iendelee kama kawaida. Anapoingia chumbani humo baada ya kumaliza
shughuli zake Bwana Raza huwa hana mazungumzo tena. Ni kuvua nguo
na kujitupa kitandani. Hapo hujigaragaza na kugeuka ubavu huu na huu.

Mara hulala kifudifudi au mara hunyanyuka ghafla na kuwasha taa akitafuta
biri na kiberiti. Akisha vipata vitu hivyo huwasha biri yake na kuivuta
nusu kiasi cha kukifukiza chumba kwa moshi wa biri na halafu hujilaza
tena kitandani. Hapo tena humgeukia Yasmin na kuanza kumpapasa na
kumtomasatomasa akimwita na kumwuliza, “Yasmin ushalala?” Yasmin
huwa kalala kweli yupo mbali katika ndoto zake za kitoto. Bwana Raza
humgeuza huku na huku na kumpapasa papasa na mara mojamoja Yasmin
huzinduka na kulala tena hapo hapo.
Kama kawaida yake, ghafla Bwana Raza aliinuka na kuwasha taa.
Alichukua kiberiti na kuchomoa biri moja kutoka katika mfuko wa shati
alilotundika juu ya rafu. Aliwasha na kuanza kuikupua mikupuo mikubwa
mikubwa na kuyajaza mapafu moshi tele. Aliutoa moshi wote mara moja
kupitia puani na mdomoni na mara hii badala ya kuivuta nusu alimaliza
yote. Moshi ulijaa chumba kizima na hata ukampalia Yasmin. Alikohoa
mpaka akaamka lakini alilala tena hapo hapo na alipoweka kichwa tu
Bwana Raza alizima taa na kulala huku akimkumbatia mkewe.

“Usinikere Bwana mimi nataka kulala.”
“Mbona unalala mapema? N’do kwanza saa mbili. Amka tuzungumze,”
Bwana Raza alinguruma. Yasmin alipuuza akalala.

Bwana Raza aliamka tena akawasha taa. Alimwangalia mkewe na
kuanza kuuchunguza uzuri wake. Huo ulikuwa ndiyo wakati wa pekee
ambao Bwana Raza anapata wasaa wa kumwangalia. Bwana Raza alirudi
tena kulala baada ya kuzima taa na mara hii alimgeuza Yasmin ikawa nyuso
zao zinatazamana. Alipotaka kujigeuza, Yasmin alihisi mikwaruzo mikali
ya visiki vya ndevu za Bwana Raza, ndevu ambazo leo ya nne hakupata
nafasi ya kuzinyoa.

Alihisi mikunjo ya uso wake na alipovuta pumzi alivuta hewa iliyojaa
kupuo la moshi wa biri. Yasmin aligeuza uso wake huku na huku
kumkimbia mumewe kijanja na mara alilala tena.

Kwa Yasmin usiku haukuwa mrefu mara kulipambazuka asubuhi
ikaingia, kazi ya kuuza duka inamsubiri kama kawaida. Shughuli
anayokuwa nayo Bwana Raza usiku kucha yeye hana habari nayo, yapitayo
usiku kucha humkuta yeye katika dunia nyingine kabisa, dunia ya usingizi.
Bwana Raza hakuwa na raha ya kuwa na mke na Yasmin ya kuwa na mume.
Maisha ya watu wawili hawa yalikuwa ya bahati nasibu na hakuna mmoja
kati yao aliyekuwa na raha na hali hiyo ilimfanya Yasmin kuondokea na tabia ya unyonge akiona kama dunia imemwonea kuozeshwa mume asiye
makamo yake wala asiyemvutia hata kidogo.

Ijapokuwa Yasmin alitumia muda wake mwingi dukani, lakini alipata
muda wa kupanga ushoga na jirani yake Mwajuma. Mwajuma likuwa
ni msichana wa Kiafrika na tabia yake ya ucheshi na masihara ilimfanya
Yasmin avunje miiko ya Kihindi ya kutoingiliana na Waafrika.

Si ajabu kwa Yasmin kuvutiwa naye kwani yeye alikuwa ni kuvutio
cha mtaa. Watoto, vijana na vizee, kila mmoja alijua namna yake ya
kuzungumza naye. Pale panapojiri mzaha, furaha na busara basi yeye
anazo nyingi.

Alikuwa ni mwanamke wa makamo tu, hazidi miaka ishirini na tano
lakini umbile lake la wembamba lilimfanya aonekane yuko chini ya umri
huo. Alikuwa na kisauti kikali azungumzapo kila jirani hujua kwamba
Mwajuma yupo.

Alikuwa na uso mwembamba uliochongoka sawasawa na macho
remburembu yaliyowafanya wenzake wampe jina la utani macho ya
urojo,” kwa kuwa yalirembuka kiasi ambacho asingeweza kutofautisha
wakati amelewa na pale asipolewa. Majirani wengine wakisema eti anakula
kungumanga.

Alikuwa mrefu wa wastani na avaapo lile vazi lake alipendalo la kujifunga
kanga moja kiunoni na nyingine kujitupia mabegani, huku nywele zake
amezisuka vizuri nne kichwa, huwezi kupita ukamtazama mara moja. Kila
alipopata nafasi, Yasmin hupenya na kumtembelea Mwajuma nyumbani
kwake, na yeye alikuwa ni mtu wa pekee ambaye Yasmin alimhadithia
dhiki anayoiona kuishi na mume zee kama lile.

Hivi leo Bwana Raza amemaliza hesabu zake mapema na kuingia
chumbani. Alikaa juu ya kile kiti cha msaji na kuanza kuvuta biri zake
bila ya kuzungumza na Yasmin ambaye alikuwa bado yu ngali macho.
Alikuwa amejilaza chali kitandani akiangalia boriti za chumba kile kama
kwamba anazihesabu. Alikuwa mbali katika mawazo akifikiri vipi ataweza
kumwepuka mzee yule, lakini kila alipofikiri hakuweza kupata kisingizio
chochote cha kumkataa mumewe.
Bwana Raza akiwa na kipande cha biri mdomoni alianza kusema, “Siku
hizi biashara hakuna. Kila nikifanya hesabu naona hasara tupu. Yule tajiri
wangu wa Kibaniani amekataa kunikopesha vitu kwa sababu sikumlipa
pesa za vitu nilivyochukua mwezi uliopita. Madeni yamenizunguka sijui nitafanya nini.” Yasmin alimtazama macho tu hakuwa na la kumjibu kwani
mambo ya biashara hayakuwa kichwani mwake aslan.

“Mimi siwezi kuendelea na biashara namna hii, lazima nikatafute
pahala pengine nifungue duka,” Bwana Raza aliendelea kulalamika
huku kipande chake cha biri amekikamata mkononi kwa ncha za vidole.

Yasmin aliyapuuza yote yale akageuza ubavu upande wa pili, mara usingizi
ukamchukua. Alipozinduka asubuhi ilikuwa ishaingia, Bwana Raza
kashughulika anafungua duka.

Haikupita mwezi Raza alimwandikia Mamdali, mjomba wake anayeishi
Mombasa na kumweleza matatizo yake ya kibiashara. Mamdali ni mtu wa
Unguja aliyekwenda huko Mombasa zamani. Alikuwa mtu mashuhuri
huko na kwa ajili ya utu uzima wake alikuwa na madaraka makubwa katika
jumuiya ya Ithnashiria Mombasa. Yeye ana duka la fahari hapo Salim Road
na wafanyabiashara wengi walimjua mzee huyo. Alikuwa na itibari kubwa
na kwake yeye haikuwa vigumu kupata mkopo wa hata shilingi laki moja
kutoka kwa tajiri yeyote yule.

Mara tu baada ya kupata barua ya Raza, Mamdari alimjibu na kumshauri
ahamie Mombasa akaanzishe biashara ya mboga mboga ambayo inatija
kubwa huko.

Yasmin na mumewe walikuwa wamekaa ukumbini wanakula chakula
cha mchana. Bwana Raza alikuwa anawaza atayaanzaje mazungumzo
ya kuhamia Mombasa. Waliendelea kula kwa muda kidogo bila ya
kusemezana halafu Bwana Raza alianza, “Mke wangu mimi naona bora
tuhame Unguja,”
Yasmin alipigwa na mshangao hakujua yameanzaje hata yakaja ya
kuhama Unguja. “Kwa nini?” aliuliza.
“Ala! Si nimekwambia kwamba biashara siku hizi haziendi vizuri.”
“Tuhame Unguja twende wapi?”
“Mombasa.”
“Tukafanye nini?”
“Kwani sikukwambia?”
“Kitu gani?”
“Kwamba mjomba amenijibu ile barua yangu.”
“Aa, mimi hukuniambia.”
“Ala! Basi labda nimesahau, mjomba amenijibu ile barua niliyompelekea
na amenishauri kuhamia Mombasa nikafanye biashara ya mboga.”
Yasmin aliinama chini akiwa na kipande cha chapatti mkononi.

“Unasemaje?” Bwana Raza aliuliza, akiwa na hamu ya kutaka kujua
mkewe atasema nini. “Ah! Haya maisha tunaoishi mimi na wewe, mimi
yashanitumbukia nyongo. Mimi nahisi bora unipeleke kwetu wakati
utakapokwenda Mombasa,” Yasmin alijibu kwa sauti ya hofu huku bado
kipande cha chapati amekikamata mkononi.

Yasmin alikuwa akimwogopa sana mumewe kwa sababu ya mafahamiano
mazuri yaliyokuwepo baina ya Raza na wazee wa Yasmin. Alihisi kumkera
mumewe ni sawa na kuwakera wazee wake, ingawa Yasmin hakupenda
kabisa kuishi na Bwana Raza. Yeye alitamani amwache lakini hakuthubutu
kumtamkia maneno hayo. Alimwomba mumewe amrejeshe nyumbani
lakini alikataa kata kata.

Bwana Raza alianza kuandaa safari mpaka ikanoga. Pasipoti yake na ya
mkewe zilikuwa tayari na lililobaki ilikuwa ni kumwariifu Yasmini siku
ya safari tu. Alisubiri wakati unaofaa kumpa habari hiyo na hapakuwa na
wakati mwingine wowote isipokuwa usiku.

Raza alikuwa keshavuta biri zake zimemtosha wamelaa yeye na mkewe.
“Yasmin,” Bwana Raza aliita taratibu.
“Unasemaje Bwana?”
“Safari imeiva, tutaondoka kesho kutwa, safari itatuchukua siku nne
kwa meli. Tutapitia Pemba na Tanga.”
“Sasa kwani vipi yale maneno niliyokwambia n’do hukuyatia maanani?”
“Maneno gani hayo?”
“Nilikwambia unipeleke nyumbani na wewe utanguliye mimi
nitakufuata baadaye.”
“Wacha maneno yako, tutafuatana mimi na wewe!” Bwana Raza alisema,
tena sasa kwa hamaki. Yasmin hakuthubutu kujibizana na mumewe kwani
hii haikuwa desturi yake. Alinyamaza kimya. Haikupita muda, kama
kawaida yake usingizi ulimchukua.
Siku ya pili duka la Bwana Raza halikufunguliwa na majirani walikuwa
washapata minong’ono kwamba bwana Raza na mkewe wanahama. Siku
hiyo kutwa Bwana Raza na mkewe walikuwa kazini wakifunga funga.
Yalifungwa makapu makubwa makubwa na siku hiyo biri zilikuwa
zinavutwa mfululizo, moja baada ya nyengine. Kazi ya kufunga ilimalizika
saa moja usiku. Yasmin aliona bora amwombe ruhusa mumewe ili apate
kwenda kumuaga mama yake hapo Kiponda. Ruhusa ilipatikana na Yasmin
alioga na kubadili nguo haraka na muda si muda alianza safari yake.

Kiasi cha saa mbili usiku alimkuta mama yake amekaa juu ya kochi
ukumbini. Kabla hakuwahi kumsalimu, Zenabhai alianza kumvurumishia
mwanawe maneno kwa, Kiswahili chake kibovu kilichosababishwa na
kujitenga kwake na Waswahili kwa muda mrefu.
“Mbona umekujisha saa hizi peke yako?”
“Nimekuja kukuaga ma.”
“Unakwendesha cha wapi?”
“Kwani Bwana Raza hakukwambia ma.”
“Kunambilisha nini?”
“Sisi tunakwenda Mombasa kufungua duka.”
“Raza hakukujisha hapa mezi nzima sasa mimi nafikirisha yeye iko
gonjwa.”
“Ah! Yeye mzima lakini kazi nyingi.”
Yasmin hakukaa muda mkubwa kwa mama yake na baada ya
kuzungumza kwa muda mfupi aliondoka kwa safari ya kurejea kwake.
Alipokuwa njiani Yasmin aliwaza kwamba haitakuwa jambo la busara
kuondoka bila ya kumuaga hata mtu mmoja mtaani, kwa hivyo kabla ya
kufika kwake alipitia kwa shoga yake Mwajuma.

Ngo, ngo, ngo, aligonga mlango. “Hodi, hodi wenyewe mmo humu
ndani?”
“Nani mwenzangu?” Sauti kali iliuliza kutoka ndani.
“Mimi,” Yasmin alijibu.
Mara Mwajuma alifungua mlango akiwa na taa ya kandili mkononi.
“Oh! Yasmin, mbona saa hizi? Kwema?”
“Hakuna lililozidi shoga yangu, ila nimekuja kukuaga tu.”
“Umekuja kuniaga, pita ndani basi.”
“Ah! Nna haraka, siwezi kupita ndani manake sikumwambia mume
wangu kama nitapitia kwako, yeye anajua kwamba nimekwenda
Kiponda kwa mama tu basi nikichelewa yatakuwa mengine kwani kama
unavyoyajua, baba lenyewe lina wivu kama nini sijui.”
“Haifai hivyo, hebu pita ndani angalau dakika mbili,” Mwajuma
alisisitiza.

“Ah! Babu we, unayajua maneno ya mume wangu tena akianza kusema
hamalizi.”
“Ah, shoga yangu we, hayo yasikushughulishe, hiyo ndiyo desturi ya
wanaume wazee wanaoowa wanawake watoto wadogo, basi maneno yake
usiyajali.

“Basi n’takaa kidogo.”
Mwajuma alimkaribisha Yasmin ukumbini. Aliipandisha utambi taa
aliyokuwa nayo mkononi ili wapate kuonana vizuri. Alimwomba akae
juu ya bao lililokuwepo ukumbini pale na yeye mwenyewe alivuta mkeka
pembeni na kukaa.
‘Ehee! Hebu nieleze za wapi tena?” Mwajuma aliuliza akitabasamu, sauti
ameishusha chini.

‘Nasafiri mimi na mume wangu, tunakwenda Mombasa.”
“Tena babu maneno hayo niliyasikia yakizungumzwa mtaani lakini
mimi sikuamini hata kidogo.”
“He! Ama kweli duniani hakuna siri, hivyo majirani washayajua?”
Yasmin aliuliza, amepigwa na mshangao.

Mwajuma aliondoka pale alipokuwa amekaa juu ya meka akakaa
juu ya bao yeye na Yasmin. Alimsogelea karibu na kumwuliza kwa
kumnong’oneza. “Ati nasikia hutaki kumfuata?”
“Ah! Mwajuma we, hata la kukwambia sina, lakini funika kombe…”
Yasmin alipoinua mkono na kuangalia saa yake alistuka, “Lo! Saa nne
kasorobo! Mtume! Si maneno hayo nikifika nyumbani, kwa heri, inshalla
tutaonana tukijaaliwa.”
“Haya kwa heri shoga, hata mimi nna safari. Hivi unavyoniona nilikuwa
nakwenda kuoga, leo kuna dansa la kukata na shoka hapo Mpirani wapigaji
wanatoka Dar.”

“Basi kama hatukuonana n’do kwa heri,” Yasmin aliaga kwa sauti ya
unyonge.
“Ahsante shoga kwa kuja kuniaga, usinisahau kwa barua ukifika
Mombasa.”
Yasmin aliondoka kwa haraka kuelekea kwake, wasiwasi umemjaa.
Baada ya kukata vichochoro viwili vitatu alijikuta ameshafika. Alifungua
mlango taratibu, alipoingia ukumbini alimkuta Bwana Raza amekaa juu
ya kiti amevimba kama kiboko.
“Mbona umekawia?” Raza aliuliza kwa kelele, amehamaki, moshi wa
biri aliyokuwa akiivuta unatokea puani na mdomoni wakati huo huo.
“Mazungumzo ya mama yalikuwa marefu na mimi ilibidi nikae
nimsikilize tu. Unajua tena akianza kusema.”

Raza alipumua kwa nguvu kama mtu aliyetuliwa mzigo mzito, “haya
basi saa zishakuwa nyingi twende zetu tukalale.”

Siku ya safari ilipofika, waliamshwa alfajiri na sauti kali ya muadhini wa
Jamatini iliyokuzwa kwa kipaza sauti kilichoifanya isikike waziwazi mpaka
Mtendeni na sehemu zote zilizopo kando kando ya mtaa huo. Yasmin
aliandaa vipochopocho vilivyotayarishwa tokea jana usiku. Walikula na
walipomaliza walianza kuvalia. Walipomaliza kuvalia walionekana kama
n’do kwanza wanatoka kuoana kasoro ujana wa Bwana Raza. Hapo Raza
alianza kumtania Yasmin, “Nilikwambia tutasafiri kwa meli lakini nilikuwa
nikikudanganya tu, tunasafiri kwa ndege. Ushawahi kupanda ndege wewe?”

Raza aliuliza, akitabasamu na kuonyesha mikunjano iliyomjaa usoni.
Yasmin hakumjibu kitu ila na yeye alibakia kutabasamu tu utasema
kwamba anaifurahia kweli safari ile. Ilipofika saa nne na nusu za asubuhi
wote walikuwa wameshughulika pamoja na wasafiri wengine ndani ya
kiwanja cha ndege cha Zanzibar. Baada ya hekaheka ya kujadiliana na
watumishi wa Idara ya Uhamiaji na askari wa forodha, waliingia ndani
ya ndege. Muda si muda walikuwa wanaelea ndani ya hewa ya Unguja
iliyokuwa ikipepea moja kwa moja kutoka baharini, wakiacha chini yao
ufukwe uliotambaa na kukizunguka kisiwa kile huku ukiwa umepambika
kwa minazi iliyokuwa ikiyumba kwa maringo hewani. Walikaa bega
kwa bega ndani ya ndege na Bwana Raza alimpisha Yasmini upande wa
dirishani ili apate kumwonyesha maajabu ya kusafiri kwa ndege.
Ijapokuwa Yasmin alipendezewa sana na mandhari aliyokuwa akiyaacha
chini yake, lakini mara kwa mara starehe aliyokuwa akiipata kwa kuangalia
mandhari yale ilikuwa ikiharibiwa na jiso la Bwana Raza lililokuwa
likimsogelea ama kumwambia kitu au kumwonyesha kitu. Walipaa juu
kwa juu na baada ya safari ndefu walisikia sauti ya muhudumu wa ndani
ya ndege akiwaarifu kwamba wanakaribia kutua. Walianza kuukabili
ufukwe wa bahari ya Mombasa na baada ya muda kidogo walitua kiwanja
cha ndege cha Mombasa. Jinsi Mamdali alivyokuwa maarufu Mombasa,
aliingia mpaka ndani ya jengo la kiwanja sehemu ambayo raia wengine
hawaruhusiwi. Aliwapokea Yasmin na Bwana Raza kwa furaha na heshima
na msisimko wa furaha ile ulifikia kiwango cha kulizana. Vauxhall kipya
lilikuwa nje likiwasubiri na baada ya safari fupi waliingia ndani ya jiji la
Mombasa.

Walipofika nyumbani kwa Mamdali waliikuta nyumba imeshatayarishwa
kwa wageni, kila kitu kimepangwa vizuri ndani ya ukumbi wa nyumba ile
uliokuwa umejaa kila aina ya mapambo ya nyumbani. Nyimbo za Kihindi
zilikuwa zikibembeleza kutoka kwenye radiogram kubwa lililokuwepo kwenye pembe moja ya ukuta wa ukumbi ule na vijukuu vya Mamdali
viliingia na kutoka vikiwa vimeshikwa na umbea wa kuwaona wageni.
Wiki moja tu baada ya kufika Mombasa Bwana Raza alitengenezewa kila
kitu na Mamdali. Lilifunguliwa duka kubwa la biashara ya mboga. Ilikuwa
hapana mboga utakayoitaka dukani hapo ukaikosa. Mchicha, kabichi,
karoti, koliflawa, njegere, kisamvu na aina ya mboga kadha wa kadha.
Bwana Raza alikodi nyumba nzuri na kuipamba kwa mapambo ya kila
aina hata ikakurubia ile ya Mamdali na mara hii chumba chake kilipambwa
vizuri tofauti kabisa na kile chumba cha nyumba yake ya Mtendeni
kilichokuwa kimejaa kila aina ya makorokocho.

Nyumba yake ilikuwa katika ghorofa ya pili ya jingo kubwa la roshani
tatu. Dirisha la upande wa mashariki ya ukumbi wa nyumba lilitazama njia
ya Kilindini jinsi ilivyonyooka moja kwa moja kuelekea bandarini na lile la
upande wa magharibi lilitazamana na dirisha la nyumba ya jirani. Nyumba
za mitaa ule zilikuwa za kizamani zilizoshikana moja baada ya nyengine, na
zile za uapnde mmoja zilitenganishwa na za upande mwengine na barabara
nyembamba za lami zilizouzongazonga mtaa ule. Kuta nene za udongo,
chokaa na mawe zilipunguza joto ndani ya nyumba zile, kwani ifikapo
mchana na, jua linapowaka mji wa Mombasa nao huwaka ukawa joto
mtindo mmoja, lakini “Mombasa kongwe” ilikuwa na afadhali.
Mtaani hapo ndipo Bwana Raza alipoanzia maisha yake mjini Mombasa,
mchana yuko sokoni jioni yuko nyumbani. Lakini tofauti na alipokuwa
Unguja ambako mkewe alikuwa humsaidia katika biashara ya kuchuuza
pilipili na bizari, biashara ya kuuza mboga sokoni Mombasa ilikuwa ni kazi
ya peke yake, na Yasmini akawa ni wa kubaki nyumbani tu.

Kwa kuwa Mombasa kongwe haukuwa mtaa wenye maduka, wakati
wa mchana ulikuwa shwari na walio majumbani kila mmoja huwa
kashughulika na lake.
Kazi ya kumsaidia Bwana Raza ingawaje ilikuwa ikimchosha lakini
ilikuwa ikimchangamsha, lakini leo wiki ya pili Yasmin anajihisi amepwaya
ndani ya nyumba amezongwa na upweke kila pembe, hana wa kuzungumza
naye. Kutwa kuchungulia madirishani. Tumbuizo pekee alilokuwa nalo
zilikuwa nyimbo za Kihindi alizosikiliza kutoka katika radiogram kubwa
lililosambaa kwenye pembe ya ukumbi.
Lakini Yasmin hakutoshelezwa na kukaa akisikiliza waimbaji wakighani
na kutetea, bali mara mojamoja husimama katikati ya ukumbi akacheza.

Huuyumbisha mwili wake, akatikisa matiti na kurembusha macho yake.

Mikono huinyanyua na kuishusha, akijibenua na kujinyonganyonga mithili
ya mkunga aogeleavyo kupitia mapangoni. Alijifananisha na mchezaji
nachi stadi wa filamu yoyote ile ya Kihindi. Siku zote afanyapo vituko
hivyo hudhani yu pekee, yuko mbali na macho ya kiumbe chochote kile
ambayo labda yangemtazama akatahayari. Ni macho ya Bwana Raza
tu ambayo hayamtahayarishi na siku ambayo Yasmin hufurahi, Bwana
Raza huwa ndiye mtazamaji pekee wa tumbuizo kama hilo. Akimchezea,
akijipakatisha mapajani na kumbusu mashavuni na hapo ndipo Bwana
Raza anapohisi maisha Mombasa yamenoga, biashara inamwendea vizuri
Yasmin anamchangamkia hana wasiwasi.

Jumapili ile kulikuwa kumepambazuka vizuri mbinguni kukiwa na wingu
kubwa lililojitandaza likawa kama mwavuli uliofunika mji wa Mombasa
usichomwe na jua. Bwana Raza alitoka mapema kukimbilia sokoni kwani
siku ile ya wiki ndiyo Wazungu na wale wanaojiweza wanapofanya
manunuzi ya mahitaji yao ya wiki nzima. Tofauti na makabwera ambao
kwao Jumapili ni siku ya kupumzika na wengine kulala mpaka saa nne
wakiyabembeleza maruirui ya pombe ya jana, kwa wafanyabiashara wa
sokoni, Jumapili ndiyo siku ya kazi hasa. Siku ya kuchuma fedha.

Yasmin naye aliamka na furaha iliyokuwa ikiendela tokea jana
walipokwenda senema na kutembea tembea madukani. Waliporudi
walikuwa na furaha. Furaha ile iliendelezwa kwa kila namna ambayo
mume na mke hufurahishana ndani ya nyumba.

Baada ya kunywa chai alijihisi nyumba imemwelemea amezungukwa
tena na upweke, akaanza kuufukuza upweke ule kwa kusikiliza muziki.
Akajiwa na shauku ya kucheza, akasimama katikati ya ukumbi akaaza
kujipinda na kujipindua. Hakuwa na habari kwamba siku zote anapokuwa
mchezoni kuna mshabiki ashki wa mchezo wake, anayemwangalia
bila ya yeye mwenyewe kujua. Ile ilipomalizika, leo yule ashki aliamua
kumpongeza, akampigia makofi na kumwambia, “Shabash.”
Alipogeuka kuangalia dirishani, dirisha la nyumba iliyotazamana na
ya kwao, akamgundua msungo aliyekuwa akichungulia unyago aliokuwa
akiucheza. Walitazamana lakini Yasmin hakuweza kuvumilia mtazamo wa
kijana yule aliyekuwa na macho makali kama kurunzi. Alisindika dirisha,
ikawa ndiyo mwisho wa mchezo kwa siku ile.

Hakutahayari kama alivyokuwa akifikiri ila aliona fahari kuwa ngoma
yake imepata mtazamaji zaidi ya bwana Raza kwani hata mwenyewe baadhi
ya wakati alikuwa hujiuliza, “Ngoma gani hii isiyokuwa na mtazamaji?

Hata ngoma ya giningi huwa na watazamaji!” Na kuanzia siku hiyo ikawa
ni desturi, Bwana Raza akishatoka kwenda kuchuuza mboga, ukumbi
wa nyumba yake huwa uwanja wa mchezo wa nachi, mchezaji Yasmin
mtazamaji jirani yake. Alikuwa kijana barobaro mwenye umbo la wastani.
Alikuwa na macho makali ya rangi ya hudhurungi na nywele ndefu za
mseto wa kipilipili na singa. Chini ya pua yake yalitambaa masharubu
machanga yaliyodhihirisha kwamba n’do kwanza anaingia katika baleghi.
Nyusi zake zilizokoza weusi zilianzia kutoka katika pembe zote mbili za uso
zikaja zikakutana chini ya kipaji. Alikuwa ametulia dirishani akimtazama
mwanamke yule jinsi anavyojibahashua mbele yake.
Kichwa cha santuri kilikuwa kinateleza juu ya njia za mwisho za sahani,
mwimbaji anahitimisha nyimbo yake na ilipomalizika Yasmini alitulia
akamtazama yule kijana, naye akamwuliza, “Nani kakufundisha?”
“Mwenyewe,” alijibu, akitikisa kichwa kuzirudisha nywele zake nyuma.
“Unaweza kuwa mchezaji mzuri wa chakacha, ushawahi kuiona ngoma
hiyo?”
“Bado.”
“Unataka kuiona?”
“Ndiyo.”
“Jumamosi Ali Mkali atapiga Sarigoi, utakwenda?”

Yasmin akaegemea juu ya kizingiti cha dirisha wakakabiliana uso kwa
uso anafikiri la kumjibu. Sasa hakuona haya tena ila ameingiwa na hamu
ya kutaka kujua zaidi juu ya ngoma ya chakacha, ngoma ambayo sifa zake
amezisikia siku nyingi na nyimbo zake nyingi amekwisha zisikia na nyengine
kuzihifadhi. Kuna nyimbo kama “kijembe,” “mgomba”, “usiniseme,” na
nyingi nyengine ambazo haipiti siku mbili bila ya kuzisikia mara mbili
au tatu redioni, naye anazipenda. Aliinama akainuka, akamtazama yule
kijana. “Nitakujibu,” alimwambia.
Azue uwongo gani kwa mumewe ili ampe ruhusa ya kutoka usiku wa
Jumamosi. Bado yungali mgeni mjini Mombasa, si jirani wala muhisani,
si mjomba wala shangazi, hana wa kumzulia angalau akapata kisingizio
cha kuomba ruhusa.

Kijana yule amempa mtihani mkubwa, wala hakumwona siku ya pili na
ya tatu. Aliendelea na mtindo wake uleule wa kucheza ukumbini lakini kila
alipoangalia dirisha la jirani aliona patupu, dirisha limefungwa. Alizidisha
sauti ya radiogram angalau kama jiraniye yuko mbali asikie ishara kwamba
ngoma imeanza, lakini wapi! Siku ya nne, wiki.

Sasa Yasmin alihisi zaidi ya kukosa mtazamaji wa ngoma aichezayo kuna
kitu kingine akikosacho. Anamkosa jirani, kijana kama yeye. Alikuwa kama
aliyekuwa kizani akaona nuru ya kumpa matumaini lakini ghafla nuru ile
ikafifia. Mawazo ya chakacha yakayeyuka kichwani mwake na zile nyimbo
alizokuwa akizisikiliza zikawa siyo za kusikiliza huku akicheza bali za
kumletea athari ya kumfikiri mtu aliye mbali naye. Jumamosi ikapeperuka
kama kishada kilichokatika arijojo bila ya Yasmini ikukumbuka kwamba
ile ilikuwa ndiyo siku aliyotaka kuipangia uongo ili aruhusiwe kutoka
akamsikilize Ali Mkali.

Sasa alibaini kwamba kumbe hamu yake haikuwa chakacha bali yule
kijana ambaye alihisi labda atampunguzia unyonge kwa ile kuwa karibu
na kijana wa rika lake, angalau akapata ile raha ya kuwa karibu nae
wakaongea, wakacheka, wakafurahi. Kutoweka kwa kijana yule kukawa
kama wimbi lililoipiga nyumba ya Bwana Raza likafagia furaha changa
iliyoanza kuchipua ndani ya nyumba ile. Mpaka Bwana Raza mwenyewe
alihisi kwamba ule uchangamfu aliokuwa nao mkewe wakati wapya ndani
ya nyumba sasa umeanza kufifia, akashindwa kuvumilia kamwuliza,”
Mbona siku hizi nakuona hivyo?”
“Vipi?”
“Si hivyo ulivyo!”
“Niko vipi?”
“Naona siku hizi…”
Kabla hata Bwana Raza hakumaliza Yasmin aliyachupia maneno, “Siku
hizi unaona nini?”
“Naona siku hizi huchangamki, hata nachi huchezi tena.”
“Kwani umenioa niwe nikikuchezea nachi? Kama unataka kuchezewa
nachi si wende senema! Una nini mtu mzima wewe?”
Ulikuwa usiku wa kawaida tu, Bwana Raza keshakoga amejifunga
kanga kiunoni amekaa kitini mguu wake wa kulia ameutundika juu ya wa
kushoto anautikisa tikisa, sigara senti iko mkononi imemkolea anaikupua
mikupou mikubwa mikubwa.
Ilikuwa karibu imdondoke lakini aliibana vizuri kwa kidole chake cha
shahada na kile cha katikati. Amekaa kinywa wazi kama aliyepigwa kofi la
ghafla, ameuachilia moshi wa sigareti ukijizongoazongoa taratibu kutoka
kinywani mwake ukatanda pale ukumbini. “Unasemaje?” aliuliza, moshi
bado ukimtoka kinywani.

“Kwani hukusikia?” naye Yasmin aliuliza, amekaa kwa maringo juu ya
kiti, ameshika tama akimtazama Raza bila ya wasiwasi, pua ameikunja,
mdomo ameufidua, jeuri ya kitoto inamwenda ndani ya damu yake.
Bwana Raza akaona sasa maji yamezidi unga, hajui la kulifanya, Yasmin
amechachamaa, amekuja juu kama mtoto wa kifuu lakini naye akajikaza
ikambidi aonyeshe urijali wake. ‘Siku hizi umekuwa huna adabu!”
“Zinauzwa wapi? Hebu kanionyeshe nikazinunue.”

Bila ya kujua anafanya nini, Bwana Raza aliinuka akakitupa kile kipande
cha sigareti alichokuwa nacho mkononi kikiungua tu bila ya kuvutwa,
akamkamata Yasmin mkono akamnyanyua.
“Niwache au nitapiga kelele kama unataka kuniua mpaka majirani wote
watoke madirishani.”
“Wewe! Nimekuchukua kwenu hohehahe! Huna mbele wala nyuma
unanuka umaskini leo umekuwa jeuri enh?”
“Nani? Mimi? Unani…”
Kabla hakumaliza aliyotaka kuyasema Yasmin alitandikwa kofi kubwa;
vimurimuri kila rangi vikawa vinameremeta mbele ya macho yake. Nuru
iliyojaa ukumbini pale ikatoweka mbele ya macho yake pakawa kiza kitupu.
“Unani…” Hajawahi kumaliza akachapwa kofi la pili. Yasmin alianguka juu
ya kochi kama mzigo anatweta kama mgonjwa wa pumu.

Bwana Raza akili hana kichaa hana, midomo inamtetemeka, maneno
yamemkwama hayatoki kinywani. Alitaka kumnyanyua Yasmin pale
alipoangukia lakini Yasmin alichomoka ghafla akakimbilia mlangoni
akaufungua. Mbio.

Bwana Raza naye akamwandama, naye mbio nyuma yake akimlaani
na kumtukana, ngazi akishuka mbili mbili, lakini kabla ya kufika ghorofa
ya kwanza kanga aliyojifunga kiunoni ilifunguka ikamvuka akawa uchi
kama alivyozaliwa. Sasa ikawa kashfa imezaa kashfa, akaona amwachilie
mbali “mwana kharam yule.” Yasmin akapotea ndani ya jiji la Mombasa.
Alipotoka nje hakujua amepotelea wapi akabaki kuizunguka nyumba
akiwa tumbo wazi, na kanga tu kiunoni. Angelitokea askari bila ya shaka
yoyote angelimkamata kwa kumtuhumu mwizi. Siku ile ilipita. Ya pili
ikayoyoma na zifuatazo zikapukutika moja baada ya nyengine, hakumtia
Yasmin machoni ng’o akabaki kuumwa ndani kwa ndani.
 
Sura ya Pili

Yasmin alifika Unguja kwa meli kiasi cha saa kumi na mbili na nusu za
magharibi, jua lilikuwa linapotea upande wa magharibi na mbingu zilikuwa
zimepambika kwa mawingu ya rangi ya dhahabu yaliyochanganyikana
na rangi ya zambarau. Abiria wote walikuwa washateremka melini na
kila mmoja alikwenda alikokwenda isipokuwa Yasmin ambaye alibakia
nje ya mlango wa kuelekea gatini, amesimama, amepigwa na bumbuwazi
hana zaidi isipokuwa kikapu alichokuwa nacho mkononi. Wachukuzi
namba walimzonga kama nzi wanapouzongea mzoga, kila mmoja katika
wachukuzi wale akitaka kujua mizigo ya Yasmin ilipo ili akamchukulie.
Yasmin hakushughulika na yeyote katika wachukuzi wale ila aliwaona
kama wendawazimu tu. Mawazo yake yalikuwa mbali na pale kilipo
kiwiliwili chake na alikuwa akiwaza na kujiuliza, “Nende wapi saa hizi?”
Alijiuliza na kujishauri moyoni mwake, “Nende kwa mama? Nikenda kwa
mama atanitukana asinibakishe. Nende kwa mjomba? Ah! Nikenda kwa
mjomba anaweza kunifukuza kwa kashfa ikawa aibu mtaa mzima.”
Yasmin alijiuliza masuali kem-kem lakini jawabu linalofaa hakuligundua
ng’o. Alianza safari yake ya kutokea bandarini kidogo kidogo akiwa na
kikapu chake mkononi lakini wapi alikokuwa akienda hata yeye mwenyewe
hakujua. Madereva wa teksi walizirambaza gari zao chini ya miguu yake
lakini kwa wakati ule rasilimali yote ya Yasmin ilikuwa shilingi tano na
kupanda teksi ilikuwa ni hasara asiyoweza kuimiliki ijapokuwa alikuwa
amechoka na njaa kali imemshika.
Alijikongoja mpaka senema ya Malindi. Alikwenda moja kwa moja
mpaka “Passing Show.” Alipinda mkono wa kulia na kutokezea kwa Amar
Waga. Hapo tena aliingia ndani ya barabara nyembamba za mtaa wa
Malindi mpaka akafika kwa Rasam na alipofika hapo alitamani kupumzika
lakini baada ya kujishauri aliona bora aendelee na safari yake. Moja kwa
moja aliendelea mpaka “Dagger Club” na baada ya hatua chache alifika
mbele ya mlango wa nyumba ya mjomba wake. Alijishauri kwanza kabla ya
kubisha hodi. Alipogonga mlango alifunguliwa na mke wa mjomba wake
ambaye kwa sauti ya mshtuko iliyochanganyikana na mshangao aliita,
“Yasmin.”
“Mjomba yupo?” aliuliza Yasmin hata bila ya kusalimu.
“Hayupo, kenda Jamatini. Mbona ghafla? Habari za Mombasa?”
“Mbaya.

Kwa nini?”
“Kwanza usiniulize maswali mengi, njaa imenishika tena nimechoka,
kama kipo chakula nigaiye kwanza nile halafu tutazungumza.”
Yasmin alikaa juu ya kiti na kukiweka kikapu chake chini. Palepale mke
wa mjomba wake aliingia jikoni na kuanza kukaangakaanga. Kinywa cha
Yasmin kilivuja mate kwa harufu nzuri iliyokuwa ikitokea jikoni na alihisi
kwamba baada ya muda mfupi atakula kikomo cha shibe yake.
Kabla ya karamu aliyokuwa akiandaliwa haikuwa tayari mlango
ulingongwa na alipokwenda kufungua alimkuta mjomba amemsimamia
mbele.
“Mbona upo hapa saa hizi? Umerudi lini? Mume wako yuko wapi?”
Yasmin hakujua ajibu lipi katika maswali aliyoulizwa. Alinyamaza kimya
kama mtu aliyepigwa na bumbuwazi.
“Nakuuliza mume wako yuko wapi?” aliuliza tena mjomba wa Yasmin.
“Yuko Mombasa, mimi nimerudi nimeshindwa kuishi naye.”
“Unasemaje? Umeshindwa kuishi na Raza?”
Mjomba wa Yasmin aliondoka pale mlangoni alipokuwa amesimama.
Aliingia ukumbini na kukaa juu ya kiti. “Enhe, hebu nieleze vizuri.”
Yasmin aliinamisha uso chini hofu imemjaa, “Mjomba, kusema kweli
thawabu, mimi nimeshindwa kuishi na Bwana Raza. Kwa hakika mimi
sikumpenda wala sikumtaka. Nilikubali kuolewa naye kwa kukuridhini
nyinyi wazee wangu tu.”
“Kama hukuweza kuishi na Raza basi na sisi hatuna pa kukuweka,”
mjomba wake Yasmin alisema kwa kelele. Kelele zilikuwa kubwa mpaka
majirani wakaanza kuchungulia madirishani. “Tena upesi tuondokee
mbele ya macho yetu utafute pa kwenda. Toka!” alifoka mjomba.
Yasmin alisita kidogo na kumtazama mjomba wake, matone ya machozi
yakianza kuteleza taratibu kutoka kwenye macho yake mazuri.
“Nakwambia toka! Nenda zako! Nenda kamtafute huyo unayempenda.”
“Niondoke nende wapi na hapa ndiyo kwetu?” alisema Yasmin kwa
unyonge.
“Hapa palikuwa kwenu kabla hujaolewa. Sisi tulikupa mume ili
tupungukiwe na mzigo. Sasa madhali umemkimbia mumeo, tafuta pa
kwenda.”
Yasmin mabega yalimporomoka, asijue la kufanya. Alitoka nje taratibu
na alipofika nje mjomba wake aliufunga mlango kwa nguvu huku akilaani
na kutukana. Majirani walikwishajaa madirishani wanamwangalia Yasmin akitoa na kikapu chake mkononi, amenywea kama aliyemwagiwa maji ya
baridi. Aliwaza na kujiuliza, “Nende kwa mama?” alifikiri, “Aa, nikenda
huko mambo yatakuwa mabaya zaidi.”
Aliendelea na safari yake mpaka Darajani na alipofika hapo alisita
kidogo. Alitia mkono sidiriani na kuzichomoa shilingi tano alizokuwa
amezifutika na kuzitazama, akiwaza ni chakula gani atakachoweza kupata
kwa pesa zile. Alikwenda mpaka kwa mchoma muhogo akanunua wa
shilingi mbili. Alijibanza pembeni na kuanza kuula, akiula huku akifikiri
na machozi kutaka kumtoka, zamani alikuwa akila muhogo wa kuchoma
kwa kuutamani tu, leo anaula kwa njaa. Aliula wote na kupangusa midomo.
Sasa alizidi kufikiri pa kwenda. Alihisi balaa limemfika na janga
limemwangukia hajui la kufanya. Palepale ilimjia fikra, “Bora nende kwa
Mwajuma, labda ataweza kunisaidia.” Alikwenda moja kwa moja mpaka
kwa Mwajuma. Alipofika hapo aligonga mlango na sauti ya Mwajuma
ilimjibu kumkaribisha. Mwajuma alipofungua mlango na kumwona
Yasmin alishangaa na kuuliza, “Yalikuwaje shoga yangu?”
“Ah, mambo makubwa, hata sijui nikwambie nini.”
“Karibu jikoni basi tupike.” Mwajuma alimsogezea Yasmin mbuzi na
kumkaribisha akae yeye mwenyewe akiendelea na mapishi.
“Enhe! Khabari za Mombasa?”
“Khabari shoga yangu mbaya. Maisha na Bwana Mkubwa yule
yamenishinda. Sina raha sina starehe, mwisho nimeona bora nirejee
kwetu kwa wazee wangu. Nimekwenda kwa mjomba nimetimuliwa kama
mbuzi na kwa mama naogopa kwenda manake maneno yake nayajua.”
Yasmin alisita kidogo na kupumua. “Sasa hata sijui la kulifanya usiku huu,”
aliendelea huku akikiweka kikapu chake alichokuwa amekikumbatia.
Alikihisi kizito ijapokuwa bidhaa zote zilizokuwemo ndani ya kikapu kile
ilikuwa ni kanzu moja na nguo za ndani mbili tatu alizogawiwa na jirani
yake kule Mombasa. Labda kilichozidi ni mswaki na dawa ya meno.
“Maskini shoga yangu. Sasa una shauri gani?” Mwajuma aliuliza kwa
huruma za dhati.
“Sina shauri lolote, nimekuja kwako kukusikiliza utaniambia nini.
Tafadhali nisitiri, nisitiri aibu yangu!”
Mwajuma alimtazama Yasmin akatikisa kichwa. “Basi karibu shoga,
tutajibana hapa hivyohivyo, ijapokuwa kitanda chenyewe kimoja,”
alimwambia na kumwongoza chumbani akipangusa mikono kwa kanga
aliyokuwa amejifunga kifuani.

Yasmin alikaribishwa chumbani. Baada ya kuingia ndani tu alikaa
juu ya kitanda na kupumua kwa nguvu kwa machofu aliyokuwa nayo
na wasiwasi uliokuwa umeyatawala maisha yake wakati ule. Mwajuma
alimwacha Yasmin akipumzika na haraka haraka alimaliza kupika. Baada
ya muda mfupi aliandaa wali mzuri uliokolea nazi, mchuzi wa chukuchuku
na mboga ya mtoriro kidogo. Ilikuwa ni bahati tu kuwa siku ile Mwajuma
hakuwa na nyendo za usiku, na baada ya kula tu walilala. Yasmin alilala
usingizi mzito kwa machofu aliyokuwa nayo. Labda alizindukana mara
mojamoja tu kujikuna mbu au kunguni aliyemtafuna, lakini alipokuja
kuzindukana hasa kulikuwa kushakucha. Huko jikoni alimsika Mwajuma
akihangaika kukosha vyombo alivyopikia jana usiku na huko nje alisikia
mlio wa kinu kilichokuwa kikitwangwa na watu wawili.
Haukupita muda, chai ilikuwa tayari na walipokuwa wakinywa
Mwajuma alionekana ana haraka. Baada ya kumaliza tu alilitafuta baibui
lilipo. Alivaa baibui, akasimama mbele ya kioo kirefu kiliomo chumbani
mwake. Alijipaka podari, akajiremba wanja machoni. Alizichana nywele
zake fupi ambazo leo hakuzisuka na baadaye aligeuka na kumtazama
mgeni wake. “Mimi natoka mara moja. Nafika hapo Mbuyuni kwa mshoni
wangu kusikiliza kama kanzu yangu iko tayari, nitarudi saa hivi.”
“Mimi utanikuta hapahapa ukirudi,” Yasmin alisema kwa unyonge
wenye kutia huruma.
Mwajuma alitoka na kumwacha Yasmin peke yake. Hapo tena Yasmin
alikabiliwa na kimya tu. Sauti za pekee alizoweza kuzisikia zilikuwa labda
zile za mwuza samaki au mwuza mboga wakitangaza biashara zao kwa
kelele.
Kwa Yasmin kimya kile kilikuwa cha sauti tu, kwani kichwani mwake
mlikuwa mmejaa mawazo yaliyokuwa yakisokotana na kumfanyia kelele
ambazo mtu yeyote hakuweza kuzisikia ila yeye mwenyewe. Aliondoka
juu ya kiti alichokuwa amekikalia na kulala kitandani. Kitanda kilikuwa
kimetandikwa vizuri kwa shuka ya rangi ya waridi iliyofumwa maua
katikati. Wakati akigaragara juu ya kitanda kile, aliuchukua mmoja wa
mito miwili iliyovikwa foronya rangi moja na ya lile shuka na kuukumbatia
halafu akajilaza kifudifudi. Hapo tena fikra zilianza kutembea kichwani
mwake na kuaza kujiuliza vipi ataweza kuyakabili maisha ilhali yu
peke yake na yeye bado yu ngali mtoto hata ubwabwa wa shingo bado
haukomtoka. Alijiuliza vipi ataweza kujiendesha? Mpaka lini ataishi kwa
Mwajuma, mtu aliyemjua kwa mazungumzo tu? Nini jamaa zake watasema wakisikia anaishi Uswahilini na Waafrika. Almureadi fikra namna kwa
namna zilikuwa zinaranda na kupigana vikumbo ndani ya kichwa chake.
Alipogeuka alikikabili kile kioo kirefu kilichotundikwa ukutani na kama
kioo kile kilikuwa kikimtua, aliinuka na kukisogelea. Sasa mawazo yote
aliyokuwa nayo yalipeperuka kwa muda na kuanza kujianglia kioni namna
alivyoumbika. Alijitazama na kujitazama tena, halafu akachukua kitana
kilichokuwepo juu ya meza ndogo iliyokuwemo chumbani mle akaanza
kuchana nywele zake na kuzilazia nyuma. Alijiona akizichana namna ile
hapendezi. Alizichana tena na kuzilazia pembeni. Aligeuka na kujitazama
huku na huku na alipohisi hajajifaidi bado, alifunga mlango. Alisimama
mbele ya kioo akavua kanzu na kubakia na nguo za ndani tu.
Alijishika kiunoni kwa mikono yake na kujitazama tena huku na huku.
Alijigeuza nyuma na kujiangalia lakini aliona bado hajajifaidi. Alivua sidiria
na kujiangalia matiti yake na kuyainuainua huku akiyachezea. Alijigeuza
tena mbele na nyuma na mara kwa ghafla, kama mtu aliyesituliwa,
aliondoka mbele ya kioo na kuvaa nguo zake kwa haraka. Alipomaliza
alijitupa kitandani na kulala kifudifudi na mara machozi yalianza kumtoka.
Zilimjia fikra za kwamba mtoto mzuri kama alivyo, mwenye mwili mzuri
kama ule, leo anaishi maisha ya dhiki na unyonge vipi atakosa kupendwa
na kijana mwenzake aliye mzuri kama yeye, tena aliye Mhindi. Kijana
ambaye angelifuatana naye wakatia ngosho njiani huku vijana wenzake
wakimhusudu. Alijiuliza, “Vipi?” Alifikiri labda Bwana Raza amemtia
kisirani au labda amekaa ndani sana hata vijana hawakuwahi kumjua.
Lakini kabla hakupata majibu ya maswali aliyokuwa akijiuliza, zilirudi
kichwani mwake fikra juu ya maisha yaliyomkabili. Aliendelea kufikiri
mpaka fikra zikamwisha, usingizi ukamchukua, akalala.
Hivi sasa Yasmin alikabiliwa na maisha mapya kabisa, maisha ambayo
hakupata kuishi kwani ijapokuwa alikuwa akiishi Ng’ambu, lakini alikuwa
haishi king’ambu. Alijuana na jirani zake wa Mtendeni kwa kuja kwao
dukani kwa Bwana Raza tu, zaidi hapana. Ilikuwa ni bahati nzuri tu
kujuana na Mwajuma, na hii ni labda kwa sababu tabia zao zimelingana.
Mwajuma, ijapokuwa ni mtoto wa kimaskini, alikuwa na roho nzuri ya
ajabu na roho nzuri yake ilichanganyika na ukarimu usiokuwa na mfano.
Alikuwa yuko tayari kumkirimu mtu chochote kidogo alichokuwa nacho.
Alikuwa mwingi wa huruma na siku zote alikuwa tayari kumsaidia yeyote
aliyemweleza shida zake, pindi akiwa na uwezo wa kumsaidia mtu huyo.

Kadhalika, alikuwa ni msichana asiyependa kujikera nafsi yake na
aliutumilia uhuru wake wa maisha kama alivyopenda. Alikuwa tayari
kufanya lolote lile ambalo alihisi litamletea furaha bila ya kujali wengine
watasema nini. Kila Jumamosi alikuwa hakosi densini na alikuwa mpenzi
mkubwa wa taarabu. Katika bahari ya muziki wa aina hiyo, alikuwa na
sifa kubwa katika chama chake cha “Cheusi Dawa” kwa ajili ya sauti yake
nyororo, kali wakati anapoimba. Asionyeshwe bi-harusi pahala popote
pale, utamkuta Mwajuma amekwisha fika, amejitia kizoro pamoja na
wasichana wenzake. Na hapo kwake, ingia toka ya vijana wa kike na wa
kiume ilikuwa haishi. Yeye alikuwa hajali kusemwa na majirani ikiwa kwa
wema au kwa ubaya, bali hufanya vile anavyopenda yeye mwenyewe.
Kiasi cha saa saba za mchana, Mwajuma alirejea kutoka safari yake
ya randaranda mitaani na alimkuta Yasmin bado amelala. Ijapokuwa
hakupenda kumwamsha, vishindo alivyovifanya wakati akibadili nguo
vilimwamsha.
“Nimekukatia usingizi wako?” Mwajuma aliuliza, akihisi amemkera
Yasmin.
“Ah, tokea hapo nilikuwa sina haja ya kulala, lakini usingizi umeniiba
tu, “Yasmin alisema akijinyoosha. “Je usharudi safari yako?” aliuliza.
“Nimesharudi lakini yule mshoni sikumkuta. Nitakwenda kumsikiliza
tena kesho.”
Baada ya kubadili nguo, Mwajuma aliingia jikoni na kutayarisha mlo na
alipomaliza walikula. Baada ya hapo alifanya kazi ndogondogo za kusafisha
nyumba. Kisha ndipo likaanza gumzo baina yake na Yasmin.
“Mimi nilikuwa nikikuhisi kwamba humtaki Bwana Raza,” Mwajuma
alianza akiwa na hakika kwamba Yasmin atazungumza sana.
“Ah, yule alikuwa si mume wa kumtaka mimi mwenyewe niliozeshwa
tu na wazee wangu na mimi sikuweza kuwavunja,” alisema Yasmin
akitabasamu na kuonyesha meno yake yaliyokuwa yaking’aa kama marmar.
Hapo tena liliendelea porojo baina ya Yasmin na Mwajuma kwa muda
mrefu akizungumzwa Bwana Raza. Walimuumba na kumuumbua mzee
huyo na mara mojamoja soga hilo lilistawishwa na hadithi za jiji la
Mombasa. Hapo ulizungumzwa uzuri wa jiji hilo, jia pana la Kilindini lenye
mataa mengi, maduka chungu nzima ya Mtaa wa Salim Road na harakati
zinazokuwapo katika jia hilo usiku na mchana. Vitambaa na mapambo kila
aina yaliyojaa ndani ya maduka yenye kupendeza. Na zinapoanza hadithi
hizo ndipo Yasmin anapopata uwanja wa kuzungumza.

Aliyakumbuka mengi juu ya mji wa Mombasa, lakini katika kuhadithia
kwake kote mwisho huangukia juu ya maisha yake na Bwana Raza na hapo
soga juu ya Bwana Raza huendelea. Mwajuma na Yasmin walizungumza
sana utafikiri hawakuonana kwa muda wa miaka kumi iliyopita. Ilipofika
jioni wakati bado wamo katika starehe yao ya kupiga soga, waliingia vijana
wawili. Walibisha hodi mara moja tu na hata kabla hawajawahi kujibiwa
walijitoma ndani moja kwa moja mpaka chumbani kwa Mwajuma.
“Halo shem! Habari za kushinda?” aliuliza Salum, amesimama
mlangoni mkono wake mmoja amekamata ubao wa mlango, mkono
mwingine ameutia ndani ya mfuko wa suruali ya kaki aliyoivaa. Mwenzake
amesimama karibu na pembe ya kitanda alichokalia Yasmin. Yasmin alikaa
katikati ya kitanda amekumbatia mto mikononi mwake.
“He! Leo umepata mgeni wa Kihindi?” aliuliza Salum bado yungali
amesimama mlangoni. Hakuonyesha heshima wala staha kwa mgeni yule
ambaye hakupata kumwona hata siku moja.
“Aaaaa! Wacha maneno yako njoo ukae huku.” Bila ya kuonyesha kwamba
amekasirika au kuonyesha dalili yoyote ya furaha, Mwajuma alimkaribisha
Salum kukaa juu ya kiti lakini badala ya kukaa pale alipokaribishwa
alikwenda moja kwa moja mpaka kitandani na kujipweteka karibu na
Yasmin.
Salum alimtumbulia macho Yasmin akaanza kumchungua tokea utosini
hadi dole gumba halafu akamwuliza, “Hujambo dada?”
Yasmin alijibu kama aliyelazimishwa kusema akishangazwa na viroja
vipya asivyopata kuviona. Aliondoka kwa haraka pale alipokuwa amekaa
na kusogea mpaka pembe ya kitanda. Salum hakumshughulikia tena ila
aligeuka upande wa pili na kumwangalia mgeni wake aliyemwandalia
matembezi kwa Mwajuma siku ile.
“Roger pita ukae, usiwe na wasiwasi.”
Halafu Salum alimgeukia Mwajuma na kumwambia, “Shem, huyu rafiki
yangu kutoka Dar es Salaam. Tulikutana mwaka jana nilipokwenda huko
kwa sherehe za Pasaka.”
“Karibu Roger,” Mwajuma alimkaribisha.
“Mbona mgeni wako kanikimbia?” Salum aliuliza akiingilia katikati ya
mazungumzo ya kujuliana hali kati ya Roger na Mwajuma.
“Eh! Basi wewe umeingia kama shetani moja kwa moja mpaka kitandani
na kuanza kumwangalia mtoto wa watu kama umeona ajabu gani sijui.”
 
Hii riwaya niliisoma miaka hiyo lakini sijawahi kuichoka. Shaffih Adam Shaffih ana kazi nyingine nzuri inaitwa " Haini"
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom