Riwaya ya kipelelezi: Wakala wa Siri

siri.jpg



WAKALA WA SIRI 07
Mtunzi; Robert Ng'apos Heriel
0693322300

ILIPOISHIA
Baada ya masaa matatu, Stanslaus alizinduka. Alijikuta yupo kwenye kichumba kidogo kisicho
na dirisha chenye giza. Alikumbuka mara ya mwisho alikuwa akipigana na Fernanda, sasa
akajiuliza yupo wapi, na nani aliyemleta. Kabla hajafika mbali katika kujiuliza, mlango
ukafunguliwa na Fernanda akatokea.

INAENDELEA
“ Habari yako, Stanslaus Mahige, muuaji mahiri. Unajionaje?” Fernanda alimsalimia Stanslaus huku akitabasamu kwa dharau.
“ Nimekaa na wewe zaidi ya masaa matatu ukiwa huna fahamu, kama ningeamua kukuua ningekuwa nimeshakuua, sasa hivi ungekuwa ni maiti, tena maiti iliyokosa maziko. Lakini nimekuacha hai kwa sababu ya jambo moja tuu. Hilo ndilo litakuwa dhamana yako. Usiponambia nakuhakikishia utakufa kwa uchungu mwingi sana” Fernanda alisema, kisha akamburuta Stanslaus mpaka kwenye chumba kingine kikubwa kilichokuwa na madirisha mawili. Alafu akambandua ile gundi aliyompachika mdomoni ili asiongee. Kisha akatoka akamuacha pale chumbani, kitambo kidogo alirejea akiwa na chupa ya wine na glass mbili. Akaiweka ile chupa kwenye stuli iliyokuwa pale chumbani, akamimina ile wine kwenye zile glass mbili. Kisha akaenda kumnyanyua Stanslaus na kumuegemeza kwenye ukuta.
“ Karibu Rafiki yangu, kunywa tufurahi, sisi ni marafiki kwa sasa, tusahau vita vyetu, fungua mdomo basi rafiki” Fernanda aliongea akiwa anajaribu kumnywesha Stanslaus wine. usisahau Stanslaus alikuwa amefungwa mikono na miguu.
“ Nambie nani amekutuma, unajua lolote kwenye jambo hili? Nambie rafiki muuaji usiye na huruma, nambie kisha nitakuruhusu uifyonze roho yangu itoke kwenye mwili wangu. Hautafurahi? Si ulisema wewe ni muuaji mahiri, sasa nataka unambie ukweli kisha uniue. Je hapo sitatenda haki kwako?” Fernanda aliongea akiwa anazunguka zunguka ndani ya kile chumba huku akiwa ameshika glass iliyojaa Wine.
“ Unataka nikuambie nini, mimi namtafuta Sajenti, adui wa nchi, huyo ndiye namtafuta, na sipaswi kurudi bila kuwa naye. Mimi ni muuaji mahiri, lakini leo nimenaswa na mshale laini wa mabua” Stanslaus alisema, macho yake yalikuwa yamejeruhika kwa kucha alizoshambuliwa na Fernanda wakati ule wakiwa wanapigana.
“ Mshale wa mabua! Haloo! Unamaneno sana rafiki muuaji. Haya tusipoteze muda, nambie unachojua kuhusu jambo hili” Fernanda alicheka kishambenga kisha kwa ghafla akabadilika uso wake ukawa wa mwanamke katili.

“ Kila usemalo wanalisikia, unajiingiza kwenye matatizo makubwa, ingefaa ungenambia alipo Sajenti huenda hiyo ndio ingekuwa ponapona yako” Stanslaus aliongea, maneno hayo Fernanda aliyaelewa. Akajua huenda Stanslaus amefungwa vifaa vya kurekodi sauti na wasiwasi uliongezeka pale alipohisi kuwa huenda hata muda ule kulikuwa na watu wanaomfuatilia na hawapo mbali.
“ Kelele nguruwe wewe! Utasema au husemi, eehe! Unadhani mimi natishwa na maneno yako ya kipuuzi, sasa utasema kwa mateso, wewe si hautaki kusema” Fernanda alisema huku akimshika Stanslaus sehemu nyeti. Stanslaus alipiga yowe kwa maumivu makali aliyoyasikia.
“ Nasema! Tafadhali niachie nitasema sasa, uuwhi!” Stanslaus alisema akijaribu kujitingisha mikono yake iliyofungwa na kubana mapaja ili kumzuia Fernanda asibinye nyeti zake. Maumivu ya kubinywa nyeti hayalinganishwi na maumivu yoyote yale, kubinywa nyeti ni adhabu kubwa na inayokaribia adhabu ya mwisho kwa mwanaume. Ilikuwa ni afadhali Fernanda amchinje lakini sio kumbinya makende yake.
“ Sema sasa, usifikiri nipo hapa kukuchekesha. Nambie nani kakutuma?” Fernanda alisema, akiwa kamuachia Stanslaus Nyeti zake.
“ Watu wabaya, wenye nia ovu na wasiolitakia mema taifa letu. Hao ndio wamenituma” Stanslaus alisema jasho likiwa linamtoka.
“Watu gani hao, sitaki maelezo mengi, wataje..” Fernanda alisema.
Ajabu ni kuwa kabla hajasema chochote Stanslaus alianza kulegea mwisho akapoteza maisha, Fernanda alishangazwa na hali hiyo, awali hakutaka kuamini kuwa Stanslaus amekufa, alidhani anamfanyia maigizo lakini ni kweli kabisa Stanslaus alikuwa ameaga dunia. Kilichomshangaza zaidi ni kuwa, stanslaus alianza kubadilika uso wake, macho yake yalibadilika na kuwa meusi tii. Hapo Fernanda akajua kuwa kilichomua Stanslaus kilikuwa ni sumu. Fernanda alienda kuchukua Gloves za mikononi akazivaa, kisha akarudi, ndipo akamkagua Stanslaus ili apate kujua kilichomuua ni kitu gani japo alishahisi ni sumu lakini alitaka kuhakikisha, akamgeuza kwa nyuma, looh! Alishtuka kuona chini ya kichwa karibu na shingo kwa nyuma ilikuwepo chipu ya kurekodia sauti. Akaigusa na mkono wake, alishangaa kuona kwa pembeni damu ilikuwa ikivuja kidogo kama kaupele kaliko tumbuka, aliposhika kale kaupele aligundua ndani kuna pini, hapo hapo Fernanda akaelewa ni kwa nini Stanslaus amekufa. Kilichomuua ilikuwa ni ile pini, ambayo iliwekwa makusudi nyuma ya kichwa karibu ya kisogo pamoja na ile chipu ya kurekodia. Pini ile huwekwa sumu maalumu ambayo endapo jasusi au mpelelezi akikamatwa na adui basi hujigongesha kwa nyuma kisha pini humchoma, na mara moja mtu hupoteza maisha. Basi Fernanda alihuzunika sana kwa kitendo cha Stanslaus kujiua kabla hajamwambia siri ya nani aliyemtuma na nani yupo nyuma ya uovu wote ule. Kwa upesi akamtoa stanslaus ndani ya nyumba na kumuingiza kwenye gari, nyuma ya buti. Kisha alirudi ndani, akasafisha nyumba kusudi kuondoa ushahidi wa aina yoyote ile. Ile meza ya kioo iliyopasuka kutokana na wao kupigana aliokota vipande vya vioo na kwenda kuvitupa kwenye shimo la taka lililokuwa nyuma ya mabanda ya kuku ya nyumba hiyo.
Jioni ilifika, Fernanda alitoka akiwa na gari alilobeba maiti ya Stanslaus. Alikuwa anaenda kuitupa katika mapori ya Bagamoyo. Aliendesha gari kwa uangalifu mpaka alipouacha mji wa Dar es salaam na sasa alikuwa ameingia katika mapori makubwa ya Bagamoyo. Njiani alipishana na magari machache na hii ndio sababu ya kuchagua mapori ya Bagamoyo ambayo magari yanayotumia njia hiyo kwa mida ya jioni yalikuwa ni machache ukilinganisha na Morogoro Road. Hivyo ingekuwa vigumu kushtukiwa.

Aliona barabara ya vumbi ikikata kulia akaamua kuifuata, akaangalia huku na huku kuona kama kuna gari inamfuata lakini hali ilikuwa shwari. Akaendesha umbali wa kilometa mbili kutoka Bagamoyo Road, hapo akaona sehemu nzuri ambayo ingemfaa kutupa ile maiti ya Stanslaus. Alisimamisha gari, kisha akaangalia huku na huku kwa Mbele hakuona mtu, alafu akachungulia kwa nyuma Kupitia vioo vya pembeni ya gari, pia hakuona mtu. Akashuka akiwa kavaa suruali nyeusi, raba nyeusi zenye soli nyeupe, juu akiwa kavalia blauzi ya rangi ya damu ya mzee na uso wake ukiwa nyuma ya miwani ya rangi ya hudhurungi.
Upepo mwanana ulimpuliza, tayari jua lilikuwa limezama, mwanga wa jua uliokuwepo ni ule wa buriani. Fernanda alisimama kama mlingoti kisha akatulia tuli kusikiliza kama kuna uwepo wa mtu eneo lile, hali ilikuwa shwari, eneo lilikuwa kimya ndege wakiimba nyimbo za kuiaga siku ile. Alienda kwenye buti la gari akafungua, kisha akaitoa ile maiti kwa kuivuta, ikatoka ikaanguka chini. Fernanda hakuweza kuibeba, hivyo aliiburuza kwa kuivuta mpaka nje kidogo ya barabara, kisha akaiburuza tena umbali wa mita thelasini, muda wote alikuwa kavaa Gloves mikononi. Alijua kuwa ile maiti muda mchache ujao itaonekana na uchunguzi utaanza. Baadaye alirejea ndani ya gari, akachukua kikopo kidogo kwenye mkoba wake. Akatoka nacho na kwenda kule kwenye ile maiti ya Stanslaus. Alipofika akaimwagia ile maiti kemikali iliyokuwa ndani ya kile kikopo. Kazi ya kemikali ile ni kupoteza fingerprint zilizogusa mwili wa marehemu, hivyo Fernanda hakutaka alama zake za vidole zibaki kwenye maiti ya Stanslaus ili kupoteza ushahidi kuwa yeye anahusika kwenye kifo cha Stanslaus.
Hatimaye alimaliza, na safari ya kurudi nyumbani kwake ikaanza. Akiwa njiani Fernanda alijaribu kumpigia simu Sajenti Warioba lakini namba ikawa haipatikani. Huzuni ilimkumba, simanzi ikamkumbatia. Alikumbuka mambo yote mema aliyokwisha kufanya akiwa na Sajenti. Hakuona mwanaume afananaye na Sajenti. Alimpenda Sajenti kuliko kitu chochote kile, alitamani muda wote awe naye, lakini leo alikuwa pekeyake bila kujua ni wapi Sajenti alipo. Punde si punde alikumbuka jambo muhimu lililomfanya asimamishe gari kwa ghafla. Wakati huo alikuwa keshakaribia Bunju, alipata wazo, akageuza gari kurudi Bagamoyo. Muda huu aliendesha kwa kasi kidogo akiwa kawasha taa za gari kutokana na giza lilikuwa limeingia. Ndani ya lisaa limoja na dakika chache alikuwa kaingia Bagamoyo, ilikuwa mida ya saa mbili na nusu. Bado maduka yalikuwa hayajafungwa, alienda kwenye vibanda vya kutolea pesa. Hapo akataka kutoa pesa kutoka kwenye simu yake. Alishangaa kuona kila akitaka kutoa pesa inakataa, alipewa ujumbe kuwa akaunti yake ilikuwa imefungwa hivyo afike ofisini kwa ajili ya kushughulikia jambo hilo. Akili ya Fernanda ikakosa utulivu, tayari alijiingiza kwenye mkondo wa balaa. Alijua kuwa akaunti zake zimefungwa makusudi ili asiweze kutoa pesa zitakazo msaidia kutoroka.

Lakini hiyo isingeweza mzuia hata kidogo, Fernanda alikuwa jasusi mbobezi wa kimataifa, tayari ameshafanya kazi nchi nyingi hivyo anauzoefu wa matata na hekaheka za namna ile. Alisonya, kisha akatoa zile laini na kuzivunja vunja, alitoa simu nyingine ambayo aliisajili kwa majina NADIA BANDA. Alijua ni muhimu kuwa na laini za simu tofauti tofauti na majina yasiyofanana ili ikitokea siku ya matatizo aweze kujinasua. Alijua ni rahisi kudhibitiwa ikiwa utakuwa na laini za simu zenye jina moja tuu, lakini ukiwa na laini zenye majina tofauti sio rahisi kudhibitiwa. Hivyo kwenye laini ya kawaida aliweka pesa lakini hakuweka pesa nyingi tofauti na laini aliyojisajilia kwa majina mengine asiyotambulika nayo.
Alitoa milioni moja na nusu kisha akaziweka kwenye mkoba, huyo akatoka na kuingia ndani ya gari lake. Akiwa njiani kutafuta Lodge ya kupumzika alitupa zile simu zilizokuwa na laini zenye majina ya Fernanda kwa kuhofia kuwa wapo watu wanamfuatilia, Moja kwa moja alichukua chumba kwenye moja ya Lodge nzuri zilizokuwa pale Bagamoyo. Aliandikisha jina Nadia Banda kisha akapewa chumba.

Aliingia kuoga alafu akatoka akakaa kitandani akazikausha nywele zake ndefu za kibrazil. Baadaye akapumzika. Akili yake ilimrejesha asubuhi alipovamiwa na jitu jeusi, ndilo Stanslaus. Kisha akakumbuka habari za Sajenti Warioba, alikumbuka penzi zito alilopewa na Sajenti mwezi mmoja uliopita. Alitamani raha zile. Alijikuta akitabasamu, alafu akasema; Nakupenda sana Otieno.
Usingizi ulimpitia akalala.

ITAENDELEA

Usisahua ku-like na kushare.

Jipatie Riwaya ya MLIO WA RISASI HARUSINI" Ambayo ipo sokoni. Hutojutia.

Kitabu Tsh 15,000


0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel.

0758216209
M-PESA
Robert Heriel
 
WAKALA WA SIRI 08
Mtunzi; Robert Ng'apos Heriel
0693322300

ILIPOISHIA
Aliingia kuoga alafu akatoka akakaa kitandani akazikausha nywele zake ndefu za kibrazil. Baadaye akapumzika. Akili yake ilimrejesha asubuhi alipovamiwa na jitu jeusi, ndilo Stanslaus. Kisha akakumbuka habari za Sajenti Warioba, alikumbuka penzi zito alilopewa na Sajenti mwezi mmoja uliopita. Alitamani raha zile. Alijikuta akitabasamu, alafu akasema; Nakupenda sana Otieno.
Usingizi ulimpitia akalala.

INAENDELEA

SURA YA 3

KIJIJI CHA MAKANYA, SAME KILIMANJARO.

Sajenti alikimbilia kwenda kujificha katika kijiji cha Nkwini kilichopo kata ya Makanya, wilaya ya Same iliyoko Mkoa wa Kilimanjaro. Huko alienda kwa Babu yake mzaa Mama. Babu yake alikaa nje kidogo ya kijiji cha Nkwini, alikuwa kazeeka sana. Mwenye umri wa makadirio ya miaka themanini hivi.
Mzee Mkwizu alishtuka kusikia mlango ukibishwa yapata saa tisa za usiku. Alipofungua mlango alishangaa kumuona mtu aliyevalia kofia iliyoficha uso wake, Mzee Mkwizu alifunga mlango kwa upesi kwa hofu. Hakutambua kuwa mtu Yule alikuwa ni Sajenti Warioba. Ni mpaka Sajenti alipojitambulisha kuwa yeye ni nani ndipo alipofunguliwa na Mzee Mkwizu.
“Karibu sana Mjukuu wangu, Kulikoni, mbona unakuja usiku mnene kama huu? Usalama upo?” Mzee Mkwizu aliongea huku akimkaribisha Sajenti ndani.
“ Nitakusimulia kila kitu Babu, kwa sasa naomba nipumzike, nimechoka sana” Sajenti Warioba alisema, kisha akatazamana kwa kitambo na Mzee Mkwizu bila kusema chochote, alafu akampita Mzee Mkwizu akaelekea chumbani. Mzee Mkwizu aligeuka kumtazama Mjukuu wake, alishangaa kumuona Sajenti akichechemea, akili yake ilishtuka, moja kwa moja akatambua kuwa kuna tatizo kubwa linalomkabili mjukuu wake. Sajenti aliingia katika chumba kisichokuwa na mlango isipokuwa pazia, akatoma ndani akimuacha Mzee Mkwizu akimshangaa.
Sajenti alijibwaga kitandani, kilikuwa kitanda kidogo cha futi tatu kwa sita. Alivua nguo alizokuwa amezivaa akabakiwa na kaptura juu akiwa kifua wazi. Kisha akajinyoosha kitandani, hapo akakumbuka mambo yaliyomtokea mchana.
Alikumbuka jinsi alivyomtoroka Fernanda pale kwenye Hotel ya nyota tatu iliyopo Ubungo. Akatoka, moja kwa moja akiwa kashika simu yake akiwa karibu na Kituo cha mabasi ya Mkoani Ubungo. Mfukoni alikuwa na shilingi laki mbili, hiyo isingemtosha hivyo akatoa laki tano, ikamfanya akawa na jumla ya shilingi laki saba za Kitanzania. Alichukua boda boda akamwambia ampeleke Stendi ya daladala ya Mbezi mwisho, hakutaka kupandia Mabasi pale Ubungo kwa kuogopa kufuatiliwa. Hiyo ilikuwa yapata saa kumi na moja za jioni.

Akiwa kwenye bodaboda mara kwa mara alichungulia kwenye vioo vya pikipiki, jambo hilo alilifanya kila mara hali iliyomfanya dereva wa bodaboda kumshtukia. Dereva wa Bodaboda alitamani kumuuliza swali kuwa mbona anachungulia mara kwa mara kwenye vioo lakini akili yake ilimuonya, aliona lingekuwa swali la kichokozi ambalo halina msingi wowote. Sajenti alibaini hofu ya dereva macho yao yalipokutana kwenye kioo cha pikipiki. Dereva aliondoa macho yake haraka, na kuuliza swali la kukaribisha mazungumzo.
“ Bwana Mkubwa, Nikushushie Mbezi mwisho ndani kabisa ya Stendi ya Daladala au nje?”
“ Nishushie mbele kidogo ya kituo cha daladala cha mbezi mwisho” Sajenti alijibu macho yake yakichungulia kwenye kioo kutazama magari yaliyokuwa yanakuja kwa nyuma.
“Huku ndio nyumbani , boss? Au umekuja tuu mara moja?” Dereva wa bodaboda aliuliza.
“ Hapana, nimekuja tuu mara moja, kuna mtu nataka kuonana naye ” Sajenti aliongea.
Tayari walikuwa wamefika Mbezi mwisho mbele kidogo ya Stendi ya daladala. Sajenti akatoa elfu ishirini kisha akampa Yule Dereva Bodaboda na kumuambia achukue tuu yote bila kurudisha chenchi ingawaje walipatana nauli ni shilingi elfu kumi na mbili. Dereva bodaboda alifurahi sana, uso wake ulishindwa kuzuia furaha ya kupata ofa ile.
“Shukrani Boss, sijui naweza kurudi kukuchukua au nikusubiri hapa hapa mbezi ili nikurudishe Ubungo?” Dereva Bodaboda alisema huku tabasamu shawishi la kibiashara likiuzingira uso wake.
“ Usijali, nitakaa huku mpaka kesho, Ahsante kwa huduma yako, jioni njema rafiki” Sajenti alimuaga Dereva bodaboda, akaondoka huku akichechemea. Alitembea hatua kumi kisha akageuka nyuma kumtazama Yule bodaboda, hakumuona tayari alikuwa keshaondoka. Hakutaka mtu yeyote ajue ni wapi anaelekea, kama angeweza hata yeye hakutaka ajue ni wapi anaelekea, alihisi hiyo ndio salama yake.
Alitembea akichechemea akaingia ndani ya stendi ya Daladala, hakuna aliyekuwa akimtilia maanani licha ya kuchechemea kwake. Tayari ilishahitimu saa kumi na mbili jioni kigiza cha usoni kikiwa kinafukuza mwanga wa mchana. Sajenti alisoma mienendo ya watu wa pale Stendi, hakuona ishara yoyote ya hatari. Hapo akaingia chapuchapu kwenye Daladala zinazoelekea Mlandizi. Kutokana na Kuwa tayari Daladala ilikuwa imejaa gari haikumaliza dakika tano ikatia moto na kuondoka.

Sajenti alikuwa amekaa siti ya nyuma kabisa, huku watu wengine wakiwa wamesimama kutokana na gari kujaa. Hapo alitulia akisoma mienendo ya abiria mmoja baada ya mwingine, aligundua abiria wengi walikuwa ni watu wa tabaka la chini, wasakatonge ambao wanajishughulisha na shughuli za ujasiriamali na baishara ndogo ndogo. Wengi wa abiria walikuwa ni wakazi wa Kibaha na mlandizi ambao kila siku hujihimu asubuhi na mapema kwenda Dar es salaam kufanya biashara, kisha jioni hurejea makwao. Hivyo ndivyo maisha yao yalivyo, hata hivyo jambo jema ni kuwa kutokana na ubora wa miundombinu ya barabara ndio unaochochea maendeleo na ustawi wa shughuli zao. Jambo kuu ambalo lilikuwa linalalamikiwa ni suala la foleni za magari katika barabara ya Mlandizi, hata hivyo tayari serikali imeshaanza kuipanua barabara hiyo iwe ya njia nne.
Sajenti alikumbuka jambo, hapo akageuka nyuma akachungulia Kupitia dirisha la nyuma la gari. Alipagawa, akili yake ilipoteza utulivu. Alimuona Yule dereva bodaboda akiwa nyuma ya gari alilokuwa amepanda. Awali hakuamini macho yake lakini baadaye alijihakikishia ndio Yuleyule bodaboda aliyekuwa amembeba akamleta mbezi mwisho. Hapo tayari walishakuwa wamepita mji wa kibaha giza likiwa limeshafunika nchi.
Sajenti sasa alihisi ipo hatari kama ataendelea kukaa ndani ya ile daladala, alimhofia Yule dereva kuwa huenda anamfuatilia. Hilo peke yake lisingemuogopesha lakini vipi kama dereva Yule katoa taarifa kwa watu wanaomtafuta Sajenti, hiyo ndio ilikuwa hofu yake. Sajenti alijua fika watu wanaomtafuta ni watu wakubwa wenye nyadhifa kubwa serikalini. Hivyo kitendo cha yeye kujulikana alipo kingehatarisha maisha yake.

Akachungulia tena nyuma ya gari kwenye kioo cha nyuma hapo alimuona Yule Dereva bodaboda akiongea na simu aliyoichomeka kwenye helmet aliyoivaa kichwani, hisia zake moja kwa moja zikamtuma kuwa dereva Yule anawasiliana na watu wanaomtafuta.
Akili ya Sajenti ikamuambia ashuke, hapo hapo akamuagiza konda wa ile daladala asimamishe gari ili ashuke. Konda akagomba akisema pale hakuna kituo wala mji wowote isipokuwa mapori, lakini Sajenti aliomba afanyiwe msaada tuu. Basi gari ikapunguza mwendo, kisha ikasimama na Sajenti akashuka. Hapo Sajenti aliiona ile Bodaboda ikipunguza mwendo ikiwa umbali wa mita hamsini.
Daladala ikamuacha Sajenti, na ile bodaboda ikapita na kwenda kusimama umbali wa hatua mia moja kama urefu wa kiwanja cha mpira.
Sajenti alitamani mguu wake wa kushoto ungekuwa mzima amkimbize Yule Dereva wa Bodaboda lakini hakuweza, mguu wake ulikuwa na jeraha kubwa la risasi aliyoipata kule katika hospitali ya Boreti. Alichechemea, kisha akapotelea kwenye mapori akimzuga Yule dereva bodaboda, punde akiwa kajificha kwenye kichaka alisikia kwa mbali sauti ya pikipiki ikiwashwa, hapo akajua Yule dereva anakuja kule alipo. Kitambo kidogo dereva wa bodaboda alikuwa amesimama pale alipokuwa ameshukia Sajenti, alishuka na kuanza kumulika mulika huku na huko, Sajenti yeye alikuwa kajibanza kwenye kichaka chenye majani mazito yaliyomfanya asionekane.
Punde alimsikia Yule dereva akiongea na simu;
“Fanyeni haraka kabla hajapotea, ameshuka muda huu, anaonekana anajeraha mguuni, kaingia kwenye mapori, mimi siwezi kumfuata mwenyewe….” Dereva Bodaboda aliongea lakini kabla hajamaliza Sajenti alijitokeza akiwa kamshikia bastola yule dereva akakata simu na kuweka mikono juu, muda huo pikipiki ilikuwa ikinguruma huku ikiwamulika.

Sajenti akamfuata, kisha akampiga kitako cha bastola Yule dereva akaanguka chini, Sajenti akaichukua simu ya dereva kisha akaikariri namba aliyokuwa anaongea nayo Yule dereva, akaingia kwenye uwanja wa meseji hakuona la maana. Akamsogelea Yule dereva pale chini aliyekuwa anagugumia kwa maumivu ya kupigwa na kitako cha bastola, akamuwekea mdomo wa bastola mdomoni,
“nambie ulikuwa unaongea na nani?” Sajenti alimuulzia Dereva.
“Tafadhali naomba usiniue, mimi sio mtu mbaya. Tafadhali nakuomba boss…”
“Kama wewe sio mtu mbaya nambie umetumwa na nani, nahesabu mpaka tatu, usiposema napasaua kichwa chako” Sajenti alisema akiufikicha mdomo wa bastola kwenye mdomo wa Yule dereva.
“ moja..! Mbili…..! Taaatu…! PAAH!” Sajenti aliongea kisha akaachia bastola iliyolenga kwenye paja la bodaboda. Hapo dereva akapiga makelele lakini Sajenti akamkemea anyamaze.
Ghafla bin vuu kwa mbali Sajenti aliona gari ikija kwa kasi ikitokea upande wa Dar es salaam, hakutaka kujiuliza maswali , alikimbilia pikipiki ya Yule dereva akapanda juu yake na kuanza kuiendesha kwa uelekeo wa Chalinze. Alichanganya gia mwendo ukawa mwendo, kasi ikawa kasi, alipishana na upepo huku akilichana giza na mwanga wa pikipiki. Ilikuwa pikipiki aina yo Boxer, moja ya pikipiki nzuri zenye mwendo mzuri usio na shaka ziwapo kwenye barabara ya lami.
Wale watu nao hawakuwa nyuma walimfungia mkia wakimfukuza kwa kasi kama mshale. Tayari walikuwa wamemkaribia kama hatua ishirini na tano tuu. Ilikuwa ni Difenda iliyokuwa ikimjia kama jini pori.

Wakaanza kumrushia risasi zilizokuwa zikimpunyua punyua, naye hakuwa nyuma kuhakikisha anazikwepa kwa kuhamisha pikipiki upande huu na upande huu, Sajenti alikoswa koswa na magari aliyokuwa anapishana nayo hata hivyo bado alichanja mbuga, akiyapita magari yaliyokuwa mbele yake, jambo ambalo Difenda iliyokuwa ikimfukuzia ikichelewa kufanya hivyo kutokana na kuhofia kusababisha ajali ya kugongana uso kwa uso na magari yaliyokuwa yanayokuja mbele yao. Hii kwa Sajenti ilikuwa nafasi nzuri ya kuwaacha wale maadui walioisaka roho yake kwa hamu bila ya nidhamu.
Punde aliingia mji wa Mlandizi, bahati mbaya pikipiki ikaisha mafuta.....

ITAENDELEA

Usisahua ku-like na kushare.
Jipatie Riwaya ya MLIO WA RISASI HARUSINI" Ambayo ipo sokoni. Hutojutia.

Kitabu Tsh 15,000


0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel.

0758216209
M-PESA
Robert Heriel
 
WAKALA WA SIRI 09
Mtunzi; Robert Ng'apos Heriel
0693322300

ILIPOISHIA
Wakaanza kumrushia risasi zilizokuwa zikimpunyua punyua, naye hakuwa nyuma kuhakikisha anazikwepa kwa kuhamisha pikipiki upande huu na upande huu, Sajenti alikoswa koswa na magari aliyokuwa anapishana nayo hata hivyo bado alichanja mbuga, akiyapita magari yaliyokuwa mbele yake, jambo ambalo Difenda iliyokuwa ikimfukuzia ikichelewa kufanya hivyo kutokana na kuhofia kusababisha ajali ya kugongana uso kwa uso na magari yaliyokuwa yanayokuja mbele yao. Hii kwa Sajenti ilikuwa nafasi nzuri ya kuwaacha wale maadui walioisaka roho yake kwa hamu bila ya nidhamu.
Punde aliingia mji wa Mlandizi, bahati mbaya pikipiki ikaisha mafuta.....

INAENDELEA

, akaingia vichochoro vya mlandizi akiwatoroka wale watu wabaya, aliitupa pikipiki kisha akakimbia akichechemea, tayari alikuwa ameshawapoteza. Alisimama mbele ya moja ya Bar za pale Mlandizi, akiwa pale Bar aliwaona mwanaume mmoja na mwanamke wakiwa wanaingia ndani ya gari aina ya Suzuki, akawafuata kabla hawajafunga mlango akawavamia. Kisha akawaweka chini ya Ulinzi, Yule mwanaume akamvalisha pingu na Yule mwanamke akampiga kidogo kwenye kisogo akapoteza fahamu.
“ Samahani Brother, sikujua kama Leah ni Mke wa mtu, Nisamehe. Nipo tayari kukupa kitu chochote lakini tafadhali naomba usinidhuru” Yule mwanaume alisema huku akilia. Hapo Sajenti akajua kuwa kumbe Yule mwanaume na Yule mwanamke hawakuwa mke na mume bali walikuwa wanafanya uzinzi.
” Sitaki kusikia kelele zako, umenichukulia mke wangu, bado unipigie kelele? Bado unataka nikusamehe” Sajenti aliongea hukua akichanganya na kupangua gia akiitafuta Chalinze. Hapo utulivu ukatokea, huku Sajenti akitafakari mambo mengi ambayo yalimfanya awe na huzuni. Malipo ya kulitumikia taifa ndio yale. Mambo yote mema aliyoyafanya leo ndio anakimbizwa na kuwindwa kama digidigi. Amegeuka mkimbizi wa nchi yake mwenyewe.
“Nawezaje kuiibia nchi yangu, nawezaje kuwa adui wa nchi, ati nimeiba chipu ya darubini ya hospitali ya Boreti, chipu ambayo imebeba siri nyingi za nchi, nimeiba Cadava na sampo mbili za uchunguzi, wakaona hiyo haitoshi sasa wanasema nimemtorosha mateka wa Ushahidi. Sitokubali, siwezi nasema”
Sajenti alisema maneno hayo akiwa kitandani baada ya kumbukumbu hizo kukatika, usingizi ulimpitia, hatimaye akalala.
*******************************

Asubuhi ilifika, siku mpya ilimkuta Sajenti akiwa katika nyumba ya Babu yake, Mzee Mkwizu. Akiwa kitandani alisikia mbuzi, kondoo na ng’ombe wakilia kwa nje. Sajenti alivaa nguo kisha akatoka nje, alimkuta Mzee mkwizu akimkamua ng’ombe maziwa. Sajenti aliwaona ng’ombe wengine wakiwa zizini, walikuwa ng’ombe wazuri walionona. Pia aliona zizi la pili, hili lilikuwa na kondoo na mbuzi, zizi la tatu lilikuwa na ndama na vitoto vya mbuzi na kondoo ambavyo vilikuwa vikililia mama zao huku vingine vikicheza cheza.
Mzee Mkwizu alikuwa mfugaji mkubwa katika kijiji cha Nkwini ndio maana aliamua kujitenga nje kidogo ya mji. Mbali na kondoo, mbuzi na Ng’ombe pia Mzee Mkwizu alikuwa anafuga kuku wa kienyeji. Vyote hivyo vilimpatia Mzee mkwizu kipato cha kuendesha maisha yake.
Kupitia ufugaji Mzee Mkwizu aliweza kujenga nyumba nzuri ya matofali ingawaje bado haikuwa na umeme wala baadhi ya vyumba ilikuwa haina milango, lakini aliweza kuweka sakafu nzuri ya vigae, bati na madirisha ya chuma. Nyumba yake ilizungushiwa na uzio wa milingoti inayotokana na zao la mkonge..
Sajenti alitaka naye ajaribu kukamua maziwa lakini alishindwa.

Hakuwa na ujuzi wa kumkamua ng’ombe maziwa, awali alidhani ni jambo rahisi ambalo angelifanya kwa wepesi lakini alijikuta akishindwa. Hatimaye Mzee Mkwizu alimaliza kukamua ng’ombe maziwa, Sajenti alienda kuwasha moto jikoni. Lilikuwa jiko la kizamani lililojengwa kama tanuru. Alichukua makorokocho kisha akawasha moto. Makorokocho ni kuni zinazotokana na katani iliyokwisha kukauka. Katika kijiji cha Nkwini Makorokocho hutumiwa kupikia.
“ Warioba, miaka kumi sasa hatujaonana, tangu ulipokuja kwenye mazishi ya Bibi yako ukapotea moja kwa moja. Umekuwa mtu mzima kweli” Mzee Mkwizu alisema kikombe cha maziwa kikiwa mkononi.
“ Hivi kumbe miaka kumi imeisha, ama kweli siku zinaenda” Sajenti aliongea, wote walikuwa wanakunywa kifungua kinywa pale sebuleni.
“Haya nambie, mbona umekuja kama mauti, umenivamia usiku kama mwizi. Tena mguu wako unajeraha. Je, umekuwa mtu wa kuja kwa mikosi, mara ya mwisho umekuja kumzika Bibi yako, mara hii umekuja kunizika Mjukuu wangu?” Mzee Mkwizu alisema kikombe akiwa kakiweka kwenye meza ya mbao.
“ Hapana Babu, usiseme maneno hayo, ingekuwa ni heri kuvumilia maumivu ya jeraha langu la risasi mguuni kuliko maumivu ya maneno yako. Sijaja kukuzika Babu, ila kuhusu mkosi sikatai, ni kweli mara hii nimekuja nikifukuzwa na jinamizi baya, siwezi kukimbia tena, wanaonikimbiza wanamiguu elfu wakati mimi ninamiguu miwili,tena mguu mmoja wameujeruhi, wanambio kuliko farasi, nimekuja huku…” Sajenti alimeza mate kisha akaendelea;
“ Njama, na hila wamenibebesha. Wamenipa jina baya lenye kunitusi mimi mtu wa watu, nimekuwa kama paka shume niliyeiba chakula cha wasela, nafukuzwa mimi. Nimekuwa adui wa nchi” Hapo Sajenti akaanza kulia sauti ikiwa inatetemeka.
“ Tafadhali usilie, nyamaza mjukuu wangu. Hila zao hazitafanikiwa. Nani amefanya haya?” Babu alimbembeleza Sajenti, aliuona uchungu aliokuwa nao Sajenti.
“ Babu nakimbizwa na watu nisiowaona kama upepo, nisiowajua kwa sura kama shetani, ingawaje sitajiongopea kuwa ni watu wabaya, wenye ukaribu na mimi. Huenda kuna mpango mbaya wa kulibomoa taifa hili, utafikiria namna chipu ya darubini ya taifa, iliyobeba siri na mikakati ya taifa jinsi ilivyoibiwa, utafikiria namna Cadava ya uchunguzi ilivyoibiwa na sampo zake, pia Mateka wa ushahidi alivyotoroshwa, yote hayo kwako utayaona kama mageni, tena mambo magumu usiyoyajua. Hayo yote ni mazito, yote nimebebeshwa mimi, ati ndio mwizi, adui na msaliti wa nchi” Sajenti alimeza fumba la mate, kisha akapumua pumzi nzito kama pumzi ya mwisho. Uso na macho yake yalieleza zaidi kuliko maneno aliyoyaeleza kwa Mzee Mkwizu.
Mzee Mkwizu alisikitika sana kusikia taarifa hizo japokuwa hakuwa anazielewa lakini alimuelewa Sajenti kwa jambo moja tuu, nalo ni kubebeshwa zengwe la usaliti, Mzee Mkwizu alijua adhabu ya msaliti ilikuwa ni kifo cha ukatili. Ingawaje hakuwahi kuwa katika nyadhifa za serikalini lakini aliwahi kusikia hadithi za watu waliosaliti nchi jinsi walivyofanywa. Kwenye ujana wake, aliwahi kusikia kuwa watu wasaliti hasa wa nchi waliuawa kwa kunyongwa ama kuuawa kwa maumivu makali mno.
Hapo akajua jambo lililokuwa linamkabili Sajenti Warioba lilikuwa ni kubwa mno.
“ Mjukuu wangu, pumzika. Kila kitu kitakuwa sawa. Ngoja niende machungani kuwalisha hawa viumbe, Usiogope, wewe ni hodari, mtu mwema usiye na hila” Mzee Mkwizu alisema kisha akamuaga Sajenti akaenda Kuchunga.
Siku zikapita nazo hazikurudi, wiki ikaisha Sajenti akiwa kwa Babu yake, sasa tayari mguu wake ulikuwa umepata nafuu hata ile hali ya kuchechemea ikawa imeisha. Mzee Mkwizu alikuwa mahiri wa madawa ya jadi, aliijua mitishamba kwa majina na matumizi. Alimtibu Sajenti Warioba Kijadi mpaka pale alipopata ahueni na mguu wake kupona. Ilichukua wiki mbili kwa Sajenti Warioba kupona kabisa.

Pesa kidogo aliyokuwa nayo Sajenti ilisaidia kwa matumizi pale nyumbani. Hata hivyo pesa isiyozalishwa huisha haraka kama barafu kwenye jua. Ndivyo ilivyokuwa, Pesa ya Sajenti iliisha. Sajenti hakutaka awe mzigo kwa Babu yake. Wiki mbili zote alikuwa ndani kama mwali, hakutoka kwenda mbali zaidi ya kuzunguka mulemule ndani kwenye eneo la Nyumba ya Babu yake.
Sajenti aliona amsaidie Babu yake kwenda kuchunga ng’ombe, mbuzi, na kondoo. Alienda kwenye mapori kwa mapori akiwaongoza mifugo kwenye malisho akiwa na Mbwa wa Mzee Mkwizu aitwaye Kajiru. Kajiru alikuwa Mbwa mkubwa mwenye miguu yenye nguvu, alikuwa mweusi, na hiyo ndiyo iliyomfanya aitwe “Kajiru” ambayo kwa Kiswahili humaanisha “keusi”. Alikuwa ni Mbwa mwenye adabu, uso wenye soni lakini ulioficha ukali na hasira, Meno yake yalikuwa yamechongoka, makali yasiyo na mzaha. Huyo ndiye Kajiru rafiki Mpya wa Sajenti awapo machungani. Sajenti hakuwahi kuwa mchungaji wa mifugo ingawaje kiasili yeye ni Mkurya kabila ambalo pia hufanya ufugaji japo sio kwa kiwango kikubwa. Hivyo Kajiru ndiye alimsaidia kuchunga hasa kuwadhibiti Mbuzi waliokuwa wasumbufu.
Mwezi Sasa uliisha, Sajenti alichoka kukaa ndani na kwenda machungani kulisha mifugo ya Babu yake. Hilo Mzee Mkwizu aliliona, Hakutaka Sajenti ajisikie vibaya, tena akose amani. Siku ya Gulio ilipofika, ndiyo siku ya Jumatano katika kijiji cha Makanya kilichopo kaskazini mwa kijiji cha Nkwini, Mzee Mkwizu alimuagiza Sajenti akanunue vitu vya ndani, alimuagiza Ngogwe ambayo pia huitwa Nyanya Chungu, nyanya, Kweme, Viazi vitamu, kahawa na vitunguu.

Sajenti hakuwahi kufika katika mji wa Makanya. Hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza. Kutokana na kukaa sehemu moja alijawa na hamu ya kuuona mji wa Makanya. Pengine alivuta picha jinsi mji huo ulivyo, au hata aliuona kabisa kwenye fikara zake. Lakini yote ilikuwa hamu ya kuufahamu mji wa Makanya. Mzee Mkwizu alitamani sana kuambatana naye kwenda Gulioni, Makanya. Lakini uzee ulishanyonya nguvu za mwili wake, miguu yake haikuwa na nguvu kabisa ya kutembea umbali mrefu, hata huko kuchunga mifugo ni kwasababu alishaifunza mifugo ile kuongozwa. Ungeshangaa namna Mzee Mkwizu akiiongoza Mifugo yake. Kila ng’ombe alikuwa na jina lake licha ya ng’ombe kuwa wengi, ajabu ni kuwa ng’ombe nao walitambua majina yao.
Sajenti alishuka stendi ya Makanya ambapo upande wa mashariki kulikuwa na Katani na safu ya milima ya upare. Katani zilikuwa zimepandwa kwa mpangilio wa mistari iliyonyooka, hakika zilikuwa zinapendeza. Kilimo cha katani ni moja ya kilimo kilichoanzishwa na wakoloni hapa nchini, ni muhimu sana kwani kinazalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo kamba nzuri za katani, mifuko ya katani na mazulia. Katani pia huzalisha mbolea nzuri Ambayo hutumika kwenye kilimo. Kilimo cha Katani Makanya husaidia baadhi ya wakazi wa kijiji hicho kujipatia kipato baada ya kulima vibarua katika mashamba makubwa ya katani.

Upande wa Magharibi macho yake yalipokelewa na mji mzuri wa Makanya uliokaa kwenye tambarare inayovutia. Aliona vifusi vifusi vya mawe meupe, hayo yalikuwa mawe ya jasi ambayo hujulikana kama gypsum kwa lugha ya kingereza. Mawe ya Jasi hutumika kutengenezea saruji kwa ajili ya sakafu, pia hutumika kutengenezea Cealing board ya gypsum. Machimbo ya gypsum ni moja ya shughuli muhimu katika mji wa Makanya, watu wengi hasa vijana huenda machimboni kuchimba mawe hayo na kujipatia kipato.
Sajenti alishangaa kuona vijana wakitafuna vitu midomoni, alipochunguza akabaini vijana wengi wa Makanya hutafuna Mirungi, bado ilikuwa ni asubuhi Sajenti akiwa pale Stendi ya Makanya akiwa amekaa kwenye kijimgahawa akiangalia mienendo ya watu pale Stendi. Tofauti na alivyozoea kuona katika stendi za miji mingine ambapo Mabasi yakifika Stendi, vijana waliobeba bidhaa mbalimbali hulikimbilia Basi na kuanza kuuza bidhaa zao, Stendi ya Makanya hali ilikuwa tofauti kabisa, aliona vijana wenye bahasha za kaki zilizotuna wakikimbilia mabasi yaliyokuwa yamesimama pale stendi, kisha wanamkimbilia dereva au konda alafu atakayewahi basi ndiye humpa moja ya zile bahasha ya kaki zilizotuna. Hiyo ikamfanya Sajenti adadisi ndani ya zile bahasha kuna nini, Looh! Kumbe ni Mirungi.
Sajenti aligundua kwamba Makanya lilikuwa ndio soko kubwa la mirungi ambalo madereva walikuwa wanatumika kama wateja na wasafirishaji wa bidhaa hiyo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Wateja wakubwa wa Mirungi walikuwa madereva wa malori yanayofanya safari ndefu, madereva wenye asili ya kisomali na kiarabu, vijana, na watu wazima.

Sajenti alimuita kijana mmoja akamuuliza;
“ Habari kijana, vipi naweza kupata mrungi?”
“ Gomba ipo Broo, vipi unahitaji kete ngapi?” Kijana alimjibu huku akiingiza mkono wake kwenye bahasha kutoa mrungi.
“ Kete moja tuu” Sajenti alijibu akiwa kajua jina jingine la mrungi kumbe lilikuwa ni Gomba. Hata hivyo alisubiri aone kete moja inalinganaje kwani hakuwahi kujua habari za mirungi.
“ Hii hapa Broo, hii sio Kilaza, hii ni Og kabisa haijalala, inatoka Tae. Si unaona mzigo ulivyo wamoto” Kijana alizungumza lugha ya kibiashara uso wake ukiwa umejawa na tabasamu.
“ Shilingi ngapi?” Sajenti aliuliza akiwa kapokea ile kete ya mrungi huku akiikagua.
“ Elfu mbili tuu braza, hiyo kitu ni mang’anyu”
“ Duuuh! Mbona ndogo hivyo, Mang’anyu ndio nini?” Sajenti alishangaa kuona kete ya mrungi ilivyo ndogo lakini bei yake ilivyokuwa kubwa.
“ Broo, huu ni msimu wa kiangazi, gomba bei yake ipo juu, miti ya gomba kipindi cha kiangazi haichipui sana, hivyo gomba inaadimika mpaka msimu wa mvua” Kijana alijibu akijaribu kuelezea kwa ufasaha ili mteja wake aelewe ajipatie kipato.
“ Kumbe! Hiyo mang’anyu ndio nini sasa?”
“Hhahaha! Broo bhana, Mang’anyu ni lugha tuu za kijiweni, maana yake ni kitu kizuri” Kijana alicheka sana, Sajenti naye alicheka baada ya kujua maana ya neno hilo.

Sajenti baada ya kuzungumza na Yule kijana, aligundua mambo mengi yahusuyo mji ule wa Makanya. Hatimaye alienda mnadani kununua vitu alivyoagizwa. Alipofika sokoni alikuta umati mkubwa wa watu wakiuza biashara zao na wateja wakinunua bidhaa. Lilikuwa soko kubwa kiasi. Lugha alizozisikia mbali na Kiswahili ilikuwa lugha ya kipare. Hapo akajua eneo lile limetawaliwa na watu wenye asili ya kabila la wapare. Pia aliwaona Wamasai wengi upande wa nyuma lilipo soko la mifugo.
Hatimaye alimaliza kununua bidhaa zote alizoagizwa, lakini alivutiwa na matunda Fulani yaliyokuwa na maganda ya rangi ya njano, alipouliza aliambiwa yanaitwa ‘Sambia’ aliyaonja, Dooh! Yalikuwa yana sukari na ukakasi, ndani yake yakiwa na mbegu za rangi ya huzurungi.
Muda ulikuwa umeenda sana, jua lilikuwa kali yapata mida ya saa sita. Sajenti akarudi Nkwini kwa Babu yake akiwa amefurahia safari yake, roho yake ilisuuzika, mji wa Makanya uliamsha chemchem ya uhai na ari moyoni mwake.
***************************

ITAENDELEA

Usisahua ku-like na kushare.
Jipatie Riwaya ya MLIO WA RISASI HARUSINI" Ambayo ipo sokoni. Hutojutia.

Kitabu Tsh 15,000


0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel.

0758216209
M-PESA
Robert Heriel
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom