Riwaya Mpya: Mpelelezi Ray Shaba katika

Sehemu ya mwisho kabla ya kitabu kutinga mtaani siku chache zijazo...

(Inaendelea)

SURA YA 13

JUMANNE ASUBUHI RAY aliingia ofisini akiwa amechelewa kidogo. Safari ya Arusha na baadaye kupitia Moshi haikuwa na mafanikio sana kama walivyotarajia. Kote huko ilikuwa ni katika kujitahidi kuwapanga maafisa wa upelelezi wa Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa kundi lililotajwa kuwa limeingia nchini linapatikana kwa udi na uvumba. Kukosekana kwa harufu yoyote ya kundi hilo kulikuwa kunaleta wasiwasi mkubwa sana ndani ya jeshi la polisi na vyombo vingine vya usalama.

Taarifa mpya zilizopatikana na jeshi la Polisi zilionesha kuwa kundi hilo lilikuwa ni miongoni mwa makundi ya watu wanaoitwa wasiojulikana ambao walikuwa wanafanya matukio mbalimbali ya uporaji na ujambazi na hata mauaji ya kisiasa katika nchi za Afrika ya Mashariki. Kundi hilo pia lilihusishwa na mauaji ya wagombea wawili wa chama cha upinzani cha NASA huko Kenya na pia mauaji ya kinyama ya Sheikh Abdulrahman Jogoo wa mjini Mombasa miezi mitatu nyuma.

Uwepo wa kundi hilo Tanzania ulikuwa unaleta mshawasha mkubwa kwa vyombo vya usalama vya Tanzania. Ray Shaba akiwa ni miongoni mwa vijana wapelelezi mashuhuri nchini aliyekuwa anapanda ngazi kwa haraka alitegemewa kuongoza kundi la wapelelezi kutoka makao makuu kuhakikisha kuwa kundi hilo la majambazi linapatikana kwa haraka kabla halijaleta madhara. Ray hakutaka kuliangusha taifa lake au kupoteza imani ya wakubwa wake.

Kutokuwepo kwa Sofia pale nyumbani nako kulimfanya apaone nyumbani hapakaliki vizuri. Hivyo, alijikuta anachelewa kulala mara nyingi pamoja na uchovu wote. Na kwa vile Sofia alikuwa anashughulia mambo mengi ya pale nyumbani majukumu hayo sasa yalimuangukia Ray peke yake. Jumanne ile alijikauta anahitaji kupitia benki kutoa fedha kwa ajili ya kufanya malipo mbalimbali ya matumizi yake ya nyumbani. Alipofika kazini asubuhi ile aliomba ruhusa kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi kuwa angehitaji kutoka mapema kidogo siku ile. Lengo lake ilikuwa ni kwenda kupeleka malipo ya awali ya shamba jingine huko maeneo ya Chanika nje ya Jiji la Dar. Shamba hilo Sofia hakujua uwepo wake wakati anaondoka kwa sababu mara Ray alipogundua kuwa mwenzie ameanza mambo ya kuuza mali za familia alianza kuweka vitu vingine peke yake. Alianza kutafuta shamba jingine mara tu alipokuta Sofia ameuza lile shamba la Kinyerezi.

Aliingia ofisini na kuanza kupitia mafaili mbalimbali yaliyokuwepo mezani pamoja na kupeleka taarifa kwa bosi wake kuhusu upelelezi mbalimbali ambao alikuwa anausimamia. Kulikuwa na kikao ofisi ya Mkuu wa Mkoa majira ya saa nane mchana. Ray alikuwa amepanga kuwa baada ya kikao kile ndiyo angetoka kwenda kushughulikia mambo yake.

Ilikuwa ni katika toka toka na ingia ingia hizo asubuhi ile ndipo akili yake ikamlazimisha kujiuliza swali ambalo lilikuwa limejibanza kichwani. Wakati anaingia kazini asubuhi ile alimkuta dada mmoja ambaye alikuwa ameketi akisubiri kwenye sehemu ya wageni mbele ya meza ya mapokezi. Ray alianza kukumbuka kuwa alimuona dada yule tangu ameingia pale na karibu saa tano na nusu dada yule bado alikuwa yuko pale akisubiria. Aliamua kwenda kwa ofisi wa zamu aliyekuwepo pale mapokezi na kutaka kujua yule dada ana shida gani. Aliambiwa kuwa yule dada alitaka kufungua shauri la kubakwa.

“Sasa ameweza kufungua?” Ray alimuuliza ofisi yule mwenye cheo cha Sajenti na aliambiwa kuwa faili limefunguliwa lakini mama mwenyewe hajaweza kumtaja mtu mwenyewe wala kutoa maelezo zaidi hadi apate nafasi ya kuzungumza kwanza na RPC. Sajenti yule alisema RPC alikuwa kwenye vikao mbalimbali. Ray alijua mara moja kuwa maafisa pale walikuwa wanamchelewesha yule dada bila sababu ya msingi.

Ray aliomba kuangalia faili lililofunguliwa na akapewa. Akiwa bado amesimama kwenye meza ya mapokezi alilipitia kwa haraka. Hakukuwa na taarifa zaidi ya jina, jinsia, anuani na kabila la dada yule. Sehemu ya maelezo iliachwa tupu. Ray alimwambia yule sajini wa polisi amuelekeze yule dada ofisini kwake kama hatojali. Aliondoka na faili mkononi kuelekea ofisini kwake.

Kabla hajaketi kwenye kiti chake mlango wake wa ofisi ukagongwa na katibu muhtasi aliyekuwa anahudumia wapelelezi wanne waandamizi Mama Stella Maliyamungu alichungulia na kumuambia kuwa kuna dada ameelekezwa aje ofisini kwake. Ray alimuambia Stella amruhusu dada yule aingie.

“Karibu, naitwa Ray Shaba ni Afisa wa Upelelezi hapa mkoani” Ray alijitambulisha huku akinyosha mkono wake kumsalimia dada yule. Aliivuta tai yake na kuiweka vizuri. Tabasamu la kirafiki liliupamba uso wake.

“Naitwa Skola Kanuti, nashukuru kukutana nawe” Skola alijibu kwa sauti isiyoonesha uchangamfu sana lakini ikionesha heshima. Aliupokea mkono wa Ray na akapiga goti kidogo kwa heshima. Hawakuwa tofauti sana kiumri lakini Skola alikuwa amelelewa kama binti wa Kiafrika kweli. Ray alimuona kama kaka yake na hivyo aliamua kumpa heshima ile.

Ray alimuelekeza kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza yake na yeye akavuta kiti chake cha ofisi na kuketi.

“Unataka kitu chochote cha kunywa?” Ray aliuliza huku akifungua faili aliloingia nalo mle.

“Maji tu yatatosha” Skola alijibu. Ray alinyanyuka mwenyewe na kumuaga Skola kwa dakika moja. Japo maafisa wengine hawakuona shida kuwaagiza wasaidizi wao kuwaletea vitu mbalimbali Ray aliamua muda mrefu nyuma kuwa kama kuna kitu anaweza kujiletea mwenyewe basi ataenda kukichukua. Hakupenda sana umangimeza na hisia ya kuwa kuna baadhi ya vitu yeye mwenyewe hawezi kuvifanya kwa vile tu yuko kwenye ofisi au cheo fulani hakuiendekeza. Alifanya hivyo pia ili awe anajiweka fiti kiafya. Utafiti unadai kuwa watu wengi wanaofanya kazi maofisini wanapata magonjwa sababu ya kukaa sana chini. Dakika moja na nusu tu baadaye alirudi na chupa mbili za maji ya baridi ya Kilimanjaro, alimkabidhi moja Skola na yeye akachukua ya kwake na kuifungua.

Alifungua lile faili na kulipitia tena haraka haraka na bila kupoteza muda alirusha swali kwa Skola.

“Skola tuhuma hizi zinamhusu nani kiasi kwamba umeshindwa kumtaja?”

“Naomba unihakikishie usalama wangu kwanza kwani ni mtu mkubwa sana” Skola alisema.

“Yuko Ikulu?” Ray alimuuliza akimkazia macho.

“Hapana”

“Basi si mtu mkubwa huyo! Mkubwa Mungu tu!” Ray alijibu.

“Mmh kwangu ni mkubwa labda kuliko wengi walioko serikalini” Skola alijibu kwa uhakika sana na kumfanya Ray atake kujua zaidi.

“Niambie kila kitu usifiche kitu chochote na nitaamua nini cha kuandika humu na ninakuhakikishia ndani ya uwezo wangu wote usalama wako” Ray alimwambia kwa sauti ya upole kama ya baba anayembembeleza mtoto wake aliyeingiwa na hofu ya giza. Maneno hayo yalimfariji Skola.

Dada yule alivuta pumzi na kama aliyepata uhai mpya alianza kujieleza kuanzia mwanzo hadi mwisho wa yaliyotokea baina yake na Askofu Mkuu Damien Ndondo. Ray alikuwa anasikiliza kwa makini huku moyo wa uhuruma ukimuingia. Wakati Skola anazungumzia jinsi alivyotishiwa bastola na Askofu Damien Ndondo Ray alijihisi hasira lakini aliizuia kwani Skola alishindwa kuendelea kuzungumza sana kwani machozi yalikuwa yanambubujika.

“Pole sana Skola, pole sana mama” Ray alisema kwa huzuni.

“Mmh sijui nitapoaje kwenye hili” Skola alijibu huku akivuta makamasi yasimdondoke. Alikuwa na leso kwenye mkoba wake aliichukua na kujipangusa usoni huku akijaribu kujizuia kuendelea kulia. Alibakia kuvuta vuta tu puani.

“Nisamehe Skola, nilipokuona mwanzoni nilidhani kama nimewahi kukuona sasa najua ni kweli, niliona video za nyimbo zako kwenye kile kipindi cha dini TBC wakati wa Pasaka mwaka jana” Ray alisema na hilo kidogo lilimtoa mawazo ya huzuni Skola. Alikumbuka kwa sekunde chache jinsi gani alikuwa maarufu sababu ya vipaji vyake lakini alihuzunika pia kuwa tangu tukio lile la kubakwa hakuthubutu kuimba na kwaya yake. Mialiko mbalimbali aliyokuwa tayari ameikubali aliifuta.

“Limekuja na gharama kweli kweli” alisema na kuacha maneno yake yaelee angani. Ray alijikuta anaandika vitu kwenye kijitabu chake kidogo cha kipolisi ili kuhakikisha anakumbuka kila kitu alichosikia. Alimuuliza tena maswali mawili matatu ili kupata usahihi zaidi wa jambo ambalo hakuwa amelielewa na Skola alifafanua vizuri tu.

“Sasa nipe kama wiki moja hivi nianze kufuatilia” Ray alianza kumwambia na kuendelea kusema kuwa “jambo hili kweli ni kubwa kwani Askofu Damien ni mtu mkubwa sana kwenye jamii na tuhuma hizi ni nzito sana”. Alimuahidi kuwa kwa vile tuhuma hizo ni nzito hivyo kunahitajika ushahidi wa kina kuweza kumuangusha mtu kama Damien kwani anajua watu wengi, na watu wengi vigogo walikuwa upande wake. Kujaribu kumgusa kwa namna yeyote kungekuja na mambo mengi mazito na hivyo anahitaji muda wa kupanga mkakati na mbinu za kipelelezi. Jambo pekee ambalo alimhahidi ni kuwa kama atahitaji kitu kingine chochote kutoka kwa Skola ambacho kitaweza kumsaidia katika upelelezi basi atampigia simu na kama Skola atakumbuka jambo jingine basi anaweza kumpigia simu. Alimkabidhi kadi yake ya ofisini ambayo ilikuwa na jina na cheo chake na namba zake za ofisini. Alitaka kumpa namba ya simu yake ya mkononi lakini alighairi.

Ray hakutaka kumdokeza Skola kwa namna gani Askofu Ndondo alikuwa anahusika na kuvunjika kwa ndoa yake na Sofia. Aliamua kuweka mambo yake binafsi pembeni lakini siyo pembeni kivile. Aliamua kuwa vyovyote itakavyokuwa atahakikisha anauangusha mti ule wa mbuyu hata kama kwa mikono mitupu. Alijua amepata nafasi ya kumshughulikia mtu ambaye hakuamini anastahili kuitwa “Mtu wa Mungu”. Skola alimpatia sababu kubwa zaidi ya kufanya hivyo.

Skola aliondoka akiwa amepata ahueni kidogo na moyo wake ulifarijika kiasi. Hakujua hata hivyo ni kwa kiasi gani yule mpelelezi angeweza kufanya uchunguzi dhidi ya mtu mzito kama Askofu Damien. Hakutaka kudhania kuwa suala lile litaenda mahali popote. Alivyoondoka alikubali moyoni tu kuwa hata kama jambo lolote halitafanyika lakini siri yake ameifungua kwa mtu mwingine na lolote litakalomtokea alijua kabisa kuwa hatokuwa peke yake. Skola hakutaka kumuambia siri nyingine ambayo ndio ilimlazimisha kwenda polisi siku ile; alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu. Alipanga kumuambia mumewe jioni ya siku ile.

Kitu pekee ambacho Skola hakujua wakati anatoka ofisini kwa Ray na pale Makao Makuu ya Polisi Mkoani ni kuwa alipoingia pale asubuhi ile tu tayari mmoja wa maafisa wa polisi ambaye alikuwa ni muumini wa kanisa la Mavuno na miongoni mwa watu ambao Suku alikuwa anawalipa kuwapenyezea habari zozote za ndani ya Jeshi la Polisi alikuwa ameshampigia simu Suku. Suku alituma ujumbe wa mkononi kwa Askofu ambaye alikuwa anajiandaa na siku ya pili ya mkutano mkubwa wa Injili kule Mwanza na kuulizia kuhusu Skola.

Jibu pekee alilopata kutoka kwa Askofu lilikuwa katika mafumbo.

Kuku apikwe, tutanunua mwingine.

Suku alielewa maana ya ujumbe ule na akapitisha ujumbe kwa mpenyezaji wao ambaye alimwambia kuwa kuku bado yupo bandani. Suku akatuma ujumbe kwa walinzi maalumu wa Askofu Ndondo kule Mloganzila na kuwapa ujumbe wa kwenda haraka iwezekanavyo pale Makao Makuu ya Polisi na kumsubiria Skola atoke. Wakati Skola anatoka na kuingia kwenye gari lake vijana wale walikuwa wanamfuata nyuma kwa pikipiki ya Yamaha XT wakiacha magari mawili tu kati yao na Skola. Skola hakuelekea nyumbani moja kwa moja bali alipita kwenye maduka ya vyakula na kununua vitu vichache hapo huku vijana wakiegesha pikipiki mita chache kumsubiria. Alipotoka hapo aliamua kupitia kwenye studio ambako alikuwa anasubiriwa kwani tangu tukio la kubakwa hakurudi kuendelea na kurekodi albamu yake ya nne. Aliwaambia pale studio kuwa kesho yake atakuwa tayari kurudi kurekodi. Alipotoka hapo alienda benki kuchukua hela kidogo ili baadaye jioni aende kutengeneza nywele zake kwenye Saluni maarufu ya Anti Didah.

Ilikuwa ni wakati anatoka benki, akiwa ameshachukua fedha zake na kuingia ndani ya gari lake na kushika barabara ya Nyerere kuelekea nyumbani kwake ndipo vijana walianza kusogea karibu zaidi. Vijana wale walizidi kusogea karibu. Skola alipofikia maeneo ya TRA kwenye makutano ya barabara ya Nyerere na ile ya Mandela vijana wale walikanyaga mafuta na kulifikia gari la Skola. Walipokuwa naye usawa mmoja yule aliyekuwa nyuma alinyanyuka kidogo huku mkono wake ukiwa umenyanyua bastola ya Glock 19. Skola aligeuka kuangalia upande ule na hakupata hata na nafasi ya kufungua mdomo kushangaa. Hata mlio wa risasi hakuusikia kwani risasi moja ilipita upande wa kushoto wa sikio lake na kupenya upande wa pili na wakati huo huo risasi ya pili ilipasua shingo yake. Gari lake lililokuwa linaenda kasi liliachia njia, na kuyumba karibu mara saba kabla halijagongana na gari jingine lililokuwa linajaribu kumpita na kusababisha kishindo kikubwa. Mlio wa magari mengine yakijaribu kufunga breki kwa ghafla ulipaa angani. harufu ya matairi yaliyochubuka barabarani ikichanganyika na harufu ya petroli iliyomwagika angani iliharibu pua za yeyote aliyekuwa karibu.

Vijana wale wawili walikuwa wameshachomoka na wala hawakusubiri kuona kama kazi yao imefanikiwa au la. Walienda mbali kabisa wakichukua barabara ya Mandela na kutoka huko wakaelekea walipoacha lori lao karibu na kituo cha mabasi Ubungo. Walipakia pikipiki yao kwenye lolir lile la Canter na kama wasio na haraka wakaanza kuondoka mjini kuelekea Mloganzila wakishika barabara ya Morogoro. Kazi waliyotumwa walikuwa wameimaliza. Familia zao zilikuwa zinatarajia fungu zuri la fedha siku inayofuatia.

Pamoja na Skola, watu wengine wawili walikufa kufuatia magari kugongana na wengine kumi walijeruhiwa walipokuwa wanajaribu kutafuta mahali pa kusimama kukwepa magari yaliyokuwa yamevaana. Wengi hawakuona kilichotokea kwani kilitokea kwa haraka sana kama vile kwenye sinema. Wasamaria wema walijitahidi kukimbia kuokoa maisha ya walio kwenye magari yale na kukosekana kwa huduma bora ya uokoaji katika Jiji la Dar kulihakikisha kuwa wahanga wale hawakuwa na nafasi ya kunusurika. Walipoteza damu nyingi pale pale.

Habari za mauaji ya Skola Kanuti zilimfikia Mpelelezi Ray Shaba alipokuwa ametoka tu kwenye kikao kwa Mkuu wa Mkoa. Taarifa zile zilimshtua Ray hadi mifupa. Maswali mengi yalimjia kwa ghafla hasa taarifa za kidaktari zilizoonesha kuwa Skola Kanuti alipigwa risasi mbili. Alitambua mara moja kuwa kitendo cha Skola kwenda Polisi kilikuwa ni sawa na kuweka sahihi hati yake ya kifo. Kilichomsumbua zaidi Ray ni uwezekano wa watu hao kufanya uhalifu mchana kweupe tena kwa kujiamini kiasi hicho. Kwamba, waliweza kutekeleza jambo hilo kwa ufanisi, wakiwa na taarifa za Skola kulimfanya Ray aamini waliohusika walikuwa ni mtandao hatari wa kihalifu.

Aliumia moyoni.

Ray alizungumza na maafisa wa polisi waliokuwa wanafuatilia tukio lile na vile vile madaktari Muhimbili. Wote walimuahidi kumpatia taarifa nyingine zozote mpya mara wakizipata. Hakuweza kuendelea na shughuli zake; alibaki ofisini kuanza kuandaa mkakati kazi wa kushughulikia tukio hilo. Mawazo yake yote yalikuwa kwa Skola Kanuti. Alijisikia hatia kuwa hakumpa ulinzi aliokuwa ameahidi na kuwa hakuchukulia tishio dhidi ya Skola kwa uzito wake uliostahili. Aliapa moyoni kuwa kama kuna deni lolote ambalo angeweza kudaiwa maisha yake yote basi ni kifo cha Skola Kanuti. Kilimshtua, kilimsumbua na kilimuumiza. Alijihisi kutetemeka kama mtu mwenye homa.

Aliapa kulipiza kisasi hata kama ni kwa damu yake.



(Itaendelea)

USIKOSE NAKALA YAKO YA RIWAYA HII YA KUSISIMUA..
(Wasiliana na Paul Mpazi # 763 316 402 kuweka oda yako sasa... wa kwanza kuoda wa kwanza kupewa.
 
Babu asante sana kitabu kinauzwa sh ngapi
Kitakuwa 17,500Tsh... na ndani yake kuna maonjo ya riwaya mpya ya Siku ya Mkosi.. Mswada uko kwa printer sasa hivi; natarajia kabla ya mwisho wa wiki toleo la kwanza litakuwa sokoni...
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom