Riwaya: Mfalme Anataka Kuniua

Mfalme Anataka Kuniua

Sehemu ya 17


Wanaume wawili walikaa pangoni wakitafuna nyama na kugugumia maji kwa wingi. Walizungumza mambo mengi, katika hayo mengi, walicheka mara nyingi navyo vicheko vilisindikizwa na ugongaji wa viganja.

“Hapa ni wapi ndugu yangu, maana naona lakini mpaka sasa sijatambua,” aliuliza Sipe.

“Tupo Pango la kifo…”

“Ati nini?” alidakia Sipe, macho kayatoa na aliyejaa hofu.

“Pango la kifo, pango la mashetani, humu ndimo tulimo.”

“Imewezekanaje?”

“Ni hadithi tu, pango halina mashetani kama watu wanavyoamini kwa miaka mingi. Baada ya kutoroka, nilizungukwa pande zote na askari wenye uchu wa kunikamata na sikuwa na sehemu ya kukimbilia isipokuwa humu ndani ya pango. Siku za mwanzo nilipata shida nikidhani mashetani yangeniua, lakini haijatokea na nimebaini hakuna kitu.”

“Ajabu sana hii…” alisema Sipe akikamata pande la nyama, “Na vipi kuhusu kufungua ardhi katika gereza?”

“Inaonekana pango hili waliishi watu hapo awali, hivyo walitengeneza njia nyingi za kutokea. Sijajua ni kwa namna gani hasa zile pedali hufanya kazi, lakini naamini ile ni kazi ya mwanadamu.”

“Ilikuwaje ukagundua uwepo wa njia hizo za kutokea?”

“Ni matokeo ya safari zangu za uvumbuzi,” alijibu Mako, wote wakaangua kicheko hata meno yakapumzika kwa muda kutafunatafuna.

Walikaa katika pango lile wakizungumza mambo mengi, hata hivyo mambo yahusuyo utawala, yalitawala zaidi mjadala wao. Mwishoni mwa mjadala, walifunga kwa mikasa ya kuchekesha.

“Kula nyama Sipe, endapo ng’ombe huyu ataisha, nitaingia msituni kuwinda. Usiyaogope yajayo.”

“Sina shaka na wewe muwindaji awindaye bila silaha. Ila ninawaza tutakaa humu mpaka lini?”

“Bado sijajua hatma ya kukaa humu, muda ni mwamuzi wa kweli. Tuliache hili, litaamuliwa na muda,” alijibu Mako, akakikamata kibuyu kilichokuwa na mdomo mpana, akamwaga maji katika koo lake nayo yakasafiri taratibu mpaka tumboni kisha akatoa sauti, “Aaaaagh,” huku akikiegemeza kichwa chake katika jiwe laini. Hakuonekana kuchukua nyama, bila shaka alishiba. Tumbo likishiba mdomo husema chochote Mako akasimulia.

“Ndugu yangu Sipe nyama hizi zimenikumbusha mbali sana. Mwaka mmoja nilikwenda jijini Dare kutembea. Huko nikakutana na kasheshe wakati napita njia jioni moja.

Niliona vijana wakibishana katika uwanja wa mpira. Niliamua kusogea kupitia kundi kubwa la watu, ndipo nikawa nimebaini kuwa, vijana wale walikuwa katika ligi ya mpira, na mpira ulifika hatua ya kupiga penati ili kumpata bingwa baada ya kuwa wamecheza kwa takribani dakika tisini bila kumpata mshindi.

Muda ule nafika, penati zilikuwa zimepigwa na ilibaki penati ya mwisho ili kumpata mshindi. Endapo mpigaji wa timu iliyosalia angepata penati hiyo, basi wangeibuka washindi. Na endapo angekosa wangeshindwa hivyo kuendelea kupiga tena. Wachezaji wa timu iliyokuwa zamu yao kupiga waliogopa wote, hakuna aliyekuwa tayari kubeba lawama. Hofu kubwa ilikuwa kwa mashabiki ambao hawakuwa na uvumilivu, mashabiki hawa wangeweza kumdhuru. Hivyo wachezaji wakawa wanatupiana mpira kila mmoja akikataa kupiga.

Basi nilijipenyeza mpaka katika fuko la jezi, haraka nikabadili nguo zangu nikionekana na watu wachache ambao hawakunijali, nikavaa kaptura ya bluu na fulana ya bluu iliyosindikizwa na mistari ya kijivu. Nikafanana kabisa na wachezaji wa timu ile waliokuwa wanaogopa kupiga penati.

Basi nikatembea kwa kujiamini sana mpaka aliposimama refa, nikampokonya mpira kisha nikauweka katika kiduara cha kupiga penati. Mashabiki walishangilia kwa nguvu na wasiohusika wakanipisha nipige penati.

Nyanda wa timu pinzani alikaa golini, nikaweka mpira katikati ya miguu yangu ili nyanda asijue natumia mguu gani. Refa akapuliza kipenga, nikarudi hatua tano nyuma kisha nikaachia shuti kali sana.”

“Nini kikatokea?” Sipe aliuliza, Mako akaendelea. “Nyanda alilala kushoto, mpira ukapita kulia, likawa goli. Watu walishangilia kwelikweli wakiulizana nani kafunga?

Wakati huo, nilikuwa nimevaa zile nguo zangu na nilisimama na kocha wa ile timu ambayo baadae niligundua iliitwa Kukurukakara FC. Nilimsimulia mkasa wangu kocha yule kisha nikamuaga. Baadae nilikuja kusikia kuwa aliandika kitabu kinachoitwa GOLI LA MPITA NJIA.

“Ha ha haaa!” alicheka Sipe, kisha akaongea, “Mako una kamba sana!”

“Mikasa yangu ni ya kusisimua, watu wengi hudhani ni kamba!”

“Umenikumbusha mbali vilevile,” alidakia Sipe, “mwaka mmoja, nilikwenda katika harusi ya rafiki yangu. Harusi ilikuwa ya kifahari sana na ilifika hatua ya bwana Harusi kumfunua Bi Harusi. Yule bwana alimfunua mkewe taratibu, lakini akasema kwa sauti, “Siyo huyu.” Ukumbi ukataharuki. Bwana harusi alidai yule hakuwa bibi Harusi, basi mama yake na Bibi harusi haraka akakimbia nje kisha akarudi na ndoo iliyojaa maji. Bila kupoteza muda, akamnawisha Bi Harusi, baada ya kunawa, jamaa akasema kwa sauti kubwa kuliko mwanzo, “Ni yeyeeeee!” ndoa ikafungwa tukala nyama.

“Ha ha haaaa,” Mako alicheka, “Bibi Harusi alijipamba mpaka jamaa akamsahau. Hatari sana hii, lakini Sipe kamba yako ni ndefu kuliko yangu.”

“Teh! Teh! Teh! Yako ni ndefu zaidi.”

“Unajua Sipe…” Mako alidakia, “Mkasa wako unafanana kidogo na mkasa wa jamaa mmoja alikuwa akioa, sasa Bibi Harusi alipoulizwa kama anakubali kuolewa, akakataa. Jamaa kwa huzuni akaugeukia umati wa watu kisha akauliza, “Yeyote anayetaka kuolewa aje mbele!”

“Ha ha haaaaa! Mako inatosha!” alisema Sipe akicheka kwa kwikwi mpaka mbavu zikauma. Kuona hivyo, Mako akajilaza taratibu huku akimsubiri Sipe kama ataongeza mkasa mwingine au atalala.

Inaendelea Kesho...

Tupate Wadhamini:

Kwa Mahitaji ya kuandikiwa CV, Barua ya Maombi ya Kazi na Masomo kwa Wanafunzi wanaorudia mitihani, Gusa Hapa Tuwasiliane Whatsapp.
Nimeipenda sana hii sehemu

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Mfalme Anataka Kuniua

Sehemu ya 19


Askari wengi walikusanyika katika uwanja wa Ikulu ya mfalme. Kwa ule uoga wao, mfalme aliwaona kama furushi la sisimizi. Basi walizunguka hapa na pale wakijadiliana hili na lile wasiokuwa na dalili za kwenda vitani. Ni katika wakati huo, ilibaki nusu saa, mfalme wa Tukutu ayalete majeshi yake kumuondoa mfalme wa Kanakantale.

Mwishoni mwa njia ya kulia huko pangoni, walisimama Mako na Sipe. Wakajadili jambo kwa muda kisha wakakubaliana kwa kushikana mikono na kutakiana kila la heri. Kisha Mako akaizungusha pedali, mlango ukafunguka, akajivuta juu na kuibukia nje. Sipe aliyebaki shimoni, akazungusha pedali kulifunga pango.

“Waoga nyinyi!” Mako alisema kwa sauti, wote wakageuka kumtazama akiwemo mfalme na mkuu wa majeshi. Hakujali macho yao yaliyojaa hofu, akatembea mpaka kwa askari mmoja aliyempanda farasi, akamnyanyua kwa mikono yake yenye nguvu na kumbwaga chini kama wanaocheza mieleka. “Hustahili kumkalia farasi huyu, askari muoga!” alisema akimpanda farasi, akampapasa singa zake zilizotambaa mgongoni, kisha akasimama juu akiwa kakanyaga pedali na kuanza kuhutubia anayejiamini kama kitoto cha mamba!

“Mnaogopa kufa mkiipigania nchi yenu ya Kanakantale. Ni kipi bora, kufa tukipambana au tuwe watumwa. Tunyanyaswe na kuteswa na Watukutu. Ni ipi faida ya maisha ikiwa yamejaa mateso! Lengo la maisha siyo kuteseka, lengo la maisha ni kuishi kwa usawa na furaha isiyo pimika. Kama maisha yetu yatakuwa ya kutumikishwa kwa maslahi ya watu wengine, tunayo mambo mawili ya kufanya: moja ni kupambana na pili ni kufa. Ni makosa kwa Mwanakantale kuwa mtumwa wa mtu mwingine. Watu wa Kanakantale wako huru kama jua, na yeyote atakayethubutu kusogea, ataungua na kuteketea.”

Mako alipumzika kidogo kuvuta pumzi na kuwatazama askari aliowahutubia. Lakini kumbe sauti yake ilivuta wakazi wengi zaidi wa Kanakantale, basi uwanja wa Ikulu ulijaa wakazi wa kila aina na wengine walikuwa nje ya uzio wakichungulia, Oma alikuwa miongoni mwa waliochungulia. Mako alipoona hivyo, akapandisha morari zaidi na sauti ikawa kubwa.

“Kazi ya askari ni kulinda raia na mali zao. Ni kulinda mipaka ya nchi yetu dhidi ya maadui. Huo ndiyo wajibu. Askari muoga anastahili kufa. Uoga ni jambo baya zaidi linalopaswa kuogopwa pengine kuliko kifo. Kwa sababu ya uoga wenu, watoto wa Kanakantale watakuwa watumwa. Wanawake wetu watabakwa hovyo pia tutapoteza ardhi yetu tuliyorithi kutoka vizazi na vizazi. Kwa sababu ya uoga wenu, mtafanya Kanakantale ifutike katika historia.

“Kwenu askari, bila vita huwezi kumtambua shujaa, hii ni nafasi yenu ya kuonesha ushujaa mlio nao. Shujaa si yule anayewaambia watu wakapigane, bali yule anayepigana mwenyewe.

“Mimi Mako, nakwenda vitani peke yangu, nakwenda kupigana na washenzi Watukutu mpaka tone la mwisho la damu yangu. Nipo tayari kufa ili nikumbukwe kama shujaa, lakini siyo kuishi ili nikumbukwe kama mtumwa na mtu muoga.”

Akiisha kusema hayo, shujaa Mako alimchapa farasi na kuanza kuondoka kuelekea uwanja wa mapambano.

“Mimi nitaungana nawe Mako… nitaipigania nchi yangu mpaka tone la mwisho.” Ilisikika sauti ya Sipe, ambaye alimpanda farasi mkubwa mweupe, kiunoni alificha panga moja katika ala, na mkononi alikuwa na panga moja. Akatembea mpaka alipo Mako na kumpa ile panga moja kisha wakaanza kwenda kupambana.”

“Mimi nitaungana nanyi!” ilisikika sauti ya mzee, Mfalme wa Kanakantale alisema akilengwa na machozi. Kama alivyofanya Mako, Mfalme, alimfuata askari mmoja aliyepanda farasi na kumtupa chini kama wanaocheza mieleka. Kisha akamwambia, “Muoga wewe!”

“Mimi nitaungana nanyi!” Mkuu wa Majeshi alisema kwa sauti. Basi akafuatiwa na askari wote ambao hatimaye walikubali kwenda vitani kupambana na Watukutu.

Iliamuliwa kwamba, haingekuwa salama kwa mfalme kwenda vitani. Japo mfalme wa Tukutu alikuwa pamoja na jeshi lake, halikuwa jambo la kuiga kwa mfalme wa Kanakantale naye kufanya hivyo. Basi mfalme aliombwa abaki ikulu akilindwa na askari watatu tu ambao walikuwa Mkuu wa majeshi, Mpambe mmoja mwaminifu na Sipe. Sipe lilikuwa pendekezo la Mako. Mako alitoa hoja kuwa, Sipe anaifahamu sehemu ya kumficha Mfalme endapo maji yangekorogeka.

“Bila shaka shimo lipo wazi pale. Basi hakikisha panajengewa kitu ili kuzuia yeyote kubaini, hali ikiwa ngumu muingize mfalme bila kumwambia ni wapi mahali hapo. Tukishinda vita, zungusha pedali kuufunga mlango na ibaki siri yetu wawili kwani hakuna faida yoyote watu wote wakijua.” alinong’ona Mako, naye Sipe akakubali na kumtakia kila la heri rafiki yake huyo.

Inaendelea Kesho...

Tupate Wadhamini:

Kwa Mahitaji ya kuandikiwa CV, Barua ya Maombi ya Kazi na Masomo kwa Wanafunzi wanaorudia mitihani, Gusa Hapa Tuwasiliane Whatsapp.
Nakufatilia sana
 
Duh mtuhumiwa wa adhabu ya kifo anaenda kuokoa jahazi la nchi nzima
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom