RIWAYA.MASHARIKI YA MBALI

HaMachiach

JF-Expert Member
Dec 15, 2015
3,399
6,077
RIWAYA: MASHARIKI YA MBALI
KALAMU YA: George Iron Mosenya

SEHEMU YA KWANZA.

Hekaheka zilizoanza takribani majuma mawili na nusu nyuma, zilikuwa zimechochea moto katika siku hii. Ikiwa ni siku moja tu kabla ya tukio lililoleta hekaheka hizo.
Katika jiji la Mainstream kilichokuwa kinazungumzwa zaidi ni kuhusiana na maandamano ya amani kupinga uteuzi wa waziri mkuu ambaye alikuwa akijihusisha na vitendo vya kishoga waziwazi. Licha ya kwamba sheria ya nchi yao iliruhusu uhalali wa vitendo vya ushoga bado wananchi hawakuridhia kabisa kuwa na waziri mkuu shoga. Walikuwa radhi kuishi na mashoga mtaani lakini sio kuwaona katika magari ya serikali wakitimiza wajibu wao.
Walishindwa kutimiza wajibu wao wa kuwa wanaume wataweza kutimiza wajibu wao kama viongozi? Hili lilikuwa swali kuu.

Baada ya kuhamasishana kwa takribani majuma mawili kwa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Maandamano haya yalikuwa habari kubwa sana nchini Semedari.
Mitaa ilingoja kwa hamu sana kuishuhudia siku hiyo ambayo waziri mkuu angepaswa kung’atuka kwa namna yoyote ile. Huku Mashoga na wanaoongoza taasisi zao wakifanya dua zao maandamano yale yasifanikiwe wabaki kuwa na waziri mkuu aliye upande wao.
Siku zikahesabika na hatimaye ikabaki siku moja tu.
Na sasa yalikuwa ni masaa.
_____

Daniel katunzi alikuwa amejifungia chumbani kwake tumbo likiwa linamuuma kwa juhudina kichwa kikigonga kwa fujo sana.
Hakuwa Daniel yule mchangamfu, huyu wa siku hii alikuwa amepooza sana. Wanafamilia kwa ujumla walitambua hali hii na kuhisi huenda anaumwa.
Lakini Daniel ni wa kushindwa kusema angali anaumwa? Hili lilikuwa swali la kila mmoja kujiuliza……
Haikuwa kawaida yake hata kidogo.

Akiwa chumbani Daniel alishindwa kulala kama alivyokuwa ameaga baada ya kushindwa kumaliza chakula, usingizi ulipaa mbali naye.
Alijigeuza huku na kule na kisha akaamua kuufungua mlango na kurejea tena sebuleni.
Chumbani palikuwa hapakaliki!!
Aliikuta familia nzima ikiwa imepooza…. Chakula kikiwa kama alivyokiacha.
“Dany.. unaumwa kijana wangu.” Mama wa familia ile aitwaye Diana alimuuliza kwa upole.
Ni kama swali hilo aliuliza kwa niaba ya familia nzima kwani kila mmoja alitikisa kichwa kuunga mkono.
“Kichwa kinaniuma sana. Na tumbo pia… lakini si kwamba ninaumwa.” Alijibu Daniel Katunzi kwa unyonge.
Jibu lile likawa moja kati ya mastaajabisho ya usiku ule.
Ati! Anaumwa lakini haumwi.
“Unamaanisha nini?”
“Ni kichwa kinauma na tumbo pia lakini mimi najua siumwi.” Alijibu huku akijibweteka katika kochi kubwa la kustarehe lililokuwa jirani naye. Likanesanesa kisha likatulia naye akatulia tuli.
“Kesho nd’o ile siku nadhani.” Alizungumza bila kujulikana kama anauliza ama anaanza kujenga hoja.
“Ndio Dany, kesho tunaingia barabarani… kila mmoja ameandaa bango lake nawe tumekuandalia moja utajichagulia lolote la kuandika. Ikiwa afya itaruhusu basi tutaenda wote. Tena kuandamana ni mazoezi… maana utatembea kidogo walau nawe uuone mji wetu ukijaa watu unavyokuwa. Uone wanavyotabasamu…” Maria, Binti mdogo katika familia ile ya watoto watatu alijibu kwa uchangamfu mkubwa.
“Tabasamu?” Dany alishtuka.
“Mazoezi?” akaujazia uzito mshtuko wake. Na hapo akaketi vyema akiwa anawashangaa wanaomshangaa yeye.
Wakashangaana!
“Napenda kuwashauri tubaki ndani tusiende katika maandamano hayo…” alizungumza akiwa katika mchanganyiko wa huzuni na fadhaa.
“Whaaat! Huo ni usaliti…. Familia yangu haiwezi kufanya dhambi hiyo…” Diana. Mama wa familia aling’aka akiwa wima.
“Daniel…”… Maria alimuita kwa unyonge lakini asiweze kusema lolote hata Daniel alipomtazama.
“Si chini ya miaka mitano ama sita imepita. Lakini kamwe sijaisahau Mashariki ya mbali. Mashariki inayokaliwa na raia kama mimi ambao akili zetu zimeruka na kukaa mashariki, ubongo umelalia mashariki bila kujua magharibi ni wapi sahau kuhusu kusini……” akaweka kituo akameza funda la mate na kuketi vyema akiwa anatazama chini.
“Hali ilikuwa kama hii niionayo kwenu, lakini sababu zetu zilikuwa tofauti. Naona yenu ni sababu dhaifu sana……”
“Sababu dhaifu! Una maana gani, yaani tunaongozwa na waziri aliyeolewa na mwanaume mwenzake halafu unasema ni sababu dhaifu. Semedari ni nchi kubwa sana kiuchumi duniani, haipaswi kuongozwa na mtu dhaifu….” Danstani alizungumza kwa mara ya kwanza katika hali ya kufoka. Huyu akiwa ni kijana mkubwa wa Diana.

DANIEL ANASIMULIA
Tembo walivamia kijiji cha Mafisa, huko Mashariki ya mbali ninapotoka. Uvamizi wao wa kwanza ulianza kwa kuharibu mazao. Wananchi walioharibiwa mashamba wakatoa taarifa katika serikali ya mtaa juu ya hili. Afisa wa serikali ya mitaa yeye hana shamba hivyo hakuguswa na habari hii, akaipokea taarifa na kuiweka katika meza yake kama taarifa isiyokuwa ya msingi. Mashamba yaliendelea kuharibiwa…. Tembo ni mnyama na hana akili…. Alipomalizana na mashamba akaanza kudhuru watu. Watoto wawili walikanyagwa na tembo na kupoteza maisha. Kwa sababu wale watoto hawakuwa wa afisa wa kata aliipokea taarifa na kuiweka katika meza yake kama taarifa ya ziada. Lakini usoni akihuzunika na kutoa pole za dhati kwa wafiwa.
Huzuni ya kinafiki!!
Mtoa taarifa akarejea baada ya siku nne kuulizia maendeleo yoyote kuhusu kuchukua hatua za kiusalama. Afisa akadai kuwa kwa takribani juma zima simu yake haina pesa za kupiga wala kutuma meseji (SMS). Na hapo akaanza kulalamika kuwa mtoa taarifa si mzalendo kabisa, ametoa taarifa lakini hakulipia hata senti tano ya kuchangia wino wa kujaza katika muhuri. Afisa akaenda mbali na kusema kuwa wananchi wanajitazama wao pekee wakipatwa na matatizo lakini hawatazami upande mwingine wa shilingi. Na hapo akatoa hitimisho kuwa wapambane na hao tembo kama watawaweza.
Mtoa taarifa akaondoka akiwa mwenye huzuni sana akawafikishia wakulima wenzake na wananchi waliokuwa katika kijiwe hicho.
Wananchi wakashangazwa sana na majibu yale, kwa jinsi walivyovimba kwa jazba hawakutaka kungoja. Wakaondoka kuelekea nyumbani kwa afisa huyo.
Hawakumkuta ofisini wakamfuata nyumbani kwake. Wakamfokea kwa maneno makali hasahasa ya kulewa madaraka yale madogo na kuwasahau wananchi.
Wakaondoka na jazba zao na kuhamasishana kuwa hawana mtetezi basi watalazimika kujiunda vikundi vikundi na kuyalinda mashamba yao pamoja na familia kwa ujumla.
La mgambo likalia na jambo lenyewe likatangazwa.
Baada ya siku mbili tembo wawili waliuwawa.
Na punde baada ya tembo wawili kuuwawa serikali ikahamia katika kijiji cha Mafisa. Walipouwawa watoto wawili serikali haikutokea hata msibani lakini tembo walipouwawa ikajaa pale kijijini na msako ukaanza wa nani aliwaua tembo.
Afisa wa kijiji kile alipofuatwa akawataja wahusika kuwa ni wale waliomfuata nyumbani na kumfokea, akawapatia majina ya wale waliomwandikia barua mbili ofisi kumpatia taarifa kuwa wamevamiwa na tembo.
Haraka sana wakakamatwa na kudhalilishwa mbele ya familia zao. Ilikuwa ni usiku wengine wakiwa uchi wa mnyama na wengine wakiwa na nguo fupi za kulalia.
Walipigwa sana huku wakishutumiwa kuwa wao ni wawindaji haramu.
Uharamu huo nd’o hatukuwahi kuufahamu, tembo hakung’olewa jino wala pembe yake….. aliuwawa tu.
Mmoja kati ya wale watuhumiwa alipoteza maisha akiwa rumande, polisi wakamtupa mitaroni na kudai kuwa alifanya jaribio la kutoroka wakapambana naye….. nchi ikasikia juu ya wengine sita kuwa wapo ndani na wana majeraha makubwa sana.
Kilio cha Mafisa kikadondosha chozi lake katika ardhi nzima ya Mashariki ya mbali.
Wananchi wakaanza kuhamasishana kuhusu maandamano ya amani kuhakikisha wakazi wale wa Mafisa wanaipata haki yao.
Kilichotokea nd’o kinachoniumiza kichwa hadi leo.
Hatukuwa na silaha, tulijitahidi hata tusitembee na kalamu mifukoni wasije wakasema ni visu vya kisasa. Hata waliokuwa na nywele ndefu tuliwaambia wazinyoe maana hawakawii kusema kuwa lile lundo la nywele limeficha bangi ndani yake.
Tulihakikisha maandamo yetu yanakuwa swafi kuliko namna tujiwekavyo kila tuendapo katika ibada.
Ule usafi tuliojitahidi uwe ukatuachia doa. Ilikuwa ni bahati sana ukivunjwa na kuachwa hai, kuna waliotolewa macho na hadi sasa wanamshukuru Mungu kwa kuwatetea…..
Kama mtu anamshukuru Mungu kwa kung’olewa jicho pekee. Jiulize wasioshukuru ni kipi ,kiliwasibu?
Nilikuwa naziona vita katika runinga lakini kule mashariki ya mbali nilijiona nipo katika vita, niliuona mlipuko wa mabomu na niliona kwa macho na sikio langu lilisikia mtu akiwa anataka kukata roho lugha mpya anayoiongea inavyoumiza kusikiliza hata kama hauelewi asemacho.
Mashariki ya mbali tuliuwawa kwa kujaribu tu kuwatetea wale waliokuwa wanafia rumande bila hatia. Na sio kwamba sisi tulitaka waachiwe huru la! Sisi tulitaka watibiwe wasije kufia rumande kama wenzao. Hilo tu!!!
Nikisema sababu yenu ni dhaifu msinihesabu kama muoga.
Nilishiriki maandamano yale ya amani ambayo yaligeuka vita kati ya wenye silaha na wasiokuwa nazo.
Kwa kifupi huko mashariki ya mbali tulipigana vita ya uonevu.
Shangazi yangu mpole kabisa alikamatwa akiwa katika mgahawa wake na mtoto wake mdogo mgongoni alipigwa na kupoteza maisha mbele ya mtoto wake. Kisa ni cha kuchekesha…..
Alikuwa anamwaga maji barabarani, bahati mbaya iliyoje yale maji yaliyokuwa na masalia kidogo ya ukoko wa ubwabwa yakalifikia gari la polisi lililokuwa likikatiza.
Wakasimamisha gari ghafla na kumvamia wakimlazimisha alioshe gari lile kwa sababu ana dharau.
Shangazi akalifuta gari pale palipoguswa na ukoko, wakamlazimisha aoshe gari lote.
Shangazi akahoji kwanini wanamfanyia vile angali amesema ni bahati mbaya.
Na hata kabla hawajamjibu mtoto wake akaanza kulia, shangazi akamjali mwanaye na hiyo kwao wakaitafsiri kama dharau kwao.
Shangazi aliuwawa!
Naomba muamini kuwa sababu yenu ya kesho ni dhaifu sana.
___________

Ilikuwa ni simulizi ya dakika ishirini na tano, simulizi iliyojenga ukimya wa hali ya juu. Na hata Daniel alipokinyanyua kichwa chake alikutana na uso wa Diana ukiwa umelowana kwa machozi, Maria alikuwa ameuficha uso wake, Danstan alikuwa anajikaza kiume kwa kung’atang’ata meno yake.
“Serikali ilitoa tamko gani kwa ukatili huo” Danstani aliuliza huku akionyesha jazba za waziwazi.
“What’s the https://jamii.app/JFUserGuide!! Ingetoa tamko gani Danstani, labda ingetangaza kuwa IMESHINDA VITA kwa kishindo..” Diana alizungumza huku akishindwa kudhibiti hamaniko lake.
“Daniel mwanangu. Huku kwetu hakuna kitu kama hicho. Tuna uhuru asilimia 100 wa kufanya maandamano kwa lolote ambalo tunaona kwamba halipo sawa. Ni wajibu wetu kuikumbusha serikali kuwa wananchi ni moja ya nguzo kuu katika serikali na tunapaswa kuiwajibisha serikali yetu kila inapokwenda njia isiyokuwa sahihi na bunge likiwa kimya.” Diana alimgeukia Daniel na kutoa ufafanuzi.
Akatoa ufafanuzi zaidi kwa kutoa mifano yakinifu ya matukio kadha wa kadha yaliyowahi kutokea nchini humo.
“Daniel na bado kila siku unasisitiza kuwa unahitaji kurudi Mashariki ya mbali.” Maria alimuuliza kwa unyonge sana.
“Hakika natamani sana kurudi Mashariki ya mbali. Ni huko nilipozaliwa na nitarejea. Si kwa sababu za kuibadilisha nchi bali kula kwa pamoja raha na karaha za ardhi ile.”
“Raha? Kuna raha gani katika nchi inayoua raia wake sasa…” Diana aling’aka
“Juma lililopita nakumbuka niliwasikia mkizungumzia juu ya waziri wa nishati aliyejiuzuru baada ya umeme kukatika bungeni kwa muda wa dakika tano.
Kule kwetu kuna raha ya aina yake, na raha nyingi tunazozipata husababishwa na karaha tunazopitia. Kule kwetu tukisikia waziri kama huyo aliyejiuzuru eti kisa dakika tano kwetu ni kichekesho kikubwa sana, na kwanza ni uzembe mno wa kimaamuzi. Umeme unakatwa kwa siku tatu mfululizo na waziri anapita tunapungia mkono kwa shangwe… sio raha hizo?
Katika hizo siku tatu umeme unapokatika tunatoa kila aina mpya ya matusi kwa taasisi husika, lakini hayo matusi tunaambizana sisi kwa sisi sio kwamba tunawatukana wao. Bado tu huioni raha?
Baada ya hizo siku tatu za umeme kukatika pindi utakaporejea tunaungana kwa pamoja nchi nzima, akina baba kina mama na watoto tunasema kwa pamoja ‘HUOO’. Hujapata tu sababu ya kufurahi?
Na kisha kila mmoja anaendelea na maisha yake, matusi yanaishia hewani na hatutukani tena. Ukijifanya unaendelea kutukana angali umeme umerejea watu wanabaki kukushangaa.
Lazima nitarejea Mashariki ya mbali.” Daniel aliweka kituo katika simulizi yake.
Nyuso za tabasamu zikatawala nyumba ile, Daniel alikuwa amewapa sababu mbili kwa pamoja. Kwanza aliwatupa katika msiba na vilio kisha akazisafisha nyuso zao na tabasamu japo lilikuwa tabasamu la karaha.
Wakaagana kwa mara nyingine wakikiacha kile chakula mezani na kila mmoja kwenda katika chumba chake kuuchapa usingizi.
Akiwa chumbani kaka mkubwa katika familia ile, Danstan alianza kuingiwa na ushawishi wa kuitembelea Mashariki ya mbali.
Hakujua nini maana ya tamanio lake hilo.

NAAAM! RIWAYA hii ya Mashariki ya bali itakuwa ikikujia muda na wakati kama huu kila siku mpaka itakapotimu tamati yake…….
Maoni yako ni muhimu sana!!
 
Good job Mkuu,imeanza vizuri naamini itakua kali sana mbele. Keep it up.

Kana kane ni kamo
 
RIWAYA: MASHARIKI YA MBALI
KALAMU YA: George Iron Mosenya

SEHEMU YA PILI

KATIKA SEHEMU YA KWANZA:
Daniel katunzi katika hofu kuu ya kushiriki maandamano katika nchi ya kigeni, anahisi yaliyowahi kutokea Mashariki ya mbali yanaweza kujiri tena huku. Wenyeji wanastaajabu… lakini anapowasimulia juu ya mashariki ya mbali… hali inabadilika….

ENDELEA
MAJIRA ya saa nne na nusu usiku, Danstani alitoka chumbani kwake na kwenda katika chumba cha Daniel Katunzi.
Alikuwa amejaribu sana kupambana na tafakuri nzito juu ya nchi iitwayo Mashariki ya mbali…..
Akiwa ni mwanafunzi wa chuo kikuu katika masomo ya utabibu na afya ya mwanadamu, simulizi ya Mashariki ya mbali ilianza kukichanganya kichwa chake.
Kwa muda ule mfupi tangu waachane na Daniel kisha kila mmoja kuingia kulala ili kuikaribisha ile siku ya maandamano tayari Danstani alikuwa ameingia mtandaoni na kujaribu kuitafuta historia ya nchi hiyo ya Mashariki ya mbali. Alichoambulia kukutana nacho ni habari njema kuhusu nchi hiyo kubwa.
Akajiuliza. “Yale aliyotusimulia Daniel, ameyatoa wapi?”
Swali hili likamwacha katika njia panda. Akapigia mstari kuwa yawezekana Daniel hayupo sawa kiakili, na ilikuwa ni jambo la hatari sana kuishi katika nyumba moja na mtu ambaye akili yake ina walakini, husussani katika familia ile ambayo kuna watoto wadogo pia.
Danstan akamkuta Daniel akiwa yungali macho bado.
“Haujalala Daniel.” Alizungumza huku akiliendea kochi na kuketi.
“Ooh! Nimelala tayari, ni usingizi tu haujaamua kunitembelea bro.” alimjibu kiutani huku akiketi kitandani ili kumkaribu mgeni wake vyema.
Danstan hakutaka kuzunguka sana, akamuuliza Daniel kwa utulivu sana juu ya nchi aliyoisimulia.
“Unakumbuka umetoka nchi hiyo lini?”
“Hapana sikumbuki.”
“Unamkumbuka raisi wa nchi yako wakati unaondoka?”
“Namkumbuka kwa jina mpaka sura yake….” Alijibu kwa kujiamini.
“Kwanini imekuwa rahisi kumkumba raisi kuliko mwaka ulioondoka huko?”
“Mashariki ya mbali pia kuna chaguzi kama nionavyo katika nchi yenu hii. Lakini uchaguzi wa kule ni wa aina yake, una vibweka vya kila aina. Lakini namkumbuka vyema kwa sura na majina kwa sababu ya mama yangu.” Akavuta pumzi na kumeza mate kisha akaendelea kusimulia.

DANIEL ANASIMULIA

Iwe katika kuuza bagia zake na visheti, iwe katika kuuza pombe zake za kienyeji, iwe katika kutupikia chakula na iwe katika kulala. Mama yangu alikuwa anafanya kampeni kubwa sana juu ya raisi na mbunge wa chama ambacho baadaye ndicho kilikuja kuchukua ushindi.
Aliwaimbgia walevi nyimbo za kukisifu chama, tulipolalamika kuwa hatuna viatu vya shule alicheka na uso wake ukionyesha nuru. Akatumia dakika kumi kukisifu chama na kutueleza kuwa raisi atakayeingia madarakani atatununulia viatu na pia ameahidi kutoa magari ya kutupeleka shuleni. Neno lake lilikuwa moja tu “VUMILIENI WANANGU MTASOMA KAMA MALAIKA”.
Tuliendelea kusubiri naye aliendelea kupiga kampeni kwa juhudi. Naikumbuka kanga jozi moja aliyopewa na mgombea udiwani huku wakikumbatiana.
Mama yangu hakuishia hizo kampeni za chinichini, hata kwenye majukwaa mama yangu aliitwa kwa heshima zote na kwenda kucheza ngoma za kijadi huku akiimba nyimbo za kukisifu chama.
Hatimaye jua la uchaguzi likachomoza na kisha wakati ile rangi ya udhurungi ya kumaanisha linazama matokeo ya uchaguzi yalianza kuonyesha ishara ya nani mshindi.
Na baada ya siku tatu matokeo yalikuwa tayari. Ikawa ni wakati wa mama kupumzika na kuingoja neema ya sisi kuishi na kusoma kama malaika.
Uhalisia ulioonekana mwanzo ukageuka mazingaombwe, diwani akabaki kuwa mwanakijiji aliyetingwa kupita wote sio yule aliyekuwa anakuja nyumbani hadi tunasonga ugali na kula pamoja. Mbunge yeye mara ya mwisho nilimwona katika luninga, sahau kuhusu raisi.
Lakini kutoweka kwao sio tatizo, ila kilichotushtua ni kwamba waliishi na sisi wakati mama anauza pombe zakienyeji na kuwachezea ngoma majukwaani.
Walipoyashika madaraka ghafla ile pombe ikawa haramu.
Mama yangu akakamatwa kwa amri ya diwani kuwa anauza pombe za kienyeji zinazosababisha watu wawe legelege na kushindwa kwenda kazini.
Nakumbuka sura ya mama yangu siku anatolewa mahabusu, ikiwa ni baada ya msoto wa siku tatu mfululizo bila dhamana.
Alitoka akiwa amekonda sana.
Na alipotoka alikuwa amevaa kanga yake ileile ambayo mbele ina picha ua raisi na nyuma picha ya diwani.
Alinitazama kwa muda kabla chozi la uchungu halijaanza kumwagika, nilimkimbilia na kumkumbatia.
Akaninong’oneza.
“Laiti kama ingekuwa ndani ya uwezo wangu ningezivua hizi kanga muda huu na kuzichoma moto. Nimeonewa mwanangu!” alizungumza kwa hisia kali.
Tulirejea hadi nyumbani.
Kwa sababu mama ndiye pekee wa kuitazama familia alilazimika kutafuta kitega uchumi kingine.
Akaanza kukata miti na kuikausha kisha kuiuza kama kuni. Ilikuwa shughuli pevu lakini ililazimika tuifanye.
Hatukutulia sana kabla hayajatokea mauzauza mengine, barua ya kuitwa katika uongozi wa kitongoji.
Mama akaelezwa kuwa anapewa onyo la kuacha kukata miti hovyo kwani anaharibu uoto wa asili.
Uoto wa asili? Tulistaajabu, yaani kijiji chetu tumeishi hivyo kwa miaka nenda rudi tukitegemea miti ile kwa ajili ya kuni leo hii imekuwa uharibifu wa uoto wa asili?
Mama akatii! Lakini ajabu alikuja kukamatwa tena siku nne baadaye japokuwa safari hii hakulazwa mahabusu.
Mama akakosa pa kuegemea na magonjwa nayo yakaitumia fursa ile kumtembelea. Alipozidiwa sana akaniagiza kwa diwani nikamweleze kuwa ‘yule mama mcheza ngoma wakati wa kampeni anaumwa’. Mama alinisisitiza nitumie kauli ile huenda diwani amelisahau jina lake lakini sio kusahau alichotenda.
Nilifanikiwa kuonana na diwani yule mjivuni wa tabia. Akanisikiliza huku anachezea simu yake. Kisha akanieleza kuwa yapaswa tumpeleke mama hospitali maana akisema aanze kutumia ofisi yake kusikiliza ripoti za wagonjwa basi hospitali haitakuwa na kazi.
“Halafu mimi nilisomea mambo ya uongozi na utawala sio madawa na tiba asilia.” Alimalizia kwa kauli ile njema kwake, mwiba katika moyo wangu.
Nikiwa kama mwendawazimu nilienda hadi kwa mama na kumweleza kilichojiri.
Nadhani nilifanya makosa makubwa, lakini yalikuwa mazito sana yale, nisingeweza kuhimili.
Baada ya siku mbili mama alitoweka.
Tulianza kumtafuta huku na kule.
Mwisho tulimkuta akiwa katika poro lile tulilokatazwa kukata vijimiti tu kwa ajili ya kuni.
Hakuwa katika shughuli ya kukata kuni, safari hii alipanda hadi juu ya mti kabisa na kisha kwa kutumia kanga zile zilizochapishwa picha ya raisi na diwani wake na maneno ya sifa kwa chama.
Mama alitumia kanga zile kujinyonga mpaka kupoteza maisha.
Niliziona zile kanga, niliziona katika mwili wa marehemu mama.
Nilipotoka ni mbali sana, Mashariki ya mbali. Lakini nitasahau mengi mno, sio sura ya raisi yule mwenye tabasamu la mauti na diwani wake yule wakala wa kifo na mateso. Diwani mnafiki ambaye jamii ikamruhusu naye kusema neno katika siku ya maziko ya mama yangu.
Akaongea kwa uchungu mkuu huku akitumia kitambaa chake kujifuta machozi, akasema kuwa mama yangu alikuwa ‘mfia chama’ na atakumbukwa sana kwa wema wake.
Hata leo nikiiona kanga inayofanania na ile nitaitambua bila kutumia sekunde kumi kufikiri.
Mama yangu alidhulumiwa uhai wake na watu aliowathamini kwa dhati angali wao wakimthamini kwa unafiki.
Ile dhuluma ilikuwa moja ya sababu zangu za kuikimbia Mashariki ya mbali.

_________

Daniel alimaliza kusimulia mkasa ule akiwa ameketi palepale kitandani.
Danstan akasimama na kumfuata pale kitandani, akampigapiga bega kumpa pole huku akimwomba radhi kwa kumkumbusha yote yaliyojiri huko Mashariki ya mbali.
“Natamani sana kwenda kuitembelea nchi hiyo…” Danstani aliongezea.
“Kwa maisha yenu haya ya milo sita kwa siku utapaweza kweli kule?” Daniel alimuuliza kwa upole.
“Mimi ni imara sana Dany, usinione hivyo. Mimi naweza kukaa hata siku nzima bila kula au nakula mara moja tu. Sitashindwa kitu….” Alijitapa Danstani.
Daniel akacheka sana kabla hajajilaza kitandani.
“Hauamini nisemacho ama… mbona unacheka.” Alihamaki.
“Nenda ukalale kwanza. Tukimaliza maandamano ya kesho unieleze tena kama unayo nia ya dhati. Ukimaanisha nitakusindikiza Mashariki ya mbali.” Daniel Katunzi alimaliza na kumuaga Danstan McDonald kijana mkubwa wa familia ile ya nchini Semedari katika jiji la Mainstream.
Danstan alipondoka, Daniel akajisemea kwa sauti ya chini.
“Kutokula siku moja ama kula mlo mmoja huyu bwana cheupe ndo anauita ujasiri. Ama kweli tembea uyaone. Karibu sana Mashariki ya Mbali Danstan McDonald”

#RIWAYA ya Mashariki ya mbali inaendelea, je? Daniel alifika vipi Semedari kutoka Mashariki ya mbali…. Na je? Nia ya Danstan kuitembelea nchi hiyo itatimia….
Tukutane tena kesho katika mwendelezo wa riwaya hii ya aina yake…..
 
RIWAYA: MASHARIKI YA MBALI
KALAMU YA: George Iron Mosenya

SEHEMU YA TATU

Goodmorning Semedari!
Ndivyo anga lingeweza kusema tena kwa uchangamfu, Semedari ilipokea mawio katika namna ya kutia tumaini, katika jiji la Mainstream ilipokuwa inaishi familia ya bibi Diana pamoja na mgeni wao Daniel, ambaye sasa hakuwa mgeni tena bali mwanafamilia kutoka Mashariki ya mbali huku napo kila mmoja alikuwa amebeba bango lake tayari kwa kuingia katika maandamano ya kitaifa kumpinga waziri mkuu anayejihusisha na masuala ya kishoga.
Ile hali ya Semedari kiujumla ilimshangaza Daniel, hapo awali alipokuwa anawaona askari alikuwa anaiandaa miguu yake kwa ajili ya kukimbia.
Ajabu na kweli! Askari waliwapungia mkono waandamanaji.
Uhuru wa aina gani huu! Alistaajabia huku akiendelea kufuata mkumbo.
“Daniel!” Danstan, kijana mkubwa wa familia hii alimwita huku akimshika mkono kumaanisha apunguze mwendo.
Daniel akatii, Danstani akamwinamia kidogo na kumweleza kwa kunong’ona.
“Unawaona hao wanaume watatu mbele yetu”
“Nawaona, si hao waliovaa masweta…”
“Ehee!! Huyo wa kushoto na huyo wa katikati nikikwambia dhamana zao hapa jijini huwezi amini na wao wameshirikiana na sisi. Nd’o maana nilikwambia hili jambo ni kubwa sana Dany…..kubwa sana” Danstan alizungumza kwa bashasha ya aina yake huku akionyesha dhahiri kuwa kila anachokizungumza anakifurahia kutoka moyoni.
“Ni akina nani?” Daniel katunzi mmoja kati ya waandamanaji wachache weusi aliuliza ili ajibiwe maana Danstan alionyesha kulingoja hilo.
“Ni waalimu!!” alisema kwa kushtukiza ili auone mshtuko wa Daniel.
Kweli Daniel akashtuka!
Danstani akabaki kuishi katika tabasamu zito la ushindi wakati anautazama mshtuko ule.
“Jiulize, waalimu na wao wameguswa wamekuja kuandamana na wananchi. Halafu useme kuwa hili jambo ni dogo, huyu mpuuzi lazima ang’oke!” sasa aliongea kwa hisia kali zaidi zilizokaribia kuwa hasira.
“Ni waalimu wa chuo kikuu bila shaka.” Alijazia maongezi Daniel katika namna ya kuuliza swali lenye jibu tayari.
“Hapana, mmoja anafundisha shule anayosoma Maria ni shule ya msingi na huyu mwingine ni wa hatua ya awali. Anapendwa sana hapa mainstream na anaheshimika… unajua mwalimu ni mzazi namba mbili kwa mwanao.” Akaweka kituo kama mtu asiyetarajia upinzani wowote.
Daniel akatikisa kichwa akiwa anasikitika.
“Tunaweza kupata nafasi ya kuzungumza tukiwa katika treni?” Daniel alimtupia swali.
“Haswaa! Bila shaka.”
“Basi tutazungumza.”
_____

Baada ya dakika kadhaa tayari walikuwa ndani ya treni ya umeme kuelekea katika eneo la makutano kwa ajili ya maandamano ya amani.

DANIEL ANASIMULIA.
Unavyozungumzia waalimu, ama kuwa mwalimu…. Huko Mashariki ya mbali baada ya miaka kadhaa neno ‘mwalimu’ linaweza kuwa mojawapo kati ya tusi la kutosha kumtia mtu hasira akarusha konde. Ukiachana na matusi yaliyozoeleka ya kutukaniwa tupu ya mama yako katika namna ya mzaha na haukasiriki.
Tupu ya mama ni jambo la kawaida sana Mashariki ya mbali.
Sitaki kuamini katika simulizi za zamani nilizowahi kuzisikia eti kuwa kuna kipindi waalimu waliwahi kuwa watu muhimu katika nchi ile.
Kwa sababu sihitaji ulaghai uliojaa katika historia zisizo’maana basi ni heri nikuelezee niliyoyashuhudia tu katika kizazi nilichokiacha huko Mashariki ya mbali.
Maelfu ya watu ambao ni waalimu wanajificha katika kujitambulisha kwa sababu ukiwa mwalimu unaweza ukakosa mke unayemuhitaji na badala yake ukapata mke atakayekusaidia kutimiza maandiko ya nendeni mkazaane muujaze ulimwengu.
Ukiwa mwalimu kuna baadhi ya wadogo zako hawatakanyaga nyumbani kwako kwa lengo la kuja kuimalizia likizo yao huko. Ukiona amekuja ni aidha amekosa pahali pa kwenda, ama la anatimiza usemi usemao kuwa damu ni nzito kuliko maji.
Yaani hata watoto wadogo wanafahamu kuwa ualimu ni ugonjwa!!
Ukiwa mwalimu jiandae kuishi maisha ya mashaka ya kutoijua kesho yako. Huku serikali haijakupa ongezeko la mshahara angali unazidi kuukaribia uzee na hakuna ulichofanya, na huku wanafunzi wanakusubiri mtaani wakuponde mawe kwa sababu uliwacharaza bakora walipofanya makosa shuleni, na hapa unapaswa kuvumilia kuhusu majina ya kishenzi watakayokuwa wamekubandika bila sababu za msingi.
Danstan! Hebu fikiria, mwanafunzi ambaye wewe mwalimu ni sawa na baba yake, anakitazama kichwa chako jinsi ulivyo mweusi na kisha anaweka kikao cha dharula na wanafunzi wenzake wanakubandika jina wanakuita ‘KOBOKO’.
Huyu anayefanya hivi ni mtoto unayeweza kumzaa.
Waalimu wa kike wanaipata shughuli zaidi; huku kwenu naona wanafunzi wana miili mikubwa lakini wana nidhamu.
Huko mashariki ya mbali, mwanafunzi ana mwili mkubwa, akili za kupima kichwani na bado nidhamu hana.
Mwanafunzi kama huyu anaenda kumtaka kimapenzi mwalimu wake wa kike.
Nidhamu ipo wapi!
Sawa, tuseme kuwa haya yanaweza kuvumilika. Vipi kuhusu kuingizwa kinguvunguvu katika siasa, yaani mshahara hauongezwi, lakini wakati wa mambo yao ya siasa wanawatumia waalimu tena ni jambo la lazima sio ombi.
Fulana za chama mtavaa, ukijifanya mpinzani jiandae kufanyiwa fitina na kuipoteza kazi yako….
Nikitumia kaulimbiu kuwa ‘waalimu wa mashariki ya mbali hawana tofauti na mpira wa kiume (kondomu), wanatumika na kukosa maana wanatupwa huko’, je? Nitakuwa nimekosea hapo?
Sijawahi kumsikia Maria akirejea nyumbani huku analalamika kuwa amecharazwa viboko shuleni.
Ama! Ule utabiri wa hayati mama yangu kuwa tutasoma na kuishi kama malaika nadhani alikuwa anazungumzia nchi yenu. Nchi ambayo hakuwahi kuota kuna siku atafika…
Waalimu wa kule kwetu wamechanganyikiwa, akili zao zimeelekea mashariki tayari. Wamegundua kuwa serikali haina mpango nao, wametambua tayari kuwa wao ni ‘mipira ya kiume’.
Na wameamua kuishi hivyo!
Mwanafunzi hapaswi kustaajabu akicharazwa jumla ya viboko arobaini hadi hamsini kisha akaongezewa adhabu ya kuchimba kisiki na shimo la kutupa taka (jaa). Mimi nashindwa kuielewa Mashariki ya mbali, hadi sasa ni ngumu kuzungumza jambo na kujikuta unautetea upande mmoja kwa asilimia mia.
Mfano waalimu na akili zao zilizolalia mashariki badala ya kuangalia wanapambana vipi na serikali yao. Wao wanatumia hasira zao kuzihamishia kwa mabinti wasiojua mbele wala nyuma.
Mwalimu wa kike kutongozwa na mwanafunzi inaonekana kama mwanafunzi amelaaniwa.
Najiuliza ni laana kilo ngapi watakuwa wamebeba waalimu wa kiume katika nguo zao kwa kuwatongoza wanafunzi wa kike na kuwaharibia lau ndoto zao ndogondogo za kumaliza kidato na kisha kuolewa.
Kosa kubwa ni pale ambapo mtoto wa kike atajaribu kukataa.
Mwalimu wa Mashariki ya mbali atageuka malaika mtoa roho na atakuwa akiisaka roho ya huyo binti kwa udi na uvumba.
Na ili usitolewe roho huna budi kukubaliana na ombi ambalo limegeuka kuwa shurti!!!
Inasikitisha, inachekesha lakini zaidi inatia hasira. Hizo jazba kwa nini usiziunganishe ukawashirikisha waalimu wenzako ili muupe likizo ule ujinga wa kuwa ‘ma-kobe’ mbele ya chama tawala, kwanini msikasirike na kukataa katakata kuwa hamtaki kuwa kama ‘mipira ya kiume’.
Kweli ni jambo la kipekee ulilonambia Danstan kuwa waalimu wameungana nanyi katika maandamano. Kule kwetu hawahawa waalimu watatekenywa kidogo na ahadi ya ongezeko wa mshahara, hiyo ikiwa hadi ya kumi mfululizo bila matekelezo.
Watakaririshwa nyimbo za kutisha na kwenda kuziimba mbele ya wanafunzi ili wasithubutu kuandamana na zaidi wakiuunge mkono chama kilichoondoa uhai wa mama yangu mzazi.
Inasikitisha sana lakini sina budi kusema kuwa waalimu wa nchini kwangu sifa kuu waliyonayo ya kipekee. Huenda ni watu wanaopokea salamu nyingi kila siku kuliko waajiriwa wengine.
Shkamoo mwalimu!
Upuuzi!
______

Danstan alikuwa amechachamaa usoni bila kusema neno lolote wakati anamsikiliza Daniel.
Uso wake ulikuwa mwekundu sana kwa hasira.
“Daniel nahitaji kufanya ukombozi katika hiyo nchi ya Mashariki ya mbali. Hao wanaoteseka ni wanadamu kama sisi… kwanini waendelee kuishi maisha hayo ya mashaka. Nahitaji sana kufanya kitu.”
Daniel akamtazama Danstani kwa sekunde kadhaa. Na bila kufungua mdomo wake akabaki kujisemea kichwani huku akiwa bado anamtazama.
“Huo uso umekuwa mwekundu bila kupigwa, wewe ukikutana na askari kijana wa kule kwetu aliyekosa mshahara kwa miezi mitatu. Akucharaze na kirungu chake kabla hajakutishia bastola…. Utakufa bila kuaga ndugu yangu”
Baada ya kujisema hayo akafungua kinywa chake. “Danstan… unataka kwenda kuwakomboa watu ambao wameshindwa kujikomboa wenyewe. Yaani ukombozi Mashariki ya mbali ni mgumu sana, kwa kusimuliwa unaweza kuuona ukombozi unawezekana lakini kiuhalisia ambao unataka kuwakomboa wao hawapo tayari. Tazama Danstan, huko Mashariki ya mbali mwanamke anaolewa iwe kwa sherehe ama iwe kwa kutolewa tu mahari na wengine mahari haitolewi. Mwanamke huyu anajikuta katika utumwa wa ndoa, majirani wanasikia kabisa jinsi anavyopigwa na mume wake mlevi, wanayaona manundu yanayoweka ‘parking’ katika uso wake. Mwanamke anapambana kuvaa vazi la hijabu ili kuyaficha manudu, hii inamaanisha anapambana kuuficha uovu wa mume wake.
Majirani wakihoji anasema hakuna kinachojiri, mpaka siku anadidimiziwa visu ndipo anapiga kelele kuomba msaada. Wewe unayejiita mkombozi unaenda kumkomboa nani Mashariki ya mbali.
Tunaelekea maandamano ya kumpinga huyo Shoga ambaye ana dhamana kubwa serikalini…. Lakini kule kwetu kwa ‘ujinga’ wao wa kuamua kuwa kimya, akinamama wengi tu wanaingiliwa kinyume na maumbile. Hawasemi wanajikaza eti kisa tu kumfurahisha mume. Na baadhi yao nd’o wale ambao kilio chao kila siku kilikuwa “Lini tunamaliza shule nikaolewe??”
Haya Danstan, kama mtu anajikaza ili kumfurahisha shetani wewe unataka kwenda kumkomboa nani?
Au unataka kwenda kuwabadili mashetani wauache ushetani wao.
Ajabu katika mashariki ya mbali, unaweza kumbadili shetani akauacha ushetani wake, halafu yule aliyekuwa anafanyiwa ushetani akaanza kulalamika ‘Shetani unafanyia wapi ushetani wako mbona mimi haunitembelei siku hizi”
Je? Unajiandaa kupasuka kichwa ndugu yangu….” Daniel aliweka pumziko akamtazama tena Danstan.
“Unamaanisha kuwa mwanamke anaingiliwa kinyume na maumbile, mume akiacha kufanya hivyo atamuuliza anafanya wapi siku hizi?” alihoji akiwa amehamaki.
“Tena kwa hasira na wivu mkali…” Daniel alijibu kwa kumalizia ile kauli ya Danstan.
Danstan alishusha pumzi zake kwa nguvu sana….. hakuamini alichokuwa anakisikia. Ni kama alikuwa anatazama filamu ya kutisha sana.
“Bado unatamani kwenda kufanya ukombozi… hayo niliyokueleza ni machache tu…..”
“Aaah! Nitaenda kutembea na kusalimia ndugu, jamaa na marafiki” Alijibu bila kujua hata anachojibu.
Daniel akatokwa na cheko kubwa sana. “Una ndugu na jamaa Mashariki ya mbali tangu lini?…” akamalizia na cheko tena.
Danstan naye akajikuta anacheka sana. Hakika hakujua alichokuwa amejibu.
Cheko lile likakoma pale treni ya umeme iliposimama mahali husika ambapo maandamamo yalipangwa kuanzia.
Daniel akamwomba Mungu lisije kutokea lolote la kusababisha vurugu, hakutaka kuyapitia tena maumivu makali aliyowahi kuyapitia hadi kujikuta akiimbia nchi yake ya Mashariki ya mbali.

NAAM! Mambo ndo yanazidi kuwa mambo…. Je? Danstan atatimiza azma yake???
Nini hatma ya maisha ya Daniel katika nchi isiyokuwa yake…..

TOA MAONI YAKO….. kisha tukutane tena kesho….
 
RIWAYA: MASHARIKI YA MBALI
KALAMU YA: George Iron Mosenya

SEHEMU YA NNE

DANSTAN hakuwa na shamrashamra ya maandamano tena, alikuwa pale kutimiza wajibu lakini kiuhalisia alikuwa na matamanio zaidi kusikia juu ya nchi hiyo; ambayo kwake yeye ilikuwa nchi ya maajabu makuu.
Mashariki ya mbali!
Daniel alishiriki maandamano yale kikamilifu, maandamano ambayo baadaye yalisababisha waziri yule mkuu kung’atuka kutoka katika nafasi yake na kukiacha kiti wazi kwa ajili ya kulinda amani ya nchi ya Semedari.
Kitendo chake chake cha kuachia ngazi kilihesabiwa kama ushujaa kwa nchi yake.
Kila familia ikarejea katika makazi yake huku wakifurahia juhudi zao.
Daniel alikuwa katika kustaajabu yaliyokuwa yanajiri katika nchi hii ya ugenini. Mambo yalikuwa yanaendeshwa kwa kutumia weledi mkubwa huku utu ukiwekwa mbele. Na demokrasia ikiheshimiwa sana.
Wakati wanarejea nyumbani ikawa ni nafasi ya Daniel Katunzi kuuliza mambo kadhaa juu ya tukio hilo.
“Inavyoonyesha huyu sio mtu wa kwanza kuachia madaraka. Maana waandishi wa habari sijaona hata kama wameshtushwa sana….”
“Haswaa! Sio tukio la kwanza, uzuri katika nchi yetu hii katiba inasisitiza juu ya kiongozi kuwajibika ama la angoje kuwajibishwa na wananchi. Huku kwetu katiba inaeleza kuwa kiongozi na mtawala ni vitu viwili tofauti. Na hatuhitaji kuwa na mtawala kwani tunaweza kujitawala wenyewe. Tunahitaji kuwa na kiongozi ambaye tunamwingiza katika ajira kwa kumpigia kura ambazo anaziomba kwetu kwa unyenyekevu mkubwa. Jijini kwetu pale kuna meya aliwahi kutoa amri ya kukamatwa mtu ambaye hakuwa ametenda kosa, mtu huyo akabaki mahabusu akiteseka kwa kuukosa uhuru wake. Baadaye ikaja kubainika kuwa hakuwa ameteenda kosa. Ilikuwa ndani ya masaa ishirini na nne tu baada ya jambo hilo kugundulika, akaomba radhi na kujiuzuru nafasi yake ya umeya. Licha ya hayo yote jamii haikuwahi kumsamehe. Alihamia jiji jingine yeye na familia yake. Huku katiba inatulinda sana..” alimaliza kujieleza Danstani.
Tabasamu hafifu liliuchukua uso wa Daniel kabla halijatoweka na kuacha hamaki iliyomweka katika unyonge na uchovu wa kufikiri.
Akajikuta katika mwayo mrefu kabla hajaanza kuzungumza.
“Uwe umeiba, haujaiba, uwe unamjua mwizi ama haumjui. Ni haki yako kuwekwa mahabusu nchini kwangu.
Uwe una umri mdogo, uwe hauna akili timamu, uwe mwendawazimu, uwe na timamu. Mahabusu ni haki yako.
Useme ukweli,useme uongo. Uwe mwanamke asiyezaa ama anayenyonyesha. Mahabusu utaingia na virungu utapigwa.
Msamiati wa kujitathmini na kuwajibika upo katika kamusi yetu lakini hautumiki tena. Kurasa zake zimeandikwa kwa lugha za kigeni ili wazawa wasiweze kuzisoma.
Umenifurahisha sana kwamba meya alijiuzuru wadhifa wake kisa kamweka rumande mtu asiyekuwa sahihi!!?.... halafu licha ya kujiuzuru na kuomba radhi wananchi hawakumpa msamaha!!
Kule kwetu, virungu unapigwa, anatukanwa mama yako aliyekuzaa jumlisha na ukoo wake wote, rumande unaingia, kosa haujafanya na baadaye ukitoka hakuna mjinga atakayekuomba msamaha. Wewe ni nani katika Mashariki ya mbali mvaa suti mmoja akuombe msamaha?? Eeh! Wewe ni nani Danstan? Si uende basi ukajionee!!” Daniel alijikuta akizidiwa na jazba.
“Basi Dany… imetosha… imetosha ndugu yangu. Nilikuwa najaribu tu kukuelezea namna gani huku kwetu katiba inatulinda sana…. Maana huku kwetu ni heri wabaki wakosaji mia moja uraiani kuliko mwenye haki mmoja kutiwa gerezani kimakosa.” Alimalizia kwa upole sana Danstan ambaye sasa alikuwa ameifuta ile dhana ya kwamba huenda Daniel ni mgonjwa wa akili. Sasa alikuwa anaamini kuwa ipo nchi iitwayo Mashariki ya mbali.
Wakati Daniel akishusha pumzi zake kwa juhudi, treni ya umeme ilisimama katika kituo kwa jili ya abiria wengine kujumuika katika safari.
Akaingia mama mjamzito, hakudumu kwa dakika moja kabla hajawa na chaguo la wapi aketi kwani kila mmoja alijaribu kumpisha katika nafasi, kwa sababu tayari nafasi zilizokuwa zimejazwa na waliotanguliwa.
Daniel akajikuta akitokwa na cheko la ghafla peke yake kati ya abiria wote.
Danstan akashtushwa na cheko lile ambalo hakujua lilipotokea.
“Kulikoni mzee!” alihoji.
“Nimekumbuka tena Mashariki ya mbali. Na sasa natamani kweli twende mimi na wewe ukajionee haya ninayokusimulia kuwa sio ya kubuni bali wakazi mamilioni wanayaishi maisha haya na wanayaita maisha ya amani na furaha.
Tazama huyo mama alivyopishwa aketi, vitendo kama hivyo huenda nd’o vinasababisha huku kwenu wanazaliwa watoto wana sura nzuri sana za kuvutia. Mashariki ya mbali basi tu tunalindwa na imani mlizotuletea ninyi wakati mnatutawala kwa manyanyaso makubwa, mkatueleza kuwa ‘Mungu ametuumba kwa mfano wake’. Basi usemi huu ndo unatulinda, hata ukizaliwa na sura inayofanania na msukule mzoefu. Unarejea ule usemi na kujitetea.
Ila kwa dhati tunaharibika tangu tumboni.
Kule kwetu mtoto anaanza kukasirika tangu akiwa tumboni, fikiria mtoto anajionea waziwazi jinsi alivyokuwa mzigo kwa mama yake halafu anafika eneo kama hili kila mtu anamuangalia tu bila kujali. Kama hiyo haitoshi mama anarushiwa tusi, mtoto analipokea akiwa tumboni. Kwanini sura isikunjamane!
Mashariki ya mbali upishwe siti?? Thubutu labda iwe katika kipindi cha ile miezi wanayoiita mitukufu, ule wa Ramadhani kwa waislamu na kwarezma kwa wakristo; maana miezi hii nd’o shahada za unafiki huongezeka huko kwetu. Kinyume na hapo jitahidi kuwa imara tu maana ukijifanya unajua kuongea ukaanza kulalama haujapishwa nafasi utalisikia jibu mubashara kutoka kwa kijana anayeweza kuwa mwanao ama mdogo wako wa mwisho. Atakuuliza swali jepesi ambalo kinywa kitaona aibu kutoa jibu.
‘wakati mnabinuka katika starehe zenu tulikuwa wote?’.
Si unalisikia hilo swali, jibu ni jepesi tu lakini hakuna awezaye kujibu. Hivyo mama mjamzito kule hana thamani ya kuwatikisa watu waguswe kumpisha nafasi kama hivi.
Na tatizo hili sio la upande mmoja, ni pande zote akinamama wa Mashariki ya mbali ni mabingwa wa kujishushia heshima wenyewe. Wanafahamu kuwa wao ni akinamama tayari lakini hawauishi umama wao. Hawa nd’o mabingwa wa kutukanana mitaani, ama unakuta hilo tumbo alo’beba ni mzigo kutoka kwa kijana umri sawa na mwanaye wa pili.
Nani akuheshimu sasa ikiwa we mwenyewe umeshindwa kuziheshimu sehemu zako za siri??
Ujue Danstan unaweza kusema mapenzi hayaangalii umri. Lakini hivi kweli mtoto mdogo ni wa kumpa siri nawe ukasema ataitunza??
Ukiweka imani kuwa mtoto mdogo atakutunzia siri, ugonjwa wa akili ulio katika kichwa chako. Tiba pekee ya kuuponya ni kukikata kichwa chako, kisha kukisaga saga, maana tukisema tukitupe. Atatokea mtu atakiokota atakivaa na kuishia kulekule.
Akinamama haohao wakishajifungua hawapitii mabadiliko yoyote, unakuta mama mtu mzima anamtukana mtoto wake matusi mazitomazito tangu masikio yanapofunguka. Mtoto kama huyu ambaye matusi sio kitu kipya kwake atashindwa vipi kumtusi mama mjamzito ndani ya gari ama treni kama hii.
Danstan! Siyahubiri haya kwa ubaya kwa sababu tu sipo Mashariki ya mbali, nayahubiri kwa wema kabisa. Kwa sababu kinywa changu kinanena ukweli mtupu. Ukweli ambao wanamashariki ya mbali wanautambua lakini midomo yao imetiwa ganzi hawawezi kusema na hata wakisema wale wasikilizaji wametia pamba masikioni hawawezi kusikia.
Na ushukuru sana wasiposikia maana wakisikia, wataacha shughuli zao zote chache za maana na nyingi za kipuuzi kisha watakushukia kama tai wa jangwani, wataing’oa shingo yako.
Baada ya hapo watajitangazia ushindi dhidi ya adui mkubwa. Wataandaa hadhira yao ambayo muda wote itapiga mbinja na vigelegele.
Danstan, ukipata likizo ya mwezi mmoja nitaomba sana twende Mashariki ya mbali.
Kabla ya kwenda huko jitahidi kuupa mwili wako wote zoezi la kukabiliana na hasira ndogondogo. Maana Mashariki ya mbali kila upande utakaogeuka unaweza kukusababishia hasira.”
Danstan alimtazama Daniel wakati anaweka kituo kikubwa.
“Unadhani nitaweza kurudi nikiwa hai. Mbona yaonyesha Mashariki ya mbali ni nchi ya kutisha sana.” Danstan aliuliza huku akiwa na dalili zote za uoga.
Kwa mara nyingine tena Daniel akazungumza bila kufungua kinywa chake.
“Ushaanza kutetemeka wakati upo katika nchi yako na umepanda treni ya umeme, hivi utakuwa katika hali gani ukiwa katika mbanano mkubwa wa garimoshi za mashariki ya mbali, kisha baada ya mbanano ukagundua kuwa katika ule mbanano kuna mtu amechukua pesa zako bila hiari yako mwenyewe. Si utarukwa na akili kaka yangu, ndugu zako waseme umetupiwa majini ya Mashariki ya mbali?”
Na baada ya hapo akafungua kinywa safari hii alizungumza na kusikika.
“Ninatokea Mashariki ya Mbali Danstan. Kuingia katika nchi yangu ni bure kabisa, lakini kuishi ni umauti, kutoka pia ni bure lakini hautatoka kama ulivyoingia…. Utatoka wewe na pumzi utaziacha mashariki ya mbali. Utarejea mzoga wako usioweza kusimulia chochote kilichojiri…… hakuna atakayejali kuhusu wewe pindi utakapotupatupa miguu yako na kuyakaribia mauti.
Sikuzuii kuzijua mila na desturi zangu….. nimekupa onyo tu ikiwa kweli nia yako ni thabiti……
Treni imefika mwisho Danstan… tushuke!”
Hata alipomkumbusha kuwa walikuwa wamefikia ukomo wa safari, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka Danstan!

#Je? Bado Danstan anaitamani nchi ya Daniel…..
Ikiwa wataenda ni kipi kitajiri…
Ni ipi historia ya Daniel hadi kutoweka Mashariki ya mbali na kufika nchini Semedari jijini Mainstream!
FB_IMG_1558112461686.jpeg
 
RIWAYA: MASHARIKI YA MBALI
KALAMU YA: George Iron Mosenya

“Katika maisha tunakumbushwa kuwa watu wa kujaribu ili tuweze kuyafikia malengo yetu. Pia tunasisitizwa kuwa kuanguka ni sehemu tu ya safari ya mafanikio.
Lakini hakuna mahali tumeelekezwa kuijaribu sumu kwa kuilamba, kuyajaribu makali ya wembe katika ngozi zetu, kuujaribu usemi wa mtoto wa nyoka ni nyoka kwa kumpatia kidole…..
Sio kila kitu ni cha kujaribu katika haya maisha….

NA HII NI SEHEMU YA TANO

GIZA lilikuwa limetanda katika namna yake ya kawaida lakini likitiwa chachandu ya aina yake na wingu zito lililokuwa limetanda angani kisha kibwagizo cha umeme kukatika kukalifanya eneo lile kuwa mojawapo kati ya maeneo ya kutisha zaidi ulimwenguni.
Kibatari kilichonyong’onyea kwa utambi wake kuikosa haki yake ya msingi ya mafuta kilisaidizana kwa ukaribu na mshumaa uliozidi kutenda wema wake wa siku zote.
Hata siku hii ulitenda wema wa kummulika mgonjwa aliyechanika vibaya mguu wake, hakuna umeme na ni kibatari na mshumaa katika kuhakikisha mtaalamu wa afya analiona jeraha na kulipatia tiba stahiki.
Tiba stahiki la! Haikuwa tiba stahiki, mtaalamu wa afya alikuwa anajaribu kufanya lolote lililokuwa ndani ya uwezo wake. Na pengine hata nje ya uwezo wake.
“Daktari hautafanya makosa kweli katika giza hili?” aliyemleta mgonjwa alimuuliza mtaalamu yule huku uso wake ukiitangaza hofu kuu.
Giza lilimstiri!
“Mimi si daktari. Nilitamani niwe lakini sikuwahi na sitakuja kuwa. Mimi ni muuguzi tu..” alijibu mtaalamu yule huku akiendelea kuyakaza macho yake kutazamana na jeraha lile linalovuja damu.
“Ati nini! Sasa utaweza vipi kushona jeraha hili angali wewe ni muuguzi tu.” Alihamanika.
“Aah! Hata hivyo nakaribia kushindwa kulishona. Nadhani muda si mrefu jibu utalipata.” Alijibu kwa utulivu mkuu huku akiwa anaendelea kutazamana na jeraha lile kana kwamba kuna mazungumzo ya siri anafanya na jeraha lile kwa kutumia lugha inayotambuliwa na pande mbili tu.
Muuguzi na jeraha!
“Tafadhali sana, hebu fanya kitu hiyo damu ipungue dakt… aah! Muuguzi.” Alikwama alipotakakumuita tena kwa kile cheo cha daktari.
“Unaweza kuendelea kuniita daktari, ndivyo wanavyoniita katika kijiji hiki kila wanapopata matatizo.” Alijibu muuguzi yule pasi na kutikisika. Bado alitazamana na jeraha.
Walifanania na majogoo yaliyotwangana na sasa kila mmoja amechoka lakini hata asiwe tayari kusalimu amri.
“Vyovyote… tafadhali fanya kitu.” Mleta mgonjwa aliendelea kuzungumza kama anayelalamika na nusu akiwa anachanganyikiwa.
“Hapa kuna njia mbili za kuikausha hii damu…” alianza kuzungumza yule muuguzi wa kike. Akaiacha ile kauli hewani kisha akageuka na kumtazama bwana aliyemleta mgonjwa wake.
“Tujaribu kumuwekea chumvi…” alisema kwa utulivu mkubwa sana.
“Aaah! Hapana, hapana…. Hiyo siyo njia sahihi. Chumvi itasaidia nini katika jeraha lote hilo. Chumvi itasaidia nini rafiki…sidhani kama ndivyo taaluma yako inavyoelekeza” aling’aka mleta mgonjwa.
“Nilisema kuna njia mbili. Ya pili ushaijua kwani?” Muuguzi akajibu kwa upole bila kujali kuchanganyikiwa kwa mleta mgonjwa.
“Sawa nieleze yaweza kuwa bora… lakini sio kumuwekea chumvi” alijibu kisharishari.
“Utalazimika kufumba macho ukemee kwa imani zako za kiroho damu hii iweze kukatika na kidonda hiki kijifunge mara moja iwe katika jina la Yesu, Mtume Muhamad, ama majina ya mizimu ya babu yako.” Alijibu kwa upole kabisa.
Mleta mgonjwa alijikuta naye anapatwa na ugonjwa wa ghafla.
Mapigo yake ya moyo yalipiga mara mbili ya kawaida, hakuamini kuwa maneno yale yanatoka kwa mtaalamu ambaye anamtegemea amtibie mgonjwa wake katika kile kiza kinene sana.
“Yaani…. Kweli kabisa unani…aaargh!” alighadhabika. Na hapo yule muuguzi akautua chini mguu wa mgonjwa yule asiyekuwa na fahamu zake. Sasa akamgeukia mleta mgonjwa.
“Njia ya tatu ipo…… ni kuendekeza maswali yako ya msingi sehemu isiyokuwa sahihi, hasira zako za kipuuzi kwa mtu aliyebeba mguu mzito wa mke wako sijui mchumba wako, hadi pale atakapokata roho ukahangaike kutafuta mahali pa kumfukia. Napenda kukukumbusha kuwa, kibatari kinakaribia kuzima, mshumaa unakata viuno kuelekea sakafuni na katika kituo hiki tuliahidiwa huduma za vyumba vya kulaza maiti. Huu ni mwaka wa kumi tangu niisikie ahadi hiyo na utekelezaji haujawahi kufanyika. Akifa huyu utambeba mgongoni….” Muuguzi alizungumza kwa ukali na alikuwa akimtazama moja kwa moja mleta mgonjwa yule ambaye alikuwa amejaribu kuyatawala maongezi hapo awali.
Mleta mgonjwa yule alijisogeza hadi nje baada ya kumwomba radhi yule muuguzi na kumsihi amsaidie mgonjwa wake.
Alipofika nje akiwa analindwa na lile giza totoro alianza kuangua kilio cha uchungu mkali.
Kilio cha mtu mzima.
Kilio kisichoambatana na sauti bali mifereji ya machozi, zikiwa ni salamu kutoka katika moyo unaougulia.
Akayafumba macho yake na kuyakumbuka maneno ya wazazi wa yule binti jinsi walivyomsisitiza.
“Danstani, huyo ni mchumba wako sawa… lakini kwetu sisi ni mboni. Jitahidi umlinde kadri uwezavyo, afike na tabasamu lake, arejee na tabasamu lake hivyohivyo.”
Maneno yale yalijirudia katika masikio yake kana kwamba yanatamkwa kwa mara nyingine tena na wazazi wa binti yule aitwaye Cherry.
Sauti zile kabla hazijatoweka vyema, akakumbuka ni kiasi gani Cherry alimkataza katakata juu ya uthubutu wake wa kufanya ziara katika nchi ya Mashariki ya mbali.
Jambo ambalo lilikaribia kuupoteza uchumba wao katika shimo la hewa.
Kama zisingekuwa busara za Cherry kuchukulia uzito wa mapenzi yao basi wangekuwa wametengana na safari ya Mashariki ya mbali ingemuhusu yeye pekee ama na mtu mwingine.
“Ni nguvu ya mapenzi inanipeleka Mashariki ya mbali pamoja nawe, kinyume na hapo nisingekanyaga huko. Wewe endelea kumwona Daniel kama tahira lakini kumbuka kuwa hata saa mbovu kuna muda wake wa kuwa timamu.”
Yalikuwa maneno ya Cherry siku ambayo anakubaliana na Danstan waweze kufanya safari ya kwenda Mashariki ya mbali.
Wapo Mashariki ya mbali, Cherry hazungumzi tena. Usafiri wa baiskeli katika vijiji unakuwa nuksi kwa Cherry, utelezi unamsomba muongoza chombo anaruka mbali na kumwacha Cherry atoe salamu za ghafla kwa ardhi iliyonuna.
Jiwe linamchana vibaya mguu wake na kulazimika kukimbizwa hospitali.
Hospitali gani kijijini?
Zahanati!!
Sawa tuiite zahanati. Kama tu! hakuna jina jingine zaidi ya hilo.
Huku wanakutana na huduma ya aina yake, umeme hakuna, kiza kimetanda na kunogeshwa na wingu zito.
Cherry Stanley aliyezoea huduma za kisasa nchini Semedari katika jiji la Mainstream sasa yupo mahali ambapo ukiwa hai unaishi na matatizo, ukipoteza uhai wewe unageuka kuwa tatizo zaidi.
Baada ya kukubaliana na hali halisi kuwa ile haikuwa ndoto bali kweli tupu. Danstan McDonald aliingia tena ndani na kumkuta muuguzi akiwa amefanikiwa kushona jeraha lile la Cherry, na alikuwa amemlaza chini akiendelea na shughuli nyingine.
“Nadhani angelazwa kitandani. Samahani kwa kuingilia utendaji wako mtaalamu.” Alizungumza kwa utulivu.
Nidhamu ilikuwa imekaa mahala pake.
"Inasemekana wazungu walimkabidhi mbunge wetu vitanda na magodoro, akavihifadhi nyumbani kwake baadhi, kisha akampatia diwani baadhi avilete katika zahanati yetu, diwani ana zahanati yake mjini, akavipeleka kule na hapa alileta vitanda viwili tu huku akiambatana na wapiga picha watatu kwa ajili ya kumuhoji na kumpiga picha akikabidhi vitanda.
Kuna siku wagonjwa waligombania kitanda almanusra wapigane. Nikamueleza daktari siku aliyopita kutusalimia juu ya tukio hilo. Alikasirika sana kisha akafanya maamuzi ya busara. Akavichukua vitanda vile na kuvipeleka nyumbani kwake. Akasema kuwa ‘wakose wote’.” Alijibu muuguzi huku akiendelea na shughuli zake.
“Yaani! Daktari anatoa maamuzi kama mtoto mdogo….” Kabla hajamaliza muuguzi akaingilia kati.
“Ni vyema unamdhihaki angali hayupo. angekuwepo angeliweza kuongozwa na pombe zake akakuchoma sindano ya sumu ukafa….”
Kauli ile ilimtia hofu ya ghafla Danstan, akajikuta anapayuka akiwa amehamanika.
“Namshtaki siwezi kukubali dhuluma na unyanyasaji wa kiwango hicho mimi. Mimi sio kama hao wengine… ajue hilo.” Alifyatuka maneno kwa jazba.
“Ubaya ni kwamba utakapomshtaki katika hiyo mahakama ya wafu ni wewe pekee utakuwa mfu yeye atakuwa hai. Malalamiko yako huoni kama yatachukua muda mrefu kusikilizwa?” Muuguzi alizungumza huku akiwa anajinyoosha mgongo wake. Hakuwa na haraka wala papara kwa lolote alilokuwa anafanya.
Danstan alijikuna bila kuwashwa. Alikuwa ameropoka na kujiona amejenga hoja.
Muuguzi akamtazama na hata asiruhusu kinywa chake kusema lolote bali akijisemeza yeye na nafsi yake.
“Kumbe hata hawa wenye rangi nyeupe wanaweza kuwa wa mwisho darasani eeh! Tazama hiki kiazi mbatata, kinaropoka tangu kilipofika hapa. Huyu darasani hata mimi ningemburuza vizuri tu.”
Na hata fikra zilipofikia ukomo akatoa tabasamu kwa mara ya kwanza kufurahia yaliyojadiliwa katika kichwa chake juu ya bwana yule.
“Ni nani aliyekufundisha kuzungumza lugha yetu adhimu. Unazungumza vizuri sana.” Akasindikiza tabasamu lake kwa kauli ile isiyomaanisha kitu.
“Samahani anaweza kurejewa na fahamu zake muda gani?” Danstani alihoji bila kujibu swali la muuguzi.
“Kama alivyoondoka tu..” kwa utaratibu wake uleule naye alijibu.
“Una maana gani?”
“Wakati anazipoteza fahamu hakumweleza mtu yeyote kuwa sasa napoteza fahamu. Na hata kwenye kuamua kuzirejesha hatamwambia yeyote. Hiyo ni siri yake” Muuguzi alijibu, jibu lile likaambatana na kibatari kuiaga dunia baada ya kuchoma sana utambi wake.
Mshumaa ukabaki kusambaza upendo.
Danstan alichoka akili, roho na mwili!

_______

#DANSTAN alifikaje mashariki ya mbali, yu wapi Daniel….. na nini hatma ya Cherry.

MAONI YAKO NI MUHIMU, PIA USIACHE KU-SHARE….
 
Aisee iko pouwa sana
 
RIWAYA: MASHARIKI YA MBALI
NA: George Iron Mosenya

Lingalipo jua usilalame kuwa lakuunguza, waliokanyaga kaa la moto waseme nini?
Acha mvua ikunyee kimyakimya, usipige kelele. Waache walalamike wanaodondokewa na theluji.
Kama lalamiko lako kuu ni kupata watoto jinsia moja mfululizo basi hakuna unalolalamikia mbele ya wasiowahi kamwe kupata mtoto katika maisha yako.
Usijijengee dhana ya kuwa mtu wa kuhisi anaonewa kila mara, tembea ujionee hautalalama tena.

NA HII NI SEHEMU YA SITA.

Katika sehemu ya tano, iliishia Danstan akipitia hekaheka nzito akiwa Mashariki ya mbali, Cherry mchumba wake anapatwa na balaa la kuanguka na baiskeli. Jiwe linauchana vibaya mguu wake anakimbizwa katika kituo cha afya ambacho kinasimamiwa na muuguzi mmoja tu. Yaliyotokea huko yanakuwa ishara ya ukaribisho kwa Danstan.
Karibu Mashariki ya mbali.

¬¬¬_________

MAJIRA ya saa nne asubuhi daktari alipita katika kituo kile, kwa kauli ya muuguzi ni kwamba daktari yule huwa anapita kuwasalimia, kusikiliza malalamiko kadhaa kutikisa kichwa kwa masikitiko makubwa kisha kuondoka kana kwamba anarejea na suluhisho.
Baada ya wiki kadhaa nd’o anarejea, hajatatua lililomsikitisha mara ya mwisho anaanza kusikitishwa na mengine tena.
Alizoeleka hivyo!
Lakini siku hii mambo yalikuwa tofauti, alipopita katika wodi ya wagonjwa isiyokuwa na vitanda aliona hali tofauti.
Sura ya mtu mweupe!
Daktari akashtushwa sana, akawaza ni misaada mingapi wazungu wamewahi kuagiza ifike katika zahanati ile badala yake akaihamishia njia ikaenda katika zahanati yake iliyopo mjini.
Hatia ikatia nanga katika moyo wake.
Daktari akaanza kujuta kimyakimya kwa udhulumati wake alioufanya. Akaiweka vyema suruali yake kiunoni kisha akajikumbushia maneno mawili matatu katika lugha ya Samaradi, ni muda sana alikuwa hajazungumza lugha ya kigeni hivyo alihofia kubabaika atakapoanza kuhojiwa na bwana yule.
“Huyu muuguzi naye mbona hakunipanga mapema nijiandae. Nadhalilika leo…” Daktari alizungumza kwa sauti ya chini na sasa alikuwa hatua kadhaa kumkaribia bwana yule.
“Habari ya asubuhi..” mzungu yule akaanza kumsalimia kwa heshima kubwa. Daktari akashtuka, akamtazama kwa makini iwapo ni mzungu kweli ama vinginevyo.
Alikuwa mzungu!
“Bila shaka wewe ni daktari. Nina mgonjwa wangu hapa. Naomba umsaidie tafadhali. Nilimleta jana usiku”
Danstan alizungumza kwa kusihi.
Daktari akafuatisha mikono ya Danstan ilipokuwa inaelekeza. Akamwona Cherry akiwa amejilaza, fahamu zikiwa zimemrejea.
Daktari akasahau ile hatia iliyokuwa inamwandama akaitazama fursa iliyokuwa inajipitisha mbele yake.
Fursa kubwa asubuhi asubuhi!! Akajisemea.
Harufu ya dolali!
______
Upesi akamwita muuguzi, wakasaidiana pamoja na Danstan wakambeba Cherry kwa uangalifu mkubwa mno mpaka katika gari ya daktari.
Wagonjwa wengine wakabaki kunung’unika kuwa mgonjwa huyu amependelewa, wao wana matatizo makubwa lakini kila kukicha ni danadana hadi wengine mauti yanawakuta kwa uzembe wa daktari huyu.
Ajabu ya mwaka! Daktari huyu mjivuni, leo hii kwa mikono yake anambeba mgonjwa.
Utumwa huu utakwisha lini? Muuguzi alisaidiana na wagonjwa wengine kujiuliza swali lile wakati gari ikitimua vumbi kwa fujo angali ikitoweka.
Haukuwa utumwa, hawakujua tu.

________

SAMARADI, MAINSTREAM

Ilikuwa barua pepe ya kwanza kutoka Mashariki ya mbali, ukiwa ujumbe umetumwa na Danstan.
Daniel alifurahi sana kupokea ujumbe kutoka nchi yake ya kuzaliwa na kukua. Na alitamani sana kufahamu ni kipi ambacho Danstan alikuwa amemuandikia, Dany anaingia chumbani kwake na kisha kuifungua barua pepe ile iliyokuwa imesheheni insha yenye aya za kutosha jumla yake yafaa kutengeneza kitabu cha hadithi kadhaa za watoto.

DANSTAN ANAANDIKA.

Salaam Daniel, nisalimie Mainstream nzima hususani familia yangu. Ya huko mengi nayafahamu… ni mgeni sana kwa haya yanayotokea huku ulipozaliwa wewe na kuishi. Hata sasa najiuliza uliweza vipi?
Nimejionea mengi na bado majibu sina. Nimejionea ng’ombe wakilimishwa shamba kubwa huku wanachapwa viboko hadi ngozi zao zinachanika. Katika vidonda hivyo inafungwa nira nzito. Kisha anapigiwa kelele alime kwa juhudi.
Hata baada ya suluba hii, waliomcharaza watajipakiza katika mkokoteni kisaha watamwamrisha tena kwa viboko ng’ombe huyu awaburute mpaka nyumbani.
Kwa mara ya kwanza nimeliona chozi la uchungu likitoka katika macho ya ng’ombe. Ni kweli watu wako hawawezi kusoma lugha nyepesi kama hii, kuwa ng’ombe anaumia?
Nimewaona watoto wadogo wakienda umbali mrefu sana kuitafuta shule, matumbo yao nje na miguuni hawana viatu. Hili ni jipya ama lilikuwepo wakati unaishi huku?
Tukiachana na hayo waliyoyazoea, kuna hili la ajabu. Huko kwetu kifo ni kitu ambacho tunafahamu kipo na ni mipango ya Mungu lakini hatukubali vifo vinavyosababishwa na uzembe. Huku kwenu kifo ni mipango ya Mungu inayoharakishwa na wanadamu wenyewe. Na baada ya uzembe wao wana kauli yao ya alipangalo Mola mwanadamu hawezi kuzuia.
Usipokuwa na pesa kifo chako kinawahi, ukiwanazo unaweza kununua maisha.
Waambie wanadamu wa huko wanaotawaliwa na usemi huo wa kisemedari wa ‘money can’t buy life’ waje huku Mashariki ya mbali pesa inanunua maisha.
Cherry alipatwa na ajali ya baiskeli na kuchanika vibaya mguuni, katika zahanati hii tulipata huduma ya kwanza kwa mbinde na hapakuwa na mwendelezo wowote, kwa macho yangu nimeshuhudia wagonjwa wakiwa wameikumbatia sakafu. Hii ndo namna yao pekee ya kulala.
Daniel! Hakuna vitanda wala magodoro, eti daktari alihamishia nyumbani kwake.
Nimeliona chozi la damu likitoka katika macho ya mgonjwa aliyelia kwa muda mrefu kwa sababu ya uchungu anaoupitia bila msaada.
Hakuna madawa katika zahanati hii, lakini hii haimaanishi kuwa kuna uhaba wa dawa katika nchi yako.
Dawa zipo, jipekue uweke pesa mbele na utaziona dawa hizo.
Mimi yamenisibu….. kuumia kwa Cherry limekuwa funzo kwangu.
Nilithubutu kumletea jeuri muuguzi ambaye ugumu wa maisha umemfanya kuugua ugonjwa uitwao ‘hakuna ninaloogopa’. Nikajaribu kuweka vitisho, badala atishike ananiuliza ni nani amenifundisha kuongea lugha yenu.
Nikalazimika kuwa mpole kwa usalama wa Cherry. Kweli akamshona na kumwacha naye akiikumbatia sakafu ya baridi sana.
Hizi ndizo zahanati za kwenu Daniel. Amakweli uliyonisimulia yalikuwa rasharasha acha nijionee mwenyewe.
Asubuhi alifika daktari na kuonyesha ukarimu wa hali ya juu.
Nilistaajabu daktari alivyonishughulikia kwa upendo na wepesi sana, nikabaki kujiuliza kuwa kumbe watu wema bado wanaishi, lakini kumbe naye alikuwa katika kuisaka ridhiki yake. Tulipofika katika zahanati ambayo inasemekana kuwa ni mali yake akishirikiana na diwani wa kata hii, mambo yakabadilika.
Nilitakiwa kununua sindano, dawa, nikatakiwa kununua chupa za dripu nikatakiwa pia kulipia kitanda na kumpatia daktari kile alichokiita ‘hela ya supu’.
Nilipojaribu kuleta ujuaji wangu kuhusu masuala ya afya akanieleza kuwa atanipatia chumba bure kabisa, niingie mimi na mgonjwa wangu kisha nikamtibu.
Niliduwaa lakini yeye hakuwa na muda na alikuwa ameanza kunipa mgongo kabla sijamuita na kumweleza kuwa nipo tayari.
Duka ambalo nilinunua vifaa vyote hivyo ni mali ya daktari huyo.
Hivyo hapo tulikuwa katika biashara ya kisasa, mteja kudhani amependelewa na anapogeuza mgongo muuzaji anachekelea.
Nilihisi daktari amenipendelea aliponitoa katika ile zahanati isiyokuwa na vitanda, kumbe alikuwa ananivuta kwenda kunufaika na mimi. Ninachoshukuru ni kwamba baada ya kuitoa hiyo pesa, Cherry ametibiwa vyema kabisa na yu buheri wa afya kwa sasa.
Nitaendelea kukuandikia kadri ninavyopata wasaa wa kufanya hivyo, nia yangu bado ni thabiti nina imani itatimia. Nisalimie familia yangu….

Wako,
Danstan Mcdonald
Mashariki ya mbali.

________

DANIEL alimaliza kuisoma barua ile huku akiishia kutikisa kichwa chake. Alijisikia aibu ndani ya moyo wake, kwa mambo ambayo nchi yake inayatenda hata kwa wageni.
Baada ya tafakari ya muda mrefu, hatimaye Daniel aliamua kujilaza kitandani ambapo aliendelea kufikiria kuhusu barua ambayo aliipokea kutoka kwa Danstan.
Daniel alisikitishwa na mengi, lakini kubwa zaidi ni kwamba aliona kuwa bado Danstan hajapitia chungutamu za Mashariki ya mbali na bado ameweza kuandika barua ile akionekana kama anayelalamika.
Magumu ya Mashariki ya mbali yakapita katika kichwa cha Daniel kwa kasi ya ajabu na bado hayakumalizika upesi, nchi hiyo isiyoisha vibweka haikuwa sawa kabisa kwa mwanaume ‘laini’ kama Danstan kuitembelea.

“Anashangaa wagonjwa kulala sakafuni? Hilo tu…. Yaani daktari kuomba pesa ya supu kwake ni ajabu la mwaka, huyu akikutana na daktari aliyevurugwa na pombe za kienyeji akamfanyia mtu upasuaji wa kichwa wakati katika vyeti amesomea magonjwa ya akinamama. Si atachangayikiwa huyu kijana.
Kabla hajachanganyikiwa huyu kijana na kisha familia yake kutupa laana katika nchi yangu ambayo ni kama imelaaniwa tayari nadhani napaswa kufanya kila namna aweze kurejea huku nchini kwao. Ya huko Mashariki ya mbali atuachie sisi wana mashariki ya mbali. Asubuhi nitazungumza na mama yake…… asije akampoteza kijana wake ghafla.”
Daniel alipitiwa na usingizi akiwa katika wazo hilo.
Lakini wakati yeye analala nchini Semedari, kule Mashariki ya mbali ndo kwanza mchana ulikuwa unaingia na Danstan tayari alikuwa katika hekaheka.
Katika hekaheka hizo, likazuka jambo!
Jambo lililozua mambo…..

***Haya tukutane katika COMMENTS wakati tunaisubiri KESHO itakayotupatia mwendelezo….
 
RIWAYA:MASHARIKI YA MBALI
KALAMU YA: George Iron Mosenya

Utafanya jitihada na kuyakwepa mengi kwa utashi wako, lakini ni jambo gumu sana kumkwepa mwenye CHUKI YA ASILI. Ukicheka naye atachukia, ukiachana naye atachukia, ukiimba, ukiongea, ukinyamaza… bado atachukia. Huyu ni yule ambaye siku ukifa atachukia na ukiendelea kuishi pia atachukia….. WAPO TUNAISHI NAO.

Na hii ni SEHEMU YA SABA.

Hali ya Cherry kiafya ilitosheleza kabisa kuitwa yenye ahueni. Japokuwa hakutanabaisha kuwa alikuwa amechukizwa na ile safari ya Mashariki ya mbali lakini dhahiri nafsi yake ilibubujikwa na machozi huku moyo nao ukijutia kuanguka katika penzi la Danstan.
Sasa penzi linauzidi nguvu uhalisia Cherry hana budi anavumilia shubiri ile. Ule usemi wa ukipenda boga, mahaba yahamishie kwenye ua lake yalitembea hadi nchini Semedari.
Danstan mtafiti yeye alianza kuburudika na maisha yale ya kujifunza kitu kipya kila siku, Cherry alijaribu kutumia mafumbo mazito kumsihi warejee nchini kwao lakini Danstan hakujifanya mwerevu wa kuyang’amua mafumbo.
Akajifanya haelewi be wala te.
Maisha yakaendelea, wakisafiri huku na kule kuifahamu vyema mashariki ya mbali, lengo la Danstan bado likiwa kufanya mapinduzi ya kifikra ili ikiwa heri basi achanganywe katika vitabu vya kihistoria na watu mashuhuri kama Mahatma Gandhi, Martin Luther King, Malcom X na wengineo wengi.
Awali aliamini katika kuwabadilisha watu waishio vijijini kwanza kisha ataingia katika miji, ajabu huko vijijini akaishia kuwa kivutio kwa watoto na mama zao. Akipita wanamshangaa na wengine kumfuata nyuma kana kwamba ni ndege aina ya tausi amekatiza huku amechanua mbawa zake za kuvutia. Nani ataacha kumshangaa?
Akijaribu kuzungumza nao wanaishia kucheka tu, mwishowe akakabiliana na balaa la muuguzi aliyechanganyikiwa.
Baada ya sakata hili akaamua kubadili mbinu.
Akazungumza na Cherry ambaye siku zote alibaki kuwa msikilizaji mkuu. Akamweleza nia yake mpya.
“Mjini kuna wengi wameelimika tuanze na hao kisha hawahawa wataelimisha ndugu zao wa huko vijijini. Maana hata hao wa mjini waliwahi kuishi vijijini” Alifanya mawasilisho yale, Cherry akakubali kwa kutikisa kichwa.
Baada ya siku tatu walihamishia makazi katika mojawapo ya jiji kubwa huko Mashariki ya mbali.
Kitendo cha kutambua kuwa wameingia jijini sasa Danstan alitarajia kuzipata zile starehe za jiji la Mainstream anapotokea. Usafiri wa kisasa usiokuwa na changamoto za kubanana na kuharibu ratiba na mengineyo.
Lakini mambo yakawa zaidi ya kinyume ikiwa pana neno linaloweza kumaanisha hivyo.
Maji ukiyavulia nguo abadani uyaoge.
Danstan akalazimika kuvumilia. Japokuwa akilala usiku zinamjia ndoto za mauzauza, anajiona yu katika daladala iliyosheheni abiria waliozidi kiasi, anakumbwa na fukuto la joto kali kutokana na ule mbanano, na bado kuna foleni kubwa sana kiasi cha kutisha.
Alikuwa anatishika yeye na Cherry tu!
Wengine walikuwa wanatabasamu huku majasho yakiwatiririka, walikuwa wanabadilishana masimulizi ya michezo na siasa kwa furaha zote. Mwisho walifika katika vituo vyao wakaagana na kukubaliana kukutana tena siku inayofuata katika karaha ile ya usafiri.
AJABU hawakutumia maneno mabaya juu ya namna ile ya usafiri! Hawakuulaani, hawakuonyesha chuki za wazi.
Nani ajuaye, yumkini walifanya hivyo miaka iliyopita. Wakalaani na kulalamika lakini hakuna lililobadilika ya nini sasa kuendelea kuipiga ngoma isiyosikilizwa na yeyote.
Kasoro Danstan na Cherry! Wao walilalamika kila kukicha.
Hawa nduguze wa hiari aliowakuta Mashariki ya mbali ni kama walikuwa na utaratibu maalumu wa kukutana katika kumbi za starehe kwa ajili ya kujipongeza kwa shida walizokuwa wanapitia.
Ama la, waliokuwa wanajazana katika kumbi za starehe pasi na kujali hii ni siku ya kazi ama la, walikuwa ni wale waliosababisha maisha yawe magumu kiasi cha kutisha.
Walinyanyua chupa zao juu na kugonganisha kwa furaha.
Wanasherekea nini hawa?
Haya yalibaki maswali ya kujiuliza. Asingetokea wa kukupatia jawabu.
________

Mwishowe penzi likawa mzigo mzito, Cherry akamwomba Danstan aanze kwenda peke yake katika hizo anazoziita hekaheka za ukombozi. Siku hii alizungumza kwa jazba sana.
“Upumbavu kiasi gani kuwabeba watu wasiobebeka. Watu hawajihurumii wewe unawahurumia, kwani umekuwa msaidizi wa Mungu ulimwenguni, kuna waraka umepewa uutimize, haupo katika njia sahihi laazizi, umebeba mzigo usiokuwa salama.” Alizungumza mengi. Danstan akamruhusu abaki nyumbani yeye ataendelea kwa muda wa siku tatu kisha watakata tikiti na kurejea nchini kwao.
Pakapambazuka. Ili ianze kuhesabika siku ya kwanza, ije ya pili kisha ifuate siku ya mwisho katika nchi ya Mashariki ya mbali.
Masaa sabini na mawili ya mwisho.
Mapambazuko yakatua habari mpya katika jiji lile.
Jiji la Fununu!
Ile Danstan anatoka nje kukiendea kituo cha daladala tayari kwa ajili ya kuzianza hekaheka, akafuatwa na watu wawili waliokuwa wakimtazama kwa makini na hadhari kubwa kana kwamba ameshika bomu na muda si mrefu anajitoa muhanga.
Danstan akahisi ni vibaka, maana alikwishayasikia mengi sana. Akajiandaa kutimua mbio iwapo watamkaribia.
Kosa kubwa sana!
Walipomkaribia kweli akaanza kurudi nyuma.
“Simama!” wakamuamuru…. Danstan akapigia mstari ile dhana yake ya awali, akaamua kutimua mbio.
Mara ikasikika amri kwa sauti ya juu sasa.
“Shoot!” ilipomalizika kauli ile iliyokuwa inangojewa kwa hamu, mlio wa risasi ukasikika. Danstan kwa macho yake akashuhudia binti asiyezidi miaka kumi na nane aliyekuwa mbele yake akirushwa mbele zaidi huku kifua chake kikifumuka na kuupunguzia moyo kazi ya kusukuma damu kila siku bila kufanikisha azma yake ya kuitoa nje.
Damu ilitapakaa! Danstan akasimama ghafla kana kwamba ni muhusika katika filamu ameambiwa agande vile alivyo.
Alikuwa anatetemeka sana. Alikuwa ameshuhudia rangi ya kifo mbele yake.
Akiwa palepale ghafla alirukiwa na watu watatu, alichoambulia kuona ni ngumi iliyolenga sikio lake, akainama kuikwepa. Hakuambulia kutambua ni kitu gani alipigwa nacho hadi akawa laini katika maungio yake ndani ya muda mfupi.
Baada ya hapo akatiwa pingu mikono ikiwa nyuma, akazongwazongwa akiwa anatazama na mitutu ya bunduki, mtaa mzima ukiwa unamshangaa yeye na lile tukio kiujumla.
Akafikishwa katika karandinga akarushwa kama mzigo wa mahindi usiokuwa na mwenyewe.
Gari ikatimua vumbi na kuwaacha wanamashariki ya mbali kila mmoja akijitengenezea simulizi yake ya kuvutia juu ya tukio lile.
Kila mmoja akaamini simulizi yake na akikataa katakata simulizi ya mwenzake.
Wakaimaliza siku na kuwahi kufunga ofisi zao ili wakawasimulie wake na waume zao nyumbani.
Ili iweje? Mi sijui labda unajua wewe!!

__________

Safari ile ilichukua dakika zipatazo arobaini na tano hadi kufikia kikomo. Akateremshwa akiwa chini ya ulinzi mkali mno. Maswali yote aliyoulizwa ni aidha asijibiwe ama la alijibiwa kwa kipigo bila kujalisha ni wapi amepigwa.
Mzobemzobe akarushwarushwa hadi akakifikia chumba alichopangiwa kuhifadhiwa.
Alirushwa humo baada ya kufunguliwa zile pingu na kisha lango likafungwa.
Harufu kali ya uvundo ikampokea. Akili yake ilikuwa malikiti, akishindwa kuunganisha ku na ni ili atambue kuna’ni kimejiri. Alibaki kulitazama jambo lile kama mchezo wa kuigiza ambao hapo awali hakuwahi kuushiriki.
Macho yake yalipokizoea kile chumba, akaona wadudu wadogo wadogo wakiwa wanatambaa. Macho yakaona na wakati huohuo mwili nao ukaanza kuhisi kuwashwa.
“Bed buds!” alitokwa na kauli ile kwa mshtuko!
Alikuwa amekutana na kunguni kwa vitendo, achana na yale aliyoyasoma kwenye daftari akiwa nchini kwao.
Walikuwa wametapakaa kila kona, na bila shaka walikuwa wameinusa harufu ya damu na ulikuwa muda wao muafaka kupata chakula wakipendacho, na baadhi tayari walikuwa wameanza kunywa damu ya Danstan.
Raha iliyoje kwa wadudiu hawa siku ya leo. Damu yenye ladha tofauti…
“Nitoe humuuuu! Nimefanya nini mimi… nitoeni!” alianza kupiga kelele, hakujibiwa hadi sauti yake ilipoanza kukauka.
Akabaki kububujikwa na machozi, kamasi zikitiririka pasi na kuzuiliwa. Kunguni wao waliendelea kufanya sherehe.
Kunguni wa Mashariki ya mbali, hawajali wewe ni mfungwa ama mahabusu kwa kudhulumiwa haki yako ama la. Unanyonywa na serikali na wao wanakunyonya kikamilifu.
Baada ya masaa tisa, akapata ugeni kwa mara ya kwanza. Mgeni huyu hakuzungumza neno lolote licha ya Danstan kujitia bingwa wa kuzungumza kauli zilizojaa vitisho.
Alichofanya yule bwana ni kumsukumia sahani ndogo ya bati isiyokuwa katika hali ya usafi.
Sahani ile ilibeba shehena ndogo ya ugali na majimaji yaliyojitia yana undugu na zile mbegu za maharage zinazohesabika. Ilimradi tu litokee la kuitwa ‘ugali na maharage’
Hakuelezwa lolote zaidi alipaswa kujiongeza.
Kwa hasira za ki-Semedari, Danstani akakipiga teke kile kisahani, ugali ukaruka kivyake, yale majimaji yakafuta undugu na mbegu za maharage kila mmoja akaishi kwake.
Mleta chakula hakutikisika hata kidogo, akaendelea na shughuli zake katika vyumba vingine.
Labda alikuwa na dharau!
Ama alikwishazoea kuziona hasira za namna ile.
Danstan alijisahau kuwa pale sio Semedari, ambapo mahabusu ukiomba kahawa yenye mchanganyiko wa maziwa na sukari kwa mbali unaletewa, ukilalamika baridi shuka zito linaletwa. Na hapo bado hujaomba mwanasheria wako afike haraka iwezekanavyo.
Masaa tisa baadaye kiza kikiwa kinene Danstan akiwa hana uwezo wa kuona kabisa, tumbo lilimkumbusha kuwa hata kupapasa ni ishara ya kutafuta na kamwe njaa haimfai mtu!!
Danstan akaanza kupapasa ni wapi ulipojificha ugali na zipo wapi zile mbegu za maharage!!
Wakati yeye anapapasa kutafuta chakula, kunguni nao walikuwa hawataki kufanyiana zamu. Walimnyonya kwa pamoja hadi akanyonyeka!!
Haikuwa ndoto!
Danstan alikuwa gereza la mahabusu nchini Mashariki ya mbali, asijue cha wala chu iliyosababisha awe pale.

#Tukutane katika ‘comments’ tupige soga… kuisubiri keshoooo katika muendelezo.
 
RIWAYA: MASHARIKI YA MBALI
KALAMU YA: George Iron Mosenya

“KIBURI CHA UZIMA ni gonjwa sugu linaloishi katika asilimia 90 ya wanadamu. Maisha ya kujisahau kuwa kuna kesho, ujivuni wa kudhani hata pumzi hii inanunulika, urefu wa kuhisi lijalo tunaliona unatuendesha. Kwa sababu maumivu si yako usidhani hautaumia kamwe, kwa sababu kiu si chako usiamini koo lako litaburudika milele. Maisha ni mchezo wa riadha, ipo siku mwenye shida atakukabidhi kijiti.

NA HII NI SEHEMU YA NANE.

Alichoambulia kupata ni kile kipande cha ugali, akajaribu kukigugumia, kilikuwa kigumu sana akajaribu kukilainisha na mate kiduchu yaliyochanganyikana na ute wa damu katika kinywa chake. Akafanikiwa kumeza tonge la kwanza japo kwa shida.
Tonge la pili la ugali ule mkavu akaliskia lilivyochubua koo lake, na hakuweza kuthubutu kumeza tonge la tatu japo alikuwa yungali katika uhitaji mkubwa sana.
Njaa ilikuwa inamsulubu. Lakini angeweza vipi kulimeza angali mate yalikuwa yamemkauka kinywani na kiu kikali kikivuma katika koo lake?
Danstan alikuwa amepatikana.

Ikawa haiwi hatimaye ikawa mapambazuko. Jua likachomoza na kuleta mwanga katika kile chumba kilichomuhifadhi yeye anayetambua mema na mabaya pamoja na kunguni wanaotambua ladha ya damu pekee.
Haukupita muda mrefu tangu mwanga ukijulie hali chumba kile, aliyeleta ugali siku iliyopita akafanya ziara tena katika kile chumba. Sasa alikuwa na kikombe kilichosheheni uji.
Kama kawaida yake hazungumzi zaidi ya kutenda. Akaiomba sahani kwa vitendo kisha akaacha uji pale.
Danstan hakuleta madeko tena na hasira za ki-semedari.
Akakitwaa kile kikombe na kufakamia kwa fujo uji ule usiokuwa katika viwango vya kuitwa uji.
Ilimradi uji! Kama una jina bora zaidi waweza kuubatiza.
Haukuwa na sukari, na mabuje yalijitengeneza kwa wingi.
Mabuje ambayo ukiyapasua ni unga mbichi kabisa.
Uji ule ukatuliza kwa kiasi kidogo njaa kali iliyokuwa ikiishi katika tumbo la Danstan.
Upweke ukaendelea kwa masaa kadhaa kabla hajasikia vishindo kuelekea upande aliokuwa, akajiuliza iwapo ni muda wa chakula tena ama. Maana alikuwa amepitiwa na usingizi na hakujua ni saa ngapi.
Naam! Ule ujio ulielekea alipokuwa yeye, lango likafunguliwa, wakasukumwa watu watatu wakaungana naye katika kile chumba. Mmoja akajikwaa katika ndoo iliyotumika kwa ajili ya kuhifadhi haja ndogo. Almanusura imwagike, ikayumba kushoto na kulia kisha ikatulia.
Ingizo lao likaambatana na harufu kali ya damu ya mwanadamu.
Walikuwa wametoka kuchakazwa kabla ya kufikishwa pale.
“Zungu vipi?” mmoja kati yao akamjulia hali kwa lugha ya mashariki ya mbali ambayo alikuwa akiitambua vyema.
“Safi! Poleni” alijibu kwa utulivu Danstan. Huku katika nafsi yake akikiri kuwa wale jamaa walikuwa wamepigwa wakapigika.
“”Mbona umetuingiza katika kesi isiyotuhusu mzee?” mwingine akamtupia swali.
Kesi! Alistaajabu Danstan.
“Kesi gani angali mimi mwenyewe sijui kwanini nimedhalilishwa namna hii mpaka sasa. Nataka niwaombe niongee na wakili wa familia yetu, afunge safari aje kutazama haya yanayotokea kama ni haki kwangu. Sikubali na sitokaa nikubali hili jambo liishe hivihivi.” Alilalamika Danstan, sasa nafsi yake ikipata nafuu kidogo kwa sababu alikuwa walau amepata mtu wa kuzungumza naye.
“Wakili? Yupo wapi wakili wa familia yako…”
“Mainstream Semedari” alijibu kwa kujiamini.
Mmoja kati ya wale watu aliangua kicheko na kusababisha wenzake nao kuanza kucheka.
“Kesi yako ni nzito sana, sisi tunakuomba Zungu, tusaidie tutoke. Sisi hatukujui wala wewe hautujui. Yawezekana umeteswa sana ndo maana umetuweka katika orodha…. Tunakuomba sana. Mfano mimi nina mke na mtoto halafu mke wangu ni mjamzito kwa sasa, kila kitu ananitegemea mimi. Sikatai kuwa nauza majani ya bangi lakini sio hii kesi niliyopewa mimi” Mmojawao aliendelea kusihi kwa sauti iliyotawaliwa na unyonge.
Danstan akalazimika kuelezea kwa ufupi juu ya ujio wake katika nchi ya Mashariki ya mbali hadi kufikia kukumbwa na mkasa ule wa kustaajabisha. Mkasa ambao hadi wakati huo hakukijua chanzo chake.
Simulizi yake ikawachanganya wale mabwana walioamini kuwa mle ndani wapo pamoja na mtu sahihi kabisa ambaye kusema kwake ukweli kutawapa nafuu katika kesi hiyo.
Kesi ya uuzaji na utumiaji wa madawa ya kulevya.
Danstan alisisimka sana kutambua kuwa amehusishwa katika kesi kubwa kiasi kile, jasho lilianza kumtiririka kuanzia kichwani, likashuka mpaka mgongoni na kisha kupenya hadi katikati ya miamba miwili ya makalio yake.
Alikuwa amechanganyikiwa!
“Ndugu yetu kama hili jambo hujafanya kweli, hata usihangaike kudai kuitiwa wakili wako. Usitarajie kuwa ataitwa…. Sembuse kukusikiliza tu.
Kama katika kukupekua ungekutwa na vipoozeo vizuri kama wenzetu watatu walioachiwa huru basi ingekuwa nafuu. Hapa Mashariki ya mbali ni tofauti sana na nchini kwenu. Hapa kwetu kumiliki kadi ya chama tawala ni turufu isiyokuwa na kifani, huwezi kujua hilo mpaka uingie matatani, wao wa chama tawala wanajiamini kuwa ni malaika watakatifu wasiofanya makosa angali wale wanaokipinga chama tawala ni mashetani wenye vichwa tisa ambao unatakiwa kuishinao kwa makini mno. Wenzetu katika kupekuliwa wamekutwa na kadi za chama tawala, hawa hawakupata mateso makali kama tuliyopata sisi, na ghafla bin vuu wameachiwa huru. Sisi nduminakuwili tusioeleweka tupo hapa tunasota na wewe.
Na wewe zungu nchi hii itakusumbua sana, kama shughuli zako nd’o hizo za kufungua akili za watu kifikra basi umefanya kosa la jinai linalofanania na kuua watu thelathini kwa kuwachinja shingo zao kisha unatarajia kushinda kesi.
Mashariki ya mbali tuachie sisi wana-mashariki, hapa mashariki wachache sana wanaojua, wengi ni wajuaji, ukijifanya unautoa ule ujuaji wao wanakupachika kile cheo chao wasichokijua wanakuita wewe mjuaji. Kumweleza mtu kuvuta sigara katika hadhara si jambo la kistaarabu na ni hatari kwa afya, hapa kwetu mtu huyo atakuhukumu kana kwamba umeutukana uchi wa mama aliyemzaa.
Sijafika katika nchi yako lakini naamini fika kuwa mtuhumiwa anaweza kumshtaki askari iwapo alimpiga ama kumnyanyasa wakati wa kumuhoji. Ila huku kwetu ni tofauti, jitazame vyema hadi sasa haujavunjika zungu, kwa kitendo hicho cha wewe kuweza kusimama wima hii ni dharau tosha kwa waliokukamata na huko walipo wanachekwa kuwa wao ni dhaifu. Uimara wa askari wetu ni kuweza kuvunja taya ya mtuhumiwa, kumtoa meno, kumvunja miguu na kumpasua kichwa. Na kuna wale wanapewa hadi vyeo kwa kufanikiwa kumuua mtuhumiwa nasisitiza ni mtuhumiwa so mshtakiwa wala mfungwa. Kwa kifupi baadhi ya askari wetu akili kichwani hakuna hata kile kielimu kidogo cha kutofautisha mtuhumiwa na mshtakiwa hawajui. Lakini naomba nisiwashushie lawama sana, naamini ule upuuzi na ushenzi wanaofanyiwa wangali katika kambi za jeshi unachangia unyama huu.
Zungu ukijiunga na jeshi la nchi yetu ya Mashariki ya mbali umejiunga katika chuo kidogo cha jehanamu kinachotoa mafunzo katika ngazi ya astashahada.
Utafundishwa matusi na kulazimishwa kuyasema katika namna ya kughani, utayumbishwa imani za dini unayoamini, utatukaniwa wazazi wako wote na utapaswa kushukuru baada ya kutukanwa.
Usiombe ukakutana na askari aliyetoka huko. Atakuviringisha asua zilizobeba kende zako huku anakutazama usoni jinsi mwanaume mzima unavyotoa machozi na kutoa kijisauti kama mtoto wa kike. Hiyo nd’o furaha yake.
Zungu jiandae kisaikolojia, wewe ni zungu la unga na ni mtu hatari sana kwa taifa hili kwa sasa. Utaviringishwa korodani zako, zikipasuka hiyo ni juu yako, utavunjwa miguu, ukipelekwa hospitali hautakuwa na uchaguzi wataamuru ukatwe, ukijifanya jeuri sana hutaki kukiri kuwa wewe ni zungu la unga. Watakuzika ukiwa hai.
Pole zungu!” alimaliza bwana yule ambaye alionekana kuwa ni mzoefu sana wa maisha yale ya jela.
Zungu akaanza kulia kama mtoto mdogo aliyefokewa ghafla na mama yake baada ya kuomba nyonyo. Na kwa mara ya kwanza kwa dhati kabisa akaijutia ile siku aliyoamua kufunga safari kuitembelea Mashariki ya mbali.
Lakini majuto yale yangesaidia nini angali tayari yu nyuma ya milango ngangari ya chuma.
Milango ambayo wachawi wanakiri kuwa hata wao wakiingizwa mule uchawi wao unakimbia kwa jinsi panavyotisha.
Alipokumbuka kauli ya asua zake kufinyangwa, alijikuta akibana miguu yake kana kwamba anazuia zisifinyangwe.

#Nini hatma ya Zungu Danstan katika mkasa huu????

TUKUTANE TENA KATIKA SEHEMU IJAYO

ANGALIZO: Ikitokea kuna neon la Kiswahili limetumika katika simulizi na hujui maana yake, usisite kuuliza katika ‘comments’….
 
RIWAYA” MASHARIKI YA MBALI
KALAMU YA: George Iron Mosenya

SEHEMU YA TISA

ILIANZA kama siku moja ya kukamatwa bahati mbaya, labda kwa kufananishwa, kisha ikawa siku ya pili na kuendelea na sasa zilikuwa zimetimia siku thenashara tangu Danstan akamatwe ghafla, na hakuna hatua yoyote iliyokuwa imechukuliwa dhidi yake. Hakuwa ameandikishwa maelezo na wala kusikia dalili ya kupelekwa mahakamani.
Zaidi aliishia kuzikariri ratiba za ugali na maharage pamoja na uji uliojitwika mabuje.
Midevu ilikuwa imeweka kambi katika kidevu chake na masharubu yakimning’inia katika namna isiyopendeza.
Alikuwa amekonda hadi kichwa kiasi kwamba macho yake yakachukua utawala na kuonekana ukubwa waake kana kwamba ameyakodoa muda wote, mbavu zake zilikuwa zinafanya maonyesho ya wazi hata mtoto anayejifunza kuhesabu angeweza kuzihesabu vyema pasi na kuzigusa.
Kwa kutumia macho tu!
Waliingizwa watu mle ndani wakatoka wakaingizwa wengine yeye akiwa palepale. Yeye pamoja na wenzake kadhaa waliounganishwa katika shtaka moja.
Danstan hakuijua hatma yake, kila wanapoletewa chakula alikuwa akimuuliza yule askari mwenye dhamana ile kuwa ni lini atafikishwa mahakamani. Askari yule aliishi kama asiyekuwa na uwezo wa kuongea lakini anayesikia.
Alikuwa akimtazama tu kisha anaendelea na shughuli za kugawa chakula kile kibovu cha gerezani.
Siku ya kumi na mbili ustahimilivu ukamshinda Danstan, akajikuta akimtolea maneno makali yule askari anayesikia na asijibu chochote.
Kama kawaida mchezo ukawa uleule, akaishia kutazamwa na kisha akapuuziwa.
Lakini siku hii alitazamwa mara mbili.
Haijawahi kutokea.
“Umeyaona macho yake yaliyokutazama mara yaa pili” Uwesu alimuuliza Danstan baada ya bwana yule kuondoka.
“Vyovyote atakavyonitazama cha msingi nimemueleza ukweli na natakiwa kupewa haaki yangu.” Alifoka Danstan.
“Nakuuliza uliyaona macho yake lakini!” Uwesu akarudia kauli yake.
“Yamefanya nini?” aliuliza Danstan.
“Yamewaka kwa ghadhabu, ni kama yupo tayaari kukuua.” Alizungumza kwa sauti ya chini huku akipambana kuumuua kunguni aliyemnasa akimnyonya dmu.
“Nipo tayari kwa lolote.ni heri waniue tu kama wamenuia kufanya hivyo.” Alisisitiza Danstan
“Unavyozungumza kishujaa utasema uliwahi kufa ukafufuka na sasa umezoea kifo.” Uwesu mmoja kati y wanaoshutumiwa kuwa pamoja na zungu la unga akamdhihaki.

_______________
Majira ya saa kumi na moja jioni, jua likiwa linaanza safari yake kuiaga Mashariki ya mbali na kuibukia kwingine. Lango la gereza lilifunguliwa kisha zikasikika hatua za mabuti mazito ya kijeshi zikipishana.
Zilianza kusikika tokea mbali na kituo kikawa ni katika lile lango alilokuwa akiishi Danstan na wenzake.
Lango likafunguliwa, mwanajeshi mmoja aliyevalia magwanda yake rasmi akapiga hatua moja kubwa.
“Wewe! Kuja huku.” Alizungumza akimtazama Danstan. Kwa hofu Danstan akasimama wima, mwanajeshi akatoka na lango likafungwa.
Danstan nyuma mwanajeshi mbele.
Walipofika nje, akapokelewa na wanajeshi wengine wanne, hawa walikuwa wamebeba mitutu ya bunduki.
Akaamrishwa kuchuchumaa chini, na amri iliyofuata ni kuwafuata nyuma huku akiwa anaruka ruka kama chura mwenye furaha.
Haikuwa safari fupi. Na wao hawakuonekana kujali zaidi ya kumpiga mateke pindi alipokuwa akipumzika.
Danstan alilia kama mtoto mdogo huku akiwalaani kimoyomoyo.
Baada ya hali kuwa ngumu Danstan akafanya kosa kubwa ambalo hufanywa na wanadamu wengi.
Ulimi wake ukateleza akaropoka, ‘https://jamii.app/JFUserGuide!!’.
Japo neno lile hakulitoa kwa kumtusi yeyote, lakini likasafiri kwa kasi hadi katika masikio ya wanajeshi wale vijana waliovimba kwa mazoezi.
Ni kama waliambizana kwa pamoja ‘tumnyooshe mbweha huyu’.
Hakuwepo wa kumzuia mwenzake katika ule ukumbi bali kupambana nani apige zaidi ya mwenzake, mwingine alikuwa na rungu kubwa akalituliza katika mguu wa Danstan, yowe kubwa likamtoka. Lakini lingeenda wapi yowe lile zaidi ya kuishia katika kuta nene za gereza, kuta zinazoficha kila aina ya uovu, uzandiki na chokochoko zote ambazo zinaileta ile maana ya jela ya Mashariki ya mbali ni sawasawa na kaburi lenye mateso makali lakini hakuna wa kuyasimulia maana ukizikwa humo hutoki.
Zile mbavu zilizokuwa zinachungulia kinachojiri ulimwenguni, zilikutana na buti zito la kijeshi, Danstan akajikunja kwa maumivu makali lakini sasa hakuweza hata kutoa sauti ‘nyee!’. Maumivu yalikuwa makali mno.
Baada ya kipigo cha paka shume aliyenaswa katika tego, Danstan alitelekezwa pale akiwa robo tatu mfu, na robo pekee akiwa na uhai.
Aliachwa katika ukumbi ule akiwa anavuja damu, na mguu wake ukiwa umekufa ganzi asijue kama umekatika, umevunjika ama vyovyote vile.
Baada ya dakika thelethini, akaburutwa na askari magereza hadi katika chumba alichokuwa amehifadhiwa awali.
Akiwa hana hali hata kidogo. Macho yake yaliishia kuona ukungu mbele yake huku masikio yakivumishwa na sauti za vipyenga vinavyorindima kana kwamba kuna lundo la watu wanashangilia jambo.
Hakuhisi uwepo wa mwili wake hata kiduchu, pua zake zilibaki kutambua harufu kali ya damu.
Damu iliyokuwa inamvuja katika paji la uso wake na popote walipoamua kumpasua.
Hatimaye macho yakajifumba na alipoyafumbua katika fikra zake akajikuta yungali nchini Semedari jijini Mainstream.
Alikuwa ameketi na Daniel katunzi wakibadilishana mawazo baada ya kuwa wamecheza mchezo wa ‘chess’ kwa muda mrefu hata wakachoka.
Danstan akamuuliza jambo.
“Mbona tulipokwenda kumsalimia Anko Paul gerezani haukuwa sawa kabisa, ni kama uliyekuwa katika mchanganyiko wa kushangaa na kukumbuka jambo. Vipi ilikuwa mara yako ya kwanza kufika gerezani, usitake kuniambia kule mashariki ya mbali ulipozaliwa watu hawaruhusiwi kutembelea wafungwa.
Daniel akaketi vyema, akajikohoza.

DANIEL ANASIMULIA.

Tunakwenda kuwasalimia ndugu zetu katika magereza.
Lakini utakapolifikia geti la kuingia gerezani ndipo utagundua kuwa mfungwa katika nchi yetu sio mwanadamu tena. Utawakuta akina mama pale nje wanauza matunda kama ndizi na machungwa. Pia wanauza karanga. Na hawa wote ukifuatilia ni wake na mahawara wa ma askari magereza. Watakuuzia kwa bei ghali na wanakusisitiza kuwa usije ukathubutu kuingia na chakula ulichotoka nacho nyumbani hata kama ni ndizi kama zao.
Unabaki unajiuliza wanaogopa nini. Wanazuia sumu gerezani ama ni kitu gani.
Vipi nikinunua hizohizo ndizi zao kisha nikazitia sumu? Itabadili maana?
Wehu!
Ikifikia sasa namna ya kusalimia ndugu ndipo utalazimika kucheka huku macho yakitoa machozi.
Mnaruhusiwa kuingia watu ishirini hadi thelathini kwa pamoja. Na wafungwa wanaingia zaidi ya ishirini. Mmetenganishwa na wavu, na vyuma vya kutosha na hapo mpo umbali unaoweza kufikia mita sita.
Unapaswa kupaza sauti haswa ili ndugu yako akusikie, naye atapaswa kupayuka ili upate jawabu.
Hakuna siri! Hakuna uhuru!
Hata kama unataka kumweleza kuwa mkewe kaolewa na bwana mwingine inabidi upayuke tu. Ama mkewe katoa ile mimba aliyomwacha nayo, bado inabidi upayuke.
Lakini hakuna la kujali we payuka tu. Hakuna anayesikiliza la mwenzake pale.

Kwanza ukishahukumiwa na kwenda jela, ile siku ya hukumu ndo siku yako ya mwisho ya kuwa na haki. Huko kwetu mfungwa ni mdogo wake na shetani baba mmoja mama mmoja na wamenyonya titi la mama mmoja kwa zamu wakipokezana katika ukuaji wao.
Mtazamo huu mmeturithisha ninyi watu weupe, mmetufundisha vitu viovu sana ambavyo ninyi hamvifanyi.
Hata nje ya gereza ujinga mwingi tu mmetupatia halafu mkatuacha tuubebe tukijidanganya na ninyi mmeubeba.
Wakati mnatutawala huko mlitunyanyasa sana, sina maana mbaya tena bali najaribu kukusimulia uifahamu vyema nchi yangu, na hii itakusaidia sana siku moja ukifika huko bahati mbaya japo natambua huwezi kufikiria kwenda huko.
Kabla ya uhuru magereza yalikuwa kwa ajili ya watu weusi pekee huko nchini kwetu, mlituweka huko na kutuacha tufe kwa mateso na kukosa chakula. Kwa makosa kama, kuchoka na kushindwa kulima mashamba yenu katika ardhi yetu, kosa la kuugua na kushindwa kupanga vyuma vya reli ambayo mtaitumia kusafirisha bidhaa zetu, kuna ambao walipelekwa jela kwa kosa tu la kukutana na ngozi nyeupe barabarani na kisha kupishana naye. Hebu fikiria kosa la kupishana na mtu barabarani bila kumbughudhi unahukumiwa kunyongwa. Hatutasahau kamwe na sidhani kama waliofanyiwa hivyo wakiamshwa katika usingizi wao sasa watakubali walau kutoa msamaha.
Kama ilivyo ada, vimbelembele huwa hawakosekani, yaani sisi wenyewe weusi kwa weusi tukaanza unafiki. Tukachomeana utambi…
Wale mabingwa wa kuchomea wenzao utambi ili wakamatwe na kutupwa gerezani wakapewa vyeo na kuwa askari wasiokuwa hata na mafunzo.
Hawa wakafanywa wahudumu wa magereza. Walijionea na kukenua meno wakitazama mweusi mwenzao akikatwa sikio, akinyongwa akichapwa viboko mbele ya hadhara.
Kitendo chao cha kuwa waaminifu mbele ya wakoloni pamoja na kuwaiga kila wafanyacho kukaimarisha urafiki wao. Wakaanza kujiona na wao ni ngozi nyeupe ndani ya mioyo yao huku wakiwa na rangi nyeusi nje kwa bahati mbaya kabisa.
Wakaanza kusahau kwao.
Hata ulipopatikana uhuru ni walewale watu weusi wanaojiongopea wana roho nyeupe walibaki kuwa viongozi wa magereza.
Ule ‘uuaji’ waliorithi kutoka kwenu ninyi wakauhamishia kwa waajiriwa wapya.
Sasa askari alifundishwa kuwa kutesa ni mojawapo ya sifa kuu za kuwa askari. Wakajazwa upepo mchafu pia wa kikoloni ulioitwa lamensia-tanganyikana. Yaani ni heri watu mia moja wasiokuwa na makosa wafie gerezani kuliko mkosaji mmoja kubaki uraiani.
Kama nilivyosema awali, mlitupa vilivyooza ninyi mkaondoka na visafi. Kwenu hata sasa naiona lamensia-anglikana. Hii inasema kuwa ni heri waasi mia moja wabaki mtaaji kuliko mwenye haki mmoja kwenda jela kimakosa.
Sasa fikiria mwenye haki yungali gerezani nchini Mashariki ya mbali, anateswa vikali sana ili akili kuwa yeye ni mkosaji.
Danstan! Fumba macho na ufikirie kuhusu hili na isibaki kuwa fikra kwani ni hayo yanatokea nilipozaliwa. Unasimamishwa mbele ya kaburi ambalo limechimbwa tayari, ghafla unasukumwa humo katika shimo hilo linalozidi futi sita, wanakueleza kuwa ukikubali kuwa wewe ni muuaji basi hawakufukii, lakini ukiendelea kukataa wanakufukia na kukuacha ufe kwa mateso wakati ukiziwania pumzi zako. Fumbua macho na unijibu….”
Sauti ya Daniel katunzi ikakoma ghafla….. Danstan akaanza kutapatapa huku na kule.
“Nakubaliii… nakubalii…. Nakubaliii nimeuaaa… nakubaliii” alipiga mayowe yale huku akizidi kutapatapa.
Wenzake waliokuwa katika chumba kimoja wakawahi kumdhibiti kwa sababu alikuwa akijibamiza ukutani na hata asijue nini kimejiri.
Walipofanikiwa kumtuliza, naye akafanikiwa kuyafumbua macho vyema.
Alikuwa yungali katika chumba kilekile cha mahabusu hali yake ikiwa taabani.
Fikra za kuwa yu Mainstream anazungumza na Daniel zikatoweka.
Alikuwa katika nchi ya Mashariki ya mbali.
Hakuwa huru! Alikuwa gerezani akiwa amepondwa akapondeka vilivyo. Uso umemtutumka mithiri ya mtu aliyeng’atwa na mdudu aina ya mavu.
Muonekano wa Danstan ulitisha, alikuwa anakoroma huku donge la damu lililogandiana katikaa pua zake likiwa linapumua kama kiumbe hai. Linavimb n kusinyaa kadri anavyozidi kukoroma.
Shabani, alilaani huku akiwasihi wenzake wafanye japo dua kwa sababu lililomtokea Danstan linakuja kwao pia.
Wesu alimtazama kwa jicho lililokataa tamaa, tayari walijiona wao si wa Mungu walaa wa shetni. Walikuwa tyari ni wanaharashi wasiokuwa na chao duniani, peponi wala motoni.
“Nawaomba ndugu zangu, mniombee hiyo dua. Sijiwezi ninakufa mimi….” Alizungumza kwaa tabu sana Danstan.
“Kama mmojawetu akifanikiwa kutoka humu akiwa hai, basi anisaidie kumtafuta mchumba wangu anaitwa Cherry. Ajue nilipofia… ajue nilipofukiwa.” Danstan alizungumza kwa uchungu mkubwa.
Shaban, alijaribu kumkandakanda lakini nafuu haikupatikna.
Shaban aliyekuwa walau na masalia ya imani kwa mwenyezi Mungu aliamua kutokaakimya. Akaanza kupig kelele akimuita askari magereza yeyote aliyekuwa karibu.
Hii ni kwa usalama wa Danstan.
Alikiona kifo kikimtwaa!

Tukutane katika SEHEMU IJAYO ya riwaya hii……
 
RIWAYA: MASHARIKI YA MBALI
KALAMU YA: George Iron Mosenya

“Ni afadhali kua na jeshi la kondoo linaloongozwa na SIMBA kuliko jeshi la Simba linaloongozwa na KONDOO.”
Tafsiri kadri ya uwezo wako.

NA HII NI SEHEMU YA KUMI.

MTAANI kila mwenye kujua kuongea aliongea, mwenye uwezo wa kuandika aliandika. Magazeti na mitandao mbalimbali ya kijamii iliendelea kuandika tena na tena.
Kila mmoja akijifanya anajua zaidi juu ya sakata la ‘zungu la unga’.
Sifa kemkem zilipeleka kwa mkuu wa majeshi ambaye aliviita vyombo vya habari kwa lengo moja tu.
Kujinadi! Akiwa ameambatana na mkuu wa mkoa.
Kujikweza juu ya mpango madhubuti uliotumika kumtia mikononi zungu la unga.
Mpango gani sasa? Hilo alitambua yeye. Alibaki kuuita mpango madhubuti mbele ya vinasa sauti vile.
Mwandishi mmoja akaomba mpango ule ufafanuliwe kidogo kwa manufaa ya wananchi, mkuu yule akaanza kung’aka kuwa zile ni siri za jeshi na mwananchi anachotakiwa kujua ni kitu kimoja tu.
Zungu la unga ametiwa mikononi mwa jeshi la polisi.
Ajabu! Hilo si tayari kila gazeti lilikuwa limeandika? Aliita vyombo vya habari kwa ajili ya kurudia kusema yaliyokwishasemwa.
Sijui gari yake ilijazwa mafuta ya bei gani kwa safari ile kuufikia ukumbi wa mikutano.
Hilo anajua yeye!
Mkutano ukamalizika waandishi wakibaki bila jipya la kuandika.
Ili wasikose yote, siku iliyofuata wakachapisha picha yake katika kurasa za mbele za magazeti, akiwa amezungukwa na vinasa sauti kutoka vyombo vya habari tofauti.
Gazeti moja likapamba picha ile na maandishi yaliyokolea ino mweusi.
“SIMBA WA MAJESHI AUNGURUMA”
Sitaki kujua alitapatwa na cheko kubwa kiasi gani kwa sifa zile kemkem.
Dhihaka!!

_________

BAADA ya kuzungumza na vyombo vya habari. Habari ile ikapaa hadi nchini Semedari katika jiji la Mainstream.
Daniel Katunzi ambaye siku kadhaa zilizopita akiwa hajapata ujumbe wowote kutoka kwa Danstan alizipa uzito habari zile zilizomtaja zungu la unga bila kutaja majina yake wala picha.
“Isijekuwa Danstan ohoo!” alimweleza mama yake Danstan huku akimwonyesha habari ile katika mitandao ilivyozungumzwa.
Diana aliachia cheko hafifu huku akioneka kutoshtushwa na taarifa ile na ulinganisho wa Daniel.
“Aaah! Danstan havuti Sigara, hanywi pombe, soda zenyewe hanywi anataka juisi pekee. Leo hii awe zungu la unga. Dunia itafikia kikomo chake.” Alizungumza katika namna ya madaha, ikia ni namna ya kumshushua Daniel Katunzi.
Daniel akashusha pumzi zake kisha akaanza kuzungumza pasi na kumkatisha Diana shughuli zake.

DANIEL ANASIMULIA.
KIPINDI cha ukoloni watu weupe waliotutawala pamoja na kuna kitu kibaya sana walituachia bila hata ya wao kujua, na hata wangejua wasingeweza kujali.
Hawajawahi kujali!
Kwa mujibu wa mababu zetu wakoloni walikuwa wanapenda sana sifa.
Yaani wakinyenyekewa wanajiona milango ya mbingu hii hapa wanaitwa waingie. Walipoondoka wakaziacha zile sifa nchini kwetu, bora hata zingekuwa sifa za maana. Walituachia zigo la sifa za kijinga.
Shuleni, katika ofisi mbalimbali. Bosi mkuu anataka sifa za kijinga mbele ya kijana wa masjala, kijana wa masjala anataka sifa za kijinga mbele ya msafisha ofisi, msafisha ofisi anaenda kuzichota sifa kwa mlinzi, mlinzi yeye hana pa kwenda zaidi ya kuzisubiri sifa za kijinga palepale getini.
Hebu fikiria unapeleka barua ya maombi ya kazi, mlinzi wa getini ambaye ana elimu ya ukakamavu pekee anataka aifungue ile barua yako aisome. Kama hautaki ondoka na uchafu wako. Akishaifungua anakutupia swali la kijinga, ‘unatafuta kazi?’. Unatamani ummeze lakini hafai hata kwa kumeza.
Unamjibu ‘ndio’ anakutazama juu hadi chini anakuuliza ‘unataka mshahara shilingi ngapi?.’
Huyo ni mlinzi anajitahidi awezavyo kuikashfu elimu yako na uhitaji. Anafanya jitihad zile kwa sababu anajua fika kuwa ukiipata kazi unayoitafuta itakuwa zamu yake kuogelea katika bwawa la sifa zako.
Hiyo ndo hali halisi ya mashariki ya mbali. Nchi imekaa kisifasifa tu.
Sifa za kijinga!
Sasa usiombe akatokea mtu akafanya jambo la maana, badala asubiri sifa zimfuate atazitafuta kwa nguvu, na akigundua haujamsifia kama alikuwa rafiki yako, basi umeingia katika kundi la maadui zake.
Kupenda huku sifa za kijinga kunaanzia ngazi za chini kabisa na kuweka makazi makuu katika ngazi za juu.
Nikikwambia hadi mkuu wa wilaya anapenda sifa za kijinga utashangaa na kujiuliza iko wapi nidhamu ya uongozi.
Tena akikaa muda wa mwezi mzima bila kupata walau sifa moja ya kijinga hapo ndo anakuwa kama mwendawazimu aliyepoteza makopo yake wakati anakula chakula. Yupo radhi kukiacha kile chakula aanze kukimbia huku na kule akiyasaka makopo yake.
Atafanya kila awezalo aweze kurejesha sifa yake.
Usipokuwa makini unaweza kudhani SIFA ZA KIJINGA zinaleta ongezeko la mshahara nchini Mashariki ya mbali.
Sasa isijekuwa Danstan amekutana na kichaa aliyepoteza makopo akaamua kulala naye mbele kwa kumshutumu kuwa ni yeye ameyaiba makopo yake.
Ile ni nchi yangu na ninaifahamu vyema, akitokea kichaa mmoja mwenye madaraka akasema ni amri kulala saa kumi na moja na nusu jioni na kuamka kumi na moja alfajiri, wewe jifanye mjinga fuata anachosema. Sifa zimjae mpaka kumwagika.
Usitake kuniuliza kama kuna sheria ama la! Nchi yangu ina sheria tena sheria zenyewe ni kali kwelikweli.
Ajabu ni moja tu, sheria zetu zinafanya kazi kwa msimu maalumu. Likitokea jambo ambalo linawagandamiza wasionacho vitabu vya sheria vitafutwa vumbi kisha kifungu nambari mia tisa na nane mlango ‘Ba’ wenye vifungu vidogovidogo vinane, katika kifungu kidogo cha nane kilichogawanyika katika mapande manne madogomadogo, lile pande la nne linasema kwa lugha ya kigeni ambayo maana yake ni kwamba ‘LILILOTOKEA KWA ASIYENACHO NI SAWA TU’.
Awe amenyongwa? SAWA TU!
Kwani wangapi wamekufa?
Labda amekatwa mikono? SAWA TU!
Kwani yeye wa kwanza kuishi bila mikono?
Ama nyumba yake imevunjwa na hajapata stahiki zake? Sawa tu, acha alale nje!
Kwani wangapi wanalala nje?

Asiyenacho anabaki analia na kusaga meno. Wanaita vyombo vya habari na kujitoa hatiani wakidai kuwa asiyenacho asilielie hii nchi inaongozwa na sheria.
Vyombo vya habari vitaanza kumnanga asiyenacho kwa kushindana kuandika maneno machungu dhidi yake.
Nchi yangu mimi kama kweli kuna mchawi anayeweza kuroga eneo kubwa namna ile basi acha niamini kuwa tulirogwa halafu mchawi akaikimbia nchi kama nilivyoikimbia mimi.
Kama Danstan amenasa katika tego la kichaa, nasikitika kuwa atapata tabu kubwa sana. Atayaonja machungu yote ya ukoloni ambayo babu yetu waliyanywa kila kukicha.
Eeh Mwenyezi Mungu muepushie ndugu yangu janga hili.”

DANIEL alimaliza kuzungumza, sasa Diana macho yalikuwa yamemtoka pima. Ule uchungu wa mwana aujuaye mzazi (mwanamke) sasa ulikuwa umeamka upya na kuutawala mwili.
Uso ukawa mwekundu kana kwamba amepakawa basbasi, akashika hiki akaacha akashika kile akakitupa.
Alikuwa amechanganyikiwa kupindukia.
“Kwa hiyo wanataka kusema mwanangu anauza madawa ya kulevya. Hapana huu ni uonevu. Yaani wawachezee haohao, sio kwa mwanangu nasema…” alifoka kama mtu aliyepandwa na maruhani. Yaani ni kama aliyekwisha ambiwa kuwa huyu wa kuitwa Zungu la unga ni mwanaye.
Daniel akamtazama hata asifanye jitihada za kumtuliza.
Kisha akajisemeza yeye na nafsi yake.
“Ukijipeleka huko, na wewe wanakukamata halafu wanaita waandishi wa habari anasema wameweka mitego yao kiintelejensia na wamefanikiwa kulinasa ‘jike la shupa’ pacha wake ‘zungu wa unga’.
Mnaijua Mashariki ya mbali mnaisikia??”
_______

Mlango wa chumba alichokuwa amelala Cherry uligongwa. Mashaka yalikuwa yamejenga urafiki wa dhati na nafsi yake. Danstan alikuwa hajaonekana .
Lugha gongana ikatawala kikao kile kisichokuwa rasmi. Kikao ambacho wajumbe wanne walikuwa wamesimama wima wakizungumza pasi na kupokezana mithiri ya chiriku.
Mjumbe aliyetembelewa ghafla akibaki kusema neno moja kwa kurudiarudia kuwa hakuna anachoelewa. Wale wajumbe walioonekana kuwa na akiba kidogo ya msamiati wa lugha ya kigeni wakapandwa na jazba pasi na sababu za msingi. Wakaanza kutumia nguvu ili waeleweke.
Wakamsisitiza Cherry kuwa mume wake yu mahututi hospitali amekumbwa na ajali mbaya ya gari.
Na hapa walilazimika kutumia lugha ya picha na maneno machache.
“Zis man is sick, very sick in accident. Les go!”
Kwa jasho sana hatimaye wakaeleweka.
Cherry akatoka nduki akiandamana nao.
Akakwea karandinga la polisi.
Likatoweka kwa fujo.

Haikuwa safari ya hospitali. Bali katika nyumba iliyoitwa salama japo usalama wake haukuonekana.
Pengine ilikuwa salama kwao kwa sababu wangeweza kukufanyia lolote na jamii ising’amue.
Akakalishwa chini!
Alipouliza mchumba wake yu wapi aweze kumuona. Akatulizwa na bwana ambaye huyu alikuwa anaweza kuzungumza vyema lugha ya kigeni.
Kwa utulivu kabisa akamweleza Cherry kuwa Danstan yupo gerezani kwa tuhuma za uzalishaji na uuzaji wa madawa ya kulevya.
“Tena baada ya kumbana sana amesema kuwa mnashirikiana bega kwa bega katika shughuli hii. Binti mrembo kama wewe unauza madawa? Kwanini sasa” alizungumza kwa utulivu aliyepewa dhamana hiyo.
Cherry ambaye alikuwa roho juu kuhofia usalama wa Danstan ambaye aliongopewa kuwa alipata ajali, akaongezewa tena hili la kutisha zaidi.
Drug cartel!

Moyo uliokwishalalamika sana kwa kuwekwa juujuu tangu anarushwa katika karandinga, ukakosa uvumilivu wa ziada. Ukapunguza zile sifa zake za kukita sana kifuani, ukanywea usiamini hata kidogo kuwa ulikuwa umebebwa katika kifua cha ‘drug dealer’. Moyo ukafanya mgomo wa kusukuma damu kwa kasi, ubongo ukaunga mkono harakati za moyo uliochukia.
Cherry akatoa kauli isiyoeleweka kisha kama mzigo akateleza kutoka kaltika kile kiti akatua chini.
Puu!

#Kizaazaa kimehamia SEMEDARI….. je? Nini hatma ya Danstan ndani ya mashariki ya mbali, na vipi mama yake akihakikishiwa kuwa mwanaye ndiye zungu la unga??
Na Cherry yamemkuta yepi??

TUKUTANE KATIKA SEHEMU IJAYO!!
Maoni yako ni muhimu sana.
 
Alosto chief
 
Back
Top Bottom