Riwaya: Kiguu na njia

KWA ANAYEKIHITAJI KITABU HIKI CHA KIGUU NA NJIA NA VINGINE VYA BEN MTOBWA KAMA DAR ES SALAAM USIKU, SALAMU TOKA KUZIMU, TUTARUDI NA ROHO ZETU NA VINGINE VINGI, NITAFUTE KWA KUPITIA 0712504985 AU 0763044459. KARIBUNI.
“Nani anasema uongo, nani anasema ukweli kati yenu?” aliniuliza. “Juzi tu,” aliongeza. “Alikuja huyu kijana, akatuambia kwamba anaitwa Cheyo na ni mtoto wa chifu Masanja. Kwa maelezo yake baba yake hataki aje shule, anataka akae nyumbani kusubiri kurithi Uchifu wake atakapokufa. Kwamba amekuja hapa shuleni kwa kutoroka baada ya jitihada za kumsihi baba yake kumruhusu kushindikana. Na kwa jina na nafasi yake ilikuwa wazi bado tumempokea na kumruhusu kuendelea na masomo. Leo umekuja wewe. Unadai wewe ni Cheyo mtoto wa Chifu Masanja na una barua yake ya kuomba upokelewe hapa. Nataka kujua nani mkweli nani mwongo kati yenu,” aliniuliza akitutazama kwa zamu. Cheyo naye alishangaa. Akageuka kunitazama. Nilijitahidi kuinua uso wangu nimtazame pia, ilikuwa kazi ngumu kuliko zote nilizopata kufanya. Hicho kidogo nilichobahatika kuona katika uso wake kilionyesha wazi kuwa si kwamba hatufahamiani tu, bali pia tulikuwa hatufanani kwa namna yoyote ile. Pale ambapo mimi nilikuwa mng’avu yeye alikuwa mweusi tii, pale nilipokuwa mrefu yeye alikuwa mfupi na mwenye kiribatumbo.
 
KWA ANAYEKIHITAJI KITABU HIKI CHA KIGUU NA NJIA NA VINGINE VYA BEN MTOBWA KAMA DAR ES SALAAM USIKU, SALAMU TOKA KUZIMU, TUTARUDI NA ROHO ZETU NA VINGINE VINGI, NITAFUTE KWA KUPITIA 0712504985 AU 0763044459. KARIBUNI.
SURA YA SABA
Lyampa Iya Mfipa
a kupotea kwa hirizi ile? Mara kwa mara niliwaza.
 
Haaahhaa nimeipenda hii :
Mwanamume akitoka ametoka. Akirudi ana kitu cha kuonyesha kijijini. Ama vyeti vya kuhitimu masomo yake ama fedha au mtaji au kujenga nyumba bora zaidi. Mimi ningerudi na aibu tupu.
 
Gari moshi liendalo Mpanda hulazimika kueleka magharibi kwa kilometa kadhaa kabla ya kuchepuka kuelekea kusini. Kwangu mimi ilikuwa sawa na kuelekea nyumbani, Kigoma. Tuliiacha stesheni ya Tabora, tukatafuna reli hadi Usoke. Toka hapo tuliingia Urambo. Tuliacha Urambo na kufika Kaliua ambako tulianza safari ya kusini.
Kama ilivyokuwa safari ya kutoka Mwanza safari hii pia ilikuwa sawa na kusafiri katikati ya bustani ya Eden. Kila upande tulizungukwa na ama misitu minene iliyoashiria kila aina ya hazina, ama mapori ya kutisha yaliyonona juu ya wingi wa mbolea katika ardhi yake.
Mara kwa mara tulipishana na wanyama ainaaina waliokuwa kando wakitushangaa, pamoja na ndege ainaaina walioruka hapa na pale juu ya miti, wakifaidi asali ya maua na wadudu wadogowadogo. Baadhi ya maeneo kulikuwa na mabwawa makubwa yaliyoshawishi kilimo cha mpunga au mito ambayo ilinikumbusha samaki wa ziwa Nyanza.
Toka Kaliua tuliingia Mfulu, baadaye Ugalla na hatimaye tukawasili Mpanda. Huo ulikuwa mwisho wa reli hii, lakini haikuwa mwisho wa safari yangu.
Pamoja na shahuku yangu kubwa ya kuondoka Tabora, ndoto yangu ya kuja Mpanda ilikuwa na malengo yake. Zilikuwepo fununu za hapa na pale kuwa maeneo mbalimbali ya huku yalikuwa dhahabu. Uchimbaji wa dhahabu hiyo sikuona kama kwa namna yoyote ile ungenishinda. Kuchimba udongo hadi ufikie mchanga maalumu kuchekecha mchanga huo hadi uone chembechembe za dhabahu na kuiokoteza, vipi kungenishinda?
Hilo lilikuwa wazo la kwanza. Wazo la pili, ambalo nilikuwa na hakika nalo zaidi ni uvuvi. Toka Mpanda hadi Ikola au Kerema ambayo ni miji ya kandokando mwa ziwa Tanganyika haikuwa safari ndefu. Ningeweza kufika huko hata kwa miguu. Nilipanga, kama kazi ya kuchimba dhahabu ingeshindikana ningeelekea huko na kujiunga na uvuvi. Ndiyo, nasikia ziwa Tanganyika lina kina kirefu kuliko maziwa yote duniani. Kama kuna ukweli kwa hilo bila shaka samaki wake pia ni wengi zaidi na watamu zaidi. Ningekuwa mmoja kati ya walaji wake. Wala nisingeishia kula tu; samaki hao wangenipatia fedha za mtaji ili nirudipo kwetu nirudi kishujaa.
Hiyo ndiyo ilikuwa ndoto yangu. Kwa bahati, nzuri au mbaya, haikwenda kama nilivyotarajia. Hali hiyo ilitokana na kukutana kwangu ana kwa ana na mtu ambaye sikutarajia kamwe kumwona tena katika maisha yangu, mtu ambaye sikupata hata kulifahamu jina lake. Alikuwa mmoja kati ya wale Wamanyema wawili waliofuatana na Mwarabu katika safari yetu ya miguu toka Buha hadi kwa Wahaya, miaka zaidi ya mitano iliyopita.
Ni yeye aliyeniona kwanza, “We mtoto wewe! Kama nakufahamu vile?”
Nikageuka kumtazama. Mara moja nilimkumbuka, “Mmanyema! Unafanya nini huku?” niliuliza kwa mshangao.
“Wewe je? Umefikaje huku?”
Sikujua nimweleze nini.
“Babu yako hajambo?”
Sikuwa na jibu. Nikainamisha uso kwa aibu.
Nadhani Mmanyema alisoma kitu fulani katika uso wangu, kwani alinitazama kwa muda kabla hajanikaribisha chai kwa mihogo ambayo alikuwa akiila. Nikapokea kikombe cha chai ya maziwa na kipande cha muhogo. Njaa iliyoanza kuninyemelea ikakimbia mara moja.
Wakati tukinywa chai hiyo yapata saa kumi na moja za alfajiri. Gari moshi lilikuwa limechelewa sana njiani kutokana na mafuriko katika maeneo mbalimbali. Ilibidi gari hilo liendeshwe taratibu sana. Tulikuwa tumeketi nje ya stesheni, kwenye benchi la chuma ambalo bila shaka lilijengwa kwa ajili ya wasafiri.
Nilishangaa pale Mmanyema aliponiambia kuwa tulisafiri katika behewa moja toka Tabora hadi hapo. Kuwa aliniona lakini hakuwa na hakika na macho yake hadi aliposikia sauti yangu na kuniona nikimkumbuka.
Alikuwa mzungumzaji sana mzee huyu. Alinieleza jinsi alivyoacha kazi ya kumtumikia yule Mwarabu baada ya kufilisika. “Yaelekea Mwarabu yule hakuwa na ujuzi wowote zaidi ya biashara ya watumwa. Kila alichojaribu kushika kiliteleza. Hata mishahara yetu alishindwa kulipa. Tukaachana naye na kuanza shughuli zetu binafsi,” Alinieleza kwamba yeye sasa alikuwa akifanya biashara ya kununua dagaa toka kwa wavuvi wadogowadogo wa kandokando ya ziwa Tanganyika na kuwauza kwa walanguzi wakubwa ambao waliwapeleka Tabora, Dodoma na Dar es Salaam kwa matumizi ya binadamu na mifugo. Kwamba sasa hivi alikuwa na mtaji wa kutosha ambao utamwezesha kupeleka mwenyewe dagaa hao hadi Dar es Salaam ili apate faida kubwa zaidi. “Toka huku nitanunua nyavu na vifaa vingine vya uvuvi na kuwauzia watu Kigoma na Kongo. Nikijaliwa miaka miwili baadaye nitakuwa mmoja wa matajiri wakubwa wa nchi hii,” alisema kwa kujipamba.
“Sasa unakwenda wapi? Mbona huku hakuna dagaa?” nilimuuliza.
“Nakwenda Sumbawanga.”
“Kufanya nini?”
Alinitazama na kucheka kidogo kabla hajasema, “Unaonekana wewe ni mtoto mdogo sana kuliko umbile lako. Hujui watu huenda Sumbawanga kufanya nini?”
Mie: Sijui
Yeye: Pole sana. Kwa hiyo, hata maana ya jina Sumba - Wanga hujui?
Mie : Sijui
Alitikisa kichwa kwa namna ya kunisikitikia. Kisha alisema, “Sumba-Wanga maana yake ‘Tupa Uchawi.’ Kwa maana ya kuwa mji huo ni wa watu wazito, watu waliokomaa. Hivyo, ukiingia huko na vijiuchawiuchawi vyako utaumbuka. Ni huko ambako watu wazima huenda kugangwa, ili wasichezewechezewe ovyo kishirikina. Huwezi kufanya biashara kama hujafundwa ukafundika.”
Ilikuwa habari mpya kwangu. Niliipokea kwa mshangao na kutoamini. “Lakini Biblia inasema…” nilijaribu kumwambia.
“Achana na Biblia. Mimi ni Mwislam. Tunatumia Msahafu wa Mwenyzi Mungu. Ulioshushwa toka peponi kwa mkono wa mtume Mohamed S.A.W.”
“Lakini hata Uislam unakataza ushirikina.”
“Kujikinga sio ushirikina. Hayo ni mambo ya wakoloni tu, walipoamua kututawala miili na mioyo yetu. Walitarajia kuwa mila na tamaduni zetu kupotea huku wao wakihifadhi za kwao. Kila binadamu ana nyota na anahitaji kuisafisha mara kwa mara. Kila binadamu ana wahenga ambao anahitaji kuwaenzi kwa sadaka na tambiko. Asiyefanya hivyo kamwe hawezi kufanikiwa.”
Lilikuwa somo jipya kwangu, somo ambalo sikuwa na ujuzi nalo. Nikaamua kunyamaza. Mmanyema alichukulia ukimya wangu kama dalili ya kumwelewa.
“Haya na wewe nieleze ukweli wa kile kilichokufanya ufike huku. Kama nakumbuka vizuri babu yako alikupeleka Uhayani ukasome. Nadhani ulipata shule kwani nilipoonana naye mwaka mmoja baadaye alinidokeza kuwa ulishaingia shuleni,” alisema.
Nusura niruke kwa shauku, “Ulionana na babu?”
“Ndiyo!”
“Wapi?”
“Nyumbani kwenu. Kasulu. Tulilala pale siku mbili na alituchinjia beberu mkubwa sana. Babu yako ni mkarimu sana.”
Bila kutegemea nilijikuta nikitokwa na machozi. Babu yuko hai! Babu alirudi salama! Sikupata kupokea habari njema kama hiyo kwa miaka nenda rudi.
Sikuiona haja yoyote ya kumficha chochote Mmanyema huyu. Nilimwona kama baba yangu. Kama malaika, kwa kuweza kunipa walao fununu tu ya habari za nyumbani. Nikamweleza kila kilichonisibu, toka mwanzo wa mikasa yangu hadi nilipofikia.
Alinisikiliza kwa makini sana, mara kwa mara akitikisa kichwa kwa masikitiko. Mwisho wa maelezo yangu alinishika mkono na kuninong’oneza, “Pole sana mtani. Usijali. Hujafika mwisho wa safari yako kimaisha. Nitakusaidia.”
Nilimwamini. Sikujua kwa nini nilimwamini haraka kiasi hicho.
* * *​
Safari ya Ikola au Karema ilikufa. Ndoto ya kuchimba dhahabu nayo ilikufa. Safari ya Sumbawanga ikazaliwa.
Tulikaa kwa siku mbili kabla ya kupata gari lililotufikisha Sitalike. Hapo tulipumzika tena kwa siku tatu tukifaidi nyama pori ambazo zilikuwa tele toka katika mbuga za Katavi. Tukaondoka hadi Kisi, Chala, Nkundi na hatimaye Sumbawanga.
Wakati huo Sumbawanga kilikuwa kimji kidogo tu, chenye wakazi wachache lakini kikiwa na mambo makubwa. Mandhari ya mji, ambayo yalipambwa na mlima Malonje wenye urefu wa mita 2418 toka usawa wa bahari, mito na misitu tele yalifanya nitamani kuishi hapo kwa muda mrefu zaidi.
Lakini Mmanyema ambaye baadaye alinitajia jina lake kuwa ni Baraka Khalfan alikuwa na ratiba tofauti na yangu. Alikuwa na majina ya vijiji mbalimbali na waganga mbalimbali ambao alipanga kuwaona. “Huku ni Ufipa, mdogo wangu. Lyampa Iya Mfipa, umepata kulisikia?”
Sikupata.
“Lyampa Iya Mfipa kwa tafsiri ya kawaida ni mlima mdogo tu, ambao unatambaa hadi kando ya ziwa Tanganyika na kupita chini hadi Kongo, katika eneo la Moba, nchi ya Watabwa. Lakini kwa wajuzi wa mambo Lyampa Iya Mfipa linabeba uzito wa pekee. Ni jiwe la tambiko ambalo ukikaangwa juu yake hakuna mtu yeyote atakayekuchoma. Na hayo hafanyiki mjini, isipokuwa vijijini kwa wazee, waliofundwa na babu zao,” alinieleza.
“Watu wengi wenye nafasi zao wamepitia huku. Watu toka sehemu mbalimbali za dunia huja huku kufanyiwa mambo. Watabwa wa Kongo nao huja huku, ingawa ni kweli pia kuwa wazee wa huku katika kuimarisha uwezo wao huvuka ziwa kwenda Kongo,” aliongeza.
Hivyo, zilianza safari za hapa na pale. Mara Chapota, mara Kasanga, mara Wampembe na kwingineko. Safari hizo zilitufikisha Pwani ya ziwa Tanganyika na kuniwezesha kuona milima ya Kongo mbele yetu na ile ya Zambia kushoto kwetu. Ziwa hilo lilinikumbusha hamu ya kurudi nyumbani, kwani kwa kuambaa nalo tu, nikielekea kulia ningeweza kufika Kigoma. Kwa bahati mbaya, sikuwa tayari kwa safari hiyo.
Mmanyema alikuwa na pilikapilika nyingi. Mara kwa mara aliniacha peke yangu na kwenda hapa na pale na aliporudi alikuwa kachanjwa chale ama za kwenye paji la uso ama katika viwiko vya mikono na miguu. Wakati mwingine alinituma kumtafutia vifaa mbalimbali kama mayai viza, mizoga ya paka au njiwa weusi.
Siku moja aliondoka alfajiri na hakurudi. Nililala peke yangu katika chumba tulichofikia cha mwenyeji wetu mmoja. Kwa kuwa nilikuwa peke yangu nililala mapema sana, mara baada ya chakula cha usiku. Nilipofumbua macho tena ilikuwa alfajiri. Baridi kali iliyotokana na upepo ziwani nadhani ndiyo iliyoniamsha. Nilipotazama huko na huko sikuweza kuyaamini macho yangu. Nililala ndani, juu ya kitanda, lakini niliamka nikiwa nje, tena juu ya mbuyu mkubwa ulikuwa mbele ya nyumba hiyo. Isitoshe nilikuwa mtupu, bila nguo yoyote mwilini!
Nilishuka harakaharaka na kuingia ndani. Nguzo zangu zilikuwa zimetupwa ovyoovyo chumbani humo. Nikaziokota na kuvaa harakaharaka. Ni wakati nikivaa nilipobaini kuwa nilikuwa nimechanjwa chale mbili katika paji langu la uso na kupakwa vitu vyeusi kama masizi ya mkaa.
Nilikosa raha. Niliduwaa katikati ya chumba hicho huku nikitetemeka kwa hasira.
Mara mlango uligongwa na kufunguka kabla sijaitikia. Mwenyeji wetu, mzee Imilio Kahigi aliingia ndani. Alikuwa akicheka huku anatikisa kichwa. “Mtoto, mbona unasafiri ukiwa mwepesi hivyo?” aliniuliza.
Sikumwelewa, hivyo sikumjibu.
“Uko mtupu mno. Mwepesi kupita kiasi. Kwani hukuaga kwenu?” aliuliza tena.
“Niliaga!” nilimjibu.
Alicheka kabla ya kusema, “Hukuaga. Na kama uliaga wazazi wako ni watoto vilevile. Jana watoto wenzako wameamua kukupima baada ya kuona huelewekiheleweki. Wakakuta ni mwepesi mno. Ndiyo maana wakakuacha pale juu ya mti baada ya kukuchezea usiku kucha.”
Sikujua mzee huyo alitarajia jibu gani kwangu. Hivyo, niliendelea kukaa kimya wima, nikiwa nimemkodolea macho.
“Utafanyaje?” aliniuliza ghafla.
Nilijua nitakachofanya. “Nitaondoka, leo hii hii,” nilimjibu.
Alicheka tena kabla hajasema, “Unadhani utafika unakokwenda?”
“Nitafika. Kwa nini?”
“Wenzako wamekutia alama. Popote utakapokwenda wajuzi wa mambo watakubaini mara moja na kukugombea kama mpira wa kona, maana una alama, alama ya shari.”
Nilizidi kuduwaa. Nadhani hata mdomo wangu niliusahau ukiwa wazi wakati nikiwa nimemtumbulia macho.
“Huyu Mmanyema unamfahamu kwa kiwango gani?” Aliniuliza ghafla.
“Simfahamu vizuri. Tulikutana naye safarini miaka mingi iliyopita. Tumekutana naye tena majuzi na kufuatana naye. Basi.”
Mzee Kahigi alitikisa kichwa kwa namna ya kunihurumia sana. Kisha aliongeza swali jingine, “Alikuambia anatafuta nini huku?”
“Waganga.”
“Wa?”
“Kujiganga. Anataka kinga.”
Mzee akacheka tena. “Humjui vizuri,” alisema. “Humjui hata kidogo. Huyu bwana anatafuta kizimba, dawa ya mali. Ametakiwa kutoa kichwa cha mtu. Alitakiwa atoe mtoto wake wa kwanza, ageuzwe ndondocha, awekwe chini ya maji kumswagia dagaa. Hana mtoto wake wa kuzaa. Anachofanya sasa ni kukutoa wewe. Utageuzwa akili, utawekwa chini ya maji maisha yako yote, hadi kifo cha kweli kitakapokutokea.”
Sikuyaamini masikio yangu.
“Mmanyema!”
“Naam!”
“Mimi!”
“Naam… tena mipango yake inakwenda vizuri sana. Kesho au keshokutwa utakufa, tutakuzika. Lakini wajuzi wa mambo tutaona tunavyozika mgomba huku wewe ukiongozwa kikondoo kupelekwa ziwani.”
Baada ya taarifa yake hiyo ‘njema’ alinikazia macho kabla hajaniuliza tena, “Utafanya nini?”
Bado sikujua alitaka nimjibu nini, “Nitaondoka,” nilimjibu.
“Nimekwishakwambia umetiwa alama. Hutafika mbali.”
“Nitaondoka nikafie mbali. Siyo hapa.”
Baada ya kuwaza sana alisema, “Nitakusadia. Utaondoka hapa salama ufike salama kokote uendako. Siwezi kukubali mtu wa kuja afanye ushenzi katika milki yangu. Kaa kama kawaida, kula kama kawaida, usiku ufunge vitu vyako vyote tayari kwa safari.”
Sikujua ilinipasa kumshukuru au la. Kwa ujumla, sikujua kama nilipaswa kumwamini au kutomwamini. Nilichojua ni kwamba maisha yangu yalikuwa katika mashaka makubwa. Unapopigania roho yako, bila kumjua nani adui nani rafiki, sio suala la mzaha.
Nilifanya kama nilivyoelekezwa. Sikumwambia mtu yeyote juu ya masaibu yaliyonipata usiku huo. Nilioga, nilikula na baadaye kutembeatembea kijijni hapo kana kwamba hakuna lolote la ajabu lililonipata.
Mmanyema alirudi mida ya saa nne hivi. Alionekana mtu mwenye furaha na matumaini makubwa. Huku akitabasamu alinivuta chemba na kuninong’oneza, “Mdogo wangu mambo yamekwisha. Kama nilivyokuambia baada ya miaka miwili tutakuwa watu katika watu. Pesa halitakuwa tatizo tena. Wewe, kwa kuwa umesoma kuliko mimi utakuwa mhasibu. Utatunza hesabu ya fedha na mali zetu zote.” Aliongeza kwa kunidokeza kuwa jioni hiyo angesafiri tena. Atakaporudi tutakuwa tayari kurudi Kigoma.
“Unakwenda wapi safari hii?” Nilimuuliza.
“Nakwenda Kipili hadi Mtakuja. Nitajitahidi kurudi keshokutwa. Nikirudi tu yamekwisha,” alinijibu. Kisha alinitazama usoni na kuniuliza “Hapo umefanya nini?”
“Nilijikuna,” nikamjibu.
Nilihisi hakuniamini. Alizikagua chale zile kwa muda mrefu kidogo.
“Sidhani,” alisema. “Nikirudi tutaangalia suala lako vilevile. Isije kuwa washenzi wanakuchezea, maana umekaa mweupemweupe kama kinda la ndege.”
Nilitamani sana kumwamini. Sikubahatika kuipata fursa hiyo.
Mara tu alipoondoka nilifunga vifaa vyangu katika begi langu. Baada ya mlo wa usiku nilijilaza mapema nikisubiri usingizi unichukue ili kesho ifike nione mzee Kahigi atanisaidia vipi ili niweze kuondoka nchi hiyo ya Wafipa salama.
Sikujua usingizi ulitokea wapi. Nilihisi ghafla kama naota, mlango ukifunguka na mzee Imilio Kahigi akiingia chumbani humo. Alikuwa mtupu, isipokuwa kwa kipande kidogo cha kaniki alichofunga mbele ya kiuno chake. “Inuka,” aliniamuru. Niliinuka. “Chukua begi lako unifuate,” nilifanya kila alichoniamuru na kumfuata hadi nje ya nyumba.
Hapo kulikuwa na ungo mkubwa wenye vikorokoro mbalimbali ambavyo sikuweza kuvifahamu. “Ingia ukae hapo,” aliniamuru tena. Nikamtii.
Mara alianza kuimba kwa lugha ya Kifipa, maneno ambayo sikuweza kuyaelewa. Akaninyunyizia kitu fulani chenye harufu mbaya kwa usinga wake huku akiendelea kuimba. Ghafla nikaona ungo ukianza kupaa. Ulipaa, ukapaa, ukapaa hadi mawinguni. Naota? Nilijiuliza. Kama ilikuwa ndoto, basi ilikuwa ndoto ya aina yake ambayo ningependa nirudie kuiota mara kwa mara.
 

Similar Discussions

14 Reactions
Reply
Back
Top Bottom