Dam55
JF-Expert Member
- Oct 8, 2015
- 5,592
- 11,831
- Thread starter
- #41
RIWAYA: JANGA
MTUNZI: richard MWAMBE
“Samahani sana, sikujua kama moshi unakudhuru,” akamwambia na kumpulizia tena, Majoti akahisi kama anakabwa, akakosa pumzi, macho yakawa mazito, akazidiwa na kuchukuliwa na usingizi mzito. Gina akavaa fulana yake, akainua mkoba wake na kupotelea nje. Tayari ilikuwa saa tano usiku alipokuwa nje ya hoteli hiyo.
SEHEMU YA 17
AFISI NDOGO
“Vipi, yuko wapi?” Madam S akamwuliza Amata.
“Yupo kwenye usaili, tumsubiri kidogo atachelewa,” Kamanda akamjibu Mada S.
Dkt. Jasmine akatua lile faili mezani na kulisukuma kwa Madam S huku akitikisa kichwa chake.
“Vipi?”
“Nimeelewa, lakini ili nijue kila kitu kilivyo sina budi kuchukua sampuli ya ngozi ili kujua kiuhalisia nini sababu. Lakini Madam, ina maana Mkemia Mkuu hajapata hili swala? Maana kama liko mahakamani basi ilipaswa ahusishwe upande wa serikali,” Jasmine akauliza.
“Kesi ya ngedele hiyo,” Madam akajibu kwa kifupi.
“Sawa, sasa inabidi tufanye hivyo, naomba niifanye kazi hii kesho asubuhi,” akaomba.
“Bila shaka! Sasa waweza kwenda kupumzika, na kazi yetu kesho itaanzia hapa,” Madam akasema na Jasmine akainuka kitini.
Jasmine akawaacha wawili hao nay eye akaondoka zake kwa maana ni siku hiyohiyo alikuwa amefika kutoka Marekani. Kamanda Amata na Madam S wakaendelea na mazungumzo yao juu ya mikakati hasa ya kutatua kadhia hiyo.
Gina alwasili ofisini saa sita usiku na kumkuta Madam S na Amata wakimsubiri, akaketi na kuwatazama watu hao.
“Umepata kazi?” Kamanda akamuuliza.
“Nimeambiwa kesho nipeleke CV zangu kwa Bwana Momba kule Utumishi,” akajibu. Akafungua mkoba wake na kumkabidhi Madam S ile mashine ya kurekodi sauti. Mwanamama huyo akaichukua na kuipachika kadi yake kwenye kompyuta ya mezani, akaiwasha na wote wakaanza kusikiliza mazungumzo ya Gina na Majoti. Mazungumzo hayo yalionekana wazi kuwafumbua macho, Madam S akawa akiandika vitu kadhaa kwenye kidaftari chake kidogo.
Iliwachukua saa kama tatu hivi kusikiliza mazungumzo hayo mpaka mwisho.
“Mh! Sasa naweza kuunganisha picha, Shekibindu kauawa, nataka kujua nani kapanga mpango, naomba tuonane asubuhi saa tatu hapa,” akawaambia.
11
Siku iliyofuata…
JAJI SHEKIBINDU AHUJUMIWA, gazeti la Mbalamwezi liliandika namna hiyo kwenye kurasa yake ya juu kabisa, kila aliyesoma habari hiyo alivutiwa na kuangalia nani mwandishi, na hakuna aliyeamini kwa kuona kuwa aliyandika habari hiyo ni Mustafa Bashiru. Kusfikia saa tano asubuhi nakala zilikuwa zimeisha na bado kila mmoja alikuwa ana hamu nalo.
Ngishu alilikunja gazeti lile na kulitupia mezani, akawatazama vijana wake, akashusha pumzi ndefu na kuwasha sigara hata kama hakuwa mvutaji.
“Huyu mtu yupo, ina maana hata jana alikuwapo mahakamani? Kwa maana jinsi habari hii ilivyoandikwa inaonesha wazi kuwa alikuwepo,” akawaambia wengine.
“Mbona hatukumwona?” Kebby akauliza.
“Kichwa kinaniuma sana, naona kama mzigo huu unatuelemea, naomba mwanze tena kumtafuta na apatikane,” Ngishu akawaambia.
“Sawa!” wakajibu kwa pamoja na kuondoka katika kijisebule hicho. Kama kuna siku ambayo Ngishu alihisi akili yake imechanganyika na damu ilikuwa hii. Alijitupan kitini, akainamisha kichwa chake na kutulia kimya kabisa akijaribu kuyapishanisha mawazo yake, la huku kupeleka kule na la kule vivyo hivyo.
HOSPITALI YA MUHIMBILI
Daktari Jasmine aliingia kwa mganga mfawidhi wa hospitali hiyo kubwa nchini, pamoja naye alifuatana na Kamanda Amata. Baada ya kuonana na mganga huyo alipewa kibali cha kuikagua miili ile kwa ajili ya vipimo zaidi. Walivuta hatua na kupita katika vijia vya kupitia watu kuelekea kwenye mawodi lakini wao hawakuelekea huko.
Kwenye mlango mkubwa wa kuingia katia chumba cha kuhifadhi maiti walikutana na mabishano ya watu kadhaa. Kulikuwa na akina mama wawili na akina baba watatu wakibishana na mhudumu wa chumba hicho kuhusu kuchukua mwili wa ndugu yao kwenda kuuzika.
“Hivi mnanielewa, hili hapa ni andiko la zuio, miili isichukuliwe mpaka amri ya serikali, kuna uchunguzi unafanyika…”
“Uchunguzi gani bwana we!” mama mmoja akang’aka na wakati huo Jasmine na Amata walikwishafika mlangoni pale.
“Jamani hili siyo eneo la mabishano,” Jasmine aliingilia kati.
“Tena we daktari ndiyo unyamaze kabisa, mgonjwa wangu hata diripu hamjamwekea mpaka kapoteza uhai, mmekalia rushwa tu, yaani nchi hii, kama huna pesa unakufa unajiona,” yule mama aliongea mpaka akaanza kulia. Wenzake wakamtuliza na kumsogeza pembeni.
“Wewe ndiye Shabani Mtemanyongo?” Amata akauliza.
“Ndiyo mimi,” akajibu. Jasmine na Amata wakajitambulisha kwake na kumwonesha kibali cha kufanya kazi hiyo kilichosainiwa na Mganga Mkuu na kutoka jeshi la polisi. Kijana yule mwenye macho mekundu, aliyekuwa ndani ya suti safi na chupa la pombe mkononi mwake akawakaribisha katika ofisi yake kwanza. Amata akaitazama ofisi hiyo kwa mapana na marefu wakati Shabani akiongea na Jasmine lugha zao za kitaalamu. Ukutani mwa ofisi ile kulikuwa na picha nyingi sana, tofauti na ofisi za kawaida ungeweza kuona picha za viongozi au watu mashuhuri na kalenda zikiwa zinaning’inia, hapa ilikuwa ni tofauti kabisa. Ukutani kulikuwa na mapicha ya maiti za kila aina, kulikuwa na kalenda ya zamani lakini kwenye eneo la tarehe kulikuwa na karatasi nyeupe iliyoandikwa ‘unaijua siku ya kufa kwako?’.
“Afande usishangae kaka, hata wewe siku moja utakuja hapa, utalala raha mustarehe,” akamtania Amata.
“Unawezaje kuishi humu?” Amata akamuuliza.
“Kama wewe unavyoishi duniani,” Shabani akajibu huku akinyanyuka, “Dokta njoo huku mama!” akaita. Jasmine akainuka na kumfuata akiwa na mkoba wake wa kazi ulioshehni zana zinazotakiwa. Amata naye akainuka kuwafuata.
“We bwana mdogo huku hakukufai, tuache sisi tunaojua kifo ni nini,” Shabani alimwambia Amata kisha akaendelea na safari yake huku chupa ya pombe ikiwa mkononi. Wakati wao wapo huko ndani Kamanda Amata akawa anapekua ile ofisi kiutaalamu sana ili kuona nini na nini vipo. Hakukuwa na la maana zaidi ya magazeti mengi sana ya Mbalamwezi, akayapekua harakaharaka na kugundua kuwa magazeti hayo yote yalikuwa na habari za kadhia ile mpaka la siku hiyo nalo alikuwa nalo.
Ana uhusiano gani na hili swala? Akajiuliza na kujikuta akizidi kupekuwa haraka haraka, katika moja ya droo akakuta picha kama tisa hivi za watu tofauti, lakini kilichomshtua na kumshangaza ni picha ya chini kabisa, ilikuwa ya Jaji Shekibindu, marehemu. Amata akahisi baridi mwili mzima, nyele zikamsimama akashindwa kuelewa. Akachomoa simu yake na kuzipiga picha moja baada ya nyingine, alipohakikisha kamaliza, akazirudisha haraka na wakati huohuo akasikia sauti za watu wakija katika chumba hicho.
“Pole, tulikuacha peke yako,” Jasmine alikuwa wa kwanza kumwambia Amata.
“Haina tabu mi nilikuwa nainjoi tu hapa,” akajibu. Punde kidogo Shabani naye akaingia na kuketi upande ule wa pili, mazungumzo machache yakatawala kisha wakaagana na kuondoka zao.
Wakiwa ndani ya gari, Amata alimuuliza Jasmine kama amefanikiwa, akahakikishiwa kuwa kila kitu kipo sawa na safaroi ilikuwa ni kuelekea Shamba ambapo kuna chumba kidogo cha uchunguzi anachokitumia daima daktari huyu.
“Una uhakika na unachokisema? Au unachokifikiri?” Mheshimiwa Kalembo alimuuliza Ngishu.
“Ndiyo, hakuna mtu mwingine wa karibu anayeweza kusikia mazungumzo yetu kama siyo Alinda,” Ngishu akajibu. Maneno haya yakamwingia Kalembo, akatulia kimya na kufikiri jambo.
“Nakubaliana nawe kwa asilimia za kutosha kwa sababu ni siku ileile ambayo Mustafa alipotea si ndiyo?”
“Ndiyo!”
“Basi litafanyiwa kazi haraka sana, nitakupa taarifa,” Kalembo akamwambia Ngishu, “Enhe haya na huyo Kebby aliuawa?” akaongeza swali.
“Ah kama ni kweli alipewa kitisho, basi muuaji ni mwoga, lakini katumia namba ya marehemu,” Ngishu akaeleza.
“Sikiliza Ngishu, kila kukicha mambo yanakuwa mengi, sasa nini mwisho wa sakata hili?” akauliza kwa wasiwasi.
“Mambo yetu ni machache tu, kumsaka Mustafa na kumuua pia huyo aliyemuua Boban lazima tumlipizie kisasi.
Mara simu ya Ngishu ikaita, akaitoa mfukoni na kuiweka sikioni.
“Kebby!” akaita.
“Asee Ngsihu, ile gari ya majuzi, Ford Ranger tumeioana hapa mitaa ya Azania Front,” Kebby alitoa taarifa.
“Na aliyemo ndani mmemwona?”
“Yeah! Na picha tumempiga,”
“Mmefanya vyema, nitumie kwenye simu mara moja labda nitamtambua,” Ngishu akamwambia Kebby na kukata simu.
“Mheshimiwa nikuache,” akamwambia Kalembo.
“Na huyu inakuwaje, mi naona mumbane tu,” Kalembo akauliza.
“Usaijali hilo tutalifanya jioni,” Ngishu akajibu huku akitoka katika ofisi ile.
Ngishu akatoka afisini na kumwacha Kalembo bado akiwa anamalizia kazi zake mbalimbali, nje ya afisi hiyo, kabla hata hajaingia katika gari yake akamwona Alinda akiwa kasimama na kijana mmoja aliyevalia sweta lenye kofia kubwa, usoni mwake alikuwa na miwani ya jua. Akawatupia macho na taratiu akaingia katika gari yake na kuufunga mlango huku kioo kikiwa chini kiasi Fulani na kumruhusu kuendelea kuwaona watu hao.
Alinda mara baada ya kutoka ofisini alasiri ile, alijikuta akisimamishwa na mtu asiyemjua, mweusi wa wastani, mrefu mwenye nywele nyingi, miwani nyeusi na mustache uliostawi vyema chini ya pua yake. Alipogeuka nyuma kumtazama na kugundua kuwa hamjua, na kumwona jinsi alivyo, aliongeza mwendo kwa maana alimwogopa. Na yule mtu naye akaongeza mwendo kumfikia, kutokana na urefu wake haikumchukua muda akamkata mkono, akihakikisha watu hawagundua tukio hilo. Akamvuta kando na kumtazama usoni.
“Usiogope, mimi ni rafiki yako, nimejibadili tu,” yule mtu akamwambia.
Alinda akamtazama asimjue, “We n’nani?” akamtupia swali.
“Mustafa!” yule mtu akajibu.
Mwanadada huyo akamtazama tena bila kummaliza.
“Usinitafute, utaniletea matatizo,” Alinda akamwambia.
“Usiwe na wasiwasi, kwanza hakuna atayejua kuwa mimi ni yule, unajua kwa nini nimekutafuta?” Mustafa akamwuliza.
“Sijui, kwanini,”
“Nataka unioneshe wale ulionambia kuwa wanataka kuniua, siwezi kujificha siku zote kwani sina pesa za kuniweka huko,” Mustafa akamwambia Alinda.
“Mh! Wewe, we elewa hivyo nilivyokwambia, kama unataka kuwafikisha kwenye vyombo vya dola … mh, sijui maana kwa kazi yako adui wengine ni wakubwa,” akaeleza.
“Sikuelewi!”
“Mustafa…”
“Niite Jack,” Mustafa akasema.
“Ok, Jack, ni hivi, mimi nilikupa taarifa tu kwa kuwa nilipita sehemu nikasikia wanazungumza habari hiyo,” Alinda akamwambia.
“Unaniweka katika mazingira magumu,”
“Najua lakini nitafanyeje, na wakijua tu kuwa nimekupa hiyo taarifa watanidhuru,”
“Ina maana unawajua?”
“Niliwaona siku moja,” Alinda akamwambia huyo kijana na mara hiyo macho yake yakagongana na Ngishu upande wa pili wa barabara. Akahisi moyo wake ukimlipuka, almanusura aanguke, akajikaza kikike na kushusha pumzi ndefu. Mustafa akakiona kitendo hicho, akamkazia macho huyo binti na kisha kugeuza uso wake kuangalia upande wa pili, yaani nyuma yake na ndipo alipomwona Ngishu, hakumtilia maanani, akarudisha macho kwa Alinda, hayupo. Alipmtzama tena Ngishu, tayari keshaingia kwenye gari. Moyo wa Mustafa ukaanza kupiga kwa fujo akajikuta katikati ya dimbwi la sintofahamu. Akaamua kujiondo taratibu labda angeweza kumwona yule mwanamke wapi kaenda au kaingia ili amwulize ni kwa nini kashtuka na kuondoka baada ya kumwona huyo mtu.
Ngishu mara tu baada ya kuketi ndani ya gari akayarudisha macho kwa wale watu na kumwona yule kijana peke yake, binti hayupo, na yeye machale yakamcheza. Mara akamwona mtu yule akitoka taratibu eneo lile na kuingia upande wa pili nyuma ya supamaketi ya Imalaseko. Akawasha gari na kueleke upande ule ule, alipoipita ile supamaketi, akakunja kulia na kumwona yule kijana akiingia katika gari moja ndogo nyeupe na kuondoka, akaamua kuifuata ajue ni wapi itaishia.
Ndani ya gari …
Alinda alipomaliza tu kufunga mkanda, mlango wa nyuma yake ukafunguliwa na Mustafa akaingia.
“Jack utaniletea matatizo Jack!” akalalama.
“Ondoa gari anakuja!” Mustafa akamwambia Alinda. Yule msichana akaondoa gari na kuingia barabarani bila kutazama, kelele za misuguano ya matairi na barabara zilisikika huku matusi yakiporomoshwa na madereva wengine walsimamisha gari zao ghafla.
“Tunaenda wapi?” akamuuliza.
“We nuache hapo mbele mi najua pa kwenda!” Mustafa akamwambia Alinda. Mita kama mia saba hivi kwenye msongamano wa magari, Mustafa akafungua mlango na kutoka nje, akajipekua mfukoni na kumtupia kadi ya kibiashara kupitia dirishani.
“Hili likiisha unitafute, kuna zawadi yako,” akamwambia kisha akapotelea kwenye msongamano wa magari. Alinda akashusha pumzi ndefu na kuisoma ile kadi, haikuficha jina la mmiliki. Akaichukua na kutia mkobani kisha akaondoa gari maana ziliruhusiwa.
Ngishu alikutana na pingamizi barabarani, akashindwa kuingia kwa wakati, akaipoteza gari ya Alinda.
“Shiiit!” akapiga ukulele na kupiga ngumi kwenye usukani wa gari hiyo, nukta hiyo hiyo simu yake ikaita, alipoinyakua akagundua kuwa ni ujumbe mfupi wa picha ‘MMS’, akaifungua na kukutana na picha kijana shababi aliyevalia kitanashati akiwa kama anatoka kwenye gari ambayo hakuiona jina lake lakini aliweza kuitambua rangi yake, akaondoa ile meseji na kupiga namba hiyo ya Kebby.
“Hello, nimeiona picha, tutamfanyia kazi huyo mtu, sasa kuna jipya huku, naomba juu chini tumtie mkononi Alinda, niwakute hapo hapo,” akamwambia kisha akageuza gari na kurudi kwa barabara aliyokuja nayo. Haikumchukua muda alikutana na vijana wake, wakaingia kwenye gari na kuondoka, moja kwa moja mpaka mwananyamala.
“Mnaona nyumba ileeeee!” Ngishu akawaonesha.
Wote wakaitikia kwa vichwa kuwa wameiona.
“Pale ndipo anapoishi Alinda, mumnase kabla hajaingia ndani,” akatoa maelekezo. Kisha wakasogeza gari yao mahali ambapo wangemwona mwanamke huyo akiingia nyumbani kwake. Hawakukosea, wakati wanafika tu eneo hilo, waliiona gari ya Alinda ikikunja kona na kuchukua barabara ambayo ingemfikisha nyumbani kwake.
Mara ghafla Subaru nyeupe ikasimama mbele yake, vijana wawili waliovalia sox usoni wakateremka na kumuwahi, wakavuta kitasa cha mlango, umefungwa, mmoja akapiga ngumi kwenye kioo, kikatawanyika. Alinda akarudiwa na akili, akaweka gia R na kukanyaga mafuta, ile gari ikarudi nyuma kwa nguvu, na mmoja wa vijana hao ambaye alikuwa akijaribu kufyatua loki ya mlango huo aiangushwa vibaya na ile gari ikarudi nyuma na kugonga nguzo ya umeme, hakujali, alikunja kona kali na kuingia barabarani mara upande wa pili gari ya mchanga ikatoke na kuigonga vibaya ile ya Alinda, ikaikanyaga boneti na kulifumua vibaya. Alinda alijibamiza kwa nguvu kwenye usukani, vipande vya kioo cha mbele vikaruka na kumuumiza vibaya. Akasikia kelele za watu na honi za magari, kishavyote vikaanza kufifia na kiza kinene kikambeba kikichanganyika na usingizi mzito.
SHAMBA
Jasmine akiwa na karatasi kama mbili hivi mkononi mwake, aliketi kitini huku mbele yake kukiwa na Madam S pamoja na Kamanda Amata. Wote wawili walikuwa wakimsubiri kwa hamu daktari huyo maana walijua wazi kuwa majibu ya vipimo vyake yangewapa mwanga wa kipi ni kipi.
“Yes Dokta!” Madam alianza. Jasmine akakohoa kidogo na kuzibwaga zile karatasi mezani.
“Nimechunguza sampuli ya ngozi ya mmoja wa marehemu na pia nimechunguza baadhi ya vipodozi tajwa ambavyo nimevinunua mwenyewe dukani. Bila shaka ndani ya jelli na losheni hizo nimekuta kuna viambato ambavyo serikali ilikwisha piga marufuku na viwanda vyake vilikwishasimamaishwa uzalishaji hapa Tanzania, sasa inaoneaka kwa sasa vipodozi hivi vinaingizwa kutoka nje, viambato nilivyovigundua ni Steroids ambayo hujulikana kama Clobetasol Proprionate, Hydrocrotis One na Triamcinolone. Sasa binadamu akitumia vipodzi vyenye kemikali hizi madhara anayoyapata ni pamoja na kuvimba mwili, muwasho, ngozi kuwaka moto, ngozi kukatikakatika, kubabuka, kuwa nyeupe isiyokuwa ya kawaida, zaidi ya hapo hupata madhara kwenye mifupa, kizunguzungu pamoja na madhara mengine mengi ikiwamo kichwa kuuma sana,” Jasmine akawaambia Amata na Madam S, akazifunga zile karatasi na kumpa bosi wake. Madam S akazipokea na kuziweka vizuri.
“Ina maana, idara ya upimaji wa viwango haijaona hili, maana haya makopo yote ukiyaangalia yana nembo ya viwango ina maana yamepitishwa kwa matumizi ya binadamu, kuna nini hapa?” Kamanda Amata akauliza kwa mashaka. Madam S akamtazama kijana huyo huku akitikisa kichwa kumaanisha amelielewa vyema swali hilo.
“Amata, Jasmine, hapa kuna kazi ngumu nimeelewa nini kinaendelea,” Madam akazungumza, “Sasa tunafanyaje?” akamtupia swali Jasmine.
“Nahitaji kuonana na madaktari wa hospitali hizi ili nipate majibu ya vipimo vya marehemu hawa na kisha nioanishe na kile nilichonacho,” Jasmine akaeleza.
“Zaidi ya hapo, inabidi tuimulike hii idara ya viwango, kuna kitu si kidogo ni kikubwa,” Amata akaongeza.
“Tunaanzia wapi?” Madam akauliza, “Maana hawa washenzi nataka kuwabana kabla kesi haijasomwa kwa mara nyingine.
“Jasmine aanzie hospitali kama alivyosema, na mimi nitaendelea nilipo,” Amata akatoa ushauri na wote wakakubaliana nao.
Kebby akakung’uta mkoba wa Alinda aliounyakua kwenye eneo la ajali, kulikuwa na simu kubwa ya kisasa, vipodzi kadhaa, pedi na vikolokolo vingine, akiwa katika kuweka kando begi hilo ndipo akaiona ile kadi ya kibiashara, akaichukua na kuisoma.
Mustafa Bashiru
Gazeti la Mbalamwezi.
Pamoja na maelezo hayo kulikuwa na namba za simu na mawasiliano mengine, akamkabishi Ngishu.
“Mzee kazi imeisha!” Kebby akamwambia Mhindi koko huyo huku akimkabidhi ile kadi.
“Aaaa ha ha ha ha basiiii, kazi imekwisha, huyu anakamatika le oleo na tunamchinjiliza mbali,” Ngishu akasema.
“Sasa tutafute mwanamke mzuri mwenye sauti tamu, ajisanye ni Alinda, kisha ampigie wakutane mahali atakuja tu,” Kebby akatoa ushauri na kila mmoja akaukubali, mkakati ukaandaliwa tayari kwa kumnasa mwanahabari huyo.
12
Pambazuko la aiku iliyofuata lilimkuta Kamanda Amata ndani ya ofisi ya gazeti la Mbalamwezi akiwa uso kwa uso na Mkurugenzi wa gazeti hilo.
“Kwa kweli, mi sijui hata huyu mtu yuko wapi,” yule mkurugenzi alimwambia Amata kutokana na swali aliloulizwa.
“Sikiliza, jana mmetoa habari ambayo imeandikwa na Mustafa ina maana mna mawasiliano naye,” Amata akamwambia Mkurugenzi yule, swali hilo lilimshtua kwa kuwa hakulitegemea na kweli gazeti lililopita alichapa habari ya mtu huyo. Hakuwa na ujanja.
“Nililetewa habari kwenye bahasha,”
“Na nani?”
“Mi simjui, lakini kwa namna fulani kashahabiana na Mustafa,” yule mkurugenzi akajibu.
“Sikiliza, mimi ni afisa wa polisi, na tunamtafuta mtu huyu kwa usalama wake, hivyo mara tu utakapomuona kaja tena hata kama si yeye, nipe taarifa haraka, maana maisha ya mwandishi huyu yapo hatarini, tunahitaji ushirikiano wako,” Amata akamwambia yule Mkurugenzi na kisha akasimama tayari kwa kuondoka.
Alipoagana na mwenyeji wake, mlangoni akakutana na mtu ambaye sifa zake ni zile alizoambiwa. Mrefu, mweusi, ana nywele ndefu na mustachi wenye afya. Kamanda Amata akamtazama haraka kwa jicho lake la tatu, akagundua kuwa mtu huyo kajivika mustachi wa bandia kwani uliinama kidogo upande mmoja. Akili yake ikamwambia kitu, hata hivyo hakusimama akaendele na safari yake mpaka kwenye maegesho akaingia garini na kusubiri. Dakika kama kumi na tano hivi alimwona yule mtu akitoka katika jingo lile la Mbalamwezi na kutaka kuingia kwenye gari moja ndogo iliyochoka kiasi.
Mustafa kwenye muonekano wa kibandia, hakupanda ile gari na moja kwa moja alikiendea kibanda cha magazeti na kukutana na habari iliyosisimua mwili wake.
MAJAMBAZI YAMVAMIA MTUMISHI WA WIZARA, habari hii ilimvuta akaisoma lakini almanusura aanguke baada ya kuona kuwa aliyevamiwa ni Alinda, mtu ambaye jana tu walikuwa pamoka kwa upande mwingine ni kama malaika wake. Akanunua lile gazeti na kulielekea gari alilkuja nalo. Ghafla akasimama na kuchukua simu yake, akaiangalia, ikampa mshangao. Namba iliyokuwa ikiita ni ya Alinda, na habari aliyoisoma ilimhusu mwanadada huyo. Haraka akaipokea na kupokelewa na sauti inayofanana na ile ya Alinda lakini ilikuwa chini kiasi. Mustafa akajua labda kwa kuwa ana maumivu hawezi kuongea vyema. Sauti ile ilimwelekeza Mustafa kuwa afike nyumbani kumwona kwani ameruhusiwa na pia ana habari nyeti ya kumpa.
Kamanda Amata akajua kwa vyovyote kuna jambo ambalo limemchanganya kijana huyo, akaifuata gari yake mara tu baada ya Mustafa kuingia barabarani.
Ngishu akamtazama Kebby, kisha akaitazama tena ile picha kwenye simu.
“Ushawahi kumwona?” Kebby akauliza.
“Hapana, sijawhi kumwona lakini nashindwa kujua kwa nini anataka kujiingiaza katika mzozo huu!” Ngishu akamwambia Kebby.
“Anaweza kuwa polisi,” Kebby akasema kwa mashaka.
“Ni kweli sasa huyu ni kuimfutilia mbali kwa risasi moja tu,” Ngishu akamwambia kijana huyo.
“Ngishu! Vijana wanasema wameshamtega Mustafa Mwananyamala…”
“Oh good! Twende zetu huko huko, kumbuka leo ni kumuua tu na si kumwachia aheme,” Ngishu akasisitiza, wakaingia garini na kuondoka kwa kasi kuelekea Mwananyamala.
“Mwanaharamu huyu, leo lazima iwe zamu yake,” Kebby naye akang’aka huku akibadili gia na kuiacha Barabara ya Gerezani na kuchukua ile ya Msimbazi kuelekea Fire. Akiwa kasi katika barabara ya Morogoro, Kebby akasikia simu yake ikiita, akainyakuwa kwa mkono wa kushoto huku ule wa kulia ukiendelea kukamata usukani. Alipoitazama akakutana na namba ya Boban marehemu, akahisi moyo wake ukiganda kwa ubaridi. Akafyatua kitufe cha kupokelea na kuiweka sikioni.
KITABU CHA ‘MPATANISHI’ KINAPATIKANA
DAR ES SALAAM, DUKA LA KONA YA RIWAYA, PIGA SIMU 0655428085
MBEYA , DUKA LA FANANI NA HADHIRA, PIGA SIMU 0754091481
“Aaaa ha ha ha ha! Jana nilikudanganya tu, lakini sasa tutakutana mchana huu,” sauti ya upande wa pili ikamwambia. Kebby akawasha indiketa na kutoa gari nje ya barabara.
“We mpumbavu vipi! Hujui tunapoteza muda?” Ngishu akang’aka.
“Ngishu, nimepokea hii simu namba ya Boban,”
“Unasema!” Ngishu akashangaa na kuichukua ile simu, alipotazama simu zilizoingia kweli akaikuta ya mwisho ni ya Boban. Hakusita, akaipiga, ikaita na kuita lakini haikupokelewa.
Kamanda Amata akatabasamu, akabadili gia na kuongeza mwendo. Watakoma, nitawafanyia mchezo huu mpaka wachanganyikiwe, Amata akawaza na kusonya. Akahakikisha haipotezi gari ya Mustafa. Walipofika Kinondoni kwenye taa za kuingia Barabara ya Kawawa, gari ya Mustafa ikapita, gari mbili za kati zikasimamishwa.
“Aaaaa come on!” akapiga ukulele na kujaribu kuitoa gari nje ili aingilie upande wa pili, a wapi! Tayari gari zilibana kila upande. Dakika tano baadae wakaruhusiwa kupita, Amata akakamata Barabara ya Mwinyijuma kwa kasi kubwa kuelekea Mwananyamala ilhali hajui wapi hasa mtu huyo aendako. Ford Ranger ilifanya ovateki za hatari barabarani na kila mtu akatahayari kwa mwendo huo. Alipofika Komakoma akapunguza mwendo na kutembea taratibu, mara ghafla kwenye kioo chake cha kulia akaiona ile Subaru nyeupe ikija kasi, akawasha indiketa na kuitoa gari yake nje ya barabara. Ile Subaru, ikampita halafu mbele kidogo ikasimama na kurudi nyuma mpaka pale gari ya Amata iliposimama. Ngishu akashuka na kuifuata ile gari, Amata akshusha kioo taratibu baada ya kumuona Mhindi huyo, ambaye sasa ni mara ya kwanza anakutana naye uso kwa uso. Ngishu akasimama pale dirishani na kumtazama Kamanda Amata, na Amata naye akafanya vivyo hivyo.
“Ukiendelea kunifuata fuata nakuua!” Ngishu akamwambia Amata kisha akamwonwsha kidole cha kati.
“Umeshaua wangapi mpaka sasa?” Amata akauliza huku akipandisha kioo.
Mustafa alifika Mwananyamala pasi na kujua wapi anatakiwa kuelekea, akapunguza mwendo ili aweze kupiga simu kwa mwenyeji wake, akiwa katika harakati hizo aistuka kioo cha gari yake kikitawanyika vibaya. Akayumba barabarani na kutoka nje ya barabara, akajaribu kuiweka gari yake vizuri lakini hakufanikiwa alipojikuta akipokea jiwe lililotua kichwani mwake na kumwachia jeraha kubwa, damu zikaanza kummwagika, maera mlango wa gari hiyo ukafunguliwa kwa ghafla, akavutwa nje na kuangushwa chini. Akajitahidi kuinuka lakini teke kali ikatua usoni na kumtupia upande wa pili.
Nukta hiyo hiyo ile Subaru ikaibuka eneo la tukio, Ngishu akafungua mlango na bastola mkononi, la haula! Kabla hajafanya lolote, gari yake kishindo kikubwa kikasikia, ile Subaru ikagongwa na gari la taka taka, Kebby ambaye bado alikuwa hajatoka katika gari akajikuta akibanwa vibaya mpaka akashindwa kupumua, Ngishu akasukumwa na kubwagwa kando, mshike mshike.
Watu wakaanza kusogea eneo hilo baada ya kusikia kile kishindo, ndani ya gari la takataka, Amata akashuka haraka, na kumwona Ngishu akijiweka sawa na bastola yake, Amata akaruka sarakasi maridadi na risasi zilizotoka kwenye bastola ya Ngishu zikamkosa, naye akatua kifuani mwa Mhindi huyo kwa miguu yote miwili na kumpeleka chini. Ngishu alianguka chini huku bastola ikimtoka mikononi.
“Tat! Tat! Tat! Tat!” risasi mfululizo zikapigwa hewani, Amata akajitupa chini akaviringika mpaka kwenye gari bovu lililosimama eneo hilo na kujificha huku akishuhudia wale jamaa wakikokotana na kuingia kwenye Regius nyekundu, wakapote a zao. Akajitokeza na kumuwahi Mustafa pale chini, akaiendea gari ya jirani na kuchomoa funguo zake zisizoshindwa, akafungua na kuimtupia Mustafa siti ya nyuma, yeye akakaa nyuma ya usukani na na kuondoka kwa kasi mpaka eneo la Komakoma alikoiacha gari yake, akamshusha Mustafa na kumpakia kwenye Ford kisha wakatokomea.
ITAENDELEA.