Riwaya: "Hujuma Nzito"

RIWAYA-HUJUMA NZITO-PART 27

SURA YA KUMI NA MBILI

Kachero Yasmine alizinduka majira ya saa 1:30 asubuhi mwanana, huku miale ya jua lisiloumiza ikianza kupenya kwenye dirisha la chumba alichohifadhiwa. Kichwani alikuwa amezungushiwa bandeji nzito kuzunguka kichwa chote. Bandeji ambayo ilikuwa na matone ya kutosha tu ya damu, iliyotonwa kutoka kwenye mishipa yake ya damu ya kichwani.

Alipotupa macho yake pembeni akaliona dripu la damu linashuka mwilini mwake huku pembeni yake kukiwa na meza chakavu iliyokuwa imetapakaa madawa mbalimbali na vifaa tiba kama sindano, pamba, mikasi na vifaa vinginevyo. Kilikuwa ni chumba kizuri wastani wake si haba ingawa kilikuwa bado hakijaisha vizuri matengezo yake.

Ukuta wa chumba hicho ulikuwa haujapigwa plasta wala juu yake kuwekwa silingibodi. Aliona taa ya Mchina ya kuchaji ndio inaangaza mwangaza mle ndani kuonyesha hamna umeme. Alipoendelea kutupa macho zaidi akaona buti za jeshi pea kama mbili na sare ya jeshi la wananchi JWTZ imetundikwa mlangoni.

Hofu ikaanza kumtawala mwilini mwake huku akishangaa na kuanza kujiuliza kuwa "yupo wapi hapa alipo na amefikaje hapo!". Akaanza kuvuta hisia ya kumbukizi kujua alipatwa na maswaibu gani mpaka ameletwa humo. Akaanza kuhisi maumivu makali sana ya kichwa yalioanza kumbangua vilivyo.

Ghafla akiwa ndani ya lindi la mawazo akaanza kusikia sauti ya ufunguo unagombana na kitasa mlango. Baada ya sekunde kadhaa mlango ukawa upo wazi akaingia mama mmoja wa makamo, amevalia sare nyeupe. Kwa muonekano ni nesi wa kike akiwa amebeba mkoba wake. Alipoingia moja kwa moja akaja pale alipo Kachero Yasmine na kumsalimia.

"Umeamkaje? pole sana kwa maumivu!" aliuliza nesi yule kwa uso wa bashasha. Kachero Yasmine akajibu kwa ishara ya kichwa kuwa yupo vizuri na kujilazimisha kutabasamu. Hakutaka kumuonyesha sana kuwa ana nguvu maana alikuwa hajui yupo wapi na kwa madhumuni gani ameletwa hapo.

"Usiwaze sana, pumzika ili mwili upate nguvu yake kwa haraka. Haya nataka nikuchome sindano ya kupunguza maumivu na itakupa usingizi muruwa". Akazungumza yule nesi na kuelekea juu ya ile meza akautua mkoba wake. Akaufungua na kutoa chupa za dawa mbalimbali. Akaanza kuchanganya michanganyiko yake kisha akaivuta dawa kwenye sindano yake kisha akaanza kumjongelea tena mgonjwa wake na kumdunga sindano ya kwenye kalio la kushoto. Alipomaliza kazi yake iliyomleta chumbani mule, akafungasha virago vyake na kuondoka zake.

Kachero Yasmine baada ya matibabu yale aliyopewa, akapitiwa tena na usingizi mzito raundi ya pili uliomlaza kwa zaidi ya saa sita mpaka majira ya adhuhuri alipozinduka toka usingizini. Alishaanza kupata nguvu kabisa, alijeruhiwa kichwani tu ambapo tatizo kubwa lilikuwa ni upotevu wa damu. Sasa kumbukumbu zake zilianza kurejea vizuri kabisa. Akakumbukia mtiririko wote wa matukio mpaka akapigwa kiti cha kisogoni na mahasimu wake.

Kilichokuwa kinamtatiza ni je bado ametekwa na mahasimu zake au yupo kwa msamaria mwema. Maana alishangaa hamna ulinzi wowote uliowekwa dhidi yake wa kumdhibiti asitoroke. Na kama kweli yupo kwa msamaria mwema kwanini asingempeleka hospitalini anampa tiba za vichochoroni anakwepa nini?. Hayo yalikuwa ni maswali yanayomtatiza Kachero Yasmine. Akawa anatamani kweli akutane na huyo msamaria mwema wake.
Adhuhuri hiyo hiyo akaletewa chakula na yule nesi, akakipiga kisawasawa kutokana na ubao aliokuwa nao. Yule nesi alipoondoka zake na kufunga mlango wa chumba, akaamka kitandani na kuanza kusogelea dirishani ili achungulie mandhari ya nje ya chumba.

Macho yake yakakaribishwa na fensi kubwa yenye urefu wa zaidi ya meta saba za waya imara, nyuma ya fensi hiyo kulikuwa na msitu mzito ulioshonana miti yake wenye nyasi ndefu, huku kwa mbali zikisikika sauti za ng'ombe wakiswagwa malishoni.

Pia sauti za ndege ndio zilikuwa kiburudisho kitamu masikioni mwake, huku akiwaona wakiruka toka mti mmoja kwenda mwingine kwa madoido. Bila kuwasahau tumbili nao walikuwa wanajivinjari katika uwanja wa nyumbani. Kwa ufupi yalikuwa ni mazingira ya porini sana sio Mjini kabisa.

Akaanza kuzunguka mle chumbani kuona huenda atakuta kitu chochote zaidi ya hizi pajama nyepesi za wagonjwa alizovikwa hakukuta chochote. Akajua ameshapoteza kila kitu chake kuanzia simu ya mkononi, funguo ya gari lake, bastola yake, flashi ya kuhifadhia nyaraka zake, mpaka nguo zake.

Alichoshukuru Mungu yupo mzima na hajabakwa kama walivyotia nia wale maadui zake. Maana kama wangemla mande sasa ingebidi apelekwe ANGAZA kwenda kupima kama ameambukizwa virusi vya UKIMWI au laa. Akamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuzidi kumpigania huku akishukuru kitabu chake cha uradi wa “Yasin Mubin” aliousoma pale Sinza huenda unemuokoa na majanga yote hayo.
Baada ya utalii huo mfupi akarudi zake kitandani na kuketi yake huku akianza kutafakari namna ya kuchomoka chumbani mule. Alijua tu gari yake ataikuta tu salama pale maegesho nje ya yale maduka ila itabidi akafuate ufunguo wa akiba nyumbani. Ila kilichokuwa kinamtatiza kuwa akitoroka ataelekea wapi maaana hajui yupo Mkoa gani na sehemu gani ya nchi.

Pia hana hata senti tano nyeusi mfukoni yupo yeye kama yeye, atafikaje nyumbani kwake?. Akafanya maamuzi magumu kuwa liwalo na liwe lakini hawezi kukubali kulala tena usiku mwingine, ni upotevu wa muda tu atatoroka na kujua huko huko msituni kitu cha kufanya mpaka akatakavyojiokoa.

Akaanza kukumbukia suluba waliozokuwa wanazipata porini enzi yupo kwenye mafunzo ya ukomandoo, jinsi walivyokuwa wanapambana na wanyama wakali wa mwituni lakini alifanikiwa kumaliza mafunzo hayo kwa usalama. Mafunzo ambayo yalimjengea ujasiri wa mapambano bila uoga kwa binadamu wa sampuli yoyote ile.

Mpaka majira ya magharibi yanaingia na kuanza kuyoyoma zake kwa kuukaribisha usiku mbichi wa saa usiku, bado hakuna mtu yoyote aliyekuwa amekuja tena kwenye kichumba kile. Tumboni bado alikuwa yupo vizuri hana hisia za njaa kabisa kwa sababu mlo alioletewa adhuhuri ulikuwa kabambe kwelikweli. Hivyo tatizo halikuwa njaa, ila alichokuwa anahitaji ni kujua yupo wapi na amehifadhiwa hapo kwa minajiri gani.

Akanyanyuka tena na kwenda kuwasha taa ya kuchaji iliyopo mezani hivyo nuru ikaanza kuenea ndani ya chumba. Kisha akasogelea dirishani tena, macho yake yakapokewa na kiza kizito na sauti za wadudu wa usiku wa porini. Kwa mbali sana akawa anasikia sauti za mbwa kubweka ovyo, akaanza kufurahi.

Zilikuwa ni dalili ya kuwa sehemu hiyo sio mbali na maeneo wanayoishi watu hivyo hatopata shida kupata msaada pindi akitoroka. Wakati anapanga mipango ya namna atakavyotoroka akasikia sauti ya gari linavuma kwa nguvu kukaribia uelekeo wa kwenye chumba alichohifadhiwa.
Kachero Yasmine akakimbilia mpaka kwenye mlango na kuchungulia kwenye tundu la ufunguo na kuchungulia nje.

Akaona gari aina ya Jeep-New Model rangi nyeusi inaegeshwa, ikiwa imewasha taa zake zote. Wakashuka watu wa wawili, mmoja mrefu sana lakini amejazia kimtindo amevalia kombati za jeshi, zilizo chafuka vyeo mabegani. Akiwa ameambatana na mwenzake mwenye mwili wa kawaida tu.

Wakawa kama kuna kitu wanajadiliana kwa muda kisha wakaanza kuja uelekeo wa chumba kile huku wamewasha kurunzi zao. Kachero Yasmine himahima akachomoka nduki kwenda kuzima taa kisha akarukia kitandani kwake.
Ikabaki kazi ya funguo wao kugombana na kitasa kugombania kuuacha mlango wazi pindi walipoufikia mlango wa chumba. Funguo wao ukashinda vita hiyo na kufanikiwa kuuacha wazi mlango. Wakaingia kwa tahadhari kubwa huku wakipiga tochi chumba kizima.
ITAENDELEA
Haya KACHERO YASMINE YUPO KWENYE TENGETEHANANI, HAJUI YUPO WAPI..,

Sent from my TECNO CC6 using JamiiForums mobile app
 
RIWAYA-HUJUMA NZITO-PART 30


Alipofikishwa moja kwa moja akapokewa na watumishi wa jumba lile ambao walishataarifiwa ujio wake hivyo kila kitu kilienda kiulaini. Bahati yake Kachero Manu ni kutekwa kwa Man-Temba hivyo taarifa zilizopo kwa Profesa ni zile zile za kuwa hamna mawasiliano mpaka ipite wiki moja na huyu Kachero Manu ndio kijana aliyetumwa na Man-Temba.

Pia taarifa itakayopelekwa kwa Profesa na Dr.Pius Chilembwa ni kuwa sasa hamna mawasiliano tena mpaka itakapopangwa upya mipango. Kinyume chake angeweza kucharangwa mapanga na kufukiwa ndani ya jumba hilo maiti yake isionekane kabisa.
Kama kawaida Profesa alikuwa amelala baada ya mkesha wa usiku, hivyo nae Kachero Manu akashauriwa apumzike maana mwenyeji wake ataonana nae usiku.

Alikuwa na mshawasha na kimuhemuhe cha kukutana na Profesa. Hamu yake ilikuwa ni kutaka kumuona huenda akawa anamfahamu. Saa zikayoyoma mara ikafika saa 4 usiku akaitwa kwenye chumba maalumu kilichopo roshani ya 4.
Akaingia kwenye chumba huku kiroho cha uwoga kinamdunda. Kile chumba kilikuwa kina kompyuta zisizopungua 10 huku zikiwa na majina ya nchi tofauti tofauti duniani. Akaelekezwa akae kwenye kwenye Kompyuta iliyoandikwa Tanzania. Akapewa maelekezo ya kuvaa vifaa maalumu masikioni mwake. Ghafla mazungumzo yao yakaanza kupitia vifaa alivyovaa masikioni.

Profesa alikuwa nae yupo kwenye chumba chake maalumu ndipo anapotoa maelekezo hayo. Kachero Manu akayakumbuka vilivyo maelekezo ya Mr.Okworonko ya kuwa amekaa chini ya Profesa miaka kadhaa lakini hajawahi kumtia machoni. Ghafla kuna kitu Kachero Manu akakumbuka, akauchomoa mkebe wake maalumu, mdogo sana na mwembamba toka kwenye mfuko wake wa suruali.

Ndani ya mkebe huo kulikuwa na vifaa mbalimbali vya kielektroniki. Akauchomoa waya mmoja aliouhifadhi kwenye mkebe mdogo akaaunganisha kwenye kompyuta anayoitumia. Kisha akauweka mkebe huo pembeni ya ukingo wa kompyuta.
Sasa akawa anamrekodi sauti Profesa yule wakati wanazungumza bila hasimu wake kung'amua. Baada ya nusu dakika tu ya kuutumia, akauchomoa huo waya na kuurudisha akiwa ameinasa vilivyo sauti ya Profesa.

Alishajua kitu atakachofanya kwa kutumia hiyo sauti aliyoidukua kuweza kuiona sura ya Profesa mubashara bila chenga wala mawenge. Alikuwa anaelekezwa kwenye mafunzo hayo njia ya kisasa ya kukwapua pesa kwenye mashine yoyote ya ATM. Alichagizwa kuwa ni aibu kwa mtaalamu wa mifumo ya kompyuta kulalamika hauna ajira wakati pesa zote za kwenye mabenki ni zako.

Kwanza alipewa lengo la yeye kuletwa pale kuelekezwa kuwa pesa zilizoibwa Tanzania zinataka kurudishwa zikafanye kazi husika. Hizo pesa zitakapotolewa zitasafirishwa kwa njia ya barabara mpaka Tanzania na kuwekwa mafichoni. Kisha kuna tangazo limetoka tayari la kuhakikisha wamiliki wote wa VICOBA wote na SACCOSS nchi nzima wafungue akaunti benki.

Hivyo kwa kutumia mtandao huo wa VICOBA uliosambaa mpaka vijijini nchi nzima itakuwa rahisi pesa hizo kusambazwa nchi nzima kwa kuweka kwenye hizo akaunti. Kisha wao kwa kutumia njia za wizi wa kimtandao watakuwa wanazitoa pesa zao kinyemela kutoka kwenye akaunti za VICOBA kwa kutumia kadi za benki bandia na kuzitumia watakavyo.

Profesa akazidi kufunguka kuwa katika pesa zilizoibwa, ni nusu yake tu ndio zitarudi Tanzania huku zingine zikiwa ni mgao wa watu wote waliofanikisha zoezi hilo la utoroshwaji na gharama zote zilizotumika kukamilisha zoezi zima.
Kachero Manu alishtushwa kusikia karibia nusu ya pesa zimeshapigwa na vigogo wa Nyasa Empire Supporters (NES). Akajiapiza kimoyomoyo kuwa pesa hizo lazima watazitapika hata kama ikibidi kwa kuwakata mafigo yao na kupelekwa nchini India yakauzwe.

Baada ya hapo sasa akaanza kuelekezwa namna ya kuongeza mapato mapya ya chama pia kwa kutumia kutumia ATM-kadi. Kwenye mbinu hii ni Kachero Manu atahitajika kutumia Kadi feki ya ATM (Clonned cards) maalumu zilizotengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu sana, ambayo ina uwezo wa kuiba taarifa za kibenki za wateja na kumwezesha mhalifu kupakua pesa kutoka kwenye akaunti mbali mbali kwa kutumia mashine ya ATM. Kadi hizi zilikuwa zimeunganishwa na programu ya MRS606 pamoja na 'malicious softwares' zingine za wizi wa mtandaoni.

Kwa maelezo ya Profesa ni kuwa hizo kadi zilikuwa zimeagizwa toka nchini Marekani kutoka kwenye magenge rafiki ya uhalifu ambayo yeye Profesa ni mwanachama pia. Gharama ya kila kadi moja ni dola za kimarekani (USD) 150,000. Hivyo akaelezwa kuwa anachotakiwa kufanya yeye ni kupambana kupata tarakimu halisi za akaunti ya benki za watu wenye uwezo wa kipesa kama Wabunge, Mawaziri, Wakurugenzi, Wafanyabiashara na hata Wafanyakazi wa umma.

Akashauriwa kuwa hizo namba za akaunti za walengwa wanaweza kuzipata kwa kuwawinda wanapokuwa benki wanajaza fomu za kutoa pesa anatakiwa ale chabo kwa kunakiri namba hizo. Pia wakiwa kwenye ATM-mashine vigogo hao kama wakitupa risiti kwenye pipa la taka. Pia alielekezwa mbinu ya kufungua taasisi ya mikopo na kujitangaza kukopesha mikopo ya riba nafuu ya chini ya asilimia 5% kwa Watumishi wa Umma na Wafanyabiashara wakubwa.

Masharti ya mikopo hiyo ni kuandika jina lako, namba ya akaunti ya benki unayoitumia mara kwa mara katika miamala yako ya kipesa na anuani ya kituo chako cha kazi au ofisi zako za kibiashara. Profesa akasisitiza kwa mbinu hizo lazima tu utapata akaunti namba ya walengwa wako.

Baada ya kuzipata akaunti namba hizo, ataichukua kadi feki maalumu zilizonunuliwa Marekani na kuziingiza kwenye mashine maalumu ambayo anaiunganisha kwenye Kompyuta. Hiyo kadi itasoma kama kadi huru. Baada ya hapo ataingiza zile tarakimu za akaunti alizopata toka kwa walengwa wake.

Muda tu ambao yule mteja mwenye akaunti halisi atakapoitumia ATM kadi yake basi 'Software' maalumu iliyopo ndani ya kadi feki, kompyuta na mashine itaweza kutoa taarifa zote za kibenki ikiwemo salio lililobaki pamoja na nywira ya akaunti namba iliyoingizwa. Baada ya hapo bila wasiwasi wowote ataenda kwenye ATM-Mashine kuchomoa pesa anazotaka kupitia kwenye akaunti ya yule wanayemtapeli.

Mafunzo ya siku ya kwanza kwa Kachero Manu yakaishia ya majira saa nane za usiku. Akaahidiwa kesho yake kuanza kufundishwa mbinu zingine kabambe ili mradi mipango ya “Nyasa Empire Supporters” (NES) isije kufeli kwa kigezo cha pesa, bali ifeli kwa uzembe mwingine tu. Kachero Manu alibaki mdomo wazi kwa jinsi Profesa huyo alivyokubuhu kwa akili za utapeli.

Akatoka kwenye kile chumba maalumu na kuelekea kwenye chumba chake huku sasa Profesa akiendelea na maelezo yake kwa vijana wengine toka nchi mbalimbali ambao nao walikuwa foleni nje ya chumba kusubiri zamu yao ya kupata maelekezo. Alipishana mpaka na waarabu na wazungu wanaosubiria kuingia kwenye kile chumba maalumu kwa mafunzo ya utapeli.


Nathanieli aliegesha gari kwenye nyumba ya jirani na nyumba anayoishi Yasmine. Nyumba ambayo Yasmine kwa maelezo yake alidai kuwa ni nyumbani kwa Baba yake mdogo. Gia aliyopanga kuingia nayo kama kweli akimkuta huyo Baba yake mdogo ni kujieleza kuwa amekuja kumtazama Yasmine kwa sababu ni mgonjwa. Na hapatikani kwenye simu yake hivyo yeye kama Mkuu wake wa kazi amekuja kufuatilia maendeleo yake ya kiafya.

Alipofika getini akaegesha gari pembeni kisha akaanza kubisha hodi kwenye geti. Baada ya kugonga mara kadha, ukimya ukatawala bila kupata muitikio wowote. Akajaribu kuangalia kama kuna kengele ya kubonyeza pembeni mwa geti, lakini hakufanikiwa kuitia machoni. Alipochunguza vizuri, kigeti kidogo kilikuwa kimeegeshwa hakijafungwa na ufunguo wala kukandamizwa vizuri.

Akapiga moyo konde na kuamua kujiongeza kwa kuingia bila kukaribishwa. Akaingia ndani ya fensi ya nyumba hiyo na kukaribishwa na mandhari ya nyumba kubwa mbele yake na upande wake wa kulia una nyumba ndogo ya mtumishi. Nathanieli akawa anaelekea nyumba kubwa kwa mwendo wa pole bila kuzalisha vishindo vyovyote vya miguu.

Mpaka akapanda kwenye ngazi za barazani, akaona madirisha yapo wazi huku kwa mbali anasikia watu wawili sauti ya mwanamke na mwanaume wanaongea kimahaba na kutoa sauti za miguno ya kubembelezana, wakionekana ni wapenzi walioshibana.

Kifua cha Nathanieli kikaanza kuchemka kwa joto kali la hasira. Joto la wivu lilimvaa mwilini, jasho jekejeke likaanza kutiririka mwilini mwake. "Ina maana huyu malaya ananibania mimi kumbe kuna mjinga kapuku tu hata gari hana tena anakuja kumbanjulia ukumbini kwake!" alinong'ona taratibu Nathanieli huku akitaka kushuhudia kabisa. Akazidi kujisogeza dirishani akajibanza kwa pembeni ya wavu wa kuzuia mbu wa dirishani asikilize kinachoongelewa humo ndani kati ya anayedhaniwa kuwa ni Yasmine na huyo mpenzi wake.

"Hans...nakupenda sana kupita maelezo, yule Bosi wangu zoba kweli ananitaka kwa gharama zote mie simpendi, na mtambi ule kama chura mwenye mimba mie nitamuweka wapi" aliongea kwa sauti ya upole ya kutokea puani yule mwanamke kueleza hisia zake kwa huyo mpenzi wake.
Nathanieli hamaki ikamvaa mwili wote huku akijiangalia tumbo lake namna lilivyoumuka akaona kabisa Yasmine ameamua kumnanga yeye kwa kebehi za uzalilishaji. Uzalendo ukamshinda baada ya kuona mihemo na makelele ya mahaba inazidi hasa kwa mwanamke ampendae sana kama Yasmine.

"Ngo...Ngo..Ngo....Ngo..., hodiii...hodiii...hodi humu ndani..!" aligonga kwa nongwa haswa ili hasimu wake asiendelee kumfaidi Yasmine. Kimya kizito cha ghafla kikatawala pale sebuleni kama vile hamna mtu. "Ngo..Ngo...Ngo..", "Karibuuu...!" sauti ya kiume ya kiunyonge ilijibu baada ya kusikia mlango unagongwa tena kwa mara ya pili. Baada ya sekunde kadhaa mlango ukafunguliwa.
ITAENDELEA

Sent from my TECNO CC6 using JamiiForums mobile app
 
RIWAYA-HUJUMA NZITO-PART 31

Ngo...Ngo..Ngo....Ngo..., hodiii...hodiii...hodi humu ndani..!" aligonga kwa nongwa haswa ili hasimu wake asiendelee kumfaidi Yasmine. Kimya kizito cha ghafla kikatawala pale sebuleni kama vile hamna mtu. "Ngo..Ngo...Ngo..", "Karibuuu...!" sauti ya kiume ya kiunyonge ilijibu baada ya kusikia mlango unagongwa tena kwa mara ya pili. Baada ya sekunde kadhaa mlango ukafunguliwa.


"Karibu Mzee, Shikamoo" aliongea yule kijana aliyefungua mlango huku akiwa ametawaliwa na wasiwasi usoni mwake. "Ina maana Yasmine anakamuliwa na Kiben-10, kweli huyu hamnazo" aliwaza Nathanieli baada ya kumuona kijana mwenyewe anayemlaki mlangoni hapo hata kwenye kiganja cha mkono hajai. "Marahaba Yasmine nimemkuta hapa kwake?" alijitutumua kuuliza swali la jambo lililomleta.


"Hapana, hayupo, Bosi Yasmine toka jana hajarudi nyumbani sifahamu alipo, akija nimwambie nani alikuja?" alijibu kwa sauti ya hasira akionekana hajapendezwa na ujio wa mtu aliyekuja kumkatia stimu ya starehe zake huku akionekana anajiandaa kufunga mlango, hataki usumbufu. Nathanieli fikra zake zilimtuma Yasmine yupo ndani ila anataka kufichwa kitu, akaupiga kikumbo mlango na kujilazimisha kuingia kwa kushtukiza.

Hamadi...! Akamkuta binti mdogo tu yuko pale ukumbini ana sura ya wasiwasi, uso umejaa soni kwa aibu tele ya kufumaniwa. "Shikamoo..Baba..!" alisalimia kwa aibu yule msichana huku ameinamisha kichwa chake chini. Nathanieli hakujibu kitu, alishagwaya kwa sababu alichokikuta ni kinyume na matarajio yake. Hapa kilichokuwa kinaendelea ni paka akitoka panya hutawala, picha ikionyesha kuwa ni kuwa Shamba-Boi wa Yasmine alimvuta dada wa kazi wa jirani kujivinjari nae kimapenzi.

Nathanieli hakuitikia salamu aliyotunukiwa zaidi ya kuondoka eneo lile kwa hamaki bila hata kuaga. Ingawa aliondoka shingo upande kwa kutomkuta Yasmine, lakini hisia zake kuwa Yasmine ni kirusi cha Makachero kilichopandikizwa ofisini kwao zikazidi kustawi na kumea akilini mwake.
Dalili zote zilionyesha ile nyumba sio ya kifamilia kabisa hamna cha baba mdogo wala mama mdogo anayeishi pale. Pia mashaka yalizidi zaidi inakuwaje mtu mgonjwa asishinde nyumbani apite kuzurura tu mpaka nyumba yake inageuzwa danguro.

"Kuanzia sasa namuwekea vijana wa kumwinda na kumfuatilia nyenzo zake, kifo ni halali yake kwa mikono yangu" alijiapiza nafsini mwake huku anaondoka na gari lake maeneo yale. Tayari alishahukumu kuwa Yasmine sio mtu anayestahili kuendelea kung'ara sura yake katika mgongo wa dunia.

Kwa upande wake Yasmine akiwa hana hili wala lile, aliingia nyumbani kwake majira ya saa 3:30 usiku akitokea hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwenye matibabu. Majibu huko ya daktari wake yalikuwa ni mazuri sana. Hakugundulika kuwa na matatizo yoyote makubwa ya kiafya hivyo alitakiwa tu auguze jeraha lake la kichogoni.

Alipofika nyumbani kwake kijana wake, Shamba-Boi alionekana kama ana wasiwasi na kama vile ana kitu anataka kumuambia lakini anaficha. Yule kijana alikuwa anataka kutoa taarifa za ujio wa mtu pale nyumbani, lakini alikuwa anahofia huyo mtu atakapoongea na Bosi wake Yasmine atamueleza kila kitu kuhusu yeye kuingiza ghashi ndani ya nyumba ya Bosi wake itakuwa msala kwake. Yasmine alishamsoma kisaikolojia kuwa kuna kitu anamficha.


Mara tu baada ya kuoga zake akaingia kwenye chumba cha CCTV-Kamera, kuangalia mienendo ya pale nyumbani kwake wakati hayupo. Yule Shamba-Boi alikuwa hajui kama matukio pale yote yanarekodiwa masaa 24. Kwa mshangao mkubwa sana akamuona Nathanieli amekuja nyumbani kwake na kaingia mpaka ukumbini kwake akawa anazungumza na Shamba-Boi wake.
"Amekuja kunifanyia taftishi, kanishtukia tayari kama nimewadukua?", Kamwambia Shamba-Boi wangu Hans asiseme ujio wake, mbona kakaa kimya?" ni baadhi ya maswali lukuki aliyokuwa anajiuliza Yasmine bila kupata majibu.

Mambo mengine aliyoyashuhudia kwenye CCTV-kamera ya Hans kumleta dada wa kazi wa nyumba jirani ndani ya nyumba kuu hakujali sana. Ulikuwa sio wakati wake kujadili upuuzi ule kulikuwa na mambo makubwa zaidi mbele yake ya kufuatilia kwanza.

"Zege halilali, nitakwenda usiku huu nyumbani kwake kumuuliza alifuata nini kwangu mchana kweupe kama sio mwanga ni nini sasa, kifo ni halali yake kwa mikono yangu..!" Yasmine alijiapiza huku akibadili nguo zake za kulalia na kuvaa za kazi ili aingie tena mzigoni. Alipanga akirudi huko kwa Nathanieli ndio atafanya mawasiliano na Kachero Manu ili wapeane taarifa wapi wamefikia katika taftishi zao za kuisambaratisha “Nyasa Empire Supporters (NES).

Akaingia kwenye gari lake na kupiga honi ishara ambayo ilimkurupusha kijana Hans chumbani kwake kuja kufungua geti ili kumruhusu Bosi wake atoke. Yasmine alipotoka tu akapita kama nyumba tatu hivi ya nne kutoka pale kwake kulikuwa na Baa maarufu tu katika mitaa ile.
Baa hiyo tayari ilikuwa imejaza watu lukuki wanafurahia maisha kwa namna wanavyoona wao inafaa kuyafurahia.

Akasimama mbele kidogo ya eneo hilo na kushuka nje ya gari, baada ya kujikuta amebanwa na kiu na hajabeba maji. Nyuma kidogo tu ya pale alipoegesha gari lake kulikuwa na gari nyingine aina ya 'Subaru-Forester' rangi nyeupe imeegeshwa kwa kujitenga kidogo na gari zingine.

Akaizunguka gari hiyo huku akimuona kijana mmoja akiwa amevalia fulana nyeupe na miwani nyeusi akiwa ameegemea kwa nje, mlango wa upande wa kushoto, kiti cha abiria anavuta sigara macho yote yapo uelekeo wa nyumba ya Yasmine. Yasmine hakumjali akampita lakini akiwa tayari ameshaikariri namba ya gari hilo kichwani mwake na kuelekea moja kwa moja kwenye njia ya kuingilia pale Baa akaenda mubashara mpaka kaunta.

Akazungumza na muuzaji baada ya sekunde kadhaa akakabidhiwa chupa kubwa ya maji. Akailipia na kuondoka zake huku akiifungua chupa hiyo njiani na kuanza kuinywa kabla hata hajafika kwenye gari yake. Alipotoka nyumbani alijigundua hajanywa maji ya kutosha, na kutokana na hali yake ya kiafya ilikuwa inamlazimu afanye hivyo kila anapopata wasaa.

Alipoingia kwenye gari yake, kabla hajaanza kuondoka, akawasha taa ya ndani ya gari kwa lengo la kukagua kilemba chake cha kichwani kama kimefungwa vizuri kusitiri jeraha lake lililozingushiwa bendeji. Akajiridhisha kuwa yupo sawa. Akaanza kuliondoa gari lake toka eneo hilo kwa mwendo mdogo mdogo na kutimka kuja maeneo ya Bamaga anapoishi Nathanieli.

Alikuwa anakwenda tu kwa mwendo wa wastani mpaka alipofika maeneo ya Tegeta Kibaoni eneo la mataa, wakati anasubiri taa za kijani zimpe ruhusa ya kuendelea kuitumia barabara hiyo ya Mwai-Kibaki alipotupa jicho kwenye kioo tu, akashtuka kidogo.

Gari ya tatu yake kutoka nyuma yake ilikuwa ni “Subaru-Forester” nyeupe ile ile aliyoitia machoni pale Baa ya jirani na kwake, na namba zake za gari ndio hizo hizo. Huku dereva ni yule yule jamaa aliyevalia fulana nyeupe aliyekuwa ameegemea mlango anajiburudisha na sigara.

Taa ziliporuhusu magari yanayoelekea Mwenge, Kachero Yasmine akachomoka nduki kwa spidi ya hatari akitaka kuwapima kama kweli wanamfuatilia yeye au wapo kwenye safari zao tu. Akajithibitishia bila mashaka kuwa wanamfuatilia yeye kwa sababu kila akiongeza kasi nao hawa hapa, akipunguza nao wanapunguza.

Walipovuka eneo la Bondeni tu, Kachero Yasmine akaongeza kasi huku akiwa yupo upande wa kulia wa barabara kuonyesha kama anaelekea Mwenge halafu ghafla tu akahamisha gari kuja kushoto na kukatiza kwa haraka sana kuja njia ya Kawe.

Kitendo hicho cha ujanja wa hali ya juu, kiliwachanganya wale maadui zake walijua anawatoroka. Nao wakatamani wahamie upande wa kushoto ili wamfuate njia ya Kawe. Dereva wao akakosa umakini alipohama hakupiga mahesabu vizuri akajikuta anakula dafrao kutoka kwenye Lori la nyuma yao lililosheheni mzigo wa makabichi likitokea Wilayani Lushoto, Tanga.

Ilikuwa ni moja ya ajali mbaya kuwahi kutokea kwenye eneo lile. Yasmine haraka haraka akaegesha gari kwenye miti pembezoni mwa barabara na kuja kushuhudia kwa macho yake, dafrao hiyo ya kutisha. "Wawaishwe hospitali haraka hawa huenda wakapona hao" yalikuwa ni baadhi ya makelele ya mashuhuda wa ajali ile.

Yasmine alipowaangalia vizuri wale majeruhi, akawakuta wapo watatu, lakini mmoja wapo ambaye hali yake ilikuwa nafuu alivunjika miguu yote, ila wale wengine walikuwa wamepata majeraha mazito ya kifuani na usoni kiasi kwamba wakati wowote walikuwa wanarejea akhera kwa Mola wao.

"Nisaidieni huyu mmoja kumpakiza kwenye gari yangu nimuwahishe Muhimbili" alipayuka Yasmine kwa sauti ya juu akijifanya ni msamaria mwema akiomba msaada wa raia wema kusaidiwa kumbeba yule mwenye nafuu kati yao. Yule jamaa kumuona Kachero Yasmine ambaye ni hasimu wao, yupo mbele yake ndio anataka kumpa msaada, akaanza kupiga kupiga kelele za kuwa wasimpeleke kwenye gari ya Yasmine.

Wale raia wema ndio kwanza hawaelewi kitu wanajua majeruhi akili zake zimefyatuka kidogo maana katika hali ya kawaida utakataaje msaada wa kuokoa uhai wako. Kumbe yule majeruhi alitambua kuwa ameshaingia choo cha kike mikononi mwa adui yake ambaye hana jema hata chembe na yeye.

Alivyopakizwa tu yule majeruhi, Kachero Yasmine akaliondoa gari lake kwa kasi akijifanya anamkimbiza hospitalini huku akiwa anatabasamu. Alikuwa akielekea kutafuta sehemu tulivu akambinye kwelikweli mpaka aropoke katumwa na nani amfuatilie.

ITAENDELEA


Sent from my TECNO CC6 using JamiiForums mobile app
 
Back
Top Bottom