Riwaya: Huba la miss Tanzania

HUBA LA MISS TANZANIA-PART 28
Dr.Sonko alikuwa alikuwa anajipeleka kwenye mdomo wa mamba bila kujua.

"Alipoona msimamo wangu ni thabiti sitaki katakata kuvunja uchumba na wewe, akakasirika sana. Akaamua anidhihirishie waziwazi kuwa yeye ni mgonjwa, ana virusi vya UKIMWI. Nilikuaga siku moja kuwa ninasafiri kikazi kwenda Mwanza kwa muda wa siku mbili. Yeye Dr.Sonko akapewa taarifa na mnyetishaji wake wa pale kazini kwetu kuwa nipo Mwanza kikazi.

Nikiwa sina hili wala lile nikashtukia Dr.Sonko amekuja hotelini nilipofikia. Nilikuwa nimeshachoshwa nae ila sina jinsi ya kujivua nae. Kwa madaraka yake alikuwa na uwezo wa kunidhuru vyovyote apendavyo kuanzia kunifukuzisha kazi mpaka hata kuondosha uhai wangu kama angependa.

Sikuwa na jinsi nikalala nae usiku wake huo. Asubuhi wakati anaenda kuoga kujiandaa aondoke zake, kwenye mkoba wake mezani nikaona kitu kama vidonge. Nikapatwa na tashwishi ya kupekenyua kujua ni vidonge vya nini. Nilipoviona tu moyo wangu ulinilipuka na kuanza kwenda mbio mbio.

Vilikuwa ni vidonge vya wagonjwa UKIMWI, ARV. Alipotoka bafuni akanikuta machozi yananitiririka mashavuni huku nimeshika mkononi vile vidonge vyake. Akacheka sana akaniambia kashaniambukiza UKIMWI hawezi kunisaidia chochote. Akaondoka zake na mimi nikakatisha safari yangu na kurejea Dar es Salaam. Sikutaka kupima UKIMWI kujua kama nimeathirika. Nilikuwa ninajipa matumaini huenda Sijaambukizwa.

Chambilecho mficha ugonjwa mauti humuumbua, siku tuliyopima wakati tunataka kufunga pingu za maisha ndipo nikagundulika nina virusi vya UKIMWI. Lawama zote nazibebesha kwa Dr.Sonko....", Shebby alikuwa amezama kwenye dimbwi la mawazo amejisahau kabisa kama mbele yake kuna mgeni mahashumu.Alikuwa anairejea kichwani barua ya mpenzi wake aliyoiacha kabla hajajitoa uhai wake.

" Hellow....mrembo hongereni kwa ugunduzi mzuri" ilikuwa ni sauti ya Naibu Katibu Mkuu, Dr.Sonko akiwa yupo mbele ya Shebby ndio iliyomzindua kutoka kwenye lindi la mawazo.

"Karibu sana Mheshimiwa sisi tumekuja na teknolojia ya paka mashine unaweza kushika umjaribu.." alizungumza Shebby kwa sauti ya kuigiza kama mwanamke kwa kuzungumzia kwenye tundu za pua huku machozi yanamtiririka.

"Ondosha uwoga binti jiamini, msaidizi wangu atachukua mawasiliano yako kwa ajili ya kuona namna nitakavyokuendeleza ha...ha... ha.. " alizungumza Dr.Sonko kwa madahiro huku anacheka na kumpigapiga mgongoni yule anayemdhania ni mwanamke kumbe ni mbaya wake Shebby.

Sasa ilifika wakati wa mgeni rasmi huyo, Dr.Sonko kujaribisha hiyo mashine paka. "Nooo... Noooo.... Noooo........." ilikuwa ni sauti ya Kachero Manu akimkataza Naibu Waziri Mkuu asijaribishe hiyo mashine huku tayari akishafyatua risasi kwenye mkono wa Dr.Sonko na risasi nyingine akimlenga Shebby kifuani mwake.

"Aaaaaaah......nakuf... aaah......"ilikuwa ni sauti ya Dr.Sonko akipiga kelele huku mlipuko mkubwa wa bomu ukitokea eneo lile la maonyesho. Mtifuano, timbwili na mkanyagano ukaibuka eneo lile, huku kila mmoja Yalabi toba! anapiga kelele kwa Mungu wake kuomba kuokolewa na madhara ya mlipuko huo huku walionusurika wakitafuta mlango wa kutokea.

Maonyesho yenyewe yakavurugikia hapo huku watu wakijeruhiana kwa kukanyagana na kupoteza mali zao za thamani.

Shambulio hilo la bomu lililotokea katika viwanja vya Sabasaba lilivurumisha kivumbi kizito nchi nzima ilikuwa inazizima. Taarifa rasmi ya idadi ya watu waliofariki kwenye shambulio hilo ilikuwa bado haijajulikana. Vidinga popo na wale habari kauzwa ndio ulikuwa uwanja wao wa kusambaza taarifa za uzushi na uwongo ili kuchochea hofu na taharuki katika jamii.

Ilipofika majira ya usiku mbichi wa saa 2:00 usiku wananchi walikuwa wamejikusanya kwenye runinga zao majumbani na kwenye kumbi za starehe kusubiria taarifa ya habari ili kujua taarifa rasmi ya serikali ya juu ya tukio hilo.

Taarifa rasmi iliyotolewa na msemaji wa serikali ilieleza kinagaubaga kuwa Shabani Zomboko ndio mhusika wa utegeshaji wa bomu hilo akiwa amejigeuza kama mwanamke na tayari ameshauawa pale pale na afisa wa usalama. Ilieleza kuwa marehemu Shabani Zomboko ndio pia mhusika wa matukio ya mauaji ya mfanyabiashara Pateli na mhadhiri wa chuo cha fedha, Profesa Kaganda. Pia ikaelezwa kuwa barua yenye maelezo ya sababu ya marehemu Shabani Zomboko kufanya mauaji hayo ya kutisha ipo mikononi mwa dola.

Pia ikatangazwa kuwa jeshi la polisi linawashikilia baadhi ya wanafunzi wa kike wa vyuo mbalimbali kwa kula njama ya kushiriki shambulio hilo ovu kwa kumruhusu mtu asiye mwanachuo kukaa kwenye banda lao. Ilitajwa kuwa idadi ya watu zaidi ya 20 wamepoteza uhai kutokana na mkanyagano wa hapo uwanjani.

Pia ikaelezwa kuwa Naibu Waziri Mkuu Dr Sonko yupo hai amesalimika kwenye shambulio hilo isipokuwa amejuruhiwa vibaya kwa kukatika mikono yake yote miwili na mguu wake mmoja, pia amepofuka macho yote mawili. Taarifa hiyo ikaishia huku ikawataka wananchi waendelee kuwa watulivu huku wakiviachia vyombo vya dola viliendelea na uchunguzi wao.

THE END OF THE STORY

Safi sana... Bonge la story...

Chapter Closed...



Cc: mahondaw
 
Back
Top Bottom