Riwaya: Hekaheka za Komando Zedi Wimba na Jasusi Honda huko Somalia

"Nadhani hatuna haja ya kubishana bwana Shafi'I; Mimi naenda zangu ila tatizo likitokea tafadhali usinishirikishe mana nitakuwa bize na kuwahudumia wagonjwa wengine." Dr Azam alitahadharisha huku akiandaa mizigo yake kwa ajili ya kuondoka.

Imamu akaona asipotumia busara basi atamkosa Dr na pia atamkosa mwanae.

"Usichukulie hasira bwana mdogo,ni mambo fulani tu yananipelekesha,usijali kaa humu usitoke hadi nitakapokuambia" Alisema Imamu huku akianza kutoka ndani ya chumba kile.

Dr Azam alirusha ngumi kwa majivuno ya kufanikiwa hila zake.

Haikuwa muda murefu sana tangu alipokaa ndani ya chumba kile mara alisikia harakati huko sebuleni na alijaribu kutazama kwa makini kama kutakuwa kuna kamera zilizofungwa mule ila hakuziona.

Alipojaribu kuangalia kama ataweza kuona nje, mara kwa juu aliona uwazi wa venti na aliona panamfaa kutizama.

Akasukuma kitanda akicholalia mgonjwa kisha akakipanda na kutazama nje kupitia vitundu vile.

Alifanikiwa kuona magari mawili ya kifahari yakiwa yamepaki huku kukiwa kuna walinzi wengi wenye silaha za kutisha.

Na katika gari mojawapo alishuka mzee mmoja aliekuwa amevaa kofia ya pama huku akichechemea kwa mbali na aliposhuka kulionekana kuongezeka ulinzi wa hali ya juu sana.

Dr Azam wa bandia aliamua kushuka na kurejesha kitanda.

Na punde mtoto aliamka.

Alimpa huduma zinazostahili kisha akakaa kwenye kiti na walibaki wanatazamana tu.


Dakika chache badae Imamu aliingia na kufurahi na mwanae, huku akijitahidi kumtania hapa na pale


"Dr unahisi mwanangu anaweza kupona sasa" Alisema Imamu..

"Yah! Kwa hapo alipofikia nadhani anastahili kupona kwa sababu nimepata dawa ya ugonjwa wake na baada ya wiki moja atakuwa sawa kiafya." Alisema Dr


"Sijui nitakulipa nini Dr ila naomba nikupe hii" Alisema Imamu huku akitoa hundi ya dola elfu hamsini na kumpa Dr; kisha akamwambia..

"Nitakuwa nakuhitaji kila mara ili unisaidie mambo fulani kuhusu afya ya watu wangu wa karibu,umenifurahisha sana kwa hili ulilofanya" Alisema Imamu.

"Sawa na ahsante sana" Alijibu Dr Azam huku akikusanya vitu vyake na waliongozana kutoka nje.

.
Utaratibu ulikuwa ni ule ule kama ni kawaida kurudishwa kwa kuzungushwa mitaani na kisha kuachwa kwenye duka la vifaa vya baiskeli.

Dr Azam alichukua gari lake na kuondoka kuelekea kazini kwake.


****

Usiku ulikuwa ni wakati wa kujadili kile walichokiona kwa siku nzima.

"Kwa mtazamo wangu naona huyu mzee atakuwa ndie Flamingo mwenyewe" Alisema Haji huku akiigeuza picha waliokuwa wamechora baada ya maelezo ya Zedi Wimba ambae alikuwa anatumia jina la Dr Azam.

"Kama ndie basi tutakuwa na kazi ya kufanya kuanzia kesho" Alisema Haji.

"Basi kesho ukiamka tu elekea pale mana inaonekana ni kikao cha siku na kadhaa hivi" Alishauri Zedi.


"Sawa" Alikubali Haji.

Makubaliano yao yalizua jambo jingine ambalo halikuwa kwenye mipango na hapo ndipo mchezo ulipokolea na Zedi kurudi kwenye hekaheka ndani ya mji wa Mogadishu.

Aliigeuza hekaheka ile kuwa ni operesheni Mogadishu.

Ahsubuhi ilimkuta Haji akiwa ameshafika karibu na jumba la Imamu Shafi'I na alikuwa makini ili nyendo zake zisistukiwe.

Kitu kimoja ambacho hakujua ni kuwa siku ile ilikuwa ni tofauti na siku zingine zote ambazo amekuwa akizitumia kupiga jicho la mwewe.

Ugeni uliokuwa pale kwa Imamu siku ile ulikuwa ni zaidi ya ugeni wa Rais wa Marekani katika moja ya nchi za bara la Africa.

Ulinzi ulikuwa ndani na nje katika hali ya kutisha, hivyo hata wakati yeye anaingia pale tayari macho zaidi ya kumi yalikuwa sambamba nae.

Jua lilipoanza kuwa kubwa ndipo Haji alipoona msafara wa gari kama nne hivi zikitoka langoni mwa nyumba ya Imamu Shafi'I.

Zilimpita nae alifuatia kwa nyuma. Gari zile zilikuwa ni za kisasa na kasi sana ila Haji alikuwa na gari ambayo haikuwa na ubora sawa na gari zile.

Msafara ule ulikuwa ni wakasi sana kiasi ambacho gari la Haji halikufua dafu kuunga msafara ule na hatimae zilimpotea machoni.

Alijisonya kwa kushindwa kufuatilia msafara ule na ule ulikuwa ni mwanzo wa kushindwa harakati zao.

Hakika ilisikitisha.

Wakati akiwa bado anazubaa barabarani mara ikatokea gari kwa nyuma na kugonga gari yake kisha ikamsereresha kwa kasi na kila alipojaribu kukwepa alijikuta anashindwa na kubaki akiwa ameshikilia usukani bila kufanya lolote na kisha kwenda kujingonga kwa nguvu kwenye gari lililokuwa mbele yake hivyo kujikuta akiwa amepata ajali mbaya sana iliomsababisha kujingonga kwenye vioo mara kadhaa na kumpasua juu kidogo ya paji lake la uso.

Akiwa bado anahangaika kujinasua ndani ya gari, wakatokea watu wawili wenye silaha na kuuvuta mlango kwa nguvu kisha kumtoa kwa mzegamzega na kumtupia ndani ya gari lao.

Alidondokea kwenye miguu ya watu wengine na alipotaka kuinuka alijikuta akipigwa kisogoni na kitako cha bunduki na taratibu uso wake ukapoteza nuru na kutanda kiza.

Akatulia tuli.

***


Masaa sita badae alikuja kustuka na kujikuta akiwa amefungwa uchi wa mnyama huku shining'inia na miguu yake ikiwa imewekwa kwenye beseni la umeme lenye kupooza maji mithili ya jokofu.

Alihisi miguu imeanza kupooza na ilikuwa inakuja kukamata mwili mzima.

Alipojaribu kutupa macho pembeni, aliona mtu akiwa ametundikwa kama yeye na alikuwa anangozi kama kuku anaeokwa na miguuni kulitandazwa chupa zilizotapakaa damu, damu ambayo alijua imetoka miguuni mwa mtu yule.

Kamba iliomfunga ilikuwa inazunguka kutoka upande mmoja kwenda mwingine na ndipo ilipozunguka na kumgeuzia uso upande alipo Haji.

Haji alitoa macho kama kinyonga.

Alikuwa anatazama uso wa Honda ambae alikuwa amechoka kwa kipigo na pia alikuwa ameiva mwili mzima kwa moto uliompata.

Hakika alitisha kutazama

*****

BADO HUJACHELEWA KUNUNUA RIWAYA HII KWA TSH 1000/= NA UTAPATA NYONGEZA YA RIWAYA NYINGINE BURE KABISA.

WHATSAPP ME 0658564341

MALIPO YAFANYIKE KWA NAMBA HII 0758573660..

JINA BAHATI MWAMBA

HAKIKI KABLA YA KUTUMA
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom