Riwaya: Hekaheka za Komando Zedi Wimba na Jasusi Honda huko Somalia

RIWAYA; URITHI WA GAIDI

NA; BAHATI MWAMBA

SIMU; 0758573660

SEHEMU YA NNE


Mfalme wa wajane alibaki akimtizama Ahmed na maamuzi yake.

Honda alikuwa katikati ya hisabati za Wasomali.

Hakujua aepuke vipi mtego wa hesabu ile, huruma ilikuwa kubwa karibu ibebe ujasiri wake.

*

Honda alibaki akiwa anazungusha akili namna ya kuepuka kumuua yule binti ambae alikuwa anamtazama Honda kwa huzuni na machozi yalikuwa yanambumbujika kwa kasi.

Honda alikoki mtutu tayari kwa kumuangamiza yule binti.
Aliusogeza mtutu usoni kwa yule binti na kidole kilikuwa tayari kipo kwenye kifyatulio na tayari alianza kuvuta kilimi cha mtutu.

Azana ikalia kutoka kwenye msikiti uliokuwa jirani na maeneo yale.

Honda alitumia nafasi ile vilivyo.
Akatupa chini mtutu na kuinama pembeni na kuanza kuswali swala ya adhuhuri.

Sozi na wenzie walibaki wakimtizama bila kutia neno na kisha alianza mmoja na kufuatia wa pili hatimae wote walijiunga na Honda kuswali.

Honda alitumia hesabu za akili kuliko walivyodhania.
Kimsingi kikundi cha AIAI; kilikuwa ni kikundi chenye mlengo wa dola ya kiislamu na lengo kuu la kukita mizizi yake katika pwani ya Somalia ni kuhakikisha wanaunda nchi ya kiislamu katika ukanda huo, hivyo ilikuwa ni karata safi alioamua kuitumia katikati ya malaika watoa roho na ukuu wa Mungu ulidhihirika.

Baada ya dakika kadhaa, wote walisimama wakiwa wamemaliza kuswali.

Sozi alikuwa bado anataka kukamilisha swala lake na alitaka Honda atekeleze.

“Ahmed shika hii” alisema Sozi huku akiokota chini silaha yake na kumpa Honda.

“Mungu hawezi kujibu maombi yetu tuliofanya sasa bwana mdogo,hivyo mtunze nitamuua katikati ya adhuhuri na jioni.” Alisema Honda p.a.k Ahmed ambae hakujishugulisha kuichukua silaha ile,badala yake alikuwa anahangaika kuunganisha nguo yake iliotatuliwa na kisu cha Sozi Mfalme wa wajane.

Sozi aliona ni dharau haraka akatoa kisu chake kwa lengo la kumshambulia Honda; ila hakujua mtu aliepembeni yake alikuwa ni mtu wa aina gani.
Kwa wepesi wa kawaida tu alikikwepa kisu kile na kumtandika Sozi ngumi moja ya shingo na kumpeleka chini bila kupenda. Washirika wa Sozi waliokuwa pale nao hawakutaka kuona Sozi akiadhirika nao wakaingilia ila kwa ustadi licha ya kudhoofu mwili aliwachapa kama mzaha vile na kujikuta wakiwa hawana la kufanya zaidi ya kumwangalia Honda ambae hakuwajali wakati huo wao walipokuwa wakiugulia maumivu.

Sozi alibaki akimwangalia Honda akiwa hana la kumfanya. Mara akawa kama aliekurupushwa kutoka usingizini akainyakuwa silaha yake iliokuwa pale chini na kumcharaza risasi binti ambae muda wote alikuwa akilia kwa hofu kwa yale yaliokuwa yanaendelea pale.

Binti aliaga dunia.

Honda alibaki akimtizama bwana mdogo Sozi aliekuwa amesimama na mtutu wake akiwa hana wasiwasi wowote.

**

Kutoka ndani ya Lugo hotel, kila kitu kilichokuwa kinaendelea kwenye karakana ile kati ya Sozi na Ahmed;kilionwa vyema kabisa na watu waliokuwa mle ndani.

“Licha ya kudhoofu ila bado anaweza kupambana, huyu kweli ni Ahmed Twalibu” alisema kijana mweupe huku akitabasamu, tabasamu ambalo hakuna aliejua linamaana gani.

“Kabla hatujaonana nae na kumdai tunachokitaka kwake, inabidi atumike kufanya jambo letu kesho kutwa na kabla ya keshokutwa hiyo kesho aingie kwenye majukumu mengine yaliopo. Hapo ndo tutajua tulienae ni Ahmed wa kweli au ni mtu tu tumeuziwa” alisema mzee wa kisomali aliekuwa mle ndani.

Wengine walikaa kimya kuhakikisha kila kitu kinachopangwa hakiharibiki.

**
Kutoka jengo lingine tena kulikuwa kuna watu wengine wawili ambao walikuwa wamekaa na vifaa kadhaa vya mawasiliano na walionekana kuwa bize kukata nyaya kadhaa za mawasiliano yale.

Hawa ndio waliokuwa kwenye kiunga cha kwanza ambao mwanzo waliwasiliana na Honda wakati akiwa ndani ya gari la AMISOM.

“Zedi; jamaa ameingia kwa hawa jamaa ila sina hakika kama atatoboa kutoka, tangu mwanzo naona ni mtu mwenye huruma sana” alisema jamaa mwingine aliekuwa amekaa kwenye kiti huku akiwa bize na kuchezea tarakilishi aliokuwa ameiweka kwenye meza.

“Haji; Huyu jamaa hatujawahi kufanya nae kazi, ila anaonekana yuko makini sana katika mambo yake Lakini pia hii tenda ya CIA itakuwa inafuta mashaka yetu kwake.” Alisema Zedi.

“ok!” alijibu kifupi Haji Makame.

“Afu keshokutwa anakuja Rais wa Kenya hapa Somalia; na kama ujuavyo hapa kuna hiki kikundi cha Al-Islamiya na kikundi cha Al-shabab na wote ni maadui wakubwa wa Kenya huoni kutakuwa kuna shida hivi” Alisema Zedi Wimba.

“Yawezekana kikosi chake cha skauti kimempa taarifa sahihi kuhusu usalama wake, tutege masikio tu” alisema Haji Makame.

Zedi alinyanyua mabega juu bila kutanabaisha liloko moyoni mwake.

“Serikali utatulaumu sana tusipomlinda Honda huko aliko” alikumbusha Haji.

“Sahihi, ila tutajitahidi turudi salama kwenye mpango huu na FLAMINGO apatikane” alisema Zedi.

“Hivi inaweza kuwa kweli Mohamed Farrah Aidid yupo hai kweli?” alihoji Haji.

“Majibu atakuja nayo Honda ila pia naamini yupo hai kwa sababu ya mateka wale wa ile vita kuwa hai hadi sasa” alijibu Zedi.

“Inawezekana pia” alijibu kifupi Haji na kuendelea kuchezea tarakilishi yake.

**

Sozi alimwongoza Honda kuingia ndani ya gari jingine ambalo kimwonekano halikustahili kuwa barabarani kisha Safari ikaanza kuelekea pembezoni kidogo mwa mji wa Mogadishu kwenye kitongoji kilichoitwa Atwa.

Baada ya mwendo wa saa moja na dakika kadhaa ,hatimae waliingia kwenye kitongoji cha Atwa.
Kwa harakaharaka Honda alitupia macho nje ya gari na kuona makazi ya watu yalivyosadifu umasikini wa hali ya juu na baadhi ya watu waliokuwa wamekaa nje ya nyumba zao walionekana kukata tamaa kabisa ya maisha,nguo chakavu na miili iliokondeana ilitangaza shida yao hadharani. Baadhi ya maeneo mengine yalikuwa yamebaki magofu ambayo kimsingi yalionekana kubomolewa na bomu ama kitu cha mlipuko mkubwa sana.

Safari iliendelea kimya kimya huku Honda akizidi kuona uharibifu mkubwa uliofanyika na hayo ni matokeo ya vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Wakiwa wanaingia kwenye kijiji fulani kilichochangamka; Honda alipata kuona tukio la kutisha sana.
Watu zaidi ya kumi walikuwa wamepangwa mstari huku wakiwa wamefungwa mikono na miguu na nyuma yao kulikuwa kuna vijana watatu waliokuwa wameshika mapanga na kisha wakaanza kuwacharanga watu wale bila huruma kabisa.

Hakika ilitisha.

“Kwanini wanafanya vile?” aliuliza Honda kwa mara ya kwanza.

“Watakuwa wamekataa kuchangia chakula na pesa na hiyo ni haki yao” alijibu Sozi huku akionekana kufurahia lile tukio na jibu alilompa Honda ama Ahmed Twalibu.

“Napenda sana kuua, ila kuua kwa upanga ni uoga” alisema Honda kwa lengo la kuteka hisia za Sozi alieonekana kupenda sana kuua kuliko hata kula.

“kwani wewe unauaje?” aliuliza Sozi huku akiwa makini sana kusikia jibu la Honda.

Honda aliguna kidogo.

“Nitakwambia siku nyingine. Kwani mkuu wenu ndie naenda kumuona au?” alijibu Honda kisha akatupia na swali.

“Aisee,hakuna kosa kubwa kama hilo,kuulizia mkuu alipo ama anaishije na yoyote anaekuja na swaga za kuumuliza huwa haishi aisee usirudie” alisema Sozi huku akionekana kukereka sana.

“ooh sawa” alijibu Honda na kukaa kimya.

*
Waliingia katikati ya kijiji cha Atwa. Huko karibia kila sehemu ilikuwa inatoa uvundo kwa mizoga iliokuwa imezagaa hovyo bila wakazi wa maeneo hayo kujali harufu hiyo, wao walionekana kuzoea mazingira ya eneo lile.

Safari yao ilienda kuishia katikatia ya jumba kubwa la kifahari lililokuwa kama limebeba hadhi dhaifu ya kijiji kile kilichokuwa kimezungukwa na umasikini wa hali ya juu na ilikuwa ni ajabu kukuta jumba zuri katikati ya mizoga ya watu.

Jumba lile lilikuwa linalindwa na vijana wadogowadogo wengi waliokuwa wamebeba silaha za moto zenye zaidi ya kilo tano.

Honda aliamliwa kushuka ndani ya gari kisha akaongozwa kuingizwa ndani ya jumba lile la kifahari ambalo lilikuwa lina wasichana wadogo wadogo waliokuwa wamevaa nusu uchi licha ya kuonekana kama ni wafanyakazi wa pale.

Sozi alienekana kuwa ni mwenyeji wa eneo lile alianza kuwachekea mabinti wale ambao walionekana kuchukia kuwapo mazingira yale.
Gafla Sozi alifanya kitendo cha ajabu kidogo.

Alimdaka binti mmoja kwa ustadi mkubwa na kumkandamiza ukutani kisha akaanza kumchojoa vinguo alivyokuwa amevaa na kuanza kumwingilia bila huruma.
Binti yule alionekana kutofurahia kabisa kitendo kile ila hakuwa na namna alitega tu na mkuyenge ukapita kunako tonkito.

Dakika tano baadae, Sozi alikuwa anachekelea tendo lile alilolifanya hadharani mbele ya macho ya mabinti wengine na Honda.

Baada ya unyama ule; Sozi alimuongoza kuingia katika chumba fulani ndani ya jengo lile, huko aliachwa peke yake aoge na kufanya usafi wa mwili wake vile anavyotaka.

Baada ya dakika kadhaa Honda alikuwa amemaliza kujiswafi na kuvaa nguo alizozikuta mle ndani kisha akatoka na kumkuta Sozi.

Sozi alimchukua tena na kuelekea chumba kingine na huko Honda hakuamini alichokiona.

Kulikuwa ni kama machinjioni jinsi kulivyokuwa kumejaa damu nyingi na vichwa kadhaa vya watu, lakini pia kulikuwa kuna mtu mmoja aliekuwa amefungwa kwenye kiti na pembeni yake kulikuwa kuna mtu aliekuwa ameshika kamera na kuilekeza kwa yule mtu aliekuwa amefungwa. Lakini pia kulikuwa kuna watu wengine wawili ambao walikuwa wamesimama na visu mikononi mwao na mmoja Kati yao alikuwa amevaa mavazi ya kijeshi na sura ya mtu yule ilikuwa ya kuogofya lakini licha ya sura hiyo lakini alikuwa anakichwa kidogo kilichokuwa kimechongoka mithili ya kichwa cha samaki Kamongo.

Sozi alionekana kumheshimu sana mtu yule mwenye kichwa kama Kamongo na alipofika alimpa maelezo kadhaa kisha akarudi kusimama karibu na Honda.

Mtu yule mwenye kichwa cha Kamongo akapiga hatua kumfuata Honda na alipomfikia akamwambia..

“Somalia ina vikundi vingi sana vinavyotaka kutawala ila sisi tunataka tusimike dola la kiislamu hapa Somalia na ukanda huu wa Africa ila hatutaweza bila kuwa na nguvu na nguvu tunaitangaza kwa kuwaua hawa wengie ili tusalie sisi” Kamongo alisema.
Honda alimtizama kwa dakika moja nzima kisha akamwambia.

“Kwa hiyo mkiua unatangazwa kama muislamu umeua au gaidi umeua?”

Kamongo alibabaika kujibu swali lile akabaki kumtazama tu.

“Kama mmenikomboa kwa wamarekani ili nije kufanya mauaji ya kidini, sitaweza kabisa na labda mniue tu, ila kama tunaua wanaofadhiliwa na Marekani na washirika wake waache kutuchonganisha waafrika, hakika nitakuwa mstari wa mbele kabisa kufanya ninachokijua” alisema Honda ama Ahmed Twalibu.

Kukapita ukimya kidogo.

“Kama mkuu wenu yupo mwambieni tubadilishe mlengo wetu na tusichafue dini ya Kiislamu kuonekana dini ya ugaidi, tupambanie haki ndani ya Somali bila kuweka udini katika masilahi yetu, tofauti na hapo sitaungana nanyi japo najua ndicho mlichonikombolea” alisisitiza Honda.

“Ok! Hayo hayatusaidii sasa ila kikubwa upo hapa kufanya kazi kadhaa na kikubwa ni kutangaza ujio wa Al-Itihaad Al-Islamiya; tulipotea miaka mingi sasa tumerejea na tunajiengua kutoka kwa Al-shabaab kwa kuua mmoja wa mpiganaji wake. Somalia ni yetu sasa” Kamongo alisema huku akimkabidhi jambia Honda na mtu alieshika kamera nae alianza kurekodi.

“Chinja huyo jamaa mana wao na Al-Qaida wanajua ni msaliti kwao hivyo waoneshe wewe sio msaliti na wamekukosea kukupa tuhuma hizo” alizidi kusema Kamongo.

Kamera iliendelea kurekodi na Honda akashika jambia huku rohoni akitetemeka. Hajawahi kuchinja mtu.

Dah!!
Honda kwenye majaribu tena.

Atachinja?

***


Nb: maoni kwangu mimi ni muhimu zaidi kuliko like mana maoni hunijenga zaidi kujua nilipokosea au kupatia na hivyo kunijenga zaidi katika kazi yangu.


Ahsanteni na karibuni kwa maoni
 
RIWAYA : URITHI WA GAIDI

NA; BAHATI MWAMBA

SIMU; 0758573660

SEHEMU YA TANO



Kamera iliendelea kurekodi na Honda akashika jambia huku rohoni akitetemeka. Hajawahi kuchinja mtu.

Dah!!
Honda kwenye majaribu tena.

Atachinja?

Honda alimsogelea yule mtu ambae alionekana yuko hoi kwa mateso aliopitia.

Kamera iliendelea kurekodi tukio lile.

Honda alishika vyema lile jambia kwa mkono wa kushoto, kisha akalipeleka shingoni kwa mtu yule na kwa kasi ya mkono wake wa kulia akapiga piga moja tata sana kwenye mfupa unaounga mifupa ya bega na shingo na ukasikikia mlio mmoja hatari kama kuvunjika kwa kijiti kikavu cha mti wa mninga.

Akatupa jambia pembeni na mtu yule akalegea na kujibwaga chini.

Hakuwa amechinja.

“Yeehaaa!” Sozi alishangilia kitendo kile cha pigo la kifo la Honda; kwake ilikuwa ni burudani tosha kwa mtu kuuwawa. Sozi alipenda kuua kuliko jambo lolote katika Dunia hii.
Kamera ilizimwa na Kamongo alimfuata Honda kwa gadhabu.

“Paka wewe! Kama isingekuwa amri ya mtawala ningekunyofoa kende keremanzi wewe.” Alifoka Kamongo baada ya kuona kitendo alichokifanya Honda sicho alichokitarajia.
Wote walitoka ndani ya chumba kile na kuelekea sebuleni mwa jumba lile kisha wakamuamuru Honda akae kwenye kiti kimojawapo mle ndani.

Kamongo aliekuwa amefinya sura kama kalambishwa kinyesi akamrukia Honda na kumkaba ukosi wa shati alilokuwa amevaa.

“We nguruwe, upo hapa leo tu ila unajifanya mkaidi eti, ndo umefanya nini pale” alifoka Kamongo huku akilamba midomo yake miembamba iliochongoka kama anakunywa supu ya moto.

Honda hakujibu!!..

“Huko tuendako nahisi tutaishia kuuana mimi na wewe bwege wewe” alikoroma tena Kamongo huku wengine wote wakiwa kimya bila kusema neno.

“Nimekombolewa nanyi ili nifokewe na wewe au kuonana na viongozi wenu waseme shida yao kwangu?” alisema kiutaratibu sana Honda.

Kamongo alitoa cheko la dharau kiasi.

“Boss ni invisible, haonekani, majukumu yako ni kutekeleza unaloambiwa na mimi ili kufidia garama zetu za kukukomboa bada ya hapo utafanya kilichokuleta hapa Ahmed” alisema Kamongo huku akitoa kipande kidogo cha karatasi kutoka mfukoni kwake na kukikunjua mezani..

Sozi na wenzie wakasogea karibu na meza ilipowekwa karatasi.

“Mipango yetu ni kuisafisha Somalia kisha tutawale jumla,na ili kufanikisha hili kuna mambo mawili inabidi yafanyike.” Kamongo akasema huku akiwatizama wenzie waliokuwa kimya wakati wote.

“Ni kukifarakanisha kikosi cha Al-Shabaab kisha tunamuua kisiki katika ukanda huu Rais wa Kenya” Alisema Kamongo huku akiitandaza karatasi kwenye meza.

“Hapa ni kijiji cha Sadaan na hapa leo usiku ama kesho kuna mzigo wa silaha unaingia kutoka kwa wafaransa na wanauleta kwa Al shabaab” alisema Kamongo huku akionesha kidole kwenye karatasi iliokuwa inaonesha ramani ya kijiji cha Sadaan kusini mashariki mwa Mogadishu na nusu kilomita kutoka pwani ya bahari.

Wote walitazama vyema ramani ile.

Tukifanikiwa kuzichukua silaha hizi kabla hawajajipanga itabidi tumuue kiongozi wao ili kudhoofisha nguvu yao” alisema tena Kamongo.

Akamtazama Honda.

“Osama alikuamini sana Ahmed na aliamini sana uwezo wako wa kupanga matukio na kuyatekeleza na ndio sababu upo hapa Ahmed.” Kamongo alisema na kumtupia jicho Honda ambae alikuwa kimya wakati wote.

“nadhani nafaa zaidi kusema na kiongozi wenu” alisema Honda.

Sozi akapiga ngumi nzito mezani na kuwafanya watu wote waangalie alipopiga.

“Chawa wewe! Nilishakwambia kumsema kiongozi ni sawa na kubeti ushuzi wa tembo kuwa unanuka kwa tani ngapi za harufu” alikoroma Sozi huku akiwa ameinamisha uso wake karibu kabisa na uso wa Honda ambae wakati huo wala hakuhangaika kufanya lolote.

“Ok! Tuachane na hayo, kikubwa tushirikiane kwa sasa kufanikisha hili jambo na dunia ijitayarishe kusafisha jina letu. Sisi sio magaidi” alisema Kamongo huku akivuta kiti na kukaa karibu na Honda.

**

Walitumia zaidi ya nusu saa kujadili namna ya kuingia katika kijiji cha Sadaan na kuzipora silaha za wafaransa wanazowauzia wapiganaji wa kikundi cha Al-shabaab.

Baada ya majadiliano yao, walielekea chumba maalumu kwa ajili ya chakula kisha wakaelekea sehemu nyingine kulikokuwa na chumba cha mateka.

Huko Honda alipata kuona wazungu wawili wakiwa miongoni mwa watu waliotekwa na kupewa mateso sana.

“Wale nguruwe mwitu walitumwa kufanya ushushu kuhusu kuibuka kwa kikundi chetu kilichopotea mwaka 2006. Bahati haikuwa kwao wapo hapa leo na kifo ndo kengele yao” alisema Kamongo huku akichukua kisu kutoka kwenye ala yake na kumsogelea mzungu mmoja na bila huruma alididimiza kisu shingoni mwa mzungu yule na kufanya damu ziruke kama mbuzi aliechingwa bahati mbaya huku akitoa mkoromo wa ajabu.

Hakika ilitisha hali ile mle chumbani.

Lakini Sozi alifurahia kwa kupiga mluzi mrefu huku akijilamba midomo yake kwa furaha ya kuona mauaji yale.

“Sasa kabla hatujaenda masikani, inabidi tupite kule Kole tukusanye chakula na madada poa kazi mbele yetu ni kubwa” Alisema Kamongo huku akimalizia kufuta damu zilizokuwa zimejaa kwenye kisu kwa kutumia nguo za yule mzungu mwingine aliebaki hai ambae wakati huo alikuwa anaomboleza kama aliefiwa na mke.

**

Nusu saa badae walikuwa kijiji cha Kole; huko walikutana na kundi lingine la wapiganaji ambao walionekana kumheshimu sana Kamongo.

Walipeana maagizo kadhaa na kuingia kusumbua wanakijiji ambao wakati huo wengi walikuwa wamejikunyata pembezoni mwa nyumba zao huku wakiwa hawajui hatima ya maisha yao.

Hekaheka zilianza, risasi zililirindima bila sababu maalumu lengo ni kuwavuruga wanakijiji wale ambao walikuwa wapo kinyonge katika himaya zao.

Mauaji yalifanyika mbele ya macho ya Honda huku mabinti wadogo wakibakwa hadharani na wapiganaji wale wa kikundi cha Al-Islamiya.

Sozi aliongoza vyema mauaji ya watu waliokuwa wanagoma kutoa chochote walichokuwanacho ama wale ambao hawakutaka kuona mabinti zao wakidhalilishwa hadharani.

Honda kuna kitu alihitaji kukifanya na katika heka heka zile akamdaka binti mmoja kama na kuelekea nae kwenye moja ya mabafu ya kienyeji.
Binti alipiga kelele za woga na hamaniko lakini Honda hakujali alizidi kutokomea nae kuelekea bafuni.

Alipokwisha kuingia nae kwa wepesi alimpiga yule binti kwa ubapa wa kiganja chake na kumpoteza fahamu.
Honda alianza kuchojoa nguo alizokuwa amevaa na kubaki mtupu kisha akamrarua yule binti nguo zake na kumwacha mtupu.
Lakini hakujihangaisha kumwingilia isipokuwa kwenye uume wake kulikuwa kuna kitu kama kata nyeusi ya raba ilikuwa imezunguka kuja usawa wa korodani,aliitoa kata ile iliokuwa imebana vyema shina la uume wake na alipoivua akaaangaza huku na huko bado alisikia makelele ya wanakijiji wakijaribu kuokoa nafsi zao.
Aliibinya pete ile mara mbili kisha akatulia.
Punde pete ile ikawaka mara mbili, hiyo ilimaanisha ujumbe umepokelewa akarudi kuivaa kama mwanzo kisha akaanza kuvaa nguo zake harakaharaka na kuanza kutoka ndani ya bafu ile.

Akasita!

Alisita baada ya kuona Sozi amesimama mlangoni mwa bafu lile akimtizama.

“Sijasikia ukifanya lolote komredi!” aliuliza kwa dhihaka bwana mdogo Sozi ambae alikuwa na kisu kilichotapakaa damu.

Honda aligwaya.

****

2: HUJUMA
JIJINI-DAR-

Akili ya Remi ilikuwa bado inazunguka kwa matukio alioyashuhudia tangu mwanzo mwa mkasa ule ambao hakujua ni nini hasa lengo lake.
Alimkumbuka bwana Kitambi.

“Hivi bwana yule anajiamini nini na ni nani hasa katika hii showtime?” alijiuliza Remi bila kuwa na wa kumpa majibu.

Sajini Vengu!!

Alimuwaza Sajini Vengu na akaona kuna haja ya kuelekea kituo cha Mwinjuma mwananyamala kuonana nae.

Kuna kitu alitaka kuweka sawa kuhusu jambo lile na alitaka kujua alipofikia Sajini kuhusu kutekwa kwa mwandishi Davis Minja na kuuwawa kwa mlinzi wa kampuni yake.

Bwana kitambi!

Nilipata kumuona wapi kabla ya leo? Alijihoji bila kupata majibu ya kutuliza ubongo wake.

**

Saa kumi jioni ilimkuta akiwa anaingia kwenye uwanja wa ccm mwinjuma kisha akashuka na kuelekea kilipo kituo kidogo kile.

Alikaribishwa kisha akasema shida yake.

Akaitwa Sajini Vengu ambae alikuwa chumba cha mahabusu na kazi nyingine.

“Sikutarajia kukuona hapa wakati huu japo nilitaka kukutafuta jioni hii” Alianza kwa kusema Sajini Vengu punde tu baada ya kumuona Remi.

“Nadhani tunapaswa kuzungumza kidogo!” Alisema Remi.

Wakaingia kwenye chumba kilichokuwa ni ofisi za kituo kile kidogo.

“Nakusikiliza Remi” alianzisha Mazungumzo Sajini.

“Nilitaka kujua tu umefikia wapi kuhusu kesi ile” Alisema Remi.

“Bado hakuna mwanga zaidi ya wewe kuonekana ni mhusika bado ambae kila sehemu upo” alianza kueleza Sajini.

“Kwanini?” alihoji Remi.

“Inaonekana mwandishi Davis Minja aliwasiliana na wewe jana na ujumbe wake ulikuwa ni wa kukupa taarifa kuhusu gari jeupe” Alisema Sajini.

Akaendelea..

“Katika ujumbe wake alisema anamtafuta jamaa hapatikani,sasa nikuulize jamaa gani alikuwa anatafutwa na Davis na kwanini akwambie wewe,na hilo gari lilitaka nini na kwa nini atekwe ofisini kwako?”

Yalikuwa ni maswali mfulululizo na yote yalikuwa yanaleta mana katika kadhia ile.

Remi akavuta pumzi nyingi na kuzishusha kwa mkupuo.

“Kwa hakika sijui alimlenga nani ila nahisi mume wangu mana ndie rafiki yake” alijibu Remi.

Umakini uliongezeka usoni mwa Sajini.

“Taarifa zinasema mumeo hajaonekana zaidi ya miaka miwili, sasa yeye alikuwaje akamtafuta na anajua kabisa mumeo hayupo?” aAlisema Sajini Vengu.

“Sijui kama hawakuwa na mawasiliano kati yao katika miaka hiyo miwili na…” Remi hakumalizia kauli yake Sajini akamkatisha.

“Remi; mumeo tumeambiwa ni gaidi na haonekani sasa iweje Davis aseme hapatikani, hivyo unajua mumeo alipo sio?” Alihoji Sajini Vengu.

“Sijasema aliulizia mume wangu, bali nimesema pengine ndie alimaanisha afande” alisema Remi.

“Watch yo step madame!!” Alitahadharisha Sajini.

Remi akagwaya!!

Baada ya mazungumzo ya dakika kadhaa, Remi aliaga na kuondoka huku akimwacha Sajini akiwa amepata jambo jipya kuhusu mume wa Remi.

Remi alipanda gari lake na lengo lake alitaka arudi tena kule ofisini kwake, alitaka kufanya jambo ambalo alijua anaweza kubahatisha kulipata!

“Walioyafanya pale ofisini sina hakika kama kweli hawajaacha kosa moja, Hakuna mkamilifu” alisema Remi huku akiipita hospital ya mwananyamala, alikuwa anaelekea Mwenge zilipo ofisi zake. Hakutaka kuendelea kuhujumiwa, alitaka kukokotoa hesabu katikati ya hujuma na mitego.

Kitu kimoja hakujua madhara ya kile alichotaka kwenda kukifanya na kama angejua basi bora angeacha tu aendelee kushuhudia showtime alioahidiwa na bwana kitambi…

Hakika hakujua madhara yake kwa alichokusudia.

**.


Toa maoni yako tafadhali
 
Mwendo huo huo Kudo no karudi nyuma na kudadeki zao hao waliokubania najua tu huko waliko wanaishuhudia show ya kibabe inaendelea kuleta utata

komando kinjekitile ngwale
 
Week end inaenda murua kabisa
RIWAYA: URITHI WA GAIDI.

NA; BAHATI MWAMBA.

SIMU: 0758573660

Vitabu vilivyopita.

• Kikosi cha pili
• Dakika za mwisho
• Mpango wa Congo
• Mbwa wa geti
• Operesheni jicho la paka
• Sauti ya mtutu



1:HISABATI


Jua lilikuwa linaelekea magharibi na kuelekea kuzamia kabisa ili kutowesha nuru ilioanza kufifia kabisa na kuliacha anga likiwa jeusi na kiza juu yake.

Ilipata saa kumi na mbili kasoro dakika kadhaa!!

Ilikuwa ni furaha kwa watu kadhaa kuukaribisha usiku huku wengi wakiwa njiani kurejea makwao kujumuika na familia zao baada ya kutoka kuhangaika kutwa nzima. Wengine pia walifurahi kwa kuwa muda huu wa usiku kwao ndio ulikuwa muda sahihi kuingia mtaani na kutafuta riziki yao hasa wezi na vibaka lakini pia makahaba.
Furaha ya giza ilikuwa ni njema zaidi kwa watu wenye baa na kumbi za miziki mana kwao giza ndio riziki yao ya halali bila wizi kwa mtu.


Jioni hii haikuwa njema sana kwa mwanadada mrembo aliepata kuwa na miaka thelathini na mbili hadi na nne hivi. Alikuwa ni mdada mwenye familia ya mume na mtoto mmoja aliepata kuwa na miaka kama mitano hadi sita hivi. Lakini pia alikuwa na mume na maisha yao hayakuwa na tabu yoyote. Familia ilijaa upendo na amani lakini pia kipato kwao hakikuwa na utata.

Milo mitatu kamili ilikuwa ni kawaida kwao.

Hakika ilipendeza!!

Lakini hayo yote sasa yalikuwa yametoweka kwa miaka miwili.
Hakuwa na furaha kama ile aliokuwa nayo mwanzo wakati anaingia kwenye mahusiano na mume wake.

Kwanini!

Kwa sababu alikuwa anaishi yeye peke yake na mwanae zaidi ya miaka miwili na miezi kadhaa huku mume wake akiwa ameondoka kwenda kwenye kazi maalumu Nchi za mbali.

Kazi gani, Hakuzijua na hakupaswa kujua.

Ilikuwa ni ahadi ya kurejea kwa miezi sita tu ila sasa ilikuwa ni miaka miwili bila mume wake kurejea na kila aliemuliza hakuwa na jibu la kumpa akaridhika.

Amekufa?

Hata!!

Haiwezi kuwa rahisi hivyo.

Alijakatalia.


Jioni hii ilimkuta mwanadada huyu mwenye urefu na uzuri wa asili akiwa ndani ya gari akitoka Mwenge kurejea nyumbani kwake Kinondoni akitokea ofisini kwake. Ofisi alioianzisha miaka kadhaa nyuma ikiwa inajishugulisha na utafiti wa mambo ya kale.

Yeye alisomea fani hiyo katika chuo kikuu cha Dar es laam.

Alikuwa ni Archeologist.

Mawazo mengi yalikizonga kichwa chake hasa suala la mume wake kutokuwa na mawasiliano nae zaidi ya miaka miwili na ushee.

Je upendo umeisha! Au huko alikoenda kakutana na mabinti wazuri kumliko basi akaamua kulowea kabisa huko?

Haiwezi kuwa!!

Alijikatalia tena.

Mawazo yake yalizidi kumuumiza kichwa chake na kupelekea jasho jepesi limtoke licha ya gari lake kujitahidi kumpa kiyoyozi bila upendeleo.

Foleni nayo ilizidi kumchosha.

Licha ya kuchoka na foleni lakini kwake aliona ni heri zaidi kuliko kurejea nyumbani na kukutana na nyumba tupu isio kuwa na uchangamfu wowote mana ilikuwa ni yake peke yake kwa sababu mume hakuwepo na mwanae wa kiume alikuwa anasoma shule za kulala huko huko hivyo kwake alikuwa ni yeye kama yeye tu.

Karaha ilioje!!.

Alisonya huku fukuto la jaziba na wivu vikimsonga hasa alipofikiria namna mume wake huko aliko anavyowabambia wanawake wa kizungu au kiafrika huku lugha yao ikiwa ni kizungu ama kihindi ama kiarabu ambazo zote mume wake alizimudu vyema kabisa.

Akasonya tena.

***

Ilikuwa ni majira ya saa mbili usiku ndipo alipoingia nyumbani kwake Kinondoni B.O.B ni baada ya kuwa amepita kwa Bonita saloon kuweka Sawa nywele zake ambazo hakuwa amezijali kwa siku kadhaa hivi.

Alipita kuzifunga tu na kuelekea nyumbani kwake.

Alishuka ndani ya gari na kufungua geti kisha akarudi na kuingiza gari ndani ya uzio wa nyumba yake ya kifahali ambayo sasa aliiona kama jehanamu ya nafsi yake.

Ilikuwa ni bora kukaa nje kuliko kurudi nyumbani kwenye nyumba pweke namna ile.

Akachukua makabrasha yake ya kiofisi na kupiga hatua kadhaa kuingia ndani kwake.

Akawasha taa na kujitupa kwenye sofa huku macho yake yakitua ukutani na kujenga kibanda.

Alibaki akiikodolea picha ya mume wake iliokuwa imetundikwa ukutani pale. Mume wake alikuwa ndani ya vazi la kiofisi huku mabegani mwake akiwa amejaa beji tatu zilizotambulisha cheo chake.

Mume wake alikuwa ni ofisa mkubwa wa jeshi la polisi.

Yeye hakuwa anakodolea vyeo vile bali alikuwa anatazama tabasamu adhimu la mume wake pale kwenye picha. Tabasamu ambalo ni nadra kuliona kwenye uso wa mumewe.
Alitazama kidevu cha mumewe kilichokuwa kimejaa ndevu zilizochongwa kwa mtindo wa Timberland.

Hakika alimkumbuka mumewe.

Pembeni ya picha ile pia kulikuwa kuna picha ya mwanae ambae nae kama baba yake alikuwa na tabasamu safi la kitoto huku akiwa ameegemea kwenye mikono imara ya baba yake.

Mwanadada alifumba macho kwa hisia kali. Kisha akanyanyuka na kuelekea maliwatoni, huko alitumia dakika kadhaa kujiswafi na kurejea sebuleni ambapo napo hakukaa sana akaelekea jikoni ambako hakufanya lililompeleka akabaki akiwa amejishika kiuno tu na kulikodolea jiko lake kama mtumishi aliesusiwa upishi.

Uvivu!!

Uvivu wa kupika chakula chake mwenyewe ndio uliomsumbua.

Hakuona umuhimu wa kupika akaamua kufungua jokofu. Humo ndani akakuta chakula cha kopo akakichukua na kukipasha kisha akarudi sebuleni na kukaa kukila huku akishushia na mvinyo mwekundu.

Dakika kadhaa badae uchovu na msongo wa mawazo vikampelekea aelekee chumbani kwake kulala huku akisahau kufunga milango.

Akalala fofofo!.

Ilikuwa yapata usiku wa saa saba kwenda saa nane hivi, mwanamke yule alipata kuhisi kitu ndani ya nyumba yake. Mwanzo alitaka kupuuzia kile alichokihisi akiwa katikati ya usingizi mnene,lakini hisia za kutambua zilizidi kumsumbua.

Akafumbua macho kisha akatulia na kusikilizia kile kilichofanya aamke.
Masikio yake yalinasa mchakacho wa miguu ya kiumbe hai ndani ya nyumba yake.
Haraka nae akaingiza mkono chini ya mto na kuibuka na bastola na kwa kuwa alikuwa amelala na nguo,hivyo hakupata tabu kuinuka na kunyata kuelekea sebuleni.

Hakusikia kitu tena.

Akafumba macho na kutuliza hisia zake.

Bado hakusikia kitu.

Akanyata hadi mlangoni kisha akachungulia sebuleni.

Ajabu!!

Alibutwaika kwa sekunde kadhaa hivi hasa baada ya kugundua aliacha taa zikiwaka kote mle ndani na sasa zinawaka chumbani pekee huku sebuleni kukiwa giza.

Akagwaya!

Mwili ukamsisimka na hofu ikamjaa!.

Mwanamke akatetereka.

Kutoka pale alipokuwa aliendelea kusubiri zaidi ili kumhadaa aliezima taa sebuleni lakini akajishitukia baada ya kukumbuka kuwa pale chumbani kulikuwa kuna mwanga na sebuleni kiza hivyo yeyote ambae angelikuwa amelikaa sebuleni basi alikuwa akimuona yeye ama kivuli chake.

Hata!!

Haraka na kwa wepesi akanesa kwa kutumia ncha za vidole vya miguu na kufikia kiongoza taa na kuzima taa ya chumbani. Wakati akirudi mlangoni, alisikia mlango wa sebuleni ukibamizwa kwa nguvu kumaanisha kuna mtu katoka muda huo.
Kwa wepesi uliokusudiwa, mwanadada yule nae akapiga hatua ndefu na kufika sebuleni kisha kwa kasi ile ile akaufikia mlango wa sebuleni na kuufungua.

Hola!!

Hakuona mtu wala kivuli cha mtu na geti lilikuwa vilevile limefungwa kumanisha hakuna mtu aliepita muda mfupi uliopita.
Mwanadada yule akaona ajaribu kuzunguka nyumba nzima pengine atafanikiwa kuona mtu aliekuwa sebuleni ila alizunguka bila kuona lau dalili ya mtu.
Alibaki akiwa anatazama mlango wa kuingilia ndani na geti kubwa la kuingilia pale ndani.

Akamakinika na kitu na kumbukumbu zilimrejea vyema.

Akasonya kwa gadhabu!!

Hakuwa amemkumbuka askari anaelinda usiku nyumbani kwa kiongozi wake na pia alikumbuka wakati anaingia hakumuona wala kuhisi uwepo wake.

Hatari kabisa!

“Yani najiwaza hadi nasahau mlinzi” alijisemea huku akipiga hatua kwa makini kuelekea kwenye kibanda cha mlinzi.

“Afande! Afande!” aliita mara mbili na aliitikiwa na sauti yake mwenyewe iliokuwa inajirudia kutokana na utulivu wa kifo uliokuwa nyumbani pale. Akazidi kuukaribia mlango wa kibanda cha mlinzi na alipokifikia akatulia na kusikiliza endapo kungekuwa na harakati zozote ndani ya kibanda.

Kimya!!

Hakuna alichokisikia zaidi ya pumzi zake mwenyewe.
Akausukuma taratibu mlango wa kibanda kile kisha akaingia kwa fujo kidogo.

Hakuna alichokikuta!!

Hakukuwa na mlinzi wala dalili za kuwapo mlinzi ndani ya eneo lile na hiyo ilimaaisha kuwa mlinzi hakuwa amefika pale siku hiyo.

Kwanini!!

Hilo hakujua na wala hakutaka kuamini kama limewekwa makusudi ama vipi.

Lakini alibaki na swali moja kichwani ya kuwa inawezekana vipi nyumba ya ofisa mkubwa jeshini tena special operation asahaulike kuletewa mlinzi.

Hata!! Ni ngumu hilo kufanyika. Lakini sasa mlinzi yuko wapi ikiwa haonekani pale ndani?

Mwanadada alipagawa.

Haraka alirudi ndani na moja kwa moja alielekea mezani kulikokuwa na rununu yake ya mkononi na kulitafuta jina la mtu aliemhitaji na kupiga.

“Ndio nakusikiliza!!” iliunguruma sauti ya mtu aliepokea simu upande wa pili ambae alionekana kutoka usingizini.

“Afande leo mlinzi aliandikishwa kufika hapa kwangu?” aliuliza mwanadada.

Ukimya ukapita kidogo.

“Kuna mambo yamebadilika kidogo na mimi sipo ofisini tangu juzi hivyo sijui kama kuna mtu aliekuwa amepangiwa hapo kwenu!!” alijibu mtu yule baada ya kukaa kimya kwa sekunde kadhaa.

Mwanadada akavuta pumzi za kushindwa kuelewa kinachoendelea.

“Kwani kuna tatizo?” alihoji mtu yule baada ya kusikia ukimya ukiwa umetawala kwenye simu.

“Kesho nitakutafuta tuzungumze Afande!” alisema mwanadada.

“Ni ngumu kesho kunipata mana nasafiri kwenda Ufaransa kwenye kikao cha wakuu wa idara za usalama wa jumuia ya madola nikimuwakilisha Mkuu wa jeshi la polisi nchini” alifafanua yule mtu.

“lakini nahisi kuna tatizo, kwanini mlinzi hajafika hapa nyumbani leo!?” aliuliza yule mwanadada .

Mtu wa upande wa pili akavuta pumzi nyingi na kuzishusha kisha akasema.

“siwezi jua pengine nikupe namba za mtu anaeshugulikia hayo kwa sasa na ambae amekaimu nafasi yangu hadi nikirejea” alisema yule bwana huku akianza kuzitaja namba hizo na alipomaliza alikata simu bila kungoja maelezo zaidi.

Suala lile likamchanganya kidogo mwanadada yule na kumuacha na maswali mengi bila majibu. Ilikuwa ni tabia mpya kuoneshwa na mtu yule tangu amfahamu na pia alikuwa ni rafiki wa karibu wa familia yake licha ya mtu yule kuwa ni kiongozi wa mumewe kikazi.

Akaguna tu na kuendelea kujishugulisha kuipiga namba aliopewa dakika chache zilizopita.

Simu ilianza kuita kwa fujo na punde ikapokelewa.

“Remi Haji; nakusikiliza”

Ebanaee! Maajabu.

Remi alitamani kukata simu dakika hiyo na kutafakari upya alilosikia. Mtu yule aliekaimu alikuwa anamjua jina lake kwa ufasaha kabisa!

Alimjuaje sasa na kwanini amjue ikiwa yeye si mfanyakazi wa idara yoyote ya jeshi la polisi?

Hakika ni maswali yaliomuacha kinywa wazi na alijikuta akikosa la kusema kwa dakika moja nzima.

“Heloo Remi!!” mtu yule aliita kwa madaha jina la Remi baada ya kuona ukimya umetawala.

“aah nimepewa namba na Kamishina wa jeshi la polisi Zenge wa Zenge.” Aliongea kwa kirefu Remi.

“elekea kwenye suala lililokufanya upige simu tafadhali ninahitaji kupumzika!” mtu yule aliekaimu nafasi ya Zenge wa Zenge alisema kwa utulivu wa majivuno.

“Hapa kwangu hadi sasa sijaona mlinzi akifika wala kuripoti nilitaka kujua nini tatizo tafadhali” aliuliza Remi.

“Kabla ya kunipigia mimi usiku huu ulipaswa kuwapigia maafisa wanaoshugulika na malindo ya wakuu wao, mimi ni mtu mkubwa sana kuulizwa malindo usiku wa manani namna hii” aling’aka bwana yule.

“Nina sababu afande za kukutafuta wewe na…” alikatishwa kusema Remi.

“Hiyo sababu ilikuwa zamani ila sio sasa. Kwa sasa utaratibu unafuatwa kuanzia ngazi za chini binti” alisema yule bwana kwa ujivuni.

Remi alibaki akiwa amezubaa kwa fadhaa na simu sikioni.

Hakupata kuona mambo haya hapo kabla.

“Naomba kesho ufike ofisini kwangu nina ujumbe” alisema bwana yule na kukata simu.

Remi alibaki akiwa hana hamu na majibu ya ujivuni ya kamishina yule wa jeshi la polisi nchini.

Akaitoa simu sikioni na kulitafuta tena jina la Zenge wa Zenge ili apige lakini alikutana na jibu lililozidi kumuacha wazi kichwani.

Hakuwa akipatikana!

Haijawahi kutokea akazima simu tangu wafahamiane miaka kadhaa nyuma wakati akiwa katika misukosuko ya Ukimbizi ndani ya nchi ya Tanzania kisa ambacho kiliandikwa vyema na mwandishi wa riwaya Bwana Bahati Mwamba.

Sasa baada ya muda wote huo eti Kamishina anazima simu.

Kuna namna si bure.

****

Remi Haji Makame; usingizi ulimpaa na hapo akakumbuka kitu baada ya kushindwa kumtafakari vvyema Zenge wa Zenge.

Ujumbe!!

Alikumbuka mchana aliona ujumbe kutoka kwa mwandishi ambae pia aligeuka kuwa rafiki wa familia hasa baada ya kuwa anaandika mikasa mingi inayomhusu mume wake. Aliupokea ujumbe wa Davis Minja ila hakushugulika nao wakati ule.

Aliufungua!

“Siku ya sita sasa kuna gari silielewi nyuma yangu mumeo sikumpata!” ujumbe ulisomeka hivyo.

Sasa hii tena inakuwaje! Alijiuliza Remi na uso wake ulielekea juu ya ukutani na kuitazama saa.
Mishale iliendelea kuwa mashariki kumaanisha ni usiku wa maanani.
Alizima taa na kuacha usiku upite akiwa amekaa sebuleni kuongojea kuona kama mtu aliemtembelea usiku ule atarejea ili amjibu kwa nini alimtembelea kinyamela na alifuata nini.

Lakini kitu kimoja hakujua ni kuwa hesabu zake zilikuwa nyuma ya hesabu za mtu aliemvizia usiku na kumwacha bila kumduhuru.

Mtu yule hakurejea tena hadi mapambazuko.

Na yakawa ni mapambazuko ya Kihisabati; hesabu za akili.

****

Ahsubuhi ilimkuta Remi akiwa amelala kwenye sofa na bastola yake mkononi. Milio ya ndege waliokuwa juu ya miti ndio waliomsitua kutoka kwenye tope la usingizi wa mang’amung’amu.

Alijisonya bila sababu na kuelekea chumbani kwake ambapo moja kwa moja alielekea maliwatoni na kutumia dakika kumi na ushee kujiswafi kisha akarejea chumbani kwake ambapo hakumaliza muda murefu akawa tayari amekwisha kujiweka sawa na kuvaa suruali ya buluu mpauko na T-shirt nyeusi kisha akachukua mkoba wake wenye nyaraka za kiofisi na kuweka bastola yake kisha akaelekea sebuleni ambako alichukua funguo za gari na kutoka nje ambako alichukua gari lake jeusi aina ya Toyota Nadia na kisha akajifungulia geti na kutoka nje na alipokwisha kutoka akarudi tena kwa miguu na kulifunga kisha akaondoka kwa mwendo wa wastani tu.

Hakufika mbali kwa kupitia vioo vya gari ama side mirror akaona jambo.

Kutoka kwenye kona moja ya nyumba yake aliona mtu alievaa kofia akichepuka na kuivuka barabara kwa kasi na kupotelea kwenye nyumba za watu mtaani pale.

Akili yake ilimwambia mtu yule hakupita eneo lile kwa bahati mbaya au labda ni mkazi wa eneo lile.
Hakika akili yake ilikataa kukubaliana na hilo.

Alikuwa pale anafanya nini na kwanini akimbie kwa kujificha namna ile? Au ndie aliemtembelea usiku na…
Alibaki kutikisa kichwa tu bila kujua kama kuna kusudi baya juu yake ama ni akili yake tu.

Kamwe hakujua mana ya matukio yote yale yalioanza kumwandama siku kadhaa nyuma.

Aliendesha gari lake huku kila mara akitizama nyuma kuona kama kuna jambo lolote lisilo la kawaida.

Hakuona!!

Safari yake ilimfikisha hadi makao makuu ya jeshi la polisi na alipokwisha kufika akapaki gari lake eneo maalumu kisha akaomba kuonana Naibu kamishina. Alioneshwa zilipo ofisi zake.

Hatua zake zilimfikisha hadi kwenye korido pana iliokuwa na ofisi nyingi kushoto na kulia. Akasoma namba za ofisi zile na vitengo vyake hadi pale macho yake yaliponasa jina la ofisi alioihitaji. Ilikuwa ni ofisi ya kitengo maalumu yani special operesheni.
Akagonga mlangoni na kukaribishwa kuingia.

Alikaribishwa na uturi ghali ulionyanyasa pua zake kwa harufu kali. Lakini macho yake hayakuhadaika na na harufu za pua bali yalimakinika kumtazama mtu aliekuwa amekaa kwenye kiti nyuma ya meza na kibao kikiwa mbele yake kilichonasibisha jina lake.

Bwana yule aliitwa P. Kagoshima ambae ndie alikuwa Naibu kamishina wa jeshi la polisi kazi maalumu aliekaimu nafasi ya Kamishina Zenge wa Zenge. Bwana yule hakuonekana kuwa na umri wa kutisha ila umri wake aliukadiria kuwa kati ya miaka arobaini na nne hadi hamsini kasoro. Alikuwa ni mrefu wa wastani ila hakufikia urefu wa Mumewe ama Kamishina Zenge wa Zenge. Sura yake ilionesha ni mtu mjivuni sana lakini mbali na hayo Remi aliona kitu ndani ya macho ya yule bwana. Remi aliona tamaa ya kifisi imejaa kwenye mboni za macho ya Kagoshima ila hakujua ni tamaa ya nini, Pesa ama kitu kingine zaidi ila ilitosha tu kujua yule bwana ni mwenye ujivuni na tamaa.

“Naitwa Remi” alijitambulisha Remi.

“Ooh karibu bibie!” alisema Naibu kamishina Kagoshima huku akiachia tabasamu la upande na kuegemea kiti kilichopokea mwili wake wa kikakamavu.

“Nimeitikia wito Afande!!” alisema Remi huku akitizama saa yake ili kuhakikisha yupo ndani ya muda na sikuchelewa pale ofisini.

“OK! Bila shaka mumeo ni ofisa wa jeshi la polisi!” alihoji Kagoshima huku akijishugulisha kupekua makablasha kadhaa yaliokuwa mezani kwake.

Remi hakumjibu.

Kagoshima aliendelea..

“Na ndie Haji Makame!”

“Afande nadhani yote hayo unayajua na unapaswa kujikita kwenye mada tafadhali” alisema Remi kwa kukereka kidogo.

N. Kamishina alitabasamu kivivu huku akichukua kipande cha gazeti na kukitupia karibu na mikono ya Remi ambae alikuwa amekaa na kuweka mikono yake juu ya meza.

Remi alikichukua kipande kile ambacho kilikuwa ni cha ukurasa wa mbele wa gazeti la Daily News la Marekani. Remi alishuhudia picha mbili kubwa na picha moja ndogo. Picha ndogo ilikuwa ni ya mtu mgeni machoni pake na picha moja kubwa nayo hakuifahamu kabisa lakini picha nyingine ilikuwa ni picha ya mumewe Haji Makame licha ya kuwa na mabadiliko makubwa katika uso wake,lakini kamwe hakuwahi kumsahau mwanaume wa maisha yake.

Akasoma kichwa cha habari cha kipande kile cha gazeti ambacho kilikuwa kimeandikwa kingereza.

Mwili ukamwingia ubaridi kwa alichokielewa. Alimtizama Kagoshima; na alikutana na uso makini ukimtizama kisha akarejesha macho yake kwenye kipande kile.

Tafsiri Kiswahili.

“Tanzania yazidi kuzalisha magaidi, Wawili wasakwa na marekani na mmoja atoweka Guantanamo”

Yalikuwa ni maelezo machache lakini yenye kuchoma akili za watu.

“Sijaelewa Afande!” alisema Remi huku dhahiri akionekana kupagawa.
Naibu Kamishina P. Kagoshima alisogeza kiti huku akiguna kusafisha koo lake na mkono wake wa kushoto akikichukua kipande kile cha gazeti kutoka mikononi mwa Remi.

“Huyu anaitwa Ahmed Twalibu” alisema huku akinyooshea picha ndogo ya jamaa mweusi alieonekana kukomaa sura yake licha ya uso wake kuonesha umaridadi wake vyema.

“Na huyu anaitwa Aahmed Boka Ghailani” alionyeshea picha kubwa ya mwanaume ambae nae hakutofautiana sana na yule aliekuwa kwenye picha ndogo licha ya kuwa walionekana kuwa ni wanaume wawili tofauti.

“Na huyu ni Haji Makame” alisema tena huku akielekeza kidole kwenye picha ya mwanaume aliekuwa amenyoa upara na kuchonga ndevu zake kwa mtindo wa Timberland. Licha ya kunyoa ambayo si tabia alioizoea Remi; lakini ndevu zilimhakikishia yule ni mumewe kipenzi Haji Makame.

Gaidi!!

Ameanza lini ugaidi hadi kutafutwa na serikali ya Marekani!? Na kwanini ahusishwe na Ahmed Twalibu ambae siku za nyuma aliaminika ameuwawa kwenye shambulizi lililotekelezwa na Wataleban walishambulia chopa aliokuwamo?

Na vipi alipona na kuhusishwa tena na ugaidi sambamba na mumewe!?

Ebanae!!

Yalikuwa ni maswali bila majibu na hesabu ziligoma kuunganisha kachumbari ile kichwani mwa Remi ambae siku zote alijua mumewe ni mstari wa mbele kupigania masilahi ya taifa kwa kupambana na ugaidi ama uvunjaji wa sheria wa aina yoyote!

Hata haiwezekani.
Remi alijakatalia kata kata.

“eeh! Hapa kuna watu wawili wanafanana majina kwa kutamkwa ila herufi tofauti yani Ahmed na Aahmed .” Alisema tena Kagoshima huku akitoa picha nyingine kubwa kidogo ambayo nayo aliitupia kwenye meza na kuchukuliwa na Remi.

Picha ile ilifanana sawa sawa na picha ndogo ya mtu alieitwa Ahmed Twalibu aliesemekana kutoroka Guantanamo na sasa anatafutwa na serikali ya Marekani.

Remi alimtizama Kagoshima kwa macho ya kuuliza.

“Ok. Huyo bwana anaedaiwa kuitwa Ahmed Reality ambae unaona picha yake hapo,tumefuatilia na kugundua sio Ahmed Reality ila ni amewahi kuwa askari wa jeshi la polisi kitengo maalumu kama mumeo anaitwa Honda Makubi. Swali tunalojiuliza ni kwanini Marekani iseme ilikuwa nae gerezani kwake na ametoroka wakati miaka miwili nyuma alikuwa anahudumu hapa nchini? Lakini pia Ahmed wa kweli anaweza kuwa miongoni mwa hawa watatu yani huyu Aahmed Ghailani; Haji Makame ama Honda Makubi na hapa anaetafutwa sana ni Ahmed Twalibu ambae nasadiki ndie huyu Aahmed” alisema Naibu kamishina Kagoshima.

Remi alibaki akimtizama akiwa hajui ni kwanini anahusishwa katika jambo lile tena kwa kuelezwa kwa marefu na mapana na kiongozi mkubwa wa jeshi la polisi nchini.

“Kwanini unanambia yote haya na mimi nahusikaje na hili sakata!” alivunja ukimya Remi.

Kagoshima aliegemea kiti chake kisha akamtazama Remi kwa tuo huku akiwa amefumbata mikono yake pamoja.

“una hakika huhusiki?” aliuliza Kagoshima.

Jama!!

Remi alibutwaika kwa kauli ile ya ofisa yule wa jeshi la polisi.

“Nahusika vipi na mambo haya ambayo ni kama hadithi za kufikirika?” alihoji Remi.

“Inaonesha mumeo anashirikiana na magaidi muda mrefu kidogo na wewe yaezekana unajua hiko kitu na ndio mana unahusika katika sakata hili mwanamke!” alisema Kagoshima huku akilambalamba midomo yake kama wafanyavyo wasanii njaa wahojiwapo na vituo vya runinga.

“Huko ni kumkosea mume wangu kabisa na kamwe hajawahi kuwa gaidi. Yani mazuri yote alioyafanya leo mnamwita gaidi?” alisema Remi huku akivuruga nywele zake kichwani kwa mikono yake.
Alihisi kichwa kinawasha kwa taarifa zile.

“Kwanza nataka nikwambie mumeo hajawahi kuwa ofisa wa jeshi la polisi na hata katika rekodi zetu hayumo,hivyo inamaanisha hajawahi kuwa ofisa kabisa na hatumtambui Haji Makame na cheo chake na tunamhesabu kama mhujumu nchi tu aliejichomeka jeshini kutimiza matakwa yake ya kigaidi” Jibu la moto kwa Remi Makame.

“Hajawahi!? Inamaana, dah..” alishindwa kuelewa aseme nini katika dakika ile Remi. Alibaki akiwa ameachama mdomo akiwa hajui ama alie ama acheke ama tabasamu, mana hakuona kama kuna utani katika uso wa Kagoshima ambae ni ofisa mkubwa tu wa jeshi la polisi.

Sasa alielewa ni kwanini hakukuta mlinzi usiku wa jana nyumbani kwake.

“Mengine inabidi utuachie kama serikali tuyashugulikie ila kwa sasa taarifa hii inaweza kukuweka pabaya ama pazuri mrembo” alisema Kagoshima huku akikenua meno kama ngiri maji.

Haaa!!
Urembo tena unaingiaje katika sakata hili!

Remi alisimama kisha akauliza.

“kwanini inaweza niweka pabaya ama pazuri?”

“ukimficha mumeo na washirika wake itakuweka pabaya ila ukitoa taarifa utakuwa pazuri” alisema Kagoshima huku akitoa kadi mfukoni mwake na kumpa Remi.

“Ukiwa na shida utanipigia nami nitakusaidia muda wowote” alisema huku akiona Remi anaitazama ile kadi.

“sina hakika kama itafikia hatua ya kukuomba msaada” alisema Remi huku akiisunda kadi ile mkobani mwake.

“unahakika hutauhitaji msaada wangu?” alihoji Naibu Kamishina huku akitabasamu. Remi alimtizama bila kumjibu na kuondoka ofisini mule huku kichwa kikimuwaka moto kwa taarifa zile.

Hakika alichanganyikiwa.

Dakika kadhaa badae alikuwa ndani ya gari lake na lengo lilikuwa ni kuelekea Mwenge zilipo ofisi zake za utafiti wa mambo ya kale.

Tatizo hakujua huko nako ni moto mwingine utakao acha akili yake ikiwaka. Ila hakujua na angejua hakika angejirudia kwake tu akalale.

***

Nb; toa maoni yako kuhusu riwaya hii. Usiache kutupia maoni yako ambayo ni muhimu
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom