Risala ya Chama cha Walimu Tanzania iliyosomwa kwa rais Magufuli na Katibu Mkuu Mwl. Deus G. Seif - JUNI 05, 2020

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,801
11,961
RISALA YA CHAMA CHA WALIMU TANZANIA KWA MGENI RASMI MH. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU - JUNI 05, 2020 KATIKA UWANJA WA CCM JAMHURI JIJINI DODOMA



Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mheshimiwa Majaliwa Kasim Majaliwa (MB), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Job Y. Ndugai (MB), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Dkt . Bashir A. Kakulwa, Katibu Mkuu wa CCM Taifa,

Mheshimiwa Jenister Mhagama (MB), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu

Mheshimiwa George H. Mkuchika (MB), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,

Mheshimiwa Seleman Jafo (MB), Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),

Mheshimiwa Joyce Ndalichako (MB), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,

Mheshimiwa Anthony P. Mavunde (MB), Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu,

Waheshimiwa Wabunge,

Komred rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA),

Komred Mwl. Leah Ulaya, rais wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT),

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama,

Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma,

Mheshimiwa Dr. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,

Komredi Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA),

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,

Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Kamishna wa Kazi,

Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi Tanzania,

Katibu Mtendaji Tume ya Utumishi wa Walimu,

Waheshimiwa Viongozi wa Serikali mliohudhuria katika Mkutano huu,

Makomredi Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi mliohudhuria kutoka ndani na nje ya Tanzania,

Makomredi Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama cha Walimu Tanzania,

Waandishi wa Habari,


Mabibi na Mabwana.


Itifaki imezingatiwa.



Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Awali ya yote tunapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema pamoja na hali iliyopo ya “CORONA” na hivyo kutuwezesha kuhudhuria Mkutano Mkuu huu.

Aidha tunatumia fursa hii ya kipekee kukushukuru wewe binafsi kwa kukubali mwaliko wetu na kuweza kujumuika na walimu katika ufunguzi wa Mkutano huu Mkuu wa kipindi cha miaka mitano licha ya kuwa na shughuli nyingi za Kitaifa. Aidha, tunawakaribisha na kuwashukuru wote kwa kukubali kuja kushiriki nasi katika Mkutano huu.

Kadhalika, tunaomba kuitumia fursa hii ya kipekee kuishukuru Serikali yako kwa ushirikiano wa hali ya juu ambao inatupa kwa kuturuhusu kufanya Mkutano huu muhimu kwa mustakabali wa Chama.

Mheshimiwa Rais,

Mkutano huu una wajumbe 1138 kutoka Mikoa 26 na Wilaya 151 za Tanzania Bara. Mkutano huu ni kwa ajili uchaguzi wa viongozi wa kitaifa, baada ya kumalizika kwa chaguzi za ngazi za Wilaya na Mikoa ambao wataongoza chama hiki kwa miaka mitano ijayo (2020-2025).

Viongozi wa Chama cha walimu Tanzania (CWT), ambao wanategemewa kuchaguliwa ni katika nafasi za rais wa Chama, makamu wa rais, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mweka Hazina, Mwakilishi wa walimu Wanawake Taifa, mwakilishi wa walimu wenye ulemavu kitaifa, Mwakilishi wa walimu vijana Taifa, mwakilishi kwenye Shirikisho la vyama vya wafanyakazi- TUCTA na wadhamini wa Chama

Mheshimiwa Rais,

Chama Cha Walimu Tanzania kinatambua jitihada kubwa zinazofanywa na serikali unayoiongoza katika kuboresha maisha ya Watanzania wakiwemo walimu. Miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), mradi mkubwa wa umeme (Nyerere), ongezeko la Hospitali za Wilaya na vituo vya Afya, miradi ya maji na miundo mbinu ya barabara, hivi vyote vinalenga kuhakikisha Maisha ya Watanzania yanakuwa bora. Tunakupongeza sana wewe na Serikali ya Awamu ya Tano unayoiongoza.

Kwa upande wa sekta ya Elimu, yapo mambo kadhaa ambayo Serikali imeyafanya kwa kipindi hiki cha muda wa miaka mitano ikiwemo:-

Ongezeko la miundo mbinu na Samani

Mheshimiwa Rais,
tunatoa pongezi kubwa kwako kwa kuhakikisha miundo mbinu na samani vinapatikana katika mazingira ya kujifunza na kufundishia kwa walimu na wanafunzi. Kufuatia wewe mwenyewe kuasisi mpango wa Elimu bila malipo, kumekuwepo na ongezeko wa wanafunzi nchini.

Upandishwaji wa madaraja na urekebishwaji wa mishahara kwa walimu

Mheshimiwa Rais,
tunaomba kutumia fursa hii kukupongeza na kukushukuru kwa kuruhusu zoezi hili la upandishaji vyeo na urekebishaji wa mishahara kwa walimu na watumishi wengine, zoezi ambalo lilikuwa limekwama kwa kipindi kirefu tangu mwaka 2014, tunasema asante sana.

Mheshimiwa Rais,
hadi kufikia tarehe 31 Januari mwaka 2020, Serikali unayoiongoza ilikuwa imewapandisha vyeo na kuwabadilishia mishahara walimu wapatao 121,534 kati ya walimu wote wa umma nchini wapatao 267,272. Tunaamini kuwa kupandishwa daraja (cheo) ni zaidi ya nyongeza ya mshahara kwa watumishi hawa. Tunashukuru sana.

Malimbikizo ya madeni yasiyo ya mishahara

Mheshimiwa Rais
, hadi kufikia mwezi Disemba mwaka 2019 Serikali unayoiongoza ilikuwa imeshalipa kiasi cha Sh 12,045,626,728.61, aidha tunaamini Serikali inaendelea kulipa kiasi kilichobakia kadri uhakiki utakavyokamilika, ili kuondoa malimbukizo ya madeni yasiyo ya mishahara. Tunayo matumaini makubwa kuwa Serikali yako itakamlisha malipo haya.

Malimbikizo ya madeni ya Mishahara

Mheshimiwa Rais,
Hadi Disemba 2019, walimu wapatao 16,969 waliokuwa wanaidai Serikali madeni ya mishahara kiasi cha 19,185,231,163.08 walikuwa wamehakikiwa na kulipwa. Tunaipongeza Serikali kwa kuwalipa walimu hao. Mpaka mwishoni mwa Januari 2020, walimu wapatao 6,781 walikuwa hawajalipwa na madai yanaendelea kuhakikiwa kwa ajili ya malipo. Tunaamini Serikali itaendelea kuwalipa walimu kama ilivyo dhamira yake ya siku zote na kadri bajeti ya Seikali itakavyoruhusu.

CHANGAMOTO

Mheshimiwa Rais,
pamoja na mafanikio mengi katika maeneo haya ambayo tumeyataja, tunaomba kutumia fursa hii kueleza baadhi ya changamoto ambazo tunaomba ziendelee kufanyiwa kazi kwa nguvu zaidi ili kuleta tija kwa walimu na hivyo kuwaongezea ari ya kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi;

Mheshimiwa Rais,

Upandishwaji wa vyeo kwa walimu walioajiriwa na kupandishwa vyeo mwaka 2014/2015


Kundi la walimu walioajiriwa mwaka 2013/2014 na waliopandishwa vyeo 2013/2014, tunaomba makundi hayo yapandishwe vyeo kwa mwaka huu wa fedha 2020/2021 ili makundi haya yasiwe na mwachano baina yao.

b) Ajira kwa walimu

Mheshimiwa Rais,
mwitikio mkubwa wa jamii kufuatia mpango wa Elimu bila malipo umezifanya shule nyingi kuwa na uhitaji wa walimu, hivyo tunaomba hali ikiruhusu Serikali itoe ajira kwa walimu nchini.

c) Uhaba wa nyumba za walimu

Mheshimiwa Rais,
tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano unayoiongoza wewe mwenyewe kwa jitihada kubwa za kuhakikisha miundo mbinu kwa sekta ya elimu inaimarika. Aidha, tunaleta ombi la kuwasaidia walimu, ili uone namna ya kuongeza nyumba za walimu ili wakae karibu na shule waweze kufanya kazi zao vizuri.

Hitimisho

Mheshimiwa Rais,
toka tulipokutana mara ya mwisho mwaka 2017 kuna mambo mengi yamefanyika kuhusiana na Benki yetu “Mwalimu Commercial Bank Plc”. Kwa upande wa uongozi tunawakilishwa na walimu wanne katika bodi ya wakurugenzi, na kwa upande wa mikopo zaidi ya 90 % imetolewa kwa walimu wakati 5.3% imetolewa kwa wafanyakazi wengine wa Serikali.

Vilevile Chama Cha Walimu kimeshirikiana na benki pamoja na PSSSF kuweka utaratibu wa walimu wastaafu kupokelea mafao kupitia benki yao, vilevile Chama Cha Walimu na Benki wamefikia muafaka kufungua tawi jijini Dodoma kabla ya mwisho wa mwaka huu. Benki yetu imeendelea na jitihada za kutumia teknolojia ya mifumo ya kidigitali kuwafikia walimu wengi katika mikoa yote.

Mheshimiwa Rais, tutakuwa wachoyo wa fadhila kama hatutashukuru kwa tamko lako lenye kutia moyo ambapo uliwambia watumishi nchini wakiwemo walimu kuwa utaendelea kuwalipa mishahara hata kama watakuwa nyumbani kutokana na janga hili la Ugonjwa wa CORONA. Bila kumung’unya maneno, niwaombe walimu tumshangilie sana Rais wetu.

Mheshimiwa Rais,

Kwa namna ya kipekee kabisa, tunatoa shukurani zetu za dhati kwa Mheshimiwa Dr. Benilith Mahenge Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, viongozi wa Serikali, Vyama vya wafanyakazi na Taasisi zingine mbalimbali kwa jinsi walivyoshirikiana na sisi wakati wa maandalizi ya Mkutano wetu.

Mheshimiwa Rais,

Mwisho, tunatoa shukrani zetu za dhati kwa jinsi ambavyo serikali yako kupitia Wizara ya Afya inavyopambana kuhakikisha wananchi wanajikinga na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona huku wakiendelea kuchapa kazi. Umewatoa hofu watanzania kuhusu ugonjwa huu kwa kuwa hofu ni ugonjwa mbaya kuliko ugonjwa wenyewe. Watanzania wamekuelewa ndiyo maana kasi ya maambukizi inapungua kila kukicha. CWT itaendelea kushirikiana na Seikali katika kutekeleza maagizo yake katika kudhibiti ugonjwa huu. Aidha, Chama cha walimu Tanzania tunaahidi uchaguzi utakuwa wa wazi na huru.

Baada ya kusema hayo Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kwa mara nyingine tena tunakushukuru kwa kutenga muda wako kuja kushiriki nasi katika Mkutano huu Mkuu na tunakutakia afya njema na baraka tele katika kutekeleza majukumu adhimu ya kitaifa huku ukiendelea kuwakumbuka walimu wenzako wa Taifa hili. Tunaamini utatuacha vizuri!

Mungu akubariki sana na akujalie afya njema wewe na familia yako.


MSHIKAMANO DAIMA!

Nawasilisha,

Mwl. Deus G. Seif

KATIBU MKUU CHAMA CHA WALIMU TANZANIA
 
Contents na utambulisho karibu zinalingana.

Hivi ni lazima kuwataja woooote hao. Ni upotevu wa muda tu.
 
Back
Top Bottom