Elections 2010 Ripoti Ya Mjadala Wa Kuadhimisha Miaka 47 Ya Muungano Wa Tanganyika Na Zanzibar

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,809
Ripoti Ya Mjadala Wa Kuadhimisha Miaka 47 Ya Muungano Wa Tanganyika Na Zanzibar
(Froud Community Centre – Uk)



(Umetayarishwa na Jumuiya ya Zanzibar Welfare Association –ZAWA)

23 April, 2011

1.0 UTANGULIZI:

Mjadala huu ulifanyika katika ukumbi wa Froud Community Centre uliopo Manor Park, London na ulifunguliwa rasmi saa 11.30 asubuhi chini ya Mwenyekiti Bw. Ahmed Seif. Baada ya kufungua mjadala, Mwenyekiti wa mjadala alichukua fursa ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Jumuiya ya ZAWA kwa ajili ya kutoa maelezo mafupi kuhusu Jumuiya ya ZAWA na pia kuwashukuru Washiriki wote waliohudhuria.

Mwenyekiti wa ZAWA aliwaeleza washiriki kuwa Jumuiya ya ZAWA imeasisiwa zamani na kina Marehemu Abdulrahman Babu na Wa-Zanzibari wengine waliopo Uingereza. Pia, Mwenyekiti aliwakaribisha washiriki wote na kuwaomba wajisikie huru katika kuchangia bila ya khofu na pia kuheshimu mawazo ya kila mshiriki.

2.0 MADHUMUNI YA KONGAMANO:

Madhumuni ya mjadala huo yalikuwa ni kujadili faida na hasara zilizopatikana katika kipindi cha miaka 47 ya Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na baadae kutoa mapendekezo ya nini kifanyike siku za baadae.

3.0 MADA YA KWANZA:

Mada ya kwanza ilitolewa na Maalim Abdalla Ali na ilizungumzia juu ya maadhimisho ya kusherehekea sherehe za kutimiza miaka 47 ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Katika Waraka huo, ilielezwa kuwa kwa muda mrefu sana kumekuwa na dhana kuwa wale wanaonekana maadui wa Muungano wakati ukweli halisi ni kuwa watetezi wakuu wa Muungano huo.

Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, nchi ilikuwa haina jeshi la kuweza kuilinda nchi ndipo Sheikh Karume alihofia kupinduliwa na kwa haraka nchi za Magharibi zilitumia ufa huo kwa kumtumilia Mwalimu Nyerere kumpelekea jeshi kwa ajili ya kumpa himaya ili asipinduliwe na wakati huo huo walimshawishi Nyerere kutumia uwezo wake kumshawishi Sheikh Karume ili waunganishe Zanzibar na Tanganyika.

Baada ya muda si mrefu kupita, na hasa ilivyokuwa Chama cha Afro Shirazi (ASP) kilikuwa kikifadhiliwa na Chama cha TANU ambacho kilikuwa Tanganyika, Mwalimu Nyerere alifanikiwa kumshawishi Sheikh Karume kuunganisha nchi bila ya ridhaa ya Wananchi wa Tanganyika na Zanzibar na kuunda kwa mabavu Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Baada ya Muungano huo, hatua za haraka zilichukuliwa kuwaondoa kina Marehemu Abdulrahman Babu, John Okelo, Kassim Hanga na wengine ambao waliokuwa tishio na kikwazo kwa utawala wa Sheikh Karume.

Ilielezwa kuwa Wa-Zanzibari wengi walishtushwa baada ya kusikia nchi yao imeunganishwa na Tanganyika kwani walikuwa hawana taarifa hizo. Pia, wengi wao wakiamini kuwa ASP walikuwa hawana nguvu za kisheria za kuuza uhuru wa Zanzibar kwa nchi nyengine ya Tanganyika.

Pia, ilielezwa kuwa Mkataba wa Muungano hauna uhalali wa kisheria maana ilitakiwa baada ya kutiwa saini na pande mbili za Muungano basi lazima ulikuwa uridhiwe na mabaraza ya kutunga sheria kwa upande wa Tanganyika (yaani Bunge la Tanganyika) na Baraza la kutunga sheria kwa wakati ule yaani Baraza la Mapinduzi (BLM).

Ilionekana kuwa kwa upande wa Jamhuri ya Tanganyika, Mkataba wa Muungano uliridhiwa na Bunge la Tanganyika lakini kwa upande wa Zanzibar hakuna kumbukumbu zinazoonesha kuwa Baraza la Mapinduzi lilikaa na kuridhia mkataba huo. Pia, kwa upande wa Zanzibar ilionekana kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar alieleza kuwa hakushirikishwa katika hatua yoyote ile ya uundaji wa Muungano huo ambao ndio uliosababisha Zanzibar kupoteza utaifa wake na pia kiti chake katika Umoja wa Mataifa

4.0 MADA YA PILI:

Mada ya pili ilitolewa na Ustaadh Mbarak ambayo ilizungumzia zaidi kuangalia nini asili ya matatizo tuliyonayo sasa hivi katika Muungano. Katika mada hii, imeelezwa kuwa matatizo ya Muungano huu yanatokana na mambo yafuatayo:-

(i) Msingi batili wa Muungano

Ilielezwa kuwa Uingereza tokea mapema ilikuwa na azma ya kuziunganisha nchi za Afrika ya Mashariki kwa dhamira kuu ya kuendeleza maslahi yao katika eneo hilo na pia kuondosha kikwazo chao katika eneo hilo ambao ni Uislamu. Kutokana na sababu hizo ndio baada ya Mapinduzi ikapelekewa kufanya kwa Muungano huo kwa haraka sana

(ii) Kutokuwepo na uwazi katika Muungano wenyewe

Ilielezwa kuwa Muungano huu hauko wazi na wala haufahamiki na Wananchi wa pande zote za Muungano maana haujulikani nini mambo ya Muungano na nini sio mambo ya Muungano

(iii) Waliotia saini sio wandaaji wa Muungano huo

Ilielezwa kuwa Muungano huo inavyosemekana kuwa umetiwa saini na watu wawili nao ni Sheikh Karume na Mwalimu Nyerere. Lakini, ukifuatilia ukweli wa mambo ni kuwa Viongozi wawili hao wamesukumwa na mataifa ya Magharibi wafanye hivyo ili kuyalinda maslahi yao.

(iv) Kufeli kujaribu kutatua Muungano


Ilielezwa kuwa, tumerithi dhana ya kulinda mtizamo wa walioutunga na kuuasisi Mungano huu ambao ni nchi za Magharibi kama vile kuleta mfumo wa Vyama vingi na kuweza kuvifunga Vyama kuwa vya kitaifa na kuweza kuweka kwenye katiba ili iweze kuulinda Muungano huu.
Mtoa mada alipendekeza kuwe na azma mpya ambayo itairudisha hadhi ya Zanzibar kiuslamu na pia kuwepo na ombi la kurirudisha Zanzibar ilivyokuwa yaani kutokea Sofala hadi Kilwa kivinje badala ya sasa tumebakishiwa visiwa viwili tu yaani Unguja na Pemba. Ombi hilo la kuidai haki ya Zanzibar irudishwe kama ilivyokuwa ifanyike kwa njia za mijadala, makongamano na maandamno.
Pia, imeonekana kuwa mustakbal wa Zanzibar katika Muungano huu utapatikana kwa ima mambo 3 nayo ni Tuuvunje Muungano, au Tuurekebishe au tudai Zanzibar iwe kama kabla ya ukoloni na baada ya hapo ndio tufanye Muungano ambao utakuwa na nguvu ambao utakuwa wameshaulizwa watu aina gani ya Muungano wanaoutaka, nini kiwe nguzo za Muungano huo, na nini khatma ya Zanzibar katika miaka inayokuja ikiwa itaendelea na Muungano huoa.

5.0 MADA YA TATU:

Mada ya tatu, ilitolewa na Rashid Ahmed ambayo ilikuwa inazungumzia Zanzibar na Jinamizi la Muungano. Katika mada hii, ilielezwa kuwa Zanzibar haitaweza kupiga hatua yoyote ile ikiwa itabakia kwenye Muungano huu tulionao maana juhudi za makusudi zilifanywa na Viongozi mbali mbali kwa ajili ya kutatua matatizo hayo lakini lakusikitisha Viongozi hao walipoteza nyadhifa zao baada ya kupigania kutatua matatizo hayo. Kwa kuongezea, mtoa mada alielezea kuwa Wa-Zanzibar walio nje wanaungana na wenzao walio ndani katika kuipigania haki na heshima ya Zanzibar irudi.

Kwa mujibu wa mtoa mada hii, ameweza kuelezea mambo makuu yafuatayo ili Zanzibar iweze kujikwamua :-

(i) Zanzibar inabebeshwa mzigo na Tanganyika

Imezungumziwa kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikibebeshwa mzigo wa matumizi katika kuchangia kwenye serikali ya Muungano ambao faida yake ni ndogo kuliwa mchango unaotolewa.

(ii) Vipi tutasimamia na kugawana madaraka katika Muungano

Ilielezwa kuwa, huu ni Muungano wan chi mbili huru. Kwahivyo, kuwe na mfumo wa kugawana madaraka sawa katika kuendesha Serikali ya Muungano na tuondokane na dhana ya kuwatia khofu Wa-Zanzibari pale wanapotaka kudai haki zao ndani ya Muungano

(iii) Nini kifanyike katika kutatua matatizo ya Muungano?

Ilielezwa kuwa kimfumo wa sasa wa muungano tunaambiwa kuwa kuna Serikali 2 yaani ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tu maana baada ya Muungano huo, Serikali ya Tanganyika ilivunjwa. Ilielezwa kuwa Serikali ya Tanganyika ipo na inafanya kazi maana kuna Wizara ambazo si za Muungano kwa upande wa Tanganyika huwa zinafanya kazi chini ya Serikali gani wakati Serikali ya Tanganyika haipo?. Kwanini Bunge la Jamhuri ya Muungano linakaa kupitisha bajeti za Wizara ambazo si za Muungano?. Huu ni ujambazi na ulaghai wa hali ya juu unaofanywa na Tanganyika.

(iv) Nini Wa-Zanzibari wanataka katika ugawaji wa mipaka ya madaraka katika Muungano?

Imeonelewa kuwa, Muungano huu unahitaji kutathminiwa upya na Wa-Zanzibari. Pia, waulizwe Wa-Zanzibari kama wanataka Muungano na kama watautaka basi pia waulizwe Muungano wa aina gani wanaoutaka?

Kiambatanisho No. 1

MAAZIMIO YA KONGAMANO

1.
Muungano upo na una matatizo mengi lakini hauko wazi. Kutokana na hayo, iko haja ya Muungano upitiwe upya kwa ajili ya dhamira ya kuboreshwa.

2. Mjadala wa Muungano urudishwe tena kwa uwazi maana Wataalamu wengi wameelezea kuwa Muungano huu hauna uhalali kisheria.

3. Imeonekana kuwa Hati ya Muungano haukupata ridhaa ya upande wa Zanzibar. Kwahivyo, kunahitajika mjadala mpana na mabadiliko makubwa.

4. Kumeonekana kuna kutoaminiana baina pande mbili za Muungano na kumeonekana upande wa Tanganyika inampiku mweziwe na ndio mwenye hati miliki.

5. Kufanyike kura ya maoni kwa upande wa Zanzibar ili Wananchi waulizwe kama wanataka Muungano au hawautaki na ikiwa Wananchi wakiridhia kuwepo Muungano basi wao ndio watakaosema ni aina gani ya Muungano wanaoutaka.

6. Ifanyike thathmini ya kina kuangalia mapungufu ya Muungano.

7. Kuangaliwe zaidi mashirikiano baina nchi na nchi badala ya kuangalia nchi moja moja kama Dunia inavyokwenda hivi sasa.

8. Kutekeleza vilivyo na kuheshimu Makubaliano ya Muungano ya 1964. Hii ni pamoja na kuunda ile Tume ya Katiba iliyotakiwa iundwe na kuitisha Baraza la Katiba ya Jamhuri ya Muungano kama ilivyoelekezwa katika mkataba wa Muungano.

Kauri Mbiu:
Tumeonewa vyakutosha, tumenyang’anywa vyakutosha na tumedhalilishwa vyakutosha kwa kuwepo Muungano huu, sasa Wazanzibari tunasema basi inatosha, tunahitaji mabadiliko.

Jipakulie hapa ripoti nzima yenye kurasa arubaini kwenye .pdf | View attachment MAAZIMIO_YA_MJADALA_FINAL_VERSION[1].pdf

Repoti hii, pia inapatikana kwenye tovuti hizi zifuatazo:
scribd.com/Maazimio-Ya-Mjadala-Final-Version | mzalendo.net
 
Back
Top Bottom