Ripoti ya Mauaji ya Arusha na kinachoendelea Bungeni juu ya ripoti ya mauaji mengine ya Watanzania

Dec 11, 2010
3,321
6,330
Wakuu.

Naomba kunakili Maneno ya Mchungaji Msigwa wakati akiwasilisha. "Kuikosoa na kuisema vibaya serikali yako hakumaanishi kuwa huna uzalendo na nchi yako, na kuisema vizuri serikali hakumaanishi kuwa wewe ni mzalendo sana na nchi yako"

Bungeni wanajadili mauwaji yaliyotokea kwa watanzania wenzetu kupitia operation tokomeza ambayo badala ya kuleta tija imeleta madhara makubwa kwa watanzania wenzetu ikiwemo vifp , kuteswa, kubakwa kwa kina mama na kusokomezwa chupa maeneo ya siri huku wanaume nao wakilazimisha kufanya mapenzi na miti.

Tukiwa tunajiuliza hayo yote, tuone hii ripoti ambayo mpaka leo serikali imegoma kuitoa hadharani na kuamua kuificha imesababisha kina nani kuchukuliwa hatu?

1.0 UTANGULIZI:
1.1 Muhtasari wa Tukio:
Tarehe 5 Januari 2011, Jiji la Arusha lilikumbwa na machafuko yaliyotokana na vurugu za kutawanya maandamano yaliyofanywa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo. Wakati Chama hiki kikidai kukamilisha taratibu zote za maandalizi na makubaliano na jeshi la polisi, tarehe 4 Januari usiku, mkuu wa jeshi hili Inspekta Generali Saidi Mwema aliyazuia maandamano hayo kupitia vyombo vya habari hususani luninga za ITV na TBC katika habari za saa mbili usiku.

Uamuzi wa kuyazuia maandamano hayo na kuruhusu mkutano wa hadhara ulidaiwa kuwa ni kutokana na sababu za ki intelijensia. Kwamba kufanyika kwake kungeleta machafuko. Pamoja na zuio hilo, Chadema iliendelea na, maandamano hayo wakiyaita ya amani..

Kufuatia tukio hilo, vyombo vya habari kwa maana ya magazeti, redio na luninga vilitoa taarifa mbali mbali kuhusiana na vurugu hizo za Januari 5, 2011 mkoani Arusha.

Miongoni mwa magazeti hayo ni Gazeti la Majira ISSN 0856 5086 Na.6211 Vol. II/4221 Ijumaa Januari 7, 2011, ISSN 0856 5086 Na.6212 Vol. II/4222 Jumamosi Januari 8, 2011 na Mwananchi ISSN 0856 7573 Na.03848 Ijumaa Januari 7, 2011, ISSN 0856 7573 Na.03849 Jumamosi Januari 8, 2011.

Magazeti mengine yalikuwa ni Nipashe ISSN 0856 5414 Na.056888 Jumamosi Januari 8, 2011 na Tanzania Daima ISSN 0856 9762 Toleo Na.2226 Ijumaa Januari 7, 2011, ISSN 0856 9762 Toleo Na.2227 Jumamosi Januari 8, 2011 na ISSN 0856 9762 Toleo Na.2228 Jumapili Januari 9.

Magazeti ya kiingereza na mengineyo yaliyotoa taarifa hizi ni pamoja na The Guardian ISSN 0856 5422 ISSUE no. 5019 na, Daily News ISSN 0856 3813 no. 10240 yote ya tarehe hiyo ya ijumaa Januari 2011.

Vurugu hizo zilisababisha watu watatu (3) kuuwawa, ishirini na nane (28) kujeruhiwa, arobaini na tisa (49) kukamatwa na kufikishwa kituo cha polisi na kati yao, thelathini na moja (31) kusomewa mashtaka mahakamani.Hii ni kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha wakati wa mahojiano na ujumbe wa Tume katika nyumba ya mapuziko (Police rest house) Arusha tarehe 10 January, 2011.

Taarifa hizo ziliendelea kueleza kuwa, kumetokea uharibifu wa mali, nyumba kuchomwa moto vituo vya polisi, kutishiwa, kuvamiwa ofisi za chama tawala, kupigwa mawe, uharibifu wa magari ya polisi na ya raia na pia mali za watu kuibiwa.

2.0 UFUATILIAJI:
Kwa mujibu wa sheria iliyounda Tume ya Haki za Binadamu, sheria namba 7 ya mwaka 2001 iliyoanza kufanya kazi rasmi 2002, sura ya pili II, kifungu cha 6 (c) kimetoa mamlaka kwa Tume kufanya uchunguzi katika jambo lolote linaloashiria au kuthibitisha uvunjwaji wa haki za binadamu na utawala bora.

Aidha kwa mujibu wa sheria hii, sura ya tatu III, kifungu namba 15 (1) (a), kwa ridhaa yake binafsi, Tume iliona umuhimu wa kufuatilia na kuchunguza tukio hili.

Tume ilizingatia pia mamlaka iliyopewa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya mia na thelathini 130 (1) kifungu kidogo cha (c) kinachosisitiza uwezo na mamlaka ya Tume kufanya yote haya.

Tume ilimteua Mhe. Kamishna Joaquine De-Mello akiandamana na afisa uchunguzi Philipo Sungu kutoka idara ya elimu kwa umma na mafunzo kufuatilia tukio hilo kwa muda wa siku tatu (3) kuanzia Januari 10 hadi 13, 2011 ili kupata picha halisi. Lengo kuu lilikuwa kubaini chanzo cha vurugu hiyo, uvunjwaji wa haki za binadamu kama ulikuwepo ili kutoa maoni na mapendekezo kwa mamlaka husika.

Tume ilifanya mahojiano na wadau mbalimbali zikiwemo mamlaka ya Jeshi la Polisi Tanzania, hususani uongozi wa juu mkoani Arusha, uongozi wa Chama Cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA), madaktari na majeruhi katika hospitali ya mkoa wa Arusha (Mount Meru) na ile ya kanisa la KKKT (Seliani) na baadhi ya wananchi kwenye sehemu yalipotokea matukio (site visit/site scene). (KIAMBATISHO II)

2.1 Maelezo kutoka Jeshi la Polisi:
Kwa ujumla maelezo ya jeshi la polisi yalielekeza shutuma kwa CHADEMA kukaidi agizo halali la mamlaka ya juu ya Polisi lililozuia maandamano.

Walidai kuwa licha ya mtiririko mzima wa majadiliano na makubaliano, utata uliojitokeza ulikuwa ni zipi ziwe barabara/njia zitakazotumika kwa ajili ya maandamano hayo. CHADEMA hadi inakwenda kwenye maandamano haikuafikiana na badala yake kuja na idai zaidi ya ile zilizopendekezwa. Askari walidai kuwa taarifa za kiintelijensia ziliashiria uvunjifu wa amani na hivyo kutumia nguvu pale amri hiyo
ilipokiukwa.

Viongozi hawa walidai licha ya kuyasindikiza maandamano haya kwa utulivu kutoka eneo la Phillips hadi Sanawari kupitia hoteli ya Mt. Meru, utata ulijitokeza pale walipofika njia panda ya Sanawari ambapo makundi makubwa ya watu yalijitokeza kutokea Kaloleni na Mianzini.

Askari wanadai hakukuwa na namna nyingine isipokuwa kutumia nguvu kuwatawanya waandamanaji kwa kutumia mabomu ya machozi, risasi za mpira na maji ya kuwasha kutawanya umati mkubwa wa waandamanaji.

Askari waliwakamata na kuwapiga viongozi ambao tayari walionyesha kupandisha hasira na pamoja na wafuasi (40) waliwekwa rumande kituo kikuu cha polisi cha mjini Arusha.

Wakati haya yakiendelea , baadhi ya viongozi wengine wakuu wa CHADEMA akiwemo Katibu wa chama Taifa bwana Wilbroad Slaa na mbunge wa Moshi mjini mheshimiwa

Ndesamburo Kiwelu waliponyoka na kuwahi uwanjani NMC ili kuwahutubia wananchi waliokuwa tayari wamewasili huko.

Askari wanasema walitishika pale viongozi hao waliokuwa jukwaani wakichochea wananchi kuvamia kituo cha polisi kwa mustakabali wa kuwakomboa viongozi waliokuwa wamekamatwa na kuwekwa rumande katika kituo kikuu cha Polisi (KIAMBATANISHO I A).

Yote haya ni kwa mujibu wa mkuu wa polisi mkoani Arusha (RPC) Thobias Andengenye na Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai ( DCI) Robert Manumba walioridhia kukutana na msafara wa Tume siku tuliyowasili Arusha Jumatatu ya tarehe 10 mwezi Januari 2011.

Mazungumzo haya yalifanyika katika nyumba ya wageni ya Jeshi la Polisi (rest house) mjini Arusha. 2.2 Maelezo kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA): Jioni ya saa kumi na mbili (12:00) siku hiyo hiyo ya tarehe 10 mwezi wa Januari, ujumbe wa Tume ukapata fursa ya kukutana na ujumbe wa uongozi wa CHADEMA katika ofisi za wakili na diwani wa chama hicho kata ya Moshi mjini, wakili Albert Msando.

Kwa upande wake CHADEMA ilidai kuonewa na kuburuzwa na jeshi la polisi tangu majadiliano ya awali ya nia ya kufanya maandamano hayo tarehe 31/12/2011. Walishangazwa na kigezo cha kupata ruhusa kutoka katika jeshi kinyume na sheria ya Polisi na ile ya vyama vya siasa inayozungumzia kutoa taarifa (notice) tu.

Walisisitiza kuwa kazi ya jeshi katika matukio haya ni kulinda amani na kuhakikisha utulivu unakuwepo katika shughuli nzima. Wanasema ni dhahiri kulikuwa na njama za kuibana na kuifadhaisha CHADEMA kwa sababu za kisiasa na ubinafsi. Kwao, tathmini nzima ya majadiliano ilikuwa ni ya ubabaishaji.

Waliendelea kusisitiza kuwa, uvumilivu ulipotea pale ambapo wakiwa katika maandalizi ya mwisho siku ya tarehe 4 Januari usiku walipopata habari kupitia wadau kwamba mkuu wa jeshi ameyafuta maandamano hayo bila hata ya kutumia njia za kimaandishi na kwa wakati muafaka.

Kubwa zaidi wanadai viongozi hao, ni utulivu na amani uliyoshamiri tangu maandamano yaanze pale Phillips kupitia hoteli ya Mount Meru hadi njia panda ya Sanawari ambapo askari walianza kwa kuwapiga na kuwapeleka viongozi mahabusu. (KIAMBATISHO I B)

Walisisitiza kuingiliwa uhuru huo wa kikatiba na uongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi ambao tangu kupatikana kwa ushindi wa kiti cha ubunge kwa jimbo hilo na mengine machache wamekuwa wakitumia mbinu mbali mbali kuwadhoofisha na kuwaadabisha tena kwa matumizi mabaya ya, nguvu ya dola.

Waliohudhuria kikao hiki kilichoisha saa tatu usiku ni pamoja na mbunge wa jimbo la Arusha Mjini Mheshimiwa Godbless Lema, katibu wa chama mkoa bwana Amani Golugwa na diwani wa chama hicho bwana Albert Msando

2.3 Maelezo kutoka kwa Madaktari na Wagonjwa Majeruhi katika Hospitali Ujumbe huu uliendelea na safari Januari, 11 asubuhi ukianza kuonana na madaktari na wagonjwa majeruhi waliolazwa katika hospitali mbili (2) za Mount Meru na ile ya Seliani.

Taarifa zilizopatikana katika hospitali hizi ni kupokelewa kwa majeruhi ishirini na sita (26) katika hospitali ya Mount Meru na wawili (2) Seliani. Majeruhi watatu (3) walipoteza maisha wakati wakipatiwa matibabu ya awali hapo hospitali ya Mount Meru, ishirini na mbili (22) walilazwa katika hospitali ya Mount Meru na watatu walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kuondoka hospitalini( moja (1) kutoka hospitali ya Mount Meru, wawili (2) kutoka hospitali ya Seliani).

Madaktari walithibitisha kuwa vifo hivyo vilitokana na majeraha ya risasi za moto. Kwa upande mwingine majeruhi walithibitisha kupigwa risasi za moto huku wakionyesha majeraha hayo kwenye miili yao (KIAMBATISHO I C) 2.4 Maelezo ya Wananchi katika sehemu za Matukio (site visit/ site scene) Tarehe 12 ujumbe wa Tume ulipata fursa ya kuzipitia barabara ambazo maandano yalipita na pia sehemu muhimu zilizokuwa na vurugu kubwa, Katika hali ya kutatanisha wananchi wengi waliohojiwa hawakuwa tayari kutoa majina yao kwa madai ya kuhofia ukatili wa askari.

Sehemu zilizopitiwa ni maeneo ya Sanawari, Kaloleni na uwanja wa NMC ulikofanyika mkutano wa hadhara. Wengi walioulizwa walionyesha kushangazwa na kusikitishwa na jinsi askari walivyokuwa na jazba wakiwatawanya waandamanaji waliokuwa watulivu. Walishangaa kuona jinsi virungu, risasi za mpira na moto, mabomu ya machozi, na maji ya kuwasha yalivyokuwa yakimiminwa kwa chuki na hasira.

Walisema kuwa vitendo hivi viliamsha ari na hasira ya wananchi na kuanza kurudisha mapigo kwa kutumia mawe. Wananchi walivunja vioo vya ofisi ya CCM mkoa wa Arusha, wakati nyumba ya mwananchi moja mfanyabiashara wa Yemen bwana Salum Ally iliyoko jirani na eneo la Metropol mjini Arusha ikiungua kwa moto uliosababishwa na bomu lililoruka kutoka katika gari la polisi.

Kwa upande wake mfanyabiashara bwana.Salum Ally alisikitishwa na hali yote ya tukio hilo ambalo yeye aliliona ni la kiuchumi zaidi kupitia njia za siasa. Alieleza kuwa kwa muda mrefu akiwa mfanyabiashara katika eneo hili ameshuhudia hali duni za maisha zinavyoongezeka na hasa kwa kundi la vijana.

Hata hivyo aliporejeshwa kuzungumzia tukio la uharibifu wa nyumba yake alikiri kuwa lilitokana na bomu la moto la kurushwa na kwenda juu kiasi kile hadi ghorofa ya pili. Alikiri isingekuwa rahisi kwa wananchi kuchoma nyumba sehemu ya juu na kuacha chini. Aliendelea kueleza kuwa amekuwa akifuatwa na mkuu wa Upelelezi wa Mkoa

(RCO) ili atoe tathmini ya uharibifu ili jeshi limfidie, dhana ambayo yeye binafsi hayuko tayari kuiridhia na hapa amenukuliwa akisema, ni gharama ndogo tu isiyozidi shilingi milioni tatu, na sioni sababu nilipwe kwani naamini bomu hili lililipuka kwa bahati mbaya tu. (KIAMBATISHO I D)

3.0 MFUMO WA SHERIA:
Wakati yote yakitokea ni vema kuangalia mfumo wa sheria ili kufikia maoni na mapendekezo ya kitaalamu yatakayosaidia kurekebisha hali hii. Ni vema pia kuangalia ni jinsi gani mifumo ya sheria invyochangia katika kujenga au kudhoofisha haki katika jamii yetu.

Tukio hili limetokea wakati nchi yetu iko mstari wa mbele katika kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ya haki za binadamu na utawala bora. Mikataba hii ina maridhiano na vipengele vizuri kwa madhumuni ya kuheshimu, kulinda, kutekeleza, kutetea na kukuza haki za binadamu. Nchi inajivunia Katiba nzuri inayoainisha vipengele mbali mbali vinavyotambua na kulinda haki za msingi za binadamu.

Jumuiya ya kimataifa kwa pamoja inawajibika kwa Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu la mwaka 1948 (UDHR) ambalo ni mama wa matamko, makubaliano na mikataba ya vizazi vyote vya haki. Vizazi hivivinahusisha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na kiutamaduni 1966 (ESCR), Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa 1966 (CCPR), Mkataba wa Kimataifa Kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu (UNCPRD), Mkataba wa Kimataifa Dhidi ya Ukatili na Unyanyasaji dhidi ya Binadamu na mingine mingi.

Nchi wanachama, Tanzania ikiwa miongoni mwao, zilizoweka sahihi na kuridhia mikataba hii zinawajibika moja kwa moja kuheshimu, kulinda, kutetea na kutekeleza haki zilizoainishwa kwenye mikataba husika. Pamoja na kutokuwa na msukumo wa kisheria nchi wanachama wanapaswa kuzingatia zaidi utashi na weledi ili kufanikisha na kutimiza azma hizi.

Azimio la ulimwengu juu ya haki za binadamu 1948, kifungu cha kumi na tisa (19 ) kinaeleza kuwa Kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake na kujieleza, haki hii inajumuisha uhuru wa kusimamia maoni yake bila kuingiliwa na kutafuta, kupokea na kutoa habari na mawazo kupitia vyombo vya habari vya aina yoyote bila kujali mipaka.

Nao Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa 1966, Ibara ya 19.-(1) unaainisha kuwa, Kila mtu ana haki ya kutoa mawazo yake pasipo kubugudhiwa, (2) Kila mtu atakuwa na uhuru wa kujieleza; haki hii inajumuisha uhuru wa kuuliza, kupokea, na kutoa taarifa na mawazo ya aina yeyote pasipokujalisha, aidha kwa kuongea au kwa kuandika au kupiga chapa ama kwa njia ya usanii ama kwa njia ya chombo cho chote cha habari alichokichagua.

Azimio hili pia katika, kifungu chake cha 20 (1) linabainisha kuwa kila mtu anayo haki ya kushiriki katika mkutano na chama kwa hali ya amani na kama inavyosisitizwa pia katika Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa 1966 katika ibara yake ya 21.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, imebeba kwa upana kwa kuzingatia haki ya kuishi, uhuru wa mtu na vikundi vya watu, haki ya faragha na usalama wa mtu, uhuru wa kwenda utakako, haki ya uhuru wa kutoa maoni, kuamini dini utakayo, uhuru wa kushirikiana na wengine na uhuru wa kushiriki shughuli za umma. Ibara ya 12 hadi ya 21 ya Katiba inajieleza vema.

Kuendana na mazingira ya tukio hili inabidi pia kuangalia sheria nyingine za ndani ya nchi zinazohusu mikutano ya hadhara na maandamano katika nchi yetu. Tukiangalia kanuni za jumla za jeshi la polisi namba 403 kifungu cha kwanza inasema;

(a) Any person who is desirous of convening, collecting, forming or organising any assembly or procession in any public place shall, not less than forty eight hours before the time when the assembly or procession is scheduled to take place submit a written notification of his impending assembly or procession to the police officer in charge of the area,. Hivyo hitaji hapa kwa anayetaka kufanya maandamano au
mkutano wa hadhara kwa mujibu wa sheria hii ni kutoa TAARIFA tu tena katika kipindi kisichopungua saa arobaini na nane (48).

b) where a person submits a notification in accordance with the preceeding paragraph, he may proceed to convene, collect, form, or organise the assembly or procession in question as scheduled unless
and until he receives an order from the Police Officer in charge of the area directing that the assembly or procession shall not be held as notified. Hii inasisitiza kuwa Polisi Officer in charge wa eneo, ambalo katika eneo hilo la Arusha mjini ni OCD wa Arusha Mjini ndiye anayeweza kutoa maelekezo ya kuzuia maandamano na sio RPC au IGP. Kwa mantiki hii, taarifa ya CHADEMA kwa Polisi ilitosha kwa wao kuendelea na mipango yao ya maandamano na mkutano kama inavyoelezwa katika kifungu (b)

Sheria Na. tano (5) ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa kifungu cha 11 vifungu vidogo vya (4) na (6). na sheria Na. 1 ya 1939 ya polisi na huduma za mgambo kifungu 43.-(1), (2), zimekidhi pia hitaji la CHADEMA kuendelea na mipango yao ya maandamano na mkutano wa hadhara kama ilivyopangwa.

Sheria Na.5, 1992 ya vyama vya siasa kifungu 11. (8) inasema; A stop order given under subsection (6) shall be in writing and, in such form as is able to easily disclose the reasons for its issuance and, state whether or not the political party concerned may hold the meeting at the venue at another time or date convenient to it in the
same area. CHADEMA wanasisitiza kwamba hawakupata taarifa ya kimaandishi nao Polisi kudai kutoa barua hiyo kupitia kwa mwakilikishi wa Chadema Estomihi Mala.Mala hakuweza kupatikana kuthibitisha madai
ya polisi na hadi ujumbe wa Tume unaondoka Arusha polisi hawakuwezesha kuwasilisha nakala ya barua hiyo kwa ujumbe wa Tume kama walivyotakiwa kuthibitisha madai yao.

Sheria ya Police - General Order No. 294 inasema; 1. The following officers ONLY are authorized to release information on police matters to the Press: - a) The Inspector General - on all matters affecting Force policy and security. b) Director of Criminal Investigation - Crime reports, wanted person notices and appeals to the public in connection with crime, accidents etc c) Chief of Public relations Police Headquarters - Routine Press
notices affecting the whole Force. d) Regional Commanders - Routine Press Notices affecting particular Region.


2. All Press and radio releases shall normally be typed or written. Verbal releases are only permissible in emergency and shall always be confirmed, in writing, at the earliest opportunity. Jeshi la polisi halikukidhi matakwa ya sheria hii kwa kushindwa kutoa taarifa ya zuio la maandamano na mkutano wa hadhara kwa taratibu zinazokubalika kisheria.

Sheria Na. 1 ya 1939 ya polisi na huduma za mgambo kifungu 45 na 46. - (4) inasema,

Any assembly or procession in which three or more persons attending or taking part, neglect or refuse to obey any order for dispersal given under the provisions of subsection (4) of section 43 or section 44, shall be deemed to be an unlawful assembly, within the meaning of section 74 of the Penal Code.Hata hivyo, kwa sababu kulikuwa hakuna taarifa ya OCD ya kuzuia maandamano, polisi hawawezi kutumia kifungu hiki cha (Penal code). Hivyo maandamano hayo yalikuwa halali.

Taarifa za ufuatiliaji zinaonyesha kuwa hata kama maandamano yalizuiliwa CHADEMA bado walikuwa na nafasi ya kudai haki hiyo kisheria kama kifungu 43.-(6) cha Sheria Na. 1, 1939 ya polisi na huduma za mgambo inavyosema, Any person who is aggrieved by the terms of a stop order issued under subsection (3) or, any order given by a police officer under subsection (4), may appeal to the Minister whose decision on the matter shall be final.

Hili Chadema hawakulifanya kwa madai kuwa hawakupata barua ya zuio la maandamano na
mkutano wa hadhara kutoka polisi.

4.0 TATHIMINI YA UVUNJWAJI WA HAKI ZA BINADAMU:
Taarifa ya kufanyika maandamano na mkutano wa hadhara tarehe 5 Januari,2011 ilitolewa kwa mkuu wa Jeshi la polisi wilaya ya Arusha Mjini tarehe 31 Desemba, 2010. Maandamano na mkutano wa hadhara uliridhiwa na serikali tarehe 4 Januari, 2011.

Maandamano yalizuiliwa katika dakika za mwisho kwa tangazo la Mkuu wa jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema kupitia vyombo vya habari usiku wa tarehe 4 Januari 2011.CHADEMA walifanya maandamano tarehe 5 Januari,
2011 kama ilivyopangwa licha ya kuepo kwa Tangazo la zuio.

Ujumbe wa Tume umebaini kuna utata wa kutolewa taarifa ya zuio la maandamano kimaandishi na kupokelewa na CHADEMA kupitia mwanachama wake aitwae bwana Estomihi Mala.Ujumbe wa Tume haukupata nakala ya barua ya zuio la maandamano kutoka pande zote mbili.

Maandamano yalifanyika kwa utulivu na amani kuanzia eneo la Phillips kupitia hoteli ya Mount Meru hadi njia panda ya Sanawari. Askari waliyasindikiza wakati huohuo wakisihi viongozi na waandamanaji kuacha
kuandamana na kutawanyika. Ilielezwa kuwa, katika hali isiyokuwa ya kawaida askari walitawanya maandamano ya amani kwa kutumia silaha mbalimbali ikiwemo mabomu ya machozi, risasi baridi na moto, maji ya kuwasha na virungu.

Askari walifanya vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya viongozi na waandamanaji hasa wanawake bila kujali hali zao; kwa mfano, mbunge Lucy Owenya na Josephine Mushumbusi walipigwa na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za miili yao. Viongozi wa CHADEMA na wanainchi wengi walikamatwa na kuwekwa rumande katika kituo kikuu cha polisi kati mjini Arusha.

Askari waliwapiga waandishi wa habari,waliwanyanganya vifaa vyao vya kazi na kufuta picha na kazi walizokuwa wanazifanya kwenye maandamano. Askari na waandamanaji walisababisha uharibifu wa magari
na mali za umma na wanainchi. Aidha walisababisha upotevu wa mali za wanaichi zikiwemo simu mbili za mkononi za Mheshimiwa mbunge wa viti maalumu Lucy Owenya na fedha tasilimu shilingi milioni mbili na laki saba (TZSH.2,700,000/=) za majeruhi Ally John Ogaga walizodai kunyanganywa na askari, wakati Ofisi ya CCM Mkoa wa Arusha ilivunjwa vioo kwa mawe na waandamanaji na nyumba ya mwanainchi bwana Salum Ally
iliungua kwa moto uliosababishwa na mlipuko wa bomu lililoruka kutoka kwenye gari la polisi.

Mkutano wahadhara ulifanyika na viongozi walitoa hotuba kwa wanainchi. Wakati wa mkutano askari walishambulia wanainchi kwa kutumia mabomu ya machozi.Wakati wa hotuba viongozi wa CHADEMA walitoa maneno ya uchochezi yaliyowashawishi wanainchi kuelekea kituo cha polisi kuwatoa viongozi waliokuwa wakishikiliwa na polisi.Hii ilisababisha vurugu kubwa iliyopelekea watu watatu(3) kupoteza maisha, ishirini na
mbili(22) kuumia na kulazwa hospitalini, watatu (3)waliumia wakatibiwa bila kulazwa na wengine wengi kujeruhiwa wakiwemo polisi.

Madaktari wlithibitisha kuwa chanzo cha vifo na majeraha vilisababishwa na risasi za moto na vipigo. Ujumbe wa Tume ulielezwa kuwa huduma za kisheria, dhamana, matibabu na faragha havikutolewa wakati muafaka kama Sheria inavyotaka, Kwenye kituo cha polisi askari walitumia lugha chafu, matusi na kejeli ambavyo viliwadhalilisha na kuwaumiza watuhumiwa kisaikolojia.

Ujumbe wa Tume ulielezwa kuwa kulikuwa na msongamano mkubwa wa mahabusu waliowekwa kwenye chumba kidogo kwa muda mrefu kwenye kituo cha polisi bila kufanyika jitihada za haraka kuwahamishia walioumia kupelekwa hospitalini na wengine katika vituo vingine vya polisi vyenye nafasi.

Askari walituimia nguvu za ziada zisizokuwa na ulazima kuzuia maandamano ya amani bila kuweka bayana sababu za msingi kuthibitisha matumizi hayo. Kitendo hiki kilipelekea uvunjwaji wa haki za binadamu
kwa kiwango cha hali ya juu, kitu ambacho hakiwezi kuvumiliwa mbele ya macho ya jamii na kuachwa kiendelee. Ni lazima hatua madhubuti zichukuliwe kukomesha hali hii.

Pande zote zinabeba lawama kufuatia tukio hili, ni ukweli usiopingika kuwa polisi wanabeba lawama kubwa zaidi kwa kusababisha mauaji, majeraha na vurugu kwa kuzuia maandamano halali ya amani kinyume cha sheria. Viongozi wa CHADEMA kwa upande wao wanalaumiwa kushindwa kuwa wavumilivu na kuwashawishi wafuasi wao kutoandamana ili hali kulikuwa na zuio. Aidha kitendo cha kutumia maneno ya uchochezi
kuhamasisha wananchi kwenda kituo cha polisi kuwatoa viongozi wao na wananchi waliokamatwa ni kinyume cha Sheria.

5.0 MAJUMUISHO:
Katika tukio hili askari walitumia nguvu nyingi kupita kiasi baada ya kupata maelekezo kutoka kwa viongozi wao wa ngazi za juu kwa madai mepesi ya sababu za ki intelijensia,badala ya kupima na kufanya kazi
kwa kufuata Sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza maadili ya kazi zao. Amri zilitawala zaidi ya weledi katika kufanya maamuzi.

Maamuzi ya mkuu wa jeshi la polisi (IGP) ambaye hana mamlaka ya moja kwa moja katika eneo husika kama sheria inavyotaka hayakuwa halali, pia hakuwa na uhalali kuingilia na kutoa tamko katika ngazi ile na kwa
wakati mfupi hivyo wakati mwenye mamlaka na eneo husika alikuepo na hakuzuia maandamano.Ujumbe wa Tume uliridhika kuwa hakukua na sababu za msingi za kuzuia maandamano, sababu za kuzuia maandamano kwa kigezo cha intelijensia hazikutumika vizuri na hazikupata nguvu za kuhalalisha (vague, speculative) zuio la
maandamano ya amani.

Kwa upande wa CHADEMA, viongozi waligubikwa na ukaidi na jazba. Utashi wa uongozi na dira ya uvumilivu havikuzingatiwa wala kupewa nafasi hasa pale walipotoa maelekezo kwa wafuasi wao kwenda kituo cha polisi
kuwatoa viongozi wao waliowekwa ndani. Kwa mtazamo wa haki za Binadamu tunaamini maandamano sio njia pekee ya kuleta suluhu katika jamii pale kunapotokea kutoelewana kwa pande mbili au zaidi.Njia za kidiplomasia kama vile majadiliano ya pamoja zimeonekana kuwa na nguvu kubwa kuleta suluhu kwa pande zilizotofautiana bila kusababisha madhara kwa jamii.

Umasikini, ukosefu wa ajira na upatikanaji wa huduma za kijamii (maji, elimu na afya), tofauti za hali ya kipato, ubinafsi na udikteta, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na uvivu vimejenga chuki na hasira
miongoni mwa jamii. Ubadhirifu wa rasilimali za nchi kwa manufaa ya wachache, ni tatizo linaloshamiri na kutishia amani ya nchi.

Ufahamu na, uelewa wa viongozi na jamii kuhusu haki za msingi za binadamu pamoja na wajibu unaoendana nao, bado ni changamoto kubwa. Dhana ya polisi jamii inadhoofishwa kutokana na vitendo vya mabavu na
ukatili vinavyofanywa na vyombo vya kutekeleza sheria hususani jeshi la polisi. Lawama hizi hazikwepeki kwa wananchi ambao nao hawazingatii wajibu walio nao mbele sheria.

Ukomavu na utashi wa vyama vya siasa bado ni changamoto katika jamii zetu kutokana na mazingira ya mfumo wa chama kimoja, Visasi na chuki vinaonekana kushamiri katika harakati mbali mbali za kudai haki. Hali
hii isiporekebishwa itahatarisha amani na utulivu uliojengeka kwa miaka mingi. Hatima yake ni uvunjifu wa amani na mara zote anaeathirika ni mwananchi wa kawaida.

Ni vizuri Jeshi la Polisi likaelewa kuwa nchi hii ni ya demokrasia ya vyama vingi, na pale chama kimoja kinapohitilafiana na chama kingine, kazi yao kubwa ni ile ya kulinda amani na sio kufanya vitendo
vinavyoonyesha hisia kuwa wanapendelea chama fulani.

Jeshi kama ilivyo serikali na wananchi ni vema wakubali dhana ya kukosolewa na kuwajibishwa tena kwa mtazamo chanya. Dhana hii ina nia ya kujitafakari, kujitambua na hatimaye kuchukua hatua madhubuti
za kujirekebisha na kuboresha demokrasia na utawala wa sheria.

6.0 MAONI YA BAADHI YA WANANCHI KUHUSU MAANDAMANO
Kwa kuwa vurugu za Arusha zilitokana na maandamano, Tume inaona ni vema kukumbuka maoni ya watu mbalimbali kuhusu maandamano kwa ujumla. Mhadhiri mmoja mwathirika wa migomo ya wanafunzi na wahadhiri katika chuo kikuu cha Dodoma alibainisha maoni yake na, tunapenda kumnukuu;

Tabia inayojengeka na kuendekezwa na serikali kukumbatia na kuagiza jeshi la polisi kutuliza hali si dalili nzuri kamwe, na ninasisitiza tabia hii ikome kwani haina mwisho mzuri. Kwa kawaida mwanadamu huchukua uamuzi wa kuandamana pale inapothibitika njia nyingine zote za muafaka zimeshindikana. Jukumu la askari katika hali hii ni lile la kulinda na kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa na si vinginevyo

Tanzania kama nchi nyingine duniani bado inakabiliwa na changamoto za kimageuzi, utandawazi umeifanya dunia kuwa kama kijiji, wananhi wetu wanaona na kushuhudia yanayotendeka kila siku duniani kote,na wameanza kuwa na uelewa mkubwa wa maswala ya demokrasia na haki za binadamu, hivyo ni vizuri serikali kusoma alama za nyakati ili kujipanga ipasavyo kukabiliana na hali hii badala ya kutumia amri na vitisho kutatua migogoro ya maandamano. Pamoja na changamoto nyingi za kiuchumi na kijamii ni vema kuweka vizuri misingi ya utawala bora na uwazi katika utekelezaji wa majukumu mbali mbali katika utendaji wa
shughuli za umma.

Wengine waliotoa maoni ni Askofu mkuu wa jimbo kuu la Dar Es Salaam, Mwadhama Kardinal Polycarp Pengo ambaye alisema, Kitendo cha watu kutegemea nguvu ya silaha wakifikiri kwamba njia hiyo ndiyo italeta
amani au wataweza kuleta ushindi wao. Huko ni kujidanganya na kumtukana Mungu, kwa vile hayo ni maandalizi ya maafa makubwa kwa ajili ya taifa la Tanzania. Aliongeza kusema, Mwenyezi atuepushe na laana hiyo. Gazeti Majira.

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, katika mkutano na waandishi wa habari alisema government intends to a lasting solution to the political unrest in Arusha region between
wrangling CCM and, Chadema parties. Aliendelea kusema, Since this dispute is of a political nature, the government will take all necessary measures to bring the disputing parties together such that
they sit on one table and, resolve their differences by having a reconcillition team.

Msajili wa vyama vya siasa bwana John Tendwa alinukuliwa kwenye gazeti la Daily News akisema, Chadema were initially allowed to stage a demo and, hold a public rally, but the decision was reversed on Tuesday. A
letter to that effect was written to Chadema secretary and, on Tuesday evening Inspector General of Police Saidi Mwema appeared on national TV announcing cancellation of the demo.

Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba aliwaeleza wanahabari kuwa his party was saddened by what happened to Chadema supporters and, the people following polices efforts to scatter their demonstration,
aliendelea kusema, Such acts by police makes us even stronger and, bold us to continue fighting for our democratic rights and, we would like to assure Chadema supporters and, people of Arusha that we will
always support them.

7.0 MAONI NA MAPENDEKEZO YA TUME
· Tume imeona kuwa, kitendo cha polisi kuzuia maandamano ya amani na halali ilikuwa ni uvunjwaji wa haki za Binadamu na ukiukwaji wa Mikataba ya Kimataifa, Kikanda na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania. Pia ilikuwa ni kinyume na Sheria, Kanuni na taratibu mbalimbali za nchi.Ukiukwaji huo ulipelekea maafa makubwa ikiwemo vifo vya watu watatu (3) na wengine wengi kujeruhiwa, uharibifu wa mali na
wananhi kukosa imani na polisi (serikali). Hivyo ni vema serikali kuchukua hatua stahiki kwa waliohusika na mauaji na uharibifu wa mali ili haki itendeke na wananchi kurudisha imani kwa serikali yao.

Ni vema kushirikiana na vyombo vinavyohusika na kurekebisha sheria kupitia na kurekebisha sheria kandamizi na zinazokinzana ili kuondoa migongano katika sheria hizo.

Kuelimisha jamii, viongozi, wadau na wataalam mbalimbali, kuheshimu maamuzi na mitazamo mbali mbali ya kisiasa, kiitikadi, kidini na kitamaduni kwa utashi, kuvumiliana na kuheshimiana. Kuna haja ya kuweka mikakati mahususi ya kuhakikisha kuwa jamii inaufahamu wa kina wa Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, elimu ya Haki za Binadamu, sheria za nchi, na mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa nchini inaeleweka na kuzingatiwa, kuheshimiwa, kulindwa na kutekelezwa.

Serikali iangalie kwa undani kero za watumishi wa umma hasa jeshi la polisi ambalo limegubikwa na changamoto nyingi za kiutendaji na kimaadili ikiwemo rushwa ili kuboresha hali za kimaisha kwa askari na
kufuata maadili ya kazi zao.

Kuandamana ni haki ya kikatiba na Katiba ya nchi inatamka wazi kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamii (civilian). Kama nchi inayozingatia demokrasia serikali haipaswi kuzuia haki ya kuandamana
bali kuhakikisha haki hii inatekelezwa bila kuathiri amani na utulivu wa nchi.

Kwamba, kazi kubwa ya jeshi la polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, hakuna namna jeshi hili litatimiza malengo haya bila ushirikishwaji wa wananchi, kwani makundi haya yanategemeana. Hivyo ni vema serikali kuhakikisha inatimiza wajibu wa kuheshimu, kulinda na kutekeleza haki za wananchi ili wananchi nao wawajibike kuheshimu, kutii na kutekeleza sheria za nchi. Hii itajenga uhusiano mwema baina ya polisi(serikali) na wananchi na kupunguza uhasama na chuki iliyojengeka kati ya makundi haya.

8.0 VIAMBATANISHO:
Kiambatanisho Na. I: Maelezo kutoka kwa wadau mbalimbali

Kiambatanisho Na. II: Orodha ya Majina ya wadau na sehemu zilizotembelewa Kiambatanisho Na. III: Barua zilizotumika kufanya mawasiliano ya tukio kutoka CHADEMA Kiambatanisho Na. IV: CD mbili (2) zinazoonyesha baadhi ya picha na video za tukio kutoka CHADEMA

Mhe. Jaji (Mstaafu) Amiri Ramadhani Manento
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora

Machi 1, 2011
 
Back
Top Bottom