Ripoti ya Hali ya Uchumi Tanzania: Benki ya Dunia yapendekeza mfumo wa ncha 3 kupambana na COVID-19 na Mporomoko wa Uchumi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
874
1,000
Leo Machi 3, 2021 Benki ya Dunia inatoa Ripoti yake ya uchambuzi huru wa hali ya kiuchumi ya Tanzania ikiwa ni toleo la 15.

Jiunge nasi tukikuletea taarifa mubashara.

LIVE:

YouTube:


Facebook:


Salaam za ufunguzi zilizotolewa na Mara K. Warwick, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Zambia, Zimbabwe na Malawi, zimetolewa kama heshima kwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Benno Ndulu ambapo ameelezwa kama kiongozi aliyetendea makubwa sekta ya uchumi, si tu kwa Tanzania bali kwa ulimwengu mzima.

Kuhusu Pr. Ndulu, Mara Warwick amesema:
Wafanyakazi wengi wa WB walipata upendeleo mkubwa kufanya kazi na Prof. Ndulu (au Benno kama alivyokuwa maarufu kwa wengi wetu) aidha akiwa mfanyakzi wa Benki ya Dunia au Benki Kuu ya Tanzania, au katika shughuli nyingi za kimataifa za maendeleo alizozifanya kwa moyo wote.

Mbobezi katika uchumi wa maendeleo na kiongozi mzuri sana aliyejikita katika mabadiliko ya kuichumi na kijamii ya #Tanzania, benno alikuwa daima katika moyo wa kazi zetu Afrika yote haya ikiwa ni Shukrani kwa uelewa wake na ukarimu mkubwa wa kuwapa wengine muda na ujuzi wake.

Alitoa mchango muhimu katika Maendeleo ya Tanzania na nje ya mipaka tangu miaka ya 1980 alipoongoza jitihada zilizosaidia kuiandaa nchi na ajenda ya mageuzi ya kiuchumi hadi kuhamia Benki ya Dunia Tanzania kisha Washington DC na kisha kurudi nchini 2008 kama Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania

“Prof. Ndulu alishirikiana na wadau wa kitaif ana kimataifa ikiwemo Sekta Binafsi kusimamia mageuzi muhimu katika maeneo ya msingi kama ujumuishi wa kiuchumi, maendeleo ya watu, mazingira ya biashara na miundombinu…”

“Hakika, #Tanzania kuongoza kwenye ajenda ya ushiriki wa kiuchumi duniani hakuwezi kutengenishwa na kujikita kwa Prof. Ndulu katika suala hilo…”

Sote hapa Benki ya Dunia tutakumbuka uongozi Madhubuti wa Prof. Ndulu na kusimamia kwake masuala muhimu ya maendeleo. Zaidi ya yote tutakumbuka mapenzi yake katika utafiti na kujenga kizazi kijacho cha Wachumi wa Afrika

Kuhusu "Kupandisha Viwango: Kufikia Dira ya maendeleo ya Tanzania", Mara Warwick anaeleza:
Sura maalum ya toleo la 15 la Tanzania Economic Update linaloitwa “Kupandisha Viwango: Kufikia Dira ya maendeleo ya Tanzania” inaangalia mafanikio ya hivi karibuni ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati Julai 2020

Pia ilijaribu kudadavua nini kinatakiwa ili kufikia malengo yaliyo katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025
Mjadala umeundwa kuzingatia misingi mitatu; kuendeleza ukuaji wa uchumi katika kipindi kifupi kijacho, kuongeza ushirikishwaji katika uchumi ili kupunguza umasikini na kuchochea uimara na ulinzi wa uchumi.

Kuingia kwa Tanzania katika nchi za uchumi wa kati za chini kunatoa nafasi ya kuchunguza ubora wa ukuaji wa nyuma na kutengeneza mchoro wa kuiongoza katika kufanikiwa kuingia katika hadhi yake mpya ili kufikia malengo yanayopimika ya maendeleo zaidi ya kipato pekee

Ni yapi yanatarajiwa kwa Tanzania ktk ukuaji na hali ya umasikini wakati dunia ikipitia changamoto? Ni vipi vipaumbele vya kisera ili Tanzania iingie kikamilifu katika nchi za uchumi wa kati?

Athari za COVID-19: Pato la Taifa kwa 2021 kudondoka kati ya 3% hadi 5.3%
COVID19 inaendelea kuleta athari za kibinadamu na kiuchumi duniani kote. Uchumi wa dunia ulisinyaa kwa asilimia 4.3 mwaka 2020, ingawa unatarajiwa kupata ahueni kwa asilimia 3.8, bado hali ya uchumi inatarajiwa kuwa mbaya kuliko hata kabla ya mlipuko huu kwa miaka kadhaa

Tanzania imefanya vizuri sana ikilinganishwa na nchi nyingine katika ukanda huu ingawa ukuaji wa uchumi umekuwa wa taratibu na umasikini unategemewa kuwa umeongezeka.

Ukuaji halisi wa pato la taifa ulidondoka kutoka 5.8% kwa 2019 hadi 2% kwa 2020.

Serikali ya Tanzania ilichukua hatua za mapema za kuondokana na athari za kiafya na kiuchumi za COVID-19 ingawa zilikuwa za kawaida sana na za muda mfupi kulinganisha na nchi nyingine katika ukanda.

Ingawa mporomoko wa kuichumi uliepukwa, kukosekana kwa taarifa rasmi kuhusu maambukizi ya COVID-19 na idadi ya vifo inaweka ugumu katika kufanya uchambuzi wa ubora wa hatua zinazochukuliwa

Hali ya uchumi wa Tanzania inabaki kuwa isiyotabirika huku athari za mlipuko wa #COVID19 ukitegemewa kupunguza kasi ya kupunguza umasikini. Kutokana na kutotabirika huku, tunataraji ukuaji wa Pato la Taifa kwa 2021 kudondoka kati ya 3% hadi 5.3%

Tanzania bado ina nafasi nzuri inayoweza kusaidia kurejesha hali yake ya ukuaji wa uchumi
Licha ya changamoto za hapa na pale, Tanzania bado ina nafasi nzuri inayoweza kusaidia kurejesha hali yake ya ukuaji wa uchumi.
Ni moja kati ya nchi ambazo hazikupata mporomoko wa uchumi 2020 na ina nafasi nzuri ya kupata mikopo kutoka nje

Benki ya Dunia inapendekeza mfumo wenye ncha 3 wa kushughulika na janga la COVID 19 na mporomoko wa uchumi unaokuja nalo. Mfumo huu umejikita katika kuokoa Maisha, Kulinda hali ya kimaisha na kulinda Tanzania ijayo

Kwanza, kuokoa Maisha kunategemea jitihada endelevu katika kukinga, kutambua na kutibu COVID-19 ikisaidiwa na uwazi wa taarifa na utoaji wa ripoti kwa wakati. Uwazi utasaidia kutambuliwa kwa mapema, kuzuia ueneaji na kuisaidia jamii

Kuwekwa kwa mfumo wa ndani kwa ajili ya ufuatiliaji wa COVID-19 itaiweka Serikali katika nafasi nzuri chanjo mpya zikizidi kugunduliwa. Tunaishauri Serikali kuhusisha wadau wenye ujuzi waandae mpango wa kutekeleza ugawaji wa chanjo ya COVID-19.

Kulinda hali ya kimaisha ya wananchi inahitaji uchambuzi yakinifu wa mipango iliyopo ya misaada na namna ya kuongeza matokeo kwa kaya na taasisi zilizo hatarini.

Mpango wa Tanzania kusaidia kaya masikini bado ni finyu
Tanzania ina mpango Madhubuti wa kusaidia kaya masikini ambao umekuwepo kwenye ripoti ya sasa ya benki ya Dunia lakini mtandao wake bado ni finyu.

Serikali ifikirie kupanua mpango huu na mingine ili kupunguza hatari kwa kaya masikini. Katika kipindi kifupi, Serikali iimarishe mbinu za kulinda ajira na kutoa msaada wa biashara ndogo na za kati.

Ufufuaji madhubuti kwa mwaka 2021 na kuendelea utahitaji mabadiliko ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara. Maeneo muhimu ni kama kuhamasisha matumizi ya suluhu za kidijitali katika biashara, kuongeza upatikanaji wa fedha kwa biashara ndogo na za kati na kutatua changamoto za sekta isiyo rasmi

Julai 2020, Tanzania ilifikia hadhi ya uchumi wa kati wa chini baada ya jitihada za miongo miwili za ukluaji na uwekezaji ukichangiwa na hali nzuri ya uchumi wa kitaifa, wingi wa malighafi za asili na nafasi nzuri ya kijiografia

Wakati haya ni mafanikio makubwa, Ajenda kuu ya maendeleo ya Tanzania bado haijaisha. Dira ya maendeleo ya Tanzania ya 2025 inaiona Tanzania ikiwa nchi ya uchumi wa kati yenye rasilimali watu iliyokomaa na viwango vya juu vya hali ya kimaisha.

Kufikia malengo haya, hatua chanya za Tanzania katika kuongeza vipato, kuboresha miundombinu na kuboresha viashiria vya kijamii lazima ziendane na kupunguza umasikini, maendeleo ya jumla na viashiria vingine vya ubora wa maendeleo

Ukuaji wa idadi ya watu, utengenezwaji wa ajira wa taratibu na usio na usawa, viwango vya chini vya elimu na uwepo finyu wa nafasi za elimu na ajira hususani kwa wanawake na wasichana vimepunguza ushirikishaji wa upanuzi wa kiuchumi wa Tanzania ukipunguza makali ya upunguzaji wa umasikini.

Kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025 kutahitaji jitihada ya kurudisha kasi ya ukuaji ya uchumi huku upatikanaji wa fursa za kiuchumi ukipanuliwa

COVID-19 imeangazia kutotabirika kwa uchumi wa dunia na uwezo wa Tanzania kubaki na hadhi yake itategemea kuimarishwa kwa ustahamilivu wake kwa matatizo huku ikiwekeza kwa mtaji rasilimali watu.

MAJADILIANO YA JOPO LA WATAALAM

Majadiliano ya Jopo la wataalamu yakiwashirikisha Prof. Honest Ngowi (Mzumbe University), Dkt. Blandina Kilama, Mtafiti Mwandamizi, REPOA na Mr. Paul Makanza, Makamu Mwenyekiti, Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF)

SWALI 1: Mlipuko wa COVID19 umepelekea kushuka kwa uchumi wa dunia na kupelekea kupungua kasi ya ukuaji wa uchumi Tanzania. Nini maoni yako kuhusu misingi ya kufufua uchumi mwaka 2021 na kuendelea? Sekta zipi zinahitaji uangalizi maalum na nini changamoto za ufufuaji huu?

Dkt. Kilama: COVID19 bado inatupiga na tunapoteza nguvu kazi katika uzalishaji. Jambo moja ambalo inabidi tuliwekee mikakati ni namna tunaweza kupangilia rasilimali watu na kuhakikisha tunaendelea kuzalisha kwa ufanisi.

Vilevile inabidi tuwe wabunifu kwa kutumia teknolojia. Ubunifu ndio njia ya kutoka kwenye mkwamo huu wa kiuchumi.

Prof. Ngowi: Kilimo ndio sekta inayobeba idadi kubwa ya Watanzania. Wananchi wanaweza kudhani COVID19 imegusa sekta nyingine kama utalii lakini kilimo hususani kilimo cha mbogamboga na matunda.

Kurejesha uchumi kwenye hali yake ya ukuaji kunahitaji mabadiliko katika seraza kifedha kama kupunguzwa kodi na misamaha.

Prof. Ngowi: Katika wimbi la kwanza la COVID19, Baraza la Biashara la Afrika Mashariki lilipendekeza Serikali zishushe VAT hadi 12% ambapo Kenya ilishusha kutoka 16% hadi 14% huku Tanzania ikibaki ile ile. Ingeshushwa ingesaidia kuzipa uhai kampuni zinazopata shida.

Mei 2020, Benki Kuu ya Tanzania ilipunguza viwango vya riba kama namna ya kusaidia uchumi kipindi cha COVID19. Natamani Tanzania ingefanyia kazi mambo haya mapema kama Kenya na Ghana ili kurejesha uchumi kwenye hali ya ukuaji wake wa awali.

Paul Makanza: Tanzania tulibahatika sana kutopata kudorora kwa uchumi ingawa hatukufikia ukuaji wa uchumi tuliotaka kabla ya kulipuka kwa COVID19, hivyo kurejesha ukuaji ni jambo la kipaumbele.
Hatua ninazopendekeza ni tatu

1. Kuhakikisha usalama wa watu wetu
2. Kuhakikisha biashara zinaendelea
3. Kuhakikisha matumizi, uwekezaji na uuzaji bidhaa nje ya nchi vinaendelea. Haya yote yanahitaji sera nzuri na nikiliangalia kwa sura ya sekta binafsi inamaanisha kufanyia kazi matatizo yetu ya muda mrefu kama upatikanaji wa ardhi, viwango na ubora wa malighafi, rasilimali watu (ujuzi na uwezo wa uzalishaji) na upatikanaji na unafuu wa mitaji.

Mazingira ya ufanyaji biashara ni lazima yaboreshwe. Tuko nafasi ya 141 kidunia kwa sasa, ni wakati wa kuhakikisha tunafika katika namba ya tarakimu 2.

Sekta zinazohitaji uangalizi maalum ni Utalii ambayo ilikuwa na 77% ya anguko la mapato, upotevu wa ajira kwa asilimia 50.

Pia sekta ya uzalishaji hususani wazalishaji wadogo na wa kati. Naamini kuwa hatua zilizochukuliwa mwaka jana kupambana na COVID19 hazikwenda mbali kiasi cha kuwasaidia wafanyabiashara wa chini.

Changamoto kubwa tuliyonayo bado ni Gonjwa lenyewe (COVID19)

SWALI 2: Katikati ya mdororo wa uchumi wa dunia kulikuwa na habari njema ya Tanzania kupata hadhi ya uchumi wa kati wa chini jambo lililosherehekewa nchini. Ni sababu zipi unafikiri zilipelekea tukafikia hadhi hii, na unadhani malengo ya maendeleo yalitajwa katika dira ya maendeleo ya 2025 yamefanikiwa?

Dkt. Kilama: Unapoweka lengo unaweza kulifikia wakati haukutarajia. Maamuzi sahihi ni kuchambua mafanikio yako yanamaanisha nini.

Faida ambayo TZ inayo kwa muda sasa ni uchumi wa mseto. Nafikiri hii ndiyo ilipelekea kufikia hadhi hii. Kufikia hapo ni kitu kimoja na kuendelea kubaki hapo ni kitu kingine, na kuelewa namna ya kufanya kazi baada ya kufikia hapo ni kitu kingine tofauti kabisa.

Kama mtafiti naweza kusema ni jambo moja kukua, lakini swali ni kuwa ni wapi hasa unakua? Tuna kilimo, viwanda na huduma. Data zinaonesha tunakua kwenye upande wa viwanda na huduma, sekta zinazohusisha watu wachache.

Kwenye upande wa huduma tulikuwa na taratibu zisizo rasmi licha ya ukuaji wetu. Baada ya COVID-19 kutupiga imekuwa ni vigumu kuinuka tena kutokana na kukosa mpangilio rasmi.

Prof. Ngowi: Habari ya Tanzania kupata hadhi ya nchi za uchumi wa kati wa chinbi ilivyotangazwa nilipokea maswali mengi sana kutoka kwa raia wa kawaida wakihoji ‘’Ni kweli mimi ni mtu wa kipato cha kati?’’

Kwakweli huu ni wastani wa nchi lakini kuna watu wenye kipato cha chini ambao hawana uhusiano wa moja kwa moja na maendeleo haya

Kiulimwengu ni kweli tumefanikiwa kufikia hadhi hii kwa kupitia miongo kadhaa ya uwekezaji na mageuzi. Mageuzi ya miaka ya 1980 hadi mwanzo wa 1990 yalibadilisha mazingira ya biashara kwa kuwaalika sekta binafsi kutoka nje na hapa ndani.

Uwekezaji tulioona kwenye mazingira ya biashara, maboresho ya sera za kisheria, kiudhibiti vimewezesha uzalishaji wa bidhaa na huduma kupitia sekta zote.

Tumefanikiwa miaka 5 kabla ya wakati, kilichobaki ni uendelevu. Katika historia kuna nchi 20 zilizowahi kurudi nyuma kutoka katika hadhi zao. COVID-19 inatuweka katika hatari hiyo kutokana na kuzuia vipato vya watu na kuwaacha wakiwa katika mstari wa umasikini hivyo hatuna uhakika kaama tutabaki tulipo

Hatujafikia malengo yetu ya 2025. Tulitaka tuwe na washindani imara na wenye nguvu, uchumi uliopangwa vizuri na bado hatujafikia hivyo. Tunajenga Roma na haiwezi kamilika kwa siku moja

Paul Makanza: Kisababishi kikuu cha sisi kufikia hadhi ya nchi za uchumi wa kati wa chini ni uwekezaji mkubwa katika uchumi wa sekta binafsi na uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDIs) katika miongo 2 iliyopita

Kwa hivi karibuni kumekuwa na uwekezaji wa umma mkubwa katika miundombinu. Ili kuendeleza hali hii tunatakiwa tuongeze pato la Taifa (GNI) kwa haraka kuzidi ongezeko la watu, kwasababu vitu hivi vinakinzana

Je, tumefikia malengo yetu ya maendeleo? Tuliweka maono kuwa hadi kufikia 2025 sekta ya uzalishaji iwe imekua kwa 12% na kwa 2020 ifike 11% lakini 2019 tulifikia 6% tu kwahiyo tunatakiwa tuweke jitihada mara mbili yake ili kufikia malengo

Taasisi zinazosafirisha bidhaa nje ya nchi tulitaka zifike 2000+ lakini namba imeshuka kutokana na sababu kadha kwa kadha.

Kwahiyo kimsingi hatujafikia malengo, lakini ni safari. Serikali inarekebisha Mkakati wa Viwanda na nina hakika watashughulikia baadhi ya masuala ambayo yamezuia kasi ya utekelezaji

SWALI 3: Japokuwa Tanzania imekuwa miongoni mwa waliofanya vizuri kikanda kwa ukuaji mkubwa wa uchumi. Kwanini hii haijapelekea upungufu wa umaskini?

Prof. Ngowi: Aina hii ya ukuaji wa uchumi tunaiita “Ukuaji usiopunguza umasikini” na kuna sababu mbalimbali kama ifuatavyo;

1. Sekta zinazokua kwa sana (Uchimbaji madini, usafiri na huduma za kifedha) zinahusisha mitaji mikubwa inayoendeshwa na mashine na mitambo ya automatiki na haihusishi watu wengi tofauti na kilimo ambayo imekuwa ikikua kwa asilimia 3 hadi 4

Sababu ya uzalishaji ndiyo inayolipwa na huku kinachozalisha ni mtaji na si watu

2. Uhusiano hafifu baina ya sekta. Sekta zinazokua kwa haraka kama vile uchimbaji madini, usafiri na huduma za kifedha hazijawa na uhusiano mzuri na sekta nyingine.

Utakuta uchimabaji madini unakua kwa kiasi kikubwa Mwanza na Shinyanga lakini wakati huo wanatumia nyama kutoka Australia au South Afrika. Kama hamna uhusiano mzuri unaounganisha sekta hizi, watu hawafaidi matunda ya ukuaji

3. Usambazaji wa faida za uwekezaji. Japokuwa baadhi ya sekta zinakua kuliko sekta nyingine, usambazaji mzuri wa mapato kupitia kodi, sera ya fedha, na ruzuku ingeweza kuinua watu ambao ni masikini. Sisemi kuwa hii haifanyiki TZ, lakini jitihada Zaidi zinahitajika

4. Ukuaji wa uchumi sio jumuishi. Sekta zinazokua zinahitaji ujuzi mkubwa, hivyo watu wasio na ujuzi hawashiriki katika ukuaji.

Hii imebadilisha mazingatio yetu kutoka katika kutoa namba za ukuaji hadi kuanza kujiuliza ‘’Je, huu ni ukuaji unaohitajika?’’ ambao ni ukuaji unaopunguza umasikini na jumuifu

Dkt. Kilama: Tunatakiwa tuwe na sera ambazo zinagusa watu walio katika nafasi za chini kama tunataka kuona maboresho katika vipato vya watu. Hatusemi kuwa kutumia mashine ni vibaya, ila sambamba na hilo tunatakiwa kutengeneza uwezo wa watu kufanya kazi, kuzalisha na kupata kipato kinachokidhi

SWALI 4: Unafikiri vipi TZ inaweza kuendeleza kasi ya ukuaji wa uchumi katika muda wa kati. Unafikiri nini nafasi ya sekta binafsi, ubora wa mazingira ya biashara, uwekezaji katika rasilimali watu katika Mkakati wa Ukuaji wa Tanzania?

Paul Makanza: 1. Tunahitaji kuongeza uwekezaji 2. Tunahitaji kutengeneza uwepo wa fursa kwa wanawake, vijana, mikoa iliyoachwa nyuma 3. Mabadiliko ya kilimo ni muhimu kwa kuwa ni sehemu ambayo watu wengi wanafanyia kazi na umasikini umetawala katika sekta hii

Kuna nafasi ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na tumekuwa tukiwahusisha Serikali mara kwa mara. Tunawekeza katika uzalishaji wa umeme lakini bado kuna masuala ya ufikiwaji na uhakika. Bado kuna kupanda na kushuka.

Kuhusu Rasilimali watu, Tanzania hatuna usawa wa kati ya tunachozalisha na tunachohitaji. Takwimu zinaonesha kuwa tunatengeneza mameneja 3 kwa ajili ya mtaalamu mmoja wa ufundi wakati mahitaji yetu ni kinyume chake.

SWALI 5: Ni jambo gani umelichukua katika uzinduzi wa Ripoti hii?

Prof Ngowi: Jambo kuu nililotoka nalo kwenye uzinduzi huu ni kushughulikia athari zote za kiuchumi kutokana na COVID19. Tujifunze kutokana na historia. Sera Pamoja na mbinu za kiafya ziwekwe ili tusirudi nyuma

Dkt. Kilama: Tusisahau picha kubwa. Hatua tunayotaka kuchukua kwa sasa haitakiwi kuingilia mtazamo wa muda mrefu tulionao ili tuweze kuhusisha watu wengi zaidi katika ukuaji.

Tunatakiwa kukumbatia teknolojia katika kuboresha ufanisi wa mitaji na rasilimali watu. Hii inatupa sisi fursa ya kuona mengi juu ya kupanda kwa watu waliokuwa wametengwa.

Tunatakiwa tuwe na sera zinazotabirika kama jamii ya biashara inavyohitaji. Ukiwa hautabirirki wanakuwa hawana uhakika wa kipi wafanye kwa wakati husika.

Paul Makanza: Tunatakiwa kubaki na hadhi yetu ya uchumi wa kati wa chini hivyo urejeshwaji wa ukuaji wa uchumi wetu ni muhimu. Ukuaji wetu uzingatie ubora ili uweze kuhusisha watu wengi zaidi.

Nasisitiza kutumia teknolojia na ubunifu. Tunaweza kutengeneza teknolojia inayoshughulikia masuala yetu.
 

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
438
1,000
Daah kwakweli bado tuna kazi kubwa sana ya kufanya kama nchi ili kuinua uchumi wetu. Naona ripoti inatuvua nguo kabisa.

Nafikiri viongozi waache kuuambia Umma kuwa uchumi unakua kwa kasi ilihali mambo bado.

Hili suala la kujiita uchumi wa kati linatulemaza sana.
 

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
438
1,000
Kuwekwa kwa mfumo wa ndani kwa ajili ya ufuatiliaji wa COVID-19 itaiweka Serikali katika nafasi nzuri chanjo mpya zikizidi kugunduliwa. Tunaishauri Serikali kuhusisha wadau wenye ujuzi waandae mpango wa kutekeleza ugawaji wa chanjo ya COVID-19...
Naunga mkono wazo hili. Tatizo lipo kwenye utekelezaji.
 

VAPS

JF-Expert Member
Jul 10, 2012
4,799
2,000
Ninacho jua uchumi wangu unazidi kuporomoka awamu hii ya 5, inafika pahala kwa record yangu hata nashindwa kujichanganya na jamii, ibaada michango na sadaka.
 

Nyendo

JF-Expert Member
Jun 4, 2017
563
1,000
Serikali ingeanza kutoa taarifa za maambukizi na vifo vitokanavyo na COVID 19 hii ingesaidia kujua hali halisi ya athari zitokanzo na janga hili.

Pia kutoa taarifa sahihi kuhusu hali halisi ya kiuchumi kuliko kuwaambia wananchi kuwa uchumi wetu umekua kwa kasi huku hali ya maisha ya mwananchi ikizidi kuporomoka.

Naona ipo haja ya serikali kupitia upya baadhi ya misimamo yake na kuibadili ili kisaidia wananchi kuepukana na janga la Corona na pia kuisaidia nchi iimarike kiuchumi.
 

mngony

JF-Expert Member
Jul 27, 2012
4,131
2,000
Sisi tuko uchumi wa kati, hayo matakwimu yao ya kibeberu wabaki nayo huko, sisi tuko vizuri wanatuobea wivu tu.

Au nasema uongo ndugu zangu
 

Auz

JF-Expert Member
Apr 6, 2016
8,728
2,000
Nukuu kutoka katika taarifa:

'Julai 2020, Tanzania ilifikia hadhi ya uchumi wa kati wa chini baada ya jitihada za miongo miwili za ukluaji na uwekezaji ukichangiwa na hali nzuri ya uchumi wa kitaifa, wingi wa malighafi za asili na nafasi nzuri ya kijiografia'

Kumbe tuko 'Uchumi wa kati wa chini', baada ya juhudi za miongo 2, Yaani miaka 20! Hapa sidhani kama bado tuko katika hadhi hiyo kwa sasa hasa ukizingatia nukuu nyingine hii:

'Ukuaji wa idadi ya watu, utengenezwaji wa ajira wa taratibu na usio na usawa, viwango vya chini vya elimu na uwepo finyu wa nafasi za elimu na ajira hususani kwa wanawake na wasichana vimepunguza ushirikishaji wa upanuzi wa kiuchumi wa Tanzania ukipunguza makali ya upunguzaji wa umasikini.'

Wanaopenda kusifia na kusifiwa, muwe waangalifu mnamsifia nani hasa, ikiwa juhudi zilianza na Marehemu Mkapa!
 

mtume wawatu

JF-Expert Member
Oct 30, 2016
573
1,000
Naona kama swali la kama Tanzania kufikia uchumi wa kati je tumefikia malengo ya dira ya maendeleo ya 2025 limepotezewa.
 

bagamoyo

JF-Expert Member
Jan 14, 2010
11,886
2,000
Haya sasa kina Johnthebaptist na Areafiftyone tunaona kuwa COVID 19 ni suala mtambuka halifichiki kama "pembe la ngombe" inabidi lijadiliwe na athari zake kiuchumi pia kijamii ikiwemo kupoteza nguvu kazi n.k .
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom