Ripoti ya CAG: Ufanisi katika uendeshaji wa Mfuko wa Uwezeshaji wa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Katika ukaguzi wa uendeshaji wa Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, CAG amebaini Mapungufu kadhaa yakiwemo;

1) 65% ya Mikopo iliyotolewa kwenye Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu haikurejeshwa. Kwa mwaka 2019/20, CAG alionesha Mamlaka za Serikali za Mitaa 130 zilitoa Mikopo yenye thamani ya Tsh. Bilioni 42.9, lakini Tsh. Bilioni 27.8 sawa na 65% ya mikopo hiyo haikurejeshwa

2) Mamlaka za Serikali za Mitaa 28 hazikupeleka Tsh. Bilioni 3.1 katika Akaunti Maalum ya Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu. Hii ni kinyume na Kanuni ya 22 (1) na (2) ya Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za mwaka 2019

Kanuni hiyo inazitaka Mamlaka ya Serikali za Mitaa kufungua na kuendesha Akaunti Maalum ya mikopo na kuhakikisha Fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya Mikopo na Fedha za marejesho ya mikopo hiyo zinaingizwa katika Akaunti Maalum ili kufanikisha shughuli za mfuko huo

Athari
Mapungufu yaliyobainishwa yanasababisha athari zifuatazo:

1) Wanufaika wa mkopo kutorejesha TZS 27.8 bilioni na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kutopeleka TZS 3.1 bilioni katika akaunti maalumu ya Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu, kunakwamisha utekelezaji wa dhana ya kuufanya Mfuko kuwa Endelevu (Revolving Fund) kama dhamira ya uanzishwaji wa mfuko huu ulivyokuwa wakati wa uanzishwaji wake

2) Mikopo inayotolewa ingekuwa inarejeshwa, ingezipunguzia Halmashauri mzigo wa kutenga kiasi kingine cha fedha ili kuwakopesha wakopaji wengine

3) Kiasi ambacho hakikurejeshwa na kiasi ambacho hakijatengwa kimefikia jumla ya TZS 30.9 bilioni ambapo kama kiasi hicho kingekopeshwa kwa vikundi vya watu 10 na kila kikundi kupewa TZS 5 milioni kingeweza kuwasaidia watu 61,800 sawa na vikundi 6,180 nchini, hivyo kuchangia katika kupunguza umaskini kwa wananchi

Ushauri
Ili kutatua Mapungufu yaliyoibuliwa na CAG, WAJIBU inashauri yafuatayo;

1) Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na Asasi Zisizo za Kiserikali zimeshirikiana katika kuandaa muongozo wa usimamizi na uendeshaji wa Mfuko wa Uwezeshaji wa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu. Hivyo, washirikiane katika utoaji wa mafunzo ya muongozo huo kwa wadau mbalimbali ili kuboresha usimamizi wa mfuko

2) Waheshimiwa Wabunge na Madiwani waitangaze mikopo hii kwa wananchi wao na wawahimize wanaokopa kurejesha mikopo hiyo bila usumbufu ili kunufaisha wananchi wengine

3) Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri wabandike orodha ya wanaodaiwa kwenye mbao za matangazo kwa kila kata kwa kila robo mwaka ili kusaidia kuhimiza urejeshwaji wa mikopo hii kwa wakati.

WAJIBU INSTITUTE
 
Back
Top Bottom