Ripoti ya CAG: Hali ya Utekelezaji wa Mapendekezo ya Miaka Iliyopita

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Sehemu hii, inazungumzia utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na CAG pamoja na maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)

Hali ya Utekelezaji wa Mapendekezo ya CAG kwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI
Ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2019/20 inaonesha kuwa, kati ya mapendekezo 15 yaliyotolewa na CAG mwaka 2018/19, OR – TAMISEMI haikutekeleza pendekezo lolote kikamilifu, mapendekezo 6 sawa na asilimia 40 yapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, mapendekezo 5 sawa na asilimia 33 hayajatekelezwa na mapendekezo 4 sawa na asilimia 27 yamejirudia.

Mwenendo wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya CAG katika Miradi ya Maendeleo

Ripoti ya CAG ya Miradi ya Maendeleo ya mwaka 2019/20 inaonesha kati ya mapendekezo 3,126 yaliyotolewa na CAG mwaka 2018/19, ni mapendekezo 1,071 sawa na asilimia 34 ndiyo yametekelezwa kikamilifu; mapendekezo 623 sawa na asilimia 20 yapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji; mapendekezo 1,024 sawa na asilimia 33 hayajatekelezwa; mapendekezo 245 sawa na asilimia 8 yamejirudia kwa kuwa hayajatekelezwa kwa muda mrefu na hayajapitwa na wakati na mapendekezo 163 sawa na asilimia 5 yamepitwa na wakati.

Kiujumla, ripoti ya CAG inaonesha utekelezaji wa mapendekezo bado upo chini ya asilimia 50. Hali hii, inasababisha kupungua kwa ufanisi na umahiri katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hali ya Utekelezaji wa Maagizo ya Kamati ya LAAC
Kamati ya LAAC, hupitia ripoti ya CAG ya mwaka husika pamoja na kuwahoji Maafisa Masuuli juu ya hoja zilizoibuliwa na CAG kisha hutoa maagizo ambayo yanapaswa kutekelezwa na Maafisa Masuuli husika

Hali ya utekelezaji wa maagizo ya LAAC katika ripoti ya mwaka 2019/20 inaonesha kwamba; kati ya maagizo 811 yaliyotolewa kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa 151, ni maagizo 350 sawa na asilimia 43 ndiyo yaliyotekelezwa kikamilifu, maagizo 278 sawa na asilimia 34 yanaendelea kutekelezwa, maagizo 161 sawa na asilimia 20 hayajatekelezwa na maagizo 22 sawa na asilimia 3 yalipitwa na wakati

Utekelezaji wa maagizo ya LAAC umepanda kwa asilimia 2 kutoka asilimia 41 ya mwaka 2018/19 hadi asilimia 43 ya mwaka 2019/20

Athari
Kutotekelezwa kwa mapendekezo ya CAG na maagizo ya LAAC kunasababisha athari zifuatazo:

1) Utekelezaji hafifu wa mapendekezo yanayotolewa na CAG unapunguza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo
2) Kukosekana kwa thamani ya fedha katika miradi inayotekelezwa, na
3) Kuwanyima wananchi fursa ya kunufaika na miradi ya maendeleo

Ushauri
Ili kuongeza utekelezaji wa mapendekezo ya CAG na maagizo ya LAAC, WAJIBU inashauri yafuatayo:

1) Halmashauri kupitia vikao vya Mabaraza ya Madiwani kuendelea kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo mbalimbali yanayotolewa na CAG. WAJIBU inashauri taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya CAG na kamati ya LAAC ifanywe kuwa agenda ya kudumu katika vikao vya mabaraza ya madiwani

2) Asasi za kiraia vikiwemo Vyombo vya Habari kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa mapendekezo ya CAG pamoja na maagizo ya LAAC ili kwa pamoja wawe na uwezo wa kudai uwajibikaji katika Halmashauri husika

3) OR-TAMISEMI kuzidi kuimarisha mikakati ya utekelezaji wa mapendekezo ya CAG na kamati ya LAAC, ikiwezekana kuweka adhabu kwa Halmashauri ambazo zitashindwa kutekeleza mapendekezo hayo bila kuwa na sababu za msingi

WAJIBU INSTITUTE
 
Back
Top Bottom