RIPOTI MAALUMU: Mtandao wa uhalifu wageukia biashara ya binadamu

sir.JAPHET

JF-Expert Member
May 18, 2012
699
133
Sunday, 12 August 2012 00:10

Waandishi Wetu
MTANDAO wa uhalifu wa kimataifa sasa umegeukia kwenye biashara haramu ya usafirishaji binadamu, Mwananchi Jumapili limebaini.Uchunguzi wa muda mrefu wa gazeti hili umebaini kuwa, wafanyabiashara haramu hao husafirisha raia wa Ethiopia na Somalia kupitia nchini Tanzania nchi jirani za Malawi na Zambia ambao pia mawakala wao huwasafirisha nchi nyingine hado Afrika Kusini ambako husafirishwa kwenda nchi za Ulaya.
Uchunguzi uliofanywa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo mipaka, unaonyesha kuwa, mtandao huo wa uhalifu wa kimataifa unajipatia mabilioni ya fedha kila wiki kutokana na usafirishaji raia hao.

Ingawa biashara hiyo imekuwa ikipigwa vita na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwamo wa Tanzania, imeshindikana kudhibitiwa kutokana na faida kubwa wanayopata watu waliopo katika mtandao huo.

Mmoja wa watu walio karibu na wanaojihusisha na biashara hiyo ya kusafirisha binadamu, anayeishi mkoani Arusha alieleza kuwa mawakala wa kazi hiyo hujipatia mamilioni ya fedha kwa mwezi.

“Haya ni mavuno mapya, huwezi kuamini mtandao wa dawa za kulevya sasa umehamia katika biashara hii, inalipa mno tena kwa haraka. Serikali haiwezi kuidhibiti,” alisema mtu huyo.

Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa mtandao huo wa wahamiaji haramu unaanzia nchini Ethiopia, ambapo kinara wa biashara hiyo ambaye pia ndiye anayeratibu mtandao huo, huwakusanya na kuwapatia usafiri wahamiaji hao hadi Kenya.
Nchini Kenya kuna wakala mwingine, ambaye huratibu safari za watu hao hadi kufika Tanzania wakitumia eneo la mpaka la Wilaya ya Longido, Arusha, Holili na Taveta mkoani Kilimanjaro.
Ethiopia yaunda kamati
Juni mwaka huu vyombo vya habari vya Ethiopia viliripoti kuwa Serikali ya nchi hiyo imeunda kamati maalumu inayoshirikisha mawaziri 13, watendaji wa Serikali, vyombo vya habari na taasisi za dini kuzuia raia wa nchi hiyo kukimbia nchi yao.
Katika mazungumzo yao yaliyokuwa chini ya Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo na Waziri wa Mambo ya Nje, Haile-Mariam Dessalegn, kamati hiyo ilikubaliana kudhibiti maeneo yote ya mipaka ya nchi hiyo ili kuzuia biashara hiyo haramu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Balozi Dina Mufti aliliambia gazeti la nchi hiyo la Herald kuwa, kamati hiyo imebaini kuwa, binadamu kusafirishwa kama bidhaa kwenda nje ya nchi ni jambo baya na kusisitiza kwamba, wadau wote watashirikishwa kulipatia ufumbuzi.

Longido
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa kutoka Nairobi, mawakala hao huwasafirisha watu hao kuingia nchini na kuwakabidhi kwa mawakala wengine wanaoishi Namanga mkoani Arusha kupitia vijiji vilivyopo mpakani katika Wilaya ya Longido.

Baadhi ya vijiji hivyo ni Matare kilichopo Kata ya Matare, Kamwanga, Sinya na vijiji vingine ambavyo wanakijiji wake hupewa pesa kwa ajili ya kuwahifadhi na kuwavusha wahamiaji hao haramu hadi eneo la Barabara ya Namanga Arusha, ambapo hupata usafiri wa malori na magari madogo kuelekea Mbeya.

Mwenyekiti wa kijiji
Mwenyekiti cha Longido, Justinian Ngemela aliliambia Mwananchi Jumapili, katika kijiji chao wameamua kuanzisha ulinzi wa Sungusungu kukabiliana na biashara hiyo.
Alibainisha kuwa, baadhi ya Watanzania wasio waaminifu ni mawakala wa biashara hiyo.
“Tumeanzisha ulinzi wa Sungusungu mitaani usiku ili kudhibiti biashara hii ya kusafirisha wahamiaji haramu kupitia kijijini kwetu,” alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema kuwa baadhi ya wanavijiji wanaoishi katika eneo la mpaka na Kenya hupewa fedha na mawakala wa biashara hiyo kwa ajili ya kuwahifadhi kwa muda kabla ya kuwasafirisha kuelekea Tunduma,
mkoani Mbeya.

Kamishna Uhamiaji
Kamishna Mkuu wa Idara ya Uhamiaji nchini, Magnus Ulungi amekiri kushamiri kwa vitendo vya usafirishaji wa binadamu nchini akisema kuwa, pamoja na biashara hiyo kuongezeka idara yake imejizatiti kuhakikisha wanauvunja mtandao huo wa watu wanaojihusisha na biashara haramu nchini.
Kamishna Uhamiaji Arusha
Kamishna Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Daniel Namomba alisema kuwa, tatizo la wahamiaji haramu lipo na kwamba wamejipanga kulidhibiti.
Alibainisha kuwa, hivi sasa wanafanya doria katika maeneo mbalimbali na kuwahamasisha wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kuzuia wahamiaji hao haramu.
Namomba alieleza kuwa, kuanzia Januari hadi Desemba 2011, waliwakamata wahamiaji haramu 328 na Januari hadi Juni mwaka huu 88 wakiwamo Waethiopia na Wasomali waliokuwa wakisafirishwa.
Hata hivyo, alisema kuwa, pamoja na mafanikio wanakabiliana na changamoto nyingi ikiwamo ukubwa wa eneo la mpaka wa Tanzania na Kenya unaofikia urefu kilometa 450 kwa Mkoa wa Arusha tu.

Njia wanayopita
Kwa mujibu wa gazeti la Herald linalochapishwa nchini Ethiopia la Juni mwaka huu, njia wanayoitumia wahamiaji hao haramu kutoka Ethiopia kuingia Kenya ni Moyale, Wajir, Horr na Turkana.

Matajiri wanaofanya biashara hiyo huwasafirisha Waethiopia hao kutoka eneo la Moyale hadi Marsabit na Isiolo nchini Kenya, ambako kuna mawakala wao.

Uchunguzi unaonyesha kuwa mawakala hao huwasafirisha hadi Nairobi, kabla ya kuwasafirisha hadi eneo la vijiji vya mpakani mwa Tanzania na Kenya.

Utafiti unaonyesha kuwa wastani wa Waethiopia 100 huingia Nairobi kila siku na baadaye kuingia nchini Tanzania wakiwa njiani kuelekea Afrika Kusini.

Wakiwa nchini Kenya, wahamiaji hao haramu hulipa wastani wa Sh50,000 za Kenya (Sh900,000 za Tanzania), kila mmoja ili kuwasafirisha kutoka Moyale na Isiolo hadi Nairobi.
Kilimanjaro
Biashara hiyo haramu ya usafirishaji binadamu inayoambatana na uingizaji wa mirungi kutoka Kenya, inazidi kushika kasi mkoani Kilimanjaro.
Habari zimedai kinara wa biashara hiyo ambaye anaratibu usafirishaji wa binadamu kupitia mpaka wa Holili na Taveta yupo nchini Kenya.
Kinara huyo huwalipa mawakala kati ya Dola za Marekani 2000 na 4000 kwa mgeni anayesafirishwa kutoka Mombasa, Kenya hadi Mbeya, Tanzania.
Wahamiaji hao haramu huingia mkoani Kilimanjaro kupitia njia za panya za mipakani zilizopo katika wilaya za Siha, Rombo, Same, Mwanga na Moshi Vijijini na kuhifadhiwa kwenye nyumba za wenyeji.
Maeneo ambayo yamekithiri kwa biashara hiyo ni Tarakea, wilayani Rombo, Kitobo, Kilototoni na Mabungo, Wilaya ya Moshi Vijijini, Chekereni na Kifaru wilayani Mwanga.
Wanavyoingizwa nchini
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kwa Moshi Vijijini, wahamiaji hao haramu huanzia eneo la Kitobo na kusafirishwa kwa pikipiki ambazo hulipiwa Sh20,000 kwa safari.
“Wakishavushwa na pikipiki hadi Chekereni wanahifadhiwa kwenye nyumba nne za wenyeji zilizopo kabla ya kuvuka reli na wengine karibu na mnada hapo Chekereni,” alidokeza mtoa habari wetu.
Wahamiaji wengine haramu huhifadhiwa katika nyumba zilizopo Mabungo, Kifaru na Kilototoni, ambapo huhudumiwa kwa kupewa chakula, mikate mikavu na maji ya kunywa ya chupa.
Kwa upande wa wilayani Rombo, huingizwa nchini kupitia vijiji vya Nayeme, Leto na Kikelelwa na kuhifadhiwa kwa muda katika nyumba za wenyeji kabla ya kusafirishwa hadi Chekereni.
Mbali na wilaya hizo, kwa Wilaya ya Mwanga wahamiaji haramu huhifadhiwa katika vijiji vya Kivisini, Ziwa Jipe,Toloha na kusafirishwa hadi karibu na Hifadhi ya Mkomazi au Ndungu.
Njia mpya
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini njia mpya kabisa ambayo vyombo vya ulinzi na usalama havijaweza kuigundua inaanzia Mwanga kwenda Nyumba ya Mungu hadi Orkasment wilayani Simanjiro.
Mmoja wa madereva ambaye amekuwa akikodishwa kusafirisha wahamiaji alisema; “Njia hiyo baadaye hutokea Wilaya ya Kiteto na kisha Mikumi na kushika Barabara Kuu ya Morogoro hadi Iringa. Njia hii haijazoeleka hata polisi hawajui; badala yake hupewa Sh20,000, hawakagui gari.”
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali wakiwamo wananchi wanaoishi vijiji vya mpakani, wamekuwa wakishuhudia wahamiaji haramu wakikamatwa na polisi na maofisa Uhamiaji usiku wa manane.
Hata hivyo, wananchi hao wamedai baadaye maofisa hao ‘humalizana’ na mawakala wa biashara hiyo.
RPC Kilimanjaro
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema biashara hiyo inazidi kushamiri kutokana na baadhi ya wananchi kukosa uzalendo.
“Tatizo kubwa ni kwamba, baadhi ya Watanzania si wazalendo wanawahifadhi kwenye nyumba zao, kuwatafutia usafiri na kuwasafirisha na kuwafundisha kukwepa vyombo vya dola,” alisema Kamanda Boaz.
Hata hivyo, Kamanda Boaz alisema kuwa, pamoja na changamoto hizo nyingi, vyombo vya dola vimefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu zaidi ya 800 kuanzia Januari hadi Julai, mwaka huu.

Jeshi la Polisi Tanga

Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Coustantine Massawe anakiri wakimbizi hao kupitia katika mkoa wake hasa Wilaya ya Handeni wakielekea mkoani Mbeya.

Hata hivyo, alisema kwa kushirikiana na wananchi waaminifu polisi wamekuwa wakiwatia mbaroni wageni.

Kamanda Massawe alisema jeshi hilo limejipanga vyema kuhakikisha kuwa mawakala wa biashara hiyo wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa, mawakala huyasindikiza magari yaliyobeba wahamiaji haramu ili kuhakikisha kuwa wanafika salama kwa kutoa rushwa ya pesa nyingi.

Habari zaidi zinadai kuwa mawakala hao huwapa askari polisi kati ya Sh5,000,000 hadi 10 milioni ili kuwaruhusu kupita.

Tunduma
Kuonyesha kuwa mtandao huo ni mkubwa na wenye nguvu, baadhi ya mawakala wa biashara hiyo waliopo Tunduma wenye asili ya Kisomali wamejenga nyumba maalumu kwa ajili ya kuhifadhia watu hao.

Nyumba hizo ambazo zipo eneo la Tunduma mjini zimejengwa zikiwa na madirisha madogo mithili ya majengo ya magereza ili waliomo ndani wasionekane kwa urahisi.

Mtu mmoja ambaye yupo karibu na mawakala hao aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa: “Pamoja na kuwa zina uwezo wa kujaza watu wengi zaidi ya 100, lakini wakati mwingine hujaa na mawakala kulazimika kukodi nyumba jirani.”
Alisema kuwa mtu akihifadhi wahamiaji wawili kwa wiki moja hulipwa Sh 350,000 wakitafutiwa usafiri wa kuingia Zambia kuelekea Afrika Kusini.
Kamanda Mbeya
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani alisema kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kwa kutumia njia za kiitelijensia kudhibiti vitendo hivyo.

Alisema huwa wanafanya msako wa kuwakamata wamiliki wa nyumba zinazotumika kuwahifadhi wahamia
 
Back
Top Bottom