Ripoti kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Ufanisi Mwaka wa Fedha 2022/23

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
3,082
12,533
CAG amewasilisha Ripoti hii Kwa mujibu wa Kifungu cha 143 (4) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na Kifungu cha 28 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma, Sura ya 418, kuhusu Ukaguzi wa Ufanisi kwa kipindi kinachoishia tarehe 31 Machi 2024

MUHTASARI

Taarifa hii ya jumla ya ukaguzi inaelezea upungufu uliobainika, hitimisho, pamoja na mapendekezo katika ripoti 14 za ukaguzi wa ufanisi zilizofanyika kwa mwaka wa fedha wa 2023/24. Ripoti hizo 14 zilihusu upatikanaji wa huduma za afya ya akili; udhibiti wa vifaatiba katika hospitali na vituo vya afya vya umma; udhibiti wa mazao ya biashara; udhibiti wa usambazaji wa mbolea kwa wakulima; udhibiti wa elimu ya ufundi nchini; uendelezaji, ufuatiliaji, na tathmini ya umahiri wa watumishi katika sekta za umma; utekelezaji wa programu za urekebu kwa wafungwa; usimamizi wa mipango miji; usimamizi na ufuatiliaji wa watoa huduma za bima nchini; usimamizi wa urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; usimamizi wa fukwe; uwezeshaji wa wachimbaji wadogo wa madini; usimamizi wa rasilimali za uvuvi; na usimamizi wa uingizaji wa mafuta nchini.

Ripoti hii inasisitiza kuwa na mtazamo na tathmini ya kina kutoka kwenye ripoti hizi 14 za ukaguzi kwa kuhusisha matokeo tarajiwa na mchango wake kwenye malengo yaliyowekwa kwenye Mpango wa Pili (2016/17-2020/21) na Tatu (2021/22 – 2025/26) wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano; na ulingano wake kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Kwa kuainisha maeneo muhimu ambayo yameonekana katika sekta tofauti, na kutathmini ufanisi wa taasisi za umma, ripoti hii ya jumla inalenga kuleta mafanikio na kutambua umuhimu wa shabaha za mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo ya rasilimali watu kwenye mipango ya maendeleo. Vilevile, inatoa mchanganuo wa kina kuhusu namna ambavyo usimamizi wa shuguli za kisekta zinavyochochea ufikiwaji wa Mpango wa Pili na Tatu wa Maendeleo wa Taifa na Malengo ya Maendeleo Endelevu, hivyo kutoa mwongozo wa maboresho ya kimkakati na utungaji wa sera.

Hata hivyo, ripoti hii haikusudii kuwa mbadala wa ripoti 14 zilizofanyika. Hivyo, kwa taarifa zaidi, msomaji anashauriwa kusoma ripoti za ukaguzi husika kama zilivyoanishwa hapo juu.

Matokeo ya Ukaguzi

(a) Upatikanaji wa Huduma Bora za Afya


Sehemu hii inawasilisha matokeo ya ukaguzi wa hali ya upatikanaji wa huduma za afya ya akili na udhibiti wa vifaatiba katika vituo vya afya vya umma.

Upatikanaji wa huduma za afya ya akili

Ukaguzi unatambua jitihada za Serikali za kuunganisha huduma za afya ya akili kwa ufanisi katika ngazi ya taifa. Hata hivyo, maeneo yafuatayo yanahitaji maboresho zaidi:

Kutofanyika kwa ufanisi utambuzi wa wagonjwa wa afya ya akili katika ngazi ya jamii: Ukaguzi ulibaini kutokuwapo kwa utambuzi wa watu wenye matatizo ya akili katika ngazi ya jamii. Badala yake, utambuzi ulilenga watumiaji wa dawa za kulevya, wazee, walemavu, watoto walio katika mazingira magumu, na wale waliopata mimba za utotoni. Hali hii lichangiwa na ukosefu wa fedha za kutosha kwa ajili ya huduma za ustawi wa jamii na kukosekana kwa Maofisa ustawi wa jamii katika ngazi za chini, vikiwemo vijiji na mitaa.

Ukosefu wa huduma za kisaikolojia katika ngazi ya jamii: Ukaguzi ulibaini kutokuwapo kwa huduma za kisaikolojia katika ngazi ya jamii. Hali hii ilitokana na huduma za matunzo ya kisaikolojia na usaidizi kutokuingizwa kikamilifu katika mipango, bajeti, sera, programu, afua, na mikakati kwa ngazi zote za vituo vya kutolea huduma za afya. Udhaifu huu ulisababisha kutokuwapo kwa huduma kamili kwa makundi mbalimbali, wakiwemo wagonjwa wa akili.

Rasilimali zisizotosheleza (wataalamu, miundombinu, vifaatiba, na dawa) na kutopatikana kwa huduma za utengamo: Ukaguzi ulibaini kuwapo kwa upungufu wa wataalamu, miundombinu, vifaatiba, na dawa katika ngazi zote za vituo vya kutolea huduma za afya. Kukosekana kwa wataalamu hao kulichangiwa na Wizara ya Afya kutokuwa na mpango wa kuajiri wataalamu wa afya ya akili na kutokuwapo kwa muundo wa utumishi unaowajumuisha wahitimu wa taaluma ya huduma za afya ya akili. Pia, kulikuwa na ukosefu wa huduma za utengamo kwa ajili ya kuendeleza ujuzi, ushirikiano wa jamii, na misaada inayozingatia urejeshaji, ambapo ilibaininka kuwa kati ya mikoa 28, ni mikoa mitano tu ndiyo ilikuwa na vituo vya utengamo kwa ajili ya huduma za afya ya akili ambayo ni Kilimanjaro, Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma, na Kigoma.

(ii) Udhibiti wa vifaatiba katika vituo vya afya vya umma

Ukaguzi unatambua jitihada za Serikali kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba Tanzani kwa kuanzisha idara ya kudhibiti vifaatiba. Pia, Wizara ya Afya imeanzisha Mfumo wa Usimamizi wa Vifaatiba katika Vituo vya Afya vya Umma. Hata hivyo, ukaguzi ulibaini maeneo yafuatayo yanayohitaji maboresho zaidi:

Kuwapo kwa vifaatiba visivyofanya kazi nchini: Ukaguzi ulibaini kuwapo kwa vifaatiba visivyofanya kazi katika vituo vya afya vya umma 18 vilivyotembelewa sawa na asilimia 27 ya vifaatiba, huku asilimia kubwa ya vifaatiba visivyofaa vikibainika katika kanda ya kati.

Kutozingatiwa ipasavyo taratibu za usajili wa vifaatiba: Ukaguzi ulibaini kuwa

Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba Tanzania haikuwa na kumbukumbu za kutosha ya asilimia 56 ya vifaatiba vilivyosajiliwa. Zaidi ya hayo, hakukuwa na uhuishaji wenye ufanisi wa vyeti vya usajili wa vifaatiba unaofanywa na Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba Tanzania. Pia, asilimia 51 ya wenye usajili wa vifaatiba hawakulipa ada ya mwaka ya kuhifadhi. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilipoteza mapato ya shilingi 10,261,473,750 ya ada ya uhuishaji wa usajili wa vyeti vya vifaatiba na kiasi cha shilingi 241,040,000 kwa ajili ya ada ya mwaka ya kuhifadhi vifaatiba vyao vilivyosajiliwa kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2022/2023.

Ukaguzi ulibaini kuwa haya ni matokeo ya kutokuwa na ufanisi wa udhibiti wa vifaatiba vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi na vituo vya afya vya umma pamoja ufuatiliaji na usimamizi duni wa Wizara ya Afya.

(b) Usimamizi wa Shughuli za Kilimo

Ukaguzi wa usimamizi wa shughuli za kilimo ulihusisha udhibiti wa mazao ya biashara na udhibiti wa usambazaji wa mbolea kama inavyofafanuliwa hapa chini.

Udhibiti wa mazao ya biashara

Ukaguzi unatambua juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Bodi za Udhibiti wa Mazao katika kufanikisha uzinduzi wa mnada wa chai wa Dar es Salaam. Lengo la mnada huo lilikuwa kuongeza mapato, kuboresha ubora wa chai, na kulinda uasili wa chai ya Tanzania. Zaidi ya hayo, serikali ilianzisha mfumo wa kidijiti wenye lengo la kufanya mnada kwa njia ya mtandao. Hatua hii itasaidia kupunguza urasimu na kuboresha uwazi. Hata hivyo, maeneo yafuatayo yanahitaji maboresho zaidi:

Kulikuwa na mabadiliko makubwa ya mchango wa tasnia ya tumbaku na chai kwenye uchangiaji wa pato la taifa: Ilibainika kuwa chai ilipunguza uchangiaji wake kwa miaka mingi, ambapo katika mwaka wa fedha 2022/23, ilipungua kutoka dola za Marekani 43,213,662 hadi dola za Marekani 32,258,827. Upungufu huo ni wa dola za Marekani 10,954,835 (sawa na asilimia 26). Wakati huohuo, Tumbaku ilikuwa na upungufu wa asilimia 28, ambalo ni anguko la dola za Marekani 81,059,709.01. Tathmini zaidi imeonesha kuwa mchango wa korosho ulishuka kutoka dola za Marekani 209,115,498 hadi dola za Marekani 139,994,994 kuanzia mwaka 2021/22 hadi mwaka 2022/23, ikiwa ni upungufu wa asilimia 33.

Sababu kubwa ilikuwa kutokuwapo kwa Maofisa ugani wa kutosha kwa ajili ya kusimamia uzalishaji wa mazao ya biashara. Hali hiyo ilisababisha kupungua kwa mchango wa kilimo cha mazao hayo ya biashara katika pato la taifa.

Bodi za mazao zilikuwa na upungufu wa wakaguzi wa mazao kwa wastani wa asilimia 53. Ukaguzi ulibaini kuwa Bodi ya Chai ilikuwa na upungufu wa wakaguzi wa mazao kwa asilimia 89; Bodi ya Tumbaku ilikuwa na upungufu wa wakaguzi wa mazao kwa asilimia 42; Bodi ya Korosho ilikuwa na upungufu wa wakaguzi wa mazao kwa asilimia 75; na Bodi ya Kahawa ilikuwa na upungufu wa wakaguzi wa mazao kwa asilimia 7. Chanzo cha upungufu huo wa wakaguzi wa mazao ni kutoweka kipaumbele kwa shughuli ya ukaguzi wa mazao, hivyo kusababisha kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya biashara.

Udhibiti wa usambazaji wa mbolea

Serikali, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea, ilianzisha mpango wa ruzuku ya mbolea kwa lengo la kupunguza gharama za upatikanaji wake kwa wakulima. Matumizi ya mbolea yaliongezeka kutoka tani za ujazo wa metriki 363,599 mwaka 2021/22 hadi kufikia tani za ujazo wa metriki 440,795 mwaka 2022/23. Hata hivyo, maeneo yafuatayo yanahitaji maboresho zaidi:

Upatikanaji mdogo wa mbolea na virutubisho vya mimea kwa wakulima: Ilibainika kuwa wafanyabiashara 1,712 kati ya 4,136 wote waliosajiliwa katika mpango wa ruzuku (sawa na asilimia 41) hawakuuza wala kusambaza mbolea za ruzuku kwa wakulima katika maeneo yao. Pia, ilibainika kuwa wakulima 2,551,239 kati ya 3,389,951 waliosajiliwa katika mpango wa ruzuku (sawa na asilimia 75) hawakupata wala kutumia mbolea kupitia mpango wa ruzuku licha ya kuwa na sifa ya kupata mbolea hiyo ya ruzuku. Hali hii ilisababishwa na makisio yasiyojitosheleza ya mahitaji ya mbolea na kutosambaza mbolea kwa wakati, hivyo kuchelewesha mbolea kupatikana kwa wakulima. Hali hii ilisababisha matumizi duni ya mbolea kwa wakulima hivyo kupunguza uzalishaji wa mazao.

Makisio hafifu ya mahitaji ya mbolea na virutubisho vya mimea: Ilibainika kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea haikuwa na utaratibu madhubuti wa makisio ya mahitaji ya mbolea nchini ili kupata mbolea ya kutosha. Ilibainika kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea haikuwa na utaratibu, mfumo, au programu madhubuti ya kuainisha mahitaji na matumizi ya mbolea ili kupata taarifa sahihi za kiwango na aina ya mbolea inayohitajika. Uhaba wa Maofisa ugani ndio ulisababisha udhaifu katika ukusanyaji wa mahitaji katika ngazi ya kijiji, ambayo yalihitajika ili kupata taarifa sahihi za kiasi cha mbolea kinachoitajika na kinachoendana na aina ya udongo katika vijiji vyao. Kutokana na hali hiyo, takwimu za makisio ya mahitaji ya mbolea yalikuwa makubwa kuliko matumizi halisi ya maeneo husika kwa asilimia kati ya 14 na 48.

(c) Maendeleo ya Rasilimali watu

Ukaguzi wa maendeleo ya rasilimali watu ulibaini udhaifu katika udhibiti wa elimu ya ufundi nchini; uendelezaji, ufuatiliaji, na tathmini ya umahiri wa watumishi katika sekta za umma; na utekelezaji wa mpango wa urekebu kwa wafungwa, kama inavyofafanuliwa hapa chini.

Udhibiti wa elimu ya ufundi nchini

Ukaguzi huu unatambua jitihada zinazofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia katika udhibiti wa elimu ya ufundi kwa kuhakikisha kuwa elimu ya ufundi inayotolewa nchini ni ya viwango vinavyoakisi mahitaji ya soko la ajira. Hata hivyo, ukaguzi ulibaini udhaifu unaohitaji maboresho zaidi kama inavyoelezwa hapa chini.

Udhibiti usiotosheleza wa utoaji elimu ya ufundi na mafunzo yenye kuendana na mahitaji ya soko la ajira: Ukaguzi uligundua kuwa, kulikuwa na kutofautiana kwa ubora wa ujuzi kutoka kwa wahitimu na mahitaji ya mwajiri au mahitaji katika sekta za umma na za binafsi. Hii hii ilichangiwa na upungufu wa tathmini ya mahitaji yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira. Hali hii ilihusishwa na idadi ndogo ya mafundi-mchundo waliohitimu kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kusababisha ukuaji mdogo wa sekta za kiuchumi.

Mchakato usioridhisha wa usajili na utoaji wa ithibati kwa taasisi za ufundi na walimu wa ufundi: Ukaguzi ulibaini upungufu katika mchakato wa usajili na utoaji wa ithibati kwa vyuo vya ufundi kutokana na kushindwa kutimiza matakwa ya usajili, kama vile uandikishaji wa wanafunzi wasio na sifa, kuwa na watumishi wachache wa kitaaluma, na kutokuwa na vifaa vya kufundishia. Pia, ukaguzi ulibaini usajili usioridhisha wa wakufunzi wa ufundi, ambapo usajili ulikuwa kwa asilimia 67 kwa mwaka wa fedha 2019/20 na asilimia 56 mwaka wa fedha 2022/23.

Uendelezaji, ufuatiliaji, na tathmini ya umahiri wa watumishi katika sekta za umma

Ukaguzi unatambua jitihada zinazofanywa na Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika kuboresha uwezo wa watumishi nchini. Hata hivyo, ukaguzi ulibaini upungufu unaohitaji maboresho zaidi kama ilivyoelezwa hapa chini.

Kuwapo kwa taasisi za umma zilizokuwa na watumishi wasio na umahiri: Ukaguzi ulibaini kuwa taasisi za umma hazikufikia ufanisi wa kiwango cha juu katika utendaji wa kitaasisi, kiasi cha kuziwezesha taasisi zinazoingiza mapato kupata faida, na taasisi zinazotoa huduma kuzalisha ziada kutokana na utendaji
madhubuti. Matokeo yake, uwezo duni wa watumishi ulichangia utendaji usio na ufanisi katika taasisi za serikali na kusababisha kushuka kwa tija, kiwango kikubwa cha watumishi kuacha kazi, kushindwa kukua kwenye soko la ushindani, kushuka kwa mauzo na faida na kushuka kwa soka la hisa.

Utambuzi na uchambuzi usioridhisha wa upungufu wa ujuzi wa watumishi katika taasisi za umma: Ukaguzi ulibaini kuwapo kwa utambuzi na uchambuzi usioridhisha wa upungufu wa umahiri kwa watumishi katika taasisi za umma zilizotembelewa. Upungufu huo uliathiri uendeshaji wa programu za kujenga uwezo wa watumishi katika taasisi za umma. Ukaguzi ulibaini upungufu kadhaa, ikiwa pamoja na mipango duni ya utambuzi wa ujuzi kwa watumishi wa umma, kushindwa kufanya tathmini ya upungufu wa rasilimali watu, na kushindwa kudumisha orodha ya ujuzi katika taasisi za umma.

Sababu kuu ya kushindwa kufanya uchambuzi wa upungufu wa rasilimali watu ni mkabala finyu wa uandaaji wa tathmini ya mahitaji ya rasilimali watu, ikiwamo kufanya uchambuzi wa mahitaji ya watumishi wanaohitaji kupewa mafunzo ya kawaida kwenye taasisi za umma. Ingawa ni muhimu, tathmini ya mahitaji ya mafunzo kwa watumishi wa umma ina mchango mmoja tu kwenye tathmini ya kina ya kubainisha upungufu wa rasilimali watu.

Maandalizi yasiyo na ufanisi ya programu za uendelezaji wa ujuzi: Ukaguzi uligundua kuwapo kwa tofauti kati ya mipango iliyoandaliwa inayolenga kuongeza umahiriwa watumishi na upungufu wa kiutendaji uliobainishwa kutoka kwa watumishi. Hali hii ilisababishwa na kutoshirikisha wadau kwa asilimia 75 kwa taasisi zote isipokuwa Wizara ya Maji ambayo upungufu huu ulikuwa ni kwa asilimia 50.

(iii) Utekelezaji wa Mpango wa Urekebu kwa Wafungwa

Serikali imefanya jitihada mbalimbali za kuboresha programu za urekebishaji wafungwa kwa kuanzisha Kitengo cha Huduma za Urekebu wa Wafungwa chini ya Jeshi la Magereza Tanzania. Pia, Jeshi la Magereza lilianzisha gereza la shule ya ufundi, Ruanda - Mbeya na gereza la vijana, Wami - Morogoro, na kuanzisha Stashahada ya Sayansi ya Urekebu kwa Maofisa wa magereza katika Chuo cha Mafunzo ya Urekebu Tanzania. Hata hivyo, maeneo yafuatayo yanahitaji maboresho zaidi.

Kuongezeka kwa kiwango cha wafungwa wanaorudia makosa kwa wastani wa asilimia 1.5 kuanzia mwaka 2019 hadi 2023: Ukaguzi ulibaini ongezeko la wafungwa wanaorudia makosa kwa wastani wa asilimia 1.5 kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, licha ya mipango ya urekebu. Hali hii inaonesha kuwa wafungwa zaidi wanarudi kwenye kufanya uhalifu. Kiwango cha kurudia kufanya makosa kilikuwa hakiendani na muda wa wafungwa gerezani. Wafungwa wengi zaidi walio na hukumu fupi walirudia makosa. Kati ya mwaka 2019 na 2023, hali ya wafungwa waliorudia kufanya makosa ni kama ifuatavyo: asilimia 59.22 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha chini ya mwaka mmoja (1); asilimia 24.65 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha kuanzia mwaka mmoja (1) hadi miaka mitatu (3); asilimia 10.14 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka 3 hadi 5; na asilimia 3.09 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka 5 hadi 10. Pia, asilimia 0.37 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka 10 hadi 15; asilimia 2.22 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka 15 hadi 20; asilimia 0.32 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka 20 hadi 30; na asilimia 0.01 walikuwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka 30.

Hali hii ilisababishwa na ukosefu wa mitaala na miongozo ya magereza kwa ajili ya uendelezaji rasmi wa mipango ya urekebu; uainishaji na utengano wa wafungwa kujikita kwenye jinsia na umri pekee; miundombinu isiyotosheleza ya uainishaji; shughuli za msingi za gereza kuamua uainishaji; na ukosefu wa sera na miongozo ya uainishaji wa wafungwa.

Kukosekana kwa mipango rasmi ya kuunganisha wafungwa wanaotarajia kukamilisha vifungo vyao: Ukaguzi ulibaini kuwa licha kuwapo kwa programu za urekebu, hakukuwa na mpango rasmi wa kuwaanda wafungwa wanaokaribia kukamilisha muda wao wa kifungo ili kuwaandaa kukabiliana na jamii watakayoenda kuishi ikiwemo changamoto kadhaa zinazoweza kuwapata katika kipindi hicho. Kukosekana kwa mfumo huu maalumu wa kuwaandaa wafungwa, kunasababisha wafungwa kuachiwa bila kuandaliwa hivyo kuwapa ugumu wa kupata huduma za jamii na misaada mbalimbali na kuchangia ongezeko la wafungwa wanaorudia makosa.

(d) Usimamizi wa Mipango Miji

Kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi, Serikali inaandaa sera mpya ya makazi, na uendeshaji wa shughuli za sekta ya ardhi kupitia Mfumo Jumuishi wa Taarifa za Usimamizi wa Ardhi, ambao umesanikishwa katika mikoa miwili. Aidha, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefanikiwa kuandaa na kupitisha jumla ya michoro ya mipango miji 8429 kati ya 8000 iliyokuwa imepangwa kutekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2019/20 hadi 2022/23, ambayo inaonesha utendaji wa jumla kwa asilimia 105. Hata hivyo, maeneo yafuatayo yanahitaji maboresho zaidi.

Usanifu na uendelezaji wa mipango miji usiojitosheleza: Ukaguzi ulibaini kuwa, Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais – Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) hazikuhakikisha kuwa usanifu na uendelezaji wa Mipango miji inajitosheleza. Mipango miji iliyoendelezwa haikuzingatia viwango vinavyotakiwa na utofauti ulikuwa asilimia 2 hadi asilimia 85 katika mamlaka 5 kati ya 11 za upangaji zilizotembelewa. Pia, ilibainika kuwa ni asilimia 61.54 tu ya mipango ya kina 79 iliyopitiwa ilijumuisha maeneo kwa ajili ya maendeleo ya baadaye. Matokeo yake, usanifu na uandaaji wa mipango miji haukufanyika kwa wakati hivyo kuchelewesha ugawaji wa viwanja au utoaji wa hatimiliki kwa wananchi.

Skimu za mipango miji iliyoandaliwa kutotekelezwa kwa ufanisi: Ilibainika kuwa miji haikuendelezwa kwa ufanisi kutokana na kutozingatia skimu za mipango miji zilizoidhinishwa wakati wa uandaaji wake. Hali hii ilionekana katika mamlaka 7 kati ya 11 za upangaji zilizotembelewa. Pia, kulikuwa na upungufu wa rasilimali kwa ajili ya kuwezesha shughuli za mipango miji katika Wizara ya Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi na OR - TAMISEMI. Vilevile, Wizara ya Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi na OR – TAMISEMI, kupitia mamlaka ya serikali za mitaa hazikusimamia kikamilifu udhibiti wa uendelezaji wa miji ili kuhakikisha inalingana na skimu za mipango miji na mipango kabambe ya maeneo husika. Aidha, ukaguzi ulibaini kufanyika kwa tathmini isiyojitosheleza ya utendaji wa mamlaka za upangaji juu ya shughuli za mipango miji. Hali hii ilisababisha kutofikia lengo lililokusudiwa la kupendezesha miji na kuwa na mazingira mazuri ya kuishi, kufanya kazi, na kuburudika.

Usimamizi wa Huduma za Bima na Urejeshaji wa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu

Sehemu hii inahusu usimamizi na ufuatiliaji wa watoa huduma za bima pamoja na usimamizi wa urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, kama inavyofafanuliwa hapa chini.

Usimamizi na ufuatiliaji wa watoa huduma za bima

Ninatambua juhudi zilizofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania katika kuwasimamia watoa huduma za bima nchini. Jitihada hizi ni pamoja na kusajili watoa huduma za bima 1,165; kuanzisha Mfumo wa Usajili kwa Njia ya Mtandao kwa ajili ya kusajili watoa huduma za bima; kuidhinisha bidhaa mpya za bima; na kutekeleza programu mbalimbali za uhamasishaji wa bima katika Kanda na Ofisi ya Zanzibar. Hata hivyo, kulibainika maeneo yaliyohitaji maboresho zaidi kama yanavyofafanuliwa hapa chini.

Usimamizi usioridhisha wa madai ya bima: Ukaguzi ulibaini kuwa madai ya bima hayakusimamiwa na kufuatiliwa ipasavyo na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania. Hali hii ilithibitishwa na kuwapo kwa ongezeko kubwa la madai ya wateja ambayo yalikuwa hayajalipwa na kampuni za bima kutoka shilingi bilioni 114.532 mwaka 2019 hadi shilingi bilioni 127.253 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 11 kutoka mwaka 2019/20 hadi 2022/23. Ukaguzi ulibaini ongezeko hilo la madai ambayo yalikuwa hayajalipwa lilichangiwa zaidi na kuwapo kwa janga la UVIKO-19 lililosababisha ongezeko la madai ya bima za maisha na ucheleweshaji wa malipo kwa madai yaliyoidhinishwa na kampuni za Bima. Kucheleweshwa kwa malipo ya madai yaliyoidhinishwa kuliathiri vibaya haki ya wateja wa bima ya wanufaika kulipwa kwa wakati na kampuni za bima. Kwa mfano, ripoti za ukaguzi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania kuanzia mwaka wa fedha 2019/20 hadi 2022/23 zilionesha kuwa shilingi milioni 439.15 hazikulipwa kwa wakati na kampuni za bima kwa wateja wao.

(ii) Usimamizi wa urejeshaji mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu

Ninatambua juhudi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu katika kusimamia urejeshaji wa mikopo kwa njia ya mapitio ya kina na kuandaa modeli ya kiotomati ya uzalishaji na uzoefu wa wateja kujifunza kupitia mashine na mbinu za kiakili-bandia chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi. Hata hivyo, maeneo yanayohitaji kuboreshwa zaidi yamebainishwa kama ifuatavyo:

Ongezeko la mikopo ambayo ilikuwa haijalipwa yenye thamani ya shilingi trilioni 3.15: Ukaguzi ulibaini kuwa mikopo ambayo ilikuwa haijalipwa iliongezeka kutoka shilingi trilioni 1.25 katika mwaka wa fedha 2015/2016 hadi shilingi trilioni 4.84 kwa mwaka wa fedha 2021/2022, sawa na ukuaji wa wastani wa asilimia 23. Kwa mfano, makusanyo ya ulipaji wa mikopo yalipungua kutoka shilingi bilioni 191 mwaka 2019/20 hadi shilingi bilioni 170 mwaka 2022/23. Hali hiii ilisababishwa na mabadiliko ya sera za utoaji wa mikopo ikiwemo sera ukadiriaji wa uhifadhi wa thamani wa kiwango cha sifuri ya mwezi Julai 2021. Pia, kubadilishwa kwa adhabu na ada za kuhifadhi thamani ya fedha hadi kiwango cha sifuri kulichangia kupungua kwa makusanyo ya mikopo.

Matokeo yake, ufadhili wa Serikali kwa mikopo ya wanafunzi uliongezeka kutoka shilingi bilioni 268.9 mwaka 2018/9 hadi shilingi bilionii 393.8, sawa na ongezeko la shilingi bilioni 124.9 kutokana na ufanisi usioridhisha wa Bodi ya Mikopo Wanafunzi wa Elimu ya Juu katika kukusanya mikopo iliyoiva ya wanafunzi inayothibitishwa na ongezeko la madeni.

Ukaguzi ulibaini pia kuwa marejesho ya mikopo kutoka kwa wanufaika binafsi yalifanywa kwa wastani wa asilimia 11 ikilinganishwa na asilimia 38 kutoka kwa wanufaika walioajiriwa. Aidha, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu

ilikusanya sehemu ndogo ya marejesho ya mikopo kutoka kwa wanufaika binafsi kwa wastani wa shilingi bilioni 38, sawa na asilimia 11 kuanzia mwaka 2014/2015 hadi 2022/23. Hadi mwaka wa fedha 2022/23, Bodi ilikusanya jumla ya shilingi bilioni 1,181.4 kutoka kwa wanufaika walioajiriwa na shilingi bilioni 104.70 kutoka kwa wanufaika waliojiajiri.

Kukosekana kwa ufanisi wa ukusanyaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika walio katika sekta binafsi kulitokana na mikakati isiyoridhisha ya ufuatiliaji ikiwa pamoja na kukosekana kwa mfumo wa TEHAMA unaoweza kusomana na mifumo ya taasisi muhimu kama vile Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii; Wakala wa Usajili, Ufilisi, na Udhamini; Tume ya Vyuo Vikuu; Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa; na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni zenye kanzidata nyingi za wanufaika. Hali hii ilisababisha kutokusanywa kwa marejesho ya mikopo, jambo ambalo linaweza kuathiri ustahimilivu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu katika kuendelea kufadhili wanafunzi.

Usimamizi wa Maliasili

Katika sehemu hii, ukaguzi ulifanyika katika usimamizi wa fukwe, uwezeshaji wa wachimbaji wadogo wa madini; na usimamizi wa rasilimali za uvuvi, na matokeo yake ni kama yanavyofafanuliwa hapa chini.

Usimamizi wa Fukwe

Jitihada zilizobainishwa katika usimamizi wa fukwe ni pamoja na utambuzi wa baadhi ya fukwe pamoja na uandaaji wa mkakati wa masoko na uendelezaji wa fukwe zilizoko kusini mwa Tanzania. Hata hivyo, yafuatayo yalibainishwa:

Uendelezaji usiojitosheleza wa fukwe katika uongezaji wa shughuli za utalii katika maeneo ya pwani: Asilimia 89 ya maeneno ya fukwe yaliyotambuliwa yalikuwa hayajaendelezwa. Hali hi ilitokana na kuwapo kwa hatua zisizoridhisha za undelezaji wa fukwe, hivyo kuzuia upatikanaji wa manufaa yatokanayo na fukwe hizi, kama vile ukusanyaji wa mapato kutoka kwa watalii wa ndani na wa kigeni.

Utekelezaji usioridhisha wa masuala ya utunzaji wa mazingira: Asilimia 82 ya fukwe katika Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizotembelewa hazikuzingatia masuala ya mazingira kwa sababu ya ukosefu wa kampeni za uelewa wa suala hili. Hali hii ilisababisha uharibifu wa mazingira, kama vile ukataji wa miti ya mikoko katika maeneo ya pwani.

Uendelezaji na utangazaji usiojitosheleza wa fukwe: Ukaguzi ulibaini uendelezaji na utangazaji wa fukwe usiojitosheleza kwa ajili ya shughuli za utalii. Hali hii ilisababishwa na mipango isiyojitosheleza ya kuwezesha kukuza na kuendeleza utalii wa fukwe, hivyo kuzuia upatikanaji wa manufaa yatokanayo na maendeleo ya fukwe hizi, kama vile ukusanyaji wa mapato kutoka kwa watalii wa ndani na wa kigeni.

Ufuatiliaji na uratibu usio na tija wa shughuli za ufukweni: Ukaguzi ulibaini kuwa ufuatiliaji na uratibu wa shughuli za ufukweni haukufanyika vizuri. Hali hii ilisababishwa na ukosefu wa takwimu za kuaminika kwa ajili ya kupima utendaji, na hivyo kuathiri utangazaji na ukuzaji wa fukwe nchini.

(ii) Uwezeshaji wa Wachimbaji Wadogo wa Madini

Ili kuwezesha shughuli za uchimbaji mdogo wa madini, Serikali ilianzisha vituo vya mfano, kununua rigi kwa ajili ya wachimbaji wadogo, kufanya utafiti wa kijiolojia, na kuanzisha masoko ya madini katika maeneo mbalimbali nchini. Hata hivyo, upungufu ufuatao ulibainika:

Wachimbaji wadogo wa madini kutowezeshwa ipasavyo: Ukaguzi ulibaini kuwa wachimbaji wadogo hawakuwa na taarifa za kutosha za kijiolojia pamoja na mashapo. Vilevile, hawakuwa na teknolojia za uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Hali hii ilitokana na ukosefu wa mbinu za kutosha za kuwasaidia, hivyo kuathiri maendeleo kutoka katika uchimbaji mdogo kwenda katika uchimbaji wa kati.

Utengaji na matumizi ya rasilimali yasiyojitosheleza katika kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini: Ukaguzi ulibaini changamoto katika kuhakikisha utengaji wa fedha za kutosha na matumizi ya rasilimali zingine katika kuwasaidia wachimbaji wadogo. Hali hii ilitokana na utambuzi mdogo wa mahitaji na vipaumbele wakati wa kupanga na kutumia rasilimali hizo. Vilevile, hakukuwa na njia zilizowekwa ili kutathmini matumizi bora ya rasilimali zilizotengwa kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini. Changamoto hii ilisababishwa na ukosefu wa taarifa za kutosha kuhusu wachimbaji wadogo, hivyo kukwamisha matumizi sahihi ya rasilimali zilizolenga kuwasaidia wachimbaji wadogo.

(iii) Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imechukua hatua mbalimbali za kutokomeza ongezeko la matumizi ya zana haramu za uvuvi na kupata manufaa makubwa yatokanayo na shughuli za uvuvi. Pamoja na jitihada hizo, mambo yafuatayo yalibainika:

Kuwapo kwa shughuli za uvuvi haramu nchinii: Ukaguzi ulibaini kuwapo kwa uvuvi haramu kutokana na kuwapo kwa zana haramu za uvuvi na wavuvi wasiosajiliwa. Hali hii ilisababishwa na ufuatiliaji na udhibiti usioridhisha.
Upungufu huu ulichangiwa na kuwapo kwa usimamizi na matumizi yasiyojitosheleza ya rasilimali za uvuvi.

Upungufu katika usimamizi wa kanzidata ya uvuvi: Ukaguzi ulibaini upungufu kama vile usimamizi usioridhisha wa nyaraka na takwimu za kila siku za uvuvi. Hali hii ilitokana na wizara zinazohusika kutoweka kipaumbele juu ya suala hili. Hali hii ilisababisha kuwapo kwa taarifa zisizo na uhalisia juu ya rasilimali za uvuvi.

Uratibu usiojitosheleza katika usimamizi wa rasilimali za uvuvi: Ukaguzi ulibaini uratibu usijitosheleza baina ya wadau kama ilivyodhihirishwa na kuwapo kwa mawasiliano duni kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mamlaka za Serikali za Mitaa, na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI). Hali hii ilisababishwa na muundo wa kuripoti usiojitosheleza kati ya taasisi hizi tendaji. Matokeo yake, kulikuwa na ushirikiano hafifu katika usimamizi wa rasilimali za uvuvi nchini.

Usimamizi wa Uingizaji wa Mafuta Nchini

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha uhakika wa ugavi wa mafuta nchini. Jitihada zilizochukuliwa ni pamoja na ufungaji wa mfumo wa ufuatiliaji mafuta wakati wa kushusha na kupakia, ujenzi wa Mfumo wa Taifa wa Taarifa za Petroli na Gesi, na ujenzi wa kituo kimoja cha kupokea mafuta bandari. Hatua hizi zinalenga kupunguza upotevu wa mafuta wakati wa kushusha, kufuatilia mafuta yaliyopo nchini kwa watoa huduma mbalimbali, na kushughulikia ucheleweshaji wa ushushaji wa mafuta. Hata hivyo, wakati wa ukaguzi, upungufu ufuatao ulibainika:

Mwenendo wa ucheleweshaji wa kuanza kushusha mafuta bandarini umeongezeka kutoka asilimia 66 hadi asilimia 68 kutoka mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2022/23. Kwa upande mwingine, ukaguzi huo umebaini ongezeko la ucheleweshaji kuanza kushusha kutoka asilimia 66 hadi asilimia 68 kati ya mwaka 2020/21 na 2022/23. Meli zilicheleweshwa kuanza kushusha mafuta kwa siku 7-14 na zaidi ya siku 14 katika mwaka wa fedha 2022/23 ukilinganisha na miaka iliyopita. Vikwazo vya miundombinu na kutofuata kwa tarehe iliyopangiwa meli kwa ajili ya ushushaji ilichangia ucheleweshaji huu, na kusababisha serikali kutozwa dola za Marekani 26,934,426.35. Pia, mwenendo wa meli kutoshusha mafuta ndani ya muda uliopangwa uliongezeka kutoka asilimia 27 hadi asilimia 35.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji haikubaini kampuni za uangizaji wa mafuta zilizohifadhi mafuta chini ya siku 15 wakati wote:

Uchambuzi wa ripoti za mafuta kwa wiki ya 1 na 3 kuanzia mwaka 2020 hadi 2023 zinaonesha kuwa kampuni za uangizaji wa mafuta hazikuhifadhi mafuta ya kuweza kutumika kwa siku 15 wakati wote kati ya asilimia 12 hadi 62, na asilimia 14 hadi 65 kwa petroli na dizeli mtawalia. Hali hii ilitokana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji kutathmini upatikanaji wa mafuta kwa jumla badala ya hifadhi ya mafuta kwa kila kampuni ya uingizaji wa mafuta, hivyo kupunguza uwezo wa kutambua kampuni ambazo hazikuhifadhi mafuta yanayotakiwa.

Aidha, kukosekana kwa ripoti ya ukubwa wa soko kwa kila kampuni na kwa kila bidhaa kulipunguza uwezo wake wa kubaini hatari kwenye uhakika wa ugavi wa mafuta.

Wizara ya Nishati kutoandaa mpango kabambe wa uendelezaji wa miundombinu ya mafuta: Kwa mujibu wa ripoti zake za utendaji kuanzia mwaka 2018/19 hadi 2022/23, ukaguzi ulibaini kuwa, Wizara ya Nishati haikuandaa mpango kabambe wa uendelezaji wa miundombinu ya mafuta kwa miaka mitano, bali iliandaa andiko la mpango kabambe wa uendelezaji wa miundombinu ya mafuta. Menejimenti ilieleza kuwa Wizara ilikuwa inatafuta rasilimalifedha kwa ajili ya maandalizi ya mpango kabambe huo. Ukosefu wa mpango kabambe unaweza kuzuia uratibu wa shughuli za uendelezaji wa miundombinu ya mafuta hivyo kusababisha kujirudia kwa juhudi za serikali na kusababisha wasiwasi kwa wawekezaji, wadau wa sekta, na washirika wa biashara.

Hitimisho la Jumla la Ukaguzi

Ukaguzi unatambua juhudi zilizofanywa na taasisi zilizokaguliwa katika kuboresha utendaji wao ili kufikia malengo ya Mpango wa Pili na wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano na Mpango wa Maendeleo Endelevu ambao lengo lake kuu lilikuwa kuboresha uchumi na maendeleo ya watu. Jitihada zilizochukuliwa zilibainika wakati wa kutekeleza maeneo mbalimbali ya kipaumbele katika maeneo ya huduma za afya, shughuli za kilimo, maendeleo ya rasilimali watu, mipango miji, bima na mikopo, maliasili na utalii, na uingizaji wa mafuta.

Licha ya jitihada zilizochukuliwa na taasisi zilizokaguliwa katika kuhakikisha kuwa malengo ya Mpango wa Pili na wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano na Mpango wa Maendeleo Endelevu yanatimizwa, ukaguzi ulibaini kuwapo kwa changamoto ambazo zilizozuia kufikia malengo yaliyopangwa.

Upungufu uliobainishwa katika maeneo yaliyotajwa unapaswa kushughulikiwa haraka ili kuhakikisha kuwa malengo ya Serikali ya kukuza ustawi na maendeleo ya watu kama yalivyoainishwa katika Mpango wa Pili na wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano na Mpango wa Maendeleo Endelevu yanafikiwa.

Mapendekezo ya Ukaguzi

Wizara, Idara, na Wakala zinatakiwa kufanya yafuatayo:


Wizara ya Afya inapaswa ihakikishe upatikanaji wa huduma za afya ya akili katka ngazi zote za vituo vya afya ili kuhakikisha kuwa wananchi wenye uhitaji wanapata huduma sahihi ya afya ya akili kwa wakati, na kuhakikisha vifaatiba vinasimamiwa ipasavyo ili kuhakikisha kunakuwa na usalama na ubora kwenye huduma za afya zinazotolewa na vituo vya afya nchini;

Wizara ya Kilimo inapaswa iteue wakaguzi wa mazao ya biashara sambamba na kuhakikisha wanakuwa na vitendeakazi, ambao watawajibika moja kwa moja kwenye bodi zao za mazao ili kurahisisha ufuatiliaji wao na kuwafanya wawajibike kwenye menejiment za bodi za usimamizi wa mazao;

Wizara ya Kilimo inapaswa itathmini ufanisi wa mifumo ya ununuzi wa mbolea kama vile mfumo wa pamoja wa ununuzi wa mbolea na mifumo mingine iliyopo, na kutumia matokeo yake katika kutatua upungufu wote ulioainishwa ili kuwezesha ununuzi na usambazaji wa mbolea kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya mbolea;

Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi wanatakiwa kufanya tathmini ya kina na endelevu ya uhitaji wa soko la ajira ili kuainisha mahitaji mapya ya ujuzi na kuhakikisha kuwa mitaala inayoandaliwa inazingatia soko la ajira;

Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Magereza wanatakiwa kuandaa na kutekeleza mitaala ya mafunzo ya urekebu kwa wafungwa ili kurahisisha utekelezaji wa programu za urekebu;

Wizara ya Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zinahimizwa kuandaa mikakati madhubuti ya kuwezesha usimamizi mzuri wa utekelezaji wa shughuli za mipango miji nchini. Mikakati hiyo inapaswa kuongeza ufanisi katika usanifu, upangaji, na utekelezaji wa shughuli za mipango miji ili kuwezesha kufikia kwa wakati malengo yaliyokusudiwa;

Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Maliasili na Utalii na Kitengo cha Uhifadhi wa Bahari na Maeneo Tengefu wanatakiwa kuboresha uratibu na ufuatiliaji wa ufanisi wa fukwe ili kuhamasisha uendelevu na kutangaza utalii wa fukwe;

Wizara ya Madini ihakikishe inawasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwezesha upatikanaji wa taarifa za kijiolojia, teknolojia za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, pamoja na utengaji na matumizi ya rasilimali za kutosha kuwasaidia wachimbaji hao;

Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wanatakiwa kuhakikisha ufuatiliaji, udhibiti, na shughuli za uchunguzi ili kukabiliana na uvuvi haramu nchini; na

Wizara ya Nishati inatakiwa kuweka mkazo uanzishaji wa mpango kabambe wa uendelezaji wa miundombinu ya mafuta na kuratibu uendelezaji wa miundombinu ya kupokelea mafuta kwa pamoja.

Pia soma:
CAG Kichere: Licha ya kupewa Ruzuku ya Tsh. Bilioni 31.55, ATCL imepata hasara ya Tsh. Bilioni 56.64, ongezeko la 61% kutoka hasara ya Mwaka 2021/22
- Ripoti 21 za CAG zatua Bungeni kwa ajili ya kuanza kujadiliwa
 

Attachments

  • Ripoti_Kuu_ya_Ukaguzi_wa_Ufanisi_kwa_Mwaka_wa_Fedha_2022-23 (1).pdf
    6.1 MB · Views: 7
Back
Top Bottom