Ripoti Benki ya Dunia: Uchumi wa Tanzania utaimarika zaidi

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,367
8,101
LICHA ya mlipuko wa ugonjwa wa COVID- 19 kuzorotesha uchumi wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, ripoti ya Benki ya Dunia (WB) imeonyesha kuwa uchumi wa Tanzania umezidi kuimarika na kupita wastani wa nchi hizo.

Ripoti hiyo ambayo ni toleo la 18 la Taarifa ya Kiuchumi ya Tanzania, pia imeeleza kwamba pato la Tanzania linatarajia kupanda kutoka asilimia 4.6 mwaka jana hadi asilimia 5.3 mwaka huu.

Sehemu ya ripoti hiyo iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam ilitaja sababu zilizochangia kukua kwa uchumi wa Tanzania ni kufunguliwa kwa shughuli za utalii, mipaka kwa shughuli za kiuchumi na mafanikio kwenye chanjo dhidi ya ugonjwa wa corona hali iliyofungua nyanja za biashara na uzalishaji.

Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo iliisifu misingi ya kiuchumi ya Tanzania kuhimili misukosuko ya kiuchumi iliyoziumiza nchi nyingi za Afrika kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa licha ya ugonjwa wa corona kudhorotesha uchumi wa nchi za Jangwa la Sahara lakini uchumi wa Tanzania umezidi kuimarika.

Pia ilisema kuwa mlipuko wa COVID- 19 ulisababisha kiwango cha umaskini kuongezeka kutoka asilimia 26 mwaka 2019 hadi asilimia 21 mwaka 2021 kwa nchi nyingi za kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwamo Tanzania.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, endapo kusingekuwapo na misingi imara ya kiuchumi, hali ingekuwa mbaya zaidi kutokana na kuwapo kwa uzalishaji mdogo.

Aidha, ripoti hiyo imetaja sababu zilizokwamisha kukua kwa pato la taifa kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa bei za mafuta kulikosababisha usafiri kuwa wa shida, kupanda kwa bei za vyakula kulikosababishwa na kudorora kwa kilimo kutokana na ukame.

Ripoti hiyo pia ilisema upatikanaji wa huduma bora ya maji unaweza kuipunguzia harasa ya kiuchumi Tanzania ya Dola za Marekani bilioni 1.9 (Sh.trilioni 4.48) kwa mwaka ifikapo mwaka 2030.

Tanzania, kwa mujibu wa ripoti hiyo, inaweza kuokoa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 2.4 ( Sh. trilioni 5.59) kila mwaka kwa kuepuka gharama za ziada za matibabu zinazopotea kutokana na ukosefu wa uzalishaji na magonjwa yanayotokana na kukosekana kwa huduma hiyo.

Ingawa nchi imepiga hatua kubwa miaka ya hivi karibuni katika kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo, ripoti ilibainisha kuwa ni asilimia 61 tu ya kaya ndizo zinazoweza kuipata jambo linaloonyesha bado kuna kazi ya kufanya ili kufikia asilimia 39 iliyobaki.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi wa WB Tanzania, Nathan Belete, alisema maji ni huduma ya msingi kwa asilimia 32 ya usafi ya vyoo, huku asilimia 48 ikiwa ni matumizi mengine ya nyumbani ikiwamo kuosha vyombo, kuoga na kufua.

"Ili Tanzania ihakikishe kuna upatikanaji wa majisafi kwa wote, uwekezaji mkubwa wa mapema unahitajika ili kuepuka matokeo mabaya ya huduma duni," alisema Belete.Alisema moja ya matokeo ya haraka ya zaidi ya huduma duni za majisafi ni vifo na magonjwa lakini uwajibikaji unaweza kuzuia vifo 31,000 vinavyoweza kuzuilika,” alisema.

Kadhalika ripoti hiyo inataka kuweka kipaumbele kwenye athari mtambuka zinazotokana na ukosefu wa huduma za majisafi kwenye ajenda kubwa ya sera ya serikali.

Mtaalamu Mwandamizi wa Ugavi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa WB, Ruth Walker, alisema utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Sekta ya Maji Tanzania (WSDP III) unahitaji wastani wa Dola za Marekani bilioni 6.5 (Sh. trilioni 15.15).

NIPASHE
 
Back
Top Bottom