Richmond sumu kali CCM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Richmond sumu kali CCM

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Pdidy, Oct 11, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Oct 11, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,249
  Likes Received: 5,631
  Trophy Points: 280
  • Wabunge wawakamia kuwasulubu

  na Mwandishi Wetu

  SAKATA la Kampuni ya Richmond Development Company (LLC), limezidi kuchukua sura mpya na huenda likaibua mjadala mkali katika mkutano wa 17 wa Bunge la Jamhuri, unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

  Katika mahojiano na baadhi ya wabunge waliopo kwenye vikao vya kamati mbalimbali za Bunge, vinavyofanyika jijini Dar es Salaam, waliiambia Tanzania Daima Jumapili kuwa mjadala kuhusu Richmond, ulioahirishwa na Spika Samuel Sitta, katika mkutano wa Bunge uliopita, utaibuka tena, huku baadhi yao hussani wale wa CCM wakiweka msimamo wa kuibana serikali.

  Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumapili kwa siku kadhaa tangu kuanza kwa vikao hivyo, umebaini kuwa suala la Richmond limekuwa mwiba, hasa kutokana na makali ya mgawo wa umeme unaoendelea kwa kasi nchini, na hadi sasa umeathiri shughuli mbalimbali za uzalishaji, hasa za wafanyabiashara wadogo wasio na njia mbadala ya matumizi ya nishati ya umeme.

  Mgawo huo ambao umewafanya watu wagawanyike katika makundi mawili, ambapo moja linaamini kuwa ni njama za baadhi ya watendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) ili kutafuta uungwaji mkono wa kuinunua mitambo ya Dowans iliyorithi mkataba kutoka kwa Richmond.

  Kundi la pili ni lile linaloamini kwamba makali ya mgawo wa umeme yanatokana na maamuzi ya pamoja ya kisiasa ya Bunge na serikali yaliyopinga pendekezo la kitaalamu la TANESCO la kuinunua mitambo ya Dowans iliyotolewa mwanzoni mwa mwaka huu.

  Mgawanyiko huo ndio unaoiweka serikali na wabunge njia panda, kiasi cha kuifanya ihofie uwepo wake endapo wabunge watachachamaa dhidi ya hatua ilizozichukua kwa watu walioingia mkataba na kampuni ‘hewa’ ya Richmond, ambayo ilisababisha baadhi ya viongozi kuachia nyadhifa zao.

  Wakati hali hiyo ikionekana kuiumiza kichwa serikali, baadhi ya wabunge, hasa wa CCM wameonyesha kukerwa na tishio la Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) iliyotaka kumvua uanachama Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kwa kuruhusu mijadala mikali bungeni kiasi cha kuhatarisha uwepo wake.

  Wabunge hao wameweka bayana kuwa mkutano wa Bunge utakaoanza Oktoba 27 mwaka huu ndio utakaoamua kuendelea kwa serikali au kuvunjwa, iwapo maazimio ya Bunge hayatatekelezwa ipasavyo.

  Sakata hilo hivi sasa limeonekana kuchukua sura mpya, hasa kwa kujitokeza kwa kundi linalodaiwa kufanya jitihada za kuhakikisha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, wanahusishwa na Richmond ili kuwamaliza kisiasa.

  Moja ya sababu za wabunge hao kumlenga Lowassa zinahusishwa na kile wanachokiona wao kuwa ni mkakati wake wa kujiandaa kugombea urais kupitia CCM ama mwaka 2010 au 2015.

  Hata hivyo Lowassa mwenyewe ameshajitokeza akikana kuwa na mkakati huo, hususan wa kugombea urais mwaka 2010, akisema bado anaendelea kumuunga mkono Rais Kikwete ambaye kwa mujibu wa maelezo yake wamekuwa pamoja kwa miaka mingi.

  Ingawa majina ya Lowassa na Rostam hayakutajwa katika maazimio 23 ya Bunge yanayohusu mkataba wa Richmond, hata hivyo hoja hiyo imekuwa ikitumiwa na wapinzani wao wa kisiasa ndani ya CCM kwa muda mrefu, kama njia mojawapo ya kuwapunguzia ushawishi wao kisiasa katika siku zijazo ili kusitokee tena kile walichokuwanacho mwaka 2005, wakati walipokuwa na nguvu kubwa kisiasa.

  Jambo jingine ambalo wapambanaji wa ufisadi wanaliona tishio ni hatua ya serikali kuwasafisha watendaji walioipa ushindi wa kuzalisha umeme wa dharura Kampuni ya Richmond, ambayo ilishindwa kuzalisha umeme kama mkataba ulivyotaka.

  Miongoni mwa watendaji ambao Bunge liliazimia wawajibishwe ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea na wengineo, ambapo serikali katika Bunge lililopita ilisema hakukuwa na mazingira ya rushwa katika kutoa zabuni hiyo, sambamba na watendaji hao kutokuwa na kosa bali walizembea kwa kutoichunguza kwa makini kampuni hiyo.

  Hofu ya wapambanaji hao ni kuonekana kuwasingizia baadhi ya viongozi walioguswa na kashfa hiyo na kulazimika kujiuzulu nyadhifa zao, akiwamo Lowassa, mawaziri wawili, Nazir Karamagi (Nishati na Madini) na Ibrahim Msabaha (Ushirikiano wa Afrika Mashariki).

  Wachambuzi wa masuala ya siasa wanabainisha kuwa pamoja na CCM kuunda kamati ya kuchunguza nini chanzo cha uhusiano mbaya miongoni mwa wabunge wa chama hicho, suluhu iliyotarajiwa haitaweza kupatikana kwa kuwa kila kundi linavutia upande wake, hasa ukizingatia uchaguzi umekaribia.

  Wameeleza kuwa ukaribu wa uchaguzi na matatizo ya umeme (mgawo), ni miongoni mwa mambo yatakayoiweka serikali katika wakati mgumu, kwa kuwa hakuna mbunge ambaye atapenda kupoteza imani na umaarufu aliojijengea kwa wapiga kura wake.

  Wachambuzi hao wanaweka bayana kuwa makundi ndani ya CCM yanaweza kufikia katika hatua mbaya zaidi mwisho wa ngwe ya pili ya Rais Kikwete kama atachaguliwa kuendelea na wadhifa huo katika uchaguzi wa mwakani.

  Wanabainisha kuwa mapambano ya hivi sasa ambayo kwa kiasi kikubwa yanalenga urais wa mwaka 2015 kwa gharama yoyote ile, yamekuwa yakiathiri hata utendaji kazi wa serikali, kwa kuwa yana ushawishi wa aina yake ndani na nje ya Bunge, serikali na chama.

  Wakati mapambano hayo yakichukua sura hiyo, kamati iliyoundwa na NEC kuchunguza uhusiano usiofaa baina ya wabunge wa CCM na mawaziri imeshaanza kazi, ambapo inatarajia kuanza kuwahoji baadhi ya wabunge ili kujua chanzo cha matatizo. Miongoni mwa watu wanaotarajia kuitwa na kamati hiyo ni Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambaye ndiye anayedaiwa kuihenyesha serikali awapo bungeni, kwa kuruhusu mijadala yenye uwezo wa kuiangusha serikali.
   
Loading...