Richmond, EPA kuibukia Butiama

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,116
Richmond, EPA kuibukia Butiama

Mwandishi Wetu Machi 12, 2008
Raia Mwema

Azimio la Butiama kuitikisa CCM
Wahusika wadaiwa kuanza kutoa rushwa

UAMUZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupeleka vikao vyake vya juu vya Kamati Kuu yake (CCM) na kile cha Halmashauri Kuu (NEC) kijijini Butiama, una ajenda nzito ya kisiasa ambayo inaelezwa kuwa mwangwi wa hoja nzito kuhusiana na kashfa kubwa zilizokielemea chama hicho na Serikali yake.

Kashfa ambazo zimeitikisa CCM na Serikali yake ni zile zinazohusiana na mradi wa umeme wa dharura uliokabidhiwa kwa kampuni ya Richmond Development LLC ya Marekani iliyosababisha kuanguka kwa aliyekua Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wengine wawili, na lile sakata linaloendelea la upotevu wa mamilioni ya fedha ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikiwamo Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).

Habari kutoka ndani ya CCM zinaeleza kwamba, vikao hivyo vitakavyofanyika mwishoni mwa mwezi huu, vitaibuka na kile kitakachofahamika kama “Azimio la Butiama” ambalo litatoa mwelekeo mpya wa chama hicho ambacho kinaendelea kushika dola pamoja na misukosuko kadhaa inayokikabili.

Ofisa Mwandamizi wa CCM aliliambia RAIA MWEMA, jana, Jumanne kwamba, vikao vya Butiama vitakavyofanyika kati ya Machi 29 na 30, mwaka huu, vitahitimishwa na maazimio yakayatolewa lakini alikwepa kubainisha aina ya maazimio yatakayotolewa mbali ya kusema kwamba maazimio yakayotolewa yatahusu “biashara na siasa”.

Pamoja na Ofisa huyo kutokua tayari kuzunguzia hasa maazimio yatakayotolewa, habari zinasema taarifa za vikao vya Kamati Kuu vya hivi karibuni na kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kuhusiana na kutenganisha biashara na siasa, vinagusa kwa karibu maazimio makubwa mawili ya chama hicho yanayopingana yaliyotolewa mwaka 1967 mjini Arusha na mwaka 1992 Zanzibar.

Wakati Azimio la Arusha lililoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere liliweka mipaka na miiko ya uongozi, Azimio la Zanzibar, lililegeza masharti na kutoa mwanya kwa viongozi na watendaji kujihusisha na biashara bila kuwapo kwa mazingira ya udhibiti wa ukiukwaji wa maadili.

Vyanzo vya habari ndani ya CCM vinaeleza kwamba matukio ya hivi karibuni ya kuhusiana na sakata la Richmond na lile la EPA, yamekizindua chama hicho kunuia kufanya mageuzi makubwa katika kujisafisha kutokana na uchafu mkubwa uliosheheni ndani yake.

Mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete amekuwa akinukuliwa akigusia kuhusu maadili ya uongozi na vyanzo vya mapato ya chama hicho ikiwa ni pamoja na fedha zinazotumika katika chaguzi mbalimbali, kauli ambazo ziliashiria kuguswa kwake na uwezekano wa kuhusishwa na fedha chafu.

Akihutubia wana CCM wenzake mara baada ya kupokea Uenyekiti kutoka kwa Benjamin Mkapa, Juni 25, 2006 Rais Kikwete alisema kuwa kuna hatari ya CCM kuhusishwa na watu wasiokuwa na uhakika nao na kuishia kupata fedheha.

“Sasa wakati umefika kwa Chama chetu kuondokana na maisha ya kutafuta fedha na rasilimali za kufanyia shughuli zake kwa taratibu za zimamoto. Kufanya hivyo kuna hatari ya siku moja kujikuta moto umekuwa mkubwa mno na hauzimiki kwa urahisi. Lakini jambo baya zaidi ni hatari ya kuhusishwa na watu tusiokuwa na uhakika nao na kupata hatari ya kuishia kupata fedheha,” alisema Kikwete.

Kauli hiyo ya Kikwete, inaashiria kwamba alibaini mapema kuhusu kutumika kwa fedha zinatokana na watu wasio safi lakini wamekuwa na umuhimu kutokana na nguvu zao za kiuchumi bila kujali uadilifu wao na hivyo kugusa moja kwa moja matukio ya hivi karibuni kuhusiana na kashfa ya Richmond na EPA ambazo zinaigusa CCM moja kwa moja.

Kujiuzulu kwa Lowassa na kutajwa kwa Rostam Aziz, ambao walikua vinara katika kampeni za CCM mwaka 2005, ni wazi kulijulikana mapema na Kikwete, lakini pia sakata la EPA bado linaisogelea CCM kwa karibu mno hususan kutokana na wahusika karibu wote kutajwa kuisaidia kwa kiasi kikubwa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2005.

Tayari kampeni chafu zinaelezwa kuanza kufanywa katika maeneo mbalimbali nchini, zikiwa na lengo la kutumia vikao vya Butiama kuwasafisha baadhi ya wahusika wakuu wa Richmond na EPA, huku kundi jingine likijenga hoja ya kuhakikisha hatua zaidi zinachukuliwa dhidi ya wahusika wote waliotajwa na wale ambao watabainika baadaye.

“Watu wameanza kujipanga na wengine wamekwisha kuahidiwa fedha lakini kwa kweli CCM ya sasa ni tofauti kabisa. Watu wameamka na wameona hakuna tija kuendelea kufumbia macho uchafu,” anasema mwana CCM mmoja ambaye atashiriki moja ya vikao hivyo vya juu.

Hii ni mara ya kwanza kwa vikao vya CCM kufanyika Butiama mahali alikozaliwa na kuzikwa Mwalimu Julius Nyerere, ikiwa ni ishara tosha ya kutaka kuwafanya wajumbe wa vikao hivyo kuzingatia yale yote yaliyosimamiwa na mwasisi huyo wa chama hicho.

Mgawanyiko wa dhahiri umejitokeza ndani ya CCM baada ya kujizulu kwa Lowassa, kundi moja likimuunga mkono kuhusiana na madai yake kwamba ameonewa kuhusiana na sakata la Richmond, huku kundi jingine likishinikiza hatua zaidi kuchukuliwa dhidi yake kuhusiana na sakata hilo na mengine ambayo yamedaiwa kuendelea “kuchimbwa kwa kasi mpya.”

Kwa upande wa watuhumiwa wa upotevu wa fedha za EPA, imeelezwa kwamba wamekuwa wakijitahidi kuwarubuni wajumbe wawatetee kwa maelezo kwamba kashfa hiyo ikiendelea itaiangusha CCM kutokana na ushahidi walionao kuhusiana na sehemu ya fedha hizo kutumika katika kuisaidia CCM katika uchaguzi wa 2005.

Tayari Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Rais Kikwete kuchunguza fedha za EPA amekwishatoa taarifa kuonyesha ‘kigugumizi’ cha kuwachukulia hatua waliochota fedha hizo.

Awali Rais Kikwete aliagiza wahusika wachukuliwe hatua za kisheria na baadaye fedha zote zilizoibwa kurudishwa lakini kinachoelezwa ni kwamba sehemu ya fedha zimeanza kurejeshwa lakini hakuna aliyetajwa kurejesha fedha hizo.

Mwanyika katika taarifa yake alisema waliochukua fedha ni makampuni na si watu halisi na kwamba kisheria inawawia vigumu kuwashughulikia kwa haraka kabla ya kufanya uchunguzi wa kina.

Kauli ya Mwanyika imechukuliwa kwa hisia tofauti ikiwa ni pamoja na kuelezwa kwamba upo uwezekano wa kuhofia kuhusishwa kwa watu wakubwa ama taasisi nyeti zaidi katika sakata hilo.
 
Naona basi lipo katikati ya mlima. Ama wakubali kupungua au lirudi kinyume nyume, bila shaka chaguo la kwanza ni la busara zaidi kuliko kusubilia la pili.
 
Hili Azimio la Butiama linasubiriwa na wengi sana kama lile la kutoa ajira millioni moja au lile la kutoa mabilioni ya Kikwete kwa wananchi.....

Kuna wakati inafikia hatua the whole governing system sasa inakuwa kama mchezo wa kuigiza!
 
Kitila,
Basi lenyewe limechakaa. Injini karibu inaanguka. Na oili inavuja na moshi mweusi wenye harufu ya kuchefua.
 
Kitila,
Basi lenyewe limechakaa. Injini karibu inaanguka. Na oili inavuja na moshi mweusi wenye harufu ya kuchefua.

Hapa ni changa la macho kwa mara nyingine wana Inji wanachapwa na JK mwenyewe .Washindwe kutaja majina ya wezi wasingizie azimio la wapi ? Wacha tungoje mimi nitakuwa Butiama pia kujua festi hendi nyuzi .Wakiwa huko naomba waongelee maji kwenye lile bwana la Mwalimu Mkapa aliyachukua kuwapa washikaji zake .
 
Hapa ni changa la macho kwa mara nyingine wana Inji wanachapwa na JK mwenyewe .Washindwe kutaja majina ya wezi wasingizie azimio la wapi ? Wacha tungoje mimi nitakuwa Butiama pia kujua festi hendi nyuzi .Wakiwa huko naomba waongelee maji kwenye lile bwana la Mwalimu Mkapa aliyachukua kuwapa washikaji zake .

na pia kuna mgodi wa buhemba ambako kumeachwa man made bonde la ufa.. labda wataliita azimio la buhemba!
 
Kitila,
Basi lenyewe limechakaa. Injini karibu inaanguka. Na oili inavuja na moshi mweusi wenye harufu ya kuchefua.

Basi halina dreva, dreva aliyeaminiwa kuliendesha kumbe leseni yake ni fake na sasa anatapatapa hajui ashike wapi na wasafiri ndio wanazidi kupandisha mori
 
Back
Top Bottom