Remnant Mission Academy na mkakati wa kuboresha elimu

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,422
911,172
Remnant Mission Academy na mkakati wa kuboresha elimu
ban.blank.jpg

Prudence Karugendo

amka2.gif
KADRI miaka inavyosonga mbele tangu taifa letu lijipatie uhuru ndivyo adui namba moja kati ya maadui watatu tuliowagundua mara tu baada ya kuwa huru anazidi kukua.


Adui naemzungumzia hapa ni ujinga, ingawa kuna maadui wengine ambao ni umasikini na maradhi.


Adui ujinga anajitokeza kuwa kinara kwa vile yeye ndiye mwenye kuwawezesha maadui wengine wawili kuwa na nguvu za kuishambulia jamii yetu.


Bila kuwepo na adui ujinga hawa maadui wengine wawili ni rahisi kuwadhibiti.


Lakini penye ujinga umasikini unachomoza kirahisi, hii ni kwa sababu uerevu ni lazima ulete mbinu za kukabiliana na umaskini.


Vilevile penye ujinga maradhi nayo yanajitokeza kiurahisi, sababu mtu mwerevu si rahisi kuyaendekeza mazingira yanayosababisha maradhi.
Hivyo ndivyo ninavyomuona adui ujinga anavyofanya kazi ya kuwawezesha maadui hawa wengine na hivyo kuufanya ukinara wake usitiliwe shaka.


Kinachofanya hali hiyo ionekane hivyo ni kushuka kwa kiwango cha elimu hapa nchini kitu ambacho kimepigiwa kelele kwa zaidi ya miaka 25 iliyopita.


Kila mwaka tumekuwa tukilalamikia kushuka kwa kiwango cha elimu yetu. Lakini badala ya tatizo hilo kuonyesha unafuu hali imekuwa ikizidi kuwa mbaya mwaka hadi mwaka.


Kutokana na tatizo hilo, ndipo serikali ikaona umuhimu wa kuruhusu uwekezaji katika sekta ya elimu.


Watu binafsi, taasisi mbalimbali zikiwemo zile za kidini zimewekeza katika elimu ikiwa ni mojawapo ya jitihada za kupambana na adui ujinga.
Kulingana na unyeti ambao mimi binafsi nauona katika uwekezaji wa elimu, upo umuhimu wa kuwatia moyo wale wote walioamua kuwekeza katika sekta hii ya elimu hasa ikizingatiwa kuwa hii si aina ya uwekezaji inayolipa sana zaidi ya wawekezaji wenyewe kuwa tu na moyo wa kutaka kupambana na adui ujinga.


Ni kwa sababu hiyo nimekuwa nikivutiwa na watu pamoja na taasisi binafsi hata na zile za kidini zilizoamua kuwekeza katika elimu.
Nimejenga mazoea ya kutembelea shule zinazoendeshwa na taasisi hizi pamoja na zile zinazoendeshwa na watu binafsi ili kujionea mwenyewe juhudi zinazofanyika katika kumkabili adui ujinga, kitu kinachoonyesha matumaini ya kulikwamua taifa letu ndani ya giza na kuliweka kwenye mwanga utakaoliwezesha kufanya mambo yake ya kimaendeleo bila ubabaishaji kwa vile kila kitu kitakuwa peupe.


Moja ya shule nilizozitembelea hivi karibuni ni Remnant Mission International Academy iliyopo Tabata maeneo ya Hai Bar.
Naimani shule hii inayotoa elimu ya chekechea hadi sekondari, jina lake si geni sana kwa wadau wa elimu nchini.


Mbali na wakazi wa eneo la Tabata, Dar es Salaam, ambako shule hiyo ipo, vilevile kwa wakazi hao wa jijini jina hilo ni maarufu kwa wale wanaofuatilia kwa karibu ubora wa elimu.


Ikiwa sasa imetimiza mwaka wa kumi tangu ianzishwe, shule hiyo imeishatoa wahitimu wa darasa la saba mara tatu.


Shule hii inayomilikiwa na madhehebu ya pentekoste ya International Evangelism Assemblies Gospel Unity Church, imefanikiwa kutimiza malengo yake mengi ikiwa ni pamoja kutoa malezi bora ya kiroho kwa watoto sambamba na elimu bora kwa wanafunzi kuanzia chekechea, elimu ya msingi na ile ya sekondari ambayo imeanzishwa mwaka huu wa 2010.


Academy hii ni maono ya Mmisionari mmoja, Mchungaji Paul Lee na mke wake Hong Sang Dan, waliofikiria kuwa elimu bora kwa Watanzania ni muhimu katika kuendeleza maendeleo ya nchi kuliko kitu chochote kingine.


Ndipo mtumishi huyo wa Mungu na mkewe wakaanzisha shule iliyoanza na jina la Faith Academy lakini katika kutafuta usajili ikabidi jina libadilike na kuwa hili linalotumika kwa sasa, Remnant Mission Academy.
Miongoni mwa mambo ambayo shule hii inajivunia ni pamoja na majengo mazuri ya madarasa na ofisi yanayokidhi viwango vya kitaifa, walimu mahiri wenye sifa na uzoefu wa miaka mingi, mazingira mazuri ya kujifunzia pamoja na makitaba iliyosheheni vitabu vya kila aina vya kiada na ziada.


Malezi bora ya watoto yanayoambatana na maadili ya kiroho na uwepo wa michezo mbalimbali ukiwemo mmoja ambao ni maarufu shuleni hapo wa Taekwondo, kwa ajili ya afya bora za wanafunzi.


Akieleza historia ya mafanikio ya shule ya Remnant tangu ilipoanzishwa, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Isaiah Malealle, anasema idadi ya wanafunzi wanaofaulu darasa la saba shuleni hapo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.


Anasema mwaka 2009 asilimia 90 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la saba shuleni hapo walifaulu kuendelea na masomo ya sekondari.


Pamoja na mafanikio hayo, Malealle, anasema kutokana na maombi ya wazazi shule hiyo imeamua kuanzisha sekondari kuanzia mwaka huu, 2010, ili kuwawezesha watoto wanaohitimu darasa la saba shuleni hapo pamoja na wanaohitimu katika shule nyingine kuendelea na masomo ya sekondari shuleni hapo.


“Shule yetu inajitangaza yenyewe kutokana na mafanikio ya kitaaluma wanayoyapata watoto shuleni hapa ikiwa ni pamoja na usalama na ulinzi tunaowapatia wanafunzi wanapokuwa mikononi mwetu bila kusahau mazingira mazuri ya kishule tuliyo nayo,” anasema Mwalimu Malealle na kuongeza kwamba kila mwaka shule hiyo, iliyopata usajili mwaka 2002, imekuwa ikikaguliwa na wakaguzi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi lakini haijawahi kupatikana na dosari yoyote.


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Wazazi wa shule hiyo, Lezile Nyambo anathibitisha kwamba kamati yake ina mikakati mikubwa ya kushirikiana na uongozi wa shule ili kuhakikisha mafanikio yaliyokwisha patikana yanaendelezwa ili shule hiyo iwe miongoni mwa shule bora hapa nchini kuanzia ngazi ya chekechea hadi sekondari.


Nyambo ambaye ni mtumishi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, anasema uzoefu wake katika kuongoza kamati za shule ni mkubwa, Remnant ikiwa ni shule yake ya tatu kuwa Mwenyekiti wa Kamati kama hiyo.


Anasema kila alipokuwa mafanikio yalionekana na kwamba mkakati mkubwa uliopo kwa sasa ni kuiendeleza shule ya sekondari ili iweze kupata mafanikio kama yale ambayo shule ya chekechea na msingi zimeyapata.


Kwa sasa shule hiyo ya sekondari ina wanafunzi wapatao 35 wakiwa wa kidato cha kwanza ambao mwaka kesho watakuwa kidato cha pili.
“Tunashukuru kwamba majengo ya kutosha tunayo na bado ujenzi unaendelea. Kadhalika miundombinu yote ya shule kama walimu na vitendea kazi imekamilika. Kinachohitajika ni juhudi zetu. Tunaamini tutafanya maajabu,” anasema Nyambo na kusisitiza kwamba jukumu lao kubwa kwa sasa ni kuitangaza shule hiyo ya sekondari ili iweze kupata wanafunzi wengi zaidi wa kidato cha kwanza na cha pili mwaka 2011 ikiwa ni pamoja na wale wanaotaka kuhamia katika shule hiyo wakitokea shule nyingine.


Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Sekondari, Mchungaji Charles Kamaleki, anasema mwanzo unaweza kuwa mgumu kidogo lakini kutokana na uzoefu wake wa miaka mingi katika kuongoza shule za sekondari ana uhakika baada ya muda mfupi shule ya sekondari ya Remnant itakuwa kimbilio la wazazi wa Jiji la Dar es Salaam.


Anasema kwa sasa idadi ya wanafunzi si kubwa sana kutokana na upya wa shule, lakini ana uhakika kwamba baada ya muda mfupi wazazi wengi watafahamu uwezo wa walimu na hivyo kuwakabidhi dhamana ya kuwajenga watoto wao kitaaluma.


“Kwa uzoefu mkubwa wa ualimu wa miaka mingi naamini tutawajenga watoto kitaaluma na kiroho,” anasema.
Shule ya sekondari ya Remnant imeanza kusajili wanafunzi kwa ajili ya mwaka mpya wa masomo unaoanza Januari 2011.


Kwa mujibu wa Mwalimu huyo masharti yanayohitajika ili mwanafunzi aweze kujiunga na shule hiyo ni pamoja na kuwa tayari kujifunza kwa kuandika na kuzungumza Kingereza, kwa kuwa lugha hiyo ndiyo mhimili wa masomo yote ya sekondari isipokuwa somo la Kiswahili.


Anasema sifa nyingine wanazozihitaji ni nidhamu nzuri na heshima kwa jamii na wanaojitahidi katika kimasomo kwa kujiandaa kuwa viongozi bora wa jamii na taifa kwa ujumla.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom