Red Cross yadaiwa kuwakata wafanyakazi PAYE lakini haiwasilishi fedha hizo Serikalini. Yadaiwa Milioni 650

miss zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
2,832
2,000

Na LEONARD MANG’OHA
CHAMA cha Msalaba Mwekundu (Red Cross) Tanzania, kinatuhumiwa kutowasilisha zaidi ya Sh milioni 650 za kodi inayotokana na mshahara au mapato ya mfanyakazi (PAYE), licha ya wafanyakazi wake kukatwa fedha hizo.

Fedha hizo ni pamoja na Sh 432,956,238 zilizopaswa kulipwa kuanzia mwaka 2012 hadi 2016, na Sh 218419,320 za kuanzia Mei 2017 hadi Agosti 2019.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Red Cross kililiambia RAI hivi karibuni kuwa, kushindwa kuwasilishwa kwa fedha hizo katika mamlaka husika kumesababisha hali ya kutoaminiana miongoni mwa wafanyakati na viongozi wa chama, wakiamini kuwa fedha hizo huenda zimeliwa na baadhi ya viongozi wa chama.

Pia chanzo hicho kilidai kuwa taarifa za kutowasilishwa kwa fedha hizo katika mamlaka husika zimewahi kuripotiwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kinondoni.

Kilisema taarifa hizo pia zilitolewa katika kikao cha Bodi ya chama hicho, ambapo baadhi ya wajumbe walionesha kushitushwa na taarifa hizo na kutaka zishughulikiwe.

RAI ilipata nakala ya taarika ya kikao hicho ambayo inaonyesha kuwa chama hicho kinadaiwa na TRA PAYE kiasi cha Sh 432,956,238 za mwaka 2012 hadi 2016 na Sh 198,604,377 za kuanzia Mei 2017 hadi Oktober 2018.

Taarifa hiyo ilitolewa na Idara ya Utawala na Fedha ya chama hicho katika kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni.

Alipotafutwa Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, kupata ufafanuzi wa tuhuma hizo, alisema kuwa sheria inaizuia mamlaka kujadili hadharani masuala yanayohusu wateja wao.

“Kama suala hilo lipo nawashauri hivyo vielelezo wavilete, ila kama wameliwasilisha suala hilo kwenye ofisi zetu za Kinondoni basi litakuwa linafanyiwa kazi kiofisi.

“Na jinsi unavyonieleza wanaolalamika inaonesha ni wafanyakazi, wanaweza kuja wenyewe kupata mrejesho,” alisema Kayombo.

Pamoja na kuibuliwa kwa taarifa hizo, viongozi wa chama hicho akiwamo Rais wa Red Cross Tanzania, David Mwakiposa ambaye pia ni Katibu Tawala Wilaya ya Arusha pamoja na Katibu Mkuu Red Cross, Julius Kejo, hawajachukua hatua yoyote.

Juhudi za kumpata Mwakiposa kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa baada ya kudaiwa kuwa yuko jijini Nairobi nchini Kenya kwa shughuli za chama.

Kejo ambaye ni Mtendaji Mkuu wa shughuli za kila siku za chama alisema kuwa hafahamu jambo, hilo na kwamba kwa sasa yuko likizo.

“Upenipigia niko likizo labda mpaka nirudi ofisini niweze ‘kucheck’ na watu wa finance,” alisema Kejo.

Licha ya kumweleza mwandishi wa habari hizi kuwa atampa mawasiliano ya Mkurugenzi wa Fedha wa chama hicho, Udrick Nichoalus, jambo ambalo hakulitekeleza na hata alipogiwa simu tena simu yake iliita bila kupokewa.

Kutokana na hali hiyo gazeti hili lilimtafuta Makamu wa Rais wa chama hicho, Lucia Pande, ili kupata majibu ya masuala hayo ambaye alisema kuwa hawezi kulizungumzia, kwa sababu si msemaji wa chama na kuahidi kuwasiliana na Kejo ili alizungumzie.

Baada ya muda alipiga simu na kumtaka mwandishi wa habari hizi afike katika ofisi za chama aonane na Mkurugenzi wa Fedha ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, jambo ambalo lilifanyika bila mafanikio baada ya mwandishi kufika na kushindwa kupata ushirikiano kama ilivyoelekezwa.

Licha ya mwandishi kuonana na Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, David Uronu, hakuweza kutoa majibu ya suala hilo na kumtaka mwandishi awasiliane na Katibu Mkuu wa chama, licha ya kuelezwa kuwa Katibu Mkuu huyo ndiye aliyemwagiza mwandishi kuonana na Mkurugenzi wa Fedha.

Baada ya kuelezwa hivyo, Uronu alitoka ofisini kwake kwa muda na akidai kuwa anaenda kuwasiliana na Naibu Katibu Mkuu wa chama, John Busungu, na baada ya kurejea ofisini alimtaka mwandishi kusubiri Busungu ambaye kabla ya siku hiyo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu yeye si msemaji wa chama.

Katika hatua nyingine, kumekuwapo malalamiko ya kuanzishwa kwa cheo cha Naibu Katibu Mkuu wa Red Cross kwa lengo la kumlinda aliyekuwa Meneja Mkaguzi wa Ndani wa chama hicho, John Busungu, ambaye awali alituhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka na kufanya kazi ya ukaguzi bila kusajiliwa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Mahesabu (NBAA) kama sheria inavyoelekeza.

Chanzo hicho kilisema kuwa nafasi hiyo iliondolewa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Red Cross, Novemba mwaka 2018 kabla ya kurudishwa tena na mkutano huo Oktoba mwaka huu.

Kiliongeza kuwa licha ya nafasi hiyo kurejeshwa na mkutano huo wa Halmashauri Kuu, utaratibu wa kuanzishwa kwake haukuzingatia matakwa ya Katiba ya chama kifungu cha 42

(ii) kinachotaka mabadiliko yoyote yanayofanyika yawasilishwe kwenye Kamati Kuu ya pamoja ya Shirikisho la Vyama vya Red Cross na Red Crescent (IFRC) na kwenye Kamati ya Kimataifa ya Red Cross (ICRC), jambo ambalo halikufanyika.

“Tunachokiona sisi ni kwamba hawa watu wameamua kumlinda huyu mtu kwa sababu baadhi yetu wamekuwa wakihoji kwanini aajiriwe, wakati ilidaiwa hana sifa, lakini majibu yanayotolewa ni kwamba nafasi ya sasa haihitaji hizo sifa.

“Japo ni kweli kwamba kwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu haihitaji mtu awe na CPA, lakini hilo halimaanishi huyu mtu ana uhalali wa kufanya kazi hiyo, kwa sababu tayari alikwisha kutenda kosa mwanzoni,” kilisema chanzo hicho.

Kilisema kuwa pamoja na kukiukwa kwa Katiba, pia utaratibu wa kupatikana kwa mtu atakayeshika nafasi hiyo haukutangazwa kama ambavyo taratibu zinaelekeza, na kwamba hata mshahara na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Busungu ni batili kwa sababu mchakato wa kupatikana kwake ulikiuka katiba.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa tangu Busungu alipopewa cheo hicho amekuwa akikitumia vibaya kwa kuwahamisha baadhi ya watu ambao anaona hawakubaliani naye katika mambo anayoyataka, na kuwapeleka sehemu nyingine na hata kuwashusha vyeo bila kufuata utaratibu.

Kilidai kuwa kutokana na hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Busungu bila kuzingatia misingi ya chama na utu, zimesababisha chama hicho kunyang’anywa baadhi ya miradi iliyokuwa ukiwamo mradi wa kuhudumia wakimbizi katika Mkoa wa Kigoma unaohusisha kambi za Nyarugusu na Mtendeli, ambazo wamekuwa wakizisimamia tangu mwaka 2004.

“Kuna barua ambayo iliandikwa Septemba 15, mwaka huu, ikimtuhumi Busungu kwa tabia anazozifanya.

Barua hiyo ilitumwa kwa Rais aliyemaliza muda wake aitwaye Mwadini Jecha, lakini inakavujishwa kwa siri na ma mtu ambaye ameficha utambulisho wake na imenakiliwa kwa wafanyakazi 23, nadhani lengo la huyo mtu alitaka watu wajue kile kinachoendelea,” alisema mtoa taarifa huyo huku akionesha barua pepe hiyo.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom