Dar es Salaam.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar Salaam, Said Meck Sadiki amesema suala la udini lilikuwa moja ya changamoto alizokabiliana nazo baada ya kupewa jukumu la kuongoza mkoa huo.
Akizungumza katika hafla ya kumuaga iliyoandaliwa na Kamati ya Amani ya Mkoa huo, Sadiki alisema wakati anaingia Dar es Salaam alikuwa na wakati mgumu kwa kuwa ulikuwa ni wakati wa vuguvugu la uchaguzi.
“Niliingia Dar es Salaam Agosti 2010 nikiwa kaimu (mkuu wa mkoa). Nyinyi wenyewe kama viongozi wa dini nadhani hekaheka za vuguvugu la uchaguzi mnazifahamu, lakini kwa sala na dua zenu tulivuka,” alisema.
“Lakini muda si mrefu tukaingia kwenye msukosuko mkubwa wa mifarakano ya kidini. Sitaki kurejea jambo hilo, huo ndiyo ulikuwa mtihani mkubwa kwangu. Naweza kusema ndiyo ulikuwa mtihani mkubwa zaidi katika kazi yangu,” aliongeza.
Alisema suala hilo lilisababisha kuanzishwa kwa kamati hiyo iliyojumuisha viongozi wa dini mbalimbali na kuundwa kamati ndogo chini ya usimamizi wa Sheikh wa mkoa huo, Alhad Mussa ambayo kwa sasa ina zaidi ya wajumbe 40.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Maonda aliahidi kufanya yale yatakayolenga kuleta maendeleo katika mkoa huo na watu wake.
Pia, aliwaomba viongozi wa dini kusaidia kampeni ya kuondoa tatizo la madawati.
“Mkoa wa Dar es Salaam una upungufu wa madawati 68,000 kwa shule ya msingi na 34,000 kwa sekondari. Najisikia aibu sana kuanza na wahisani wakati sisi wenyewe tupo, hivyo ningependa kuanza na nyinyi viongozi wangu wa dini,” alisema.
Katika hafla hiyo, Sheikh Kassim Dewji na mfanyabiashara , Scaba Skuba walichangia madawati 150.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani, Sheikh Alhad aliwataka viongozi wa dini kuhakikisha kuwa waumini wao wanaunga mkono juhudi za Makonda kwa maendeleo ya Watanzania.
Sadiki alihamishiwa Mkoa wa Dar es Salaam mwaka 2010 akitokea mkoani Lindi.
Awali, mkuu huyo wa mkoa alikaimu nafasi hiyo mkoani humu. Kwa sasa amehamishiwa katika mkoa wa Kilimanjaro kuendelea na wadhifa huo.
Chanzo: Mwananchi