RC Kagaigai: Ukame Kilimanjaro umeua Ng’ombe 841, Kondoo 406 na Punda 10

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,802
11,961
Salaam Wakuu,

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, amepata 40% ya bajeti ya Maendeleo. Mkoa bado umeathiriwa na Ukame.

====

TAARIFA FUPI YA MKOA WA KILIMANJARO KWA
MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TAREHE 22 JANUARI, 2022


1. UKARIBISHO:

Mheshimiwa Rais,
Nitumie fursa hii kukukaribisha kwa mara nyingine tena Mkoani Kilimanjaro katika uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni ambalo wewe ni Mgeni Rasmi. Tunakushukuru kwa dhati kwa kukubali mwaliko wetu katika tamasha hili. Aidha, hali ya usalama katika Mkoa wetu imeendelea kuwa shwari na hivyo kuwapa fursa wananchi kuweza kuendelea na shughuli za kujiletea maendeleo bila hofu wala bugudha. Naomba pia nitumie fursa hii kutoa taarifa fupi ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo Mkoani hapa.

2. MAPOKEZI YA FEDHA ZA MAENDELEO MKOANI KILIMANJARO
Mheshimiwa Rais,
Tunakushuru sana, wewe na Serikali unayoiongoza kwa kuendelea kuupatia Mkoa wetu fedha nyingi za maendeleo ambapo katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2021, Mkoa ulipokea kiasi cha shilingi Bilioni 57.39 sawa na asilimia 40 ya bajeti yote ya maendeleo iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kupitia Sekretarieti ya Mkoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, TARURA, RUWASA na TANROADS.

Hiki ni kiwango kikubwa cha fedha za maendeleo kuwahi kupokelewa Mkoani hapa katika Nusu ya Kwanza ya mwaka wa fedha wa Serikali. Mheshimiwa Rais kwa niaba ya Wana-Kilimanjaro ninakushuru sana sana!!


Mheshimiwa Rais,
Katika fedha zilizopokelewa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa zinajumuisha fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 (TCRP) Shilingi Bilioni 7.88; fedha za tozo ya miamala ya simu Shilingi Bilioni 2.48; fedha za ruzuku ya maendeleo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa Shilingi bilioni 18.01, ujenzi wa shule mpya za sekondari za Kata Shilingi Bilioni 4.2 na fedha za Mpango wa Elimu kwa Matokeo (EP4R) Shilingi 418,119,997.

Mheshimiwa Rais,
Fedha zilizopokelewa kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa barabara ni shilingi Bilioni 22.44 na fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji zilipokelewa Shilingi Bilioni 1.9.

3. UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

Mheshimiwa Rais,
Fedha zote hizo zimeelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya utoaji wa huduma kwenye sekta ya Afya, Elimu, Maji, Barabara na Madaraja kwa mujibu wa maagizo na maelekezo ya Serikali.

Sekta ya Elimu

Mheshimiwa Rais,
Kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19, Mkoa wa Kilimanjaro umeweza kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 276 katika shule za Sekondari na madarasa 18 ya vituo shikizi vya elimu ya Msingi ambapo ujenzi wa mabweni mawili kwa ajili wanafunzi wenye mahitaji maalum unaendelea. Aidha, hivi sasa Mkoa unaendelea na maandalizi ya ujenzi wa shule mpya tisa za sekondari za Kata na ukamilishaji wa maboma 19 ya vyumba vya madarasa. Vilevile, kufuatia kuanza kwa mhula mpya wa masomo kwa mwaka 2022 Mkoa unaendelea na zoezi la uandikishaji wa watoto kwa ajili ya darasa la awali na la kwanza ambapo jumla ya wanafunzi 33,906 wa awali na wanafunzi 35,500 wa darasa la kwanza wanatarajiwa kuandikishwa.
Mheshimiwa Rais,
Kwa upande wa elimu ya Sekondari, jumla ya wanafunzi 30,710 walifaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2021 na wote kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022. Hii imewezekana kutokana na vyumba vipya vya madarasa 276 yaliyojengwa na Serikali kupitia jitihada zako binafsi na Serikali unayoiongoza. Mheshimiwa Rais, tunasema asante kwa moyo wako wa kipekee ulionao kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla.

Sekta ya Afya:

Mheshimiwa Rais,
Katika sekta ya Afya kwa sasa Mkoa wetu unaendelea na ujenzi wa majengo ya huduma za dharura katika hospitali za Halmashauri za Wilaya ya Rombo na Same, ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga na katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi. Miradi mingine ni ujenzi wa nyumba saba za watumishi wa afya zenye uwezo wa kuchukua familia tatu kila moja na pia ujenzi wa vituo vya afya tisa unaotekelezwa katika majimbo yote ya uchaguzi mkoani hapa.

Sekta ya Miundombinu:

Mheshimiwa Rais,
Katika sekta ya miundombinu kuna jumla ya miradi 28 inayoendelea kutekelezwa na miradi mingine mitano ipo katika hatua ya taratibu za ununuzi chini ya usimamizi wa Wakala TARURA na TANROADS. Miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa barabara mpya kwa kiwango cha lami, upanuzi wa barabara, matengenezo ya muda maalum na matengenezo ya maeneo korofi. Kukamilika kwa miradi hii ni dhahiri kutaimarisha huduma za usafiri na usafirishaji mkoani hapa na hivyo kuwa ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi na kipato cha wananchi.



Sekta ya Maji:

Mheshimiwa Rais,
Kupitia Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), Mkoa unatekeleza jumla ya miradi minne ya upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya maji katika wilaya za Siha na Same ambapo wananchi wa vijiji sita vya wilaya hizo watanufaika.

4. UTOAJI WA CHANJO DHIDI YA UVIKO-19

Mheshimiwa Rais,
Katika kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa wa UVIKO-19 Mkoa wa Kilimanjaro umeendelea na zoezi la uhamasishaji na utoaji wa chanjo ya hiari kwa wananchi ambapo lengo la Mkoa ni kuchanja watu 1,165,832 ifikapo mwezi Juni 2022. Mikakati inayotumika ni pamoja na ushirikishwaji wa jamii na wadau wengine mbalimbali kupitia viongozi wa ngazi ya jamii, taasisi za dini na mashirika yasiyo ya kiserikali.

5. MIRADI YA KIMKAKATI

Mheshimiwa Rais,
Kwa sasa, katika Mkoa wetu tunao mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Moshi unaotekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali Kuu na Manispaa ya Moshi kwa gharama ya shilingi Bilioni 17.86. Kiasi kilichotumika hadi sasa ni shilingi Bilioni 7.3 ambapo kwa sasa ujenzi umesimama na unatarajiwa kuendelea mara baada ya Halmashauri kupokea fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, kiasi cha shilingi Bilioni 10.56. Kukamilika kwa Mradi huu kutarahisisha utoaji wa huduma za usafiri kwa wananchi na wasafiri katika ukanda huu wa Kaskazini mwa nchi na pia kuongeza mapato kwa Serikali.


6. CHANGAMOTO
Mheshimiwa Rais,
Changamoto kubwa inayowakabili wananchi mkoani Kilimanjaro kwa sasa ni kutonyesha kwa mvua za vuli hali iliyosababisha ukame na ukosefu wa malisho ya mifugo katika baadhi ya maeneo hususan kwa Wilaya ya Mwanga na Same ambapo jumla ya Ng’ombe 841, Kondoo 406 na Punda 10 wameripotiwa kufa hadi sasa kwa kukosa malisho na maji.

Mheshimiwa Rais,
Pamoja na kuwepo kwa changamoto hizo, naomba nikuhakikishie kwamba, Mkoa umejitosheleza kwa chakula. Hii ni kutokana na kuwa na ziada ya ulizalishaji wa chakula tani 40,790 za Wanga na tani 10,147 za Mikunde (Protini) katika msimu wa mvua za mwaka 2020/2021.

7. HITIMISHO
Mheshimiwa Rais,
Kwa kuhitimisha, tunaendelea kuishukuru Serikali unayoingoza kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za wananchi wa Mkoa huu za kujiletea maendeleo. Hii imedhihirishwa na kiasi kikubwa cha fedha za maendeleo ambazo zinaendelea kutolewa na Serikali. Pia, tunakushukuru wewe binafsi kwa utayari wako kwani kila ulipoombwa kujumuika nasi katika shughuli za uhamasishaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ulikubali. Hii inatupa faraja na matumaini makubwa kwa uongozi wako. Mwenyezi Mungu azidi kukubariki na kukutia nguvu ya kuendelea kuwatumikia Watanzania ambao wameonyesha kuwa na imani na matarajio makubwa kwako
Mheshimiwa Rais, naomba kuwasilisha.

KILIMANJARO HOYEE !!!

MHESHIMIWA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN HOYEE !!!

Stephen N. Kagaigai
MKUU WA MKOA
KILIMANJARO
 
Ukame ni laana ya kumbambikia chief Abobakar Mbowe KESI ya kuchonga ya ugaidi.
 
Back
Top Bottom