Mwanahabari wa Taifa
JF-Expert Member
- May 27, 2020
- 1,450
- 799
Kampuni ya kichina ya CHICCO yatekeleza agizo la RC Kafulila, tayari imekamilisha marudio ya barabara yenye urefu wa kilometa 10 zenye thamani ya tzs15bl.
==
Kampuni ya Kichina ya CHICCO inayotekeleza ujenzi wa Barabara ya Mwigumbi - Maswa yenye urefu wa kilomita57, ilianza ujenzi tangu mwaka 2018 kwa thamani ya zaidi ya shilingi za kitanzania billion 75. Wachina hawa walikwaa kisiki baada ya kutakiwa kurudia ujenzi wa vipande vya barabara vinavyofikia kilometa 10 kutokana na kujenga chini ya kiwango kilichowekwa.
Agizo hilo la kutakiwa kurudia ujenzi lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe David Kafulila Juni 5, 2021 ikiwa ni wiki moja tu baada ya kuripoti mkoani Simiyu kama Mkuu wa Mkoa mpya. Leo ikiwa ni mwaka mmoja sasa tangu agizo hilo, RC Kafulila akihojiwa na kituo cha EATV amekiri kuridhishwa na kazi iliyofanywa na kwamba ujenzi upo zaidi ya asilimia 96% kwa viwango vinavyokubalika.
"Nakumbuka ilikuwa ni wiki ya kwanza baada ya kuripoti kama RC, hii barabara niliona wakati nakuja kuripoti Simiyu. Nilifanya ziara na Bodi ya Barabara na kuelekeza marudio ya barabara na kumwelekeza mkandarasi kurudia. Nilimsisitiza barabara yake haitapokewa na Mhe. Rais ikiwa chini ya kiwango" alisema Kafulila na kuongeza kuwa, "mbali ya kurudia barabara, pia mshauri mwelekezi(consultant) alibadilishwa. Sasa watu wote wakipita wanafurahi kuona serikali sasa itapokea barabara imara sawa na thamani ya fedha zao wanazozitoa kupitia kodi na tozo mbalimbali."
"Huu ni ujumbe wangu kwa wakandarasi wote mkoani Simiyu, hakuna mradi utakaopokelewa ukiwa chini ya kiwango. Kwasasa nina amani hata Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan akipita kukagua nina amani kwamba fedha iliyoletwa ndani ya mkoa wetu kwajili ya barabara na hata miradi mingine, thamani ya pesa(value for money) inaonekana. Wakandarasi wababaishaji hawana nafasi, nimeshavunja na nitaendelea kuvunja mikataba na kila mbabaishaji aliyepata mradi kwa bahati mbaya Simiyu," alisisitiza zaidi.
"Serikali inalaza mabilioni ya fedha barabaran ndio maana lazma kuhakikisha tunabanana. Yaani gharama kilomita 1 ya lami ni takribani 1.5 bn., pesa ambazo zinatosha kukamilisha majengo ya kituo cha afya. Sasa upewe mabilioni yote hayo na bado ukabidhi barabara ambayo baada ya mwaka tu imeharibika na kuhitaji mabilioni mengine ya ukarabati? Huu ni ushenzi ambao hauwezi kupewa nafasi ndani ya awamu ya sita, na kwa upande wetu tutatimiza kipande chetu Simiyu, " alimalizia.
#SISITUKO TAYARI KUHESABIWA TAREHE 23/08/2022,WEWE JEE?!