Nimeshindwa kuelewa kama hii ni spinning ama ni makosa ya mwandishi wa habari? Kichwa habari kama hicho ukisoma haraka haraka unaweza kudhani kwamba Mkuu wa Mkoa ameagiza watu wajichukulie sheria mkononi kwa kuwatwanga risasi wahujumu wa korosho. Lakini kumbe ni usanii wa wana siasa wa Bongo. Huyo Mhagama mwenyewe sina hakika kama ana maanisha hayo aliyoyasema, si ajabu alikuwa akiwakejeri wakulima wa zao la korosho ambao ndiyo watakao umia, maana inawezekana korosho zikanunuliwa na bado wakulima wasilipwe haki yao kwa wakati muafaka! Hii ndiyo Bongo bwana, longolongo kuanzia juu mpaka chini.
RC aagiza wahujumu korosho wapigwe risasi
Na Mashaka Mgeta, Mtwara
Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Bw. Beno Mhagama, amevitaka vyombo vya ulinzi, kuwapiga risasi watumishi wa umma, watakaobainika kuwahujumu wakulima wa korosho mkoani hapa.
Bw. Mhagama, alitoa kauli hiyo juzi, mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Anatory Tarimo, wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya kamati maalum iliyoundwa kushughulikia ununuzi wa zao hilo, kwa mfumo mpya wa stakabadhi ya maghala.
Msimu wa ununuzi wa korosho ulioanza Oktoba mwaka huu, mkoani hapa, unaendelea, huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakulima na wanunuzi wa zao hilo.
Kwa upande wao, wakulima wanadai kuwapo mazingira yanayoashiria kutolipwa fedha wanazostahili kwa awamu ya pili, huku wanunuzi binafsi wakidai mfumo wa uuzaji korosho kwa njia ya zabuni, unafanywa kwa siri, na hivyo kuweka mianya ya kuwahujumu.
``Kwa vile tupo hapa na wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, naomba niseme tukishindwa kutimiza wajibu wetu, tukawahujumu wakulima wa korosho, basi mtupige risasi, lakini ninaamini hatutashindwa,`` alisema.
Hata hivyo, Bw. Mhagama, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati maalum iliyoundwa na Bw. Tarimo, alisema hakuna mpango wa kutimiza matakwa ya wafanyabiashara, kwa kubadili mfumo wa uuzaji korosho kwa njia ya zabuni.
Alisema, mfumo huo unatoa wigo mpana wa ushindani na hivyo kulifanya zao hilo kuwa na thamani kubwa. Hoja hiyo iliungwa mkono na Bw. Tarimo, aliyehoji uhalali wa wafanyabiashara hao kutaka uuzaji wa korosho kuwa wazi, wakati wenyewe (wafanyabiashara), hawaelezi bei ya korosho katika soko la nje.
Aidha, kuhusu malipo ya pili kwa wakulima wa korosho, Bw. Mhagama, alisema yanatarajiwa kulipwa kabla ya Desemba 31, mwaka huu.
Pia, Bw. Mhagama, alisema ununuzi wa korosho ya daraja la pili, itanunuliwa kabla ya kumalizika kwa msimu wa mwaka huu, tofauti na taarifa zilizoenea kuhusu kutokuwapo mpango wa kuzinunua.
Bw. Mhagama, alisema kuna hatari kwa baadhi ya korosho kushindwa kusafirishwa kutoka katika baadhi ya maeneo, yanayokabiliwa na ubovu wa barabara, pindi mvua zitakapoanza kunyesha.
Kutokana na changamoto hiyo, Bw. Tarimo, aliwaagiza wakuu wa wilaya mkoani hapa, kuhakikisha kuwa jitihada za makusudi zinafanywa, ikiwamo kutoa kipaumbele cha usafirishaji wa korosho zilizopo katika maeneo yenye tatizo hilo.
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Mtwara, Bi. Catherine Ndahani, alisema kasoro zilizojitokeza katika msimu wa uuzaji wa korosho, zinakiathiri chama hicho na Serikali kwa ujumla.
``Sisi ni wanasiasa, tumezunguka hadi vijijini na kilio cha wakulima wengi, ni kutokuwa na uhakika wa kulipwa fedha zao za korosho kwa awamu ya pili, sasa tunaomba watu waliopewa dhama hiyo, kuhakikisha wanaziondoa kasoro hizo,`` alisema.
SOURCE: Nipashe