nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,862
- 5,797
Wednesday, 21 September 2011 20:19 |
Kizitto Noya KADA wa CCM, Mohamed Raza, amehoji mantiki ya dhana ya 'kujivua gamba' kama baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi hawataki kuwajibika, wala chama kuwawajibisha.Akizungumza Dar es Salaam jana, Raza alisema ana shaka na umakini wa CCM kusimamia mambo yake, huku akihoji sababu zinazowafanya watuhumiwa wa ufisadi wang'ang'anie kuwapo ndani ya chama hicho tawala. "Kuna maswali ya kujiuliza hapa, hivi kiburi hiki hawa wenzetu (watuhumiwa) wamekitoa wapi au ndiyo ile tabia ya mambo ya kujuana na kubebana kwa viongozi?" alihoji Raza na kuongeza: Tunaamini chama hakimwonei mtu kwa rangi wala kabila, kwa sababu hakuna mtu maarufu kuliko chama. Hivi kama kila unakopita watu wanakung'ong'a, kwa nini usijiondoe? Kuna watu leo wanashindwa kupita Manzese, Mbagala hata Kariakoo kwa aibu, kwa nini wasitoke?" Alisema tuhuma za ufisadi zinazowakabili watuhumiwa hao, zinatosha kuwafanya wawajibike kama kweli wanakitakia mema chama, vinginevyo wanakifanya chama na Serikali yake vipoteze umaarufu kwa wananchi. Raza ambaye hakuwataja kwa majina watuhumiwa hao wanaotakiwa kujivua gamba, alikigeukia chama chake cha CCM na kwamba, iwapo watendaji hawataacha unafiki, nchi itayumba. "Hivi kweli CCM tunahitaji kusubiri wapinzani watuletee majina ya mafisadi? Hawajulikani au tunawalinda?" alihoji Raza ambaye alieleza kuwa urafiki na kujuana, ni mambo yanayokivuruga chama hicho. Aliendelea: "Mabilioni ya fedha yanaibiwa, lakini sisi tunaishia kuunda tume kama siyo kujuana ni nini. Kulikuwa na haja gani ya kuunda tume kwa ajili ya kuchunguza wizi wa EPA ambao uko wazi na watuhumiwa wapo? "Zimeshaundwa tume nyingi tu hapa. Hata kwenye chama kuna kamati ya Mwinyi ambayo majibu yake bado ni kitendawili...tabia hii ya kuunda tume halafu matokeo yake hayatangazwi haina msingi wowote zaidi ya kujuana. "Kuna tume ya kuchunguza jinsi fedha za EPA zilivyoibwa, tume ya kuchunguza mikataba ya madini, lakini mpaka leo bado tunasubiri wapinzani wakatuibie matokeo yake waje kututangazia." Katika hatua nyingine, Raza alizungumzia mchakato wa katiba mpya, akisema Wazanzibari wanataka kuwe na Miswada miwili; Muswada wa Wazanzibari na Muswada wa Watanganyika. "Kumekuwa na mambo mengi watendaji wetu hawawi wakweli. Tunaupenda Muungano, lakini tunataka Watanganyika wasitulazimishe kwa kuwa hatukulazimishana kuungana. Katika umoja huu, tuheshimiane, tuvumiliane na tujadiliane," alisema Raza na kuongeza: Tusikubali kwenda kujadili Katiba mpya kama hakutakuwa na miswada miwili, vinginevyo Zanzibar itakwisha...The world is talking about peoples power (dunia inazungumzia nguvu ya umma), kama viongozi hawataki, wakae pembeni, wawaache wananchi wajadili masuala yao." Raza alisema anaamini Katiba itakayopatikana baada ya kuwasilishwa miswada miwili bungeni, itakidhi matakwa ya wananchi wa Tanzania kuliko katiba itakayopatikana baada ya muswada wake kuwasilishwa na Serikali ya Muungano, ambayo kimsingi ni Serikali ya Tanganyika. "Kuna kasoro nyingi kwenye katiba ya sasa, ambayo kama hatutakuwa makini kuzirekebisha kupitia mchakato sahihi wa mabadiliko ya katiba, zitaendelea kuwapo na kuwatafuna Watanzania na vizazi vyao, alisema. |