Raza aishangaa CCM: Uamuzi wa NEC Butiama

Mtu wa Pwani

JF-Expert Member
Dec 26, 2006
4,191
674
Raza aishangaa CCM
UAMUZI WA NEC BUTIAMA



na Mwanne Mashugu na Saada Said, Zanzibar



MFANYABIASHARA maarufu wa Zanzibar na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mohammed Raza, ameeleza kushangazwa na uamuzi wa halmashauri kuu ya chama hicho kutaka kuitisha kura ya maoni kuhusu serikali ya mseto visiwani hapa.

Raza alionyesha mshangao huo alipozungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Kibweni, mjini Zanzibar kuhusu mwafaka uliofikiwa kati ya vyama vya CCM na CUF, na suala la muungano yanavyoiathiri Zanzibar.

Alisema pamoja na Halmashauri Kuu ya CCM kuamua suala la kura ya maoni, kimsingi halina faida kwa wananchi kutokana na uelewa mdogo walionao na pia uamuzi huo hauna nguvu kisheria.

Mfanyabiashara huyo alisema kura iliyoamuliwa kuitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM ni jambo lisilowezekana, kwa vile hakuna sheria inayozungumzia suala hilo katika sheria za uchaguzi Zanzibar.

Pia alisema Zanzibar hakuna chombo huru kitakachoweza kusimamia kura ya maoni, hivyo kuleta suala hilo ni kubebeshwa mzigo serikali na kupoteza fedha za walipa kodi, hasa ikizingatiwa muda uliobaki ni mfupi kuweza kukusanya maoni hayo.

“Tuwe wawazi jamani, kura ya maoni inayoletwa mbona hatuna muda tena wa kwenda kwenye kura ya maoni? Unaposema wananchi wapige kura ya maoni unamaanishi nini? Na ya nini?” alihoji Raza ambaye pia aliwahi kuwa mshauri wa mambo ya michezo katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kipindi cha utawala wa Rais mstaafu Dk. Salmin Amour Juma.

Alisema haoni sababu ya kuwapo kura ya maoni, kwa kuwa tatizo kubwa linaloikabili Zanzibar ni matokeo ya uchaguzi, hivyo hata kura ya maoni haitaweza kusaidia kitu.

Hata hivyo, alisema mpasuko kisiasa Zanzibar unaweza kutatuliwa kwa saa tatu iwapo viongozi wa CCM na CUF wataweka nia ya kweli kumaliza matatizo ya Wazanzibari.

Alisema wananchi wa Zanzibar wana uwezo wa kutatua matatizo yao wenyewe isipokuwa hadi sasa nia njema haipo na ndiyo maana miafaka miwili imekwama, ukiwamo ule uliosimamiwa na Jumuiya ya Madola mwaka 1999.

“Mwafaka wa Zanzibar unaweza kupatiwa ufumbuzi na Wazanzibari wenyewe kwa kuamua kukaa pamoja badala ya kukimbiana,” alisema Raza.

Alieleza kuwa wawakilishi wa CCM na CUF wapo, wana uwezo wa kukaa kujadili matatizo ya kisiasa Zanzibar, kwa vile wao ndio wawakilishi wa wananchi.

Alisema kwakuwa Rais Amani Abeid Karume amebakisha muda mfupi kumaliza kipindi chake, ni vema vyama vya CCM na CUF kutumia muda mwingi kuweka mazingira mazuri yatakayosaidia uchaguzi ujao kuwa huru na wa haki.

“Vyama vya CCM na CUF ni vyema vikae vitazame yale mapungufu yanayotokea katika chaguzi zetu, ili kuepuka mambo yaliyotokea Kenya,” alisema Raza.

Alieleza kuwa matatizo ya kisiasa yaliyotokea Kenya ni funzo kubwa kwa Wazanzibari na hakuna njia ya kutatua matatizo ya kisiasa zaidi ya viongozi kukaa pamoja na kumaliza tafauti zao.

“Lazima tukumbuke kila mtu aliyeiumiza Zanzibar, fimbo ya Mwenyezi Mungu itamgusa,” alionya mfanyabiashara huyo.

Alieleza kwamba Zanzibar hivi sasa inakabiliwa na fitina na majungu, hali iliyosababisha wataalamu wengi kuikimbia, hivyo uchumi wake kurejea nyuma.

Alitoa mfano kuwa yeye mwenyewe aliweka mabango ya biashara Uwanja wa Amaan na kulipia mamilioni ya fedha, lakini baada ya mabadiliko ya uongozi alijitokeza mkubwa mmoja na kusema yaondolewe, bila ya kuzingatia faida iliyokuwa ikipatikana.

Raza alisema Zanzibar hivi sasa inakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi kutokana na Tanzania Bara kuibana kiuchumi.

Pia alisema kero za muungano zitaweza kutatuliwa kwa muda mfupi iwapo viongozi wastaafu, akiwemo Dk. Salmin Amour, Aboud Jumbe Mwinyi, Mzee Rashid Kawawa na Cleopa Msuya watashirikishwa.



tanzania daima
 
Back
Top Bottom