Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya 14 Katika Katiba ya Tanzania

nivoj.sued

JF-Expert Member
Jul 14, 2009
220
250
1583602839078.png

Wadau,

Nimepitia uzi wenye jina "Utumwa wa Tume ya Uchaguzi Tanzania" na kupenda mjadala ule ambao mpaka sasa umeshirikisha watu 9000. Pia nimepitia mabandiko mengine yenye kujadili mada hii tangu mwaka 2015. Hivyo nimeshawishika kuandika rasimu ya mabadiliko ya katiba yanayojadiliwa. Nayaweka hapa chini. Karibuni...

=============================KIAMBATANISHO==========================

RASIMU YA MUSWADA WA SHERIA YA MABADILIKO YA KUMI NA TANO KATIKA KATIBA YA NCHI, YA MWAKA 2020

Sheria Na. YXZ ya 2020

NINAKUBALI
…………………………………………………….
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

YALIYOMO

1. Utangulizi
2. Jina la sheria na tarehe ya kuanza kutumika
3. Mipaka ya matumizi ya sheria
4. Kufanya mabadiliko katika katiba
5. Kufanya mabadiliko katika ibara ya 39
6. Kufanya mabadiliko katika ibara ya 41
7. Kufanya mabadiliko katika ibara ya 66(a)
8. Kufanya mabadiliko katika ibara ya 66(b)
9. Kufanya mabadiliko katika ibara ya 74
10. Nyongeza ya ibara mpya ya 74A
11. Kufanya mabadiliko katika ibara ya 77
12. Kufanya mabadiliko katika ibara ya 78

Utangulizi

Sheria ya kufanya mabadiliko katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kurekebisha mambo kadhaa kutokana na maoni ya wananchi yaliyotolewa kupitia Tume za Jaji Nyalali mwaka 1991, Jaji Kisanga mwaka 1998, Jaji Warioba mwaka 2011 na wananchi baki baada ya Tume hizo tatu, kuhusu kiwango cha uhuru wa vyombo vya kusimamia uchaguzi na kiwango cha ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi ya kisiasa nchini. Sheria hii imetungwa kihalali na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jina la sheria na tarehe ya kuanza kutumika

1. Sheria hii itakuwa na jina lake rasmi na tarahe rasmi ya kuanza kutumika.
(1) Sheria hii iitwe Sheria ya Mabadiliko ya Kumi na Tano katika Katiba ya Nchi, ya mwaka 2020.
(2) Sheria hii itaanza kutumika tarehe 1 Julai 2020.

Mipaka ya matumizi ya sheria

2. Sheria hii itatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Kufanya mabadiliko katika katiba

3. Masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya Mwaka 1977, ambayo katika ibara zifuatazo za sheria hii itatajwa tu kwa kifupi kama “Katiba,” yanabadilishwa kwa namna ilivyoelekezwa katika ibara za Sheria hii zifuatazo.

Kufanya mabadiliko katika ibara ya 39

4. Ibara ya 39 ya Katiba inafanyiwa mabadiliko kwa kuongeza ibara ndogo ya (3) yenye maneno yafuatayo:

(a) Kofia ya madaraka ya urais na kofia ya madaraka ya uenyekiti wa chama cha siasa zitatenganishwa kwa mujibu wa Katiba hii.

(b) Hakuna mtu atakaye kuwa na sifa za kuchaguliwa kushika kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano kama ni Mwenyekiti wa chama cha siasa.

(c) Ikitokea kwamba tayari kuna mtu amekwisha kuchaguliwa kushika nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano akiwa bado amevaa kofia ya uenyekiti wa chama cha siasa, basi atapoteza kofia hiyo mara tu baada ya sheria hii kuanza kufanya kazi.

Kufanya mabadiliko katika ibara ya 41

5. Ibara ya 41 ya Katiba inafanyiwa mabadiliko kwa kufuta maneno yote yaliyo katika ibara ndogo ya (7) na badala yake kuweka maneno yafuatayo:

(a) Mtu yeyote ambaye ni mpiga kura anaweza kufungua kesi katika Mahakama Kuu kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais Mteule ndani ya siku saba baada ya siku tangazo la matokeo ya uchaguzi wa Rais lilipofanywa.

(b) Ndani ya siku 14 baada ya kesi kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais Mteule kusajiliwa, Mahakama Kuu itasikiliza kesi na kuitolea uamuzi na uamuzi wake utakuwa ni wa mwisho.

(c) Endapo Mahakama Kuu itaamua kwamba uchaguzi wa Rais Mteule ni haramu, basi uchaguzi mpya itapaswa kufanyika ndani ya siku sitini baada ya siku ya uamuzi huo.

Kufanya mabadiliko katika ibara ya 66(a)

6. Ibara ya 66 ya Katiba inafanyiwa mabadiliko katika ibara ndogo ya (1) kwa kufuta maneno yote yaliyo katika kifungu cha (a) na badala yake kuweka maneno yafuatayo:

Wabunge waliochaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi, ambao watakuwa katika makundi mawili:

(i) kundi la kwanza litakuwa ni wabunge wa kuchaguliwa wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi;

(ii) kundi la pili litakuwa ni wabunge wenza katika majimbo ya uchaguzi waliochaguliwa baada ya kuteuliwa na wabunge wa kuchaguliwa wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi;

(iii) litakuwa ni sharti la lazima kwamba, kila mbunge mwenza awe na jinsi iliyo kinyume cha jinsi ya mbunge wa kuchaguliwa aliyemteua;

Kufanya mabadiliko katika ibara ya 66(b)

7. Ibara ya 66 ya Katiba inafanyiwa mabadiliko katika ibara ndogo ya (1) kwa kufuta maneno yote yaliyo katika kifungu cha (b) na badala yake kuweka maneno yafuatayo:

(i) Kila mgombea wa jimbo la uchaguzi atamteua mtu mmoja mwenye jinsia iliyo tofauti na yake, na mwenye sifa zote za lazima kwa ajili ya kugombea ubunge, kuwa mgombea mwenza katika nafasi ya ubunge wa jimbo husika, na mtu huyo aliyeteuliwa atasimama kama mgombea katika nafasi ya mbunge mwenza;

(ii) Ndani ya siku saba baada ya kuteuliwa kwa mgombea wa jimbo la uchaguzi, litakuwa ni jukumu la mgombea wa jimbo kumfahamisha msimamizi wa uchaguzi, kwa kutoa taarifa zote muhimu katika fomu maalum, juu ya kuteuliwa kwa mgombea mwenza wa ubunge, na taarifa hiyo itatosheleza mahitaji ya kisheria kwa ajili mgombea mwenza kutambuliwa na msimamizi wa uchaguzi”;

(iii) Tume ya Taifa ya Uchaguzi itamtangaza mgombea mwenza wa jimbo la uchaguzi ambaye alichaguliwa na mgombea wa jimbo la uchaguzi aliyeshinda kuwa mbunge mwenza.

Kufanya mabadiliko katika ibara ya 74

8. Ibara ya 74 ya Katiba inafanyiwa mabadiliko kwa kufuta maneno yote yaliyo katika ibara hiyo na badala yake kuweka maneno yafuatayo:

(1) Kutakuwepo na Tume Huru ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano itakayotekeleza majukumu yote yanayohusiana na uchaguzi na kura ya maoni;

(2) Majukumu ya Tume Huru ya Uchaguzi yatakuwa ni:

(a) kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Rais, Wabunge, Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Jamhuri ya Muungano;

(b) kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais, Wabunge, Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa;

(c) kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge, lakini kwa kuzingatia masharti yafuatayo: msongamano wa watu, miundombinu ya kijamii, mshikamano wa kihistoria na kitamaduni, gharama za uendeshaji, maoni ya wananchi wanaoishi katika eneo husika, malengo ya kusogeza huduma karibu na watu, na mazingira ya kijiografia;

(d) kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura na uendeshaji wa uchaguzi wa madiwani; na

(e) kutekeleza majukumu mengine yoyote kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.

(3) (a) Tume Huru ya Uchaguzi itakuwa na wajumbe kumi ambao watakachaguliwa kwa mujibu wa Katiba hii;

(b) Katika ngazi ya Taifa kutakuwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, pamoja na wajumbe wengine nane;

(c) Uteuzi wa wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi utafanyika kwa kuzingatia tunu za Taifa, elimu, uzoefu, uadilifu na kanuni ya uwiano, ambapo idadi ya wajumbe wote kwa pamoja, inapaswa kuakisi tofauti za jiografia na nasaba za watu wa Tanzania;

(d) Uteuzi wa Makamu wa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi utafuata kanuni kwamba endapo Mwenyekiti ni mtu anayetoka sehemu moja ya Muungano, Makamu wake atakuwa ni mtu anayetoka sehemu ya pili ya Muungano.

(4) (a) Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi watakuwa ni watu walio na elimu, uzoefu, uadilifu, na weledi wa kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kasi na ufanisi stahiki;

(b) Mwenyekiti wa Tume atakuwa ni mtu mwenye sifa zinazomwezesha kushika nafasi ya Ujaji wa Mahakama Kuu;

(c) Vigezo vifuatazo vitamwezesha mtu kupata sifa ya kuweza kuteuliwa kuwa mjumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi, yaani, endapo mtu huyo: (i) ni raia wa Tanzania; (ii) anayo shahada kutoka chuo kikuu kinachotambulika; (iii) anao uzoefu uliothibitika katika mojawapo ya nyanja zifuatazo: masuala ya uchaguzi, au utawala, au fedha, au uongozi, au uchumi, au sheria, au elimu ya maendeleo;

(d) Chochote kati ya vigezo vifuatazo kitamzuia mtu kupata sifa ya kuweza kuteuliwa kuwa mjumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi, yaani, endapo mtu huyo ni: (i) Waziri; (ii) Naibu Waziri; (iii) Mbunge; (v) Diwani; (vi) Kiongozi wa chama chochote cha siasa; (vi) Mtu ambaye ni mtumishi wa umma kwa wakati uliopo; (viii) Mtu ambaye ndani ya miaka mitano iliyopita, ameshika madaraka, au kugombea katika nafasi ya: ubunge, au udiwani, au uongozi wa chama chochote cha siasa; (ix) mtu mwenye madaraka ya aina yoyote iliyotajwa mahususi na sheria iliyotungwa na Bunge kwamba ni mwiko kwa mtu mwenye madaraka hayo kuwa mjumbe wa Tume ya Uchaguzi;

(5) Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya ibara hii, Mjumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi atakoma kuwa Mjumbe litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo:

(a) akimalizika muda wa miaka mitano tangu alipoteuliwa; au

(b) ikiwa litatokea jambo lolote ambalo, kama asingekuwa Mjumbe wa Tume, lingemfanya asiweze kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi.

(6) uteuzi wa wajumbe wa tume waweza kusitishwa lakini baada ya kufuata utaratibu wote wa kusimamia nidhamu ya watumishi wa umma kwa mujibu wa sheria

(7) Kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu yake yaliyoainishwa katika ibara hii, Tume ya Uchaguzi itakuwa ni idara huru inayojitegemea, itafanya maamuzi yake rasmi kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa vikao, na mtendaji mkuu wake atakuwa ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye atateuliwa na kufanya kazi kwa mujibu wa masharti ya sheria iliyotungwa na Bunge.

(8) Tume ya Uchaguzi yaweza kutekeleza shughuli zake bila ya kujali kwamba kuna nafasi miongoni mwa viti vya wajumbe au kwamba mjumbe mmojawapo hayupo, lakini kila uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ni lazima uungwe mkono na wajumbe walio wengi kati ya wajumbe wote wa Tume ya Uchaguzi.

(9) Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti ya kuweka utaratibu wa kuwateua Wajumbe wa kusimamia uchaguzi wa Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi na, bila ya kuathiri masharti ya Sheria kama hiyo au maagizo ya Tume ya Uchaguzi, madaraka ya Tume ya Uchaguzi ya kusimamia uchaguzi yaweza kutekelezwa na wajumbe hao, kwa kuzingatia sharti kwamba wajumbe hao wasiwe wamewahi kuwa watumishi wa serikali ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.

(10) Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii, Tume ya Uchaguzi haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya Serikali, au maoni ya chama chochote cha siasa.

(11) Isipokuwa kama imeelezwa vinginevyo na Katiba hii, hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.

(12) Katika utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii, Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano itashauriana mara kwa mara na Tume ya Uchaguzi ya Tanzania Zanzibar.

(13) Itakuwa ni marufuku kwa watu wanaohusika na uchaguzi kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu kwamba kila mmoja wao atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa kwa mujibu wa Katiba hii.

(14) Kwa madhumuni ya Katiba hii watu wanaohusika na uchaguzi ni– (a) Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi; (b) Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi; (c) Wajumbe wote wa Tume ya Uchaguzi; (d) Mkurugenzi wa Uchaguzi pamoja na watumishi wote wa Tume ya Uchaguzi; (e) Wasimamizi wote wa Uchaguzi katika miji na wilaya zote.

Nyongeza ya ibara mpya ya 74A

9. Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi watapatikana kwa mujibu wa utaratibu uliotamkwa ndani ya Katiba hii chini ya ibara hii.

(1) Ndani ya siku 7 baada ya kuanza kwa sheria hii, baada ya Spika kushauriana na Kamati ya Uongozi ya Bunge, atateua Jopo la Kuajiri Tume, litakalojumuisha: (a) mwanamke na mwanamume walioteuliwa na Rais; (b) mwanamke na mwanamume walioteuliwa na Waziri Mkuu; (c) mwanamke na mwanamume walioteuliwa na Tume ya Ajira ya Mahakama; (d) mwanamke na mwanamume walioteuliwa na TAKUKURU; na (e) mwanamke na mwanamume walioteuliwa na chama cha wanasheria wa Tanganyika.

(2) Haraka iwezekanavyo, kila mamlaka ya uteuzi wa wajumbe wa Jopo la Kuajiri Tume iliyotajwa hapo juu itamwandikia Katibu wa Bunge ili kuwasilisha majina ya watu wawili walioteuliwa.

(3) Mara tu baada ya kupokea majina ya watu walioteuliwa, Katibu wa Bunge ataitisha kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge, ambacho kitapitia majina yote na ama kuyathibitisha yote, au kuyathibitisha baadhi, au kuyakataa yote au au kuyakataa baadhi.

(4) Katibu wa Bunge atazifahamisha mamlaka za uteuzi wa wajumbe wa Jopo la Kuajiri Tume kuhusu kukubaliwa au kukataliwa kwa majina yaliyopendekezwa na mamlaka za uteuzi.

(5) Endapo Kamati ya Uongozi ya Bunge itayapitisha majina ya watu waliopendekezwa, Katibu wa Bunge atapeleka orodha hiyo kwa Spika, naye Spika atawateua wahusika kuwa wajumbe wa Jopo la Kuajiri Tume.

(6) Kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao, wajumbe wa Jopo la Kuajiri Tume watakula kiapo cha uaminifu kwa mujibu wa sheria.

(7) Mara tu baada ya kuteuliwa na Rais, wajumbe wa Jopo la Kuajiri Tume watakaa na kuchagua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Katibu kutoka miongoni mwao, na kisha kuwajulisha wadau wote na umma baki, lakini watazingatia sharti kwamba, endapo mwenyekiti anatoka Tanzania Bara, basi makamu mwenyekiti atoke Tanzania Zanzibar.

(8) Endapo Kamati ya Uongozi ya Bunge itakaa majina yote mawili yaliyopendekezwa na mamlaka ya uteuzi, Katibu wa Bunge ataiomba mamlaka ya uteuzi husika kuwasilisha majina tofauti na mchakato wa kuwachunguza utaanza upya.

(9) Kwa ajili ya utekelezaji bora wa kazi zake, Jopo la Kuajiri Tume litajiundia kanuni za kuwaongoza katika utendaji kazi.

(10) Ofisi ya Katibu wa Bunge itabeba jukumu la kuwapatia wajumbe wa Jopo la Kuajiri Tume eneo la kufanyia kazi.

(11) Ndani ya siku saba baada ya kiapo, Jopo la Kuajiri Tume, litatangazi nafasi za ajira kutoka kwa watu wenye sifa na kasha kichapisha majina ya watu wote wataoomba nafasi hizo kwenye magazeti mawili yanayofika nchi nzima na kwenye tovuti ya Bunge.

(11) Jopo la Kuajiri Tume litayafanyia kazi maombi yote, kuchukua watu wenye sifa zilizo bora zaidi, kuwafanyia usaili, ambapo usaili huo utafanyika kwa namna ambayo inaruhusu umma kufuatilia kinachofanyika mbashara.

(12) Baada ya usaili, Jopo la Kuajiri Tume litawachagua watu watano wenye sifa za kujaza nafasi ya mwenyekiti, na watu wengine 25 wenye sifa za kuwa wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi, na kisha majina haya yatapelekwa kwa Katibu wa Bunge kwa ajili ya kujadiliwa, kuthibitishwa na kuteuliwa.

(13) Ndani ya siku saba baada ya kuanza kwa kikao cha karibu cha Bunge kitakachokutana baada ya majina husika kukabidhiwa Bungeni, au mapema zaidi kadiri hali itakavyoruhusu, Bunge litajadili kwa uwazi majina yote yaliyowasilishwa kwake, kufanya uamuzi, na hatimaye kupendekeza kwa Rais jina moja la mwenyekiti, jina jingine la makamu mwenyekiti, na majina nane ya wajumbe wa Tume.

(14) Baada ya Bunge kufanya mapendekezo yake, Katibu wa Bunge, ndani ya siku saba baada ya ridhaa ya Bunge, atayawasilisha majina hayo kwa Spika kwa ajili ya uteuzi wa mwisho.

(15) Ndani ya siku saba, Spika atachapisha majina husika kwenye tovuti ya Bunge na magazeti mawili yanyofika nchi nzima, akimtaja mwenyekiti, makamu mwenyekiti na katibu wa Tume Huru ya Uchaguzi kama walivyopendekezwa na Bunge.

(16) Baada ya Spika kuchapicha majina ya viongozi wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi gazetini na kwenye tovuri ya Bunge, viongozi wapya wa Tume wataanzisha mchakato kama waliopitia wao kwa ajili ya kuajiri wafanyakazi wake katika ngazi ya wilaya, ambapo wafanyakazi hao watapaswa kuchujwa na kuthibitishwa na Kamati ya Uongozi ya Bunge kabla ya kuanza kufanya kazi kama wasimamizi wa uchaguzi, waandikishaji wa kura na kazi nyingine husika kwenye ngazi ya wilaya.

(17) Bunge litakuwa na mamlaka ya kukubali au kukataa ama jina lolote au majina yote yatakayopendekezwa na Jopo la Kuajiri Tume. Pale Bunge linapokataa jina lolote lililoletwa mbele yake, haraka sana iwezekanavyo, Spika wa Bunge atalazimika kulijulisha Jopo la Kuajiri Tume. Ndani ya siku saba, Jopo la Kuajiri Tume litapaswa kuwasilisha Bungeni orodha mpya kutoka kwenye majina ya watu waliofanyiwa usaili hapo awali. Halafu mchakato wa kuwachuja wahusika utaanza upya.

(18) Uhai wa Jopo la Kuajiri Tume utakoma mara tu baada ya spika kuchapisha gazetini majina ya viongozi wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi.

Kufanya mabadiliko katika ibara ya 77

10. Ibara ya 77 ya Katiba inafanyiwa mabadiliko kwa kufuta maneno yote yaliyo katika ibara ndogo ya (2) na badala yake kuweka maneno yafuatayo:

“Isipokuwa pale ambapo Tume ya Uchaguzi, kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au Sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo, itaagiza vinginevyo, kutachaguliwa Mbunge mmoja tu katika jimbo la uchaguzi, ambaye kwa mujibu wa Katiba hii atamteua mgombea mwenza aliye na jinsi tofauti nay a kwake ili washirikiane kufanya kampeni za uchaguzi.”

Kufanya mabadiliko katika ibara ya 78

11. Ibara ya 78 ya Katiba inafanyiwa mabadiliko kwa kufutwa kabisa baada ya kupoteza maana kufuatia utaratibu wa wabunge wa viti maalum wanawake kufutwa kwa njia ya mabadiliko yaliyopendekezwa chini ya ibara ya 66(b) hapo juu.

Imepitishwa na Bunge tarehe …………………. 2020

………………………………………………………….

KATIBU WA BUNGE


Note: Kwa maelezo marefu angalia viambatanisho hapa chini
 

Carlos The Jackal

JF-Expert Member
Feb 6, 2017
16,769
2,000
Asante kwa Bandiko lako Mkuu , naendelea kusoma kwa utulivu mkubwa


Ukiiacha siasa ,umepunguza uwezo wa kufikiria.


KATIBA ndio Maisha ya Mtanzania.
 

Marunde

JF-Expert Member
Jun 9, 2008
532
1,000
Mkuu kubadilisha katiba lazima wananchi wahusishwe kwa kupigia kura hayo msbadiliko, hicho ulichokiandika ni kama wanataka kubadilisha sheria hapo binge litafanya tu
 

nivoj.sued

JF-Expert Member
Jul 14, 2009
220
250
Mkuu kubadilisha katiba lazima wananchi wahusishwe kwa kupigia kura hayo msbadiliko, hicho ulichokiandika ni kama wanataka kubadilisha sheria hapo binge litafanya tu

Nimekuelewa. Lakini mapendekezo yote haya yametokana na maoni ya wananchi kupitia tume za Nyalali, Kisanga na Warioba.

Wananchi wamekwishapata fursa ya kusema wanachotaka. Mawazo yao yaliminywa tu. Yamefufuliwa. If so kuna haja ya consultation juu ya haya?
 

PTER

JF-Expert Member
Dec 28, 2014
13,801
2,000
Jambo jema kuna baadhi ya ibara kuna mkanganyiko wa lugha.

Hivyo utakapo Hariri nakala ya mwisho jaribu kuifanya iwe error free and unambiguous.

Otherwise umejitahidi sana kugusa kila sehemu.

Sent using Jamii Forums mobile app
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom