Rangi za bendera ni ujumbe, uzalendo au urembo?

John Mnyika

JF-Expert Member
Jun 16, 2006
712
1,240
Rangi za bendera ni ujumbe, uzalendo au urembo?

Nilizikuta enzi za kuimba nyimbo za kizalendo zikiwa ukingoni, wakati huo nikiwa kinda. Bendera ya taifa ikipandishwa, tulisimama wima! Hata nzi akikugusa, hakuna kutikisika. Bendera ikipanda, kichwani ulisikika mwangwi wa mirindimo ya nyimbo za kusifia bendera yetu ya taifa. Nyimbo inayotaja idadi na rangi za bendera yetu. Ama kwa hakika ilikuwa njia nzuri ya kukariri na kuamini. Rangi ya kijani, ikiwasilisha misitu yetu. Rangi ya manjano ikibeba madini na rasilimali zingine. Bluu ikiwasilisha bahari, mawaziwa na maji. Huku nyeusi, ikisadifu uafrika na rangi yetu. Naam, hiyo ndio bendera ya taifa la Tanzania.

Naandika makala haya, nikiitazama picha ya mtoto wa kitanzania! Ambayo kwa upekee wake nimeiweka katika kumbukumbu zangu. Picha hii imepigwa Mwanza, wakati wa mechi ya kandanda kati ya Taifa Stars na Simba wa Teranga-Senegali!. Picha zinazoshabihiana na hii ndio zilikuwa picha za wiki, mara baada ya mechi hiyo. Pengine ni hamasa kama hii ndiyo iliwasukuma vijana kufanya kile ambacho wengine tulijua hakiwezekani "Kuifunga Burkina Faso nyumbani kwao!". Naam; tuliwalamba bao moja kwa nunge. Naikumbuka tena Picha ya Mtoto iliyotoka baada ya mechi na Senegali, akiwa amepambwa au amejipamba kwa rangi za bendera ya Taifa letu, huku ameshikilia bendera ya Taifa letu, kifuani ameandikwa herufi "JK".

Naitazama picha hii nikiwa na hisia mbili zinazokinzana! Mosi, hisia ya furaha, kwamba uzalendo umeanza kurejea katika taifa letu. Hizi ni kelele ambazo tumeguwa tukizipiga sana; kwamba bila uzalendo, hakuna utaifa, bila utaifa hakuna kutanguliza mbele maslahi ya taifa; bila kutanguliza mbele maslahi ya taifa; maendeleo ya nchi yanawekwa rehani! Ishara mojawapo ya uzalendo ni matumizi ya alama za kitaifa. Suala ambalo huko nyuma limekuwa likiminywa.

Nakumbuka jinsi ambavyo serikali iliijua juu CHADEMA kwa kutumia rangi za bendera ya Taifa katika mabango yake. Baadaye, Disemba 30 mwaka huohuo 2005 baada ya uchaguzi, Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya kuzindua bunge, akakubaliana na sera hii ya uzalendo pamoja na kwamba haikuwepo katika ilani ya CCM-na kutangaza rasmi kwamba ni ruksa kwa raia kuvaa rangi za bendera ya taifa, ni muhimu kwa wananchi kuwa wazalendo. Binafsi nilipiga makofi katika hili. Upinzani ni visima vya fikra mbadala; zinapokubalika na serikali; maslahi ni ya wote bila kujali itikadi- hata katika hili la matumizi ya rangi na taswira za bendera katika maisha ya kila siku ya wananchi. Naam, nilipoona mtoto huyu alivyojipamba, niliona kabisa ameitika mwito!

Pili; hisia ya huzuni- kwa kuona herufi "JK" kifuani pake. Si kwamba sizipendi herufi "JK", na wala sijui kama ni kifupi cha jina la mtoto yule ama ni kifupi cha jina la Rais wetu Jakaya Kikwete kama ilivyozoeleka. Lakini jambo moja lilinipa huzuni, nalo ni "kufikisha ujumbe tofauti, katika mazingira tofauti". Katika mazingira yale, nilitaraji lengo la uzalendo wetu ni taifa letu.

Nilitaraji, hamasa ya msingi wapewe vijana wetu wa taifa stars. Ningefurahi zaidi kama herufi zile zingekuwa "TZ", yaani Tanzania au "JMT" yaani Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Ama zingekuwa "TS" kifupi cha Taifa Stars. Hapo ujumbe wa uzalendo ungefika vizuri zaidi.! Utaifa ungewekwa mbele zaidi. Naamini watanzania walijumuika pale Kirumba kushangilia taifa lao, na si kumshangilia "JK"! Sina umalaika wa kujua nia ya herufi zile; lakini najua katika maisha-wapo ambao hubeba mabango ya sifa; kwa lengo la kupata fadhila. Natumaini mtoto yule malaika wa Mungu hayupo katika kundi hilo. Walau akikua ataitazama picha ile na kukumbuka uzalendo uliotukuka!

Picha hii imenifanya nitafakari. Nikumbuke bendera mbalimbali. Na kuanza kujiuliza; je, zinabeba ujumbe, uzalendo ama ni urembo tu? Naitafakari bendera ya chama kinachotawala hivi sasa Tanzania- CCM. Rangi zake, alama yake!. Bendera hii ina rangi mbili; Kijani na Njano. Kijani ambayo wengi ya wanachama wake hupenda kuivaa. Nafakari, hivi inawakilisha kitu gani-Je, ni misitu katika nchi ambayo imeanza kugeuka jangwa kutokana na uharibifu wa mazingira? Je, ni misitu katika nchi ambayo wazawa wawindaji wanaendelea 'kuswagwa' toka misitu hiyo kupisha 'wawindaji wawekezaji'; je ni misitu katika nchi ambayo mkazi wa pembeni ya mbuga ya wanyama hajui mapato yanayotokana na idadi lukuki ya wageni wanaokuja kutembelea mbuga za wanyama yanakwenda wapi?

Watalii hawa wengi wao fedha za malipo yao hubaki nchini mwao kutokana na utaratibu wa kulipa huko huko(package tourism)! Je, inawasilisha kilimo katika nchi ambayo serikali ya awamu ya tatu chini ya chama hicho imekiri kwamba haikutoa kipaumbele katika kilimo huku serikali ya awamu ya nne ikiwa imetenga asilimia sita tu ya bajeti katika kilimo kwa mujibu wa makidirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2007/08 iliyowasilishwa bungeni? Kwa miaka 30 toka chama hiki kianzishwe, wakulima sehemu kubwa ya nchi yetu hawajaona matunda ya rangi hii ya kijani. Labda, ipo siku; ile alama ya jembe, itageuka kuwa zana ya ukombozi kwao katika karne hii ya sayansi na teknolojia!.

Halafu kuna rangi ya njano, rangi ambayo Timu ya Simba, hupenda kuwatania watani zao Yanga kwamba ni 'Yebo Yebo', nayo inawakilisha nini? Je, ni zile rasilimali na madini ambayo huchimbwa na makampuni makubwa ya kigeni na watanzania kuambulia mrahaba wa asilimia tatu huku tukiachwa na mashimo? Wapo wapi wale wafanyakazi bora watumie zana ile ya nyundo; kuvunja miamba ya unyonyaji- na kuhakikisha watanzania wananufaika na yale ambayo mwenyezi Mungu amelijalia Taifa hili tajiri wa rasilimali?Je, tuna umaskini wa uongozi na fikra mbadala? Ndio maana, niamua kufungua huu mjadala-Rangi za bendera ni ujumbe, uzalendo ama urembo?

Naendelea kutafakari; nakikumbuka Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) na bendera yake. Mara baada ya uchaguzi, CHADEMA ilituma timu katika wilaya teule, kukusanya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba na kanuni za chama hicho. Moja ya mambo yaliyoguswa katika mabadiliko hayo ni pamoja na bendera yake. Hatimaye katiba na kanuni mpya zikapitishwa na Mkutano Mkuu wake uliofanyika mwaka 2006, na Bendera Mpya ya CHADEMA ikazinduliwa ikiwa ni ishara ya Tumaini Jipya! Nikiitafakari bendera hii nayo.

Bendera ya CHADEMA ina nembo ya kiganya cha mkono kilichonyoosha vidole viwili katika mfumo wa V kama ishara ya USHINDI. CHADEMA ni chama kinacholenga kushinda kidemokrasia na hatimaye kuleta ushindi wa maendeleo ya taifa. Bendera ya CHADEMA ina rangi nne: Nyeusi, Bluu bahari (light blue), nyeupe na nyekundu.

Rangi:

NYEUSI inawakilisha WATU WA TANZANIA. Hii ni rangi ya wazawa asili wa nchi yetu. Ni rangi ambayo inabeba pia falsafa ya NGUVU YA UMMA. Rangi ya BLUU BAHARI (LIGHT BLUE) ni rangi ya asili ya CHADEMA. Ni rangi ambayo inawasilisha HAKI. Rangi nyeupe inawasilisha UWAZI na UKWELI. Huu ni msingi muhimu wa CHADEMA. CHADEMA ni chama ambacho kitasimamia uwazi, ukweli na uadilifu kwa njia ya demokrasia.Rangi ya BLUU ISIYOKOZA iko juu ya rangi NYEKUNDU kama ishara kwamba kama taifa tumevushwa na mashujaa kuelekea katika jamii yenye haki, na hivyo CHADEMA ni chama cha siasa kinasimamia haki.

Rangi nyekundu inawakilisha MASHUJAA. CHADEMA inathamini historia ya nchi yetu ikiwemo damu ambayo imewahi kumwaga katika kutetea haki wakati wa vita dhidi ya mkoloni na matukio mengine ambayo ni chimbuko la uzalendo na nia yetu ya kuendeleza amani katika nchi yetu.

Mintaarafu bendera ya Tanzania imepatikana kutokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilihali visiwani kuna historia ya damu kumwagika ama kumwagwa wakati wa mapinduzi? Kama kweli tuna serikali ya mapinduzi Zanzibar na utawala wa Chama cha Mapinduzi(CCM), je ni mapinduzi yasiyo na ‘rangi nyekundu'?.

Rangi nyekundu ni hidaya kwao waliomwaga damu wakati mapambano kadhaa na Mreno na Mwarabu. Tuzo kwao waliopigana na Ujerumani wakati wa utawala na mliomwaga damu katika vita vya dunia. Heko kwao ambao damu walisafisha safari ya kumng'oa Nduli Amin. Heri yake Sethi Benjamini na wote waliopotesha maisha katika hekaheka za kueneza Azimio la Arusha. Kumbukumbu kwao waliotoa damu katika mikikimikiki ya mfumo wa vyama vingi kutoka Zanzibar mpaka bara. Damu yao iliyomwagika haizoleki, ukiwa waliouacha hauzoeleki lakini fikra walizosimamia hazizeeki. Mapambano bado yanaendelea!

Kwake Bushiri bin Salim wa Tanga, suriama wa kiarabu na kiafrika, pamoja na nia yake tenge ya kulinda maslahi katika biashara ya utumwa ulimwaga damu kwa kunyogwa Pangani baada ya kuongoza maasi makali dhidi ya kuingia kwa ukoloni wa Kijeruamani-damu yake ilimwagika pamoja na damu za wapiganaji wa Pwani, Morogoro mpaka uhehe. Kwake Mtemi Meli, uliyewashinda wadachi mpaka mwenzake Sina alipomsaliti hatimaye yeye na mashujaa wenzake wakamwaga damu kaskazini wakilinda uhuru.

Tunamkumbuka Chifu Mkwawa, aliovyowaunganisha wahehe-toka Kalenga, Tosamaganga mpaka ulipoamua kuimwaga damu yake mwenyewe kuliko uhuru upotee mikononi mwake. Mtemi Isiki wa Tabora uliendesha mashambulizi ya kishujaa, hatimaye akaamua kumwaga damu yake na ya familia yake kwa kujilipua na baruti ili tu asipate aibu ya uhuru kuchukuliwa mbele ya macho yake. Tunamkumbuka Mtemi Makongoro wa Musoma, alipambana kwa ushujaa mpaka ilibidi kikosi cha wanamaji kiletwe kupitia miji ya Mombasa na Kisumu kummaliza.

Tunamkumbuka Kinjeketile kwa kuongoza vita vya kutisha vya Maji Maji kwa miaka kadhaa vilivyoanzia vilima vya Matumbi karibu na Kilwa. Wao walitaka kumwondoa mkoloni kwa nguvu na walikuwa tayari kumwaga damu kuliko kuendelea kuishi bila ya uhuru. Mapambano yao yalisambaa maeneo mengi ya ardhi yetu. Hawa walikuwa mashujaa kweli kweli waliojua umuhimu wa imani na falsafa katika mapambano-wakawapa watu ujasiri kwa dawa ya "Kugeuza risasi, Kuwa maji". Pamoja na kushindwa vita na wazalendo zaidi ya laki moja kupoteza maisha katika wakati ambao ardhi ilikuwa na watu wachache yapo mapigano ambayo walishinda. Pamoja na machifu 47 wa Kingoni kunyongwa damu yao ilileta mabadiliko katika utawala. Kwa vyovyote vile damu nyingi kiasi hiki iliyomwagika kwa sababu ya kudai uhuru haiwezi kupuuzwa. Hivyo rangi nyekundu ni kumbukumbu yao.

Karibu kila eneo katika nchi yetu yupo shujaa ambaye anaweza kukumbukwa laiti kama historia zenu zingejulikana kizazi hata kizazi na kuwa chimbuko la kujiamini, kujithamini na uzalendo miongoni mwa Watanzania. Kushindwa kwao na hatimaye ukoloni kuingia ama kuendelea hakuondoi historia kuwa mlimwaga damu kwa ajili ya kulinda uhuru wa ardhi hii tukiyoirithi! Rangi nyekundu ni ishara kwamba; sio siri, kwa sera bila silaha, mapambano bado yanaendelea mpaka mabadiliko ya kweli yatakapopatikana!

Rangi nyeupe iko mbele ya rangi zote kama ishara kwamba chama kinatanguliza UWAZI na UKWELI katika nyanja zote. Pia rangi nyeupe imebeba nembo ya chama kwa kuwa usafi ni msingi muhimu sana kwa chama. Nembo ya chama iko mbele kama kama ishara ya CHADEMA kuwa chama kiongozi katika kuchochea misingi muhimu katika kuleta mabadiliko na maendeleo katika Taifa. Nafungua mjadala; rangi za bendera ni ujumbe, uzalendo au urembo?
 
Kabla hatujavamiwa na wajerumani, nchi yetu (Bara na Visiwa vya Zanzibar) ilitawaliwa na Sultan wa Zanzibar chini ya Sultan wa Oman. Bendera ya Sultani wa Zanzibar ilikuwa hii hapa chini.
om-old.gif

Baada ya mikataba ya Carl Peters and Berlin conference, nchi yetu yote iliwekwa chini ya utawala wa Mjerumani. Mjerumani hakuwa na interest katika visiwa vya Zanzibar, hivyo akaingia deal na Uingereza. Walitaka Uingereza iwape visiwa vya Heligoland vilivyoko North Sea, wao watoe visiwa vya Zanzibar kwa Uingereza. Hivyo Zanzibar ikwa chini ya mweingereza, ambaye aliamua kumwacha sultan aendelee kuula. Bara ikaitwa Deutsch-Ostafrika (German East Africa). Bendera ya mjerumani hapa bara ilikuwa hii.
deutsch-ostafrika-fahne.jpg
Kwa Zanzibar kulikuwa na bendera mbili. Ya kwanza ilikuwa ya mwingereza; ilikuwa na sura hii hapa:
tz-zzrs.gif
Bendera ya pili huko Zanzibar ilikuwa ya Sultan ambaye alikuwa hana uhusiano na Sultani wa Oman tena kwa vile alikuwa chini ya waingereza. Bendara yake ilibadilishwa na kuwa ifuatavyo:
800px-flag_of_the_sultanate_of_zanzibar_svg.jpg
Baada ya ujerumani kupoteza makoloni yake kufuatia kushindwa vita ya dunia ya kwanza, sehemu ya bara iliwekwa chini ya mwingereza. Huyu ndiye aliita sehemu ya bara kuwa "Tanganyika" akimaanisha ili nyika iliyo nyuma ya Tanga. Bendera ya Tanga ilikuwa hii:
tz-tang.gif
Katika kipindi cha utawala mwingereza, tulitumia bendera za aina kama tatu hivi lama ifuatavyo:

br-tanganyika.jpg


tztgclb.gif


tztgr.gif
Gavana wa kiingereza yeye alikuwa akitumia bendera tofauti kama invyoonyeshwa hapa chini

governors-flag.gif
Kunako May 1961 tulipata madaraka ya ndani chini ya Nyerere. Katika kipindi hicho tukawa tunatumia bendera ya kiingereza zilizoonyeshwa hapo juu na bendera ya madaraka ilikuwa kama ifuatavyo
tztng61.gif

hata hivyo inaaminika kuwa Nyerere alipendelea zaidi ile bendera ya TANU
tztanu.gif
Ilivyofika December 1961 tukapa uhuru na hivyo bendera ya mwingereza ikashushwa. Tukapandisha bendera ya kwanza ya Tanganyika iliyokuwa kama ifuatavyo:
independent-tanganyika.jpg
hata hivyo baada ya uhuru, tuliendelea kubaki chini ya malkia aliyekuwa anawakilishwa na Governor General, Sir Richard Turnbull; bendera ya Governor General ilikuwa kama ifuatavyo:

governor_general.gif

Ilipofika December 1962 tukawa jamhuri na hivyo kuondokana kabisa na alama za kiingereza ispokuwa pesa (Siku nyingine nitatoa historia ya pesa zetu). Kwa bahati mbaya sikuweza kupata bendera ya rais mara baada ya kuwa Jamhuri


Kwa upande wa Zanzibar, waliendelea kuwa chini ya mwingereza na sultani hadi december mwaka 1963 ambao mwingereza aliamua kutoa uhuru kwa zanzibar chini ya Sultan. Bendera ya Zanzibar huru ( Sultanate of zanzibar) ilikuwa sura nyekunu na karafuu mbili. Sura halisi ya karafuu haijulikani sawasawa. Ila bendera hiyo ilionekana kama mojawapo ya hizi mbili:

tz-zan63.gif


tz-zz63.gif

hata hivyo serikali hii haikudumu zaidi ya siku 33, ikapinduliwa kwa nguvu na chama cha ASP. Baada ya mapinduzi, iliundwa serikali ya Jamhuri ya Zanzibar. Mwanzoni, bendera ya Jamhuri ya Zanzibar ilikuwa hii hapa chini
tz-za64a.gif
lakini baada ya muda mfupi ikabadilishwa na kuwa kama ifuatavyo huku ikiwa na rangi za bendera ya ASP
tz-za64b.gif
Katika kipindi kifupi sana wakati wa machafuko ya mapinduzi yale, Pemba ilijitangaza kuwa ni nchi huru ya jamhuri ya pemba, lakini nadhani walidhibitiwa haraka sana na majeshi ya ASP. bendera ya Jamhuri ya Pemba ilikuwa kama ifuatavyo:
tz_pemba.gif

Katika kipindi cha miezi mitatu baada ya mapinduzi, visiwa vya Zanzibar viliunganika tena na bara baada ya kutenganishwa kwa miaka ipatayo 80. Muungano huo ulijulikana kama jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuanzaia wakati huo, bendera ya Tanzania ni kama ifuatavyo:
tz.gif
Ile ya rais wa jamhuri ya muungano iko kama ifuatavyo:
tz_pre.gif

Mwaka 2005, Zanzibar waliamua kuwa na bendera yao. bendera hiyo ni mchanganyiko wa bendera ya mwisho ya jamhuri ya zanzibar na ile ya jamhuriu ya muungano wa Tanzania. Inaonekana kama ilivyoonyeshwa hapa chini.
tz-za05.gif
Rais wa Zanzibar naye akatengenezewa bendera yake ambayo inaonekana kama ifuatavyo hapa chini
tz-zapr.gif
Kama nimekosea sehemu yoyote katika mapitio yangu ya historia ya bendera nchini Tanzania, naomba marekebisho. Safari nyingine nitapitia historia ya fedha zetu; najua itakuwa ndefu sana lakini nitaigawa katika sehemu sita Kipingi cha Mjerumani, Kipindi cha mweingereza, Kipindi cha Nyerere, Kipindi cha Mwinyi na baada ya Mwinyi.
 
Asante sana Kichuguu,

Kumbe uhasama kati ya Pemba na Unguja nimeufahamu fika kiini chake. Juzi (Jumanne) wakati wa kipindi cha "Je Tutafika" (Channel Ten) Lipumba aliulizwa hili swali na Makwaia, lakini alionekana kujiuma uma.

Ebu endelea kushusha vitu. Hapa nazidi kujifunza mengi.
 
nataka mawazo yako wewe kuhusu rangi katika bendera ya Tanzania tubadilishe rangi ili iwatambue wote waliopo humu nchini?

BLUE inawakilisha mito, maziwa na bahari
NJANO inawakilisha madini na vito vingine vya thamani
KIJANI mimea na uoto wa asili
NYEUSI inawakilisha raia wa nchi hii, afrika ambao ni weusi.

sasa tujadili;tunasababu ya kuwaambia raia wa nchi hii ambao sio weusi kuwa hawatambuliki kwa misingi ya uraia, kuzingatia bendera yetu?

wale wasio weusi waombe bendera ibadilishwe ili wasibaguliwe na maelezo ya rangi za bendera yetu, hasa NYEUSI?
 
Nani kakwambia nyeusi ni watu weusi?

Hii inawakilisha rangi asilia ya watu wa bara la Africa na sio watu weusi.

Tujadili ufisadi.
 
umesahau hata rangi asili ya watu wa africa kwamba ni nyeusi ama tunaoitwa nyani huko ulaya sio sisi weusi?

ufisadi umeanzia kwa hao unaokataa kuwajadili kwa uasilia wao ama umesahau makampuni tunayoyatuhumu yameanzishwa na hao mafisadi yanajumuisha wasio na asilia ya afrika kutumia hao weusi?

jukwaa la siasa linajumuisha mapambano ya ufisadi wetu pia lakini, katiba isipotamka bayana mahitaji yetu ya kupambana na uonevu huo huoni pia ufisadi utatumika kutupatia hao hao mafisadi? hii ni muhimu kubainisha nani ana uchungu na nchi hii! jenga hoja usikimbie kama huna la kuchangia uwe kimya tunataka kila kitu kitamkwe bayana katika katiba sio ujanja, tafsiri za vitu kama rangi za bendera ni vitu muhimu kwa mustakabali wa taifa letu, kuna bara la ASIA, AFRICA, ULAYA,AMERIKA KUSINI na KASKAZINI walikosea kusema rangi asilia ya Afrika? ndio nataka uchangie, kubadili ama kukubali tupate tafsiri mpya, naomba usipindishe hoja yangu!hoja kwa hoja sio kubadilisha.
 
Hivi kweli kuna mtu mweusi au mweupe, au pink au Dark ? Nakumbuka kuna speech ya Mandela ya Black man in whites court" alimwambia hakimu you are not white to me you look more pink than white.

Any way unajua visiwa vya papua new guinea, vanuatu, india, Sirilanka,Palau, Australi etc kuna watu wana randi kama zetu?

Nadhani rani nyeusi inaonyesha rasilimali watu na kwa ubaguzi kama unavyoweka hapa.
 
nataka mawazo yako wewe kuhusu rangi katika bendera ya Tanzania tubadilishe rangi ili iwatambue wote waliopo humu nchini?

BLUE inawakilisha mito, maziwa na bahari
NJANO inawakilisha madini na vito vingine vya thamani
KIJANI mimea na uoto wa asili
NYEUSI inawakilisha raia wa nchi hii, afrika ambao ni weusi.

sasa tujadili;tunasababu ya kuwaambia raia wa nchi hii ambao sio weusi kuwa hawatambuliki kwa misingi ya uraia, kuzingatia bendera yetu?

wale wasio weusi waombe bendera ibadilishwe ili wasibaguliwe na maelezo ya rangi za bendera yetu, hasa NYEUSI?
Kwanza bendera ya taifa haina rangi ya njano, pole mwalimu wako wa shule ya msingi alikudanganya!

Ukweli replace rangi ya njano kwa rangi ya dhahabu... tulijua tuna dhahabu na madini mengine tangu miaka hiyo; kamata ukweli huu hapa

au kula kilaini hapa

The National FlagRatio length to breadth: Three to two, e.g. 3ft. x 2ft., 6ft. x 4ft. 12ft. x 8ft.
Description: Green - Golden - Black and Blue, having the black center stripe centred on diagonal rising from flag-mast to top edge of the fly, two smaller golden stripes dividing the upper triangle portion which is green and the lower triangle portion which is blue.
Proportions of colours: Black center stripe, centred on diagonal of flag of 6ft. x 4ft., is 13/48 of fly and 13" wide. Golden stripes are each 1/16 of fly and 3" wide.
Colour Code and Significance: B.S. No. 2660: 1955

Black: B.S. No. 9-103 - the People

Green: B.S. No. 0-010 - the Land

Blue: B.S. No. 0-012 - the Adjoining Sea

Golden: B.S. No. 0-002 - the Mineral wealth

Uwiano wa Urefu
Kwa Upana:-

Maelezo:
Tatu kwa mbili, mfano ft.3 x ft.2, ft.6 x ft.4, ft.12 x ft.8
Ina rangi za Kijani, Dhahabu, Nyeusi na Bluu ambapo rangi nyeusi imepita katikati ya bendera kuanzia pembe ya chini kwenye mlingoti na kuishia pembe ya juu kulia. Rangi hii huigawa bendera katika sehemu mbili zenye umbo la pembe tatu. Rangi nyeusi imetenganishwa na pember tatu ya juu yenye rangi ya kijani na pembe tatu ya chini yenye rangi ya bluu kwa mistari miwili midogo yenye rangi ya dhahabu.

Viwango vya rangi na maana zake.
Nyeusi - Kiwango na. 9-103 - Watu

Kijani - Kiwango na. 0-010 - Ardhi

Bluu - Kiwango na. 0-012 - Bahari + Maziwa

Dhahabu - Kiwango na. 0-002 - Madini
Uwiano wa Rangi:
Rangi nyeusi kwa bender ya

Ft.6 x ft.4 ni 13/48 kwenda juu na

Ft.13 upana. Mistari ya dhahabu ni 1/16 kwenda juu na 3" upana kila mmoja.
 
mzee uko deep nimekukubali kwa kukariri hadi dimensions za bendera kwa hili hongera sana.

nimeongeza ujuzi tena kuwa rangi ya dhahabu inajulikana hata kwa bibi yangu huko kijijini hivi ni wanafunzi wangapi wanajua rangi ya dhahabu? walimu wao wanafundishaje wakati hata dhahabu hawajaiona? au tuseme mwanao, mdogo wako ama mtu wa uhusiano wowote na wewe aliye mdogo wa kiwango cha shule ya msingi anayejifunza kwa kutumia lugha ya kiswahili anajua hiyo rangi ya dhahabu? mbona inaitwa manjano? sasa tuongeleee hii rangi nyeusi inayoitwa "watu" nidokezee mwalimu Nyerere alisemaje kuhusu nafasi ya hao watu na rangi nyeusi, kuna uhusiano upi?

ukijibu hilo nitakukubali sana!
 
Unajua nimejitahidi siku nyingi kuchambua maana ya hiyo rangi nyeusi katika bendera yetu, kumbe hakuna mweusi wala mweupe hivi hii niliyoambiwa rangi asilia ya afrika ikatajwa na mtu mmoja akasema ina maana ya watu.

Huko ulikotoa mifano nilitumia kama references zangu kujenga hoja nikajikuta nikijifariji kuwa ni wahamiaji ama watu waliopelekwa huko na biashara ya utumwa ama na sababu mbalimbali, kwahiyo ukiwatumia unaniongezea utata nilionao tayari kuhusu maana ya rangi hii kumbe sio hata afrika pekee yake. Ndio maana nikasema tubadili kama kuna tofauti ya vitu vilivyotajwa huko kabla katika tafsiri ya rangi katika bendera yetu.

kutoa mifano na misemo aliyotumia mandela yaweza isiyo njia sahihi bali kujifariji kuwa kuna vitu vilisemwa na sasa tunajikomboa kisaikolojia, hebu tutengeneze yetu iliyo na tafsiri ya Tanzania sio ya waheshimiwa hao, nina kasumba moja mbaya kwamba sio kila quote naiamini kabala ya kuifanyia kazi! huu unaweza kuwa mjadala wa kitaifa ili tusijiofariji wakati hatujui ukweli.

Naweza nikawa sijui mimi leo lakini majibu nitakayopewa yakaleta changamoto mpya na majibu yaliyojificha!
 
kilitime said:
Ukweli replace rangi ya njano kwa rangi ya dhahabu... tulijua tuna dhahabu na madini mengine tangu miaka hiyo;

Hivi kwenye kiswahili fasaha tuna rangi inaitwa rangi ya dhahabu?
 
naona watanzania tumechoka kweli tunaambiwa kuwa rangi ya bendera njano inaitwa dhahabu?

au kuna upotoshaji wa ukweli hapa?

mimi najua almasi ina rangi nyeupe inayong'aa sasa yenyewe sio madini?

nashangaa hoja za maana waTz tunakuwa shallow kiasi hiki? nategemea mtafanya hili kuwa suala la kitaifa!
 
UMEIONA BENDERA YETU

Kuelekea maadhimisho ya miaka 47 ya Uhuru wa Tanzania Bara na 46 ya Jamhuri nimepata wazo. Ni wakati wa kuiinua bendera yetu juu kama ishara ya umoja wetu na kama ishara ya utaifa wetu. Bendera zimekuwa zikitumika katika historia kuashiria ushindi, kuonesha utambulisho na kutangaza uhuru wa watu. Bendera yetu vivyo hivyo ni ishara ya ushindi wetu, alama ya watu wetu, na zaidi ya yote ishara inayoonekana ya Uhuru wetu! Tunapoinyanyua juu siyo tu tunaona fahari kuwa sisi ni Watanzania bali tunautangazia ulimwengu na maaduzi zetu wote wa ndani na wa nje kuwa na sisi ni huru na tunayo nafasi katika jumuiya ya mataifa ya Ulimwengu!! Uhuru tulionao ni ule wa kuweza kujiamulia mambo yetu wenyewe na kuamua hatima ya maisha yetu wenyewe na siyo uhuru wa “bendera” ambapo tumebakia kupepea bendera wakati wengine ndiyo wanatuamulia kila kitu! Ni uhuru wa kujiamulia hatima yetu wenyewe ndio tunataka ulimwengu utambue na kufahamu na ya kuwa wana na mabinti wa taifa letu wako tayari kujitoa mhanga kulinda uhuru huo!!

Ni kwa sababu hiyo basi natangaza zoezi la kuinyanyua na kuipepea bendera yetu kwa njia ya mtandao kwa kuposti picha ambapo bendera yetu inaonekana au rangi nne za bendera yetu (bluu, nyeusi, kijani na njano) zinaonekana. Yawezekana kuwa ni picha za mahali, watu wakifurahia, jengo, au kwa makusudi ukachukua bendera yetu na kwenda kupiga nayo picha mahali fulani na kuwaonesha Watanzania hiyo “Fahari ya Uhuru wetu”. Picha zote ambazo zitakidhi masharti rahisi yafuatayo zitachapwa kwenye tovuti ya KLH News hadi siku ya uhuru Disemba 9, 2007 na baadaye zitahamishwa na kuwekwa kwenye photo gallery ya tovuti yetu mpya.

a. Mwenye kutuma picha hizo awe na haki nazo au ziwe ziko kwenye public domain.
b. Picha za bendera au rangi za bendera ziwe katika mazingira ya maadili mazuri.
c. Picha ziambatane na maelezo ya ni nani au wapi picha hiyo ilipigwa au maelezo mengine yoyote.
d. Picha itakayovutia watu wengi zaidi itajipatia ujiko wa aina fulani wa kuweza kuoneshwa kwa Watanzania wengi zaidi nyumbani! na kama mambo yatakuwa mazuri tunaweza kutoa zawadi kidogo kwa picha hiyo.
e. Picha hizo lazima ziwe na bendera au rangi za bendera (wachezaji n.k)..
f. Picha zilizo kwenye public domain iliyo ya kwanza ya aina ile ile ndiyo itakayopostiwa.Yeyote mwenye picha waweza kuzituma kupitia:

Bm1280(at)hotmail.com au mwanakijiji(at)jamboforums.com

Mfano:
jamboonormal_uh18.jpg

chipukizi kadondoka... guess what hakidondoki..

stars.jpg

Taifa Stars wakicheza na Brazil wametinga jezi zenye rangi za Taifa

77658444ip5.jpg

Zitto akiingia jijini Dar baada ya sakata la Buzwagi (mkononi ana kitambaa chenye rangi za Taifa)


jamboonormal_forum5.jpg

sijui ilikuwa wapi.. ila unaweza kuziona rangi zetu za Taifa!

jamboonormal_majura.jpg

mwana fani mwenzangu huyo akiwa hana mpinzani..

jamboonormal_uh10.jpg

Umeziona rangi za bendera yetu, kwenye sherehe za miaka 45 ya Uhuru

jamboonormal_bndera2.jpg

mtoto anaangalia maji... au bendera...?

jamboonormal_nyirenda.jpg

Nyirenda ikiipandisha bendera yetu juu ya mlima Kilimanjaro.. usiku wa Uhuru!
 
Hiyo ya mwisho ndio yenyewe ona ile mistari yake ,izo zingine ni za muungano ila wazzanzibar wanasema eti rangi ni zile zile,The real Tanganyika flag.
tz-tng61.gif
 
Sifa, uzito na umuhimu wa bendera ya taifa ni kubwa. Sote tunayatambuwa haya. Nakumbuka baada tu ya uhuru wa Tanganyika aklitokeya mzungu mmoja akasherehekeya uhuru kwa namna yake. Alimvalisha mbwa wake bendera ya taifa. Kagundulika la alikiona cha mtema kuni. Mwishowe alifukuzwa nchi.

Tangu lilipoamka jazba jipya la taifa stars bendera yetu tuipendayo nayo imetumika kivyake. Kwanza mfadhili akaishoneya jezi shati la juu. Hivi karibuni bendera hiyo hiyo ikapepeya juu ya kila mlingoti wa daladala, teksi, basi, lori, baiskeli, pikipiki na kadhalika. Wengine wakaigeuza skarf ya shingoni na hata kilemba cha kichwani. Barabaraa sherehe hiyo.

Nilisikitika na kusononeka nilipomuona dereva wa teksi anaikoshea gari na mama mpita njia kaikaushiya jasho la usoni. Bendera yetu hii hii. LA HAULLAH!!!

Hakika bado tunakwenda. Si mbali tutakapo ona bendera yetu hii tuipendayo na kuiheshimu imeshonwa chupi au sidiriya kama wafanyavyo wamarekani na waingereza. Muhimu kwa sasa ni elimu husika kwa umma. "A stitch in time saves nine." Tuwajibike wakati ni huu.

Mh. spika naomba iungwe mkono hoja.
 
uzalendo Wa Namna Hii Ni Nje Ya Scope, Lazima Elimu Itolewe Kuhusu Heshima Kwa Bendera Yetu. Nashangaa Sisi Ni Wepesi Sana Kujifunza Mambo Yasiyo Ya Msingi Toka Nje. Mfano Sasa Hivi Tumeanzisha Madanguro, Kutembea Nusu Uchi Nk. Lakini Ukienda Nchi Za Wenzetu Huwezi Kuona Mtu Akijisaidia Ovyo Barabarani, Huwezi Kuona Mtu Akitupa Matakataka Kila Mahali Kama Sisi. Sasa Hili La Bendera Kuanza Kudhihakiwa Tutaenda Na Mtu. Vinginevyo Tunauchafua Utaifa Wetu.
 
ile si bendera, bali ni rangi zilizomo katika bendera yetu.
mtu yoyote atakayeishusha bendera kwenye mlingoti wake akaishonea nguo za ndani, huyo anafaa kuchukuliwa hatua za kisheria. lakini kutumia tu rangi zilizoko ndani ya bendera, sijaona kosa hata kidogo
 
ile si bendera, bali ni rangi zilizomo katika bendera yetu.
mtu yoyote atakayeishusha bendera kwenye mlingoti wake akaishonea nguo za ndani, huyo anafaa kuchukuliwa hatua za kisheria. lakini kutumia tu rangi zilizoko ndani ya bendera, sijaona kosa hata kidogo

Kweli wewe umechanganyikiwa mno. Kwani mke mpaka awe kitandani ndiyo anakuwa mke wako? Akiwa mtaani huko huyo si mkeo. Tuachie bendera zetu we baki na mirangi rangi yako.
Wengine wanapeperusha bendera ya taifa katika magari ya kubeba takataka sijui polisi wako likizo???
 
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom