Randama ya Rasimu ya Katiba Mpya: Hivi ndivyo inavyosema kuhusu Serikali tatu

farryandy

Member
Jun 27, 2012
55
28
SURA YA SITA
MUUNDO WA JAMHURI YA MUUNGANO Ibara ya 60 Muundo wa Muungano
a. Maudhui ya Ibara

Ibara ya Rasimu ya Katiba inaainisha muundo wa Muungano wa Shirikisho la Serikali tatu, ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Pia inaiinisha mihimili mikuu ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahkama ya Jamhuri ya Jamhuri ya Muungano.

Aidha inazungumzia utekelezaji na usimamizi wa shughuli za Jamhuri ya Muungano. Ibara hii pia inatambua kwamba mambo mengine ya kiutendaji yasio ya Muungano yataainishwa katika Katiba za Nchi Washirika.
b. Madhumuni na Lengo

Madhumuni na lengo la Ibara hii ni kutambua mamlaka tatu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo ni Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, Mamlaka yasio ya Muungano ya Tanganyika na mamlaka yasio ya Muungano ya Zanzibar.
Aidha, kuipa kila mamlaka kuwa na Serikali yake kusimamia maeneo yake yaliotajwa katika Katiba hii ikiwa ni pamoja na vyombo vyake vya utekelezaji na kwa hivyo kutenganisha mamlaka hizo au kuziweka bayana.
Hali kadhalika madhumuni na lengo ya Ibara hii kuweka masharti ya Kikatiba ya kutambua kuendelea kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano. Vilevile lengo jengine ni kuimarisha na kudumisha Muungano wa hiari wa pande mbili zinazohusika.
Lengo jingine ni kutunza utambulisho wa kihistoria na kiutamaduni wa nchi Washirika wa Muungano zilizoamua kuungana kwa hiari. Hiyo itaondoa hofu ya Zanzibar kumezwa na Tanganyika lakini pia, itahifadhi utambulisho wa Tanganyika na kuondoa taswira kwamba ndiyo imevaa hadhi ya Serikali ya Muungano.

c. Sababu ya Mapendekezo
Sababau ya mapendekezo haya ni kutambua kuwa, kwa kawaida panapokuwa na muungano wa hiari wa nchi mbili huru na yakaainishwa mamlaka ya mambo ya muungano na mamlaka ya mambo yasio ya muungano, na yakatenganishwa mamlaka ya Mambo ya Muungano na mamlaka mambo yasiyo ya Muungano, muundo huo unapaswa kuwa ni muundo wa shirikisho la Serikali Tatu.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 katika Ibara za 4, 34, 64 na 102 inatambua mamlaka tatu ndani ya Jamhuri ya Muungano. Kwa upande wa Katiba ya Zanzibar, 1984 katika ibara za 5A na 99 inatambua mamlaka tatu ndani ya Jamhuri ya Muungano. Mamlaka hizo tatu ni mamlaka ya Mambo ya Muungano, mamlaka ya mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika na mamlaka ya mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar.

, kuwepo kwa mamlaka hizo kumefafanuliwa na Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha "Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania" katika ukurasa wa 15, kwamba:
"Nchimbili zinapoungana na kuwa Nchi Moja mifumo ya kawaida mifumo ya miundo ya Katiba ni miwili: Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake, na Nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja. Katika mfumo wa pili kila nchi itajivua madaraka Fulani ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho, na itakuwa na serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliobaki. Mambo yatakayoshikwa na serikali ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka ya nchi zilizoungana, basi kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi moja, bali zinaendelea kuwa nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani.Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni nchi moja yenye serikali tatu, Serikali ya shirikisho na serikali mbili za zile nchi mbili za awali zilizoungana kuzaa nchi mpya moja."
Pia Mwalimu alifafanua zaidi kuhusu jitihada za kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki alisema:
"Kama jambo hilo lingetokea, nina hakika kabisa kwamba mfumo wa nchi mpya ambayo ingezaliwa ungekuwa ni wa Shirikisho; ama shirikisho la Nchi Tatu zenye serikali nne, au Shirikisho la Nchi Nne lenye Serikali Tano. Kwa kweli hata kesho nchi za Afrika Mashariki zikiamua kuungana na Tanzania ikawa ni mshiriki, naamini kuwa ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania yenye Serikali Mbili- ya Zanzibar na Tanganyika- kuliko Tanzania yenye Serikali Mbili, ya Tanzania na ya Zanzibar."

Hata hivyo, tangu mwaka 1964 hadi mwaka 2014, mamlaka ya Mambo ya Muungano na mambo ya Tanganyika yasiyo ya Muungano yaliwekwa katika Katiba moja na Serikali moja yaani, Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mamlaka ya mambo ya Zanzibar yasiyo ya Muungano yaliwekwa katika Katiba ya Zanzibar na yanasimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Muundo wa Muungano unaelezewa katika Ibara ya 60 ya Rasimu ya Katiba, unazingatia matakwa ya kifungu cha 9(2) (a) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yaliyoielekeza Tume pamoja na mambo mengine kuzingatia kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kudumisha Muungano.
Rasimu imependekeza muundo wa Serikali tatu baada ya kufanyika uchambuzi wa takwimu na kuchanganua sababu zilizotolewa na makundi mbalimbali inapendekeza muundo wa Seikali tatu ili: kuitambua Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, kuendelea kuitambua Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuondoa kero za muda mrefu zinazotokana na muundo uliopo wa Serikali mbili na kuthamini mapendekezo yaliyotolewa na Tume na Kamati mbalimbali zilizoundwa hapo awali kuhusu mfumo wa Serikali.

Muundo huo uliochanganya Mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano ya Tanganyika katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano kimantiki umeshindwa kueleweka kwa wananchi. Aidha muundo huo ndio chimbuko kuu la ubishi, migogoro mivutano (zinazojulikana kama kero) kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kiuhalisia, katika utekelezaji wa Mambo ya Muungano, Serikali zote ama kwa kukubaliana au kujiamulia zenyewe zimebadili taswira ya muundo wa Muungano katika utendaji wake ambao umekiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.
Utata na mkanganyiko unaouzonga Muungano unatokana na kuwepo kwa malalamiko kutoka kila upande wa Muungano. Kwa upande wa Zanzibar baadhi ya malalamiko yao kuhusu utekelezaji wa Mambo ya Muungano ni:

1. Serikali ya Tanganyika imevaa taswira/koti la Serikali ya Muungano ambalo linaisaidia Tanganyika zaidi kuliko Zanzibar. Taswira hiyo imeifanya Tanganyika kuwa ndiyo Tanzania na Watanganyika ndiyo wamekuwa Watanzania; na Wazanzibari wamebaki kuwa Wazanzibari.
2. Mambo ya Muungano yamekuwa yakizidi kuongezeka na hivyo kuathiri uhuru wa Zanzibar (Autonomy) na kufifisha hadhi ya Zanzibar (Identity).
3. Kuvunjwa kwa makubaliano ya Hati ya Muungano kwa kuificha sura ya Tanganyika katika Muundo wa Serikali ya Muungano.
4. Kumuondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
5. Kutokuwepo kwa uwazi wa mapato na matumizi ya fedha za Serikali ya Muungano.
6. Kutokuanzishwa kwa Akaunti ya Fedha ya Pamoja.
7. Kuwepo kwa mkanganyiko wa ugawaji wa mapato na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.
8. Kuwepo kwa chumi mbili tofauti zinazoshindana katika nchi moja.
9. Zanzibar kutoshirikishwa kikamilifu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika masuala ya kupata misaada na mikopo kutoka nje ya nchi.
10. Malalamiko kuwa viongozi wakuu wa Zanzibar wanachaguliwa Dodoma na sio Zanzibar kwenyewe.
11. Zanzibar inalalamika kuwa kuna baadhi ya mambo yamefanywa kuwa ya Muungano kupitia kutungwa kwa sheria na Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa mambo yasio ya Muungano na baada ya hapo mambo hayo kupata hadhi ya Muungano.
Malalamiko haya ya Zanzibar kwa kiwango kikubwa yanatokana na muundo wenyewe wa Muungano. Kuyaweka mambo ya Tanganyika chini ya Serikali ya Muungano, kumesababisha Serikali ya Muungano kujishughulisha zaidi na mambo ya Tanganyika, hasa mambo ya maendeleo.
Kwa mfano, Serikali ya Jamhuri ya Muungano inashughulikia sana mambo ya kilimo, viwanda na biashara, ujenzi, uchukuzi, mawasiliano, nishati na madini, maji, elimu, huduma za afya na maliasili na utalii kwa upande wa Tanzania Bara ambayo siyo Mambo ya Muungano.
Ingawa Bunge ni la Mungano na kinadharia kutarajiwa kushughulikia mambo ya Muungnao kwa kiasi kikubwa lakini linashughulikia mambo yaliotajwa hapo juu ambayo ni ya Tanganyika kwa uzito mkubwa.

Kwa hali hiyo inavyotokea ni kuwa Wabunge kutoka Zanzibar kwenye Bunge la Muungano huwa hawashiriki katika mijadala kwa mambo ya Tanganyika lakini pia huonekana ni kuwapotezea muda Wabunge hao kutoka Zanzibar katika Bunge ambalo linajadili mambo yanayowahusu kwa uchache sana.
Wakati wa kikao cha bajeti mambo yanayohusu Tanganyika ndiyo mambo yanayotengewa siku mbili au tatu za majadiliano; wakati Mambo ya Muungano kama vile: ulinzi, mambo ya ndani na mambo ya nje yanatengewa siku moja au nusu siku. Aidha, hata ziara za Kamati za Bunge la Jamhuri ya Muungano kukagua shughuli za maendeleo zinafanywa Tanzania Bara tu. Mambo haya bungeni yanasimamiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ambaye, kihalisia hana mamlaka wala madaraka yoyote kuhusu Zanzibar.

Muundo uliopo sasa wa Serikali mbili pia umesababisha kuwepo kwa wizara au taasisi zenye sura au zinazotekeleza mambo ya Muungano pekee; mambo ya Tanzania Bara na mambo ya mchanganyiko; kwa maana ya Mambo ya Muungano na mambo yasiyo ya muungano hali ambayo inapelekea ugumu wa kutofautisha gharama za muungano na zisizo za muungano katika wizara au taasisi hizo. Hakuna njia ya kubadili hali hii kwa sababu Serikali ya Muungano haina mamlaka juu ya mambo ya maendeleo kwa upande wa Zanzibar. Mawaziri katika Serikali ya Muungano wamelazimika kufanya mipango na kutafuta rasilimali kwa ajili ya Tanganyika tu. Zanzibar inalazimika kufanya mipango yake wenyewe na ili kupata rasilimali kama vile misaada na mikopo ni lazima ipitie Serikali ya Muungano, jambo ambalo utekelezaji wake una matatizo mengi. Njia pekee ambayo ingefanya mambo ya maendeleo kwa upande wa Zanzibar yapewe uzito sawa na Serikali ya Muungano ingekuwa ni kuyaweka mambo hayo chini ya Serikali ya Muungano, yaani hiyo ingekuwa Serikali Moja badala ya mbili; lakini hilo lingefanyika, Zanzibar ingekuwa imemezwa na Tanganyika.

Kwa upande wa Tanzania Bara, baadhi ya malalamiko kuhusu utekelezaji wa Mambo ya Muungano ni haya yafuatayo:
1. Zanzibar imekuwa nchi huru, ina bendera yake, ina wimbo wake wa Taifa, ina Serikali yake na imebadili Katiba yake ili kujitambua kuwa ni nchi.
2. Zanzibar imebadili masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo inasema Sheria za Muungano zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano zitumike sehemu zote za Muungano, badala yake Katiba ya Zanzibar inaelekeza kuwa ili Sheria itumike Zanzibar ni sharti ipelekwe mbele ya Baraza la Wawakilishi. Maana yake ni kuwa, Katiba ya Zanzibar ipo juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

3. Zanzibar imetunga sheria kuhusu fedha ambalo ni suala lililo kwenye madaraka ya Muungano.
4. Zanzibar imetunga Katiba ambayo imechukua madaraka ya Rais yaliyomo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano yanayoeleza kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano ana madaraka ya kugawa nchi katika maeneo ya kiutawala. Marekebisho ya kumi ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 yameitambua Zanzibar kuwa ni nchi na yanampa mamlaka Rais wa Zanzibar kuigawa nchi katika maeneo ya kiutawala.
5. Katiba ya Zanzibar inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni wa nchi mbili lakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza kwamba, Tanzania ni nchi moja.
6. Masharti ya Kikatiba yaliyowekwa na Katiba ya Zanzibar kuhusu mchango wa Zanzibar katika uendeshaji wa Mambo ya Muungano yanapingana na masharti ya Katiba ya Muungano. Mifano kwenye Katiba ya Zanzibar
7. Muundo wa Muungano uliopo umepoteza utambulisho wa kihistoria wa Tanganyika na fursa ya watu wa Tanganyika kutetea maslahi yao ndani ya Muungano.
8. Wananchi wa Tanzania Bara kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa upande wa Zanzibar wana haki hiyo Tanzania Bara.
9. Pia Wabunge wa Tanganyika kulalamika kuwa Wabunge wa Zanzibar huchangia mijadala kwa mambo yasio ya Muungano na ambayo kwa uhakika wake ni mambo ya Tanganyika na kwamba Wabunge wa Tanganyika hawana nafasi ya kuchangia katika Baraza la Wawakilishi kwa mambo yasio ya Muungano na yanayohusu Zanzibar.
10.Kwa mujibu wa Sheria ya Mzanzibari, 1985 Watanzania ambao ni wa Watanganyika hutakiwa kutimiza sifa maalum ili kuweza kupata haki za kiraia huko Zanzibar ilhali Mzanzibari huweza kupata haki ya kiraia wakati wowote na popote katika ardhi ya Tanganyika. Haki hizo za kiraia ni pamoja na kugombea uongozi na kupiga kura.

Tangu mwanzo wa Muungano ilikubalika kwamba, Zanzibar ibaki na hadhi yake (identity) na iwe na uhuru wa maamuzi kuhusu mambo yasiyo ya Muungano (autonomy). Katika utekelezaji, Zanzibar imechukua hatua za kuimarisha hadhi yake: kwa maana ya kuwa na Bendera, Wimbo wa Taifa, Nembo na Ukuu wa nchi kamili. Pili kwa makubaliano na Serikali ya Muungano, baadhi ya Mambo ya Muungano yamebadilishwa kwa kiwango kikubwa ili kuipa Zanzibar uhuru wa kuamua (Autonomy).

Hivi sasa mambo mengi ya Muungano hayatekelezwi kikamilifu kimuungano. Mambo hayo ni pamoja na kodi, bandari, leseni za viwanda, usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, takwimu, posta na simu, gesi na Mahakama ya Rufani.. Baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa yameleta mgongano kati ya Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar, hasa kwenye vipengele vinavyohusu kodi, Madaraka ya Bunge kutunga Sheria, Madaraka ya Rais kuigawa Nchi, tafsiri ya nchi na uraia.

Mambo haya yamebadilishwa bila kubadili Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na kwa maana hiyo mabadiliko hayo yamevunja Katiba.
Kuna njia mbili za kurekebisha mambo hayo. Njia ya kwanza ni kuyarudisha chini ya Muungano mambo yote yaliyobadilishwa. Kiuhalisia jambo hili haliwezekani. Serikali zote mbili zilifikia makubaliano kuondoa mgongano wa Katiba kwa mambo fulani, kama vile Madaraka ya Bunge, Uraia na kodi, lakini utekelezaji wake ulishindikana kupitia Taarifa ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu jitihada za kuondoa mambo ambayo ni vikwazo katika kutekeleza shughuli za Muungano ( Taarifa ya Kamati ya Shelukindo.

Hata hivyo miaka kadhaa baadae Ripoti ya Shelukindo imeshindwa kutekelezwa kwa ukamilifu wake na kubakisha hali ya mivutano na mizozano ndani ya Muungano, kama ambavyo imekuwa kwa Tume nyengine nyingi ambapo inaonekana zaidi mtizamo wa Tume hizo ni kuiridhisha zaidi Zanzibar ibakie ndani ya Muungano kuliko kutafuta suluhu ya kudumu ya kero za Muungano na kuwa na maslahi kwa pande zote mbili za Muungano.
Hali inakuwa ngumu zaidi kwa sababu baadhi ya mabadiliko yatahitaji kura ya maoni kwa upande wa Zanzibar. Na hata kama ingewezekana kuyarudisha kwenye Mamlaka ya Muungano, matatizo na kero za Muungano zisingemalizika bali zingeongezeka.

Njia ya pili ni kuyakubali mabadiliko yaliyofanywa na kuongeza mengine ambayo yataipa Zanzibar uhuru wa kuamua (Autonomy) mambo yake ya uchumi. Hili linawezekana lakini likitokea ni lazima Tanganyika nayo ipate uhuru wa kuamua (Autonomy). Kwa maana hiyo kutakuwa na Serikali tatu na Serikali ya Muungano itabaki na mambo ambayo itakuwa na madaraka nayo kamili.

Kutokana na malalamiko yanayotolewa na wananchi wa pande zote mbili ambayo Serikali zote mbili zimeshindwa kuyapatia ufumbuzi wa kudumu kwa muda mrefu, baadhi ya wananchi wa Zanzibar wanauona Muungano kuwa ni kero na baadhi ya wananchi wa Tanzania Bara wanauona Muungano kuwa ni mzigo.
Aidha, wananchi wa Tanzania kwa kutumia Tume mbalimbali zilizoundwa kwa mfano Tume ya Nyalali na Kamati ya Kisanga walipendekeza Muungano wa Serikali tatu. Maoni hayo ya wananchi yamependekezwa tena mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na maoni hayo, Tume pia, ilipitia taarifa mbalimbali za utafiti na uzoefu wa nchi nyingine zenye changamoto za muungano. Katika kutoa mapendekezo hayo yenye lengo madhubuti la kuendelea kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ilizingatia ya wananchi yanayoakisi matakwa na matarajio yao ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Tume nayo ilifanya utafiti na kuandaa ripoti juu ya Muungano inayopatikana katika ripoti za utafiti kuhusu Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tatizo la msingi kabisa kwa Muungano wa Tanzania ni la muundo wenyewe wa Muungano wa Serikali mbili badala ya tatu ambao umetoholewa kutoka mifano ya miungano ambayo imeundwa kutokana na chimbuko la ukoloni kama ilivyokuwa kwa muda
 
  • Thanks
Reactions: SMU
Ni "Ramanda" au "Randama"?

Btw, unaweza kutuwekea document zima kama unayo? Please.
 
Binafsi tangu nikiwa mtoto nacheza gwaride la watoto "mapinduzi" shuleni sijawahi kuelewa na kukubali sababu inayotolewa juu ni kwanini tuna serikali mbili, Kwanini hakuna serikali na Rais wa Tanganyika na kwanini Kuna serikali na Rais wa Zanzibar. Kila nikiiambiwa nasita kuyakubali na kuyaamini majibu ninayopewa kama ndiyo hayo kweli ninayopewa na wakubwa zangu, ninahisi kama vile Kuna mchezo mchafu umechezwa au unataka kuchezwa huko mbele ya safari. Huwa ninajiuliza kwanini USA Ina serikali moja kuu na Rais mmoja wakati Kuna nchi zilikuwa ndogo sana wakati wa kuungana?

Hakutakuwa na tabu, dhiki, Mashaka, kiu, Wala hofu kama tutaufanya Muungano wetu uwe ya serikali moja tu la sivyo uwe wa serikali tatu sio mbili. Huu wa serikali mbili umejaa utitii wa maneno, Kuna kila dalili kuwa utapatwa na shida huko mbele kidogo hata kama sio Leo kabisa. Maana Kama Babu, mtoto na mjuu hawaelewi vizuri kwanini hakuna serikali ya Tanganyika lakini Iko serikali ya Zanzibar je, vitukuu vyetu vitakuja kuelewa na kukubali?
Kwanini sisi Leo tusinuse na kuiondoa hiyo harufu mbaya Leo ili vitukuu vya Muungano visiikute na kuwakera?

Kama ni lazima serikali ya Zanzibar iwepo basi Tanganyika Ina options mbili TU, kuwa na serikali yake au kuwa na serikali za majimbo yenye hadhi ya serikali ya Zanzibar chini ya mkuu wa jimbo.

Binafsi serikali moja ndio chaguo la vijana hata kule Zanzibar. Nimefanya utafiti usio rasmi sana kule Zanzibar ulioshirikisha vijana 100 TU conveniently selected niliokutana nao sehemu mbalimbali zikiwemo zile za darajani, forodhani wakati wa jioni, vijiwe vya kula maduriani, pweza, urojo, kule baharini wanakochemsha majongoo, kwenye boat wakati tunasafiri na wete Pemba.

Niliwahoji kuhusu muungano wetu wanauonaje, pamoja na mambo mengine waliojibu lakini zaidi ya 87% wanatamani waende kuishi Tanzania Bara, kule Pemba ilikuwa 94% Yao walitamani kuondoka kwenda kuishi Bara ila wanashindwa TU waendeje huko. Nilipowauliza kwanini wanapenda kwenda kuishi Bara wakasema maswala ya fursa za kiuchumi, usalama, uhuru na nafasi (anonymous).

Hapo nikafahamu kuwa kumbe wanaong'ang'ania lazima serikali mbili au tatu ni wanasiasa TU sio vijana wenyewe ambao ndio wengi. Kama tukiwahesabu wazanzibar wanaoishi Bara Leo unaweza kuona ubaya wa serikali mbili au tatu. Hata ukizitizama mboni za macho ya Mwl Nyerere, Mzee Mwinyi, Samia,, SheIn na Dk Mwinyi unaiona dhamira ya serikali moja kwenye macho Yao. Maana faida ni kubwa sana kuliko hasara.
 
Serikali moja kuu ndio mfumo wa kueleweka.
Kuwepo na majimbo upande wa Tanganyika na jimbo la Zanzibar chini ya serikali za magavana.
 
Serikali moja ndio mpango ila haitowezekana
Serikali moja ndio iliyokuwa ndoto na Siri ya serikali mbili za Sasa, jambo hili linafichwa hadi lini?. Ni jambo la ajabu kuona wanasiasa wanalionea aibu swala la serikali moja huku wakifahamu kuwa wazanzibar kwa maelfu na wabara kwa mamia wanaishi na wanapenda kuisahi popote ndani ya Tanzania bila kuhojiwa Wala kuulizwa kama watanganyika au wazanzibar. Hizi jamii mbili sasaa zimeingiliana mno kwa damu, kifamilia, kijamii, kiuchumi na kisiasa. Tanganyika hakuna Siri tena ambavyo wazanzibar hawalijui.
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom