Rais wangu JPM, Fanya haya urudishe imani yetu.

Fabian the Jr

JF-Expert Member
Aug 4, 2012
756
738
Salaam,
Awali ya yote nikupe pole kiongozi wangu kwa kazi hii kubwa sana ya kuliongoza taifa letu, Naam sio kazi rahisi kuongoza nchi kubwa kama hii yenye watu wengi kiasi hiki na huku kila kundi likihitaji kutimiziwa mahitaji yao. Ni dhahiri kwamba kadri siku zinavyozidi kwenda imani ya sisi wananchi tuliokupigia kura inapungua siku baada ya siku. Sina uhakika sana iwapo ungepata ushindi ule ule iwapo ungeitishwa uchaguzi wakati huu, ukapambanishwa na uliyemshinda uchaguzi uliopita. Kwa maoni yangu fanya haya mambo na watanzania watakuwa na imani tena na wewe.

1. Jenga umoja na mshikamano miongoni mwa watanzania na sio kuuvunja. Kwa miaka takribani 50 tangu uhuru wetu viongozi wetu wamekuwa mstari wa mbele kuhubiri umoja kati ya watanzania. Kazi hiyo ndio inasababisha leo mimi Msukuma nataniana na kucheka vizuri sana na Mchaga, naweza kwenda kuishi au kuoa popote pale nchini. Kwa maneno yako uwe chachu ya kuujenga huu mshikamano na sio kuchochea kuuvunja.

2. Ongoza nchi kwa mujibu wa katiba. Mh, ni katiba hiyo ndo inakupa wewe mamlaka uliyonayo, hiyo ndo inakuruhusu wewe kuteua wakuu wa mikoa, wakurugenzi, wakuu wa idara na kadhalika, ni katiba hiyo imeruhusu mfumo wa vyama vingi nchini, na ikaeleza majukumu ya vyama hivyo vya siasa na kazi zake. Ulipokuwa unaapa uliahidi kuilinda katiba, tafadhali mh, Usiivunje katiba na kufanya maneno yako wewe kuwa ndio katiba. Katiba ndio muongozo wako, ndio maneno ya wananchi wako walivyokubaliana na kuamua kuishi, tafadhali rudi kwenye katiba na ufanye kila unalofanya kwa kuzingatia katiba.

3. Usiongoze peke yako, Ongoza na wenzako. Mwalimu Nyerere inasemekana alipokuwa kwenye vikao vya baraza la mawaziri yeye alikuwa haongei, alikuwa anasikiliza mawaziri wake wanamwambia nini, alikuwa anasikiliza wapinzani wake wanasema nini. Viongozi uliowateua, wape fursa ya kutekeleza majukumu yao kwa uhuru, mijadala ya kitaifa ijadiliwe na watu wote, na isiwe wewe ukilala ukaamka unatoa agizo la kufanya bila kujadiliana na wadau husika. Ruhusu watu waongee, waseme waliyonayo mioyoni mwao, na wewe ufanya maamuzi bila upendeleo kwa kuangalia maslahi mapana ya nchi yetu.

4. Kama upinzani unakuzuia, una mamlaka ya kuuondoa. Kama ukiona hauhitaji upinzani kwenye serikali yako, peleka mswaada bungeni turudi mfumo wa chama kimoja, Naumia sana ninapoona mawazo mazuri sana yanatolewa na upinzani lakini yanaonekana ujinga tu kisa yametolewa na upinzani. Wataalamu kina Zitto Kabwe, Kina Tundu lissu na wengine wengi wanahitajika kuitoa nchi hii ilipo kusogea mbele, lakini ni mara ngapi wanasikilizwa? Kama kuwa kwao upinzani ni tatizo ondoa vyama vya upinzani wote warudi CCM tuijenge nchi yetu.

5. Mheshimiwa, aliyefanya kazi anastahili thawabu yake. Wakati nakua nilikuwa naambiwa, " Mwanangu jitaidi kusoma ili upate maisha mazuri" siku hizi hata kumwambia hivyo mwanao inakuwa tabu, wamemaliza vyuo vikuu wako mtaani hawana ajira, wenye ndugu zao kwenye vitengo ndo wanaaniriwa, rudisha hadhi na heshima ya elimu yetu, aliyesoma kwa bidii basi apate nafasi stahili.

6. Sikiliza maoni ya wataalamu / wasomi kabla ya kufanya maamuzi yoyote yanayolihusu taifa. Nchi yoyote iliyofanikiwa lazima inatilia maanani mchango wa wasomi katika maamuzi yake. Tunao wasomi wanaoweza kuisaidia sana nchi hii, kina Prof Shivji, Jen, Ulimwengu, Prof Mhongo, Prof Lipumba, Mh Mwigulu nk ni wataalamu waliobobea kwenye fani zao, watumie vizuri hawa.

7. Yatafakari sana yanayosemwa na wabunge wa chama chako, naamini wengi wanaongea maneno ambayo wanajua utayapenda, wengi hawakwambii ukweli wa mambo, yatafakari kwa kina kabla hujayapitisha. Kuna watu wanaweka maisha yao rehani ili tu kukufikishia ujumbe, sikiliza ujumbe wao.

Bado nina imani na wewe Rais wangu, naamini unaweza kuipeleka hii nchi kwenye ustawi. Kumbuka wewe ni Rais wa taifa, na sio JPM tena, weka hisia zako pembeni unapofanya maamuzi ya kitaifa na uangalie maslah ya taifa lako kwanza. Usitubague kwa vyama, kanda na makabila. Tupende raia wako kama tunavyokupenda Raisi wetu.
 
TUIMBE WOTE:

Tanzania, Tanzania,
Nakupenda kwa moyo wote,
Nchi yangu Tanzania,jina lako ni tamu sana,
Niamkapo nakuwaza wewee.......
 
Back
Top Bottom