Rais Wa Nchi Anapotoa Machozi Hadharani! ( Raia Mwema Jana Jumatano)

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Na Maggid Mjengwa,



KUNA wakati, katika mwaka huu, vyombo vya habari vya dunia vilimwonyesha Rais Hamid Karzai wa Afghanstan akitoa machozi hadharani. Ni pale alipotamka kwa uchungu akielezea hali ya nchi hiyo kukosa amani: “ Watoto wangu watakwenda kuishi uhamishoni kwenye nchi za kigeni…”, akaanza kububujikwa machozi.




Rais Karzai alizungumza na kutoa machozi kutokana na kuona hali halisi ya nchi yake. Kwamba kuendelea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kukosekana kwa amani kutapelekea hata watoto wake mwenyewe ( Rais) kukimbilia uhamishoni. Jambo hilo lilimuuma sana. Tuna cha kujifunza.




Kufuatia Uchaguzi Mkuu wetu uliopita na matokeo yake, sauti za Watanzania kutaka uwepo wa Katiba Mpya zimeongezeka zaidi; mijini na hata vijijini.
Matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu yamedhihirisha jambo moja kuu ; Watanzania wanataka mabadiliko. Hii si ajenda ya chama cha siasa, ni ajenda ya Watanzania kwa ujumla wao. Vyama vya siasa vina wajibu wa kusaidia kufanikisha azma hii.
Kwa Chama tawala kuruhusu kuanzishwa kwa mchakato wa kupata Katiba mpya si tendo la kuwafanyia ’hisani´wapinzani wa kisiasa; bali ni wajibu wa kisiasa kwa maslahi ya nchi na kuna maslahi ya kisiasa hata kwa Chama tawala.




Idadi ya Watanzania wanaonyesha kuchoka na hali iliyopo inaongezeka. Wanataka uwepo wa misingi imara zaidi ya demokrasia. Wanataka haki zaidi za kidemokrasia na hivyo kuweza kupiga hatua zaidi za maendeleo ya mtu mmoja mmoja, kikundi cha watu na nchi yao kwa ujumla.


Ni dhahiri, kilio cha kutaka Katiba mpya kinazidi kusikika. Hata kabla ya Uchaguzi Mkuu, tulimsikia Jaji Mkuu Augustino Ramadhani akitamka; kuwa Katiba ni Nyaraka inayoishi ( A living document ). Kwamba inaweza kubadilika ili kukidhi mahitaji ya wakati husika. Na juzi hapa tumemsikia Jaji Manento pia naye amezungumzia Katiba mpya kwamba wakati umefika kuwanayo.




Na hata juzi hapa, pale Waziri Mkuu wa Kenya Bw, Raila Odinga alipotua Mwanza aliweka wazi, kuwa Katiba ni jambo la wananchi. Inapofika wakati wananchi wanapohitaji marekebisho ya Katiba, ni vyema jambo hilo likafanyika. Wao Kenya wamesubiri kwa miaka 47. Na sasa wameamua kuondokana na Katiba iliyotokana na mkoloni.
Ndio, Katiba tuliyo nayo ya tangu mwaka 1977, kwa macho, si ya wasomi wetu tu, hata watu wa kawaida, imeonekana haikidhi matakwa ya wakati uliopo. Ndio msingi wa hoja ya uwepo wa Katiba Mpya.


Maana; katika nchi zetu, Katiba zimetokana na Katiba za mkoloni. Vifungu vingi vya Katiba imekuwa ni kama kazi ya kunakiri na kupachika ( copy and paste) kutoka Katiba ya mkoloni. Kwa Wakoloni waliotawala nchi zetu, Katiba ilikuwa na maana moja kubwa; Wachache kuandaa utaratibu wa kuwatawala walio wengi.


Waafrika tulio huru kutoka minyororo ya wakoloni, tunapaswa sasa kuandaa Katiba za kutuwezesha kujitawala na si kikundi kidogo cha Waafrika wenzetu kututawala.
Ni makosa kuiacha kazi hiyo kufanywa na kikundi kidogo cha watu katika nchi, kwa maana ya chama cha siasa. Kukipa jukumu lote la kutunga Katiba ya nchi kwa niaba ya makundi mengine yote.




Maana; chama cha siasa nacho ni mkusanyiko wa kikundi cha watu katika nchi. Kikundi ambacho, moja ya malengo yake, ni kupewa dhamana ya uongozi wa nchi.
Yawezekana kuwa mazingira ya tangu mwaka 1961 hadi 1977 yaliruhusu hali hiyo ya chama cha siasa kushika hatamu na hata kutunga Katiba ya nchi. Lakini sasa tumeingia mwaka 2010. Ni karne ya 21. Wakati umebadilika, na dunia pia.




Watanzania wa leo, kama tunaona kazi ya kutengeneza Katiba mpya ni ngumu, basi, ni heri kunakili na kupachika Katiba ya jirani zetu wa Kenya kuliko kuendelea kuendesha mambo yetu kwa Katiba hii ya mwaka 1977. Kila kizazi na jukumu lake.
Kwa kuendelea kufanya hivyo, basi, ni kwa makusudi kabisa tunakubali kulisaliti jukumu la kizazi chetu, kwa kutanguliza ubinafsi wetu. Na hakika, kwa kutanguliza ubinafsi wetu, tunawaandalia watoto na wajukuu wetu mazingira magumu ya kuishi kwa amani katika nchi yao.




Katiba Mpya kwa Tanzania ya leo, kesho na keshokutwa, ni urithi wa maana na wa kistaarabu tutakaowaachia watoto na wajukuu zetu. Na mathalan, Tume Huru ya Uchaguzi, ni DHAMANA ya kipekee ya Amani na Utulivu tutakayowaachia Watanzania wa vizazi vijavyo.




Maana; katika nchi zetu hizi, mara nyingi watu huanza kuchinjana kutokana na kukosa imani na wenye kuhesabu kura - Tume ya Uchaguzi.
Watanzania tushukuru kuwa uchaguzi wa mwaka huu haukusababisha vurugu za umwagaji damu. Lakini tumeona dalili kuwa uchaguzi mkuu ujao, kama utafanyika bila uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi, unaweza kabisa kutuingiza Watanzania katika vurugu za umwagaji damu. Tushtuke na unyasi hata kabla hatujaumwa na nyoka.




Kwa nini ni kazi ngumu kuelekea kwenye kupata Katiba mpya? Kuna baadhi watakaofanya kila wawezalo kuzuia au kuchelewesha ujio wa Katiba mpya katika nchi yetu, maana, kwao wao, Katiba mpya ni sawa na kiyama cha kisiasa.
Si tu wanahofia kupoteza mamlaka zao za uongozi, wana hofu kuu juu ya hukumu ya dhuluma walizolifanyia taifa letu. Hawa si kama yule Hamid Karzai, Rais wa Afghanstan. Hawatatoa machozi. Watakuwa tayari watoe bure mapanga ili Watanzania wachinjane. Wanako pa kukimbilia, na kwao ni fahari kwa watoto wao kuishi uhamishoni, iwe Ulaya au Marekani. Wanachotanguliza ni ubinafsi wao, kwa gharama zote, na si maslahi ya taifa.




Katika moja ya makala zangu (Raia Mwema) nilipata kuirejea kauli ya ya Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo juu ya amani. (Mwananchi, Novemba 5, 2010). Mwadhama Kardinali Pengo alizungumzia umuhimu wa uwepo wa amani.
Katika makala yangu hiyo, nilikwenda mbele zaidi. Nilibainisha kuwa pasipo haki hakuna amani. Na swali ni je; haki inapatikana vipi? Nikaongeza kuandika kuwa swali tusilopaswa kujisumbua kujiuliza ni juu ya nani atakuwa Rais wetu mwaka 2015; bali tujisumbue kwa kujiuliza; Je, Rais wetu wa 2015 tutampata kwa Katiba ipi, na kwa mfumo gani wa uchaguzi?






Sote, wakiwamo viongozi wa dini, tuna lazima ya kuyatafuta majibu ya maswali haya. Kwa mfano, wenzetu kule Marekani Katiba yao ina zaidi ya miaka mia mbili. Kubadili kipengele tu katika katiba ya Marekani inaweza kuwa ni mchakato wa miaka kumi.
Hakuna hata Rais wa Marekani anayeweza kuichezea Katiba ya Marekani kwa maslahi yake, anaweza kuishia gerezani anayejaribu kufanya hivyo. Wamarekani wale hata wakimweka ‘mwendawazimu’ Ikulu wanajua namna ya kumdhibiti kikatiba. Ni tofauti na sisi.




Mwanafalsafa Charles Montesque aliyeasisi nadharia ya mihimili mitatu ya dola alikuwa na maana pia ya kumpunguzia Rais nguvu nyingi. Wakati huo huo alitaka kuongeza nguvu kwa Bunge na Mahakama. Katika nchi zetu hizi, unapozungumzia kuliongezea nguvu Bunge na Mahakama, ina maana pia ya kutoa tafsiri ya kuipunguzia nguvu Serikali na kwa maana hiyo kumpunguzia nguvu Rais.




Leo tunatumia muda mwingi kujadili nani atateuliwa kuwa waziri kwenye baraza jipya. Kesho tutajadili nani atateuliwa kuwa mkuu wa mkoa. Keshokutwa tutajadili nani atakuwa mkuu wa wilaya. Ndio, tunajadili vyeo na watakaoshika vyeo hivyo. Ndivyo tulivyo. Hatujadili namna tutakavyowafanya wateule hao watakavyowajibika kwa wananchi.




Tuachane na ukale huo. Tuanze sasa kujiuliza; Je, tunawapataje wateule hao? Maana, hapo tutaanza kujadili Katiba na mfumo wetu wa uchaguzi. Sentesi hiyo ya mwisho ndio inayopaswa tukae chini na kuumiza vichwa vyetu kuijadili. Ina maslahi mapana kwa nchi yetu, leo, kesho na keshokutwa. Nahitimisha.
hs3.gif

Simu:
0754 678 252

Barua-pepe:
mjengwamaggid@gmail.com

Blogu:
mjengwa.blogspot.com
 
Umesomeka vizuri sana... Ni jukumu letu sote kupingania mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya....

Maggid, ungekuwa hivi siku zote ungekuwa msaada mkubwa sana kwa Watanzania, hivi unajua ni kiasi gani ulipotosha watu na makala zako za kipindi cha uchaguzi?
 
kaka mjengwa,nimekuelewa vizuri sana ktk hiyo thread yako,ni kweli tunaongozwa na katiba ambayo tumeachiwa na wakoloni na haina tija kwa wakati huu tulionao,mimi kinacho ni shangaza ni hawa viongozi wakubwa wa hii nchi inamana hawalioni hilo? na kama hawalioni je hata maoni ya watu hawayaoni juu ya katiba mpya? nimekuwa nikijiuliza sana juu ya haya maswali,mwishowe nikaja na jibu kuwa,wanaelewa kila kitu ila kwa kuwa katiba inawagusa wao wachache hawaoni umuhimu wa kufanya mchakato wa kupata katiba mpya,kwani ktk hii nchi ukiona kiongozi mkubwa anashabikia jambo juwa kuwa linamgusa yeye na familia yake hata kama halitakuwa na faida kwa taifa.
hivyo kama ulivyo sema kaka mjengwa umefika wakati sasa wa kuamsha mapambano ya kudai katiba mpya,tusihofu juu ya hilo kwani hata uhuru ulipiganiwa na watu wachache na sasa watu zaidi ya mil 29 tunafaidi uhuru huo,hivyo tuanze sasa kwani ngojangoja huumiza matumbo.
hakuna sababu ya kukopi katiba ya wenzetu jilani kwani mda tunao na pesa tunazo za kuweza kufanya kazi hiyo,hapa kinachogomba ni utayari wa hawa viongozi wa juu ambao wapo kimaslahi zaidi kuliko taifa hili

lolote lile lawezekana ilimradi tu uwepo ushirikiano na ujasiri wa kudhubutu

naunga mkono hoja

mapinduziiiiii daimaaaaaaaa 15202425864
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom