#COVID19 Rais wa Marekani, Joe Biden aahidi msaada zaidi wa chanjo kwa Afrika

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Rais wa Marekani Joe Biden ameahidi msaada wa dozi milioni 17 za chanjo ya corona kwa bara la Afrika wakati alipomkaribisha rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na kuahidi pia ushirikiano zaidi na bara la Afrika.

Wakikutana katika ikulu ya White House mjini Washington, Biden na Kenyatta waliahidiana kushirikiana kukabili mabadiliko ya tabia nchi na kumaliza machafuko katika pembe ya Afrika.

Biden alitangaza kuwa Marekani itatoa mara moja msaada wa dozi milioni 17 ya Johnson & Johnson kwa Umoja wa Afrika, ikiwa ni nyongeza ya dozi milioni 50 ambazo ilishatoa.

Biden amesema anatumai chanjo hizo zitasaidia nchi za Umoja wa Afrika. Ameahidi kutoa misaada zaidi ya chanjo dhidi ya COVID-19 kwa Kenya ifikapo mwisho wa mwaka.

Rais Kenyatta ameukaribisha msaada huo akisema zitasaidia kampeni ya utoaji chanjo Afrika.

"Ni furaha kusikia tangazo lako jipya la nyongeza hiyo ya chanjo kwa sababu kama mjuavyo, kama bara tunajikokota nyuma ya mabara mengine kuhusu uwezo wa kuwachanja watu wetu. Kwa hivyo nyongeza yoyote ya msaada kama ambavyo Rais Biden ametaja inakaribishwa sana na tunatumai kushirikiana zaidi,” amesema Rais Kenyatta.

Biden ameahidi lengo jipya, kuzingatia demokrasia, tofauti na mtangulizi wake Donald Trump aliyekuwa karibu viongozi waliongoza kwa mabavu, lakini pia ambaye hakuficha kutoipenda Afrika.

Kenyatta ndiye kiongozi wa kwanza wa Afrika kuzuru ikulu ya Marekani chini ya utawala wa Biden, mnamo wakati ziara na mikutano ya kilele imepunguzwa kama hatua ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Ziara ya Kenyatta ambaye ameahidi kupambana na ufisadi, imejiri mnamo wakati akikabiliwa na ukosoaji kufuatia ufichuzi wa siku chache zilizopita kwenye nyaraka za Pandora uliomtaja yeye na watu sita wa familia yake kumiliki kampuni sita zenye thamani ya dola milioni 30 nje ya Kenya.

Biden hakugusia madai hayo walipozungumza na waandishi wa habari lakini alitoa wito wa kuimarishwa kile alichokitaja kuwa "uwazi katika mifumo ya fedha.” Alimshukuru Kenyatta. Kwa uongozi wake wa kulinda amani, usalama na demokrasia ya nchi yake na kanda nzima.

"Nchi zetu zinashirikiana kwa dhati kuhakikisha kuna haki, heshima na usawa, na nimejitolea kuimarisha ushirikiano zaidi na Kenya nan chi za Afrika nzima- lakini Kenya ni mshirika muhimu kwa hili," amesema Biden.

Kenya ndiyo inashikilia kwa sasa urais wa kupokezana wa Baraza La Usalama la Umoja wa Mataifa, na imetumia nafasi hiyo kutaka machafuko ambayo yamewaacha maelfu ya watu bila makao na wengi kung'ang'atwa na njaa katika nchi jirani Ethiopia yakomeshwe.

Kenya pia ni mshirika wa muda mrefu wa Marekani katika masuala ya usalama, wakishirikiana karibu kupambana na wanamgambo wa Alshabaab katika taifa jirani la Somalia.

Rais Kenyatta alisema alikuwa anazungumza na Biden kuhusu "vita dhidi ya ugaidi” lakini pia kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, kuelekea mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika Glasgow mwezi ujao.

Hata hivyo matumaini ya Kenya ya makubaliano ya kibiashara huenda hayakutimia.

Afisa mmoja wa ngazi ya wa Marekani ambaye hakutaka kutambulishwa amesema utawala wa Biden utafany akazi kwa karibu na Kenya kuhusu biashara lakini akaongeza kwamba bado wanafikiri jinsi ya kushughulikia biashara ya kigeni.

Chanzo: DW Swahili
 
Na tusisahau kwamba nchi za ulaya hazitambui baadhi ya chanjo zikiwemo zile tulizodungwa, majina yake mnayajua wenyewe.
 
Back
Top Bottom