Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awe Mbunge wa kuchaguliwa

Filosofia ya Rorya

JF-Expert Member
Sep 20, 2021
3,214
3,587
Kwa minajili ya kuleta uwajibikaji mzuri wa serikali na usimamizi mzuri wa mhimili wa bunge kwa serikali, muda sasa ni muafaka kwa taifa letu kuanza kutafakari uwezekano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kuwa mbunge pia wa kuchaguliwa na kwamba hii iwe ni sifa mojawapo ya lazima ya kustahili nafasi ya Urais. Hii pia ni namna mojawapo ya upanuzi wa demokrasia ya nchi yetu.

Moja ya faida zinazoweza kupatikana kutokana na utekelezaji wa dhana hii ya Rais kuwa pia mbunge wa kuchaguliwa ni kwamba Rais kama mbunge atashiriki maamuzi ya kibunge awapo bungeni na kwamba Serikali itakapohitajika kutekeleza maamuzi ya bunge basi Rais kama kiongozi mkuu wa serikali hiyo hatasitasita madhali ameshiriki kupitisha maamuzi hayo katika ngazi ya bunge akiwa kama mbunge pia na hivyo atasaidia katika kuhimiza utekelezaji wake pasina shaka.

Rais-mbunge asiruhusiwe kuchaguliwa au kuteuliwa kushiriki nafasi za dhamana za uongozi wa bunge kama Spika, Mwenyekiti au Mjumbe wa kamati za kudumu na tume za bunge kwa sababu kuu mbili: kwanza majukumu ya Urais, Amiri Jeshi Mkuu, Mwenyekiti wa chama, Ubunge na nafasi zingine anazoshika katika medani za kimataifa tayari ni majukumu mazito na makubwa sana yenye kuhitaji muda mwingi sana katika kuyasimamia hivyo kutokuteuliwa na kutokuchaguliwa katika asasi za kibunge kama kamati na tume kutasaidia kumfanya ajikite katika kutafuta tija zaidi kwa nafasi zake hizo za msingi.

Rais kama mbunge aruhusiwe kuwa na kura katika kupitisha maamuzi ya kibunge isipokuwa yeye kama kiongozi wa nchi kwa nafasi ya Urais ambapo anaongoza wananchi wote pasina kujali itikadi, vyama, rangi, dini na makundi mengine yote ya kimaslahi katika jamii, aruhusiwe kupiga kura huru, yaani katiba ya chama chake isimbane kupiga kura fungamani kuunga mkono hoja za chama chake tu ndani ya bunge isipokuwa awe huru kupiga kura kuunga mkono hata hoja ya chama kisicho chake au makundi asiyofungamana nayo, kwa maana kwamba asiwe na maslahi katika kupiga kura isipokuwa kura yake izingatie mantiki, nguvu, lengo na mwelekeo wa hoja kwa manufaa ya wananchi wake wote anaowaongoza.

Rais kuwa mbunge pia kutasaidia kuimarisha mahusiano kati ya bunge na serikali ambavyo vyote hivi viwili dhamira yao ni moja ya kuwatumikia wananchi, ila ni muhimu kuzingatia kuwa Rais awapo bungeni kama mbunge, alazimike kuwa chini ya mamlaka ya Spika kama kiongozi wa juu wa chombo hicho, ila madaraka ya Rais ya kuzindua na kuvunja bunge yaendelee kubaki kama utaratibu ulivyo hivi sasa.

Rais pia afaidike na utaratibu uliopo wa kugombea ubunge katika jimbo lolote nchini ikiwemo Tanzania bara na visiwani isipokuwa tu majimbo ya taasisi za elimu ya juu [kama yataanzishwa] kutokana na unyeti wa taasisi hizi. Hii pia itasaidia kuimarisha muungano wetu pale ambapo Rais ataamua kugombea ubunge katika upande wa pili wa muungano.

Kiongozi wa shughuli za serikali bungeni aendelee kuwa Waziri Mkuu kama kawaida. Bendera ya Rais ipandishwe nje ya ukumbi wa bunge pale tu Rais ama anapolizindua au anapolivunja bunge na siyo anaposhiriki vikao vya kawaida vya bunge. Hii ifanyike ili kuondoa mkanganyiko wa kiitifaki wa Rais kama mbunge wa kawaida kuwa na uhalali wa kuvunja na kuzindua bunge, hivyo Rais akipandishiwa bendera yake wakati wa uzinduzi na uvunjaji wa bunge basi upandishaji huo wa bendera yake utampa mamlaka ya zaidi ya ubunge, kwa tafsiri nyepesi ni kuwa atakuwa mbunge mwenye nguvu ya ziada [MP Extraordinary] lakini Spika bado ataendelea kuwa kiongozi mwenye mamlaka ya juu bungeni.

Ikumbukwe kuwa Spika pia ni mbunge lakini mwenye mamlaka zaidi ya wabunge wa kawaida. Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwenye sura ya tatu, sehemu ya kwanza, ibara ya 62, ibara ndogo ya [1] inasema Rais pia ni sehemu ya bunge [yaani bunge lina sehemu mbili: wabunge na Rais]. Rais pia kama mbunge ashiriki kupiga kura kuthibitisha jina la waziri mkuu mteule.

Uwepo wa Rais bungeni kama mbunge utafanya watendaji walio chini yake serikalini na kwenye chama kuongeza bidii na nidhamu ya kazi wakizingatia kutunza heshima ya Rais, serikali na chama bungeni; ambaye yeye Rais pia ni mwajiri wao mkuu.

Ubunge wa Rais ukome pale bunge linapovunjwa na kwa minajili ya kuendeleza baraza la mawaziri [ambalo ni chombo nyeti katika kuendesha serikali] baada ya bunge kuvunjwa ili kuondoa ombwe la kukosa baraza la mawaziri, napendekeza Rais apewe mamlaka ya kuwateua Mawaziri wale kuwa wabunge wa kuteuliwa na Rais wa muda mfupi [MPs Emeritus] kuelekea Rais mpya atakapounda serikali mpya. Mamlaka yale ya Rais kuteua wabunge 10 yatumike katika wakati na fursa kama hii na kwamba uteuzi ule wa wabunge 10 wa Rais usiwepo tena isipokuwa baada ya bunge kuvunjwa tu na uhusu mawaziri pekee.

Hapa Rais atateua wabunge ambao ni mawaziri hawa ambao ubunge wao wa kuchaguliwa ulikoma pale Rais alipolivunja bunge. Spika apewe mamlaka ya kumteua Rais kuwa mbunge baada ya bunge kuvunjwa kuelekea kuundwa serikali mpya na wote Rais na mawaziri wake ubunge wao wa kuteuliwa wa muda mfupi baada ya bunge kuvunjwa ukome pale serikali mpya inapoapishwa.

Nafasi ya Urais inapokuwa wazi kwa sababu yoyote zaidi ya uchaguzi ubunge wake nao ukome; Makamu wake atashika kwa muda nafasi yake ya ubunge ili wapiga kura wa jimbo hilo wasipoteze haki yao ya kuwa na mwakilishi bungeni. Hapa Makamu wa Rais atalazimika kula kiapo kwanza ili aweze kushiriki vikao vya bunge.

Endapo Rais mpya atapatikana lakini akawa ameshindwa katika nafasi ya ubunge, Spika apewe mamlaka ya kumteua kuwa mbunge ili kuepuka gharama za zoezi la kurudia uchaguzi wa Rais kwa sababu tu ameshindwa kiti cha ubunge. Na hii iwezekane pale tu ambapo serikali siyo ya mseto.

Nafasi ya ubunge wa Rais ikipingwa na kutenguliwa mahakamani na kumpa ushindi mpinzani wake, napendekeza Spika apewe mamlaka ya kumteua Rais kuwa mbunge wa kuteuliwa ili kunusuru taifa na gharama kubwa za zoezi la uchaguzi wa Rais kurudiwa kwa kigezo tu cha kutenguliwa ubunge wake na mahakama.

Kama itatokea kuwa Rais amefariki dunia, na kwamba uchaguzi unalazimika kurudiwa kabla ya ratiba ya kawaida ya uchaguzi mkuu kutimia, basi mgombea Urais mpya aruhusiwe kugombea ubunge katika jimbo la Rais aliyefariki dunia na kama atashindwa ubunge lakini akashinda Urais napendekeza Spika apewe mamlaka ya kumteua kuwa mbunge.

Katika jimbo hili, wote wanaogombea Urais kupitia vyama vyao vya siasa na wale ambao siyo wagombea Urais lakini walioamua kugombea ubunge, wote waruhusiwe kugombea ubunge kupitia jimbo hili.

Rais akijiuzulu Urais, basi alazimike kujiuzulu na ubunge pia ili kutoa nafasi kwa wagombea wapya wa Urais kupata jimbo la kugombea ubunge.

Faida nyingine ya mgombea urais kuwa mgombea ubunge pia ni kuwa kama dhana hii itatekelezwa, itawawezesha wale wagombea urais wazuri kwa ujenzi wa hoja watakaoshindwa kiti cha Urais lakini wakashinda kiti cha ubunge waingie bungeni na kuwezesha wapiga kura, bunge na taifa kwa ujumla wake kufaidika na michango yao pevu Bungeni ambapo ndipo jukwaa maalum yanakofanyika maamuzi yenye mustakabali wa taifa kuliko ilivyo hivi sasa ambapo wakishindwa kiti cha urais basi wanabaki kwenye vyama vyao tu ambavyo siyo majukwaa halali kisheria ya kufanya maamuzi yenye kuathiri kwa matokeo chanya mustakabali wa taifa na mara nyingi tumeshuhudia makabiliano na vyombo vya dola pale walipojaribu kuweka misimamo yao ambayo mara nyingi imedhaniwa inasighishana na sheria za nchi.

majwalaoriko@yahoo.co.uk
 
Back
Top Bottom