Rais Samia, zungumza mambo haya 10 na vijana wa Kitanzania

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,074
Rais wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameahidi kuzungumza na vijana wote wa Tanzania kupitia vijana wa mkoa wa Mwanza.

Hii ni fursa kubwa kwa Raisi kuweza kusikia kutoka kwa vijana, lakini pia kuwashirikisha vijana wa Tanzania mwelekeo wake na mategemeo yake kutoka kwao.

Mimi kama kijana wa Tanzania, na ambaye nimefanya kazi kwa karibu na vijana wengi wanaopambana kuyajenga maisha yao, kuna maeneo makubwa kumi ambayo nayaona yanahitaji kujengewa msingi sahihi kwa vijana ili nchi yetu Tanzania iweze kupiga hatua kubwa.

Kwa kuwa sitapata nafasi ya kushiriki mazungumzo hayo moja kwa moja, nashirikisha maeneo hayo kumi na kwa nguvu ya teknolojia nina hakika yatamfikia Raisi.

vijanawatanzania.jpg

Kumekuwa na usemi kwamba vijana ni taifa la kesho, usemi huu siyo sahihi. Vijana siyo taifa la kesho, vijana ndiyo taifa lenyewe. Ni vijana ndiyo wenye nguvu ya kupambana usiku na mchana kwenye shughuli mbalimbali za kulijenga taifa.

Na hata tukikubali kwamba vijana ni taifa la kesho, hilo taifa linaandaliwaje leo?

Kwa kufanyia kazi maeneo haya 10 ninayoshirikisha hapa, kuna nafasi nzuri ya kujenga vijana imara na wenye mchango mkubwa kwenye taifa letu.

1. Biashara na Ujasiriamali
Serikali haina uwezo wa kuwaajiri vijana wote waliohitimu elimu katika ngazi mbalimbali. Hata sekta binafsi pia haiwezi kuwaajiri wote wanaotaka kazi. Lakini jamii zetu zina mahitaji na changamoto mbalimbali ambazo zikipata utatuzi wapo tayari kulipia.
Hii inatoa fursa kubwa ya vijana kuweza kufanya biashara na ujasiriamali wa aina mbalimbali kulingana na mahitaji yaliyo kwenye jamii.

Vijana wanaziona sana fursa hizo na wapo tayari kuzifanyia kazi, lakini mazingira yamekuwa siyo rafiki kwao kuchukua hatua.
Kuanzisha na kurasimisha biashara kwenye nchi yetu kimekuwa kikwazo kwa wenye nia ya kufanya hivyo.

Tunashukuru usajili wa biashara umerahisishwa sana kupitia BRELA, ila eneo la kodi bado lina changamoto kubwa. Kijana anayeanzisha biashara mpya anatakiwa kuanza kulipa kodi kabla hata biashara haijaweza kuzalisha faida. Biashara yoyote ile ina hatari ya kufa hasa kipindi cha mwanzo. Kama ukiwekwa utaratibu wa vijana kupata neema ya kodi katika miaka miwili ya mwanzo ya biashara, huku wakiwa wanazifanya biashara zao kwa mfumo rasmi, itasaidia sana.

Taifa litapata mapato zaidi kupitia mzunguko unaotengenezwa na biashara mpya zinazoanzishwa na vijana kuliko linavyopoteza kwenye kodi.

2. Fedha na Uchumi
Hali ya uchumi wa kijana wa Tanzania bado iko chini sana kutokana na ushiriki wake mdogo kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Na kikwazo cha kwanza ni fedha, vijana wengi hawana vipato kabisa na wale walio navyo haviwatoshelezi kwenye mahitaji yao.
Hilo linakuwa kikwazo kwao kushiriki shughuli za uchumi kama kuanzisha biashara na hata kuwekeza pia. Huduma za kifedha zimekuwa zinawatenga vijana kwa sababu hawakidhi vigezo muhimu vilivyowekwa, kama kuwa na dhamana ili kupata mikopo.

Kwa kuwa serikali imeweza kuwakopesha vijana wengi wakapata elimu ya juu, inaweza pia kuwakopesha fedha za kuwawezesha kushiriki shughuli za uchumi. Vijana wajengewe uwezo wa kuwa kwenye vikundi ambavyo vitapewa mikopo ya kutumia kwa shughuli za uchumi na kuilipa kwa njia nafuu kuliko mikopo ya taasisi za kifedha. Pia elimu ya kijana iweze kutumika kama dhamana ya kupata fedha kwa shughuli mbalimbali anazofanya.

3. Kilimo na Ufugaji
Uhitaji wa chakula ni mkubwa kwenye nchi yetu na nji za jirani. Nchi yetu imejaliwa kuwa na eneo kubwa la ardhi ambayo bado haijatumika kabisa. Hayo yanatoa fursa kubwa ya vijana kuweza kujishughulisha na kilimo na ufugaji. Lakini changamoto kwenye eneo hilo ni kubwa mno. Kuanzia kwenye uzalishaji mpaka kufika sokoni, kijana anakumbana na mengi yanayomuangusha kabisa.

Vijana wengi wamejaribu kilimo na ufugaji na hawajaweza kurudia tena kutokana na anguko ambalo wamepitia. Kukosa miundombinu bora, kama kutegemea mvua badala ya kuwa na nyezo za umwagiliaji imekuwa inaathiri sana uzalishaji. Na hata pale kwa bahati nzuri kijana anapoweza kuzalisha vizuri, akifika sokoni bei inakuwa siyo rafiki kwake, anapata hasara na kushindwa kurudi tena shambani.

Kutengwa kwa maeneo ya kilimo na ufugaji ambayo yamewekewa miundombinu muhimu hasa ya upatikanaji wa maji ya uhakika itasaidia sana kwenye hili. Pia kufungua masoko hasa ya nje itampa kijana wigo mpana wa kuuza kile anachozalisha.

4. Sayansi na Teknolojia
Sayansi na teknolojia vinakua kwa kasi kubwa mno na hakuna anayeweza kuvizuia. Ukuaji huu wa kasi wa teknolojia umefungua fursa za vijana kuweza kujiajiri kwa urahisi kabisa kwa kutumia mtandao wa intaneti. Lakini kijana wa Tanzania bado anakutana na vikwazo vingi anapojaribu kutumia fursa ya teknolojia kujiajiri. Changamoto ya kwanza ipo kwenye urasimishaji wa biashara ambazo kijana anaweza kufanya mtandaoni akiwa hata nyumbani. Hilo linawafanya washindwe kukua kwenye biashara hizo na hata kupata huduma nyingine muhimu.

Changamoto nyingine kubwa ni kulipwa kutoka nje ya nchi. Teknolojia imerahisisha mtu kuweza kuuza huduma mbalimbali za kidijitali kwa mtu yeyote aliye popote duniani. Lakini kupokea malipo kutoka nchi za nje, jasa nje ya Afrika Mashariki ni kitu kigumu sana. Kuna mifumo ya kupokea malipo mtandaoni kama Paypal na Stripe, lakini haifanyi kazi kwa hapa Tanzania. Ni wakati sasa wa kufungua mifumo hii ya malipo ili vijana waweze kutumia teknolojia kuuza huduma zao na kupokea malipo popote duniani.

5. Elimu na Ubunifu
Mfumo wetu wa elimu pamoja na mapungufu yake mengi umeweza kuzalisha wahitimu wengi kwenye ngazi mbalimbali.
Kuna changamoto kubwa mbili zinazomkabili kijana kwenye eneo hili.

Changamoto ya kwanza ni kuhitimu huku akiwa hana uwezo wa kufanya chochote. Elimu yetu kwa sehemu kubwa imekuwa ni ya kukariri na kujibu mitihani. Vijana wanahitimu wakiwa na ufaulu mkubwa lakini hakuna wanachoweza kufanya. Ni wakati sasa wa kufanya mapinduzi kwenye mfumo wetu wa elimu, ili uzalishe vijana wenye uwezo wa kufanya vitu vyenye tija kwa jamii.
Elimu ikuze ubunifu wa vijana katika kuyatumia mazingira yao kuzalisha thamani zaidi kwao na kwa wengine pia. Iwajengaa kujitambua na kujiamini kwenye yale wanayofanya.

Changamoto ya pili ni mzigo mkubwa wa deni la elimu ya juu kwa wale waliopata nafasi ya kusoma elimu hiyo kwa mkopo.
Mikopo ya elimu ya juu imekuwa na msaada mkubwa, kwani wengi tusingeweza kugharamia elimu hiyo bila mkopo.
Lakini mkopo huo umekuja kuwa kikwazo kikubwa kwa kijana kujinasua kiuchumi.

Anayepata ajira anakatwa kiasi kikubwa kulipa deni hivyo hawezi kubaki na fedha ya kutosha kumwezesha kufanya shughuli za kiuchumi. Ambaye hajapata ajira deni lake linaendelea kukua zaidi na zaidi.

Mabadiliko yafanyike kwenye sera ya urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu ili impe kijana ahueni ya kuweza kushiriki shughuli nyingine za uchumi.

6. Ajira na Kujiajiri
Pamoja na kwamba serikali haiwezi kuwaajiri vijana wote, bado ina uwezo wa kutengeneza fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa vijana. Bado taifa lina uhitaji wa wafanyakazi na watoa huduma zaidi kwenye jamii zetu. Jamii bado haijapata wahudumu wa kutosha hasa kwenye sekta za afya na elimu.

Hivyo serikali inapaswa kuwekeza kwenye kuajiri vijana zaidi na kupitia kufanya hivyo inajenga nguvu kazi kubwa zaidi. Lakini pia serikali inapaswa kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kuweza kuwaajiri vijana wengi. Kadiri mazingira ya kibiashara yanavyokuwa mazuri, ndivyo sekta binafsi zinavyostawi na kutoa nafasi zaidi za ajira. Na kwa wale ambao wanakosa nafasi za kuajiriwa serikalini au kwenye sekta binafsi, wawe na mazingira mazuri ya kuweza kujiajiri wenyewe kama tulivyoona kwenye sekta mbalimbali hapo juu.

7. Uongozi na Usimamizi
Vijana wanahitajika sana kwenye nafasi mbalimbali za uongozi. Hili linaleta damu mpya kwenye uongozi lakini pia linatengeneza viongozi wazuri kwa ajili ya siku zijazo. Hakuna njia bora ya kujifunza kitu chochote kile kama kufanya. Hivyo vijana watajifunza uongozi kwa kupewa nafasi za uongozi. Kwa bahati mbaya sana kizazi cha sasa cha vijana kimepita kwenye vyuo vikuu ambavyo havijaweza tena kutengeneza viongozi kama zamani.

Serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu hazipo tena huru kama zamani, hivyo vijana hawajifunzi kuwa viongozi huru wanaofanya maamuzi yao wenyewe. Tunakokwenda tunatengeneza taifa la viongozi wasiokuwa na msimamo wao wenyewe hasa kwa maslahi ya taifa.

Kumekuwa na mabaraza ya vijana ndani ya vyana vya siasa, lengo lake yamekuwa ni kutengeneza viongozi. Lakini hayawezi kufanya vizuri kwa sababu ndani ya vyama vijana wanaegemea zaidi kwenye itikadi. Na hata kupata nafasi hauangaliwi uwezo, bali kuonekana na kujipendekeza.

Ni muhimu nafasi za uongozi na usimamizi zitolewe kwa vijana kwa kuangalia uwezo wao. Na siyo tu uwezo kwenye ufaulu wa kielimu, bali kuangalia mambo ambayo kijana ameweza kufanya mwenyewe bila ya kusimamiwa na yeyote.
Uwezo ukitumika katika kuwapa vijana uongozi, itawezesha kupata viongozi wazuri, na pia kuwajenga kuwa viongozi bora zaidi.

8. Viwanda na Uzalishaji
Hakuna nchi inayoweza kupiga hatua kiuchumi bila ya uzalishaji. Serikali imekuwa inaimba wimbo wa viwanda lakini mtazamo umekuwa zaidi kwenye viwanda vikubwa vinavyolenga wawekezaji kutoka nje. Nchi yetu inazalisha kila aina ya malighafi, lakini bidhaa nyingi tunaingiza kutoka nje. Kuna fursa kubwa ya vijana kuweza kujiingiza kwenye shughuli za viwanda na uzalishaji ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi.

Mambo yanayohitajika katika kuwezesha hili ni elimu ya uzalishaji na viwanda itolewe kwenye vyuo vyetu vya ufundi.
Mchakato wa kuanzisha kiwanda ufanywe kuwa rahisi hasa kwa wazawa ili kupunguza urasimu unaokuwa kikwazo kwa wengi.
Upatikanaji wa mitaji na miundombinu mengine muhimu kwa ajili ya viwanda. Sehemu kubwa ya bidhaa tunazoagiza nje zinaweza kuzalishwa hapa nchini na vijana kama wakiwekewa mazingira mazuri.

9. Afya na Ustawi
Bila afya ya vijana taifa haliwezi kustawi. Afya ndiyo mtaji wa kwanza na muhimu kabisa kwa maendeleo ya taifa. Vijana wana changamoto nyingi za kiafya, kuanzia afya ya uzazi, ulevi na uraibu, kushindwa kumudu gharama za afya na kukosekana kwa huduma bora za afya hasa maeneo ya vijijini.

Elimu ya afya ya uzazi na afya kwa ujumla inapaswa kutolewa kwa vijana ili wajue thamani ya afya zao na kujikinga na maradhi.
Elimu ya afya ya akili inapaswa kupewa kipaumbele kikubwa, kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa ya akili na ambayo hayashughulikiwi vizuri kutokana na watu kukosa uelewa wa magonjwa hayo.

Vilevi na madawa ya kulevya vinapaswa kudhibitiwa sana ili visiharibu nguvukazi ya taifa. Bima za afya kwa kila kijana ni muhimu ili kuweza kupata huduma za afya bila kuwepo kwa kikwazo cha gharama. Na huduma za afya zinapaswa kuwa bora kwenye kila eneo ili kijana aweze kuzipata pale anapozihitaji.

10. Tafiti na Maandiko
Kila kijana ambaye amefika elimu ya juu na kupata shahada, kuna utafiti amefanya. Lakini tafiti zote hizo huwa hazina manufaa yoyote kwa taifa. Zinachukuliwa kama sehemu tu ya mtu kupata shahada yake. Hili siyo sawa, taifa linahitaji tafiti nyingi mno ili kujua nini kinaendelea kwenye kila eneo na nini kinaweza kufanyika.

Tafiti zinasaidia sana kuweza kufanya maamuzi sahihi kwenye mambo mbalimbali. Vijana wanaweza kufanya tafiti na kuandika mambo yenye manufaa kwa taifa letu. Badala ya kuiga kila kitu kutoka kwa wengine, tunaweza kufanya tafiti kwa mazingira yetu na kujua kipi tunaweza kufanya na kikawa na tija. Uwepo wa takwimu sahihi zinazohusu vijana pia ni hitaji muhimu katika kupima maendeleo ya vijana na ufanisi wa hatua mbalimbali zinazochukuliwa.

Mfano kujua vijana wangapi wenye elimu za ngazi mbalimbali na taaluma mbalimbali, kujua wangapi wameajiriwa serikalini, sekta binafsi au kujiajiri wenyewe. Kujua wangapi wapo kwenye kilimo, teknolojia na sekta nyingine. Kwa kuwa na taarifa sahihi itasaidia kufanya maamuzi yenye tija kwa vijana.

Maeneo haya kumi yamegusa karibu kila eneo la maisha ya kijana na hata Mtanzania kwa ujumla. Tafiti zaidi zinahitajika kwenye kila eneo ili kuweza kufanya maamuzi bora na yenye tija kwa vijana na taifa.

Imani yangu kubwa ni vijana wakiwezeshwa kwa kujengewa uwezo wa kuweza kuzitumia fursa nyingi zilizo kwenye jamii zetu, taifa letu litanufaika kwa kiasi kikubwa mno. Taifa liwekeze kwa vijana, matokeo ya baadaye yatakuwa makubwa sana.

Kocha Dr Makirita Amani.
www.amkamtanzania.com
 
Addendum;
11. Sanaa na Michezo.
Hii ni sekta ambayo imebeba vijana wengi na inauwezo wa kutoa fursa kubwa za vijana kuajiriwa na hata kujiairi mwenyewe.
Iwapo sekta hii itapewa kipaumbele na vijana waliopo kujengewa uwezo pamoja na kupata hatimiliki na manufaa ya kazi zao, itakuwa mkombozi mkubwa.
 
12. Malezi Na Maadili.
Malezi na maadili ni eneo linalopaswa kupewa kipaumbele kwa vijana kwa sababu wapo wenye uwezo mzuri lakini wanapotea kwa kukosa malezi mazuri.
Kwa vile pia vijana wanaiga kile wanachoona kwa waliowatangulia ni muhimu misingi ya maadili kufundishwa kwenye kila ngazi na kuiishi kwa mfano ili vijana waweze kusimama imara.
 
Back
Top Bottom