Rais Samia Suluhu ana hofu ya Mungu hataki laana, tumsaidie

Kufuatia kifo cha Rais Magufuli, Rais mpya ameanza kutekeleza majukumu yake kusonga mbele. Rais mpya Mama Samia Suluhu Hassan ameonyesha nia yake njema na ya dhati kabisa kuendelea pale alipoachia Mtangulizi wake Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhakikisha anakamilisha miradi ya kimkakati na mipango yote waliyoanza na Marehemu Rais Magufuli kipindi hicho yeye akiwa Makamu wa Rais.

Katika kuhakikisha anatekekeza adhima hiyo, Mama Samia ameweka wazi kwa kile alichokisema kwamba miradi yote ya kipaumbele aliyotuachia Rais Magufuli pamoja na ile yote kuwa ni urithi wetu. Rais Mama Samia anasema ukifanya vibaya kwenye urithi Mungu anakulaani au aliyekuachia urithi anakuwa hana radhi nawewe na kwamba Mungu hatokuwa nawewe.

Rais Mama Samia alikazia kwa kuwaomba sana watendaji wote kwenda kuisimamia miradi hii mikubwa ya kipaumbele na kimkakati kwa nguvu zote kuhakikisha inakamilika na kuacha tabia ya kuchelewesha malipo kwenye miradi hii jambo linalokwamisha miradi yenyewe na kuifanya kuwa ya gharama kubwa kwasababu ya kuongezeka kwa riba ya kuchelewa kwa malipo kwa wakandarasi.

Ukimsikiliza Mama Samia anaeleza wazi kuwa hataki kupata kile alichokiita laana kwa kutokamilisha miradi hii mikubwa ya kimkakati na kipaumbele aliyoiita ni kama urithi aliotuachia Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli kwetu.

Na kwa kudhihirisha kwa vitendo kwamba Mama hataki hii laana ya kutokamilisha urithi wa hii miradi mikubwa tayali alimtuma Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa kwenda kwenye mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere la kuzalisha umeme kule Rufiji kuangalia na kufuatilia utekelezaji wake ambako alikuta mambo ni mazuri na kazi inaendelea.

Zaidi Mama Samia hakuchelewesha mambo na wiki iliyopita Jumapili Aprili 11 alisafiri mpaka nchini Uganda kukutana na Rais wa nchi hiyo Mzee Yoweri Museveni na kusaini nae mikataba ya utekelezaji wa mradi mkubwa kabisa duniani wa Bomba la kusafirishia mafuta ghafi lenye urefu wa Km 1,445 kutoka Hoima nchini Uganda mpaka Chongoleani mkoani Tanga ambao Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa uhai wake alitoa mchango na msukumo mkubwa katika utekelezaji wa mradi huo mkubwa kabisa duniani.

Zaidi Serikali yake kupitia kwa Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa imeeleza wazi mpango wake wa kuendelea kuliimarisha Shirika la ndege(ATCL) ambalo lilifufuliwa na Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhakikisha ndege zote 3 zilizobaki kuingia nchini zinaingia na Waziri Mkuu amethibitisha hiyo kwa kusema Serikali imekamilisha malipo ya ndege 3 zilizobaki na muda wowote zinatarajia kuingia.

Kwa mifano hii pekee na matamko aliyoyatoa Mhe Rais Mama Samia Suluhu ni dhahiri kabisa Mama hataki kabisa kile alichokiita mwenyewe laana kwa kushindwa kuitekeleza na kuimalizia miradi hii mikubwa ya kipaumbele na kimkakati aliyoitaja kama urithi.

Sasa hapa jukumu ni kwa watendaji na watumishi wote walioko ndani ya Serikali kuhakikisha wanamsaidia vyema Mama ili kukamilisha miradi na mipango hii yote aliyotuachia Marehemu ili tusije kupata kile alichokisema Mama kama laana kwa kutoendeleza urithi huu mkubwa ambao kwa mapana zaidi ina maslahi makubwa mno kwa maisha ya Watanzania wote na zaidi uchumi wa nchi yetu.

Kila mmoja kwa nafasi yake analo jukumu la kuhakikisha haya yote yanatekelezwa kwa kufanya yote yanayopasa kwenye nafasi na maeneo yao. Tumsaidie Mama. Rais wetu Mama Samia Suluhu ana nia njema kabisa na nchi hii na ndio maana kwa kipindi cha muda mfupi tu toka achukue mamlaka haya ameweza kutoa dira nzuri sana kwa nchi yetu na namna ya kwenda mbele zaidi baada ya jaribu hili kubwa na zito la kumpoteza Kiongozi wetu Mkuu wa nchi.

Watu wakafanye maamuzi, wakafanye kazi, wakatangulize uzalendo na maslahi ya watu na Taifa letu ili tumuepushe Mama na nchi yetu laana kama hatutotekeleza miradi hii ya urithi.

ASANTE JOHN
Ninakubaliana na Rais kwa hekima na Busara ya kuendeleza miradi hii, ni kweli kabisa Tanzania historia imetufundisha kitu kwa vile miaka ya 1970 hadi 1980 Mwalimu alianzisha na kukamilisha miradi mikubwa iliyofuatana na kuanzisha mashirika mengi kupelekea kuwepo na uchumi imara,lakini tuliitelekeza na kuitaifisha matokeo yake tumeanza upya.
 
Back
Top Bottom