Rais Samia ni Rais kamili, hamalizii Urais wa mtangulizi wake

Hamatan

JF-Expert Member
Nov 10, 2020
3,183
7,645
Kuna watu wanateseka, tena bila sababu. Wanataka tutembee katika upotofu. Hawataki kusikia kuwa utawala wa awamu ya Hayati Magufuli umekoma kwa namna mojawapo ya zile zilizotajwa na katiba.

Mnachotakiwa kujua ni kuwa kiongozi akiaga Dunia, hakuna utawala wala Serikali yake anayoiacha nyuma.

Serikali ya Mh. Rais Samia ni ya Awamu ya Sita. Kwa maelezo yao potofu wanataka iendelee kuwa awamu ya tano.

Watu hawa hawaelewi kinachotengeneza awamu. Awamu haitengenezwi na ilani bali inatengenezwa na jina la kiongozi mkuu.

Awamu ya kwanza ni ya Mwalimu Nyerere, wengine waliita awamu ya kwanza, japo wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere hata hilo neno awamu halikuwahi kutumika.

Awamu ya uongozi wa Mwinyi iliitwa ni awamu ya pili, kwa maana ya Rais wa pili. Imekwenda hivyo mpaka wakati wa awaku ya uongozi wa Magufuli.

Kwa sasa tuna Samia kama Rais wa 6. Hii ni awamu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Awamu inakuwa na Rais mmoja tu. Wapotoshaji wanataka awamu moja iwe na Viongozi wakuu wawili. Hawa wanaotaka hivyo, au wana dhamira ya kumtweza Rais Samia aonekane ni Rais nusu na kumkweza Marehemu aonekane aliikaimisha awamu ya utawala wake lakini aliendelea kuwa mtawala hata baada ya kifo. Na lengo lao kubwa ni kulinda ubinafsi wao.

Wanataka wasiondolewe kwenye nafasi walizowekwa na Hayati Magufuli maana waliwekwa na Rais kamili, hivyo wasiondolewe na Rais anayekaimu.

Hayati Magufuli ameondoka, hayupo Duniani, hana utawala wala Serikali yake aliyoiacha huku nyuma.

Aliyepo ndiye Rais. Ni Rais kamili, wala hakaimu nafasi ya marehemu. Na atawajibika kwa lolote chini ya utawala wake. Hakuna atakapojitetea kwa kumtaja marehemu.

Kiapo alichokila hakina tofauti na kile alichokila Mkapa, Mwinyi, Kikwete au Magufuli. Hakuapa kuwa anamalizia awamu ya marehemu au anakaimu Urais wa marehemu, bali aliapa kuwa Rais huku akiwa na mamlaka kamili ya Urais.

Awamu ya uongozi inaweza kwisha kwa kujiuzulu, kupigiwa kura na Bunge ya kutokuwa na imani, maradhi ya kutomfanya Rais kutekeleza kazi zake, kwisha kwa kipindi cha uchaguzi, kutochaguliwa tena baada ya miaka mitano au kwa njia ya kifo. Awamu ya Magufuli imehitimishwa na kifo. Huo ndio ukweli tunaotakiwa kuukubali. Hili ni jambo la kawaida kwa maisha yetu wana wa Adam. Uwe Rais, Meneja, Mwalimu Mkuu, Daktari wa Mkoa, ukiondoka Duniani, atakayekuja kuiziba nafasi yako, anakuwa kamili, hawi kaimu wa marehemu.

Katiba kuelekeza kusiwepo na uchaguzi wa kumpata Rais mwingine baada ya yule wa mwanzo kufariki kulilenga zaidi kuzuia uwepo wa ombwe la uongozi linaloweza kusababisha machafuko, na pia kuepuka gharama za uchaguzi wa nchi nzima. Kwa mfano mbunge akifariki, tunafanya uchaguzi mwingine, na anayekuja anakuwa mbunge kamili, hamalizii ubunge wa marehemu.

Hii ni awamu ya uongozi wa Samia, ukipenda unaweza kuita awamu ya sita, lakini kilicho sahihi kabisa ni kuwa ni AWAMU YA UONGOZI WA SAMIA SULUHU HASSAN. Tutaupima utawala wake kwa ukamilifu kwa sababu kwa kupitia katiba, tumempa utawala na mamlaka kamili, na wala hajajiegemeza kwa Hayati Magufuli. Atahukumiwa kwa yale yaliyotendeka katika utawala wake.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom