Rais Samia nakukumbusha kuwa siku hazigandi, zayoyoma. Samaki mkunje angali mbichi, akikauka hakunjiki

Mag3

Platinum Member
May 31, 2008
13,060
22,755
Rais wetu Mh. Samia Suluhu Hassan, ada ya mja hunena, mwungwana ni kitendo na siku njema huonekana asubuhi.

Wewe ni Rais wetu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliyoapa kuiheshimu, kuilinda na kuitetea.

Kupitia hiyo Katiba sisi wananchi tuliamua rasmi na kwa dhati kujenga jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani.

Mh. Rais, tarehe 29 Machi, 2021 uliapishwa kuliongoza Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar-es-Salaam.

Leo tarehe 9 Mei, 2021 ni siku ya arobaini toka ulipoapishwa na kuwa Kiongozi Mkuu wa taifa hili lenye watu karibia milioni sitini (60,000,000!)

Kama kiongozi matendo yako ni lazima yalete faraja na matumaini kwa Watanzania wote na kuhamasisha zaidi ushiriki wao katika hatma ya taifa.

Pamoja na kuapa kuiheshimu, kuilinda na kuitetea Katiba, epukana kabisa na matendo yanayoweza kutafsiriwa kwamba yanapingana na Katiba.

Mh. Rais kumbuka kauli huumba hivyo epukana pia na zile kauli ambazo zinaweza kutafsiriwa na wasaidizi wako kama ruhusa ya kuvunja Katiba.

Hali hii inahusu hasa yale maagizo yanayotolewa papo kwa papo bila kupima yatakavyopokelewa na watendaji wakuu wa vyombo vya dola.

Mh. Rais tuko wengi ambao kuapishwa kwako kulitupa japo faraja kutokana na mizengwe ya awali iliyokuwa ikifanywa na mahafidhina.
Amini usiamini asilimia kubwa ya wananchi bila kujali tofauti zao walipokea mabadiliko ya uongozi wa juu kabisa wa nchi kwa matumaini.

Yawezekana walisukumwa na sababu mbali mbali lakini lililowaunganisha ni uhitaji wa hewa safi kupitia dirisha ambalo ujio wako ungewafungulia.

Ni hilo dirisha lingewezesha kiapo chako kiwe na maana kwa kuturudisha kwenye utawala wa sheria unaoheshimu, kulinda na kutetea Katiba

Ingawa wengi tulikupokea bila kujali unatoka miongoni mwa watu wale wale na chama kile kile, tuliguna kidogo uliposema kazi iendelee.

Kiongozi bora hafuati tu nyayo za aliyemtangulia, hapana, huyo si kiongozi bora, ni mfuasi, kiongozi bora huvumbua njia salama wapite anaowaongoza.

Tafadhali Mh. Rais, acha kupaka ukuta rangi nyumba ipendeze huku msingi una nyufa; shughulikia kwanza msingi nyumba iwe imara na salama.

Tunayo Katiba ya mwaka 1977 lakini cha ajabu ni kuwa hata hii, pamoja na mapungufu yake, tunashindwa kuiheshimu, kuilinda na kuitetea!

Tunayo Rasimu ya Warioba lakini kwako Mh. Samia Suluhu Hassan, hata kuitaja tu imekuwa shida, shida ni nini? Je kuku wetu anataga kwenye miba?

Mwanga uliojitokeza unaanza kufifia ghafla huku safari hatujafika hata nusu, je kulikoni? Chukua hatua na katika kuidai Katiba mpya sahau suluhu.

Shughulikia sheria zote ambazo zinaisigina Katiba kwa namna moja au nyingine kwani tuna kiu kubwa ya utawala unaozingatia haki na usawa.

Ngoja Ngoja yaumiza matumbo na linalowezekana leo lisingojee kesho; kwa kweli baada ya miaka minne ya giza uvumilivu uko mashakani.
 
kitendo cha kutupa katiba pembeni kina nipa mashaka sana. Hata kama sio leo lakini haoneshi nia yoyote huko mbeleni
Anasahau kuwa mdharau mwiba mguu huota tende. Linalonipa wasi wasi ni kuwa anaonekana anaweza akasalimu amri kwa wale wadhalimu wa miaka yote waliotufikisha tulipo. Akithubutu hakuna suluhu, itabidi mapambano yaendeleee.
 
1. SGR

2. JNHPP -- Maporomoko ya Mto Rufiji....
Looo, nilikuona mahala nikadhani una kiasi cha uelewa wa mambo, kumbe uko hivi? Wewe bado ni mwanafunzi wa sekondari?

Kwa nini usitumie muda wako humu ukisoma na kujifunza namna ya kujadili hoja.

Umesoma yaliyoandikwa kwenye mada?

Sasa haya yanahusikaje na mada inayojadiliwa hapa! Unafanya udharaulike bure.
 
Katiba yenyewe ya sasa bado inavunjwa tu na viongozi wengine Kama spika ndugai. Sijui mpy ya nn. Waafrika tujifunze kwanza kuheshimu Sheria na katiba yetu.
 

Kuna watu wengine ni wazito katika kumsoma mtu. Wengine anaweza akakaa na mtu wiki au wiki mbili tu akakwambia huyo ni mtu wa aina gani na mwingine hata baada ya mwaka anakuwa hajamjua huyo mtu ni mtu wa aina gani. Mama kishasema yeye na dhalimu magufuli ni kitu kimoja huku akitoa kauli ambazo matendo yake ni SIFURI.

Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari.
Kuhusu kuheshimu na kuitetea katiba.
Kuhusu kutenda haki kwa vyama vya upinzani.
Sijaona ubaya wa Mama Samia mpaka sasa, lakini ni kama kuna watu hawawezi kuishi bila kumpa mtu lawama.
 
Katiba yenyewe ya Sasa bado inavunjwa tu na viongozi wengine Kama spika ndugai.Sijui mpy ya nn.Waafrika tujifunze kwanza kuheshimu Sheria na katiba yetu...

Cc Mag3 wewe Mag 3 kwanini unang’angania katiba mpya wakati iliopo inavunjwa na supika kama alivyosema mtoa mada au wewe unapenda nguo mpya tuu?
 
Back
Top Bottom