Rais Samia hachukuliwi poa kwa sababu ya jinsia yake. Kwani Mama Anna Makinda hakuwa Mwanamke?

MOSintel Inc

JF-Expert Member
Mar 24, 2016
812
585
Kumekuwa na minong'ono ya hapa na pale kuwa watu/wanasiasa Wengi wamekuwa waongeaji tofauti na ilivyokuwa katika utawala wa Magufuli, na kwamba sababu kuu ni kwasababu aliyepo madarakani ni mtawala mwenye jinsia KE. Just ambalo sikubaliani nalo kabisa.

Kwa Nchi yetu ya Tanzania si mara yetu ya kwanza kuwa na kiongozi wa mhimili mmoja wapo ambaye ana jinsia KE. Hapo awali ninyi ni mashahidi tumekuwa na spika wa bunge ambaye ni mwanamke, Spika mstaafu Mama Anna Makinda. Na wote mtakubaliana na Mimi kuwa; hakuna wakati mgumu kwa Spika mwenye bunge lililo changamka kama kipindi kile cha Anna Makinda. Ndicho kipindi ambacho bunge lilikuwa limesheheni wabunge vijana wasomi na wachambuzi wa mambo yanayoibua hoja za kitaifa.

Mtakubaliana nami kuwa ndicho kipindi ambacho yaliibuliwa mambo mengi ya ufisadi na bunge lilisimama kujadili pasipo kuonyesha nafasi yoyote ya upendeleo katika kuzuia mijadala. Anna Makinda alikuwa wa chama tawala, lakini haikuwahi kutokea hoja yoyote ya kusema kuwa:

"Anna Makinda ni mwanamke na sio Mwanaume kama Samuel Sitta, ndio maana wanamdharau".

Leo katika utawala huu uliopo madarakani umeanza kutetewa kuwa wale wanaoleta hoja zao kwasasa ambazo hawakuzitoa kwa utawala wa Magufuli, wanafanya hivyo kwakuwa aliyepo madarakani kwasasa ni Mwanamke. Ajabu sana.

Hoja ya Katiba na Tume huru ya uchaguzi sio hoja ambazo zimeibuka katika utawala wa wa sasa. Ni hoja ambazo zimekuwepo kwa kipindi kirefu tangu hata mchakato wa kuandika Katiba ya wananchi haujaanza. Kusema kuwa wanaodai Katiba kwasasa wanafanya hivyo kwakuwa wanamdharau mtawala wa sasa kwa jinsia yake, ni udhaifu mkubwa.

Na kama kweli kuna watu leo hii wanampima mtawala wa sasa kwa jinsia yake; basi watu hao yawezekana wamezaliwa mwaka huu na hakuna chochote walichojifunza kupitia uongozi wa Mama Anna Makinda bungeni.

Leo hii ukiniuliza ni Spika gani wa bunge unayemkubali tangu uanze kufuatilia mijadala ya bunge, nitakujibu ni Spika Mstaafu Mama Anna Makinda. Sitakujibu hivyo kwasababu ya jinsia yake, bali juu ya uwezo alio nao wa kiuongozi na kiutawala kwa anaowaongoza na kuwatawala bungeni. Kuna wakati alitawala, na kuna wakati aliliongoza bunge.

Kuna nyakati aliweka pembeni uspika na cheo chake na kuAct kama "Mama". Kuna wakati aliweka pembeni uChama wa chama chake CCM, na kuweka mbele maslahi ya Taifa lake. Na kuna wakati ali Act kama mtawala na kulinda heshima ya bunge. Ni kiongozi ambaye alimaliza wakati wake katika kuongoza mhimili wa bunge kwa mapungufu madogo sana. Alitengeneza na kuitunza heshima yake si kwa kushindana na akina Lissu, Lema, Msigwa, Mbowe au kafulila; Bali ni kwa kutoa nafasi kwa wabunge wote wenye nia njema na ustawi wa Taifa letu.

Kuna wakati alimtumia Lissu katika mambo ya Sheria. Kuna wakati alimtumia Zitto katika mambo ya uchumi. Kuna wakati aliwapa nafasi akina Kafulila na wabunge wengine katika kuibua ufisadi; tume zikaundwa na ripoti zikasomwa bungeni na mijadala yake kwenda mpaka masaa ya usiku, zaidi ya saa za kawaida za vikao vya bunge. Hakufanya hayo yote kwasababu alikuwa ni Mwanaume au Mwanamke. Alifanya hivyo kwasababu alivaa vazi la kitawala na kiuongozi katika kiti ambacho ni cha moja ya mihimili muhimu ya Taifa letu la Tanzania.

Hoja ya Katiba Mpya na Tume huru ya uchaguzi haijadiliwa sasa kwasababu ya mtawala aliyepo madarakani si wa jinsia ya kiume. Hoja hiyo imekuwa ikijadiliwa kwa muda mrefu ikiwa ni hitaji ambalo kizazi cha sasa kinaona kuna umuhimu wa kuwa na utaratibu mpya wa kisiasa, kiutawala, kiuchumi na kijamii, tofauti na ule wa mwaka 1977 unaotumika mpaka sasa. Swala la ni nani anataka Katiba Mpya si mjadala wenye mashiko. Kila anayehitaji maisha mapya yenye ustawi endelevu ndani yake , anahitaji Katiba Mpya. Na ni jukumu lake kuitafuta na kuipata Katiba hiyo bila kujali kuwa ni Mwanasiasa, Mwananchi, Mwanaharakati, Mwanasayansi au Mwalimu.

Niwatakie mwanzo mzuri wa mwaka 2022, tunapoumaliza mwaka 2021 salama. Katika mwaka huo tuendelee kuvumiliana, kuheshimiana na kupendana siku zote 366, huku tukiwaombea wepesi wale wote waliopo katika kuta za magereza pasipo na hatia yeyote ile. Kwaheri 2021.

Ahsanteni na mbarikiwe mno.

31.12.2021

Photo 1(credit:EATV) : Anna Makinda

Photo 2(credit: EATV): Sehemu ya maoni ya Watanzania kuhusu uongozi wa Anna Makinda bungeni.
images%20(15).jpg
Screenshot_20211231-170935.jpg
 
Back
Top Bottom