Rais Samia, anza na mambo haya kwa vijana. Tutakushukuru

chidy abidal

Member
Mar 4, 2015
6
4
Na; Hamis Abeid Baruani
0769808725


Mama kwanza pole na hongera kwa majukumu ya kulitumikia Taifa letu tukufu la Tanzania, kama kijana wako wa Tanzania nina maoni yangu kadhaa ningependa kukupatia kuhusu kutusaidia sisi vijana wako, mengi mazuri yalisemwa na uliyasema pale Mwanza naomba nami niongezee kidogo kwa kifupi kwa wenzangu waliyoyasema

1. FAO LA KUJITOA
Mama kutokana na kuwa na uhaba wa ajira serikalini vijana wengi wanafanya kazi za mikataba ya muda mfupi mfupi kwenye taasisi binafsi/mashirika n.k ili kuendesha maisha na kuenzi falsafa ya Mwl Nyerere ya "Ujamaa na Kujitegemea" hivyo mikataba ikiisha wanateseka kupata stahiki zao zote toka mifuko ya hifadhi za jamii punde mikataba yao inavyoisha na kupelekea pengine kuishi kwa tabu huku hela zao walizotolea jasho zikiwa zimehifadhiwa.

Mama hizi hela zikiwa zinatoka zote kwa mara moja kwa vijana wanao maliza mikataba yao sehemu wanazofanyia kazi zitawasaidia sana kuendesha miradi yao au kufungua biashara zao ambazo zitasaidia kuongeza ajira kwa vijana wengine na kuongeza kodi kwa Taifa tofauti na zikikaa hadi wafike umri wa kustaafu.

Mama kama ikionekana inafaa tunaomba hili jambo liangaliwe kwa jicho la huruma, na tutakushukuru mno.

2. 4% YA FEDHA ZA HALMASHAURI KWAAJILI YA MIKOPO KWA VIJANA

Mama mfumo uliopo sasahivi ni kikundi hadi kiwe na watu kuanzia watano na kuendelea, changamoto ya hapa ni hela inatoka kidogo ambayo haiendani na uwiano wa idadi ya watu kwenye kikundi mfano kikundi cha watu 12 wanapewa mkopo wa Milioni 5 kiukweli haisaidii na matokeo yake hela vijana wanagawana na kutumia kujikimu na kushindwa kurejesha.

Mama unaweza pata takwimu kubwa kuwa vikundi vingi vinapata hela hizo ila ukifatilia miradi yao inakuwa sintofahamu.

Kama ikikupendeza Mama iangaliwe namna idadi ya wana kikundi ipungue hadi watu wawili au hata mtu mmoja ambae atakuwa na wazo zuri ambalo linatekelezeka ambalo akipewa hela atafanya mradi na kuajili wengine au Halmashauri kusimamia hatua zote za awali za hilo wazo la huyo kijana na kumkabidhi kila kitu yeye aanze tu, Tutakushukuru mno Mama.

3. ROBO YA FAIDA ITOKANAYO NA MIRADI INAYOENDESHWA NA MIFUKO YA HIFADHI ZA JAMII IPELEKWE BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU
Mama katika hili naomba nieleze mambo mawili
i) Hizi hela zikiongezwa kule zitasaidia kama sio kupunguza tatizo la vijana kukosa mikopo basi litamaliza kabisa, tukichukua hii robo ya faida tukaiongeza kwenye hela inayotokana na bajeti ya serikali tutasaidia sehemu kubwa sana ila pia wazazi wa watoto wanaosoma vyuo watalipokea kwa furaha maana zile ni hela zao wanazochangia toka kwenye jasho lao hivyo kwenda kutumika kuwasomesha vijana wao itakuwa jambo jema sana Mama.

ii) Bodi ya Mikopo iunde kitengo kitakachokuwa kinahusika na kusaidia kiuchumi wanufaika wake waliomaliza chuo, bodi ya mikopo haipati hela nyingi kwasababu mdeni wake akiishamaliza chuo anamtelekeza hamjali tena wala hajui yuko wapi na atalipa vipi, hiki kitengo kisaidie kutambua wahitimu wenye mawazo bora na wanaohitaji msaada wa kifedha kutekeleza miradi yao alaf bodi iongeze mikopo kwa hao vijana ili wafanye miradi walipe deni lote na kunufaisha wengine tofauti na sasahivi ambapo bodi inategemea mtu hadi aajiriwe ndio wakakate hela.

4. YAUNDWE MADAWATI YA KUSHUGHULIKA NA KUENDELEZA VIJANA KWENYE MIRADI/KAMPUNI YAO

Mama hapa napenda kuongelea zaidi BRELA, SIDO na Halmashauri zetu.

i) BRELA wao wanasajili kampuni zote hivyo wanajua kampuni zote zinazoundwa nchini, dawati la vijana likiwepo litakuwa linaangalia kampuni/biashara zote zilizofunguliwa na vijana zinaendeleaje, changamoto zao, wapi wasaidiwe na wape waonyeshwe mwanga.

Mama, dawati hili likiwepo BRELA litasaidia kuokoa kampuni nyingi za vijana ambazo zinafunguliwa na kufa pengine tu kwa kukosa uangalizi na ushauri.

ii) SIDO nao wakiwa na dawati la vijana watakuwa wanafatilia ukuaji na ufanyaji kazi wa viwanda vyote vidogo vidogo vilivyoanzishwa na vijana wako Mama, hii itasaidia mno hivi viwanda vya vijana kuwa imara na kuongeza munkali ya kazi.

iii) Halmashauri hawa ndio wanatoa vibali kwenye maeneo yao endapo dawati la vijana likiwepo litakuwa linaangalia vibali vyote vilivyotolewa kwa vijana kama biashara zao zinafanyika, changamoto zao na wapi wamekwama hii itasaidia sana kuamsha vijana na kujituma.

5. KUUNDWA/KUBORESHWA KWA SERA YA KUJITOLEA (VOLUNTEERING & INTERSHIP) MAKAZINI
Mama kutokana na uhaba wa ajira vijana wengi wanafanya kazi nzuri na nzito sehemu mbali mbali ila malipo yao ni kiduchu au hawalipwi kabisa kwa kisingizio cha kujitolea au mafunzo kazini.

Mama sehemu hii imekuwa ikinufaisha makampuni/mashirika/watu kwasababu wanaona kuajiri sio tatizo tena maana vijana wa kujitolea ni wengi kutokana na uhaba wa ajira hivyo vijana hufanya kazi kunufaisha wengine huku wao maslahi yao yakiwa hafifu.

Mama tunatuweza punguza kodi kidogo kwa makampuni/mashirika yanayochukua vijana wa kujitolea na mafunzo kazini, hiyo kodi inayopungua isimamiwe na itumike kuwapa hawa vijana wawapo eneo hilo itumike kama hela ya kujikimu.

6. Kufanyiwa mapitio upya sera ya vijana ya Mwaka 2007.

7. Kuundwa kwa baraza la vijana la Taifa.

8. Kutambulika kwa shughuli zinazofanywa na vijana kuwa kazi rasmi kama udereva malori, mabasi, daladala, bodaboda pamoja na wauza chips n.k zitambulike kama kazi rasmi nao wapate stahiki zao kama bima ya afya n.k

Mama kwa leo naomba niishie hapa uendelee na majukumu mengine, nisikuchoshe Mama yangu.

wabillahi taufiq
Hamis Abeid Baruani
 
Back
Top Bottom