Rais Samia anaweza kuanzisha mkoa mpya wa Chato endapo haya yatazingatiwa…

Mama Amon

JF-Expert Member
Mar 30, 2018
2,021
2,477
1622623551034.png

Ummy Mwalimu, Waziri wa TAMISEMI, akiwa anatafakari juu ya muundo wa serilkali ya Tanzania Bara kuanzia Ikulu hadi Vitongojini.

Usuli

Mwongozo wa kuunda mikoa wa 2014 unataja vigezo hivi: idadi ya watu isiyopungua 3% ya watu wote nchini, changamoto za kijiografia zisizoweza kutatuliwa nje ya umoja wa kimkoa, uwepo wa miundombinu ya kiutawala itakayoruhusu mkoa mpya kutekeleza kazi zake, na ukubwa wa himaya ya usimamizi (jumla ya wilaya, tarafa, kata, vijiji, vitongoji na mitaa) unaoruhusu uongozi wa mkoa kutekeleza kazi zake kwa ufanisi na kwa kasi.

Nachunguza kiwango cha uzingatiwaji wa vigezo hivi katika pendekezo la kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Chato.

Kwa ajili hii andiko hili limegawanyika katika sehemu zifuatazo: utangulizi; hoja za kutea pendekezo la kuwepo kwa mkoa mpya wa Chato; mapingamizi dhidi ya pendekezo hili; majumuisho ya hoja husika; hitimisho na mapendekezo.

Hatimaye naonyesha kuwa, kama mjadala huu ukitazamwa kwa jicho la mchambuzi huru anayeelewa umantiki wa kanuni nne za kuunda mikoa za mwaka 2014, itathibitika kwamba pendekezo la kuundwa kwa mkoa mpya wa Chato linaweza kukidhi vigezo vyote vinee.


Hata hivyo, nitaungana na wachambuzi baki kupinga wazo la kuifanya wilaya ya Chato kuwa makao makuu ya mkoa huo.

Kusudi Rais aweze kutumia kanuni tajwa kufanya maamuzi sahihi, namwalika Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu, kuboresha mwongozo wa kuunda mikoa wa 2014 kwa kutaja bayana kiwango cha chini cha ukubwa wa himaya ya usimamizi katika ngazi za mikoa.

Kwa sasa kanuni ziko kimya juu ya jambo hili. Hazitaji kiwango cha chini cha idadi ya wilaya, vitongoji na mitaa kama mahitaji muhimu kabla ya kuamua uwepo wa mkoa. Hili ombwe linapaswa kuzibwa.

Utangulizi

Kwa mujibu wa ukurasa mmoja wa tovuti ya Wizara ya TAMISEMI inayoongozwa na Waziri Ummy Mwalimu, Tanzania Bara inayo mikoa 26, wilaya 139, na Halmashauri 185.

Aidha, katika ukurasa mwi
ngine ndani ya tovuti hii tunaambiwa kuwa kuna kata 3,956, vijiji 12,319, vitongoji 64,384, na mitaa 4,263.

Tangu mjadala kuhusu ombi la kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Chato uanze, tarehe 26 Mei 2021, kuna orodha ndefu ya hoja za kutetea ombi, kwa upande mmoja, na hoja za kupinga ombi hilo, kwa upande mwingine.

Hapa napendekeza kufanya usanisi wa hoja za pande zote mbili, katika mipaka ya taarifa nilizoziokota kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo mitandao ya kijamii.

Nafanya uchambuzi kwa kutumia mawazo ya
Profesa Tibaijuka, Askofu Bagonza, Askofu Niwemugizi, Baraza la Mashauriano la Mkoa wa Geita, Baraza la Madiwani la Geita, mchambuzi wa masuala ya kisiasa aitwaye Charles Makakala, na vyanzo vingine pia.

Mapendekezo ya waleta hoja (thesis)

Mpaka sasa nimebaini hoja sita za kutetea ombi hili:

Sababu ya kwanza ni kwamba, Kuenzi legasia ya hayati Magufuli, kwa kutekeleza miradi ambayo alitamani kuitekeleza wakati wa uhai wake.

Sababu ya Pili ni kwamba, kupunguza changamoto za kijiografia katika eneo husika kwa kupeleka huduma za utawala wa kimkoa karibu na wananchi wa wilaya za Chato, Bukombe, Kakonko, Biharamulo, Ngara, na baadhi ya Kata za Muleba, zitakazotumika kuunda mkoa mpya wa Chato.

Hoja hapa ni kwamba, kuundwa kwa mkoa mpya wa Chato utawasaidia wananchi wa wilaya husika kupata nguvu ya pamoja ya kiuchumi wasiyoweza kuwa nayo wakibaki nje ya mkoa mmoja unaopendekezwa.

Sababu ya Tatu ni kwamba, Kuundwa kwa mkoa mpya wa Chato, kunakidhi matakwa ya kanuni ya utawala kuhusu kiwango cha chini cha ukubwa wa himaya ya usimamizi katika ngazi ya mkoa kwa ajili ya kuleta kasi na tija.

Mkoa unaopendekezwa utakuwa na wilaya 5, tarafa 18, kata 87, vijiji 360. Taarifa niliozikusanya hazitaji idadi ya vitongoji vilivyomo katika eneo hili, lakini tuseme ni vitongoji X. Hii ni sawa na ukubwa wa himaya ya usimamizi yenye watendaji 465+X.

Mwongozo wa 2014 unataja vigezo vifuatavyo kama kiwango cha chini: angalau tarafa 15, angalau kata 45, na angalau vijiji 150. Mwongozo hautaji kiwango cha chini cha idadi ya wilaya wala kiwango cha chini cha idadi ya vitongoji vinavyotakiwa.

Tuseme kuwa kiwango cha chini cha wilaya zinazotakiwa kikanuni ni Y na kwamba kiwango cha chini cha vitongoji vinavyotakiwa kikanuni ni Z.

Hivyo, kwa mujibu wa mwongozo wa kikanuni, kiwango cha chini cha ukubwa wa himaya ya usimamizi katika ngazi ya mkoa unaopendekezwa ni watendaji 210+Y+Z.

Tofauti kati ya takwimu za Chato inayopendekezwa na takwimu zinazotajwa katika mwingozo wa kianuni ni 155+X-(Y+Z).

Kwa kuwa X ni kubwa kuliko (Y+Z), basi, 155+X-(Y+Z) ni namba chanya. Hivyo, kigezo cha kikanuni kuhusu ukubwa wa himaya ya usimamizi unaoweza kuleta kasi na tija katika ngazi ya mkoa kinazingatiwa.

Lakini, Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu, anapaswa kuhakikisha kuwa mwoingozo husika unatamka bayana kiwango cha chini cha vitongoji na wilaya kinachotakiwa ili uundwaji wa mkoa uweze kuhesabiwa ni halali kitarakimu. Hizi alijebra za 155+X-(Y+Z) hazileti afya kwenye masikio ya mtu wa kawaida.


Sababu ya nne ni kwamba, mkoa unaopendekezwa utakuwa na idadi ya watu zaidi ya 3% inayotakiwa na kanuni za 2014.

Kijiografia, Chato inayopendekezwa itakuwa na watu wasiopungua 1,557,139. KImahesabau, 3% ya watu milioni 50 wa Tanzania ni watu 1,500,000. Kwa hiyo, katika Chato inayopendekezwa kuna ziada ya watu 57,139 juu ya kiwango cha chini cha matakwa ya kikanuni.

Sababu ya tano ni kwamba, changamoto za kijiografia zilizomo katika wilaya zitakazounda mkoa mpya wa chato (milima, mabonde, visiwa na mapori) zinaonyesha kuwa ukosefu wa mkoa mmoja unaoziunganisha wilaya hizi ni kikwazo kinachozuia wanancho husika kushirikiana katika kujiimarisha kiuchumi.

Na sababu ya sita ni kwamba, tayari kuna maeneo kadhaa ya Biharamulo yanayofaa kuwa makao makuu ya mkoa mpya unaopendekezwa, kwani yana miundombinu ya kiutawala inayoweza kutumiwa na uongozi wa mkoa.

Mapingamizi dhidi ya pendekezo (antithesis)

Wakati kuna sababu sita za kuunga mkono pendekezo la mkoa mpya wa Chato, kuna mapingamizi matano nimeyaona:

Mosi, hoja ya kuenzi legasia ya hayati Magufuli, inapingwa kwa njia hii: Magufuli alikuwa ni binadamu; kila binadamu anayo mapungufu yake; kwa hiyo, matakwa yake yanaweza kuwa na dosari; matakwa yenye dosari hubainika kwa kuchambuliwa moja baada ya jingine; hivyo kila takwa la Magufuli linapaswa kuchunguzwa kivyake kabla ya kutekelezwa.

Pili, hoja ya kupunguza changamoto za kijiografia kwa kupeleka huduma za kiutawala karibu na wananchi wa wilaya za mkoa mpya inapingwa kwa maelezo yafuatayo:

Kwa upande mmoja, Wilaya ya Ngara iko umbali wa 300km kutoka makao makuu ya mkoa wake wa sasa; Biharamulo iko umbali wa 173km kutoka makao makuu ya mkoa wake wa sasa, na Kakonko iko umbali wa 284km kutoka makao makuu ya mkoa wake wa sasa.

Na kwa upande mwingine, wilaya ya Chato ambayo inapigiwa chepuo kuwa Makao Makuu ya Mkoa Mpya wa Chato, iko kwenye umbali wa 218km kutoka Kakonko na kwenye umbali wa 130km kutoka Ngara.

Hivyo, inadaiwa kuwa, inadaiwa kuwa, kupeleka makao makuu ya Mkoa Mpya katika mji wa Chato sio suluhisho la kikwazo cha umbali.

Wadau wanasema kuwa, kama umbali mrefu kati ya makao makuu ya mkoa na wilaya zake ndilo tatizo pekee, basi, Biharamulo au Nyakanazi ndiyo inapaswa kuwa makao makuu ya mkoa mpya wa Chato, na sio kwenye mji wa Chato.

Tatu, hoja kwamba kuundwa kwa mkoa mpya wa Chato kwa kumega mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita, kunatokana na matakwa ya kanuni ya utawala kuhusu ukubwa wa himaya ya usimamizi unaoweza kuleta kasi na tija huko Kagera, Kigoma na Geita, inapingwa kwa madai kwamba inaongeza mzigo wa himaya ya usimamizi wa kiutawala unaofanywa na Rais kwa kuongeza mikoa ya Tanzania Bara kutoka 26 hadi 27.

Nne, hoja nyingine ya kupinga kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Chato inasema kuwa mikoa itakayomegwa ili kuunda mkoa mpya wa Chato inaweza kufa kiuchumi kama ambavyo wanawake wenye mimba iliyotungiwa nje ya mji wa mimba (ectopic pregnancy) hufa pale mimba inapotolewa.

Kinachoongelelwa hapa ni rasilimali za kiuchumi kama vile ardhi, migodi, madini na biashara ya mpakani iliyoko mkoani Kagera, kwa mfano, itaondoka na kuhamia mkoa mwingine.

Tano, inadaiwa kuwa, kuugawa mkoa wa Kagera kwa kuondoa Wilaya za Ngara na Biharamulo na kuzipeleka kwengineko ni kuvunja umoja wa kimapokeo (tribal unity) uliokuwepo mkoani Kagera tangu karne ya 14 ukoo wa Bahima ulipovamia mkoa huu na kuunda utawala wa kichifu chini ya utamaduni mmoja.

Majumuisho ya hoja husika (synthesis)

Baada ya kupitia hoja za watetezi na wapinzani wa mkoa Mpya wa Chato hapo juu nimejiuliza swali moja la haraka:

Je, vigezo vya kikanuni katika mwongozo wa mwaka 2014 kwa ajili ya kuigawanya nchi katika kanda za kijiografia zinazoitwa mikoa vinasemaje kuhusu uwezekano wa kuundwa kwa mkoa mpya wa Chato?

Kama mjadala husika ukiangaliwa katika muktadha huu, mpaka sasa, kuna mambo yafuatayo ya haraka ambayo nimeyaona:

Kwanza, hoja ya kuenzi legasia ya hayati Magufuli imenyongwa hadi kufa. Sitaiongelea tena.

Pili, hoja ya mkoa mpya kama njia ya kupeleka huduma za kiutawala karibu na wananchi wa wilaya za mkoa mpya imenyongwa lakini haijafa.

Bado changamoto za kijiografia zilizoko katika wilaya za mkoa mpya zinashawishi wilaya hizo kuwekwa chini ya usimamizi wa mkoa mmoja.

Kwa hiyo, hata kama mji wa Chato sio mwafaka kwa ajili ya makao makuu, bado kuna sababu ya kutafuta eneo mwafaka kwa ajili hiyo.

Tatu, hoja ya idadi tosha ya watu kwa mkoa mpya wa chato na mikoa jirani yake imenyongwa hadi kufa. Idadi ya kikanuni inatimia.

Nne, hoja ya eneo la mkoa unaopendekezwa kuwa na miundombinu imara inayoweza kutumiwa na viongozi wa mkoa mpya wa chato imeshinda.

Tano, hoja kwamba kumega mkoa wa Kagera ni kuvunja umoja wa kikabila uliojengeka chini ya ukoo wa Bahinda haina mashiko hata kidogo.

Ukabila na utaifa ni pande mbili za shilingi ya nchi yetu. Tumekuwa tukiua ukabila ili kujenga utaifa kwa kutumia sheria za Bunge.

Kuna sheria ya kufuta uchifu, sheria ya ardhi ya vijiji inayofuta ardhi ya koo, sheria ya mtaala mmoja wa elimu, sheria ya lugha ya Taifa, na kadhalika. Utaifa una kipaumbele kikubwa kuliko ukabila.

Sita, hoja kwamba kumega mikoa kama vile Kagera ni kuudhoofisha mkoa kiuchumi ni dhaifu pia. Ni kweli kwamba katika orodha ya mchango wa kila mkoa kwa Taifa kutakuwa na maporomoko.

Lakini kitaifa hakuna athari yoyote kiuchumi, isipokuwa kama mkoa mpya unaoundwa ungekuwa unapelekwa nchi ya jirani.

Na saba, hoja kuhusu madai kwamba mapendekezo ya mkoa mpya wa Chato yanakidhi matakwa ya kanuni ya utawala kuhusu ukubwa wa himaya ya usimamizi unaoweza kuleta kasi na tija imeshinda.

Lakini, ufafanuzi wa kikanuni bado unahitajika ili kuipiga msasa hoja hii.

Kwa hiyo, natumia sehemu hii kuichunguza hoja hii kwa kina ili kuonyesha jinsi inavuoweza kuimarishwa.

Maneno “ukubwa wa himaya ya usimamizi” yanamaanisha “span of control” kwa Kiingereza. Na kuna aina mbili za himaya ya usimamizi.

Kwanza kuna himaya ya usimmaiz yenye wigo wa majukumu kuanzia juu kwenda chini, yaani “vertical span of control.” Hapa tunajiuliza, matakwa ya kanuni ya utawala kuhusu ukubwa wa himaya ya usimamizi unaoweza kuleta kasi na tija, ni kwamba mtendaji awe na ngazi ngapi za utawala chini yake?

Na pili, kuna himaya ya usimamizi yenye wigo wa majukumu unaoanzia kushoto kwenda kulia, yaani “horizontal span of control.” Hapa tunajiuliza, matakwa ya kanuni ya utawala kuhusu ukubwa wa himaya ya usimamizi unaoweza kuleta kasi na tija, ni kwamba mtawala awe na watu wangapi chini yake na wenye kuripoti kwake?

Mkuu wa Mkoa ni mteule wa Rais na anamwakilisha Rais katika kusimamia majukumu ya serikali mkoani, wilayani, tarafani, katani, kijijini, hadi kitongojini.

Hivyo, hapa, neno “mtawala” linapaswa kumaanisha Rais, mkuu wa mkoa (RC), mkuu wa wilaya (DC), Mtendaji wa Tarafa (DEO) Mtendaji wa Kata (WEO), Mtendaji wa Kijiji (VEO), na Mtendaji wa Kitongoji (KEO).

Kwa hiyo, maswali makuu mawili yanaibuka: Mosi, Matakwa ya kanuni ya utawala kuhusu ukubwa wa himaya ya usimamizi unaoweza kuleta kasi na tija, ni kwamba RAIS au RC au DC au WEO au VEO au MEO au KEO awe na ngazi ngapi za utawala chini yake?

Na pili, Matakwa ya kanuni ya utawala kuhusu ukubwa wa himaya ya usimamizi unaoweza kuleta kasi na tija, ni kwamba RAIS au RC au DC au WEO au VEO au KEO awe na jumla ya watu wangapi chini yake na wenye kuripoti kwake?

Maswali haya yanaweza kujibika kwa kutumia ushahidi wa kinadharia (theoretical evidence) au ushahidi mbashara (empirical evidence), au vyote kwa pamoja.

Kwa mujibu wa matini niliyopewa na mwalimu wangu wa somo la Utawala na Uongozi maswali mawili hapo juu yanaweza kujibiwa kwa kutumia fomula za kinadharia zilizobuniwa na kina V.A. Graicunas pamoja na Ralph C. Davis.

Wataalam hawa wanasema kuwa, kwa wastani, ukubwa wa himaya ya usimamizi kuanzia juu kwenda chini ni watendaji 5-10. Ni vivyo hivyo kwa ukubwa wa himaya ya usimamizi kuanzia kushoto kwenda kulia.

Kuanzia Ikulu hadi kwa mtendaji wa mtaa ni kama kuna ngazi saba za utawala, yaani: Rais, mkuu wa mkoa (RC), mkuu wa wilaya (DC), Afisa Tarafa (DEO), Mtendaji wa Kata (WEO), Mtendaji wa Kijiji (VEO), Mtendaji wa Mtaa (MEO)/Mtendaji wa Kitongoji (KEO).

Ukubwa wa wigo wa majukumu ya usimamizi kuanzia juu kwenda chini unategemea mambo kadhaa kama vile: umahili wa wasaidizi wa bosi; kiwango cha mahitaji ya weledi wa kupanga kazi kuhusiana na nafasi husika; kiwango cha kasma ya madaraka inayotolewa kwa ngazi za chini na kueleweka katika ngazi hizo; uwepo wa miongozo, miiko na viwango rasmi ya utendaji wa kazi kwa watendaji husika, uwepo wa mazingira yanayoruhusu mawasiliano yenye kasi na tija, na kiwango cha mgawanyo wa majukumu unaohitajika kulingana na utofauti wa kazi zinazofanyika.

Kwa mujibu wa takwiku za 2014 nilizozipata mtandaoni, Tanzania Bara inao ma-RC 26, ma-DC 139, ma-WEO 3,337, ma-VEO 12,423, ma-MEO 3,741 na ma-KEO 64,616.


Mchoro: Muundo wa Uongozi wa Serikali ya Tanzania ukionyesha mfumo wa mawasiliano

Kwa hiyo, wigo wa majukumu ya usimamizi uko kama ifuatavyo: Ngazi ya Rais inasimamia watu 26; kila mkoa unasimamia wastani wa watu 6; kila wilaya inasimamia wastani wa watu 24; kila kata inasimamia wastani wa watu 4; na kila kijiji inasimamia wastani wa watu 6.

Je, kwa mujibu wa takwimu hizi, kanuni ya himaya ya usimamizi kuanzia juu kwenda chini inazingatiwa? Kwa maoni yangu, jawabu ni “ndiyo.”

Na je, kanuni ya himaya ya usimamizi kuanzia kushoto kwenda kulia inazingatiwa? Kwa maoni yangu, jawabu ni “ndiyo” kwa ngazi za mkoa, kata na kijiji. Lakini, jawabu ni “hapana” kwa ngazi za Taifa na wilaya.

Katika ngazi ya wilaya, dawa yaweza kuwa ni kupunguza wigo wa usimamizi kutoka watu 24 hadi tuseme watu 10 kwa kuongeza idadi ya wilaya hadi 350. Wilaya 350 zinamaanisha kuwa wigo wa usimamizi katika ngazi ya mkoa umekuwa watu 14, ambayo ni zaidi ya wastani.

Hii maana yake ni kwamba katika ngazi ya mkoa, tunalazimika kupunguza wigo wa usimamizi uliojitokeza kutoka watu 14 hadi tuseme watu 10 kwa kuongeza mikoa 9, na hivyo kuwa na mikoa 35.

Na katika ngazi ya Taifa tutalazimika kupunguza wigo wa usimamizi uliojitokeza kutoka watu 35 hadi tuseme watu 7 kwa kuunda Kanda 5 za kiserikali.

Kanda hizi tano zinaweza kusimamiwa na Wakuu wa Kanda Watano au Makatibu Wakuu Watano ndani ya TAMISEMI. Nimewahi kusema kuwa TAMISEMI ni dude kubwa lenye kuhitaji makatibu wakuu wengi.

Hitimisho na mapendekezo

Kwa sasa, mwongozo wa kuunda mkoa unataja vigezo vifuatavyo kuhusiana na kiwango cha chini cha ukubwa wa himaya ya usimamizi ya RC: angalau tarafa 15, angalau kata 45, angalau vijiji 150, lakini bila kusema lolote kuhusu idadi ya vitongoji.

Ni muhimu mwongozo huu ukamilishwe kwa kuondoa pengo hili kusudi kuiwezesha serikali kujua kwa uhakika ukubwa wa himaya ya usimamizi kuanzia ofisi ya RC kwenda chini.

Marekebisho haya yakifanyika yatawapa WDC, DCC na RCC msingi thabiti wa kutambua wigo wa himaya ya usimamizi na kutoa mapendekezo ya kitakwimu kwa Rais kwa kuonyesha ni RC gani anao wigo mkubwa na RC yupi anao wigo mdogo wa usimamizi.

Ni katika mazingira haya, Rais Samia atakuwa na sababu nzuri ya kikanuni katika kuamua ama kuunda mikoa mipya, ukiwemo mkoa mpya wa Chato, au vinginevyo.

Hivyo, Waziri Ummy Mwalimu afanye hima kuweka bayana ukubwa wa himaya ya usimamizi kwa kila RC.

Kwa sasa hatuna jawabu kwa swali lifuatalo kutoka kwa Waziri wa TAMISEMI: Kama tukijumlisha ma-MEO, ma-KEO, ma-VEO, ma-WEO, ma-DEO, na ma-DC, ukubwa wa himaya ya usimamizi (span of control) kwa kila RC hapa nchini Tanzania ni timu ya watendaji wangapi?

Jawabu la swali hili linahitaji takwimu za wilaya, tarafa, kata, vijiji, vitongoji na mitaa.

Lakini, dalili zote zinaonyesha kuwa upatikanaji wa takwimu sahihi za mitaa, vitongoji, vijiji, kata na tarafa utampa Rais Samia sababu ya kikanuni ya kuunda mikoa mipya, ama kwa kuigawanya baadhi, au kuiunganisha baadhi, au kwa kuifumua na kuifuma upya baadhi.

Mapendekezo ya mkoa mpya wa Chato niliyoyaona yanaweza kuhalalishwa na kanuni ya utawala inayohusu kwango cha chini cha ukubwa wa himaya ya usimamizi.

Kanuni za utawala na uongozi ninazozifahamu zinamruhusu kufanya hivyo hata bila kusubiri Katiba mpya.

Hata hivyo, kulingana na hoja za wadau nilizoziona, kama mkoa mpya wa Chato utaundwa haiytakuwa sawa kuweka makao yake makuu wilayani Chato.
 
Hawa ndio wasomi wetu hawana hoja kabisaa weupee pee hii ndio shida ya kukariri
Ni hoja za kisomi,lakini sie akina kapuku la saba B tunaangalia ramani ya Tanzania kuona ni eneo gani kubwa.

Tumeangalia mkoa wa morogoro tukaona mkoa wa geita unaotaka kumegwa unaingia mara mbili na nusu.

Kwanini isiwe morogoro maana ni kubwa sana mwenye ramani ya Tanzania atuwekee.

Hiyo mnaita regasi sijui nini,nani mwenye regasi Kati ya magufuli na mwalimu?basi butiama iwe mkoa kuenzi regasi ya babu.
 
Umechambua kisomi big up ila hitimisho mkoa mpya uitwe biharamulo na makao makuu yawe biharamulo. Kama ni ishu ua jina chato.mkoa wa Geita uitwe Chato.
 
Huo mkoa mpya wa Chato unalazimishwa tu kuwepo, lilikuwa ni wazo binafsi la Magufuli kwa utashi wake ila kama ulivyosema pale juu nae alikuwa binadamu ana weakness zake, tatizo naloliona hapa ni Rais kutaka kulazimisha kuenzi kila aliloanzisha mtangulizi wake hata kama kwa kufanya hivyo hapatakuwa na tija kwa umma wa watanzania.

Ningependa Samia aendeleze mambo kama ujenzi wa miundombinu aliyoanzisha Magufuli kwasababu imeshakula pesa za walipa kodi na haitakuwa vizuri kuiacha nusu, mfano. SGR na Stigler's yenye tija kwa watanzania muhimu ikamilishwe, lakini hilo la kulazimisha mkoa mpya wa Chato tena kwa "kupora" baadhi ya wilaya toka mikoa mingine ya jirani liachwe.

Mapendekezo ya kupinga hoja kwa mtazamo wangu yamekuwa na nguvu zaidi, mikoa tuliyonayo inatosha, muhimu sasa serikali ihakikishe inawekeza zaidi kwenye upatikanaji wa uhakika wa huduma bora za jamii, ikiwepo maji safi na salama kila wilaya nchini, kuliko serikali iendelee kujibebesha mzigo kwa kuanzisha mkoa mpya.
 
Mama Amon,

Kama nimekuelewa haya ndio mapendekezo yako.

1. Kuundwa kwa KANDA 5 za kiutawala.

2. Kuundwa kwa mikoa mipya 9 na kufanya jumla ya mikoa kuwa 36.

3. Idadi ya wilaya iwe 350 toka wilaya 136 zilizopo sasa hivi.

Maswali:

1. Hii mikoa mipya 9 utaipata kwa kugawa mikoa gani iliyoko sasa hivi?

2. Kanda 5 ulizopendekeza zitajumuisha maeneo / mikoa gani?
 
Hongera Mtoa mada. Upo vizuri sana. Tusubiri busara na hekima za Viongozi kwa sababu wana mamlaka kubwa sana. Si lazima watekeleze Mawazo yetu.

Binafsi siungi mkono hili suala. Na kwa busara ya kawaida yafaaa wananchi wote wa mikoa husika na hata tz yote tupige kura kuridhia hili suala kwa sababu linaenda kutuongea mzigo mpyaaaa wa Matumizi yasiyo ya lazima na lawama za kupeana vyeo kwa kujuana.

Ningalikuwa nasikilizwa, joja ingezimiwa kwenye bia tu, tamisemi wabebeshwe zigo liwe kwenye yatokanayo kwenye vikao mbaimbali mwishowe homa ifungwe maisha yaendeleee. Wakomae na kumalizia hilo daraja la busisi, SGR na huo umeme wa Mwl. Nyerere
 
Huu ni UPUUZI unaofanyika Tanzania labda na nchi nyingine chache za Kiafrika. Nchi za majuu hakuna UPUUZI huu wa kuwaongezea mzigo mkubwa walipa kodi usio na tija yoyote ile zaidi ya kuongeza gharama kubwa za uendeshaji. Huwezi kusikia leo hii jimbo la California au Florida limekuwa kubwa sana hivyo ligawaywe na hivyo kutoa majimbo mengine mawili au matatu.

Ukiwauliza wahusika wote kama kuna TATHMINI yoyote iliyofanywa katika mikoa hiyo iliyomegwa na Mikoa mipya iliyoongezwa imeboresha vipi maisha ya Watanzania katika mikoa husika hakuna atakayejibu kwa ufasaha zaidi ya kung’aa macho lakini pamoja na kuwa hakuna TATHMINI bado wanaendelea KUKURUPUKA kila miaka michache na huu UPUUZI wao wa kuwabebesha walipa kodi gharama ambazo hawazinufaishi kwa namna yoyote ile.
 
Maswali:

1. Hii mikoa mipya 9 utaipata kwa kugawa mikoa gani iliyoko sasa hivi?

2. Kanda 5 ulizopendekeza zitajumuisha maeneo / mikoa gani?
Najibu kwa kama ifuatavyo:

Swali la 1: Hii mikoa mipya 9 utaipata kwa kugawa mikoa gani iliyoko sasa hivi?

Jawabu la 01:Mikoa mikubwa inayoweza kugawanywa ni kama vile Morogoro, Lindi, Singida, Mbeya, Rukwa, na Tabora. Jambo muhimu hapa ni kwamba, katika ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa, lazima uamuzi wa kiutawala kwanza ufanyike kuhusu ukubwa wa wigo wa majukumu ya usimamizi ambao unaweza kuleta tija na kasi stahiki.

Swali la 2: Kanda 5 ulizopendekeza zitajumuisha maeneo / mikoa gani?

Jawabu la 01: Ukiangalia Tanzania ya leo, tayari kuna kanda za kiutawala. Kwa mfano, kuna Kanda za TRA, BIMA, OSHA, NEMC, nk. Mimi napendekeza kanda zifuatazo: (1) Kanda ya Kati, (2) Kanda ya Kaskazini Magharibi, (3) Kanda ya Kaskazini Mashariki, (4) Kanda ya Kusini Mashariki , na (5) Kanda ya Kusini Magharibi.
 
Kwanini sisi Tanzania,Afrika ndio tunaona haja ya kuongeza maeneo ya kiutawala kama ndio silver bullet ya matatizo ya wananchi, kuwapa wananchi huduma Za maji, afya, Elimu, ajira huitaji kuongeza manyampara,ongeza viwanda, Miundombinu.

Mara ya mwisho USA imeongeza jimbo kwa kumega jimbo jingine ni lini!? Nchi hii inabidi tupunguze wilaya,mikoa,kata,majimbo ya ubunge yawe 100 tu,wizara ziwe 15.

Tujenge viwanda, tufsnye kilimo, tuwe na huduma za afya bora, Watumishi wa umma ni wengi mpaka wanaiba mchana kweupee na hawafanywi kitu.
 
Huu ni UPUUZI
1. Kamusi Kuu ya Kiswahili (BAKITA 2015, Toleo la 2) inasema kuwa "upuuzi" ni "jambo la kipumbavu lisilo na maana," na "upumbavu" ni "tabia au hali ya kufanya mambo yasiyokuwa na maana kutokana na udhaifu wa akili."

2. Bandiko hili limejenga hoja yenye kuanzia kwenye kanuni rasmi za utawala na uongozi (principled argument), kanuni ambazo zinafahamika na kukubalika kwa watu wote wenye akili timamu, yaani watu wasio na udhaifu wa akili.

3. Kwa hili, hoja ya bandiko hili inaweza, na inapaswa kujibiwa kwa kuleta hoja mbadala yenye kuanzia kwenye kanuni asmi za utawala na uongozi (an alternative principled argument), badala ya kutumia maneno yasiyo na uwezo wa kubomoa hoja iliyo mbele yetu.

Jaribu tena.
 
Nchi hii inabidi tupunguze wilaya,mikoa,kata,majimbo ya ubunge yawe 100 tu,wizara ziwe 15, Tujenge viwanda,tufsnye kilimo,tuwe na huduma za afya bora, Watumishi wa umma ni wengi mpaka wanaiba mchana kweupee na hawafanywi kitu.
Mtu ambaye amewahi kufanya kampeni za ubunge katika majimbo ya mikoani kama kule Tabora na Shinyanga hatakubaliana na hoja yako ya kupunguza wabunge.

Mtu ambaye amesafiri kwa gari na kuizunguka Tanzania hatakubaliana nawe kuhusu habari ya kupunguza mikoa na wilaya.

Pia, wazo la kupunguza Wizara linahotaji kujengewa hoja. Kwa sababu ya ukubwa wa nchi, muundo wa serikali umeunganisha geographical, functional and matrix departmentation principles.

Ni katika mazingira haya unapaswa uonyeshe ni wapi kupunguzwe na kwa vipi. Kutamka tu hakuna msaada.
 
Naam ndiyo kusudio langu kuonyesha hii ya KUKURUPUKA na kugawa Mikoa bila ya kuwepo na TATHMINI ya kina kuonyesha hiyo mikoa iliyomegwa na mipya Wananchi wa Mikoa hiyo WAMEFAIDIKA vipi na zoezi hili kwa maisha yao kuboreshwa, vipato vyao kuongezeka etc.

Bila kuja na TATHMINI ya kina basi narudia tena sera hii ni UPUUZI MTUPU! Miaka 60 ya uhuru lakini Serikali inajiita eti ni “Serikali ya Wanyonge” miaka 60 ya chama kimoja madarakani iweje hadi hii leo kuna Watanzania Wanyonge ndani ya Nchi yao huru!? Sera kama hizi za KIPUUZI ni moja ya sababu nchi hii katika kila Sekta haina chochote ambacho Watanzania tunaweza KUJIVUNIA.

GARBAGE IN GARBAGE OUT!

1. Kamusi Kuu ya Kiswahili (BAKITA 2015, Toleo la 2) inasema kuwa "upuuzi" ni "jambo la kipumbavu lisilo na maana," na "upumbavu" ni "tabia au hali ya kufanya mambo yasiyokuwa na maana kutokana na udhaifu wa akili."...
 
Miaka 60 ya uhuru lakini Serikali inajiita eti ni “Serikali ya Wanyonge” miaka 60 ya chama kimoja madarakani iweje hadi hii leo kuna Watanzania Wanyonge ndani ya Nchi yao? Sera kama hizi za KIPUUZI ni moja ya sababu nchi hii katika kila Sekta haina chochote ambacho Watanzania tunaweza KUJIVUNIA. GARBAGE IN GARBAGE OUT!
Unayoyaandika hapa yanakutia hatiani kwa kutumia kanuni ya GARBAGE IN GARBAGE OUT. Dhana ya "serikali ya wanyonge" ni zao la Katiba ya Tanzania (1977), ibara ya 9(i).

Kwa mujibu wa ibara hii, jukumu la serikali ni kuratibu upatikanaji wa maslahi ya pamoja kwa ajili ya kuwainua wanyonge walio katika makundi matatu: wajinga, wagonjwa na maskini.

Siku wanyonge wakiisha, hata serikali itakosa uhalali. Kwani, kama kila kaya inaweza kujenga shule yake, hospitali yake, barabara yake, jeshi lake, mahakama yake, serikali haina sababu, mahakama haina sababu, bunge haila sababu.

Mabandiko yako mengi yanaonyesha kuwa unao welewa mkubwa juu ya masuala ya kitaifa, isipokuwa kuhusu hili suala la constitutionally warranted political philosophy .

Kwa kuandika haya umejiweka kundi moja na wabunge kama vile Musuka na Conchesta Lwamulaza waliomsimanga Makamu wa Rais, Phillip Mpango, eti kwa kuwa anajinasibisha na "serikali ya wanyonge."

Nimekushangaa sana.

1622631724597.png
 
Uundwaji wa mikoa mipya nchini, faida yake ni kubwa ukilinganisha na hofu za uanzishwaji wa mikoa hiyo, ni kuwasogezea wananchi huduma karibu

Gharama za kiuendeshaji, Mimi Naamini serikali inaweza, Kwa kuwa serikali hupoteza fedha nyingi Sana kutokana na Matumizi yasiyoyalazima, kama posho zisizo na tija na wizi uliokithiri serikalini.

Tena ikiwezekana, mikoa iongezwe Kwa kila mji inayokidhi kupewa hadhi ya mkoa.
 
Kwa hiyo kuwepo Wanyonge ndiyo uhalali wa kuwepo Serikali!!!!! 😂😂😂😂😂😂😂

Nashukuru sana kwa Compliments 🌹🙏🏾
Unayoyaandika hapa yanakutia hatiani kwa kutumia kanuni ya GARBAGE IN GARBAGE OUT. Dhana ya "serikali ya wanyonge" ni zao la Katiba ya Tanzania (1977), ibara ya 9(i).

Kwa mujibu wa ibara hii, jukumu la serikali ni kuratibu upatikanaji wa maslahi ya pamoja kwa ajili ya kuwainua wanyonge walio katika makundi matatu: wajinga, wagonjwa na maskini.

Siku wanyonge wakiisha, hata serikali itakosa uhalali. Kwani, kama kila kaya inaweza kujenga shule yake, hospitali yake, barabara yake, jeshi lake, mahakama yake, serikali haina sababu, mahakama haina sababu, bunge haila sababu.

Mabandiko yako mengi yanaonyesha kuwa unao welewa mkubwa juu ya masuala ya kitaifa, isipokuwa kuhusu hili suala la constitutionally warranted political philosophy . Nimeshangaa sana.
 
Back
Top Bottom