Zanzibar 2020 Rais Mwinyi amuapisha Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar. Maalim Seif asema haukuwa uamuzi rahisi

Replica

JF-Expert Member
Aug 28, 2017
1,444
7,808
Kutoka Zanzibar, maandalizi yameshakamilika kwa ajili ya kumuapisha Makamu wa kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad kutoka chama cha ACT-Wazalendo. Kuwa nami kukujuza yatakayojiri kutoka visiwa hivi vya karafuu punde kutoka sasa.

PIA, SOMA=> Rais Dkt. Mwinyi amteua Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

==========

6:00 Mchana: Wageni wameshawasili na anaesubiriwa kwa sasa ni Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi. Miongoni mwa waliofika kwenye hafla hii ni kiongozi mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe pia makamu wa kwanza wa Rais anaesubiri kuapishwa, Maalim Seif.

6:11 Mchana: Rais wa Zanzibar ameingia ukumbini na Maalim Seif amekabidhiwa na kuapa kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa katiba.

Maalim.jpg

MAALIM SEIF: Mheshimiwa Rais, kwa upande wetu uamuzi wa kuingia katika serikali, baraza la wawakilishi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haukuwa uamuzi rahisi na mwepesi.

Ulikuwa ni uamuzi uliotufikirisha sana, tumejadili sana na tumepishana sana hatimaye tukafikia uamuzi. Moja ya sababu iliyotufanya kufikia uamuzi huo ni imani yetu kwako wewe binafsi, maneno yako, vitendo na ishara zako ambazo zimetushawashi kuwa unayo nia njema na dhamira safi ya kututoa tulipokwama na kuibadilisha Zanzibar yetu katika nyanja zote.

Tumeona wewe ni mtu tunaeweza kufanya nae kazi, tumeweza kusikilizana na tunaweza kukupa nafasi uthibitishe nia yako njema mabyo ndio iliyotufanya sisi tutangulize nchi kwanza licha ya madhila yote yaliyojitokeza katika uchaguzi uliopita.

Wenzangu walipokuja na wazo hili la sisi kuungana na wewe na baada ya kushikiana na wanachama wetu, niliwashauri kuwa sasa ni wakati wangu mimi kupumzika na kupeleka jina la damu mpya, hawakunikubalia, waliniambia wewe ndio ulioongoza maridhiano na Rais Amani Abeid Karume mwaka 2009 na ndie ulishiriki serikali ya kwanza ya umoja wa kitaifa na Rais wa wakati huo, Dkt. Ali Mohammed Shein.

Serikali ya umoja wa kitaifa na katiba ya Zanzibar ilikusudiwa kuwa chombo cha kusimamia, kuratibu na kuongoza juhudi za wazanzibari katika maridhiano na umoja wa kitaifa.

Haikuwa na bado sio leongo la serikali ya umoja wa kitaifa kuwa chombo cha kugawana vyeo kwa kambi za kisiasa, ni vyema jambo hili tukalikumbuka kila wakati.

Katika kuwasaidia wale wenye imani na ufahamu potofu juu ya serikali ya umoja wa kitaifa, napenda kutumia mfano rahisi, serikali ya umoja wa kitaifa ni sawa na chombo cha usafiri, kwa msafiri yeyote, awe wa baharini, angani au nchi kavu. Lengo lake sio kuingia katika meli, ndege au gari, lengo lake ni kufika safari aliyoipanga.

Safari ya wazanzibari ni maridhiano ya kweli, mshikamano na umoja wa kitaifa. Chombo chetu cha kufika safari hiyo kwa wakati ni serikali ya umoja wa kitaifa hivyo ni wajibu wa viongozi sote ambao tumepewa jukumu la kuongoza serikali kuhakikisha kwamba tunaitekeleza au tunakifanikisha chombo hiki katika safari yetu hiyo.

********
RAIS MWINYI: NATARAJIA TUTAWEKA PEMBENI TOFAUTI ZETU KUIJENGA ZANZIBAR
-
Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi amesema yeye ni muumini wa Umoja wa Kitaifa, mshikamano, udugu na maridhiano akiamini ni njia nzuri ya kujenga umoja na ustawi wa nchi.
-
Amesema maridhiano ya kweli yanajengwa kwa Dhamira, Uvumilivu na Kuaminiana akiongeza kuwa, Viongozi hawana budi kufahamu maslahi ya wananchi ndio jambo la msingi.
-
Ameongeza, tofauti zao zisiwe kikwazo cha maendeleo huku akihimiza wananchi wote kuwa kitu kimoja na kuunga mkono juhudi hizo zinazolenga kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Rais Mwinyi: Maridhiano ya kweli yanajengwa na mambo makuu matatu.

1. Dhamira ya kweli 2. Kuvumiliana, kustahimiliana na kusahau yaliyopita 3. Kujenga utamaduni wa kuaminiana.

Mafanikio ya Maridhiano yatategemea Wananchi kuzipa kisogo tofauti zetu. Mimi na Seif tumeridhiana.

==============

Hotuba ya Maalim Seif Sharif Hamad

=============
_________________________________________________________________
Mhe Dkt Hussein Ali Hassan Mwinyi,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Waheshimiwa Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali na
Waheshimiwa Wananchi wa Zanzibar,

Mheshimiwa Rais,
Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyenzi Mungu muumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake kwa kutuwezesha kukutana hapa kwa salama na amani kufanikisha shughuli yetu hii adhimu. Sala na salamu zimfikie Mtume wetu Muhammad S.A.W.

Pili, niwashukuru sana Wananchi wa Zanzibar kwa imani kubwa walioyonayo juu yangu, kwa hakika hujikuta nipo katika wakati mgumu kila ninapojiona ninaishiwa nguvu za kuwatumikia ndipo imani yao huongezeka na kunipa nguvu kubwa. Imani ya wananchi hawa kwangu umekuwa ni wito mtakatifu unaonilazimisha kusimama kuendelea kuwatumikia.
Tatu, nakishukuru sana chama changu kwa kuwa na imani nami na hivyo kupendekeza jina langu kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Mwisho, lakini si mwisho kwa umuhimu, nakushukuru wewe Mhe Rais kwa nia yako thabiti uliyoionyesha ya kujenga maridhiano na kukubali pendekezo la chama changu na kuniteua kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais.

Mheshimiwa Rais,
Kwa upande wetu, uamuzi wa kuingia katika Serikali, Baraza la Uwakilishi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haukuwa uamuzi rahisi na mwepesi. Ulikuwa ni uamuzi uliotufikirisha sana, tumejadili sana na tumepishana sana. Hatimaye tukafikia uamuzi. Moja ya sababu zilizotufanya kufikia uamuzi huo ni imani yetu kwako wewe binafsi, maneno yako, vitendo na ishara zako ambazo zimetushawishi kuwa unayo nia njema na dhamira safi ya kututoa tulipokwama na kuibadilisha Zanzibar yetu katika nyanja zote. Tumeona wewe ni mtu tunayeweza kufanya naye kazi, tunayeweza kusikilizana na tunayeweza kukupa nafasi uthibitishe nia yako njema. Nia yako ambayo ndiyo iliyotufanya na sisi tutangulize nchi kwanza licha ya madhila yote yaliyojitokeza katika Uchaguzi uliopita.

Wenzangu walipokuja na wazo hili la sisi kuungana na wewe, na baada ya kushauriana na wanachama wetu, niliwashauri kuwa sasa ni wakati wangu mimi kupumzika na kupeleka jina la damu mpya. Hawakunikubalia. Waliniambia, wewe ndiye uliyeongoza maridhiano na Rais Amani Karume mwaka 2009 na wewe ndiyo uliyeshiriki Serikali ya Kwanza ya Umoja wa Kitaifa na Mheshimiwa Rais wa wakati huo Dkt. Mohamed Ali Shein. Wakaniambia maadam wewe ndio umelianza, basi ulimalizie. Wakasema wewe mtu mzima na utu uzima dawa. Wakanitaka nikubali ili nije kusaidia azma hii ya kutibu majeraha ya Zanzibar na kuyastawisha maridhiano. Sikuweza kuwakatalia. Niliwakubalia na ndio maana leo niko hapa.

Mheshimiwa Rais,
Serikali ya Umoja wa Kitaifa [SUK] iliyoasisiwa na Katiba ya Zanzibar kupitia Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya mwaka 2010 ilikusudiwa kuwa chombo cha kusimamia, kuratibu na kuongoza juhudi za Wazanzibari kufikia Maridhiano na Umoja wa Kitaifa. Haikuwa na bado sio lengo la Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuwa chombo cha kugawana vyeo kwa kambi za kisiasa. Ni vyema jambo hili tukalikumbuka kila wakati.

Katika kuwasaidia wale wenye imani au ufahamu potofu juu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, napenda kutumia mfano rahisi. Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni sawa na chombo cha usafiri. Kwa msafiri yeyote awe wa baharini, angani au nchi kavu, lengo lake sio kuingia katika meli, ndege au gari. Lengo lake ni kufika safari aliyopanga. Safari ya Wazanzibari ni Maridhiano ya Kweli, Mshikamano na Umoja wa Kitaifa. Chombo chetu cha kufika safari hiyo kwa wakati ni Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hivyo, ni wajibu wa viongozi sote ambao tumepewa jukumu la kuongoza Serikali kuhakikisha kwamba tunaelekeza chombo hichi katika safari hiyo.

Mheshimiwa Rais,
Maridhiano yale yalilenga sio tu kuwa na mfumo shirikishi katika uendeshaji wa nchi bali yalikusudia kuondoa kabisa siasa za mivutano zilizotawaliwa na chuki, uhasama na visasi ambavyo kwa njia moja au nyengine vimekwamisha ustawi wa nchi yetu kwa muda mrefu sana. Tulitarajia pia kupitia maridhiano yale tungetoka katika diwmbi la historia ya kuwa na chaguzi za mivutano ambazo zimekuwa ni sababu ya maafa makubwa kwa wananchi wa Zanzibar.

Kwa masikitiko makubwa sana, Maridhiano yale yalikwama njiani. Kwasababu hii basi uchaguzi wa mwaka 2020 umeturejesha tulikotoka. Uchaguzi umetuacha na uhasama mkubwa ZAIDI, umetuacha na maafa makubwa zaidi. Haya ni mambo ya aibu sana na fedheha kwa nchi yetu. Hili ni doa katika historia ya nchi yetu na hatuna budi kuchukua hatua thabiti za kulifuta doa hili kwa njia itakayowaridhisha waathirika na wananchi kwa ujumla. Kuja kwetu Serikalini na kuingia kule Barazani, ni ishara ya nia yetu njema ya kutaka kushirikiana na wewe kutafuta majawabu wa kudumu ya matatizo haya.

Mheshimiwa Rais,
Uchaguzi Mkuu uliopita na changamoto zilizojitokeza zimetufunua macho kuwa majawabu ya kisheria na kikatiba pekee hayatoshi kutufikisha katika matamanio yetu ya maridhiano. Tunao wajibu sawia wa kutafuta majawabu pia ya kutafuta muafaka wa kijamii. Zanzibar iliyogawika haiwezi katu kupiga hatua yoyote ya maendeleo. Maridhiano, amani na utulivu ndio jawabu la kuivusha Zanzibar kutoka ilipo sasa kwenda kuwa Zanzibar iliyopiga hatua kubwa kimaendeleo.

Kwasababu ya mwelekeo huu ndio maana chama changu cha ACT Wazalendo na mimi mwenyewe binafsi tumekubali kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kusaidia na Kuijenga Zanzibar mpya. Ni imani yangu binafsi na Chama Changu kuwa wajibu wa mwanzo wa Serikali hii ya awamu ya 8 utakuwa ni kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar kuwa wa moja. Kwa muktdha huo basi tumekubali kuja kushirikana na wezetu katika kuhakikisha kuwa yaliyotokea kabla, wakati na baada ya Uchaguzi wa Oktoba 2020 hayajirudii tena.

Mheshimiwa Rais,
Leo si siku ya kusema sana. Bila shaka tutapata wasaa mwingi wa kukaa pamoja, kushauriana na kutafakari mustakhabali wa Zanzibar yetu na nini kwa pamoja tunaweza kufanya. Nikuhakikishie juu ya dhamira yetu safi mimi na wenzangu ya kufanya kazi na wewe kwa manufaa ya Wazanzibari wote.
Nimalizie kwa kukupongeza Mhe Rais kwa kuanza kazi vizuri. Nimpongeze pia Ndugu yangu Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais. Aidha niwapongeze Mawaziri wote waliobahatika kuteuliwa pamoja na Wakuu wa Mikoa. Niwapongeze pia wawakilishi Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazuri na Mheshimiwa Omar Said Shabaan kwa kuteuliwa na wewe kuwa Wawakilishi.

Mheshimiwa Rais,
Mwisho kabisa nitoe wito kwa Wazanzibari wote waliopo ndani na nje ya nchi wakubali kunyoosha na kupokea mkono wa Maridhiano. Tumeze machungu yanayotakana na Uchaguzi.. Historia yetu imejaa kila ina ya majeraha, ni wakati wa kuzika historia hiyo na kushikamana kuijenga Zanzibar yetu. Maridhiano ndiyo yatayofungua milango ya kuiwezesha Serikali kuchukua hatua za marekebisho na kujenga upya pale palipovunjwa, pale palipovurugwa, pale palipoharibika na pale palipokosewa.
Bila ya hatua hii, mageuzi tunayoyataka hayataweza kufanyika na kusimamiwa ipasavyo kwa kiwango cha kukidhi matarajio ya wananchi. Na sisi viongozi tuonyeshe njia kwa wananchi wetu kwa kutibu majeraha haya kwa waathirika kwa kuwaonyesha kwa vitendo kwamba tunayo nia ya dhati ya maridhiano ili tujenge Zanzibar moja, Zanzibar yenye kuheshimu haki na kulinda misingi ya kidemokrasi tuliyojiwekea.

Mungu Ibariki Zanzibar!
Ahasanteni kwa kunisikiliza.
 
Yule Balozi wa Marekani ametuma salamu za pongezi kwa Raisi wa JMT na wa SMZ😂😂😂😂
 
Makamu wa Rais serikali ya Zanzibar kuapishwa na Rais wakati makamu wa Rais serikali ya muungano anaapishwa na jaji tafsiri yake nini?

Wataalamu wa mambo ya katiba na sheria tuelimishane jamani. Nipo gizani.
 
Makamu wa Rais serikali ya Zanzibar kuapishwa na Rais wakati makamu wa Rais serikali ya muungano anaapishwa na jaji tafsiri yake nini?
Wataalamu wa mambo ya katiba na sheria tuelimishane jamani. Nipo gizani
Huyu wa Muungano amechaguliwa na kura za wananchi na huyo wa visiwani ameteuliwa na Rais wa SMZ baada jina kupendekezwa na ACT
 
Watu wamevunjwa miguu mzee sasahivi yupo ndani ya V8
Waliovunjwa miguu walifatwa majumbani mwao?? Usiko tii sheria utashurutishwa...hebu geukia kwa mzee hapo uganda amesemaje kuhusu raia wanaorushia mawe polisi?? Nchi yetu ina amani hadi imepitiliza
 
1) 2020 Hussein Ally Hassan Mwinyi kamuapisha Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wake namba moja

2) 1984 Ally Hassan Mwinyi alimuapisha SEIF SHARIF HAMAD kuwa Waziri Kiongozi wa Znz

Historia kubwa sana kaweka

'Son of a Lord will be a Lord…'

Mzee Mbishi hatare
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom