Rais Magufuli una nafasi kubwa sana ya kuokoa maisha ya Watanzania kuliko mtu yeyote

Hamatan

JF-Expert Member
Nov 10, 2020
3,183
7,645
Naomba niwe mkweli wa dhamira yangu ili nisinene kwa unafiki au ushabiki wa aina yoyote. Na wachangiaji wote, ningefurahi wakichangia kwa mtazamo huo huo.

Rais Magufuli anaogopwa, karibia na kila mtu, kuanzia wasaidizi wake, wateule wake, hata na watu wa sekta binafsi. Rais Magufuli akiagiza jambo, mara nyingi, kesho yake nchi nzima linaanza kutekelezwa likisimamiwa na wateule wake kwa nguvu zote.

Hali hii ina faida na hasara yake. Faida Ni kwamba kama Jambo analotaka lifanyike, ni jambo sahihi, basi kuna uhakika wa kutekelezwa. Hasara ni endapo analotaka lifanyike, likawa siyo jambo sahihi, hakuna atakayenyanyua mdomo kumpinga, sana sana watu wataishia kumpinga kwenye mitandao yetu hii yenye majina yasiyo halisia.

Kwenye corona, sasa hivi, baadhi ya wasaidizi wake, wakiwa maeneo mengine wanavaa barakoa lakini wakiwa mbele ya Rais au kwenye tukio official ambako wanahisi Rais atawaona, hawawezi kuvaa barakoa kwa sababu wanaamini Rais hataki.

Tunachomsihi Rais Magufuli, ajue kuwa vita hii ya Corona, kutokana na hali ya kuogopwa aliyojijengea, ni yeye ndiye mwenye kura ya turufu.

Kuna mambo 4 yanatajwa kuwa kila mahali yamethibitika kupunguza sana maambukizi:

1) kuzuia mikusanyiko
2) uvaaji barakoa
3) kunawa mikono kwa maji tiririka
4) upimaji ili walioambukizwa wapewe huduma za kuwasaidia kabla ya kuugua

Kwa hali aliyoijenga, nina hakika, Rais ukitangaza kuwa kufikia keshokutwa, maeneo yote ya ofisi, biashara , vituo vya mabasi, maeneo ya ibada kuwe na maji tiririka; Akasema watu wote wanapotoka majumbani na kwenda maeneo public lazima wavae barakoa; Akasema mikutano yote, sherehe na mikusanyiko isiyo ya lazima imezuiwa; na ile ya lazima izingatie umbali wa mita 2 toka mtu mmoja hadi mwingine; na pia hospitali za imma na binafsi na taasisi nyingine, wanaruhusiwa kuwapima watu kwa lengo la kuwapa huduma za kuwasaidia wenye maambukizi badala ya kusubiri mpaka waugue; binafsi nina hakika, ndani ya siku 2 kila kitu kitabadilika. Hakuhitajiki fedha wala nyenzo zozote toka Serikalini (labda kwenye vipimo tu) kuyatenda haya, ni kauli yake tu, lakini atakuwa amepunguza maelfu ya vifo.

Upimaji, na hasa kwa vijana, utasaidia kujua hali zao ili Kama wana maambukizi waweze kujizuia kwenda kuonana na wazee ambao ni kundi lililoko kwenye hatari. Wazee kuanzia miaka 60 kwenda mbele ilikuwa ni muhimu kuwapima wote ili walioambukizwa wapewe msaada wa tiba zinazosaidia kufubaza virusi, kabla ya kuanzia kuugua.

Najua Rais Magufuli, wewe ni mgumu sana kupokea ushauri, hasa kama ushauri huo haupo katika kike unachokiamini, lakini angalao kwenye hili , tunaomba uwaonee huruma watanzania. Hatutamaliza tatizo lakini tutaokoa wengi. Roho za watanzania zipo mikononi mwako, zikipotea kwa sababu ulishindwa kuutimiza wajibu wako kama kiongozi mkuu, ambao ni kuwalinda wao na mali zao, hakika una mashtaka mbele ya Mungu, sawa tu na yule aliyeua kwa kukusudia.

Tunaomba Mungu akujakie hekima, na wala shetani asiushupaze moyo wako. Tanzania ni ya wengi, wewe ni mmoja tu, ni muhimu usikilize mawazo ya Watanzania wote, uyachambue kwa umakini kwa kushirikiana na watu walio wakweli wa nafsi zao, siyo wanafiki kama hao wengi waliokuzunguka. Wakiwa na wewe barakoa wanaweka mifukoni au kuacha kwenye magari. Ina maana wanatenda wasichokiamini. Hawa Kama endapo mambo yataendelea kwenda vibaya, ujue kamwe hawatasimama na wewe katika shuhuda Bali watakuwa miongoni mwa watakaokuhukumu kwa uongozi mbaya.

Watanzania wanakufa sana nchi nzima kwa Covid 19, hatujui Ni wangapi Ila Ni wengi maana kila unayeongea naye anazungumzia msiba wa jirani, mtu anayemfahamu, rafiki au wanatamilia. Binafsi, nikihesabu ndugu, maratiki, ndugu wa marafiki zangu, na watu niliowafahamu kwa maana ya kuwa jirani nao, ambao wamefariki kwa dalili zinazoashiria tatizo la Covid 19, mpaka leo, ndani ya mwezi mmoja ni watu 15. Hali hii haijawahi kutokea hata mara moja katika maisha yangu yote.

Tushirikiane kupambana na corona, tushirikiane kumshauri au hata kimshinikiza Rais. Hatufanyi hivyo kutaka kumdhalilisha au kumdhihaki bali kwaajili ya kuokoa maisha yetu na ya ndugu zetu. Mioyo yetu imejaa simanzi kubwa kwa kupoteza wapendwa wetu, lakini simanzi kubwa zaidi ni kuona Rais anaona kama Ni kitu cha kawaida. Inaumiza sana. Yinamwomba Mungu Tena Tena, ampe ufahamu Mh. Rais ili alione tatizo katika uhaoisia wake.
 
Back
Top Bottom