Uchaguzi 2020 Rais Magufuli: Uchaguzi 2020 utakuwa huru na wa haki

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,490
54,884
Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema Serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, 2020 unakuwa wa amani, uhuru na haki.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema utakapofika uchaguzi huo, nchi na taasisi mbalimbali zitakaribishwa Tanzania kushuhudia.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Januari 21, 2020 alipokutana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania katika sherehe za mwaka mpya 2020 na chakula cha jioni zilizofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Amebainisha kuwa uchaguzi ni jambo muhimu, Serikali imejipanga kuandaa mazingira mazuri katika uchaguzi huo.

“Mwaka 2020 mwezi Oktoba nchi yetu itafanya uchaguzi mkuu, zoezi la uchaguzi ni muhimu kwa nchi yoyote inayofuata misingi demokrasia, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu unafanyika katika mazingira ya amani, uhuru na haki” amesema Rais Magufuli.

Amesema ukikaribia uchaguzi huo nchi mbalimbali na taasisi za zitakaribishwa Tanzania kushuhudia.

“Kama ilivyo kawaida yetu wakati ukifika tutazikaribisha nchi na taasisi mbalimbali kuja kuangalia uchaguzi wetu ili kujionea jinsi nchi yetu inavyokomaa katika nyanja ya demokrasia,” amesema Magufuli aliyeapishwa kuwa Rais wa Tanzania Novemba 5, 2015.


Zaidi soma:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewashukuru Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Serikali ya Awamu ya Tano na hivyo kuwa Sehemu ya mafanikio makubwa ya yaliyopatikana nchini Tanzania katika miaka 4 iliyopita.

Mhe. Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo tarehe 21 Januari, 2020 katika hafla ya kuukaribisha Mwaka Mpya aliyowaandalia Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa (Sherry Party) na kufanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amesema miaka 4 ya tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 – 2020, mipango ya kimataifa na kikanda na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka 5 (2016/17 – 2020/21) iliyolenga kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.

Ametaja baada ya mafanikio hayo kuwa ni kulinda na kudumisha amani na usalama wa nchi, kuimarisha Muungano ambao Aprili 2020 utatimiza miaka 56, ukuaji mzuri wa uchumi wa wastani wa asilimia 7, kudhibiti mfumuko wa bei hadi kufikia asilimia 3.5 na kuongeza akiba ya fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani Bilioni 4.123 hadi kufikia Dola za Marekani 5.579 zinazotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kwa kipindi kisichopungua miezi 6.3.

Mafanikio mengine ya kiuchumi ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa shilingi Bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia shilingi Trilioni 1.5 (ambapo Desemba 2019 ilifikia shilingi Trilioni 1.9), kuvutia uwekezaji wenye thamani ya shilingi Trilioni 30 uliozalisha ajira laki 1, kuogeza biashara ya nje kutoka shilingi Trilioni 11.5 hadi kufikia shilingi Trilioni 16.6, kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara kutoka tani 796,512 hadi kufikia tani 1,141,774 (ongezeko la asilimia 43.3) na kujenga viwanda vipya 4,877.

Aidha, katika kipindi hicho mauzo ya dhahabu nje ya nchi yameongezeka kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.469 hadi kufikia Bilioni 1.743, mapato ya Serikali kutokana na madini yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 168 hadi kufikia shilingi Bilioni 346, idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii Milioni 1.1 hadi kufikia Milioni 1.5 na mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.9 hadi kufikia Bilioni 2.488.

Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa katika kipindi hicho Serikali imetekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge railway) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma utakaogharimu zaidi ya shilingi Trilioni 7, ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme utakaogharimu shilingi Trilioni 6.5, ujenzi wa kilometa 2,500 za barabara za lami na nyingine 2,400 zikiendelea kujengwa, kilometa 7,087 la barabara za lami zikiwa katika maandalizi ya kuanza kujenzi na kukamilisha ujenzi wa madaraja makubwa 8.

Miradi mingine ni kufufua reli ya Dar es Salaam – Tanga – Moshi iliyokuwa haitoi huduma tangu miaka zaidi ya 20 iliyopita, kupanua bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga, kukarabati meli 7 katika maziwa makuu, kukamilisha ujenzi wa jengo la 3 la abiria katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (Terminal III), kujenga viwanja vya ndege 11, kununua rada 4, na kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) baada ya kununua ndege mpya 11.

Kwa upande wa huduma za kijamii amesema mbali na kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, Serikali imejenga njia ya umeme ya Iringa – Shinyanga, Makambako – Songea na Lindi – Mtwara, kupeleka umeme vijijini ambapo idadi ya vijiji vilivyofikiwa na umeme imeongezeka kutoka 2,018 hadi kufikia 8,587, kujenga vituo vya afya 352 na Hospitali za Wilaya 69, kuajiri watumishi wa afya 8,000 na kuongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba kutoka shilingi Bilioni 31 hadi kufikia shilingi Bilioni 270 kwa mwaka.

Amebainisha kuwa Serikali inatoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari ambapo imeshatumia shilingi Trilioni 1, mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka shilingi Bilioni 341 hadi kufikia shilingi Bilioni 450, imetekeleza miradi ya maji yenye thamani ya shilingi Trilioni 3 na hivyo kuongeza upatikanaji wa maji kutoka wastani wa asilimia 56 hadi kufikia asilimia 71, kuongeza mapambano dhidi ya rushwa na Serikali kuhamia Dodoma.

Mhe. Rais Magufuli amesema kwa kuongozwa na sera ya diplomasia ya uchumi, Tanzania imeendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na nchi mbalimbali duniani ambapo pamoja na kufanya ziara katika nchi mbalimbali, Balozi mpya 7 zimefunguliwa na kushiriki katika shughuli na mipango mbalimbali ya kimataifa ikiwemo ulinzi wa amani ambapo kwa sasa askari 2,297 wa Tanzania wapo katika ulinzi wa amani katika nchi mbalimbali.

Ameahidi kuwa katika mwaka 2020 Serikali imejipanga kuendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, kudumisha amani na usalama, kukuza zaidi uchumi, kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, kuongeza ukusanyaji wa mapato, kukuza sekta kuu za uzalishaji yaani kilimo, viwanda, ujenzi, madini na utalii pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ambapo amewaomba Mabalozi hao kuwashawishi wafanyabiashara wa nchi zao kuja kuwekeza nchini Tanzania.

Pia, amewahakikishia kuwa katika mwaka 2020 ambapo Tanzania inafanya Uchaguzi Mkuu, Serikali imejipanga kuhakikisha unafanyika kwa misingi ya kidemokrasia na katika mazingira ya amani, uhuru na haki, na amezikaribisha nchi na taasisi mbalimbali kuja kuangalia jinsi Tanzania ilivyokomaa kidemokrasia pindi wakati ukifika.

Ameahidi kuwa Tanzania, itaendelea kukuza ujirani mwema, kushirikiana na nchi mbalimbali na kutekeleza majukumu ya kimataifa ikiwemo kuwahudumia wakimbizi na kuwarejesha makwao kwa hiari, lakini ameeleza kusikitishwa na hujuma na propaganda zinafanyika kwa lengo la kukwamisha zoezi hilo.

Akizungumza kwa niaba ya Mabalozi hao, Kiongozi wa Mabalozi (Dean of Diplomatic Corps) Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi mzuri aliouonesha katika kipindi cha miaka minne ambapo miradi mikubwa ya maendeleo imetekelezwa, kukua kwa uchumi, ustawi wa watu na ameahidi kuwa Mabalozi wataendelea kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

21 Januari, 2020
 
Mpaga bhona ya ng'wa Toma.

Kama hutaelewa maana. Tafsiri yake kwa ufupi ni kile kisa cha Yesu na mwanafunzi wake Thomas aliyesema nisipoona na kupapasa mahali alipogongelewa misumari, sitaamini.

Hivyo nami nafata principle ya Thomaso ya kwamba, mpaka nione huo mwezi wa kumi, tofauti na hapo ni porojo tupu.
 
Anawazuga hao mabalozi, ukweli ni kuwa yeye hasa ndio tatizo la chaguzi zetu kwa sasa. Kama kweli anaamini katika chaguzi huru na haki, tuwe na tume huru ya uchaguzi isiyoundwa wala kuchukua maagizo kutoka kwake. Kinyume na hapo ni kuwa anaongea maneno ya kufurahisha genge.
 
Back
Top Bottom