Rais Magufuli tafadhali tuondolee hizi mbio za mwenge na utuachie mwenge wetu wa uhuru

Apr 23, 2012
76
71
Martin Maranja Masese,

Nianze kwa kunukuu maneno ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, maneno yake ambayo aliyatoa wakati mwenge wa uhuru unawashwa juu ya kilele cha mlima Kilimanjaro, alisema maneno yafuatayo ;

"Tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu; ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini; upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau."

Mwenge huo uliwekwa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro na Luteni Kanali, Alexander Nyirenda. Mwalimu Nyerere alisisitiza kwamba Mwenge una umuhimu mkubwa katika kuijenga Tanzania yenye umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa watu wote.

Ieleweke vyema sana, mimi ni mtanzania wa kuzaliwa, nimezaliwa na baba/mama wote ni watanzania, nathamimi utu, desturi, mila na tamaduni zote za mtanzania, naheshimu sheria, taratibu, kanuni zote zinazoongoza nchi yetu!

Naamini wengi kati yetu tuliopata kusoma miaka ya 1970-1980-1980, tutakuwa tunakumbuka ule wimbo maarufu wa mwenge, ulikuwa ukiimbwa hivi ;

"Sisi tumekwisha uwasha Mwenge, tumekwisha uwasha Mwenge..., na kuuweka juu ya mlima, Mlima Kilimanjaro..., kuwasha Mwenge, Kuwasha Mwenge na kuuweka Kilimanjaro..., kuwasha Mwenge, Kuwasha Mwenge na kuuweka Kilimanjaro."

Sifahamu sana kama kizazi hiki cha 2000' kitakuwa kimeimba wimbo huu katika maeneo yao ya shule!

Naelewa mantiki ya mwenge wa uhuru (Uhuru Torch) lakini sikubaliani hata kidogo na kitu kinaitwa 'Mbio za mwenge' au 'Uhuru Torch Race' nchi nzima.., (nieleweke vyema hapo).., dhana ya MWENGE WA UHURU ni tofauti sana na MBIO ZA MWENGE...,

Kwa ninavyoelewa mimi.., Mwenge wa Uhuru (Uhuru Torch) ulianza Disemba 9, 1961, siku ya Uhuru wa Tanganyika. Wakati bendera ya Malkia wa Uingereza ikishushwa Uwanja wa Taifa, maarufu sasa kama shamba la bibi.., bendera ya Tanganyika ilipandishwa, sambamba na Mwenge wa uhuru kuwashwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Hiyo inadhihirisha kwamba Mwenge wa Uhuru una maana kubwa sana kwa uhuru wa nchi hii... (ndiyo maana nimeomba kwa dhati sana, tuendelee na MWENGE WA UHURU na tuondolee MBIO ZA MWENGE WA UHURU...., mwenge wa uhuru ni alama ya mwanga wa ukombozi kwa taifa letu, ni kumbukumbu yakinifu kuonesha ukombozi wa taifa hili...

Nimepita katika tovuti kuu ya serikali, Tovuti Kuu ya Serikali: Mbio za Mwenge wa Uhuru na kwa mujibu tovuti ya Serikali ya Tanzania, Mwenge wa Uhuru huzunguka nchi nzima ukiwa na ujumbe wa matumaini, upendo, heshima na amani. Mwenge huo huanzia katika mkoa wowote utakaochaguliwa kila mwaka na mbio hizo hufika tamati Oktoba 14, siku ambayo Taifa huadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Vilevile, tovuti ya Serikali inaongeza kwamba Mwenge huwa na ujumbe tofauti kila mwaka, kulingana na vipaumbele vya maendeleo vya mwaka husika.

Binafsi naamini kabisa kwamba, lengo la 'mbio za mwenge' ni kujikumbusha kuhusu wajibu wetu kama wananchi kuwa na umoja, mshikamano, upendo na amani... Ndiyo dhima kubwa ya mbio za mwenge!

Lakini hadi sasa, miaka ya karibuni, mambo yamebadilika sana, mbio za mwenge zimepoteza maana ya uwepo wa mwenge wa uhuru, kwa watu kutumia mwenge wa uhuru kupiga pesa za umma, kujinufaisha na kufuja mali... na athari nyingine nyingi...

Nitakuja na ushauri mbadala wa nini kifanyike na kipi kiachwe.., tuendelee!


Tarehe 27-5-2014 siku ya Jamanne, saa 4 asubuhi, kwenye kipindi cha maswali na majibu, bungeni mjini Dodoma, aliyekuwa naibu waziri wa habari vijana, utamaduni na michezo (wakati huo), Juma Nkamia alieleza makadirio ya gharama za kukimbiza Mwenge wa Uhuru nchini kwa mwaka 2014.

Juma Nkamia alisema yafuatayo, naomba kumnukuu;

"Serikali kuu hutenga kiasi cha fedha kulingana na mahitaji na gharama halisi ya wakati husika.. Mwaka 2012 jumla ya shilingi Bilioni 43 zilitumika ambapo kati ya hizo Bilioni kumi na moja (11) zilitengwa na serikali na Bilioni 32 zilichangwa na mashirika, taasisi, makampuni na wadau mbalimbali walioombwa kuchagia kwa ajili ya kuadhimisha uzinduzi na kilele cha mbio za mwenge wa uhuru."

Taarifa zinaonesha kuwa mwaka 2014 inakadiriwa jumla ya Shilingi Bilioni 120 zilitumika kama gharama ya kukimbiza Mwenge nchi nzima..., kwa mujibu wa Juma Nkamia mwenyewe, alisema;

> Serikali kuu hutenga kiasi cha fedha kulingana na mahitaji na gharama halisi ya wakati husika
> Mwaka 2012 jumla ya shilingi milioni mia sita hamsini (650) zilitengwa kwa ajili ya kuadhimisha uzinduzi na kilele cha mbio za mwenge wa uhuru
> Kati ya hizo milioni 450 zilitumiwa na Wizara na milioni 200 zilitumiwa na mkoa uliokua mwenyeji wa sherehe za kilele (650,000,000/-)
> Kwa ujumla mwaka 2012 Wananchi walichangia zaidi ya BILIONI 11 na milioni 500 (Tsh 1,500,000,000/-)
> Halmashauri za wilaya na manispaa zilichangia shilingi BILIONI arobaini na tano ( Tsh 45,000,000,000/-)
> Wahisani na watu binafsi walichangia zaidi ya shilingi milioni 52 (Tsh 52,000,000/-)

Hizi ni hesabu za mwaka 2014.., huu ni mwaka 2016 (mahitaji lazima yatakuwa yameongezeka baada ya kupita miaka 2 sasa).. Tuendelee kutumia takwimu hizo kujenga hoja yetu hapa....

Tutazame faida tanzu za mwenge kama zinavyoelezwa mara kwa mara na serikali kupitia wizara husika na ukimbizwaji mwenge huo (kisha tulinganishe, faida hizo na gharama zinazotumika kuukimbiza nchi nzima)

(i) Kuendelea kutunza historia na falsafa ya ukombozi wa taifa letu,
(ii) Kuhamasisha Wananchi kuhusu umuhimu wa kuendelea kuenzi amani,
(iii) Kuhamasisha mshikamano, upendo, amani, utulivu miongoni mwa jamii zetu,
(iv) Kupambana na ubaguzi wa aina zote katika jamii zeti, haswaa ubaguzi wa dini, rangi au ukabila.
(hutumika kuhimiza miradi ya maendeleo kwa kufungua mawe ya msingi katika maeneo mbalimbali.

Pesa zinazotumika katika kukimbiza Mwenge huo wa uhuru, tunaweza kuzielekeza kwenye maeneo mengine, zikafanya kazi yake..

(i) Kuzielekeza kwenye wizara ya afya, kujenga miundombinu mbinu ya afya mfano Zahanati, wodi, maabara, ofisi.

(ii) Kulipa mikopo ya wanafunzi ambao wengine wamekosa na wengine wanacheleweshewa kwa sababu mbalimbali.

(iii) Kuboresha huduma ya usafiri wa majini, kwa kununua boti za mwendokasi na meli kubwa au za kati katika njia ya ziwa na bahari.

(iv) Kuboresha usafiri wa anga, kwa kununua ndege za kutosha na kuwekeza katika sekta ya huduma ya usafiri wa anga.

(v) Kununua dawa na vifaa tiba katika hospitali za umma nchi nzima, Vituo vya afya, zahanati na hospitali za umma zinakabiliwa na uhaba wa dawa na vifaa tiba.

(vi) Kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kujenga miundombinu mbinu rafiki ya kujifunza na kufundishia, (kujenga vyoo, madarasa, nyumba za walimu, madawati,

(vii) Kuelekeza pesa hizo katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja na pia reli.., miundombinu ya nchi bado siyo imara.

(viii) Kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya kibiashara, masoko makubwa na majengo ya umma kwa ajili ya biashara.

(ix) Kuzielekeza pesa hizo katika idara ya mahakama, kuna halmashauri hazina mahakama, wanachi wanatumia mwendo mrefu kwenda kwenye kesi zao, pesa zikakenge mahakama.

(x) Kuboresha viwanja vya ndege, mikoa mingi haina viwanja vya ndege, vilivyopo mikoani havina ubora wa kutoa ndege kubwa.

(xi) Kujenga vituo vya watoto vya michezo mbalimbali nchi nzima, taifa linakabiliwa na ukosefu wa 'Academy' za michezo ya watoto.., zipo chache, tena za binafsi.

Zipo kazi nyingi sana ambazo pesa hizo zinaeweza kuelekezwa na zikafanya kazi yenye kupigiwa makofi na kila mtanzania... (tunaomba mwenge wa uhuru uendelee kuwepo, lakini mbio za mwenge wa uhuru nchi nzima, zifike tamati sasa)..., kama kweli tunataka kubana matumizi..


Miaka ya hivi karibuni, wananchi wengi sana wanaonekana wamekosa 'muamko' na wamepoteza imani na mbio za Mwenge wa uhuru.., wengine wanafikia hata kusema 'Mwenge wa uhuru' ni mtumishi hewa, kutokana na sababu kadhaa wa kadhaa..., wananchi hao wanamiliki sababu zao za msingi kabisa, ambazo ni muhimu uongozi wa nchi una kila Sababu ya kuzisikiliza.

Moja kati ya sababu kubwa ni kwamba mbio za Mwenge kwa kiwango kikubwa, zinaonekana kutumia pesa nyingi kwa mwaka, pesa inayotumika kuzunguka nchi nzima ni kubwa sana, pamoja na posho na usafiri kwa wale wakimbiza Mwenge wote na gharama za chakula, malazi na makazi kwa muda wote wa kukimbiza huo mwenge.

Ongezeko kubwa sana la magonjwa ya kuambukiza haswaa magonjwa ya zinaa, mwenge ukifika eneo fulani, lazima utakesha hapo, watu watacheza muziki na ngoma usiku kucha (sehemu mwenge huo ulipolala).., vitendo vya uzinifu huchukua nafasi yake kubwa, hivyo inaaminika kwamba mkusanyiko wa mbio za mwenge ni sehemu nyingine ya ongezeko la magonjwa ya kuambukiza yatokanayo na zinaa..

Mbio za Mwenge wakati mwingine hutumika kama upenyo wa kufanya zinaa isiyo salama., ukifanya uchunguzi mdogo mwenge wa uhuru ulipolala, asubuhi unaweza kukusanya mipira ya kiume zaidi ya ndoo nzima au zaidi (kuna wengine ambao hawakutumia kabisa mipira hiyo wakati wa tendo hilo).

Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2016, rasmi mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2016 zilizinduliwa Aprili 18, 2016. sherehe hizo za uzinduzi zilofanyika katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro., na zilizinduliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan (makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania)

Ushauri wangu ;

Ni wazi watu hawaelewi kabisa historia na dhima ya uwepo wa mwenge wa uhuru.., (ndiyo maana sishangai kabisaa wale wanaotaka mwenge wa uhuru uondolewe kabisa)...,

Hivi, watu wanajua kwamba Mwenge wa UHURU ni alama ya Taifa, na kwamba upo kwenye ngao ile ijulikanayo kama 'Bibi na Bwana?'

Watu wanaelewa kwamba Mwenge ukifutwa, maana yake ni kwamba unakuwa umefuta historia ya nchi na huenda hata ile ngao ya Taifa itabidi ibadilishwe kwa kuwa imebeba alama za Taifa? Watanzania wanahitaji kuelimishishwa kuhusu hilo...

Mimi na wengine wengi tunapenda sana mamlaka za nchi hii, zifute kabisa MBIO ZA MWENGE WA UHURU lakini ziache MWENGE WA UHURU (uhuru torch).., mwenge wa uhuru uwashwe kama kawaida, uwekwe pale Makumbusho, au ujengewe eneo maalum, na utawaka mwaoa mzima bila kuzimwa, na maadhimisho yake yaendane na siku ya UHURU wa Tanganyika na siyo kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere... (sioni mantiki ya kukumbuka kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na mwenge wa uhuru)

Watanzania wanapaswa kufahamu kuhusu historia ya Mwenge wa uhuru, Kubebwa na kuwashwa kwake na Luteni Nyirenda juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro... (waelimishwe, wataelewa)

Watanzania pia wanapaswa kufahamu kuhusu kauli ya 'amani, upendo, mshikamano na matumaini' iliyotolewa na hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati mwenge wa uhuru unapandishwa katika kilele cha mlima Kilimanjaro...

Hebu jaribu kujiuliza..., Kama shughuli za kuuzima mwenge wa uhuru (siku moja) kwa kuhitimisha mbio zake pekee, huko Bariadi, Simiyu, kwa waliokatazwa kwenda zimeokolewa bilioni 6 (kwa mujibu wa taarifa), vipi mbio za mwenge wa uhuru zilizofanyika nchi nzima, zimetumia kiasi gani cha pesa!!?

Una kila sababu ya kusema "Rais Magufuli Tafadhali Tuondolee Hizi Mbio Za Mwenge Na Utuachie Mwenge Wetu Wa Uhuru "

Ahsante;

Martin Maranja Masese
Mwananchi wa kawaida
martinchizzle@gmail.com
 
1476361586313.jpg
kazi ya mwenge wa uhuru ... Bilion 222for this
 
... mwenge miaka nenda miaka rudi unakimbizwa eti kuaangaza na kufichua wala rushwa na majizi kumbe badala yake unawamulikia taa na kuwasafishia njia ili waone vizuri, na ndio maana kila mwaka majizi ya mali ya taifa yanaongezeka, chaaa! Watanzania bana! Siku wakiamka usingizini watalia sana kwa ujinga ambao wamekuwa wakiukumbatia karne nenda karne rudi...
 
Uhuru tayari tumeshapata .kazi tuliyonayo kwa sasa ni kupambana na maadui wakuu 3.Umaskini,maradhi na ujinga.Tujiulize hizo mbio zinatusaidiaje kuwaondoa hawa maadui.
 
Hata uutete vp mwenge hauna faida kwa sasa, kama ni ufisad ndio unazd , vita ya kisasa tubadili n mbinu ziwe za kisasa
 
IMG_4668.jpg
hii si kauli mbiu ya katiba mpya?mwenge wa uhuru ubaki laa sivyo mshikamano wa watanzania utatoweka.
 
Haya mambo yatakuja kuondok ila taratibu sana coz kumkatia mtu ulaji sio kazi Rahisi ata kidogo inaweza mcost ata Rais mwenyew huwez jua kuna wakuu wangap wanakula apo kwe mwenge shangaa Rais anatawal miaka 5 tuu anakuja mwingine.... But bora hasara kuliko lawama fyekelea mbali mbio za mwenge mkuu naunga mkono hoja
 
Mambo ya mwenge, mimi yangu ni haya


P
 
Mambo ya mwenge, mimi yangu ni haya


P
 
Back
Top Bottom